Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, November 23, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-29


Docta aliposikia mimi naitwa, akasema

‘Ngoja mimi nikaongee naye kwanza…’akasema na nilitaka kumpinga maana mume wangu kaniita mimi, ni wajibu wangu kuitika wito wake kwanza, lakini docta akaniwahi na kukimbilia huko nje alipo mume wangu, ikabidi nisubirie tu.

Nikiwa nimebakia pale peke yangu, niliweza kuipitia ile taarifa ya rafiki yangu kwa makini,  na mpaka nafika mwisho nilianza kubadilika, kuwa huenda wanayoongea wenzangu yana ukweli fulani. Kwenye hii taarifa rafiki yangu alijaribu kama kuficha jambo, na kujihami kwa namna fulani, japokuwa haionyeshi wazi wazi kuwa kweli anahusika ..

Kwa maelezo ya taarifa hiyo, Muosha magari anasema aliosha gari la mume wangu, na pia la mdogo wa mume wangu kuonyesha kuwa wote wawili walifika hapo siku  hiyo, lakini docta anasema mdogo wa mume wangu alikuwa kwake wakiangalia mpira,..je muda gani alitoka hapo na kwenda huko…. nikjiuliza.

Hapo nikaona kuna muhimu wa kuonana na mdogo wa mume wangu kwa haraka iwezekekanavyo, lakini nisingeliweza kuondoka hapo, nikachukua simu na kumpigia huyo shemeji yangu, lakini simu haikupokelewa.

‘Nitampata tu….’nikasema na muda huo docta akaingia akisukuma kile kigari cha mume wangu, na mume wangu alikuwa kakaa kinyonge, akitikisa kichwa kama kukubali jambo fulani kwenye maongezi yao..na walipofika ndani docta akasema;

‘Tumemalizana na rafiki yangu, …mimi nataka kuondoka…’akasema

‘Sawa mimi nipo na mume wangu, sikusindikizi…’nikasema

‘Ni wajibu wako, lazima mleane kwa shida na raha…’akasema

Mume wangu akawa anakiendesha kigari chake peke yake na kuelekea chumbani, nikamuangalia docta, na docta akaniashiria nimfuate mume wangu, basi ikabidi niagane na docta, yeye akaondoka, na mimi nikamfuata mume wangu ndani.

‘Mbona unakuja huku, mgeni anabakia na nani, msindikize mgeni au..?’ akaniuliza

‘Anaondoka, nimeshaagana naye, kaondoka…’nikasema

‘Mimi nipo safi mbona, sasa hivi nataka nilale tu, nasikia kulala tu, nahisi macho mazito…’akasema

‘Uliamuka kabla dawa haijaisha nguvu yake…’nikasema

‘Niliota ndoto mbaya…’akasema

‘Ndoto gani…?’ nikamuuliza

‘Docta, ananiibia mke wangu…’akasema sasa akiniangalia huku anatabasamu kama utani vile

‘Hahaha, kama nikukuibia basi angelikuibia zamani, sio sasa, keshachelewa, na uzee huu anatakia nini tena kwangu, hizo ni ndoto za shetani usiziamini…kwanza yeye ana mke wake mnzuri..’nikasema

‘Mhh,..ni kweli lakini wewe ni mnzuri zaidi yake…, na .. na una mengi ambayo mke wake hana…’akasema

‘Kama yapi, …?’ nilimuuliza lakini nikiwa na tahadhari.

‘Mali, familia yako ina julikana…na mengine mengi..’akasema

‘Na wewe umenioa kwa hayo pia, au sio…?’ nikauliza

Ofcourse yes, uzuri wako, na hayo mengine vilinifanya nijisikie nina mke wa maana sana,..ndio hivyo, mitihani hii inanifanya nijutie kwa niliyoyafanya, …lakini nakuahidi mke wangu hayo yaliyopita sitarudia tena…’Nilitaka kumuuliza yapi kayafanya, lakini nikaogopa, haitakiwi, nikabakia kimia.

‘Sikiliza mke wangu, ngoja nipone, nina uhakika nikipona, na nguvu zangu zikirejea vyema, kila kitu kitakuwa sawa, niamini, kila kitu kitarejea kama kilivyokuwa awali…,nimeligundua kosa langu....’akasema


‘Hilo neno mume wangu…, utapona tu, usijali…’nikasema

‘Niahidi mke wangu, kuwa hutaniacha…’akasema hivyo na kunifanya nishtuke kidogo, ni kauli yenye utata, sikufahamu ni kwa muda huo au ana lengo gani, lakini sikuruhusiwa kuanzisha mijadala, na pia, sikupenda kusema uwongo

‘Mume wangu dawa itakuwa haifanyi kazi, tukiendelea kuongea, wewe lala kwanza, umeshaharibu kwa kuamuka mapema, sasa inabidi ulale tu…ukiamuka tutaongea, unasikia, usipuuze maagizo ya docta, ukifanya makosa hutapona na ndoto yako haitatimia..’nikasema

‘Ndoto…!’akasema  kwa mshangao

‘Ndio za kuendeleza miradi yako, au sio…’nikasema

‘Haya bosi, ngoja nilale..kweli nasikia kulala, lakini sitaki niote hiyo ndoto tena, lakini naomba usiondoke hapa kitandani kabisa, nataka ukae hapa karibu yangu, nikiamuka tuongee, nataka niongee na wewe mambo mengi mazuri, ma-zzzrrr..’akasema

‘Haya lala…’nikasema nikiwa nimekaa karibu yake, na baada ya muda nikasikia akitoa ile sauti ya kuonyesha kuwa kweli kalala.

***************

Siku nyingine, nilikuwa nimekaa nyumbani, sebuleni, na mume wangu alikuwa amelala chumbani baada ya kupata dawa.  Na nilipohakikisha amelala, nikaona nitoke kidogo nje, kitahadhari, maana akiamuka akaona sipo karibu yake,  ni mtihani,..nikasema leo nataka nifanye jambo, angalau nitoke hata kufika madukani,.

‘Nani huyo tena…nikasema, niliposikia mtu anagonga geti la nje

 Muda huo nilikuwa varandani nakagua kuwa kila kitu kipo sawa, kwa vile najua kuwa mfanyakazi wetu wa ndani yupo, atafungua geti sikuhangaika kutok nje, lakini haikuwa hivyo, mfanyakazi alikuwa hayupo karibu na huyo mtu akawa anaendelea kugonga,..

‘Kaenda wapi huyu binti…’nikawa naongea peke yangu, nikachungulia kupitia dirishani, na muda huo, huyo mtu akawa anafungua geti mwenyewe, kabla sijajiuliza ni nani, mara akatokea mfanyakazi wetu, kumbe alikuwa anafanya usafi sehemu za ndani.

‘Nani kagonga geti na sasa anafungua geti mwenyewe…?’ nikamuuliza

‘Hata sijui ni nani ..ngoja nikaangalie…’akasema na kukimbilia nje.

Haikupita muda, nikasikia watu wanaongea huko nje na vicheko…nikaingiwa na hamasa ya kumtambua huyo mtu ni nani, maana ni sauti ya kime, nikachungulia dirishani, alikuwa ni mdogo wa mume wangu.

Mdogo wa mume wangu mhh, kajileta…!!

 Kwa haraka nikatoka nje, nilitaka nimuwahi,  kwani sikutaka mtu yoyote kumsumbua mume wangu, japokuwa nafahamu kuwa mdogo wake huyo, akijua kaka yake kalala hawezi kumsumbua, kwani anafahamu utaratibu ulivyo,japokuwa sijaonana naye muda sasa, lakini moyoni nilikuwa na hamu sana ya kuongea na huyu mtu!

‘Hii ndio nafasi pekee…’nikajisemea kimoyo moyo nikitokeza kwenye mlango.

 Sasa hivi nakuwa na tahadhari, sio kama zamani, mume wangu anaweza kunywa hizo dawa ghafla akaamuka, na akiamuka huwa hapendi kukaa ndani, anapenda kuzungushwa nje na kigari chake cha kukokotwa. Ndio maana nikaona nimuwahi mapema huyu mtu kwa tahadhari.

Nilihakikisha nimeusindika mlango nyuma yangu, na sasa nikawa naangaliana uso kwa uso na shemeji yangu huyu, alikuwa mlangoni alitaka kufungua,.. inaonekana ni kama vile hakutarajia kuniona hapo nyumbani, akabakia mdomo wazi akishindwa hata kuongea, nikatabasamu ili kumuondoa wasiwasi, na yeye kwa aibu akatizama chini..

‘Habari yako shemeji, mbona unaonekana kama umeona kitu cha kukuogofya, hukutarajia kuniona mimi hapa nyumbani nini, au una wasiwasi gani, naona unajaribu kunikwepa kinamna?’ nikamuuliza

‘Ni kweli, nilijua labda haupo, labda umetoka kwenda kazini kidogo, sasa kazi inakuwaje shemeji, …mmh, huu ni mtihani, lakini yana mwisho au sio, si kukwepi shemeji ni shughuli tu....’akasema.

‘Kuna nini kinaendelea kati yako wewe na mfanyakazi wangu?’ nikamuuliza, nilimuuliza hivyo nikiwa na maana yangu, japokuwa ulikuwa ni utani.

‘Hakuna kitu shemeji, hahaha, shemeji naye bwana, na mfanyakazi wako hakuna kitu kama hicho kabisa ...mimi nimekuja kwa ajili ya kumwangalia kaka, na kwa muda sasa sijafika, nilikuwa nimesafiri kidogo, na unajua nikiwepo basi inabidi nije, na ikibidi nikae hapa, ili nisaidie saidie,..na kiukweli mnisamehe sana, sijafika muda kumuona mgonjwa,....’akasema,

Nilimwangalia alivyokuwa akipata taabu ya kutaka kujieleza , na baadaye nikasema

‘Usijali shemeji nakutania tu, karibu, lakini kaka yako kalala na dawa anazotumia hatakiwi kusumbuliwa, unasikia sana…’nikasema.

‘Kama kalala basi …niwasalimie kidogo niondoke zangu, …nilijua nitakuta keshaamuka,..jana alinipigia simu kuwa nijitahidi tuonane…’akasema

‘Alitaka muonane mbona hajaniambia..?’ nikauliza kwa mshangao, hata yeye akaonekana kushangaa, na akasema

‘Kwakweli mimi sijui, ila alinipigia, simu, tukawa hatuelewani, mawasiliano, maana nilikuwa kwenye gari, akasema nijitahidi nionane naye…’akasema

‘Ok, labda kapitiwa kuniambia, hamna shida, ngoja tuongee kwanza

‘Ndio shemeji niambie…’ akasema

‘Unajua shemeji, wewe ni sawa na mdogo wangu, ....nakuona hivyo licha ya kuwa wewe ni shemeji yangu, ndio maana wakati wote nimekuwa nikihakikisha kuwa maisha yako yanakuwa bora, ili uweze kusimama kwa miguu yako mwenyewe, na natumai hayo yameshakamilika...na hapa ni nyumbani kwako, wakati wowote unaruhusiwa kufika, nilishangaa tu, kukuona kama unani kwepa, hasa pale hospitalini, nikajiuliza kuna nini...’nikasema.

‘Hapana sijakukwepa shemeji hizi hisia zako tu, kwanini nikukwepe..’akasema.

‘Hakuna tatizo kaka yako ana maendeleo mazuri tu, ila kuna mambo muhimu sana tunahitajika kumsaidia, …ndio najua mengi ni majukumu yangu, maana huyo ni mume wangu, au sio, ....’nikasema.

‘Ni kweli shemeji, ila kama kuna lolote la kusaidia wewe niambie tu …’akasema.

‘Usiwe na wasiwasi, sio jambo kubwa sana,..’nikasema, nikimuelekeza huyo shemeji yangu twende bustanini, kuna sehemu maalumu tumetengeneza ya kuongelea, upepo wake ni mwanana, kama upo ufukweni mwa bahari, na mume wangu hupendelea kuja kukaa hapo.

‘Tuletee vinywaji, na hakikisha kuwa mume wangu akiamuka unaniita mara moja...unasikia.’nikasema.

‘Nitafanya hivyo dada.....’akasema.


*********

‘Shemeji, nataka tuyafupishe  mazungumzo yetu iwezekanavyo, kwani kaka yako akiamuka natakiwa niwe naye karibu, kwahiyo nakuomba nikikuuliza mambo fulani fulani ujitahidi kunijibu kwa ufasaha, bila ya kuogopa....’nikamwambia.

‘Uliza tu shemeji.’akasema.

‘Ninachotaka kukuuliza ni mambo ya kawaida tu usiwe na shaka...’nikasema.

‘Sawa nakusikiliza,...lakini kama ni kuhusu kaka, mimi sijui lolote...’akaanza kwa kujitetea.

