‘Mnaweza
kwenda kumuona mgonjwa, yupo katika hali nzuri tu, ila kwa tahadhari,
msimuongeleshe sana, au kumuuliza maswali ya kumfanya afikirie sana, na mengine
bado tunayafanyia kazi, bado yupo kwenye uchunguzi, ....kwa ujumla hali yake
inaendelea vyema...’
Tuendelee na kisa chetu…..
**************
Nilisimama nikiwa siamini,…au docta alikuwa
ananidanganya,….nikatulia, nikawa namuangalia mume wangu, ambaye kwasasa uso
niliouona awali ukitabasamu sasa umekuwa hauna nuru tena, uso ukawa kwenye
kukunjamana kwa maumivu au hasira.
Unajua wakati nafungua mlango nilikuwa nimepanga kumuuliza maswali
yaliyokuwa yakiniumiza akilini, na nilipomkuta kakaa kitandani, nikafurahia
kuwa sasa nitaweza kupata majibu ya hayo maswali, ...
‘Swali la kwanza nilitaka nimuulize, je ni kweli kuwa ana
mahusiano yoyote na mwanamke mwingine zaidi yangu mimi mke wake, jibu liwe ndio au hapana, hakuna maelezo, sitaki
nimchoshe..
‘Swali la pili je ana mtoto nje ya ndoa ...jibu ni ndio au
hapana.....’ na kama majibu ya maswali hayo mawili yatakuwa ni ndio....basi hakuna
jinsi, akipona tu, ndoa imekwisha, kila mtu ashike mipango yake, mkataba wangu
na yeye basi, ...niliwazia hilo nikiwa na dhamira ya dhati.
Lakini nilijipa moyo kuwa majibu yake yatakuwa hapana, kwani mume
wangu hana tabia mbaya, hawezi kunisaliti,….
Lakini kabla ya maamuzi ya kuvunja ndoa, kwanza awe amepona kabisa, pili, ni lazima
nimfahamu huyo mwanamke shetai ni nani,…ni lazima nimfahamu huyo mwanamke ili
abebe dhamana yake, ni lazima nimfunze adabu, mbele ya.....’
Na nilipofika hapo nikawa nimeshafungua mlango, na ndio hapo
nikajijuta namuangalia mume wangu akiwa kakaa kitandani.
******************
‘Mume wangu umepona…’nikasema nikiwa bado nimesimama siamini. Mume
wangu alikuwa kakaa, lakini mikono miwili huku na huku imeshikilia kitanda,
alikuwa kama anajilazimisha kukaa sawa…nilihisi mikono yake ikitetemeka.
Ghafla , nilipotoa kauli hiyo mume wangu akadondokea kitandani, na
kilichofuata hapo ikawa heka heka, maana yule mtu aliyekuwa kakaa, kwa shida,
maana ilijionyesha kuwa alikaa vile kwa kujilazimisha, kwa jinsi
nilivyomuona,.. sasa anatikiswa na bora alidondokea kitandani miguu imening’inia
, akawa sasa anatikisika, anatikiswa mwili mnzima.
Hapo sasa nikachanganyikiwa kwa haraka nikaanza kuita madocta, kuomba
msaada, na haikupita muda, madocta wakaja, na nikaambiwa nitoke humo ndani
haraka…nikawa siwezi hata kuinua mguu, na kwa muda huo docta rafiki alishakuja,
akanishika mkono, akawa sasa ananikokota, kunitoa nje ya kile chumba.
‘Umefanya nini sasa…?’ akaniuliza docta kwa ukali
‘Mimi sijui, sijafanya kitu…’nikasema
‘Uliongea nini na yeye, si nilikuambia…usimsemeshe kitu cha kumpa
mawazo..’akasema
‘Sikuwahi kuongea naye, nimeingia, akiwa kakaa kitandani, miguu
chini..anatizama mlangoni akiwa na tabasamu, cha ajabu aliponiona tu, akakunja
uso…’nikasema
‘Unasema ulimkuta kakaa kitandan, haiwezeani,…?’ akaniuliza sasa
akishangaa
‘Ndivyo nilivyomkuta hivyo…’nikasema
‘Mhh…matokeo mazuri hayo,…kama ulimkuta kakaa kitandani, basi tuna
matumaini sasa….una uhakika…alikuwa kakaa kukaa..?’ akauliza
‘Ndio docta…..kwani wewe ulimuachaje..?’ nikauliza
‘Nilimuacha kalala, baada ya kumpatia mazoezi, kiukweli mwili wake ulikuwa bado haujawa tayari kukaa
wenyewe bila msaada, basi nilipomaliza kumfanyia usafi, nikamuacha akiwa
amelala..’akasema
‘Sasaa, mhh…najiuliza ni kwanini …’nikasema
‘Unajiuliza nini…hiyo ni iashara nzuri, kama hukuongea naye, na
ulimkuta amekaa peke yake bila ya msaada wa mtu, ujue ni kumbukumbu zinarejea
na pia mwili umeshaanza kukubaliana, …’akasema
‘Ninachojiuliza mimi ni kwanini alikuwa na furaha kama alitarajia
kitu na nilipotokea mimi furaha hiyo ikatoweka…..na hali hiyo ikaja ?’
nikauliza.
‘Hapo ina maana kuwa kumbukumbu zinaanza kurejea, huenda katika
kumbukumbu zake, alitarajia kuona kitu alichokuwa akikiwazia…lakini ikatokea
tofauti na matarajio yake…, inaweza ikawa hivyo, au alipokuona alikumbuka
jambo, ..linalomsumbua, akashtuka…vyote au jingine yaweza kuwa hivyo…’akasema
‘Sasa mbona naanza kuogopa….’nikasema
‘Usiogope, hiyo kwetu ni ishara nzuri..kama kaweza kuinua ule
mgongo, na miguu peke yake, basi matajio ni mazuri sasa, ni swala la muda tu…’akasema.
‘Sasa alitarajia nini, au kuna kitu gani ananiogopea mimi, au ndio
keshajenga chuki na mimi kabisa, au nikuulize wewe ulisema uliwahi kuongea na
yeye,, si ulisema mliwahi kuongea naye..?’nikauliza.
‘Sikiliza, …usipende kujitwika mzigo kabla haujatua kichwani mwako,
utachoka kabla huo mzigo haujatua kichwani, umenielewa, …mume wako hapo alipo
anapambana na mitihani mingi, hatujui kilichosababisha hayo yote ni nini..’akasema
‘Sasa tutamsaidiaje..?’ nikauliza
‘Cha kumsaidia ni kuhakikisha ukija una hali ya kumpa
moyo,..usiongee lolote la kumuumiza kichwa, na nahisi kuna kitu anakitegemea au
mtu anapenda aje aonane naye, nahisi ndio maana ulipotokea wewe tabasamu
likapotea…’akasema
‘Ni nani sasa huyo anayetaka kuonana naye…?’ nikauliza
‘Hapo mimi na wewe hatujui..tunawazia hivyo tu, lakin wewe ni mke
wake, unahitajika kufika, kwasababu kutokufika kwako, kunaweza kumfanya
afikirie vibaya zaidi, cha muhimu nikugundua ni kitu gani anakihitajia kwa sasa…’akasema
‘Nani ataligundua hilo…?’ nikauliza
‘Mimi nitagundua anahitajia nini, usijali…’akasema
**********
Basi siku ile ilipita,
nikawa nafika, namkuta kalala, haongei,..nikimsemesha ahasemi neno, ikawa sasa
mimi sina raha…hata rafiki yake, yaani docta akaniambia hali ya mume wangu
imekuwa tofauti na matarajiao yao.
Siku moja, nikafika hospitalini, nilimkuta mume wangu kalala tu,
kaangalia juu, kama kawaida yake, nikamsaidia kumgeuza geuza japokuwa
alishafanyiwa mazoezi
Sasa nikamgeuza aniangalia, nilitaka kujua kama ananifahamu mimi,
akawa ananiangalia tu, kama mtu mgeni kwake kabisa, moyoni nikaanza kuingiwa na
wasiwasi, nikihisi vibaya, mbona huyu mtu kawa hivi, ni kama mwili mtu....
Ghafla sasa nikaona hisia
za uhai kwenye macho yake, nilimuona
akigeuza mboni za macho yake, na mara
machoni niliona machozi yakimtoka...nikasogeza mono na kuyafuta machozi
yake..nikawa najiuliza ni kwanini machozi hayo yanamtoka, anahisi maumivu au
kuna nini, .nikatulia, na hapo huruma, woga, wasiwasi na kukata tamaa, vikanitawala,
...
‘Mume wangu mbona upo hivyo, niambie kinakusumbua nini jamani..?’
nikauliza
Nilichoona ni machozi yakiendelea kumtoka kwenye macho yote mawili
na mimi nikawa nakazana kumfuta hayo machozi;
‘Mume wangu unalia nini, niambie anagalau na mimi nijue, ..mimi ni
mke wako, unavyokuwa hivyo mimi naumia sana, niambie kitu ili niwe na amani
moyoni, unalia nini, nimekukosea nini…?’ nikauliza
Mara mume wangu akawa anahangaika kupanua mdomo, unakuwa kama
unatetemeka, kuashiria anataka kuongea jambo;
‘Kama huwezi basi usijilazimishe, ila ujue mimi mke wako nakupenda
sana…’nikasema na hapo macho yakameta meta, kuashiria uhai, na hali ya
kutikisika tikisika kichwa, nikaogopa kuwa huenda ile hali iliyowahi kutokea
inaweza kutokea tena, lakini haikuwa hivyo, mara akasema;
‘Mke -wangu,…m-ke..w-w-wwngu..’akasema
‘Mimi hapa mume wangu, ..’nikasema
‘Ni-ni-samehe…na-na- na-kuomba ni-ni-s-s-samehe…’akasema
‘Mume wangu hujanitendea ubaya, hata hivyo usiwe na wasiwasi, sina
tatizo na wewe…’nikasema
‘Ni-ni-ni…..me-me-ku-ku-kosea….’akasema
‘Nimekusamahe mume wangu japokuwa sijui …’nikasema
‘Yah---ohhhhh……’hapo akavuta pumzi halafu akatulia kwa muda, macho
yapo wazi nayaona, na…machozi hayatoki tena…’halafu nikaona kichwa inatikisika,
ilichukua dakika chache kikatulia, ikaanza kwikwi….hapo ikabidi niwaite madocta…
Nikaambiwa nitoke, nikatoke pale na mimi machozi yakaanza
kunitoka, nahisi huzuni, namuonea huruma mume wangu anavyopambana na hiyo hali
na siwezi kumsaidia ..
Nilikaa nje kwa muda, mara docta akaniita,…nikaingia, na docta
akasema
‘Haya mwambie mke wako unachotaka kumuambia…’akasema docta
‘Mke wangu, so-so-sogea….’akasema na mimi nikasogea na kukaa
kitandani karibu yake.
‘Ni-ni-sa-mehe..m-m-mke wangu…ha-ha-ya yo-yo-te ya-ya-na-na-natokea
ku-ku-ku-toka-ka-kana na dh-dh-dhambi zangu, ni-n-nisamehe sa-ss-sana...’akasema
‘Dhambi gani mume wangu...’nikasema na safari hii nikawa
nimeshusha sauti na kuongea kiupole
‘Wewe kubali kuwa umeshamsamehe, na itoke moyoni…’akasema docta
‘Nimekusamehe mume wangu uwe na amani, upone, nakuhitajia sana
nyumbani..’nikasema, na nilijikuta pale siwezi kujizuia, machozi yakaanza
kunitoka, na nilibakia vile mpaka nikahisi mtu akinishika begani sikutaka
kugeuka kumwangala ni nani nikasema;
‘Mume wangu ana tatizo gani..mbona kawa hivi tena jamani...?’nikauliza
huku nimeshika kichwa.
‘Ni tatizo la muda mfupi, litakwisha na ataweza kutembea cha
muhimu ni kufuata masharti ya dakitari, dakitari bingwa wa mambo hayo
keshamwangalia , kasema hilo litakwisha, hali iankwenda vyema kabisa, kuna kitu
anakihitajia, labda ilikuwa ni hiyo kukuomba msamaha,lakini bado, kuna kitu
anakihitajia....’akasema.
Niligeuka kumwangalia huyo aliyeongea haya, alikuwa docta rafiki wa mume wangu, na kwa muda huo
nilitamani nimkumbatie, ili nisianguke, maana miguu ilikuwa haina nguvu,
nilihitajia mtu wa kunifariji na kusema mume wangu atapona tu, hakuna
tatizo.....
Nikageuka kumwangalia mume wangu, na nilimuona akiwa sasa akiwa
kaangalia juu, hatikisiki , alikuwa kama gogo tu, alikuwa kama mwili wa
marehemu, lakini unachojua kuwa yupo hai ni machoni, akiyapepesa na kuyageza
huku na kule, na sasa machozi yanamtiririka.
Pale...moyoni nikaingiwa na huruma, woga ukachukua nafasi
nikiwazia mbali zaidi, kuwa sasa mume sina tena, kauli hizi ni za kuniaga, ....na
ile hali ya hasira chuki ..vikayeyuka...sasa
namkabili mungu anisamehe, kama nina kinyongo na mume wangu mimi sina tena
amponye mume wangu tu.
‘Ndio maana nilikuwa nakuzuia sana, usiingie bila ya mimi….’akasema
docta.
‘Hali kama hii hata ingelikuwa ni wewe…’nikasema na mara sauti ya
mume wangu ikasema
‘Mke wa-wa-ngu, ...usiondoke kabla hujanisamehe, na-na-na taka
nikifa niwe huru, na-jua ni-meku-kosea sana, nisa-mehe mke wangu...na
baba-ya-ko, ani-sa-sa-mehe..na-na deni…na..na..mto-ooooh..’hapo hakuweza kumalizia,
akawa kimia
Milio ya mashine ya hatari ikaanza kulia, hapo ikawa heka heka kwa
madocta na mimi nikatolewa nje kwa haraka…hapo ndio nikajua sina mume tena,…..nililia,
na kulia….
Sitaweza kuisahau siku hiyo…
NB: naishia hapa kwa leo
WAZO LA LEO: Katika maisha yetu, katika kuhangaika
kwetu, maana yabidi tuhangaike, tutafute riziki za halali,..yabidi tupambane na
mitihani ya maisha magumu, kuna wenye maradhi ,madeni nk..yote ndiyo maisha
yetu, vyovyote iwavyo, hata kama tupo kwenye raha, hatuna shida, tunakula na
kusaza…bado sisi ni waja wa mola, hatuna jinsi, tupo kwa rehema zake,…tuyakumbuke mauti, kuwa ipo siku
yatatukuta, hata tukiwa nani,…muhimu kwetu, ni kujiuliza je tumejiandaaje na
siku hiyo, siku ambayo roho itauwacha mwili,…
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment