Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, November 3, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-19


‘Kakupigia nani,…rafiki yangu…?’ nikamuuliza

 Na docta akaikata ile simu, …haikuipokea ikanifanya niwe na mashaka, ni kwanini docta hakutaka kuipokea nikiwemo.

‘Ni kwanini unaikata hiyo simu…ni kwanini hutaki kuongea na yeye,labda anahitajia huduma yako ya kidakitari..?’nikauliza.

‘Hapana , tokea jana anataka kuongea na mimi, ..siwezi kuongea na yeye mpaka nimalizane na wewe…’akasema.

‘Sijakuelewa hapo,…kuna nini kinachoendelea kati yako na rafiki yangu, ..?’ nikamuuliza.

‘Kiukweli,…sijui…alinipigia simu, akasema nikipata muda, anataka tuongee mimi na yeye, nikamuuliza kuhusu nini, akasema ni maswali ambayo hataki kuyaongelea kwenye simu,…nikamuuliza je yanahusu mtoto, au yeye, akasema mtoto….nikamwambia mimi nipo likizo, akasema hahitaji kuongea kiofisi…’akasema

‘Unahisi anakuhitajia nini…?’nikamuuliza.

‘Yeye anafahamu wewe ni rafiki yangu, nahisi ..yale yale ninayotakakujua kutoka kwako, huenda anataka kuyafunika, kinamna.. au…..’akasema

‘Mimi siwezi kukuelewa kabisa,  wewe una hisia zako mbaya dhidi ya rafiki yangu au hebu nikuulize kwanini unawazia hivyo…?’ akaniuliza

‘Kuwazia hivyo kuhusu nini…?’ akaniuliza

‘Kuwa huenda huyo mtu aliyekuja wakati nipo kwa rafiki yangu anaweza akawa ni mume wangu, kwanini, rafiki yako unamuhisi vibaya, kwanini lakini..?’ nikamuuliza

‘Kwanza tukubaliane, upo tayari tusaidiane kwa hili, la kumtafuta huyo mtu ni nani, au kumtafuta mwanaume aliyezaa na rafiki yako ni nani, na tuyafanye hayo kwa nia njema kabisa, sio kwa ubaya…?’ akaniuliza

‘Halafu ukishamfahamu,…?’ nikamuuliza

‘Tutakuwa tumemaliza tatizo, sasa itabakia kuona jinsi gani ya maisha yaendelee..nina imani wewe utakuwa huru,..hutahangaika tena, na mume wako atapona haraka….’akasema

*****************

‘Kwahiyo unatakaje hivi…?’ nikamuuliza

‘Ninachotaka mimi, ni wewe kuwa muwazi, uwe mkweli, ….’akasema

‘Kama hayo yatamsaidia mume wangu sawa, nitafurahi sana, lakini kunisaidia mimi, sijui unataka kunisaidia nini hapo, sijakuambia kuwa nina tatizo…?’ nikauliza

‘Nina imani yote yanaendana…kwanza tuanze hivi,..kwanini mume wako akawa mlevi hivyo wakati awali hakuwa hivyo, naomba unijibu kwa uwazi, ili tufike kunakotakiwa…?’ akaniuliza

‘Kiukweli, labda nijenge hisia tu…mume wangu kuna kipindi tulijadili kuwa tuzae, tupate watoto, na wazo lake kubwa ni kupata mtoto wa kiume, sijui kwanini analihitajia hilo sana…’nikasema

‘Ikawaje…mjadala huo uliishia wapi…au wewe ulisemaje..?’ akaniuliza

‘Nilimshauri kuwa hilo lisiwe kipaumbele chetu kwanza, kwasababu tupo kwenye harakati za kujiimarisha kiuchumi, lisubirie, akadai kuwa yeye anahitajia watoto mapema iwezekanavyo, ..hataki kuja kuzaa uzeeni…’nikasema

