Nilipomaliza kuongea na baba, nilihisi mwili mnzima ukinicheza
cheza kwa hasira, lakini sikujua namkasirikia nani, au naogopa nini, lakini anayoongea ni kama ana uhakika nayo,..awali nilijua ni ile chuki kuwa nimeolewa na mtu wasiyemtaka, lakini haya anayoongea sasa yananifanya nianza kuingiwa na mashaka
Wakati anaongea akili yangu ilikuwa mbali, ikijaribu kuunganisha matukio yaliyofuatana, kujifungua kwa rafiki yangu mtoto anayefanana na watoto wangu, ajali ya mume wangu, ambayo ina utata, na inaonekana alitokea upande anapoishi rafiki yangu.
Sasa kuna mtu kaiba bahasha , bahasha ambayo nahisi ilikuwa na ushahidi,…sikupata hata nafasi ya kuifungua,..kwa hali
hiyo akili ikaanza kunionya kuwa kuna kitu...kuna mtu, ananichezea, ..ni nani huyo
Mume wangu, ...hapana, mume wangu anaumwa, hajiwezi,
Rafiki yangu....…
‘Unasikiliza wewe bint...'baba akaongea kwa ukali kwenye simu
'Nakusikiliza baba...'nikasema
'Nimekupigia simu, kuwa kampuni ya mume wako, ipo
karibu kufilisika, na kuna madeni mengi sana…una hiyo taarifa…?’ baba akauliza
‘Baba ndio nimerudi nyumbani, sijapata hata muda wa kuipitia ile
taarifa uliyonipa, mimi sijui lolote kuhusu kampuni yake, alikuwa akiendesha
mambo yake na mimi yangu…’nikasema
‘Unaona sasa, hiyo ndio ndoa mnayoitaka nyie uhuru wa kufanya mtu
apendavyo, hata kwa mke na mume, aah…kila mtu kivyake, ..nikuulize hivyo ndivyo
tulivyokufunza…’akasema baba na mimi nikabakia kimia.
‘Sasa sikiliza mimi sitaweza kutoa chochote tena kwenye kampuni ya
mume wako, au hata yako, maana nyie sasa mnajiweza, au sio…na hayo madeni ya
mume wako mtajua jinsi gani ya kuyalipa, kama ni kufilisi mali za kampuni
mtajua wenyewe, ila mjua kuwa mnahitajika kurejesha mtaji wangu…’akasema
‘Baba, hatuwezi kufanya hivyo wakati mtu yupo mahututi
hospitalini…’nikasema
‘Na huyo rafiki yako alizaa na nani…?’ akanishtukiza na swali
ambalo lilikuwa kama mtu kazabwa kibao usoni.
‘Mi-mi…baba, sijui…’nikaweza kusema hivyo
‘Una uhakika…?’ akauliza
‘Mi-mi..sijui baba, kama mwenyewe hajawaweza kunieleza, nitajuaje,
nahisi hataki watu walifahamu hilo…’nikasema
‘Mtoto wake anafanana na watoto wako au sio…’akasema kama kuuliza
‘Mhh, baba umeyajuaje hayo ina maana umeweza kumuona huyo mtoto…?’ nikauliza na
mara kwenye simu yangu kukaingia ujumbe , sikutaka kukatiza simu ya baba, ila
yeye akasema.
‘Tazama hiyo picha niliyokutumia kwenye simu yako…’akasema ikabidi
niache kuongea naye nitazame hiyo picha.
‘Huyo ni nani…?’ akuliza
‘Hawa ni mapacha wangu, watoto wangu wakiwa wadogo…’nikasema
Baadae ukaingia ujumbe mwingine akionekana mtoto mchanga, .alikuwa
mtoto wa rafiki yangu, na pembeni wamewekwa watoto wangu kama kuwafananisha na
huyo mtoto, kiukweli wanafanana sana, hana tofauti na watoto wangu kwa sura,
isipokuwa yeye hana nyusi nyingi…sura ya kiume ilionekana usoni mwake.
‘Hata usemeje,….mtoto wa rafiki yako anafanana sana na watoto
wako…sasa niambie ukweli kuna nini hapo, je sio kweli kuwa mume wako anashirikiana na rafiki yako au
kuna nini kinachoendelea kati yenu, mimi nisichokifahamu…’akasema baba
‘Una maana gani baba…!!, kuwa rafiki yangu anaweza kutembea na
mume wangu…?’ nikauliza
‘Nikuulize wewe sasa…’akasema
‘Haiwezekani baba, unataka kusema nini kuwa mimi nimeshirikiana na
rafiki yangu kulifanikisha hilo, au…’nikasema
‘Sasa hilo utajua wewe mwenyewe na mume wako na huyo unayemuita
rafiki yako kipenzi…ndugu yako…, lakini kama ikatokea kuwa ni hivyo, sitaweza
kuvumilia upuuzi huo, kwanini ukaruhusu hilo, au ulitaka rafiki yako awe mke
mwenza wako…au?’akasema baba kwa ukali
‘Baba unanijua nilivyo, mimi siwezi kuruhusu kitu kama hicho, na
sio kweli baba, kufanana kwa watoto sio ushahidi wa kulithibitisha hilo, ndio
hata mimi niliingiwa na mashaka hayo, lakini rafiki yangu hawezi kunifanyia
hivyo baba, sio kweli…’nikasema
‘Sasa ilikuwaje…jiulize hilo kwa makini,…je ni mume wako
kakuzunguka au unataka kusema nini, jitetee sasa….?’ Akauliza
‘Baba huyo anaweza akawa mdogo wake mume wangu, anaweza akawa
ndiye baba wa huyo mtoto, niliongea na huyo rafiki yangu, na kasema hivyo,
hanificho kitu, kiukweli siwezi kuamini hayo, baba haiwezekani, …’nikasema
hivyo japokuwa sina uhakika
‘Na iwe hivyo…..vinginevyo, utaniambia, mimi kama mzazi nimeshajua ukweli, lakini
siwezi kwanza kuliingilia hilo, …isome hiyo taarifa niliyokupa, halafu na hayo
yaliyogundulikana , kila kitu kipo wazi, ukiunganisha hiyo taarifa, matukio na
picha, utakuja kuniambia….umesikia, …’akasema na kukata simu
‘Bahasha haipo, sasa itakuwaje..siwezi kumuambia baba ukweli kuwa imeibiwa,
ataniona mimi ni mzembe..sasa nifanyeje…’nikawa naongea peke yangu
Akilini nikajua kuwa baba
atakuwa aliandaa taarifa inayohusiana na mume wangu, huenda na ….ingenisaidia
sana, sasa nifanyeje, na ni nani kaiba hiyo bahasha?
‘Sasa hiki ni kitendawili kwangu….’ Nikasema nikikaa kwenye sofa,
nikashika kichwa nikiwaza…nifanyeje
Kwa haraka nikachukua simu yangu.
***********
‘Umefikia wapi…?’ nikamuuliza
‘Kuhusu hiyo kazi eeh… bado sijapata lolote la muhimu, ila kuna
jambo nalifuatilia bado halijawa sawa, nikiwa na uhakika nalo nitakuambia…’akasema
‘Wewe na mume wangu mumeanza lini mashirikiano ..?’ nikamuuliza na
nilihsi hali ya kupumua kwa nguvu kutoka kwa rafiki yangu huyo
‘Una maana gani sijakuelewa hapo…?’ akauliza
‘Yoyote yale…najua unaelewa ninachokuuliza..?’ nikauliza
Kukapita ukimia fulani, halafu nikauliza tena
`Umenisikaa nilichokuuliza....?’ nikauliza .
‘Nimekusikia lakini sijakuelewa bosi, una maana ganu kuuliza
hivyo, sijui unachokiongea bosi...’akasema
‘Kwanini unakuwa tofauti hivyo, sio kawaida yako unanipa mashaka ,
mara nyingi nikikuuliza swali unakuwa mwepesi kulitafsiri na majibu yako
yanakuwa ya haraka…na mara nyingi yanakuwa ya ukweli, tunageukana siku hizi…’nikasema
kwa ukali
‘Rafiki yangu, mimi
sijakuelewa,o-bosi, sina mashirikiano yoyote zaidi ya yale tuliyokubaliana,
ukiniagiza nifenye ndivyo nafanya, na zaidi subiria taarifa ya kazi
uliyonipatia, kwani kuna nini bosi…’akauliza, kiukweli tukiwa kwenye maswala ya
kikazi hupenda kutumia neno hilo bosi.
‘Ukweli utadhiri,…endelea na kazi niliyokupatia, ila ujue mimi sio
mjinga, kukuamini kiasi hicho sio kwamba nimefumba macho na kuziba masikio,
akili yangu inafanya kazi vizuri tu, …unanielewa…’nikasema
‘Nakuelewa bosi….’akasema
‘Watu wanasema , na sio mmoja sasa, na hili kama limefika kwa baba
ni hatari sana, kama kaamua mwenyewe kulifuatilia, sijui itakuwaje, mimi
nilipomuona mtoto wako kufanana na watoto wangu niliingiwa na mashaka, hayo
kama binadamu, lakini najua wewe kama rafiki yangu huwezi kunisaliti…’nikasema
‘Ni kweli…siwezi kufanya hivyo….’akasema
‘Je kuna kitu unanificha…?’ nikauliza
‘Bosi unakumbuka ni wewe uliyenishauri kuwa
nikatembee nje ili nipate mimba, na ukanishauri nitafute hata mume wa mtu…’akasema
‘Ndio ukaamua kutembea na mume wangu…?’ nikamuuliza
‘Hapana bosi, mimi najiuliza ni kwanini wewe unapaniki kiasi hicho…’akasema
‘Kwasababu lisemwalo lipo…na wewe hutaki kuniambia ukweli, haya
basi niambie baba wa huyo mtoto ni nani…kama hayo yanayosemwa sio ukweli…?’
nikauliza
‘Yanasemwa mengi bosi na sio yote yana ukweli, …niamini bosi mimi
sifanyi kitu kinyume na ulivyoniagiza….na..hebu kwanza subiria nimalize kazi
uliyonipa ili tukiongea tuwe na ushahidi….wewe si ndio unataka huo, sasa
subiria….’akasema
‘Mume wangu ana kitu
kinamsumbua, mdocta wananiuliza kuna jambo gani kalifanya ambalo halimpi amani,
nataka kulifahamu, sasa kama ni hilo, ..na wee unamjali shemeji yako, niambie,
sema ukweli tuone jinsi gani ya kumsaidia…’nikasema
‘Sizani kama …’akatulia
‘Huzani nini, ..?’ nikauliza
‘Kuwa yeye kuna jambo linalohusiana na mimi au mtoto linamsumbua,
sizani, nahisi ni mambo yenu wewe na yeye, au mambo ya kazini kwake…’akasema
‘Aliwahi kukuambia hivyo…?’ nikauliza
‘Nasema tu..na yote utakuja kuyaona, si umenipa kazi, sasa subiria…’akasema
‘Kwahiyo katika ugunduzi wako, umeliona hilo..sawa…?’ nikauliza
‘Ndio nahakiki ukweli, siwezi kukujibu kwa sasa unajua nifanyavyo
kazi yangu, niamini bosi…’akasema
‘Lakini baba anahitajia majibu nitamjibuje mfano akinipigi asimu
sasa hivi…?’ nikauliza
‘Mwambia tunalifanyia kazi bosi…’akasema
‘Sasa nisikilize sana, acha maneno hayo, ya kunizunguka, naona unapima
hasira zangu, acha kauli za kufanya niondoe uaminifu wangu kwako, nimeongea na
baba, na nimemthibitishia kuwa huenda mtoto wako anafanana na watoto wangu kwa
vile ulitembea labda na ndugu za mume wangu, sasa tafuta ushahidi wa
kulithibitisha hilo, kama ni kweli, vinginevyo, hutaamini nitakachokifanya…’nikasema
‘Kwani kamuonea wapi mtoto wangu, mbona hajawahi kuonana na mimi…?’
akauliza
‘Mimi sijui yeye kanitumia picha ya mtoto wako, na mimi
nilipoichunguza kiukweli mtoto wako anafanana sana na watoto wangu, kwa mtu
yoyote atafikiria hivyo, kuwa wewe umetembea na mume wangu…’nikasema
‘Rafiki yangu, ...najua itafika muda ukweli utadhihiri, wa-ache
watu wasema, lakini ukweli utabakia pale pale, na ukweli mwingine kama sitaki
ujulikane hakuna wa kunilizimisha, hata awe nani…’akasema
‘Kwahiyo unataka kusema nini…?’ nikauliza
‘Kuwa subiria taarifa ya kazi yako, halafu utakuja kuamua mwenyewe…’akasema
‘Kwahiyo ni kweli…?’ nikauliza
‘Kuhusu nini sasa…?’ akauliza
‘Usitake kunifanya mimi kama mtoto mdogo, unajua nimekuuliza
nini…’nikasema kwa ukali
‘Hapana, sio kweli, kama ni hivyo unavyofikiria wewe, japokuwa
sijui ina maana gani hapo, ukweli wote nitakuambia mimi ambao ni lazima uujue, ngoja nimalize hii kazi uliyonipatia
kwanza…’akasema
‘Narudie tena, mimi nimeongea na baba yangu nikamthibitishia hilo,
kuwa mume wangu hawezi kufanya upuuzi huo, kwani kama ni kweli, itakuwa kashfa
kubwa sana kwenye familia yangu, unalifahamu hilo…’nikasema
‘Mhh…nakuomba kitu kimoja,kwanini usisubirie kwanza nimalize hii
kazii uliyonipatia, kila kitu kitakuwa wazi, na hata baba yako, ataamini tu,
usiwe na wasiwasi kabisa, …’akasema
‘Nakuuliza tena, je kuna ukweli wowote wa hizi shutuma kuwa huenda
wewe na mume wangu mna mashirikiano fulani, ambayo yamekwenda zaidi hadi
kuingilia ndoa yangu…?’ nikamuuliza
‘Sio kweli….’akasema
‘Nataka ushahidi…wa kumthibitishia baba yangu,,unanielewa, kesho
niupate, nakupa muda huo hadi kesho, unanielewa…’nikasema na kumuuliza
‘Sawa bosi….’akasema.
‘Kama ni kweli, umenithibitishia hilo, basi mimi nataka ukweli
wote kuhusu mume wangu, nataka kujua ni kwanini hayo yakatokea, nataka kufahamu
huyo mwanamke mwingine aliye na
mashirikiano naye, nilikuambia utafute huyo mzazi ni nani, nimeambiwa, hakuna
mzazi mwingine sasa ni nani zaidi yako…’nikasema
‘Utamfahamu bosi, kila kitu nimekifuatilia …’akasema.
‘Sawa, kwa ajili ya urafiki wetu, kwa ajili ya kupona kwa mume wangu
nakusubiria wewe, natumai haitafikia muda tukawa maadui,...’nikasema
‘Ni kweli, haitatokea hivyo, niamini, …’akasema
‘Una uhakika..?’ nikauliza kama anavyopenda kuuliza baba yangu.
‘Siwezi kukuangusha bosi, ndio maana nataka kila kitu kiwe wazi,
ili nikikuletea hiyo taarifa, kusiwe na kigugumizi tena, unanielewa nifanyavyo
kazi zangu, najua baada ya taarifa hiyo hata baba yako, hatakuwa na tatizo tena,
itabakia wewe kuchukua hatua zako...’akasema.
‘Sawa ……na nitaichukua hatua ambayo hutaweza kuamini…’nikasema
‘Oh, hatua gani…?’ akauliza
‘Nimeliwazia sana hilo,…limeniumiza sana kichwa changu, huyo
shetani nikimpata, kuna watu nimewapanga, kuna wale mabaunza, niliwahi
kukuambia walishaifanya hiyo kazi kwa rafiki yangu mmoja, unakumbuka yule binti
aliyejiua, nataka iwe hivyo kwa huyo shetani, harabiwe kiasi kwamba hatatamani
kuishi tena....’nikasema.
‘Mungu wangu....’akasema.
‘Lakini kwanini kufanya unyama wa aina hiyo …?’ akauliza.
‘Wewe kafanye hiyo kazi…kuna
jambo jingine nilitaka wewe ulifanyie kazi, lakini naona nitalifanya peke
yangu, kuna watu wanataka kunichezea…wameingia
hadi kwenye anga zangu…sitaki baba anione mimi sijui kazi,…baadae nakwenda
hospitalini kwanza...’nikasema na kukata simu.
**********
Nilifika hospitalini, na kabla sijaenda wodini, akaja docta rafiki
yangu, kumbe yeye alihawahi hapo hospitalini, …nilipotoka kwenye gari langu tu,
akajitokeza na kuniwahi, akanisalimia kwa haraka halafu akasema;
‘Niliongea na docta anayemshughulikia mume wako, hali yake ipo
salama kuna mambo kidogo yapo kwenye uchunguzi, na docta wamesema unaweza
kwenda kuongea na yeye, japokuwa anaongea kwa shida, kumbukumbu zake bado
hazijawa sawa, ni kawaida tu…zitakuwa sawa taratibu, nab ado hajaweza kujiinua mwenyewe
kitandani…’akasema
‘Mhh..kwahiyo unataka kusema nini… kuwa hakumbuki kilichotokea au
hakumbuki watu….?’ akauliza.
‘Yah, kwa hivi sasa hata ukimuuliza atakuwa kama anatafakari,
kujiuliza, sasa kwa hivi sasa haitakiwi kumuuliza uliza maswali kama hayo,
..ndio maana walizuia watu kuonana naye, kwa hivi sasa wanaruhsu watu wachache
wanaomfahamu..lakini kwa tahadhari hizo…’akasema.
‘Sawa nimekuelewa, ..lakini
huenda kukatokea athari gani nyingine, hata kama ni huenda, nataka kujua
tu..’nikasema.
‘Mhh…athari nyingi ni za muda tu, Inawezekana ikatokea , asiwezi
kuzaa tena, inawezekana sio lazima, athari
nyingine ndio hizo kama hiyo kushindwa kutembea kwa muda, kukosa kumbukumbu nk,
lakini mengi ni ya muda tu,...’akasema.
‘Unaposema kuwa anaweza kushindwa kuzaa, ina maana gani, kuwa
hataweza kabisa ku-ku....’nikasema kwa kigugumizi.
‘Kufanya kazi ya uanaume..sio hivyo…atafanyakazi kama kawaida, ila..kuzaa,
hata hivyo, sio lazima kuwa hivyo…’akasema
Mara akaja, docta aliyekuwa akimshughulikia mume wangu, alikuwa
anataka kuongea jambo, na huyo rafiki wa mume wangu akamuwahi kabla hajasema
lolote, na kitendo hiki sikukipenda, niliona kama anazuia nisisikie jambo
fulani, nikawasogelea na yule docta akasema kwa haraka;.
‘Mnaweza kwenda kumuona mgonjwa, yupo katika hali nzuri tu, ila
kwa tahadhari, msimuongeleshe sana, au kumuuliza maswali ya kumfanya afikirie
sana, na mengine bado tunayafanyia kazi, bado yupo kwenye uchunguzi, ....kwa
ujumla hali yake inaendelea vyema...’akasema, na mimi nikataka kumuuliza swali,
docta rafiki wa mume wangu akadakia na
kusema,..
‘Hakuna shida docta, mimi nitahakikisha mgonjwa hapati shida,
...na tunashukuru sana, nitakuja tuongee vizuri....’akasema na yule docta
akaondoka, na mimi nikageuka kumwangalia docta na kumuuliza.
‘Hivi kwanini unakuwa hivyo, inakuwa kama kuna jambo hutaki mimi
nilisikie kutoka kwa huyo docta, mimi ni mke wake, nina haki ya kufahamu kila
kitu...kwanini mnataka kuniweka roho juu...?’ nikauliza.
‘Sikiliza mimi ni docta, na pili mimi niliwahi kuwa mpenzi wako,
nakufahamu ulivyo, ndio maana nataka habari zote kwako ziwe kwa maslahi yako,
zisije zikakufanya ukawa na mshituko, na pia usije ukafanya kitu kikaja
kumuathiri mgonjwa..’akasema
‘Kwahiyo kuna kitu unanificha…?’ nikauliza
‘Hakuna…ni tahadhari tu,…niamini mimi, nayafanya haya kwa nia jema
kabisa..nilikupenda na nitaendelea kukupenda…na namjali rafiki yangu…sitaki aje
kudhurika wakati nafahamu …’akasema na mimi nikamtupia jicho na kuangalia
pembeni.
‘Wasiwasi wangu ni kuwa inavyoonekana kuna tatizo la kiafya kwa
mume wangu, na nyie hamtaki kuniambia, ndio wasiwasi wangu huo...’nikasema.
‘Ninachotaka hapa ni hekima, mara nyingi docta akisema mgonjwa
wako anahisiwa kuwa tatizo, watu hulichukulia kama ndio tatizo, uvumi husambaa,
na hata kumfikia mgonjwa, kwa hivi sasa hatutaki mgonjwa apate kitu cha
kumuumiza kichwa, ....inaonekena ana mfadhaiko fulani unaomkera,, unampa shida
sana, sasa hilo ndilo ninalotaka baadae tuongee....’akasema.
‘Mfadhaiko....?’ nikauiliza kwa mshangao.
‘Ndio kunaonekana kuna jambo lina mkera, linampa shida,na kwa
minajili hiyo, anajikuta hana amani...au nafsini mwake, anaogopa kuwa kuna kitu
kitatokea kibaya, lakini yupo kwenye hali ambayo hawezi kufanya kitu..naweza
kusema hivyo...’akasema.
‘Mhh, hapo mimi sijuii....’nikasema.
‘Ndio maana nataka utumie hekima kubwa katika kuliongelea hili ,
tumia hekima sana kuongea na mum e wako, na kwepa sana kumshinikiza kwa maswali
magumu na shutuma, ndio maana nilitaka wakati unaongea na yeye na mimi niwepo,
kipindi kama hiki kwake ni kigumu sana, ... na hebu nikuulize, je mwenzako hana
tatizo jingine kubwa unalohisi kuwa kalifanya....’akaniuliza.
‘Kiukweli sijui, labda mambo ya kazini kwake, lakini nitajitahidi
kutafuta kama kula lolote zaidi…kuna watu wanalifanyia kazi………’nikasema
‘Rafiki yako..au sio?’ akaniuliza
‘Yawezekana…’nikasema
‘Una uhakika hakuna kitu kingine kinamsumbua mume wako ambacho
wewe unakifahamu na unaweza kukifanya kumsaidia ….ili awe na amani…?’ akauliza
na mimi sikutaka kumuambia hayo aliyoniambia baba, kuwa huenda ni madeni, …
‘Sina uhakika, ndio maana nasema , labda maswala ya kikazi, huko
ofisini kwake, na mimi sina ushirika na yeye huko….’nikasema
‘Ya kikazi hayo mhh, ni ya kawaida, watu wanadaiwa wengi tu…nahisi
kuna jingine kubwa ya hilo,…wewe ndiye mtu wake wa karibu wa kulisaidia
hili’akasema. Na kabla sijasema kitu simu ya docta ikawa inaita na yeye
akaangalia mpigaji na kusema;
‘Tutaongea baadaye hii simu ni muhimu sana...wewe tangulia huko
kwa mgonjwa, nakuja, ila kumbuka,....usimuulize maswali mengi ya kumuumiza
kichwa’akasema docta huku akianza
kuongea na hiyo simu yake.
Nikawa natembea kuelekea huko kwa mgonjwa, nafsini nina wasiwasi, …nitaongea
nini na yeye, na nashindwa kuvumilie mengina yanayotokea, nimesikia mengi, nay
eye ndio mwenye kauli ya kukubali au kukataaa..je nitaweza kujizuia..
Nikashika kichwa nikiwaza,;
‘Lakini kwanini niteseke kwa mawazo wakati muhusika yupo...kwanini
nisimuulize tu, hapana nitasubiria, lakini nikisubiria baba anahitajia majibu,
je kama ni kweli, kuwa mtoto wa rafiki yangu ni wake, nitajuaje, hapana sio wa
kwake..mmh, sijui nifanyaje....’nikajisemea mwenyewe kwa sauti ya chini chini.
‘Nitamuuliza tu, kinamna
ambayo sitamuumiza…’nikasema, na nikageuka nyumba, kumuangalia docta, alikuwa
bado anaongea na simu, sasa akawa ananionyeshea ishara kuwa nisubirie kwanza...mimi
sikumsubiri nikaingia ndani kukabiliana na mume wangu...
‘Nitamuuliza tu….’nikasema na nilipoingia nilishangaa, mume wangu
alikuwa kakaa kwenye kitanda, miguu chini, nikashikwa na butwaa, walisema
hawezi kujiinua mwenyewe, mbona…na kwa mdua huo alikuwa …anaangalia mlangoni
kama anasubiria mtu, akiwa na tabasamu mdomoni, na aliponiona mimi, tabasamu lililokuwa
mdomoni likatoweka, akakunja sura…
**********
WAZO LA LEO:
Mwili wa binadamu ni mdhaifu sana, na kosa dogo linaweza likaharibu utaratibu
mzima wa mwili wa binadamu, mfano angalia wengi waliofikiwa na matatizo ya
kupatwa na kiharusi, kupooza kwa viungo, ...ukichunguza sana utaona kuwa tatizo
hilo lilitokea baada ya jambo dogo tu, kwako wewe mzima, uliona ni jambo dogo
tu, lakini kwa mwenzako mwenye tatizo, alishindwa kuhimili, hasira kidogo, au
mshituko kidogo tu, na vitu kama hivyo, vimeharibu utaratibu mzima wa
mwili wake, na kupelekea kupooza sehemu za viungo vyake.
Ni muhimu, tunapokabiliana na watu wenye matatizo kama hayo iwe ni
matatizo ya moyo, shinikizo la damu, sukari, au vidonda vya tumbo, tuwe na
hekima ya kuongea nao, tujaribu kufuata
masharti ya dakitari, na tusipuuze, maana tunaweza kuja kujuta wakati
tumeshaharibu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment