Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, November 7, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-21



‘Docta ana mambo yake, ana shuku shuku zake..mimi sijamuelewa, najua ni kwanini,…muhimu kwangu, wewe uifanye hiyo kazi niliyokupa…sasa.., wewe ondoka ukaianze hiyo kazi mara moja, mengine niache mimi na docta tutayamaliza…’

Tuendelee na kisa chetu….

***************


Docta alikuwa anakuja, akiwa kashikilia simu yake mkononi, kama anaandika kitu kwenye simu yake, nahisi alikuwa akiongea na mtu fulani muhimu kwake…kuna muda alikuwa akiongea huku anageuka kidogo kutuangalia, ikanipa mashaka kuwa huyo anayeongea naye, anaweza akawa na jambo na sisi..lakini sikuwa na shaka na hilo.

Niliona kamaliza kuongea na sasa alikuwa akija pale tulipokaa mimi na rafiki yangu, lakini  alikuwa hatuangalii, anaangalia simu yake,.. na alipotukaribia tu ,simu yake ikaita tena, ikabidi ageuka na kurudi pale  alipokuwa awali, akaendelea kuongea na simu yake, na kwa muda huo rafiki yangu alikuwa kasimama hajui afanye nini,…

‘Sasa wewe unasubiria nini, nenda kaifanye hiyo kazi, ukimsubiria docta…akija hapa, ataanza kukudodosa, kwa maswali mengi ya ujanja ujanja…na lengo lake jingine anataka kumuona mtoto, nahisi kuna jambo analifahamu, anataka kulithibitisha,..au kuna jambo analifuatilia….’ nikasema hivyo.

‘Mhh,…ni kweli naondoka…ila mimi sijakuelewa hapo.., maana unachotaka ni kama mtu kuchunguza kivuli chako, ni mambo ambayo hata wewe mwenyewe unayafahamu,..’akasema

‘Nayafahamu kwa vipi, sijakuambia uchunguze mambo yetu, mimi ninachotaka ni wewe kuchunguza hili tukio la mume wangu, chanzo chake, na ni nini kipo nyuma ya haya yote, unajua…mimi sitaki mambo ya kusikia,..nataka ukweli, nataka uhakika,..sawa hisia hizo zipo, watu wanasema hili na lile, lakini mimi sio mtu wa kihivyo….nataka tuupate ukweli…’nikasema

‘Kwahiyo eeh, hili….’akasema na kabla hajamaliza, nikamkatiza kwa kusema;

‘Sitaki nikufundishe kazi…. siku zote nikikuelekeza kazi unasema nisikufundishe nimeshakupa kazi basi nikuachie wewe mwenyewe utajua jinsi gani ya kuifanya,…iweje leo,  kulikoni, unajua naanza kukutilia mashaka,…’nikasema na yeye hapo akabakia kimia.

‘Katika jambo silitaki, ni kuwatilia mashaka watu wangu ninaowaamini…wewe nakuamini sana, nilikupeleka shule usomee ujasiri, ujua jinsi gani ya kujilinda, na uje kunisaidia na mimi, …unilinde kwa kila hali, unakumbuka, uliapa mbele yangu, ndio, urafiki upo pale pale, lakini mengine ni dhima, unanielewa hapo….’nikasema

‘Aaah,..ndio..naelewa…lakini kabla sijaifanya hii kazi, ni lazima tukubaliane…eeh, kuna utata hapa…’akasema

‘Kukubaliana husu malipo au, kama ni malipo hakuna shida, toka lini nikakupa kazi bila kukulipa, wewe angalia gharama zako nipatie ankara ya deni,…au unataka kusema nini…?’

‘Kwahiyo, mmh, unataka nimchunguze shemeji….mmmh….’akasema

‘Ndio…umchunguze, …kwa masilahi yake, na masilahi ya familia,….fanya ufanyalo, ila cha muhimu, nakuomba, na nasisitiza, mimi sitaki kashifa kwenye familia yangu, ..na hili tumeshaonywa na wazazi wangu mara nyingi, hata wewe uliwahi kusikia wakati baba akiongea, ..sasa kama kuna tatizo nataka tuliwahi mapema kabla halijafika kwa wazazi wangu,...’nikasema

‘Nikuulize tu, samahani bosi… kabla sijaondoka, sasa kama ni kweli  mume wako kahusika na hicho unachokiita kashfa,..itakuwaje…?’ akauliza na mimi nikamuangalia kwa macho makali, nikasema

‘Ninacho-kiita mimi kashfa..una maana gani, lugha gani hiyo…..ok, sikiliza…mimi sitalivumilia kashfa yoyote kwenye familia yangu, hasa zile zenye kuharibu biashara, zenye kuharibu ndoa, zenye kuleta jina baya kwenye familia yangu, zote unazielewa..sitake nianza kuzitaja…’nikasema

‘Mhh…’akaguna hivyo.

‘Wazazi wangu unawafahamu walivyo, walinikataza nisioane na huyo mume wangu kisa ni kuhusu familia yao, kuwa eti imegubikwa na mambo hayo…mimi sikuamini hayo, najau tabia mtu anaijenga mwenyewe..mimi niliwahakikishia wazazi wangu kuwa kashfa mbaya hataiweza kutokea kwenye familia yangu…’nikasema

‘Lakini kashfa yaweza kutafsiriwa vingine,..kama jambo limefanyika kwa makubaliano linawezaje kuwa ni kashfa…muhimu tuliweke sawa,..kuna mambo labda yalifanyika hivyo, sasa labda imekuwa kinyume kutokana na kutokuelewana…sasa sizani ni kama ni kashfa, labda iwe ni kashafa kwa mtizamo wa watu wengine……’akasema

‘Kwa makubaliani!!! Weeeeh, makubaliano na nani..kuwa mimi nitendewe ubaya, kwa vipi sasa, kuwa mume wangu, mbona haiji akilini… kuwa yeye akazini nje ya ndoa au, tuchukulie kashfa hiyo ni ya ndoa, mimi sijui..yaani mimi, nikae na mume wangu kuwa akafanye hivyo,…au nimwambie mume wangu akaibe au..najua mume wangu hawezi kufanya hivyo, hata siku moja,..na mimi sio kichaa wa kukubaliana na ujinga kama huo, hata dunia itanicheka au unataka kusema nini…’nikasema.

‘Sawa…lakini nikuulize kitu kingine kutokana na hali ya shemeji, ukagundua kuwa kafanya hivyo, na hali kama hiyo, .. utachukua hatua gani, huoni unaweza kumuua mume wako bure....?’ akaniuliza na mimi nikageuka kumuangalia docta, alikuwa bado anaongea na simu, nikasema.

‘Kwanza tujue ukweli, unanielewa,, ....cha kufanya baada ya ukweli.. , nitajua mimi  mwenyewe, hiyo sio kazi yako… ila kiukweli, kama ni kweli wanavyosema watu mimi bado siamini,…huyo aliyemghilibu mume wangu, huyo shetani mtu…kama kweli kaghilibiwa, maana mume wangu hakuwa na tabia hiyo,..huyo mtu, huyo shetani,,… nitahakikisha kuwa  hanisahau maishani , na atajuta kuingilia ndoa za watu kupoje…’nikasema kwa ukali, na uso wangu ukiwa sasa umebadilika kabisa,….

Mdada aliniangalia usoni, akionyesha wasiwasi mkubwa, mpaka, akawa anarudi kinyume nyume..halafu akasimama ..rafiki yangu  ni jasiri..alipitia mafunzo ya ujasiri, kwahiyo anajua aweje kwa wakati gani…, lakini kwa hali aliyoniona nayo usoni nahisi hakutarajia,…kabisa….

‘Ina maana utamuua au,…ha-ha- hata kama…?’ akaniuliza akionyesha wasiwasi, akasita kumalizia.

‘Wewe subiria tu…utaona nitakachokifanya, unajua nimevumilia sana, nimekuwa mtu wa watu, nawapenda sana watu wangu wa karibu, nawabeba kwa mbereko....sasa ina maana kwa hali hiyo watu wanipande hadi kichwani, hapana,..hata awe ni nani …’nikasema


‘Mhh, rafiki yangu siamini hili kabisa, lakini mume wako ni mtu mwema sana, na kama kafikia kulifanya lolote baya, atakuwa na sababu…sizani kama anaweza kufanya jambo ambalo analifahamu ni kinyume ..msamehe tu…’akasema

‘Nimsamehe nini sasa…kwanza, eeh, nisikilize, sio tukurupuke, kwanza, tujue kosa lake ni lipi,…ili tujue jinsii ya kumsaidia,…unajua  yapo makosa ya kusamehe, mimi ni binadamu, nitayapima, …lakini sio kosa la kuingilia ndoa za watu…watu hao wanatakiwa kuuwawa…unasikia, ku-uwawa, sasa mimi niwachekee, ndoa sio kitu cha mchezo bibie…, ..’nikasema

‘Sikiliza…mimi naomba urejee yale mazungumzo yetu, mbona….’akasema

‘Mbona mbona nini…ile ni kitu kingine…najua unachotaka kukisema…ndio maana nilikusihi iwe siri…sasa kama na wewe umelikoroga huko, acha mwenye mali afanye kazi, yake utajua mwenyewe, na mimi natetea ndoa yangu…sasa nikuulize uUtaifanya hiyo kazi au huwezi nimpatie mtu mwingine..’nikasema kikazi zaidi.


‘Mimi naona sitaiweza hiyo kazi, ..na ukizingatia nina mtoto, si unajua tena….’akasema

‘Sikiliza, sitaki kusikia kauli hiyo…na nataka uifanye wewe….na nataka iwe siri kubwa, unanielewa, siri kubwa,  sitaki watu wengine waje kuligundua hilo kabla yako, kuna watu wameshaanza kutaka kulifuatilia hilo tatizo la mume wangu,  wanataka kujua kwanini mume wangu akawa hivyo,…hiyo ajali sio ya kawaida,…wameshaanza kutunga hadithi…najua wakitaka jambo watalipata tu…’nikasema

‘Akina nani hao…?’ akaniuliza akionyesha mashaka

‘Docta anataka na yeye kulichunguza kwa nia ya kumsaidia rafiki yake, najua sio hivyo tu,…najua kabisa… wazazi wangu watakuwa wamemtuma kufanya hivyo,…sasa sitaki aje kugundua kitu kabla ya yako, nataka wewe ukishagundua tunahakikisha hakijulikani kitu tena…unanisikia, umeona jinsi gani jambo hilo lilivyo nyeti,…umenielewa hapo…’nikasema

‘Mhh, mbona imekuwa ni tatizo, sikujua kuwa haya yote yanaweza kutokea,…sasa huyu docta anataka kutafuta nini,…ina maana ndio maana umeniita hapa, ili…na wazazi wako wanalifuatilia hili, mungu wangu …mimi sasa naanza kuogopa, naona nijiondokee tu kwenda kusoma haraka iwezekanavyo, ….’akasema sasa akirudi kinyume nyume

‘Sikiliza wewe ni rafiki yangu ninayekuamini, ndio maana kila kitu tunaambizana, na huwa tunashauriana kwa kila jambo, sawa si sawa....wewe ndio mimi, na wewe huwezi kufanya jambo la siri kinyume na makubaliano yetu, sizani kama wewe unaweza kunigeuka mimi…nimekuwa nikikulinda kwa kila hali, mpaka sasa.…’nikatulia

‘Ni kweli….’akasema sasa akiwa kainama chini kama mtoto mbele ya wazazi wake akiwa kakosa au kuona aibu. Ni lazima awe hivyo kwangu mimi licha ya urafiki lakini mimi nimekuwa kama mlezi, nilitumia gharama nyingi kumjenga huyu binti kutoka kwenye hali ya kukata tamaa hadi akafikia sehemu ya kujiamini..

***********

Rafiki yangu huyu, niliamua kumsaidia  kutoka kwa wazazi wake, hii ni kutokana na ule ukaribu wetu, sikutaka nimsaidie kipesa tu, lakini pia kumjenga katika hali ambayo anaweza kufanya jambo lake kwa kujiamini.

Sisi kwenye familia yetu japokuwa tuna uwezo, lakini wazazi wetu walifanya juhudi kubwa ya kutujenga kihali ambayo mtu anaweza kufanya jambo bila kutegemea wazazi, walitujenga kujiajiri zaidi, pamoja na elimu yetu, na mimi nikaona nimsaidie rafiki yangu awe hivyo hivyo...