‘Huoni kuwa ana ukweli fulani  hapo, kama wewe ulivyomshauri rafiki yako kuwa azae mapema, mbona wewe hukujiangalia au kuna tofauti kati yako na rafiki yako, unajiamini vipi hapo ..?’ akuliza

‘Tofauti yangu na rafiki yangu ni kuwa mimi nina mume na muda wowote nikihitajia kuzaa, kabla sijafikia ukomo,  nitazaa kwa majaliwa ya mungu offcourse , lakini yeye mpaka ahangaike kumpata mwanaume na zaidi anayemtaka yeye, pili awe na uhakika wa ..…na huenda katika kulifanya hilo ikachukua muda, na jinsi gani ya maelewano a huyo mwanaume…’akasema

‘Kwahiyo ukamshauri akazae vipi hapo…?’ akauliza docta

‘Hilo la kuzaa vipi au na nani, nilimuachia yeye mwenyewe, sikutaka kumuingilia hayo…., si unajua alivyo, kwahiyo kama alizaa na nani, sio muhimu sana kwangu, kama hakuna tatizo…’nikasema.

‘Kama hakuna tatizo, nahisi sasa kuna tatizo….ok, ..Je hukuwahi kuongea kuwa azae na kundi gani, walio-oa, au wasio, oa…au azae baada ya kufunga ndoa..najua hilo la kufunga ndoa lilikuwa ni gumu kwake, au sio, kwa jinsi alivyojiwekea misimamo yake,…ya kuchagua chagua sana..sasa ulimshaurije hapo?’ akaniuliza, kiukweli sikutaka kumwambia ukweli wa hicho tulichokubaliana na rafiki yangu.

‘Nimeshakuambia hilo la kuzaa na nani, nilimuachia yeye mwenyewe, …’nikasema na kukaa kimia.

‘Una uhakika?…anyway, sasa hebu nikuulize, baada ya wazo hilo, ni kwanini asitafute wanaume ambao hawajaoa…?’ akaniuliza

‘Aaah, mbona maswali yako ya kujirudia rudia, jibu nimeshakupatia, na sijui alitafuta nani, sijui…’nikasema

‘Nasema hivyo nikiwa na maana.  kiukweli mara nyingi huko nyumba alikuwa mbali sana na wanaume za watu, lakini ghafla nikaja kumuona akiwa karibu na wanaume wali-oa….au…mmm mlipanga iwe hivyo…?’akasema

‘Docta, mimi sina tabia ya kufuatilia maisha yake, kama wewe una muda huo, mimi sina muda huo kabisa, ..kwahiyo sikujua ni nani na nani alikuwa karibu naye…kama ni wewe au mwanaume mwingine yoyote…’nikasema

‘Au shemeji yake…’akasema docta na kunifanya nimtupie jicho

‘Shemeji yake..!!? Nani, mume wangu au…na wanini unamtaja yeye, nilishakuambia yeye ni shemeji yake, na hata wakiwa naye, hakuna shida, ..na na…au  wewe unamshuku kuwa huenda ana mahusianio ya siri na mume wangu…mbona unantia mashaka ambayo sikuwa nayo kabisa..?’ nikamuuliza, nikimuangalia moja kwa moja usoni, na yeye akatabasamu na kusema;

‘Sijamshuku,… ila nataka kuwa na uhakika, ili tuweze kumsaidia mume wako…, nahisi mume wako ana tatizo kubwa, sasa ni tatizo gani, hilo mimi kama rafiki yake linanisumbua kichwa sana, ....’akasema.

Na hapo tukakaa kimiya kwa muda, mimi akilini nikawa nawazia hiyo kauli ya docta, kwanini ni kama anamshuku mume wangu, na nafahamu kuna muda mwingi baada ya kazi wanakuwa naye..japokuwa sio sana

Nilimuangalia docta, …huku nikiendelea kuwaza,..labda,  inawezekana kukawa na lolote kati ya rafiki yangu na mume wangu, ..hapana hilo siwezi kabisa kuliamini, ...yule ni rafiki yangu mpenzi nimemuweka kwenye kundi la ndugu, siwezi hata siku moja kumfikiria vibaya, lakini huyu ni docta, na hana tabia mbaya, ni kwanini aliwazie hili, hapa nikaingiwa na mashaka....