‘Usijali,....wewe utaongea tu kile unachokifahamu, sio swala la kesi au swala la kulazimishana, kitu ambacho hukijui hukijui,…ila haya yote nayafanya kwa manufaa ya kaka yako…’nikasema

‘Ni kweli….’akasema

‘Mimi,sizani kama wewe unafurahia hiyo hali aliyokuwa nayo kaka yako,  na sizani utataka hilo litokee tena, ina maana ni lazima na sisi kama tunamjali tuone tunamsaidiaje, na kabla ya hilo tujaribu kuona kama kuna sababu iliyosababisha hilo kutokea, ili lisije kutokea tena, umenielewa hapo....’nikasema.

‘Kwakweli shemeji mimi sifurahi kabisa hiyo hali, kaka na wewe ni watu muhimu sana kwangu,  wazazi wetu kama unavyowafahamu, hawana mbele wala nyuma, wewe ndiye umeisaidia familia yetu kupitia kwa kaka,sasa naogopa sana kaka asije akaondoka..sijui itakuwaje, japokuwa nimeanza maisha lakini bila ya nyie bado najiona sina uhakika wa maisha,...’akasema.

‘Basi kama unafahamu hivyo ni vyema, tukamsaidia kaka yako, kwani japokuwa kiafya anaendelea vyema, lakini mpaka sasa sijajua ni nini kilichomfanya hadi afikie hapo, je ni jambo la dharura tu, au kuna jambo jingine ambalo huenda bado lipo, na kama lipo ni nini, ,..’nikasema na hapo akakaa kimia tu.

‘Unaposema hivyo shemeji unahisi kaka kapatwa na hiyo ajali kutokana na jambo fulani au, mimi nilijua kuwa ni ajali ya kawaida tu, ambayo anaweza kupatwa mtu yoyote’ akasema.

‘Ajali ni ajali ndio, lakini kuna ajali inakupa maulizo mengi kutegemea ilivyotokea, ndio maana nataka nikuulize wewe ambaye muda mwingi akirudi kazini, au…ikitokea dharura mnakuwa naye,…’nikasema.

‘Shemeji mimi sio kwamba mchana kutwa nakuwa naye, unafahamu hilo, kwani hata mimi ninakuwa kwenye mishe mishe zangu,... na mimi najaribu kutafuta jinsi ya kusimama mwenyewe... wakati mwingine huwa nafanya kazi za kaka, lakini sipendi mimi nifanye kazi  kwenye ofisi yake, kama tulivyowahi kuongea..’akasema.

‘Ni kweli, sasa turejee kwa kaka yako, tumsaidie, kuna onekana kuna tatizo, na hueda tatizo hilo lipo nje…kuna kitu kinamsumbua, na huenda kakuitia kwa hilo, kaka yako hatakiwi awaze sana, ndio maana najitahidi kuchuja kila jambo, unanielewa, sasa hebu uwe muwazi kwangu, hajakuambia anakuitia nini, au huna fununu ya jambo fulani…’nikasema

‘Nijuavyo mimi , biashara za kaka, huko kazini zilifikia kubaya, hakuna wateja, ..na ikawa watu hawalipo madeni, kwahiyo na yeye akawa hawezi kulipa madeni, hilo likawa linamsumbua sana, na mara nyingi ananituma kwa wateja wake kufuatilia madeni, labda ndio hivyo…’akasema

‘Unaona vitu kama hivyo mimi nilikuwa sijui, haniambii,..’nikasema

‘Kaka huwa ni msiri sana, hata akiwa na shida hapendi kusema huwa anapambana kivyake, hata mimi nilimshauri akuambie akasema hawezi, atapambana kivyake, kwahiyo sijui, zaidi…ila nilisikia siku moja akilalamika kuwa watu wanaomdai, wanataka kufungua mashitaka…’akasema

‘Unawafahamu kwa orodha…?’ nikauliza

‘Kwa kichwa hapana, ila ukitaka ninaweza kukutafutia huko ofisini…’akasema

‘Hilo liache kwanza, je hakuna kitu kingine umesikia, akilalamika au…ni kwanini akatokea kunywa pombe sana…?’ nikamuliza

‘Shemeji mimi nijuavyo, na aliwahi kuniambia ni sababu ya mawazo, amekuwa kwenye wakati mgumu na nahisi anaona kama hana mtu wa kumliwaza vile, ni yeye na kazi yake, na anaogopa kusema kashindwa, ,….nahisi ni hivyo shemeji..madeni, na…sijui, kama kuna tatizo jingine mimi siwezi kufahamu…’akasema

 ‘Unavyosema hivyo..kumliwaza.., ni kama vile aliwahi kulalamika, kama unavyosema anahisi hana mtu wa kumsaidia, mimi si nipo mkewe jamani,je hujawahi kusikia akilalamika mbele yako, kuwa kuna tatizo analipata dhidi yangu?’ nikamuuliza.

