‘Ningefurahi nimuone, tukiwa pamoja sote.....kuna mambo nashindwa kukuambia, maana nikikuambia kwa hivi sasa utaona kama nakudanganya, najaribu kuwaza kuhusu baba wa huyo mtoto, kabla ukweli haujabainika...’akasema.
‘Mimi sijakuelewa hapo, lengo lako hapo ni nini, ni kutaka kujua baba wa huyo mtoto au unahisi labda huyo mtoto ni wa kwako kwa vile uliwahi kutembea naye nini..nikuambie ukweli, sio wa kwako, kwasababu hafanani na wewe kabisa, umenielewa…?’ nikamwambia
‘Anafanana na nani…?’ akauliza akiniangalia kwa uso wa udadisi
‘Anafanana na mama yake....’nikamdanganya, na yeye akacheka kicheko cha dharau
‘Kweli..umemuangalia vyema..una uhakika kuwa anafanana na mama yake..?’ akaniuliza akitikisa kichwa kwa mashaka
‘Nina uhakika kwa vile mimi nimemuona, …kwahiyo kama nia yako ni hiyo basi zoezi lako liishie hapa, na kwanini unatia shaka na jibu langu?’ nikamuuliza.
‘Ok….mimi huko sipo kabisa, hayo unabuni wewe, siwazii lolote kuwa huyo mtoto ni wangu maana sio kweli kuwa niliwahi kutembea naye,.na kufanana na mtu fulani wakati huu, sio tija, maana watoto wachanga wengi hufanana, subiria akue kue, utajua anafanana na nani...’akasema na mimi nikatabasamu
‘Kwanini umetabasamu,.....?’ akaniuliza.
‘Kwa vile jibu lako limenipa faraja, na kuniondoa wasiwasi niliokuwa nao...nahisi itakuwa hivyo...’nikasema bila kusema zaidi
‘Sasa fanya hivyo basi usipoteze muda, mpigia rafiki yako uone utakavyofanya ili aje hapa..nina imani akifika hapa, tutagundua meng nyuma ya pazia, niamini mimi
‘Ok, hilo hakuna shida maana rafiki yangu ninamuamini sana, kama nilivyokuambia kuwa ni zaidi ya rafiki, ni ndugu yangu..., kama ni kulifanyia kazi hilo, kwa kupitia kwake, basi hakuna shaka, nitamuita aje na mtotoni sitaki kashifa kwenye familia yangu,...’nikasema.
‘Sijasema hilo...na sioni kwamba kuna kashifa hapo, usijali, na wala usiwe na wasiwasi....’akasema.
Nilitulia kidogo nikiwazia hilo wazo la huyo docta, kwa namna moja nilikuwa nimeliunga mkono, huenda kweli mume wangu yupo kwenye matatizo, makubwa, lakini hataki kunihusisha, ila siungu mkono ya kuwa mume wangu huenda ana mahusiano na wanawake wa nje, hususani kutembea na rafiki yangu
‘Kweli atakayeweza kunisaidia kwa hili na kuondoa hii taswira iliyoanza kujengwa nafsini mwangu ni rafiki yangu, na docta atabakia mdomo wazi, ngoja nimuite.
Nikampigia simu rafiki yangu huyo, kwa muda huo alikuwa kakaa nyumbani kwake anaangalia runinga, na aliposikua kuwa ni mimi akawa na hamasa sana ya kuongea na mimi…
‘Nakuomba uje hapa hospitalini, alipolazwa shemeji yako, mara moja…’nikasema
‘Kuna nini..!!! Ina maana..she-she-, shemeji anaendeleaje kwani..?’ akuliza akionekana kuchanganyikiwa kwenye simu
‘Tafadhali nakuomba uje tu,…’nikasema
‘Sasa na…oh, na mtoto itakuwaje…?’ akauliza
‘Njoo naye, usimuache, tafadhali…’nikasema na kukata simu.
Nilijua atafika tu, maana mimi nimekuwa nikimtumia sana kwenye shughuli zangu nje ya kazi yake, ili kumsaidia kuongeza kipato, na anafahamu nikimpigia simu ya namna hiyo, basi ni jambo la haraka, na anaitikia alifanyie kazi mara moja.
‘Una uhakika atakuja…?’ akaniuliza docta
‘Atakuja…ila naona kama nimempa hali ngumu,…asije akapatwa na mengine…’nikasema
‘Hamna shida, rafiki yako huyo ni shupavu, namuaminia sana, mtu anaweza kupigana ngumi na wanaume, sio mchezo…’akasema na kucheka kwa mdhaha…
‘Lakini sio kwa mambo kama haya, yanashtua sana, sio vitu vya kuchezea, au kumjaribu mtu..hapana, utani mwingine uufanye lakini sio kwa afya, kifo, na…hapana, hayo, hayana uvumilivu…’nikasema
‘Ni kweli, hata sisi madocta tunalifahamu hilo, ndio maana hata mimi najaribu kuliweka hili jambo, liwe rahisi kwenu..najua tutalimaliza salama, na rafiki yangu atapona kwa haraka, tushirikiane tu…’akasema na mimi nikamtupia jicho la kujiuliza
‘Unajua kiukweli, umenifanya nafsi yangu ianze kufikiria mambo ambayo sikutaka kabisa kuyafikiria,..nimekuwa nikiyapiga vita sana…lakini kila hatua unanifanya nianze kuwaza mengine..mungu anisamehe tu…’nikasema
‘Usijali, kama yametokea yametokea, kama hayapo basi, tutayamaliza kwa amani, ila mimi ninachotaka ni kuhakikisha, kuwa hakuna cha kulaumiana..hakuna cha kumuongezea mgonjwa mawazo, na yote ni sisi watu wake wa karibu..tufanye jambo, nakuomba ten asana ulifahamu hilo…’akasema
‘Mbona wanachelewa hivyo…?’ nikauliza, nikikwepa maongezi yake, maana muda huo akili yangu ilikuwa kwingine kabisa, namuwazia mume wangu, nahisi kama kuna kitu hakipo sawa, miguu inaanza kuniisha nguvu..
‘Ngoja nikaangalie nahisi watakuwa tayari, labda kuna kitu wanakisubiria…’akasema docta na kuondoka kuelekea huko. Na mimi pale nilitaka nimfuate nyuma,lakini sheria ikanikwaza.
*************
Baadae docta akarudi…hakuonyesha furaha usoni, japokuwa alikuwa akijaribu kujificha kinamna kwa tabasamu la uwongo na kweli, na hali hiyo ikanizidisha mashaka, nikamuuliza kwa haraka haraka…
‘Vipi huko ulipokwenda wanasemaje, mume wangu anaendeleaje, maana ungechelewa kidogo tu na mimi ningelikuja huko huko..?’ nikamuuliza
‘Hali yake inendelea vyema usiwe na shaka, …wamemchunguza na kuona kila kitu kipo sawa…’akasema
‘Sikuamini docta, kwanini…na mimi niende nikamuona tu jamani…’nikasema huku nikishika kichwa.
‘Shemuuuh, …huaniamini…anaendelea vizuri, hali ya jana sio ya leo, leo anatizamika, ika kwa vile alikuwa kwenye uchunguzi, lazima hali kama hiyo itakuwepo, kuinuliwa, hivi na vile…wamechunguza wamesema hakuna sehemu iliyovunjika…’akatulia kidogo.
‘Na mashaka yao walioyokuwa nayo awali yameondoka, kwani walihisi huenda kuna athari za ndani kwa ndani..kiukweli hakuna athari yoyote iliyojificha ya ndani kwa ndani, ila bado wanaendelea kumfanyia uchunguzi zaidi , kwani bado alikuwa analalamika maumivu, lakini ni kwasababu ya kashikashi hizo, yatakwisha, ndio maana nataka wewe na rafiki yako, tuje tuongee vyema, kwa hili mtaniona mbaya….’akasema
‘Kwahiyo uliweza kuongea naye…?’ nikamuuliza bila kujali kauli yake hiyo.
‘Bado hawajaruhusu kuongea na mtu, niliongea na docta wake tu, wakati wanamrejesha wodini, na kweli nilimsikia akilalamika maumivu, hasa ya mgongo na kiuno,...inawezekana ni kutokana na hali halisi, kama nilivyosema… na kule kulala muda..unajua mwili ulivyo…, lakini yupo vizuri, yupo… yupo vizuri...’akasema
‘Unasema kutokana na hali halisi kwa vipi….?’ Nikamuuliza nikimkazia macho.
‘Kwa vile ajali hiyo imegusa uti wa mgongo, kwahiyo kuna maumivi sehemu kubwa ya mwili, kwa hivi sasa bado wanaendelea naye , tuwape muda wafanye kazi yao, ili kuhakikisha kila kitu kipo sawa, usijali mambo yatakuwa sawa...’akasema huyo rafiki wa mume wangu.
‘Lakini, niambie ukweli, wewe kama docta unahisi vipi, huko kulalamika mgongo na kiuono, inawezekana ni jambo la muda, litakiwisha ni kweli hakutakuwa na athari zingine zinaweza kujitokeza huko baadae?’ nikamuuliza.
‘Mhh, hakuna,..maana vipimo vinasema, ila ngoja tusubirie wamalize kazi yao, nitaongea nao, nitakagua ripoti zao, lakini yale muhimu yanayotuhitajia sisi, tuyafanye, tuhakikishe tunakwepa yale yote yanayoweza kumkwaza, maana kama kuna athari zitakuja kujitokeza zitakuwa ni za kibinadamuu, mimi sina wasiwasi na hilo....’akasema.
‘Kwahiyo sasa hivi yupo macho , nikienda naweza kuongea naye…?’ nikauliza
‘Ndio yupo macho, kazindukana, lakini bado madocta wanamfanyia uchunguzi wa hapa na pale, naona wamekutana wote, kuhakikisha kuwa hawafanyi makosa, na hilo la kulalamika, nina uhakika na kutokana na hiyo mitikisiko ya kumuinua, inua, itakwisha tu, ....’akasema.
‘Mhh, hapo mimi bado nina mashaka, mpaka nionane naye…na kama wameshindwa wasema tumpeleke juu zaidi, au...?’nikasema.
‘Hawajashindwa bwana, …nakuhakikishia hilo, huniamini mimi shemeji,…ila mimi nilikuwa nakushauri kitu,naona wewe una shughuli nyingi umeziacha bila ya maagizo,kwa vile mimi nipo likizo, ninaweza kubakia hapa, ili niendelee kuona hali ya mgonjwa kwa ukaribu zaidi na kama kuna lolote la kusaidia, nisaidie, unaonaje,…’akasema
‘Kuondoka…haaah weeeh!!! Hapana, kwanza umesahau ulichoniagiza au…?’ nikauliza
‘Oooh…hilo achana nalo,muhimu ni wewe na shughuli zako, najua hilo tutalifanyia kazi, maana lina umuhimu wake, hasa kwa mgonjwa, …. Mgonjwa pamoja na matibabu, lakini kuna mazingira akiyaona, akisikia kauli zenu, anaweza akatatizika, hili muwe makini sana …’akasema
‘Sasa ndio unanishauri niende nyumbani, akiona sipo, huoni atajisikia vibaya…?’nikauliza
‘Hapana, kwa vile mimi nipo najua jinsi gani ya kuongea naye…hilo lisikutie shaka, maana tunaweza kuacha mgonjwa, kwa ajili ya mgonjwa mwingine…’akasema
Mimi sikukualiana na wazo lake hilo, la mimi kwenda nyumbani bila kumuona mume wangu, nikawa nimekaa kimia, akilini nikimuwazia mume wangu, ina maana kitu kidogo tu kinaweza kumfikisha mwanadamu hapo, ooh, sijui ni kosa langu au kuna tatizo, jingine kama ni kosa langu sijui nitajijutiaje, ......hapo nikahisi machozi yakinilenga lenga.
Nikainua kichwa kumuangalia docta, nikamuona akinichunguza kwa macho, na muda huo machozi yanakuja kwa kasi,… kabla sijaathirika na hiyo hali, nikageuka upande mwingine, docta akaitambua hiyo hali na kusema;
‘Usiwe na shaka, ...nakuhakikishia kuwa mume wako hana matatizo, ...ni swala la muda tu, utakuwa naye, ajali ni ajali, na hiyo ajali yake ilikuwa ni kubwa sana, hutegemei mtu aliyetoka pale awe hai, uhai wake bado mkubwa sana, hata yeye sizani kama ataamini kuwa aliweza kutoka hapo salama....’akasema na mimi sikusema.
Na ni wakati nainua kichwa kuangalia sehemu ya nje, kwenye mlango mkubwa ndio nikamuona rafiki yangu akija kwa mbali, na wakati huo huo docta akawa anaongea na simu yake. Na alipomaliza kuongea na simu, akanigeukia na kusema;
‘Ni vyema kwa leo, hata kama tutaruhusiwa kumuona mgonjwa, wewe hakikisha huruhusu watu wengi kuonana na mume wako, hata kama ni rafiki yako, mimi mwenyewe nitalisimamia hilo ...’akasema
‘Kwanini,…si umesema yupo sawa, ..ok, tutawasikiliza madocta watakavyosema au sio,. Kuonana na watu kwa wengine ni faraja au…’nikasema
‘Hata mimi ni docta, au huniamini, kwa vile kuna mambo nimeshayaona, nisingelipenda akaja mtu akamzidishia mawazo, hasa nyie wawili,…’akasema
‘Ndio maana maana ya kumuita rafiki yangu au..sasa na mtoto ni wa nini,…?’ nikamuuliza, na je rafiki yangu akija hapa, hatamuona mgonjwa,…?’ nikamuuliza
‘Yeye kumuita hapa, awali nilitaka iwe hivyo, tumuone mgonjwa pamoja, nyie ni marafiki au sio, lakini kuna kitu nilitaka kiwe wazi,…lakini baada ya kumuona tena mgonjwa alivyo, naona hata akija rafiki yako, tutaongea naye tu,.’akasema
‘Haitakuwa vyema, tutamuambia asifanye lolote …amuone tu…’nikasema
‘Mhh….kiukweli hivi sasa mume wako hahitaji mshutuko wowote, hahitaji, kitu cha kumpa mawazo, ni bora akutane na wewe tu na mdocta mpaka hapo hali itakapo kuwa sawa…’akasema
‘Sawa , hilo halina shida, kama umesema hivyo, hakuna shida,..nitafanya hivyo hivyo, ila tutakuwa tumemsumbua rafiki yangu aje tu, bila kumuona mgonjwa, sio vizuri, lakini sawa, nimekuelewa…’nikasema
‘Ok, sasa unaonaje wazo langu, la wewe kurudi nyumbani kidogo, umalizane na mambo ya kazi, halafu utarudi, ikibidi,..nahisi huyo rafiki yako hatafika....na kwa vile ni mzazi, tumuache tu, tutakuja kuongea naye hata nyumbani.....’akasema , alikuwa hajamuona huyo rafiki yangu maana sasa alikuwa anakuja muelekeo wetu lakini docta alikuwa kampa mgongo.
‘Anakuja..nashukuru kaja,…hata hivyo, mimi ninachotaka nikaonane na mume wangu kwanza,…au…hapa sina amani kabisa, …’nikasema.
‘Mumeo anaendelea vyema, usiwe na wasiwasi, tutakwenda kumuona lakini tukishamalizana huku, najua mengine, au mpigie rafiki yako asije tutaongea naye huko huko…’akasema hivyo.
‘Kaja…ili tuweze kuyamaliza haya mambo, ili na wewe uweze kuondoa hofu yako dhidi yake ..’ nikasema na huyo rafiki yangu akawa sasa keshafika, kasimama nyuma ya docta.
‘Sawa kama una uhakika …kuwa atafika, sawa, nina mambo yatakuwa sawa, mimi nilikuwa nimekitaka ni kumbana rafiki yako, aseme ukweli, …lakini kwa vile kuna hii hali ya sasa, …haina haja ya kulazimishana…ila nyie kama binadamu ningeliwaomba muwe wawazi, ili na mimi niweze kutoa ushauri unaofaa, kama mtakwua mnanificha ficha mambo, inaniwia vigumu, haya ngoja aje tuone atatusaidiaje, nina uhakika….’kabla hajamaliza rafiki yangu akakohoa na kusema;
‘Sam-samahanini kuwakatili kwenye mazungumzo yenu, maana mtoto nimemuacha nje, Haya nipeni habari za mgonjwa, .maana umenifanya nitoke wangu wangu hata bila ya kubadili nguo, niambie kuna usalama huku...’akasema kweli akionyesha mashaka.
‘Oh….’docta akashtuka, akisikia rafiki yangu akiongea nyuma yake, akaguna hivyo, halafu kwa haraka akasema;
‘Wewe umemuacha mtoto nje ndani ya gari, na nani?’ akauliza docta kwa mshangao.
‘Kuna mtu yupo naye, usitie shaka, hahaha, naona ulivyoniangalia, ulifikiri nimemuacha ndani ya gari peke yake, hapana,…weeh, hapa kwenye natamani nirudi, siamini mtu kabisa...’akasema huku akiniangalia mimi machoni.
‘Karibu…’nikasema
‘Haya niambieni hali ya shemeji ipoje..nakuona kama unalia...kuna usalama kweli…?’akasema rafiki yangu huyo akiniangalia usoni kwa mashaka, na mimi nikapitisha leso machoni.
****************
‘Kuhusu mume wangu,...mhh, bado,...sijaonana naye tangu wamchue , wanasema wanataka kumchunguza zaidi leo, uchunguzi wa kawaida, …. lakini kwa taarifa za kupitia huyu rafiki yake,…docta…. wanasema hajavunjika mahali,....ila analalamika maumivu kwenye kiuno...na mgongo, na hilo kwangu mimi naona ni hatari au...’nikamwambia huyo rafiki yangu.
‘Kwenye kiuno..na mgongo mhh, au huko kulala lala namna moja bila kujigeuza kwa muda, lakini vipimo vitasema au sio docta,.. mimi sioni kwanini uwe na wasiwasi....kwani majeraha ya hiyo ajali yamegusa mgongo, kichwa, au…?’ akasema huyo rafiki yangu
Docta aliposkia hivyo alimuangalia huyo rafiki yangu kwa makini…na baadae akasema;
‘Hajapata athari kubwa sehemu hizo, kiukweli hali yako haipo mbaya kihivyo, uchunguzi wa leo ni wa kujirizisha tu,.... tumpe muda, tuwape muda madocta wafanye kazi zao au sio.....’akasema huyo docta akimwangali huyo rafiki yangu, na huyo rafiki yangu akawa kama hataki kuongaliana na docta, akawa ananiangalia mimi na kusema;
‘Kwahiyo eeh,…. Ulivyoniita kwa haraka hivyo…nahisi kuna jambo la dharura,…unajua mimi nilipanga kuja kumuona lakini ulivyoniita nikajua kuna tatizo jingine kubwa, ooh, umenishtua kweli, ..sasa eeh, hiyo ajali ilitokeaje?’ akaniuliza
‘Hata mimi sijajua vyema , mambo yamekuwa ya harakaharaka sana, ila watu nilio-onana nao wanadai kuwa eti mume wangu alikuwa kwenye mwendo kasi, ...ndio ikatokea hiyo ajali, gari likawaka moto...’ nikasema.
‘My, my ….mbona mkosi huu…mhh, unajua najiuliza mbona shemeji hana tabia hiyo ya kuendeshe gari kwa mwendo kasi, ilikuwaje lakini, nahisi …oh,…au.., alikuwa anakimbia nini, kuwahi kitu gani, ....aliogopa nini…mmh hapo kuna tatizo....’akasita kidogo na kugeuka kumwangalia huyo docta, na haraka akaniangalia mimi na kusema;
‘Na hiyo ajali ilitokea wakati anatokea aah....wapi?.’akasita kidogo na kumalizia hiyo `wapi’ kwa kusita, na kugeuka kumwangalia docta inaonekana hakuwa na amani kuwepo huyo docta. Na huyo docta akawa anajifanya hatuangalii sisi
‘Sina uhakika sana....maana kama ninavyokuambia mambo yametokea kwa haraka sana,..sijapata muda wa kulifuatilia hilo,...sina uhakika sana alikuwa katokea wapi...’nikasema na doca akasema.
‘Atakuwa alitokea maeneo ya huko kwenu, na sio kazini, kama angelitokea kazini angekuwa upande mwingine wa barabara...ukiangalia lile gari lilivyokuwa ...’akasema docta, na huyo rafiki yangu akasema.
‘Yaah, itakuwa hivyo.........’akasema na huyo docta akamkatiza.
‘Kwani uliwahi kuonana naye kabla ya hiyo ajali...?’ akauliza na mimi nikainua kichwa kumwangalai rafiki yangu ambaye alikuwa katulia na nilipoona hajibu kitu, mimi nikasema;
‘Kama alitokea huko kwako, mimi …si tungeliliona hilo gari likipita maana pale ndani tukiwa tumekaa tunaona bara barani, eti, wewe uliliona gari la mume wangu likipita , yawezekana labda, alitaka kuja kumuona mzazi, sasa kwanini akapita..na kuna muda nilimpigia simu akasema yupo kazini, sasa hapo mimi naona ..lakini tuyaache tu, nitakuja kuyafahamu yote hayo..’nikasema.
‘Alikuambia anakuja kumuona mzazi sio ...?’ akauliza docta
‘Ndio anakwenda, kumuona mzazi ….’nikasema
‘Mzazi gani huyo…?’ akauliza
‘Nakumbuka …unajua hata wakati mzazi huyo yupo hospitali alikwenda kumuona na nahisi ndio huyo alikuwa anakwenda kumuona nyumbani kwake…’nikasema
‘Ni nani huyo…sizani kama kuna mzazi mwingine zaidi ya huyu rafiki yako, ,…na nakumbuka mimi niliwahi kuongea naye, akaniambia rafiki wa mke wake kajifungua, sasa sizani kama kuna mzazi mwingine, hajaniambia …au …?’ akauliza akimuangalia rafiki yangu.
‘Yupo mwingine bwana….nahisi anaweza akawa mke wa mfanyakazi mwenzao, au ..mfanyakazi mwenzao, …sina uhakika, maana sikupata muda wa kumuulizia zaidi….’nikasema
‘Mhh…labda….’rafiki yangu akaguna na kusema hivyo..
‘Sio labda, ni kweli…’nikasema
‘Sizani…ehe, hebu rafiki yako atusaidie hapo…’akasema docta na kabla hajamaliza rafiki yangu akadakia kwa kusema;
‘Unajua nimekumbuka, kuna watu walikuwa wakiongea, kuhusu ajali iliyotokea kwenye kona ya barabara ya kuingia barabara inayotokea bara bara kuu, wanasema ni ajali mbaya, na hakuna mtu aliyepona, ina maana ndio hiyo…?’akasema rafiki yangu na kuuliza.
‘Itakuwa ndio hiyo…’akasema docta
‘Kwakweli hapa nilipo nashindwa hata cha kuongea, maana sielewi, ni kitu gani kilimfanya aendeshe gari kwa mwendo kasi, ...sijui alikuwa kalewa, au alikutwa na janga gani, maana siku hizi kama unavyojua, mume wangu kabadilika, amekuwa mlevi...’nikasema.
‘Nahisi ana tatizo, nilikuulizia hilo ..lakini sasa,…tuseme ajali haina kinga…sasa eeh.. hebu niambieni kinachoendelea maana kama nilivyowaambia mtoto yupo kwenye gari, sitaki kukaa sana, ninaweza kwenda kumuona mgonjwa mara moja, ....?’ akauliza rafiki yangu.
‘Mhh,…hapana… kwa hivi sasa haitawezekana, tulitaka iwe hivyo, kabla hujapigiwa simu, lakini nilivyokwenda kumuona kwa hivi sasa hitawezekana, rafiki yako alitaka uwe karibu naye karibu …kwa muda huo.., unajua tena mlivyoshibana namuona , ..ana wasiwasi sana, nimemuambia hakuna cha kuhofi…’akasema
‘Mhh…ni kweli hata ingelikuwa ni mimi….’akasema rafiki yangu.
‘Ila hata hivyo nina mazungumzo mimi na wewe na…shemeji hapa, muhimu sana tukaongea, sasa sijui, na kama huna haraka, basi tusubirie ndani ya gari, maana mgonjwa hatakiwi kwasasa kuongea na watu wengi, mkewe sawa, anaweza kwenda kumuona mara moja, haijuzu…’akasema
‘Maongezi kuhusu nini hasa …?’ akauliza kwa mashaka, nakuniangalia mimi
‘Kuhusu mgonjwa, …na mengineo yake, wewe utanisaidia sana kwa hili, kama utakuwa mkweli, na halikadhalika rafiki yako, ni muhimu sana hili jambo, mkawa wawazi ili tuone jinsi gani ya kuliweka sawa,..ok, sasa sikilizeni,..eeh,…umesema mtoto yupo kwenye gari, nilikuwa nataka nimuone, unamficha sana, kwanini, unaogopa nini…, hahaha,, ...’akasema huyo docta akimwangalia huyo rafiki yangu, na huyo rafiki yangu akawa anamkwepa wasiangaliane, na kugeuka kuniangalia mimi, na mimi nikadakia na kuuliza
‘Mtoto wa nini bwana, wewe kwa sasa hutakiwi kuondoka hapa, mimi naona ..eeh ...’nikasema kabla sijamalizia simu ya docta ikaita
Docta akasema samahani aipokee hiyo simu, ni mteja wake muhimu…na kuchepuka pembeni, na mimi nikabakia na rafiki yangu, na hapo nikaona ni nafasi nzuri ya kuongea nilichotaka kukiongea, na sikutaka maongezi yangu hayo yasikiwe na huyo docta, nikamgeukia rafiki yangu na kusema;.
‘Nilikuwa nataka unifanyia kazi maalumu, ni kazi ambayo sikuwa nataka ifanywe na mtu mwingine...,lakini kwa sasa sina jinsi, na kutokana na maongezi yangu na huyu docta, nimeingiwa na mashaka …kuna kitu mume wangu ananificha…, nataka wewe unisaidie kwa hili, uchunguze ni kwanini mume wangu alikuwa na haraka hivyo, nina imani hiyo ajali sio ya bure bure, kuna jambo,…’akasema
‘Hata mimi naona hivyo, sio kawaida yake, kuna jambo..sizani kama …’akasita.
‘Sasa tuache dhana,..nataka uutafute ukweli, fuatilia nyendo zake, alikuwa anatokea wapi…maana alikuwa kwenye kikao, kwanini akatoka kwenye kikao kwa haraka, kuna nini alikuwa akifuatilia, na ni kwanini akaendesha kwa mwendo wa kasi hivyo, kuna kitu hapo…umenielewa hapo...’nikasema
‘Mhh…kwani docta kasemaje..?’ akaniuliza.
‘Docta ana mambo yake, ana shuku shuku zake..mimi sijamuelewa, …muhimu kwangu, ifanye hiyo kazi, wewe ondoka ukaifanye mengine niache mimi na docta tutayamaliza…’nikasema
‘Hujamuambia docta kuhusu mambo yetu, ..?’ akauliza
‘Yapi…?’ nikamuuliza
‘Si haya ya mtoto, tulivyokuwa tumepanga, mpaka ikatokea hivi, unakumbuka tulipanga nini, tukasema iwe siri yetu hata iweje tusije kuitia au sio, kumbuka,….ahadi ni deni….’akasema
‘Ni siri ...hilo siwezi kusahau, jamaa kanidadisi wee kafika sehemu kasalimu amri sasa anataka kupata taarifa kupitia kwako, mimi nakuahidi kuwa itaendelea kuwa siri, niamini hilo, unasikia, na wewe usije kunisaliti, ufunge huo mdomo wako, maana huyu docta ni mjanja sana, umenielewa…’nikasema
‘Sawa nimekuelewa,...kama ni hivyo nimekuelewa sana aheri umenishtua maana sikujua umeniitia nini..., lakini sasa kuhusu hiyo kazi mbona ni inakuja kuturudia, eeh, hebu elewa hapo…’akasema kwa kusita
‘Sikiliza mimi, kuturudia kwa vipi, na wewe bwana, haya yetu hayaguswi, unaonaeeh,..ninachotaka ni hivi, nijue kila kitu, kuhusu mume wangu... , sio kawaida yangu kufanya hayo lakini sina jinsi...'nikasema
'Nahisi kuna kitu, naanza kuingiwa na mashaka, sasa nataka kujiaminisha mwenyewe, je ni kweli wanayosema watu kuwa mume wangu ana tabia chafu, kuacha hizo za ulevi,...je kuna jambo la kunitia aibu, unajua kazi zetu zilivyo, kashfa zinaua soko, na wazazi wangu wakijua, nitaumbuka...'nikasema
'Mhh..lakini....'akataka kujitetea
'Mapema nikijua ni bora zaidi, tutajua jinsi gani ya kuyafukia mashimo, unanielewa hapo, hakuna jinsi, kama kafanya kafanya, lakini...kafanya nini...kama ni kazi za hivi hivi kupata soko, sawa, lakini kama ni mambo ya kibinadamu, labda...nasema mfano...tuone jinsi gani tutamsaidia...'nikasema
'Kama inatuhusu sisi wenyewe je...?' akauliza
'Kwa vipi...?' nikauliza
'mfano hii soo yetu...naona kama inakuzwa, na sijui docta kazungumzia nini, ndio nilitaka niongee na yeye nijue anajua nini, labda kasikia kitu...'akasema
'Hajasikia lolote, ndio ananichota chota mimi, nimuelezee, na mimi siwezi kuyaongea mambo yetu, kwa vile ni sirii yetu, sasa wewe tafuta bwana mtafute huyo mume muongee naye mliweke sawa, unanielewa...nilitaka nionane naye, lakini naona ..hata sijui kwanini umeninfanyia hivyo...'nikasema
'Kwahiyo....?' akauliza
'Mii ninachotaka ni kufahamu nyendo za mume wangu, ilikuwaje mpaka ikatokea hivyo, nikijua nitajua jinsi gani ya kumsaidia..nataka hilo ulifanye haraka iwezekanavyo, namuombea apone tu….nampenda sana mume wangu,
sitaki aje kukutana na kashfa mbaya, sijui kwanini,...ila nahisi kuna kimwanamke kinamsumbua, kama kipo nataka nikifahamu haraka iwezekanavyo, na nitajua jinsi gani ya kumfanya, atahama jiji...atajiua kabla hayajamkuta mauti…’nikasema
‘Mungu wangu, ina maana utamfanya kitu kibaya...?' akauliza
'Hutaamini kama nini, mimi na wewe ni rafiki, lakini hujawahi kuifahamu sehemu ya pili ya nilivyo..hutaamini...'nikasema nikionyesha uso ambao hajawahi kuuona kabla, nilimuona akitikisika.
'Kama ni hivyo, hapana......siwezi...'akasema
'Eti nini huwezi...acha tabia hiyo,…umeshanifanyia kazi zangu nyingi zaidi ya hii, hii ni muhimu kwangu kuliko, nataka nifahamu hili kabla mume wangu hajakaa sawa…unanielewa, na mengine uniachie mimi mwenyewe, nitajua ni nini la kufanya, 'nikasema
'Mungu wangu kwanini ....mbona imekuwa hivyo tena...'akasema
'Ogopa kuchezewa ndoa yako...unakuja kulifahamu hilo ukiolewa...'nikasema
'Kwahiyo, hata kama aliyefanya hivyo ni mtu wako wa karibu...?' akauliza
'Mtu wangu wa karibu hawezi kunifanyia hivyo, hilo halipo, ...sizani, ni nani huyo, hapana, sizani, eti docta anakushuku wewe...'nikasema
'Docta, kasemaje....?' akauliza kwa mashaka.
'Achana naye, ...sasa sikiliza fanya hivi, sehmu ya kuanzia, hebu jaribu kugundua huyo mzazi ni nani, huyo mzazi aliyekwenda kumuona hospitalini, na baadaye akaenda, au akataka kwenda kumuona nyumbani, ni nani,…nahisi ukianzia hapo unaweza kufika mahali, nahisi kuna kitu hapo, sitaki kumshuku mume wangu vibaya, lakini huyo mzazi ana lake jambo, nahis ndiye kidudud mtu….’akasema
‘Mzazi…!! Mzazi gani huyo…na kama ni kweli..?’ akauliza
‘Sipendi…unasikia, sipendi... nimekutuma kazi, fanya kazi…au…mbona una mashaka mashaka…sio kawaida yako, …utaifanya hi kazi au hutaifanya…?’ nikamuuliza na mara docta huyo akaja..
WAZO LA LEO: Ni vyema tukajenga tabia ya kuhakiki mambo, tusikimbilie shuku, au dhana mbaya. Ukiangalia kwa makini, dhana mbaya zinachukuliwa kwa uharaka zaidi kuliko dhana nzuri, watu wanafikia kuchukiana kisa , kasikia, kisa, kaambiwa....!Waliokuwa marafiki wanakuja kuwa maadui, na hata vita vingi duniani vimeanzia huko..watu wanafikia kuuana, kisa ni dhana, kisa alisema fulani, na maadui wanatumia mwanya huo, kuongeza fitina na propoganda potofu. Tujaribuni kuwa na uhakika na mambo ya kusikia, tusikimbilie hatua, kabla ya kujirizisha,.
No comments :
Post a Comment