‘Shemeji huenda utaniona, kuwa naingilia ndoa yenu, huenda ukahisi kwa vile nilikukosa wewe ndio maana najaribu kuona kila mlitendalo sio jema,..au kama unavyodai wewe…, kuwa wazazi wako wamenituma, kufanya lolote ili kuiharibu ndoa yenu, ..lakini kwanini tufanye hivyo..

‘Nikuulize wewe…’nikasema

‘Sio kweli, mimi nina nia njema kabisa na ndoa yenu, ndio maana nilikuomba sana mapema tu, nilipoona rafiki yangu anabadilika, anakunwya kupitiliza, nikakuomba sana ukae  uongee naye, wewe ukapuuzia, mimi nahisi mume wako ana kitu kinamsumbua...’akasema

 ‘Mimi bado hapo sijakuelewa, tuongee nini hasa kuhusu starehe yake ya kulewa,..., mimi huko sina muda huo, kama kaona ni starehe yake muache endelee..au wewe unahisi kuna tatizo gani jingine...,mimi ninaanza kuingiwa na wasiwasi,  kuna nini kutoka kwa rafiki yako ulichokiona kingine…, niambie, mimi si rafiki yako unaogopa nini sasa…’nikasema

‘Hapana, mimi sijui kitu,..ningekuwa na uhakika ningelikuambia mapema kabisa, ila ninachotaka mimi ni kujua ukweli…, nataka kuwa na uhakika, na uhakika huo nitaupata zaidi kutokwa kwako, na akili yangu inanituma, kuwa kuna kitu ambacho huenda kimesababishwa na mahusiano yenu wawili, wewe na mume wako, na kikaenda hadi kwa rafiki yako, sasa ni kitu gani hicho…’akasema

‘Una maana mimi nimemfanya mume wangu atembee nje ya ndoa, …labda kwa vile..si ndio hivyo…na aliyekwenda kutembea naye, au anayetembea naye ni rafiki yangu, kisa kwa vile umewaona wakiwa naye karibu, au sio, na matokeo yake ni huyo mtoto, au sio..niambie ukweli….’nikasema

‘Unaweza ukawa , haupo mbali na hisia zangu,…unanifahamu nilivyo, mimi ni docta, au sio, siwezi kutibu ugonjwa bila kujua vipimo, ndio maana natadadavua kuupta huo ukweli, na wewe hutaki kutoa ushirikiano…’akasema

‘Kwahiyo…unataka kunipima nini…niambie…’nikasema

‘Ukweli…nataka ukweli kutoka kwako…’akasema

‘Hebu niambie kuna nini kinachoendelea kati yako wewe na rafiki yako, naanza kuhisi vibaya, kuwa huenda kuna jambo kalifanya, au kuna jambo unalifahamu dhidi ya rafiki yako, labda mlishirikiana wewe na yeye, sasa wewe unatafuta namna ya kujikosha kwangu, ili usionekane kuwa na wewe unahusika, sasa ...niambie rafiki yako kafanya nini?’ nikamuuliza kwa ukali.

‘Shemeji siwezi kujua zaidi , ...yule ni rafiki yangu, lakini tuna mipaka yetu, sio rafiki wa kujua kila kitu, kuna yake anayafanya mimi siwezi kuyafahamu,..lakini naomba unielewe , mimi nilichokiona ni hiyo tabia yake ya kunywa kupita kiasi, ilianza tu…nikamuuliza akasema kaamua tu, na unielewe  sio kila siku ni kitoka jioni ninakuwa naye, hapana. Hebu nikuulize je hajawahi kulala nje...?’

‘Kulala nje!!!..., hapana, hawezi kulala nje, kwanini alale nje, wakati ana nyumbani yake, labda kuwe na sherehe ya kukesha huko kazini kwao, hilo linatokea…, na hilo kwa siku hizi halijawahi kutokea, ...kuchelewa hilo nalikubaliana au kurudi akiwa kalewa sana huwa inatokea, na yah, …kuna siku alichelewa sana mpaka nikawa na mashaka, kama mara mbili tatu hivi…karudi alifajiri....lakini yeye ni mtu mzima, ulitaka hapo nifanye nini mimi, nijiumize kichwa na starehe za mtu, kaamua, tumuache, dunia itamfunza...’nikasema.

‘Na akiwa kalewa sana ni nani anamleta nyumbani kama mimi sipo naye…, maana akilewa sana nikiwa naye, huwa mimi namleta mwenyewe, je kama sipo, ni nani mwingine  anapenda kumleta nyumbani, maana hapo huwezi kunificha kuwa halewi kiasi cha kutokujitambua?’ akaniuliza.

‘Wewe unafahamu bwana, kuwa mara nyingi ni mdogo wake anayemleta, huwa akiona kalewa kupitiliza kiasi  cha kutokujitambua, sijui kwanini mtu mzina kama huyo anafanya hivyo…mimi nijuavyo kama haupo, anamuita mdogo wake, na mdogo wake, anafika hapo alipo anamchukua...’nikasema.

‘Kwahiyo …eeh, mdogo wake atakuwa anafahamu mengi kuhusu kaka yake ambayo mimi siyafahamu, …sawa hapo eeh,.. umenipa wazo, jinsi  ya kulifuatilia hili jambo, huyo ni mtu mwingine anaweza kutusaidia, umeliona hilo hata wewe.....?’ akawa kama ananiuliza

‘Mmhh,…kuliona …!!Lakini nikuulize kwanza, ni kwanini unamshuku rafiki yako, kaua, kafanya jambo gani baya sana,  maana unavyouliza ni kama vile kuna kesi ya mauaji,..., au hahaha, kufamaniwa, …hapana huyo sio mume wangu, …ka-kafanya nini kikubwa hivyo, mbona hutaki kuniweka wazi?’ nikamuuliza.

‘Sijasema kuwa kafanya lolote baya, hilo uliweke akilini, ninachotaka kukifanya hapa ni kutafuta kama kuna tatizo, ta-ti-zo ...je  huko kuendesha gari kwake kwa kasi huoni kuwa kuna kitu kilitokea akawa anakimbia, au kuna jambo alikuwa akilifuatilia nyumbani kwa haraka, huenda alikuwa anakuja kuku....’akakatisha

‘Unataka kusema alikuwa anakuja kutaka kunifumania au....acha hayo mawazo hayo docta, wewe ni msomi bwana…na familia yangu ni ya watu wastaarabu, hakuna mwenye tabia chafu kama hiyo...kama unayo wewe usifikirie kila mtu ana tabia kama hiyo.’nikasema kwa hasira.

‘Hahaha…lakini, unanifahamu sana, nilivyo, lakini vyovyote iwavyo, sote sisi ni wanadamu inaweza kutokea  mtu akateleza, jua ibilisi mkubwa wa mwanadamu ni mwanadamu .., huwezi jua,...hata wewe unaweza kughilibiwa ukajikuta umefanya jambo ambalo baadaye linakuja kukuleta matatizo, ukawa unatafuta njia ya kujisafisha, lakini wenzako wameshaliona na huenda wamekuweka kati, dunia hii ina watu wabaya.....’akasema

‘Mpaka sasa sijakuelewa msingi wa maswali yako...unachokitafuta hasa ni nini, kuwa mimi nina matatizo au mwenzangu ana matatizo?’ nikamuuliza.

‘Sijawa na uhakika na hilo ndio maana nakuuliza ...maana kama wewe ungeliweka wazi, kuwa kuna tatizo, kwako au kwa mwenzako, ningejua jinsi gani ya kufanya, na nini  nifanye ili niweze kusaidia, lakini naona nyote mnanificha, ndio maana najaribu kuwa mpelelezi, kwa nia njema kabisa ....’akasema.

‘Yatakushinda....siku hizi umeacha kazi yako ya udakitari unaanza kufuatilia ndoa za watu, haya na ili upate faida gani...’nikasema na yeye akaangalia saa yake, halafu akasema;

‘Kuna watu wawili wanaweza kutusaidia kwa hil tatizo , ...ili kugundua kuwa huenda mwenzetu ana tatizo gani, hadi sasa kwa uoni wangu nimeona kuwa kuna tatizo, sasa ni tatizo gani, ni muhimu sana tusaidiane kulitafuta haraka iwezekanavyo kabla hali haijawa mbaya zaidi, ...’akasema.

‘Umeona kuwa kuna tatizo, umeona kuna tatizo gani,..kuwa huenda ajali hiyo ilikuwa na msukumo fulani, si ndio maana yake hiyo, au..?’nikasema kwa upole, kwani hapo niliona kuna hoja ya msingi.

‘Ndio ...hebu angalai hili bila kujali kuwa mimi ndiye nalifuatilia, angalia kwa nia ya kumsaidia mwenzako, na hatimaye kuisaidia ndoa yako, na urafiki wenu na huyo rafiki yako, huenda tatizo limeanzia kwako bila kufahamu ...’akasema.

‘Nani na nani wanaweza kutusaidia sasa, maana hili naona umelivalia njuga, na ukianzisha jambo lako mpaka upate majibu, haya ili tuyamalize haya, ni nani anaweza kutusaidia, nataka uwe huru, kuwa unavyohisi sio kweli, ni nani atatusaidia....?’ nikauliza na yeye akasogea karibu yangu, na kusema kwa upole.

‘Wa kwanza ni mdogo wa mume wako, ....japokuwa kwenye ajali hiyo hakuwepo , lakini nahisi anafahamu mengi kuhusu mienendo ya kaka yake....huyo naweza kuongea naye mimi, naona uniachie mimi huyo mtu,..nitambana mpaka atanieleza...’akasema

‘Sawa nakuachia wewe hilo…na mwingine au huyo anatosha…?’ nikamuuliza, hapo nilianza kuingiwa na mawazo , nikijiulia kweli ni kwanini mume wangu aliendesha gari kwa mwendo huo, na ni kinyume na tabia yake, ...basi kulikuwa na jambo, lakini mbona hata mimi niliendesha kwa mwendo kasi,nilipopewa ujumbe huo kuja nyumbani haraka,kumbe  inawezekana ikatokea hivyo ..

‘Kama ni kujua kwanini alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi, mimi naona hakuna cha muhimu hapo, mbona hata mimi , leo nilijikuta nikiendesha kwa mwendo kasi  uliponipigia simu kuwa nije nyumbani kwa haraka, kwasababu kuna tatizo huku nyumbani...na sikujua kabisa kuwa nilikuwa naendesha kwa mwendo kasi.....’nikasema.

‘Unaonaeeh,wewe ulifanya hivyo kuja nyumbani kwasababu hiyo ya msingi, je mume alifanya hivyo kwasababu gani ya msingi.., nikuulize swali ili uone kuwa kuna tatizo, je mume wako ana tabia ya kuendesha gari kwa fujo, hapana au sio namafahamu sana?’ akaniuliza.

‘Hana kabisa tabia hiyo, ndio maana nashindwa kuelewa,.....’nikasema.

‘Unaonaeeh, sasa tunaanza kuwa pamoja..?’ akawa kama ananiuliza.

‘Ninaona nini hapo, kuwa pamoja kwa vipi, mimi nataka nifane unavyotaka wewe, sawa, hisia zipo, na kiukweli sio kwamba sina hisia kama zako, lakini nazipotezea, maana hao ni watu nawaamini, sasa kama kuna walakini, haya ngoja tuutafute, sawa?’ nikamuuliza.

‘Ndio maana yake mimi nina imani kuwa  mume wako alikuwa akikimbia tatizo,....maana kama wewe huna tabia anayoihisi mume wako,...na alifahamu kuwa haupo nyumbani, basi huenda alikuwa akikimbia jambo, sasa alikuwa akikimbia jambo gani, au alikuwa akifuatilia jambo gani, ataulizwa hilo na watu wengi wakiwemo watu wa usalama, bima nk......’akasema, na mimi hapo nikatulia kidogo nikiwaza.

‘Yawezekana ndio,…ndio maana hata hakutaka kwenda hospitalini...’nikasema.

‘Kwahiyo huyo mmoja, anatosha kutusaidia….?’ nikauliza

‘Mtu wa pili ambaye anaweza kutusaidia ni rafiki yako, ....’akasema.

‘Kwani vipi shemeji ....rafiki yangu anahusikanaje na mambo yangu ya kifamilia..au ajali ya mume wangu, hapo ….ok, ok, ….lakini kama na yeye ni muhusika, atanisaidiaje,, hebu niambie hapo,?’ nikamuuliza .

‘Akusaidie kujua kama anafahamu lolote, kuhusiana na mume wako, kama kuna tatizo linalomsumbua, maana inawezekana mume wako yupo kwenye mtego wa watu wanaomtishia amani, labda kama asipofanya hivi au vile anaweza akaingizwa kwenye matatizo, ....nasema tu, kama mfano, ....'akasema

'Mhh, huko umekwenda mbali, rafiki yangu amrubuni mume wangu, na amwambie kuwa asipofanya hivyo, atafanya vile..kwanini..hapana, kwa maana hilo alilofanya rafiki yangu, tulishauriana mimi na yeye, sasa kwanini ...'nikasema

'Mlishauriana, ndio, lakini umesema, hkumshauri amtafute mume gani, au sio..je kama alimtafuta mume wako,...?' akaniuliza na kunifanya nishtuke

'Acha hayo maneno kabisa, usinichafue...hivi nikuulize kuna mtu anaweza kutembea na shemeji yake mwenye akili timamu, unazungumzia hapo rafiki yangu, unamfahamu kabisa alivyo, hapendii kabisa kutembea na wanaume  za watu, ...usimzushie rafiki yangu uwongo....'nikasema

'Kuna kitu nataka tukihakiki...je wewe unaweza kufanya hivyo, kuongea na rafiki yako, au, nina wazo, hebu fanya hivi, unaweza ukamuita rafiki yako , akaja hapa hospitalini, na ikiwezekana aje na mtoto wake, anaweza kuja, au sio..?’ akaniuliza.

‘Aje na mtoto, ...mhh, kwanini lakini, yupe bado ni mzazi, kwanini tumsumbue, atoke ahuko na mtoto kwanini lakini...na huyo mtoto wake unamuhitajia nini...hahaha nimeshakuelewa, unataka kufanya nini...hapana siwezo...’ akasema.

'Sikiliza...ni muhimu sana...fanya hivyo, kuna kitu nimekiona , fanya hivyo, muite rafiki yako aje hapa hospitalini,..na mtoto, ....unaweza kufanya hivyo...?' akasema

'Mhh.....' nikaishia kuguna, na sikuelewa kabisa docta anataka nini, lakini, ....

NB: Docta anataka nini hapa, …mtoto…mtoto wa nini…?

WAZO LA LEO: Urafiki wa kweli ni wa kujaliana, mwenzako akipatwa na tatizo, iwe ni kama wewe umepetwa na tatizo hilo. Ni faraja sana ukiwa na tatizo rafiki yako akawa anatafuta njia ya kukusaidia.


Ni mimi: emu-three

No comments :