Wazazi wake kuna kipindi walitaka binti yao aolewe na mtu waliyeona kuwa atamfaa, na binti yao hakuwa tayari naye, kama alivyokuwa hayupo tayari kwa wanaume wengi waliomtaka kumuoa kabla ya huyo ambaye wazazi wake, waliamua kumshurutisha aolewe naye...ndio maana tatizo lake nikalichukulia sawa na la kwangu..kuwa hata mimi nilikataa kuolewa na chagua la wazazi wangu

‘Hawa wazazi wangu siwaelewi, kama wamenichoka, na huenda wanaona mimi ni mzigo kwao, waniambie, lakini sio kunitafutia mwanaume,....hivi wananionaje mimi, eti niolewe na yule mzee, ..eti kwa vile ni tajiri, ....hapana, siwezi kuishi na yule mzee, hata siku moja....’akaniambia.

‘Lakini yule sio mzee,ukiangalai umri wako na yeye, huwezi kumuita yule mzee, yule ni saizi yako kabisa, au unataka kuolewa na dogodogo, usidanganyike, huko umeshakupita, sio kwako tena, huyo unayemuona ni mzee, ndiye saizi yako...’nikamshauri.

‘Simpendi, na simtaki....’akasema na mimi nikamuelewa, nikaona nimsaidie na nione vipi nitaweza kumfanya aishi maisha bila ya kutegemea wazazi wake, , kwani kwa muda huo alikuwa ameshakosana na wazazi wake  kabisa..na wazazi wake, walisema kuwa binti yao huyo kazidi kwani kila mchumba anayemfuata yeye anamkataa,

‘Basi rafiki yangu mimi naona nikusaidie kwa hilo, unaonaje tukiwa washirika, ....?’ nikamuuliza.

‘Washirika kwa vipi, sisi ni marafiki tangia zamani, hilo la ushirika la kitu gani tena,…?’ akauliza.

Mimi namfahamu sana rafiki yangu huyo , hawezi kupata kazi ya kuajiriwa akatulia, sizani kama anaweza kuhimili sheria na taratibu za kazi, mara ngapi anaajiriwa na baada ya hata mwezi kuisha keshakosana na muajiri wake,...nikataka nimbadili kabisa aondokane na hulika hiyo, japokuwa hiyo ya kuchagua wanaume nilishindwa.

Nakumbuka wakati tunasoma rafiki yangu huyu alikuwa akipenda sana kazi za upelelezi, kutokana na kusoma vitabu mbali mbali vya hadithi za kipelelezi, na kuangalia sinema za namna hiyo,na hiyo ilikuwa ni ndoto yake kuwa akimaliza shule atajiunga na kazi za upelelezi.

Kwa bahati mbaya, ndoto yake hiyo haikuweza kufanikiwa, tulipomaliza shule, akajikuta akifanya kazi nyingine kutokana na matakwa ya wazazi wake, ambazo hakuweza kuzifanya itakiwavyo, akaanza kutafuta sehemu nyingine, na hata huko hakuweza kukaa muda mrefu,ikawa mtu wa kubadili kazi, mara leo yupo hapa , kesho yupo kule.

Basi siku hiyo alipokuja kwangu na malalamiko hayo juu ya wazazi wake, kutaka aolewe, mimi nikakumbuka ile ndoto yake hiyo, nikaona kwa vile tumekuwa watu wakusaidiana, kupendana, toka utotoni, ngoja na mimi nijaribu kumsaidia nionavyo mimi, na ndipo nikamapa wazo langu hilo nikamwambia;

‘Rafiki yangu mimi nataka kuifufua ile ndoyo yako ya shuleni, upo tayari....?’nikamwambia na yeye akawa kama hakunisikia,kwani wakati huo alikuwa anacheza na simu yake, nafikiri alikuwa akiandika ujumbe kwa watu wake, na baadaye akasema;

‘Ndoto ipi...?’ akaniuliza kwa dharau, na huku akiendelea kuangalia simu yake.

‘Kwanza rafiki yangu nakutaka unielewe, nikiongea na wewe uhakikishe kweli unaongea na mimi, ....kama bado una tabia za utoto, hutafika mbali, weka hiyo simu pembeni, nataka tuongee kikubwa....’nikasema kwa sauti ya ukali, na yeye aliponiangalia usoni akakutana na uso wa kazi, uso unaoashiria amri, akashangaa, kwanza, halafu akabetua mdomo, na kusema.

‘Ok. Bosi, maana kwa vile wewe ni bosi kwenye kampuni zako unafikiria kila mtu utamsimamia hivyo hivyo..lakini kwa vile nimekwama, nitakusikiliza bosi....’akasema huku akiiweka simu yake pembeni.

‘Nakumbuka wewe ulikuwa na ndoto ya kuwa askari mpelelezi...lakini haikuwezekana, sasa nataka hilo liwezekane, hujachelewa, utakwenda kusomea hilo, lakini sio askari mpelelezi wa kipolisi, nataka uwe mpelelezi wa watu binafsi,...mpelelezi muhutasi,  hiyo si inawezekana...?’ nikamuuliza. Na yeye kwanza akawa kama haamini hilo kwani muda umeshapita, na huenda hakuwa na wazo hilo tena.

‘Mhh, hilo nilishalitoa akilini, hayo yalikuwa ya kishule, ...sijui kama inawezekana, sina uhakika na hilo.na hiyo kazi inapatika kweli, maana nahisi nitahitajika kwenda jeshini, na huu mwili sizani kama utakubali shuruba, na amri.....’akasema.

‘Inawekana,....kwanini isiwezekane, kila kitu ni nia, kila kitu ni utashi, na dhamira ya kweli, sasa hivi vipo vyuo vingi tu vya kutoa hayo mafunzo, na hata kwenye mitandao kuna elimu kama hiyo, tuifanyie kazi, ...na na kwa vile mimi nakuhitajia kwenye mambo yangu,...tushirikiane, tutaweza...upo tayari....?’nikamuuliza.

‘Sijui...tuone ,..’akasema na mimi nikafahamu kuwa yupo tayari, nikamwambia ili aonyeshe dhamira ya kweli, basi ahangaike mwenyewe kuvitafuta hivyo vyuo, na mimi nitamsaidia kwa hali na mali. Na kweli baada ya siku kadhaa akasema keshapata chuo cha namna hiyo, na yupo tayari kwa masomo, na mimi nikamwambia nitawasiliana na wahusika wa hicho chuo.

‘Kwani ni mpaka wewe uwasiliane nao, cha muhimu ni maombi, na maombi nimeshatuma na wao wameshanikubali, kilichobakia na malipo..hakuna zaidi....’akasema.

‘Usijali..malipo nitalipa, lakini kama nilivyokuambia, mafunzo hayo ni kwa ajili ya kazi zangu, kwahiyo nataka niongee nao, nione jinsi gani wanaweza kukupika nitakavyo mimi....’nikasema na kweli nikaenda kuonana na wahusika wa hicho chuo, na tutakakubaliana, kwani nilitaka kwanza wamjenge huyo binti kikakamavu, na kuondoa ulegelege wa kutegemea wazazi,..na wao wakasema hiyo kwao ni kazi ndogo tu.

Sikuamini, huenda ni kwa vile, alikuwa na ndoto hiyo, au ni dhamira tu, ilimtuma ajitume hivyo, kwani, aliweza, na akafuzu vizuri sana, na kuna muda aliombwa ajiunge na askari polisi, lakini yeye mwenyewe alikataa, na akaja kwangu na kusema yupo tayari kwa kazi zangu, na tukaingia naye mkataba, akawa ni mtu wangu nikimuhitajia, lakini hapo hapo akawa kaajiriwa kwenye kazi fulani.

Nikawa kila nikipata kazi inayohitajia mambo hayo, nimampa ananifanyia, namlipa vizuri tu, au wakati mwingine anapata kazi zake nyingine binafsi akikutana na mawakili binafsi kuchunguza kesi fulani, basi ikawa ndio kazi yake nje ya ajira yake.

Kwa hali kama hiyo tukawa ni kitu kimoja, na kikazi mimi ni bosi wake, na  haikutokea siku nikampa kazi, akaikataa,...

Kwahiyo ni mtu nilishibana naye, na ananiheshimu mimi na familia yangu, na alishaapa kuwa hataweza kunifanyia jambo baya,…je kwa hali kama hiyo ninaweza kuamini mambo ya kusikia tu…hapana, ilihitajia mud asana kuyaamini maneno ya watu

****************
‘Kwahiyo umenielewa, nikamuuliza , wakato docta naye anaongea na simu

‘Nitafanyaje sasa..inabidi…’akasema

‘Unajua ni kwanini nataka hili, ni ili  jamii isije kuniona mimi mjinga, kuwa nafuga nyoka,…hilo linawezekana kweli, kuwa nilifanya yote hayo kwa mtu ambaye atakuja kunizunguka, …’nikasema

‘Lakini…..’akataka kujitetea

‘Sikiliza…mimi sitakubaliana na mawazo yao hata mara moja kuwa wewe rafiki yangu unaweza kunisaliti mimi, nitauweka wapi uso wangu…sasa ni wewe kuilinda hiyo hali, sizani kama unaweza kufanya jambo kama hilo…sizani, …au ..niambie ukweli hapa hapa, je ni kweli…?’ nikamuuliza

 ‘Mim naondoka….’akasema sasa akitikisa kichwa cha kuchanganyikiwa.

‘Sawa, mimi nakuamini, na..unasikia,  …mimi nimeosha mikono yangu, nimechukua dhamana yako mikononi mwangu.., na wewe usije kuniangusha kwa hilo,…umenielewa lakini, na nataka hata wazazi wangu ikiwezekana wasijue kuwa mume wangu kapatwa na ajali, nataka tufanye namna ambayo, sawa ni ajali, lakini kwa mazingira yasiyo kuwa na kashfa, sawa..umenielewa hapo..?’ nikamuuliza

Nilimuona kama anataka kutoa machozi, lakini mimi sikujali,..najua sio mtu wa kutoa machozi, labda kitu kimemuingia machoni,…na muda huo nilikuwa kikazi zaidi,  sikutaka kupoteza muda, nilitaka yeye aifanye hiyo kazi, na nione ukweli wake kupitia kwake yeye mwenyewe…., nilikuwa na maana yangu kubwa tu.

‘Ninataka wewe….uifanye hiyo kazi, sitaki utani, nataka tumfahamu huyo mtu, ni nani anaweza kuingilia ndoa yangu, au kama kuna jingine, tulijue mapema…, kwanini mume wangu awe hivyo…hapo kuna mawili, kashfa ya ndoa, au…kuna tatizo kazini, mimi sijui, wewe ni mtaalamu wa mambo hayo, sasa mimi  nahitaji msaada wako, hii ni kazi nimekupa…’nikasema kwa hasira

‘Mimi naondoka….’akasema sasa akitaka kuondoka

‘Ondoka bwana,… mimi naondoka, mimi naondoka…ila kumbuka mimi…sitaki utani, …unanielewa, sitaki utani kwenye ndoa yangu kwenye kazi yangu, kwenye maisha yangu…ole wake huyo mtu, sitajali ni nani…hili nakuambia wewe kama rafiki yangu, ukisikia mimi nimefanya jambo, hutaamini….’nikasema kwa jaziba.

‘Sawa bosi....naondoka…’akageuka na nikahisi kuna mtu nyuma yangu nikageuka kwa haraka, nikiwa sasa naangalina uso kwa uso na baba yangu mzazi.

‘Baba…….’nikasema kwa mshangao mkubwa, wenye wasiwasi,

‘Kuna nini kimetokea…?’ ilikuwa sauti ya baba ya kiaskari

WAO LA LEO: Mara nyingi tunapokuwa na shida, tunasahau kuwa wenzetu pia na wao wana shida kama hizo za kwetu au huenda shida zao ni zaidi ya shida zetu, wakati huo wa shida, hatujali shida za wenzetuo,cha muhimu kwa wakati huo ni shida zetu, tunachotamani  ni jinsi gani ya kusaidiwa, ni jinsi gani, shida zetu zitachukuliwa kipaumbele, na hapo utaanza kuwachuja marafiki zako, na rafiki utakayemuona ni wa kweli kwako ni yule atakayesimama kwenye shida zako, na kutetea hoja zako.


 Tukumbuke kuwa,sisi sote ni wanadamu, na shida zimeumbiwa kwetu, na kwahiyo sote ni wahitajia,kama ni hivyo basi,  ili tuwe sawa, tujaribu kuona shida za wenzetu zina umhimu sawa sawa na shida zetu.

Ni mimi: emu-three

No comments :