‘Baba umerudi lini…?’ nikasema, nikiwa nimenywea, maana ili sura
ya kutisha ilipotea ghafla, na uso ukawa wa aibu,…uso wa kujipendekeza. Kwa
muda huo, baba alikuwa kanikazia macho tu, akimaanisha anasubiria jibu la swali
aliloniuliza. Nilipoligundua hilo, nikasema ;
‘Ni ajali tu baba,….mume wangu kapatwa na ajali….’nikasema
‘Nimeshaonana naye na nimeshapata taarifa zote kutoka kwa dakitari,
na bado nasubiria taarifa nyingine, maana ajali hiyo sio ya kawaida,…kuna kitu
ndani yake. Ni lazima kujiuliza ni kwanini, akaendesha gari kwa mwendo kasi
kiasi hicho, alikuwa kalewa..’ akawa kama ananiuliza
‘Hapana….’nikasema
‘Una uhakika….?’ Sasa akaniuliza
‘Mhh…ndio baba, maana hata Docta wamesema hakuwa kalewa, na hakuwa
amekunywa kabisa siku hiyo….’nikamtetea mume wangu.
‘Lakini kulewa sasa imekuwa kawaida yake au sio…? Ni kwanini
anafanya hivyo…?’ akaniuliza
‘Ni starehe zake tu baba, lakini litamalizika hilo…’nikasema
‘Una uhakika…?’ akauliza akiniangalia kwa makini
‘Baba….’nikasema hivyo na kutulia.
‘Nauliza swali langu tena….kuna nini kati yako wewe na mume wako,
nilishakuuliza hilo swali awali ukasema ni mambo ya kawaida tu…, nilikuambia,
nikusaidie ukasema hapana,..mtayamaliza wenyewe, sasa kwa hili, sitaweza kusubiria , nataka
kujua kila kitu, au uniambie mwenyewe kuna nini…?’ akauliza
‘Baba …ni mambo ya kawaida tu ya ndoa, sizani kama wewe na mama
mpo na furaha wakati wote, ..kuna muda kunatokea hili na lile, na sizani yote ya
ndani ya ndoa nahitajika kuyasema kwako, tutayamaliza tu kwa amani baba, hii ni
ajali tu…’nikasema
‘Bint, mimi sio mtoto mdogo wa kukuuliza haya, nimesoma, nina
uzoefu wa maisha zaidi yako,…unanielewa,..sitaki nikukumbushe kila kitu…kuwa
tulikuambia, tulikuambia,.. hukutusikia…, na asiyesikia la mkuu hufanya
nini…’akasema
‘Lakini baba, nilishawaambia, mimi nitaweza, na ninaweza…, haya ni
maisha yangu na mume wangu, tuachieni wenyewe…, maana tumeshaoana sasa…, sizani
kama ni busara tukarudia yale yale malumbano ya zamani, sasa hivi tuna watoto,
tuna familia..baba maji nimeshayafulia nguo nitafanyaje sasa, hebu niambie baba…’nikasema
‘Nafahamu hilo..utasema hivyo, utajitetea tena na tena…., si umekuwa
bwana, unajiweza au sio…..haina shida,… ila lile linalogusa familia yangu…,
lile linakuja kunigusa na mimi mwenyewe.., sitaliacha lipite hivi hivi, hebu
nikuulize ikitokea tatizo, la kikashifa kwako, utaambiwa wewe ni binti wa
nani..?’ akaniuliza
‘Kuna kashfa gani baba imetokea, mbona baba mnataka kuyakuza
mambo, a kuna nini umesikia kibaya,…baba hakuna kashafa yoyote,…kama umesikia
hivyo, ni ….watu tu, kama ujuavyo wanadamu hatuna wema, …mimi nakuhakikishia
baba haya mambo nitayamaliza mwenyewe,…niamini baba…’nikasema
‘Una uhakika …..?’ akaniuliza, baba akikuuliza hivyo ujue hilo
jambo analifahamu , anakupima tu.
‘Baba…’nikasema na yeye akageuka kuangalia nyuma, ..nahisi alikuwa
akimuangalia docta, nikaangalia kule anapoangalia, lakini docta hakuwepo..sijui
alikuwa kaenda wapi…lakini badala yake nilimuona jamaa mmoja kasimama, akiwa anatuangalia..alipoona
baba anamuangalia, kwa haraka akaja alikuwa kashikilia bahasha kubwa mkononi
‘Binti yangu..nilikuwa safarini, lakini hata nikiwa huko nimekuwa
nikiiwazia familia yangu, na familia yangu ni pamoja na wewe…mimi nina hisa
kwenye kampuni zenu, nilifanya hivyo makusudi, maana siwezi kutoa pesa zangu ziwekezwe tu,
bila ya mimi kujua kinachoendelea,....hii hapa ni taarifa ya kibishara ya
kampuni yako na mumeo ..umeshawahi kuipitia vyema…?’ akauliza
‘Ndi-ndio baba lakini….eeh, kuna matukio mengi yamepita hapa
karibu, sijapata muda wa kuipitia vyema, ila naifanyia kazi, kwangu, kwa mume
wangu sijawahi kukaa naye, sijui kinachoendelea, nitakaa naye nione tatizo lipo
wapi…’nikasema
‘Kwanini biashara imeshuka kiasi hiki, hasa ya mumeo…?’ akauliza
‘Baba ni hali halisi, sio sisi tu,…na ngoja nitakuja kuipitia,
mimi nina nakala zangu, au hii ni nyingine zaidi..?’nikasema
‘Na hizo pesa nyingi alizochukua mumeo, ni za nini, ni kwa ajili
ya nini, umeshawahi kumuulizia mumeo pesa hizo kazifanyia nini…?’ akauliza
‘Pesa gani baba…?’ nikauliza maana sijui kama mume wangu alichukua
pesa nyingi kwenye kampuni yake, mimi siingilii kampuni ya mume wangu.
‘Anyway..hilo sio tatizo
kwa sasa…, lakini ndani ya bahasha hiyo kuna kitu kingine, kuna taarifa ya
biashata ya mumeo pia, na mengine utakuja kuyaangalia humo ndani, halafu
tutaongea…utaniambia hayo yote yana maana gani..’akasema
‘Sawa baba, nita-ipitia..’nikasema
‘Na kingine je wewe unakubaliana na hali hiyo ya mumeo …au ni
maisha gani mnaishi hivyo…, nataka majibu kutoka kwako, sio leo, tukikutana
unanielewa, maana hujalelewa hivyo, sitaki aibu kabisa....’akasema
Alinikabidhi ile bahasha, na kwa mashaka nikaipokea, na kabla
sijataka kufanya chochote, akasema;
‘Ile hali ya mumeo itachukua muda kupona….na ina maana shughuli nyingi
alizokuwa akizisimamia yeye, zitasimama, na..zaidi hatujui mapesa yote
aliyochota aliyachukua kufanyia nini…sasa, kazi ni kwako, kabla mumeo
hajazindukana, ulifanyie hilo kazi, fuatilia kinachoendelea , baada ya hapo,
mimi mwenyewe, nitajua la kufanya, sikutoa mataji wangu upotee bure, umenielewa…’akaangalia
saa yake.
‘Baba hapa sio mahali pa kuulizana maswala ya biashara baba…mume
wangu yupo hali mbaya, nina mawazo kuhusu afya yake, nipe muda kidogo kwa haya…,
naomba hayo tuyaache kwanza…’nikasema
‘Haya, ninayokuuliza....ni moja ya sababu ya kuchanganyikiwa kwa
mumeo, kuna mengine kati yako na yeye, usipoziba ufa utajenga ukuta, akipona
akirudia tena, itakuwaje,..ni bora ujua cha kufanya kuanzia sasa..’akasema
‘Sawa baba nimekuelewa…’nikasema
‘Kuna maelezo muhimu humo, ila mengine..eeh yanafanyiwa kazi, ikithibitishwa
kuwa ni kweli…unajua ni nini kitafuta,…maana tulishakubaliana hilo, na sitarudi
nyuma tena, unanielewa…?’ akauliza nakabla sijamjibu akasema
‘Nilikuambia na narudia tena,…kunguru hafugiki, sasa yanaanza
kujitokeza, usizarau maneno ya wazee wako, ukataka kushindana nao, sasa ni lako
hili, ila lisiharibu familia yangu kwa ujumla, sitarudia tena hili…’akasema
Hapo nikabakia kimia tu…nikiwa nimeishikilia ile bahasha kubwa
mkononi.
‘Mume wako, ….kabla niliwahi kuongea naye, nikamwambia nikirudi
nahitajia majibu na maelezo…. sasa sijui ni sababu hiyo au kuna jambo jingine,
nahisi pia kuna jambo jingine limejitokeza…ila ninachotaka isije ikawa ni
kashfa kwenye familia…sitavumilia hilo kabisa…’akasema.
‘Sawa baba, nina imani hiyo, kuwa hakuna kashfa mbaya….’nikasema
‘Na iwe hivyo, na iwe-hivyo,….’akasema akiangalia saa
‘Sawa baba, niamini mimi…hakuna jambo baya …’nikasema
‘Na huyo rafiki yako, unamuamini sana eeh…’akaniuliza
‘Yupi baba…?’ nikauliza
‘Huyo mzazi….’akasema na mimi hapo moyo ukalipuka paah.
‘Baba huyo ana nini tena…’nikasema
‘Najua unamtetea sana,…, niliwahi kukuambia, unachokifanya wewe,
ni kama kufuga nyoka mwenye sumu chumbani kwako, ipo siku atakuuma wewe
mwenyewe, sikiliza binti, huwezi
kumbadili mtu aliyeshindikana na wazazi wake, hu-we-zi, umepanda mbegu juu ya
jiwe…’akasema
Hapo nikakaa kimia,… nilikawa nawaza mbali kuwa huenda docta ndiye anafanya kazi na baba, anachukua
kwangu anayapeleka kwa baba, na hili la rafiki yangu inaokena limekwenda mbali,
litanisumbua sana, sasa nitafanya nini…lakini moyoni, nikajipa imani kuwa
nitalimaliza mimi na huyo rafiki yangu..sizani kama kuna jambo kubwa kiasi hicho.
‘Huyo rafiki yako, ndiye atakayekuangamiza,..unajua kuwa yeye anashirikiana
na mume wako…?’akasema kama ananiuliza, na mimi hapo nikamwangalia baba yangu
kwa macho ya mshangao, ila sikuwa nimemuelewa ana maana gani hapo…
‘Anashirikiana na mume wangu, kwenye nini baba, hapana, ni kawaida
tu….!!’nikasema kwa mshangao.
‘Una uhakika…’akauliza na mimi nikakaa kimia
‘Ndio maana nakuambia…kuna tatizo, na tatizo hilo linaweza kuleta
taswira mbaya kwenye familia, na …narudia tena sitaki kashfa mbaya kwenye
familia yangu, muuguze mume wako apone,…na apone kweli, maana sitarudia tena.
….’akasema na kuondoka.
************
‘Huyo-huyo rafiki yako,
ndiye atakayekuangamiza, akishirikiana na mume wako…’ ilikuwa sauti
iliyokuwa imebakia akilini mwangu, na kunifanya niduwae kwa muda, hadi pale
nilipohisi mtu kunikaribia.
Nikainua kichwa kuangalia ni nani huyo, …alikuwa ni docta.
‘Vipi, mwenzako ndio keshaondoka….?’ Akaniuliza docta
‘Wewe ulikuwa wapi..?’ nikamuuliza swali kabla sijajibu swali
‘Unajua nilimuona docta kwa mbali, akitoka, nikaamua kumkimbilia
kumuwahi kabla hajaondoka, kwahiyo sikuweza kuwaambia,…na kweli alikuwa
akitoka, ,…na nimeweza kuongea naye na
kwenda kumuangalia mume wako, bado amelala, ila yupo sawa, hana tatizo….’akasema
‘Kwahiyo mimi siwezi kwenda kumuona…?’ nikauliza
‘Kwa mujibu wa dakitari, ndio huwezi kwenda kumuona, kwa vile
anatakiwa kulala ili dawa zifanye kazi....ila unaweza kwenda kumuona tu, kwa
mbali, kama unataka, muhimu usije kumghasi, mpaka hapo atakapozindukana kutoka
usingizini yeye mwenyewe, …’akasema
‘Oh….hata hivyo, ni bora nikamuone tu…’nikasema
‘Sawa twende….’akaanza kutembea kuelekea huko alipolazwa mume
wangu, na mimi nikawa namfuatilia kwa nyuma hadi chumba alicholazwa mume wangu,
alikuwa kweli kalala, ..nilimuangalia kwa muda, na kuhis machozi yakinilenga
lenga, akilini sikuwa na wazo jingine zaidi ya kumuombea apone haraka
iwezekanavyo.
‘Haya umemuona, …twende maana tumejiiba tu, haitakiwi mtu kuja
kumghasi, mpaka wakija kuhakikisha kuwa sasa hana maumivu tena….’akasema,
lakini nilikuwa kama simsikii, hadi pale aliponishika mkono na kunivuta
tuondoke humo ndani.
‘Mume wangu jamani…’nikasema
‘Atapona ….’akasema docta
*********
Tulipokuwa nje, docta
akaniuliza;
‘Kwanini rafiki yako kaondoka kwa haraka hivyo, tuiliongea nini na
wewe umafanya nini, ..kuna kitu gani mnataka kukificha, mimi, eeh...nilikuwa
nataka kuongea naye maswala mengine….’akasema.
‘Ulitaka kumuona mtoto ili utake kuthibitisha uvumi na hisia zako,
au…ndio keshaondoka hivyo, ..’nikasema.
‘Haya sawa, hamna shida, unaonaje sasa twende nyumbani,…maana kwa
hivi sasa utakaa tu, na kwa mahesabu yao, mgonjwa ataamuka baada ya kama masaa
manne hivi,…chini au juu ya hapo… na akiamuka watamchunguza kwanza..ili
kuhakikisha kama yupo sawa kabla hawajawaruhusu watu kuongea naye, ….’akasema
‘Sawa…’nikasema hivyo tu, na tukatoka hadi tulipoweka magari yetu,
kila mmoja akaingia kwenye gari lake na ikawa ni safari ya kurudi nyumbani. Na
sikutaka kabisa kusimama kwa docta, moja kwa moja nikaelekea nyumbani kwangu.
Nilipofika kwangu, kwa haraka nikampigia
simu rafiki yangu.
Kwanza simu iliita kwa muda bila kupokelewa, …nikatulia dakika
moja hivi nikapiga tena, ikawa hivyo hivyo,…lakini wakati inataka kukatika, ndio
ikapokelewa, na mimi nikamuuliza mdada, kwa haraka ni kwanini hapokei simu
anajua namuitia nini.., yeye akajibu kwa haraka tu;
‘Nilikuwa naanika nguo za mtoto nje, sikuweza kusikia simu ikiita,
na wakati naingia ndio nikasikia ikiita, nikaiwahi, habari za mgonjwa, kuna
lolote jipya tangia tuachane….?’akasema na kuniuliza.
‘Vipi umefikia wapi, au umeamuaje..?’ nikamuuliza , bila kujibu
swali lake
‘Mhh…nimeongea na watu wa usalama barabarani kujua kinachoendelea
kwanza, wamenipa picha halisi ya ajali yenyewe,…nilikuwa sijaipata hiyo, zaidi
ya kusikia kwa watu, sasa nimeweza kujua ajali ilivyotokea…zaidi ni mwendo kasi
na wakati anakata kona kuingie ile bara bara nyingine ndio wakakutana na lori, …kiukweli
ni ajali mbaya…’akasema
‘Ndio hivyo, …kwahiyo umeshaianza hiyo kazi…au..?’nikamuuliza
‘Ndio nimeianza hivyo…bo-si’akasema na kumalizia neno la mwisho
kwa kukata
‘Najua umetoka kujifungua na ulihitajia muda wa kupumzika, hilo
nalifahamu sana, na sikuona kama kazi hii ina uzito wa kukufanya ushindwe
kuifanya kutokana na hiyo hali,…’nikasema, na nilisikia mlio wa simu kuingia,
sijui ni ya kwake au ni yangu
‘Nitaangalia….’akasema, nahisi alitaka kukata simu.
‘Mimi nionavyo, ni kazi unayoweza kuifanya hata bila ya kutumia
nguvu, kwani wewe una vyanzo vyako vingi vya kukusaidia bila ya hata ya wewe
kutoka hapo nyumbani kwako..'nikasema
'Sawa...'akasema
'Cha..., muhimu ni kuhakikisha kabla hawajafanikiwa watu
wengine kujenga hoja za fitina, uwe umeshajua ni nini kinachoendelea, na je umeshaweka mikakati yako tayari...?’ nikamuuliza, nikasikia
mlio wa kuingia ujumbe nahisi ni simu yake.
‘Sawa nimekuelewa …’akatulia kwa muda, halafu akasema
‘Bosi…, nafahamu nipo kwenye mkataba na wewe, na niwajibu wangu
kutimiza kila utakachoniambia, lakini nilitaka nikuweke wazi, kabla ya kazi
yenyewe ndio maana uliniona nasita sita...’akasema sasa kwa sauti ya kujiamini
kidogo.
‘Kwahiyo umeshaelewa, au bado unasita sita, …’nikasema
‘Nitafanya kama utakavyo, hamna shida…na nilimuona baba yako, hapo
hospitalini,....mliongea nini na yeye au…?’ akaniuliza.
‘Ni mambo ya baba na binti yake, ..ni yale yale…yeye hawezi
kunizuia mimi nisifanye kazi yangu, ila kuna jambo..ndio maana nataka ulifanyie
kazi, kabla mambo hayajawa mabaya ....’nikasema
‘Sawa..nitaifanya tu, hamna shida… ila nami unielewe, ndio
nimetoka kujifungua, kitoto changu bado kichanga, hali yangu bado haijawa safi,
nahitajia muda wa kutulia kwanza, nahitaji muda wa kukaa na mwanangu na pia
nipo kwenye maandalizi ya ile safari ya kwenda nje kusoma, kwahiyo huenda nisiifanye
hiyo kazi kwa muda unaotaka wewe,.....’akasema rafiki yangu huyo.
‘Hamna shida, mimi naelewa hilo….ila fanya uwezevyo, kabla wengine
hawajagundua lolote, kama kuna kashfa ya mume wangu nataka niifahamu mapema ni
kashafa gani, na …mengine nitayafanyia kazi mimi mwenyewe …’nikasema
‘Hamna shida, nitafanya hivyo…bosi…’akasema kwa kujiamini.
Ndio hapo nikakumbuka ile bahasha,..
‘Haya badae nitakupigia…’nikasema na kukata simu.
Nikakumbuka kuwa
sikuichukua ile bahasha kwenye gari, haraka haraka hizi bwana, na mawazo mengi
kichwani,….nikatoka hadi kwenye gari, ..nakumbuka niliiweka kwenye kiti cha
mbele, kwanza nikawasha kiwambo cha gari ile niweze kufungua mlango,..kwa
haraka nikafungua mlango,
Hakuna kitu…! Bahasha haipo….!
‘Haiwezekani…’nikasema nikikagua kila mahali, na kujaribu kuvuta
hisia za kumbukumbu yangu kuwa labda niliondoka nayo, …hakuna kitu….
‘Nina uhakika sikuondoka nayo!..ilikuwa hapa..’nikasema mwenyewe.
Mara simu yangu ikaita,…nikaangalia, alikuwa ni docta
‘Unasemaje , una mzigo wangu…?’ nikajikuta namuuliza hivyo kwa
haraka.
‘Mzigo gani…?! ‘akauliza kwa mshangao, halafu akaendelea kusema
‘Nataka kukuambia hivi, wakati tunakuja,…nikiwa nyumba yako,
..niliona kama kuna mtu alikuwa akikufuatilia kwa pikipiki,…hukumuona…?’
akauliza
‘Hapana…sikuwa makini kukagua nje. Mbona zilikuwa pikipiki nyingi
tu, una uhakika ….ni nani…?’ nikasema na kuuliza
‘Lakini sizani kama alikuwa na nia mbaya, mimi nilipoona
kapitiliza ulipokuwa unaingia kwako, nikajua labda ni hisia zangu tu, kuna
lolote limetokea…?’ akaniuliza
‘Huyo mtu aliishia wapi, hakuingia kwangu…?’ nikamuuliza
‘Alipitiliza, hakusimama, sikumuona akisimama,..kwani kuna
tatizo…?’ akauliza
‘Hakuna tatizo,..ila…lakini sina uhakika, kuna kitu wamechukua
kwenye gari langu…’nikasema
‘Haiwezekani, muda gani sasa huo..! Ina maana labda,… alirudi
akaingia kwako, maana mimi nilipoona kapitiliza, niliingia kwangu, siwezi kujua
kama alirudi au laa..hakuna mtu hapo nje kwako unaweza kumuulizia…?’ akasema
‘Hamna shida, sio kitu muhimu sana…’nikasema
‘Kama wamehangaika kukichukua, kitakuwa muhimu kwao..jaribu
kufanya uchunguzi…na kama unahitajia msaada wangu niambi..’akasema, na mimi
nikakata simu,
Nilipokata simu kuongea na docta,nikatoka nje na kukagua..sikuona
dalili ya mtu, hata gari,…sikuona dalili kuwa mtu alilifungua, kwa vipi lakini…nikataka
kumpigia rafiki yangu simu, yeye ndiye msaada wangu wa vitu kama hivi, lakini kabla
sijaanza kupiga simu, simu ikaanza kuita, ….alikuwa ni baba!
NB: mambo ni mengi lakini tutafika tu
WAZO LA LEO: Wahenga walisema hata mbuyu ilianza kama
mchicha au mche wa harage ukichipua..Na hata matatizo, yana chanzo chake, kidogo
kidogo huja kuwa tatizo kubwa, …nibora kuchukua tahadhari kabla tatizo halijawa
kubwa, tusizarau matatizo, na kuyasubirisha , kama lawezekana kushughulikiwa
lifanyie kazi haraka iwezekanavyo, ya leo yaweza yasiwe ya kesho.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment