Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, November 21, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-28



Siku kadhaa zikapita na mume wangu akatakiwa kurejeshwa nyumbani, na kabla ya kurejeshwa nyumbani, docta aliyekuwa akimuhudumia, akaniita ofisini kwake, na kunishauri mambo mengi ili kuhakikisha mume wangu anaondoka kwenye hatari na kupona mapema.

'Unasikia wewe ni mke wake, na mtu muhimu kwake, wewe ndiye utamfanya apone haraka au....unasikia, muhimu tena sana,jitahidi kuwa karibu sana na mume wangu, na kukwepa kauli yoyote ya kumkwaza...unasikia...'akasema docta akinisisitiza hilo sana

'Nakusikia docta...'nikasema

'Mume wako, yupo kwenye hali ambayo akipata mshtuko tu inaweza kuzua tatizo kubwa ambalo litamfanya ashindwe kutembea kabisa....na ukijitahidi akawa hana mawazo, mazoezi...na kufuta masharti nilikuambia awali, ...atapona haraka tu...'akasema docta

‘Sawa docta mimi nitajitahidi kadri ya uwezo wangu, maana huyo ni mume wangu, sina jinsi…ila nimegundua kitu, hivi sasa ni mbishi sana, na  ubishi huu hakuwa nao , nahisi  umeanza baada ya hili tatizo, kila kitu anataka nimsikilize yeye tu, sasa sijui nikiwa naye huko nyumbani itakuwaje...’nikasema.

‘Ndio hivyo, jitahidi uwezevyo, kama kweli unamjali mume wako na unataka apone haraka, basi acha kila kitu kwa ajili ya mume wako …’akasema docta

'Sawa docta...'nikasema

Kabla ya kuondoka hapo hospitalini baba akanipigia simu, baba siku hizi amekuwa kila mara akinipigia simu , hasa baada ya kushuhudia  nikipoteza fahamu hapo hospitalini, tukio hilo limemfanya awe karibu na mimi, kuliko alivyokuwa baada ya mimi kuolewa..;

‘Vipi hali yako na ya mume wako…?’ akaniuliza

‘Hajambo jambo, kama walivyokuwa wamesema leo tunaweza kuondoka naye…hapa tu, tupo nje tunataka kuondoka kurudi nyumbani..’nikasema

‘Ok, vizuri…sasa ok, naaah, umefikiriaje wazo langu..?’ akaniuliza kwa lugha ya upole, sio tabia ya baba akiongea na mimi, hasa nilipolazimisha kuolewa na mume ambaye hawamtaki.

‘Baba mengine yasubirie kwanza, ngoja nibebe hili jukumu la mume wangu maana nimejitakia  mwenyewe, na sihitajii msaada kwenu baba, nitajimudu mwenyewe…’nikasema

‘Usiwe mkaidi kwa hilo, hilo ni tatizo kubwa sana, kama unafikia kupoteza fahamu, sio kitu kidogo hicho, sisi wazazi wako hatuwezi kukaa kimia, na mama yako atakuja akae nawewe, tuone jinsi gani ya kukusaidia, unasikia…’akasema

‘Baba hapana, mama mwenyewe mbovu, tutazidi kumchosha tu bure, nakuomba hilo liacheni kama lilivyo, ikibidi nitawaambia…’nikasema

Kila nikiombea na baba ni lazima akimbilie kwenye lawama, akasema;


‘Nilishakuambia huyo mwanaume hakufai, atakuhangaisha mwishowe atakuepeleka  kubaya, utaumwa, unaweza hata kupooza mwili, mwishowe  utaingia kaburini, wenzako wanastarehe..kitu ambacho kinatuuma sana sisi wazazi wako...'akasema

'Baba...'nikataka kujitetea lakini hakunipa nafasi akaendelea kuongea

'Nikuambie ukweli mume wako halijali hilo, la afya yako,... yeye anachojali ni masilahi yake tu, na anataka akukamue mpaka basi,..na sasa hivi utayaona  hayo, hatukuombei mabaya, lakini yale tuliyowahi kuyasema sasa utaanza kuyaona kwa macho yako,..huyo mume wako atakusumbua sana...'akasema

'Baba lakini ni mume wangu...'nikasema

'Sawa..ni mume wako,....ngoja tuone itakavyokuwa,….ila ukikwama usiache kutuambia, mimi nitajitahidi kufika kwako mara kwa mara, kulifuatilia hili mimi mwenyewe…’akasema

‘Baba nashukuruni kwa kunijali, lakini nakuomba usisumbuke sana kwa ajili ya hili, sasa hivi mume wangu anaumwa, na naona akikuona wewe anakuwa hana amani, kwa hivi sasa, anahitajia, huruma, na baba sio kwamba sitaki ufike, ila ukifika naomba sana baba usije kuzungumza maneno ya kumweka kwenye wakati mgumu, ongea naye maneno ya kumfariji, asiogope, kama alivyotushauri docta...’nikajaribu kumtetea.

'Hilo sio la kunifundisha, nafahamu sana,...muda utafika nitapambana naye, sio sasa..usiwe na wasiwasi kwa hilo...'akasema

'Nashukuru sana baba...'nikasema

‘Ila kuna kitu nataka uniambie, siku ile nilipofika hospitalini nilisikia akiongea maneno, kama anakuomba msamaha, na akasema kitu kama  wewe ulikuwa humjali kitu kama hicho, sikusikia vyema, alikuwa akiongea nini..?’ baba akauliza

‘Baba , ....mgonjwa alikuwa anaongea hivyo ni katika hali ya kuchanganyikiwa tu, kwasababu ya huko kuumwa, yeye alijiona kama ni mtu wa kufa tu, kwahiyo ndio akawa anajaribu kujitakasa, akihisi hili kakosea, basi anaomba msamaha, hata wewe ungelikuwepo angalikuomba msamaha ni katika kuhangaika tu baba…’ nilisema sikuelewa baba alisikia kiasi gani, na docta akawa anaongea baadae akasema

‘Vyovyote iwavyo mimi  nataka maelezo,..najua kakuoa akiwa na malengo yake binafsi,..yeye kama hawezi kuishi na binti yangu labda ana mipango yake mingine au alikuwa na ndoto zake nyingine , basi awe muwazi tu, nimegundua mambo mengi ambayo hayafai kwa familia yangu…’akasema

‘Baba mengine ni ya kuharibu bora tuyapuuze tu..’nikasema

‘Sikiliza…anyway,a sitaki nikuumize kwa mawazo, hayo ni yake anatakiwa kuwajibika nayo, sasa.. ngoja apone, sawa poleni sana binti yangu, usijali mimi nitapambana na hili jambo mpaka nione mwisho wake, unasikia, usijali, nipo pamoja na wewe,  …’akawa anaongea hivyona kipindi hicho ndio nimepata fahamu.

‘Baba, usiwazie hivyo…mengine yametokea tu, ile iwe sababu ,  mimi nina imani yatakwisha tu, ni sehemu ya changamoto za maisha, sasa nyie kama wazazi wangu sitaki mnitenge mimi tofauti na mume wangu, ….sipendi hivyo baba…’nikasema


‘Binti yangu usione nasema hivyo, sisi wazazi wako tunakupenda sana, lakini tunaumia, tunajitahidi kadri tuwezavyo ili uondokane na shida hizi, lakini wewe unakuwa mkaidi, sisi tunafahamu tatizo lipo wapi, hich ni kizalia , asili ya hulka ya mtu, hutaweza kumbadili mume wako, abadani…’akasema na mimi nikataka kuongea lakini hakunipa nafasi, akasema

‘Mengi tunayaona lakini hatusemi, lakini kwa hili, hapa lilipofikia, sisi kama wazazi tutalifuatilia mpaka tuone mwisho wake ni nini, ina maana gani ya ndoa eeh, niambie…, na kama nilivyosema awali, sitaki kashfa katika familia yangu…, na  anyway, wewe angalia afya yako, unasikia, kama kuna lolote linahitajika niambie….’alisema .

 Na leo ndio akanipigia simu akitaka kujua mimi nimefikia wapi, kwani anahitajika kutoa maamuzi kwenye kikao cha wakurugenzi, ..anasema hicho kikao ni muhimu  , hata kama mimi sitakuwepo au mume wangu, maamuzi ya wengi yataheshimiwa.

‘Baba mimi naomba usifanye lolote kwenye kampuni ya mume wangu, utoe hija kuwa kwa upande wa hiyo kampuni tusubirie kwanza, …itakuwa sio vyema, hata kama inafirisika, …na madeni yabakie tu, kama wadaiwa wanataka kushitaki waache tu wafanye hivyo, tutapambana huko mahakamani…’nikasema

‘Sio rahis hivyo binti yangu…mimi kama mwenyekiti wa makampuni yote, siwezi kukubali hali hiyo ifikie huko, kuna wakurugenzi wa hisa kwenye hiyo kampuni, wananihoji,…wamewekeza pia huko, unataka niwaambieje…wewe sikiliza, wewe endelea na mume wako, mengine niachie mimi, ninajua ni nini cha kufanya, unasikia eeh,…tuliza kichwa chako, ila mume wako akipona nataka nipambane naye mimi mwenyewe, …hilo sitaki majadala…’akasema

‘Baba…’nikalalamika

‘Kwahiyo leo mimi sitakuja huko , nitakuwa na kikao, na nitakuwa napitia taarifa za uchunguzi, kuhusu mume wako, kuna mengi yamegundulikana, lakini mengine sitaki yawepo kwenye hiyo taarifa, ni aibu, uliweza kuisoma ile taarifa niliyowahi kukupatia ile kila kitu kipo, na mengi ambayo siamini...hebu nikuulize kwanza huyo rafiki yako kwanini kasafiri na mtoto mchanga..?’ akaniuliza

‘Ilibidi afanye hivyo kwa vile muhula wa masomo umeanzia hapo, na hakutaka kusubiria, tukaona ni bora tu aende….na huko kuna watu watamsaidia hatapata shida…’nikaongea kujifanya na mimi nimehusika kwenye maamuzi ya rafiki yangu kuondoka.

‘Una uhakika,…??... sio kuwa kakimbia,…?? anaogopa ukweli ukija kugundulikana awe keshajipanga vyema kimaisha, binti yangu hao watu wanakutumia vibaya, huyo rafiki yako, anataka ahakikishe hata likitokea jambo awe anajiweza mwenyewe..sawa sio mbaya, lakini kwanini aharibu nyumba iliyombeba..’akasema

‘Baba hayo mengine hata sitaki kuyafikiria kwanza,…’nikasema

‘Sawa sawa, usijali…nitapambana na hao watu mimi mwenyewe, ilimradi…’akasema na kukata simu.

**********

Mume wangu akawa hataki mimi niondoke karibu yake , ikawa ni kero, ina maana nisitoke au kwenda mbali na yeye, hata akija mgeni, anataka atoke awe pembeni nikiongea na mgeni,..kwa maagizo ya docta nikawa nafanya kila atakavyo, ila moyoni, pamoja na huruma kila nikiwazia hayo yanayosemwa nilimuona mume wangu kama sio yule ninayemfahamu.

 Nilitaka niwe na nafasi ya kuipata ile taarifa aliyotayarisha rafiki yangu, lakini sikutakiwa nisome mbele ya mume wangu,..ikafika muda nikaagiza niletewe  hiyo taarifa nyumbani,…lakini muda gani wa kuisoma nikawa sina,

Ikatokea siku moja mume wangu amelala kutokana na madawa nilikuja kugundua akinywa hizo dawa anaweza kulala hata saa nzima au zaidi..na siku hiyo ilipoletwa hiyoo taarifa ya rafiki yangu, nikaona nitumie huo mwanya..., ndio nikaanza  kuipitia hiyo taarifa ni ndefu kidogo...;

Taarifa ya uchunguzi wa ajali ya mume wangu, aliandika jina la mume wangu, na akaelezea ilivyotokea, kuwa ni sababu ya mwendo kasi, katika kukata kona akakutana uso kwa uso na lori,..akajaribu kulikwepa, na gari likapinduka na kugeuka mara mbili…
Dereva aliwahi kutoka, hapo haijulikani aliwezaje kutoka katika hali hiyo, ni kwa uwezo wa mungu tu.

Je kipindi ajali hiyo inatokea mlengwa alikuwa katokea wapi, taarifa inasema alitokea kazini, akapitia sehemu za wateja wake, ndivyo alivyoaga kazini, lakini akiwa kwa wateja wake, akaamua kwenda sehemu nyingine …(yawezekana,) akaandika hivyo na kuzungushia hayo maneno,...

Kuna kauli za watu kuwa kwa muda huo ndio alimua kwenda kumuona mzazi,  huyo mzazi ni nani, (bado sijamtambua)!.

 Hili la mzazi halina uzito, ila limetokana na maelezo ya siku kadhaa nyuma kuwa aliondoka kazini akisema anakwenda kumuona mzazi, hospitalini, huyo mzazi hospitalini hakuweza kugundulikana ni nani..(kwahiyo ili kupata jibu kamili, aulizwe yeye mwenyewe)!

'Ssshti...'nikajikuta nikisema hivyo.

Kabla hajapatwa na ajali, gari lilisimamishwa kwenye geraji, sehemu ambayo pia panaoshwa magari kwa pembeni yake..., na wakati gari lake linafanyiwa usafi, yeye alikwenda mgahawani, kupata chochote,..lakini hakunywa kilevi…akiwa hapo, inaonekana alipokea simu , ya haraka, na kutoka hapo akaenda kulichukua gari kuwa muosha magari,

Muosha magari anasema ni kweli, aliwahi kuosha gari la mtu huyo, na ...hata la mdogo wake, na anachokumbuka, yeye, mlengwa,  aliondoka hapo  kwa mwendo wa kasi, lakini sio kasi kubwa, kama ilivyokuwa huko alipopatia ajali... ila alionekana ana haraka, hata chenji ya pesa yake hakuichukua.

Kwahiyo hapo akahitimisha kuwa,.simu aliyopigiwa inaonyesha ilikuwa na jambo, la kumfanya aharakishe kufika nyumbani na sivyo kama watu wanavyosema kuwa huenda alikuwa akikimbia jambo la hatari, hata hivyo bado haijafahamika simu hiyo ilitoka kwa nani, na kwanini aliharakisha hivyo (haijafahamika bado). Na huyo aliyefika kwake ni siri yake...akaandika hivyo!

‘Hii taarifa haina maana kabisa..’nikasema ni kuiweka pembeni.

Na wakati nawazia hiyo taarifa : huyo mzazi  ni nani huyo au ni nani huyo alimpigia simu mume wangu na kumfanya awe na haraka kihivyo, ndio akaja docta rafiki, akanikuta nipo kwenye mawazo, akaniuliza kuna nini kimtokea…

‘Mambo ya kazi tu…na nilikuwa naipitia ile taarifa aliyoacha rafiki yangu, lakini hakuna alichokifanya, sio kawaida yake, ni taarifa ya mtu ambaye hajui kazi kabisa, sio yeye aliyeitayarisha…’nikasema

‘Hiyo taarifa ina muhimu gani kwako kwa hivi sasa…?’ akaniuliza

‘Bado nawajibika kuufahamu  ukweli, najua baada ya hili, mume wangu akipata nafuu, nitahitajika kukaa kikao na baba, na wawekezaji wengine, kuna maswali mengi nitaulizwa, nitayajibu vipi kama siufahamu ukweli..’nikasema

‘Ukweli kuhusu mumeo au ukweli kuhusu maswala ya kikazi…ama kuhusu mume wako yeye alishakuambia kila kitu, sasa kama hayo yanaweza kuingiliana na kazi yake, ni jambo jingine linaelezeka... kwa hivi sasa mimi siioni kwanini unabeba mzigo kabla haujatua kichwani mwako…utachoka hata kabla hujahisi uzito wake, tulia kwanza..’akasema

‘Unajua siwezi nikaamini yale aliyoongea mume wangu moja kwa moja, na hakuwahi kusema ni kitu gani alikifanya, mpaka afikie kuniomba msamaha..tunahis tu..pale aliongea akiwa kachanganyikiwa, sawa yawezekana ni hilo kuwa kafanya madhambi…lakini mbona taarifa ya rafiki yangu haijabainisha hilo. Sawa naweza kuhitimisha hivyo kuwa ni kweli, labda ni kweli, je hilo latosha tu, hapana ni lazima niwe na ushahidi....’nikasema

‘Nikuambie kitu hiyo taarifa ya rafiki yale lengo lake ni kuvuta muda, kuhakikisha kuwa anakuchanganya ili yeye aweze kutimiza haja zake,..na huyo mzazi mume wako aliyewahi kuaga kuwa anakwenda kumuona, sio mwingine ni huyo huyo rafiki yako, amini usiamini huo ndio ukweli….’akasema docta

‘Sawa, tunaweza kusema ndivyo hivyo, haya nipeni ushahidi, hapa anasema mdogo wake siku hiyo alifika pia kuosha gari,...swali gari lipi, na muda gani, hajaelezea hapa…kama kweli ni yeye, maana kama ni kweli, basi, huyo sio rafiki yangu ninayemfahamu mimi...'nikatulia kidogo.

'Mimi sio mjinga wa kukataa kauli za watu...najua nahisi hata mimi hivyo hivyo, ….lakini siwezi kukubali hivi hivi tu, na kuchukua hatua hiyo kubwa niliyodhamiria moyoni, maana ni kweli nitafanya hivyo,...je nichukue haua hiyo bila ya kujirizisha, ushahidi, upo wapi, unanielewa hapo,…au wewe unao huo ushahidi.?’ nikauliza

‘Kwasababu rafiki yako anajua kafanya makosa, anajua yeye alishirikiana na mume wako kulifanikisha hilo, ...'akasema

'Ushahidi...'nikasema

'Ndio tunaweka nadharia hii sawa,...kuna kitu nataka unielewe, kuwa huenda rafiki yako, alipanga hivyo, au kuna kitu kilimsukuma kufanya hivyo, na kitu hicho akakitumia kama ngao yake, lakini yanayokuja kutokea sasa imekuwa kinyume na alivyotarajia, ndio maana kaamua kukimbia ili kuepusha shari, naanzia hapo…’akasema docta.

‘Mimi nataka ushahidi maana baada ya huo ushahidi, mimi nitachukua hatua kali, hutaamini, na sitaweza kurudi nyuma kwa hilo..bila kujali ni nani, sitak nadharia za kuhisi hisi, wewe ni docta, au... …’nikasema

‘Sasa hebu nikuulize utachukua hatua kwa nani,  kwa mumeo au kwa huyo rafiki yako...maana kam ni kutenda kosa wametenda wote, ?’ akaniuliza

‘Ndio maana nataka ushahidi..na nikiupata huo ushahidi…, sitaojali kuwa ni mume au rafiki yangu, yoyote ataumia,…na kila mtu ataumia kutegemeana na kosa lake yeye mwenyewe, wewe ngoja utaona nitakachokifanya…’nikasema

‘Kwa maelezo ya mume wako, wewe ulishirikiana na rafiki yako kulifanikisha hilo, sasa sijui kwa vipi, yeye kadai kuwa wewe ulimtuma, afanye hivyo ni kweli si kweli, ulisikia mwenyewe akiongea pale hospitalini, …’akasema docta, kama ananiuliza

‘Mimi nina kichaa!!!…hahaha, hivi kweli inaingia akilini hiyo, mimi nimtume rafiki yangu akazini na mume wangu, hata wewe unaweza kuliamini hilo…?’ nikauliza

‘Ili kuweza kulijibu hilo, labda nikuulize wewe, je hamkuwahi kukaa na rafiki yako mkapanga kuwa labda rafiki yake ajitahidi kupata mimba, kwa...sio lazima useme kwa mume wako, kwa yoyote, labda yeye akaona kwa mume wako, au...hatuna uhakika bado hapo, nasema hivyo kukuuliza wewe...?’ akauliza

‘Wewe uliwahi kuongea na rafiki yangu akakuambia hivyo...?' nikauliza

'Hapana, baada ya kujifungue amekuwa makini sana, hata nikiongea naye ahataki nimuulize chochote,...'akasema

'Sasa umelitolea wapi hilo, kuwa mimi nimtume rafiki yangu akazini na mume wangu, au sio…ndio una maana hiyo, kuwa mimi nilimshauri hivyo, na ...yeye akaona kwa mume wangu ndio kwenye usiri ..huo ni ujinga haliji akilini kabisa, rafiki yangu mwenyewe, sawa na ndugu yangu aje kufanya hivyo...ingelikuwa wewe ungelifanya hivyo kweli hebnu jiulize kwanza kabla ya kutoa nadharia yako?’ nikauliza

‘Yawezekana mlikaa mkaongea kwa namna ambayo aliona akifanya hivyo haitaleta walakini, lakini sio kwa moja kwa moja kuwa akafanya hivyo kwa mume wako, yawezekana ushauri wako,..ndio uliomsukuma kufanya hivyo labda…’akasema

‘Hakuna kitu kama hicho,..kama kweli yeye ni rafiki yangu ananijali na kujali masilahi ya familia yangu, asingeliweza kufanya kitu kama hicho, yeye anafahamu mambo mengi ambayo kama mimi, au mume wangu akiyafanya hakutakuwa na huruma kwa baba, hilo analifahamu, na anamfahamu sana baba yangu, ..ndio maana mimi siamini kuwa kafanya hivyo, ndio maana nataka ushahidi, baba anauhitajia pia huo ushahidi.., …’nikasema

‘Baba yako keshajua hilo, kuwa huenda huyo mtoto wa rafiki yako kazaa na mumeo,a u mdogo wa mume wako, keshaniulizia hilo, akataka ushauri wangu kama docta , mdogo wa mume wako, hataki kusema ukweli, ukiongea naye, unaweza ukahisi ndio yeye, kwa jinsi anavyojiuma uma, lakini lengwa mkubwa ni mume wako, unahisi ni kwanini...?’ akauliza

‘Baba taarifa alizo nazo ni kama nijuavyo mimi..bado anafuatilia, kasema kama ni kweli, basi, na yeye atakuwa na maamuzii yake, mimi sitaki kusimamia mambo ya wazazi wangu maana nafahamu hukumu yao ni nini…mimi nina namna yangu ya kuhakikisha hao watu, kama ni kweli, wanapata kitu ambacho hawataweza kukisahau maishani mwao…’nikasema

‘Hebu niambiea ukweli wako..utachukuaje hukumu, wakati labda na wewe unahusika, ni kwanini hutaki kusema ukweli kuwa wewe na rafiki yako mlikaa mkakubaliana jambo fulani..?’ akauliza

‘Hata kama tulikaa tukaongea tukajadili mambo, lakini tunakaa sana, tunaongea sana, lakini sio kwa ….hapana, siwezi mimi na akili zangu nimwambie akatembee na mume wangu, na yeye...'mara kukawa kama kuna sauti, nikahisi huenda ni mume wangu, lakini kwa hizo dawa, bado atakuwa kwenye usingizi.

'Anaweza kufanya hayo kwa malengo fulani, au ...kutokana na jinsi mlivyoongea, mimi sijui....na kama anafahamu kuwa kitu kama hicho kikitendeka, yaweza kuharibu kabisa ndoa yako, au..mimi sijui, ...ni kwanini afanye...huoni kuwa kuna kitu ndani yake, na baba yako ndio anakitafuta...'akasema


‘Mimi sijui, ila nijuavyo, baba hataki kashfa, hatua ya kwanza ambayo nahisi ataanza nayo, akiugundua ukweli, ni yeye  kutoa hisa zake, na kujitoa kwa baba kwenye kampuni ya mume wangu, ndio kuiua , maana baba ndiye mdau mkubwa wa hiyo kampuni...'nikasema

'Na kuna madeni,...'akasema

'Ni kweli hata ukiangalia hii taarifa kampuni hiyo ina madeni, ya nje, baba mwenye anamdai pesa nyingi…je hao wanaodai wengine watalipwa na nani…kiufupi kampuni ya mume wangu haipo…na hili ni moja ya mambo yanayomuumiza mume wangu..nimemuambia baba, na sio hayo anayofikiria yeye,…’nikasema

‘Je baba yako alisemaje, hawezi kusaidia vyovyote..?’ akauliza

‘Kasema anaweza kusaidia iwapo, hakuna kashfa, kama kuna baya, kuna kshfa mbaya, kaifanya mume wangu yenye  kutia dosari, familia yake hataweza kusaidia kwa lolote lile, na atajitoa, na kudai pesa zake zote, na atachukua hatua nyingine kubwa zaidi…’nikasema

‘Na wewe huwezi kusaidia chochote..?’ akauliza docta

‘Mimi, hahaha...siwezi, maana hata mimi kampuni yangu haifanyi vizuri..na tatizo ni kuwa kampuni ya mume wangu, inataswira fulani  kwa wateja wangu pia, sijui kwanini, kuna wateja wangu wameanza kukimbia kisa ni kutokana na mwenendo wa kampuni ya mume wangu,.. unajua siasa za biashara zilivyo, kuna vita ya chni kwa chini, katika ushindani wa biashara, wateja wengine, hutafuta visa tu,…’nikasema

‘Je unahisi kilichotokea kwa  mume wako ni sababu hizo za kibiashara, au kuna jingine limajificha…?’ akauliza

Nikaichukua ile taarifa, nikamuonyesha naye akaipitia halafu akasema;

‘Unaona sehemu zote alizoweka mabano kuwa haijakamilika ni zile ambazo zinamgusa yeye…na simu ya mume wako  mmh, haiwezi kusaidia kitu, ...lakini itasaidia nini hapa, kuna mambo kayafunika kiaina, ila haya kuwa mumeo anadaiwa, kampuni haiwendi vizuri, kaongea ukweli, na kayachukua kama sababu kubwa, huoni ni kitu kama kimelengwa kinamna fulani..?’ akaniuliza

‘Simu ya mume wangu haijulikani wapi ilipo hata yeye anasema hakumbuki, huenda iliungua kwenye gari, au iliibiwa..na nimejaribu kuulizia watu wa mitandao kama wanaweza kunisaidia wamesema hilo ni vigumu kwao…’nikasema

‘Ulishaongea na huyu muosha magari, kuhakikisha kuwa huyo aliyeondoka hapo kweli alikuwa mume wako au ni mdogo wa mume wako, maana hapa kwenye taarifa ni kama kulikuwa na watu wawili, huyo hapa alikwenda kupata kitu mgahawani, na huyo aliyekuja kwa rafiki yako ni nani.?’ akaniuliza

‘Huyo muosha magari, hayupo…kasafiri, na hata simu yake haipatikani…’nikasema

‘Je sio mbinu za kumuondoa hapo Dar….hana jamaa yoyote anayemfahamu, tukajaribu kumfuatilia, nahisi hapa tunaweza kugundua kitu..?’ akauliza

‘Sijaweza kufuatilia kiasi hicho, nitategemea hili angalifanya huyo rafiki yangu, lakini ndio hivyo…kama unavyoona, hii sio taarifa ya mtu aliyesomea kazi hiyo, ni kama kaandikiwa na mwanafunzi wake..’nikasema

‘Huku kwenye maelezo, ya uoni wake, katupia lawama ndoa yenu kuwa inaweza ikawa sababu nyingine, unahisi kuna ukweli wowote hapa…?’ akauliza

‘Sizani, kama kuna ukweli, kwanini hilo lisitokee nyuma, lije litokee siku hiyo..nakiri kuwa mimi nina madhaifu yangu, lakini haijafikia hadi yatendeke hayo,…na ndio maana bado sijaamini..’nikasema

‘Hujaamini nini sasa hapo..?’ akauliza

‘Kuwa kwanza ajali hiyo inatokana na matendo ya nyuma, pili, hapa kuna matatizo ya mume wangu na kampuni yake kwa upande mmoja, na huku kuna huyo mtoto wa rafiki yangu, lipi lenye uzito, tatu.... rafiki yangu anahusikanaje na mume wangu kwenye kusababisha kampuni ya mume wangu kufikia hapo ilipo, maana baba kalisema hilo. ukiangalia kuna mkanganyiko, na kwanini mdogo wa mume wangu ananipiga chenga, unajua ananikwepa sana, huoni anaweza kuhusika kama sio yeye…’nikasema

‘Baba yako anasemaje kwa ujumla wake..?’ akauliza

‘Baba yeye hataki kusema lolote mpaka sasa, anasema kuna taarifa anaisubiria, akiipata ndio itampa mwanya wa kusema jambo, ila kaahidi kulifuatilia hili tatizo la familia yangu na kampuni zote, hadi mwisho wake, na kasema sasa hatarudi nyuma, …’nikasema

‘Atasamehe tu, nyie ni watoto wake,…maana vyovyote iwavyo, itasaidia nini sasa eeh, atamfukuza, atavunja ndoa yenu, unaonaeeh, hawezi, na ukiangalia kwa makini,.. kampuni ya mumeo ikifa, mumeo atakuwa anategemea ajira yake tu…ambayo haiwezi kumkidhi haja zake,..na nimesikia huko kazini kwake kuna matatizo pia ni kweli…?’ akauliza

‘Nimesikia sasa hivi na kusoma kwenye taarifa ya huyo mdada, nilikuwa sijui, kiukweli kuna matatizo,…sijui alifanya nini huko…’nikasema

‘Mdada hakuelezea hilo…mmh, hapa…ngoja nisome, anasema, alikopa pesa, na kujikopesha bila idhini,…mmh, kwanini alifanya hivyo, …hapa anasema bado uchunguzi unaendelea…sasa mume akifukuzwa itakuwaje na kampuni ndio hiyonayo inayumba…huo sasa ni mzigo wako ambao sizani kama utaweza kuubeba…’ akasema

‘Hilo sio tatizo kwangu, yeye ni mume, na mengi kajitakia yeye mwenyewe, lakini je hayo ndio yamesababisha hayo yote, hiyo ajali sabau ni hayo, au ...na mmh, bado kichwa changu kina giza, ?’ nikauliza

‘Jibu hasa la haya yote tutalipata kutoka kwa mume wako,... je atakubali kusema ukweli…?’ akauliza

‘Akipona, ni lazima asema ukweli, nitahakikisha hilo analifanya na nitajua la kufanya, wewe subiria tu…’nikasema

‘Lakini usije kuongea chochote kwa hivi sasa, wala kumuuliza..’akasema docta

‘Nafahamu hilo sana, hapa nipo kama mtumwa, kila analotaka nalifanya, kila kitu kimesimama, nitafanyaje, lakini kuna ukweli huo nautaka, ..hata kabla hajapona, nautaka niufahamu, je ni kweli kuwa mume wangu kazaa na rafiki yangu, nikiwa na uhakika na hilo, basi mengine yote hayana maana kwangu, ….mimi na baba tutakiwa hivi, …’nikasema nikishikisha vidole viwili kwa pamoja.

Nikashtuka kusikia mtu anakohoa nyuma yangu,, …nikageuka na kumkuta mume wangu akiwa kwenye kigari chake anatuangalia …akiwa anatokea huko alipokuwa amelala…nikamuangalia mume wangu, alionekana kakasirika kakunja uso..

‘Kwanini umefanya hivyo mume wangu…unatakiwa ulale, hizo dawa zinahitajia wewe ulale, unakwenda wapi sasa…?’ nikamuuliza lakini hakunijibu, akawa anakiendesha kigari chake na kuelekea nje

‘Kasikia nini…?’ akauliza rafiki yangu

‘Sizani….’nikasema, nikiwa sina uhakika.

‘Basi ngoja nikaongee naye,..na wewe hakikisha hiyo taarifa unaificha asije kuiona, pili, nataka tuje tuongee mimi na wewe baadae…nataka.., nikusaidia kulimaliza hili jambo, nitahakikisha unaufahamu ukweli wote, na ushahidi unaoutaka, ila uniahidi jambo…’akasema

‘Jambo gani…?’ nikauliza na mara mume wangu akawa ananiita huko nje..



WAZO LA SIKU: Maisha yalivyo, inafikia muda inabidi ukope, ili kukidhi haja fulani, ni muhimu tukikopa tujue jinsi gani ya kuja kulipa deni la watu, wengine hukopa tu, akisema tutajua huko mbele kwa mbele, na ukianza kudaiwa, unakimbia, unajificha au unajibu jeuri. Tukumbuke kuwa deni ni deni, na deni haliishi mpaka ulipe au mwenyewe kwa ridhaa yake akusamehe. Tusipende kudhulumu tukidaiwa, deni halitaondoka hata ukiondoka hapa duniani,..utaenda kulikuta huko kwa hakimu wa mahakimu.
Ni mimi: emu-three

No comments :