‘Shemeji hapana, lakini mimi nimeishi na nyie, kwahiyo mengine nayafahamu, wakati mwingine nilikuwa natamani kuwa kama nyie wachapakazi, mkirudi nyumbani hamna muda wa kuongea ni kazi tu….’akasema

‘Naomba uniambie waziwazi, nitafurahi sana ukianiambia ukweli, kuwa labda katika maisha yetu uligundua kasoro fulani, maana wewe tumeishi nawe, ukisoma mpaka ukapata kazi, niambie ukweli shemeji,kuna jambo gani tunakosea, au mimi nimekosea mpaka namkwaza kaka yako?’ nikamuuliza.

‘Mhh, shemeji mimi sioni walakini ndio maana nasema natamani niwe kama nyie, lakini kwangu ukifanya hivyo mke ataanza kulalamika, unanielewa hapo, wake zetu sisi, kisomo kidogo, ukiwa nyumbani wanataka usifanye kitu, uwe unawasikiliza wao, ukishika simu ugomvi, uki..ndio hivyo,…mimi hata laptop naogopa kwenda nayo nyumbani….’akasema

‘Ina maana kumbe labda hata kaka yako yupo hivyo, kuwa labda alikuwa hapendi hali hiyo ya mimi kuwa na kazi hata nyumbani, lakini hata yeye alikuwa akifanya hivyo au sio…’nikasema

‘Kiukweli, nyie mnaishi kama wazungu, ..sizani kama kaka anaweza kulilalamikia hilo, mimi sijui kabisa…’akasema

‘Kwahiyo kwa uoni wako, kaka yako …hiyo ajali haijasababishwa na jambo fulani,, unavyohisi wewe…?’ nikamuuliza

‘Yaweza ikawa na sababu kwa jinsi nilivyosikia kuwa aliendesha kwa mwendo kasi, na kaka hana tabia hiyo ya kuendesha gari kwa mwendo kasi, ndio maana wengi wanahisi kulikuwa na jambo zito.., hata mimi mwenyewe nimejiuliza sana hilo swali, lakini ajali ni ajali tu shemeji…’akasema.

‘Kwahiyo wewe unahisi tatizo la kaka yako ni madeni na sio labda kuna mataizo ya kifamilia, labda, kitu kama hicho...?’ nikamuuliza.

‘Inawezekana kuna tatizo nje, mimi na wewe hatulijui, lakini kwa uoni wangu mdogo, nahisi kama alikuwa na msongo wa mawazo, kwanza madeni, pili nahisi alihitajia mtu wa karibu sana wa kuyaondoa hayo mawazo ya kazini, lakini wewe upo, sijui kwanini hakutaka kukushirikisha, na sijui zaidi shemeji…’akasema

‘Hapo sasa unaanza kusema ukweli…kuwa pamoja na yote hayo, nahisi ananiona kama sipo karibu naye sana, anaogopa kuniambia, ataonekana mdhaifu…’nikasema

‘Sawa sawa shemeji…’akasema

‘Kwahiyo akaanza kunywa, kuondoa mawazo…’nikasema

‘Sawa sawa shemeji…’akasema

‘Na ulevi, nisikiavyo, raha yake uwe na wenza, marafiki, wa kike na wa kiume mnakunywa mnacheka, au sio…’nikasema

‘Ndio hivyo hivyo…’akasema

‘Na kaka yako ni binadamu au sio, na ni mwanaume au sio, ni lazima akiwa anakunywa alikuwa na marafiki, anakunywa nao ..au sio…?’ nikauliza hapo akasita halafu akasema

‘Yawezekana…ndio anakuwa nao, ni kawaida hiyo…’akasema

‘Na marafiki wanaweza kuwa wa kike na kiume na wewe unawaona , sema ukweli wako, kumbuka, tunaongea ili kupata namna ya kumsaida kaka yako…’nikasema

‘Ni sawa shemeji, kwnye kunywa hivyo vipo, na nijuavyo kaka pia alikuwa na marafiki zake, na wakati mwingine ndio, wanakuwepo wanawake…’akasema

‘Na wengi ni wale wa mara kwa mara ..au sio, maana ni lazima mzoeane, huwezi ukawa na marafiki wa siku moja moja, au sio,…?’ nikauliza

‘Ni kweli shemeji, ni wale wale marafiki zake….’akasema

‘Sasa nataka tu kuliweka sawa, hao marafiki zake, nimeshawafahamu, yupo docta,..yupo wale wafanyakazi wenzake, wapo wale majirani wake wa kazini, na wanawake ni nani na nani…?’ nikauliza

‘Mhh…mara nyingi,..wapo, lakini anayekuwa karibu naye ni…unamfahamu shemeji, ni yule…yule mdada rafiki yako, na wanawake wengine ni wapenzi wa marafiki zake,…’akasema

‘Kuna kipindi analewa kupitiliza…au sio…?’ nikauliza

‘Ndio, hilo siwezi kukukatalia, hata yeye hawezi kulipinga…’akasema

‘Na kuna muda aliwahi kulala nje, kwasababu ya kulewa sana…’nikasema

‘Mhh..shemeji…lakini mimi namchukua na kumleta nyumbani…’akasema

‘Haijatokea nyie mkalala nje na mkaja karibu na asubuhi..au yeye akaja karibu na asubuhi..?’ nikamuuliza

‘Mmmh labda kukiwa na sherehe…’akasema

‘Lakini ilishatokea au sio..?; nikauliza

‘Kiukweli….eeh, ndio ilishatokea…’akasema

‘Na muda mwingine huyo mdada rafiki yangu alikuwepo…?’ nikauliza

‘Sio muda wote..inatokea tu, na mara nyingi huyo mdada anaondoka mapema..’akasema

‘Na ile siku mlichelewa, mkawa mumelewa mkaenda kulala kwa huyo rafiki yangu je,ilikuwaje..?’ nikamuuliza hapo akashtuka na kusema;

‘Shemeji, …siku zile, hahaha, nani alikuambia,..ndio..lakini sio kulala, kaka yeye aliondoka, unajua ilikuwaje, tulipotoka kule tukampitisha shemeji kwake, mara kukazuka maongezi, akatukaribisha kwake,..ujuavyo pombe hatukuangalia muda, wengine wakajikuta wamelala kwenye sofa…’akasema

‘Yeye ndiye aliwakaribisha, au sio…?’ nikauliza

‘Ndio, …na muda huo kaka kalewa, akawa naye anakubali haraka, …basi tukaingia kwake, tukaendelea kunywa, kuongea, wengine usingizi tena,…lakini kaka aliondoka…’akasema

‘Kaka yako aliondoka, wew ukabakia na rafiki yangu, mkalala naye hadi asubuhi si ndio hivyo…?’ nikauliza

‘Ilibidi mimi nibakie, kwa maaagizo ya kaka, kuhakikisha, kuna usalama, ndio sababu hiyo, sio vinginevyo shemeji, na asubuhi aliponiona huyo mdada akanifukuza…’akasema

‘Huyo mdada alilewa hajitambui, na wewe ukachukua nafasi hiyo kufanya ulichodhamiria siku nyingi ni kweli si kweli, usinidanganye nimeshafahamu kila kitu..’nikasema

‘Hahaha, shemeji bwana, hakuna kitu kama hicho, kaka angeniua, hapana..’nikasema

‘Kwanini kaka yako akuue…?’ nikauliza

‘Unajua tena shemeji, yule ni sawa na wewe, hatafurahia kama nitafanya jambo baya dhidi yake…’akasema


‘Na hiyo hali ya kwenda kulala kwake, sio mara moja ni zaidi ya mara moja au sio..?’ nikauliza

‘Mhh, kama mara mbili, au tatu, sikumbuki vyema…’akasema

‘Kaka yako hakuwahi kuingia kulala na rafiki yangu..?’ nikauliza hapo akashtuka na kusema

‘Ha-hapana shemeji…mimi sijui , sikuwahi kuona, ..unajua anamuheshimu sana yule mdada, sizani, mimi hapo siwezi kuwa na uhakika…’akasema

‘Mdada ana mtoto, na nikuulize tangia ajifungue uliwahi kwenda kumtembelea huyo mdada..?’ nikamuliza

‘Hapana shemeji, mimi na yule mdada hatuivani sana, inatokea siku na siku akiwa na shida zake ndio ananiona wa maana, vinginevyo, sina habari na yeye kabisa…’akasema , mara nikahisi sauti kama ya watu wanaongea, nikatega sikio, kukawa kimia, nikaanza kuingiwa na wasiwasi, mume wangu asije akawa kaamuka

‘Hebu kidogo…’nikasema na kusimama kusikiliza, nilikuwa sijamalizana na huyo mtu, nikasema

‘Sasa sikiliza shemeji…, mimi ninakupa wewe muda wa kuyatafakari haya kwa makini, nataka uniambie ukweli, kuhusu mahusiano ya mume wako na rafiki yangu, je kaka yako hana mwanamke mwingine yupo naye karibu..?’ nikamuliza

‘Mhh..mimi simfahamu…’akasema

‘Sasa  nitaongea na wewe tena kesho, lakini sio hapa nyumbani, nataka tuyaongelee haya na mengine tukiwa wawili, nataka uniambie ukweli, unasikia, kwa manufaa ya kaka yako, unanisikia,....’nikasema.

‘Shemeji hamna tatizo kabisa , lakini yote nimeshakuambia, ..sizani kama kuna jambo ninalolifahamu …’akasema

‘Nimefurahia sana maongezi yako ya leo, hatujawahi kukaa na kuongea hivi, ukaniambia ukweli kutoka moyoni mwako,,..nimefurahi sana, na wakati wote ninakuona kuwa ni mtu mwema, unayejali, wale wanaokujali, nimefurahi sana...sasa ili kulihakiki hilo, nataka tena tuongee, kuhusu rafiki yangu, unajua mtoto wake anafanana sana na wewe…’nikasema.

‘Eti nini, anafanana na mimi, hapana shemeji, sio kweli, haiwezekani sio kweli….’ Akasema na kushtuka, na muda huo simu yake ikawa inaita lakini hapokei ni kama kachanganyikiwa fulani.

Na muda huo nikasikia sauti ya wazi, kuwa mfanyakazi wangu anaongea na mtu ndani, nikajua mume wangu ameshaamuka kwahiyo mimi kwa haraka nikawa nakimbilia huko ndani, na nilimuona shemeji akisikiliza simu na huku anatoka nje....

**************

Nilifika ndani na kukuta kupo kimia, na wakati nataka kwenda chumbani ndio nikasikia watu wakiongea nje, nilipochungulia nje kwa kupitia dirishani nilimuona yule msaidizi wangu akiwa anasukuma kile kigari cha mume wangu, na mume wangu akiwa kakaa na alikuwa kaegemeza kichwa huku kashika shavu, a macho kayafumba kama lasinzia,  hiyo ilikuwa ni dalili, kuwa alikuwa na mawazo.

Kumbe mfanyakazi alimchukua mume wangu na kutoka naye nje wakati tunaongea na shemeji yangu,inaonekana mume wangu aliamuka akanikuta sipo na wakati huo mfanyakazi wangu alikuwa anafanya usafi, au….mume wangu alisikia yupo akamuita, na akamuambia amtoe nje

Niliwaangalia, na mfanyakazi alikuwa akikisukuma kigari huku na kule ndivyo anavyopenda mume wangu, kufanyiwa hivyo, hataki kukaa sehemu moja kwa muda mrefu.

Kwanza nikaingiwa na wasiwasi, nikijiuliza huyu mtu alitoka muda gani, isije ikawa,walifika hadi kule bustanini, wakasikia maongezi yetu na shemeji yangu,kitu ambacho muda wote nilikuwa nikikikwepa, nikaona nithibitishe hilo, nikafungua mlango na kutoka nje,....

Mume wangu alipoisi kuna mtu anakuja akafungua macho na aliponiona akajitahidi kutabasamu, lakini lilikuwa tabasamu la kujilazimisha,  kwanza aliniangalia machioni, mimi nikatabasamu, yeye akabenua mdomo, ila ya dharau au kujifanya anajua jambo

‘Mume wangu samahani, nilikuwa na mgeni nikakuacha chumbani peke yako..’nikasem

‘Mdogo wangu kashaondoka, mbona hajanisalimia, nilitaka kuongea naye.....’ akasema

‘Ndio kapigiwa simu ya haraka, labda atarudi baadae lakini kwanini hukusema , kuwa umeamuka, nije, huyu mfanyakazi sio kazi yake hii, hii ni kazi yangu,..’ nikasema

‘Unajua upepo, na hali ya bustanini ni kama dawa kwangu nilipoamuka tu, nikaona haupo nikajua umetingwa na jambo, nikamuambia mfanyakaz anisaidie nitoke nje,..na wakati natoka ndio nikawaona mnaongea, nikaona nisiwasumbue, ….’akasema

‘Hutusumbui bwana…yule ni ndugu yako na mimi ni mke wako, wote tunawajibika kwako...’nikasema

‘Aaah, ni kweli, lakini na mimi ni binadamu, nakuonea huruma, na…..yawezekana na wewe ulikuwa unatafuta njia za kunisaidia nipone haraka, na mimi nataka kupona haraka, au sio…’akasema na kunifanya nihisi kuwa huenda alisikia jambo.

‘Mume wangu na wewe siku hizi una maneno, …’nikasema

‘Mke wangu hata mimi sijui yametoka wapi,..ila mengine uwe unaniuliza mimi mwenyewe nitakuambia kila kitu, usiogope kuniuliza mke wangu…nakupenda sana mke  wangu usije kuniacha, ukiniacha na mimi nitaicha hii dunia ya mateso,..naumia mke wangu, kweli hujafa hujaumbika…’akasema kwa unyonge

‘Mume wangu kwanini unaongea hivyo…?’ nikauliza

‘Najua na wewe unajua, kuwa nimekosea sana, na kiukweli mke wangu, mengine tuyasahu tu, tusonge mbele, ukiwasikiliza sana wazazi wako tutaharibu kila kitu, kiukweli mimi najua nimekosea wapi, na mimi kwa hali kama hii, nimepata fundishi kuba sana, na kwahiyo naahidi sitarudia tena, najua kazini kupoje lakini najua jinsi gani ya kupainua tena, hata bila ya msaada wa baba yako…’akasema

‘Hayo usiyawazie sana mume wangu…muhimu ni wewe kupona, muhimu ni afya yako, ukiyawazia hayo hutapona, na kazi zipo tu, muhimu ni afya yako…’nikasema

‘Kupona kwangu ni pamoja na kufahamu kuwa wewe upo na mimi na kamwe hutaweza kuniacha…hata iweje ..lakini najua nipo kwenye kuti kavu, kwa hali kama hiyo nitawezaje kupona…, mawazo yataishaje, wakati najua kupona kwangu ni kuingia kwenye jela nyingine ya sintofahamu, najua yote hayo, baba yako, anasubiria tu, nipone, au sio…’akasema.

‘Sikiliza mume wangu…’nikasema

‘Nisikilize nini bwana,..hata ujifanye vipi najua, wewe na baba yako mpo kitu kimoja, najua..rafiki yako kaharibu kila kitu najua…lakini itasaidia nini kwa sasa, ila nikuambie ukweli, mimi nikiwa hivi miaka nenda rudi, na kama nitaendelea kuteseka hivi, aah, kwanini bwana niwasumbue watu…’akasema

‘Mume wangu hayo yametokea wapi, tulishaongea ukasema utajitahidi ili upone haraka…’’nikasema

‘Yaaah…nitapona haraka, …ili niingie kwenye kizima cha kesi, …unajua baba yako anatamani sana, ukaishi na watu kama docta, sio watu kama mimi, kwahiyo anatafuta kila namna, ndio maana alinitega, nimeliona hilo kwenye ndoto, na..mke wangu nasema hili kwako, kama ni hivyo, sawa, lakini utanikumbuka, labda, nikiwa huko kuzimu…’akasema na kuanza kusukuma kigari kuondoka.

‘Mume wangu…unaongea nini sasa..’nikasema lakini huyoo akasukuma kigari kuelekea ndani. Na muda huo nikahisi kichwa kinaniuma ni hiyo ni dalili mbaya kwangu…

NB: Kwa leo inatosha ....



WAZO LA LEO:Katika maisha yetu ya ndoa, na katika maisha yetu ya kila siku, tujifunze kuwa wakweli, kila mmoja amwamini mwenzake , awe mkweli kwa mwenzake....kwani, ukweli wakati wote, ni kinga ya uhasama,...japokuwa kuna wakati mwingine inatulazima kukwepa kusema ukweli kwa maana fulani, ili kukwepa madhara..tukihisi tunafanya hivyo kwa nia njema….lakini kama tukianza hivyo kusema uwongo, kidogo kidogo hujenga mazoea, na tutajikuta tunahasimiania, unafiki unatawala nafsi zetu..kwa vyovyote iwavyo, tujifunze kuwa wakweli kwa wenza wetu, ili kujenga uaminifu, upendo na furaha na kujenga familia zilizo bora
Ni mimi: emu-three

No comments :