Hatukuweza kuafikiana siku hiyo, hadi siku nyingine tukakutana
tena hospitalini, na docta akafufua yale mazungumzo yetu…
‘Unakumbuka nilikuuliza jambo, tukawa hatukuelewana…nahisi
hukunielewa dhamira yangu,..nimeliwaza sana hilo nikaona ni lazima tuliongee na
tufikie muafaka, sijui unanielewa….?’ akaniuliza na mimi nikawa nimeinama
nikiwaza mengi kichwani. Nimekuwa mtu wa mawazo sana kiukweli. Sipati usingizi
kabisa, na nahisi itanieletea matatizo, kwahiyo nikaona ni vyema nisikilizane
na docta tu..
‘Lakini, mimi sijaona kosa langu, sijaona kuwa nina matatizo
kihivyo…, sioni kabisa, kichwa changu kimetaliwa na kazi zangu za kiofisi mambo
mengine ni ya kifamilia zaidi, ni mambo ya kawaida tu na nina imani yataisha tu…,sasa ukiniambia nikuambie kila
tatizo la familia yangu unakosea….’nikasema
‘Shemeji, umesema una matatizo ukayataja matatizo kuwa yapo
matatozo ndani ya nyumba yako..ambayo uliyaita ni ya kifamilia, ambayo naona umeshindwa
kuyasema ni matatizo gani, kwangu nahisi huenda yakawa ndio chanzo cha yote
hayo mengine..sijui lakini nahisi hivyo, maana hujanifafanulia...’akasema na
mimi nikawa nimetulia tu.
‘Lakini pia ulisema kuwa kuna matatizo ya huko kazini kwako, hayo
ukasema ni matatizo ya kawaida tu ya
kikazi , au sio, siwezi kuingilia mambo ya utawala wako wa kikazi, sawa
nimekubali kwa hilo, huko ni kwako na utaalamu wako…?’
‘Yap…ya kawaida..napambana nayo, …’nikasema
'Hata hivyo nakushauri, hayo mambo ya kikazi, usiyaweke akilini
sana, yakawa ndio kipaumbele chako,
kiasi kwamba yanameza maswala ya familia yako, kwani unafany akzi ili
iweje, ni kwa masilahi ya familia yako, au sio…sasa ukiumiza kichw ahuko, kazi,
ukaupa mgongo, ndo ayako utakuwa umefanya nini…unielewe hapo…’akasema
‘Sawa nimekuelewa docta….’nikasema
‘Lakini kuna hili,…ulisema kuwa kuna matatizo huko kwa rafiki
yako,…kuna kitu nataka tuje kukijadili, sio kwa utesi,..sipendi tabia hiyo,
bali nataka tujenge na kuondoa tatizo kama lipo…kwa kulianza hili je huko kwa
rafiki yako kuna tatizo gani hasa la
kukusumbua kichwa, maana huyo ni rafiki yako, kama nilivyo mimi, au sio…,?’
akaniuliza
‘Huko kwa rafiki yangu ni matatizo ya kawaida pia, wala
yasikuumize kichwa, yule ni rafiki yangu namuona kama mdogo wangu , japokuwa
tunalingana ki- umri. Kwahiyo mimi kama mzazi lipo ndani ya uwezo wangu....’nikasema
na yeye akaendelea kusema;
‘Hata kama ni ya kawaida...kama unavyodai, kitu ambacho sikiamini,
kwa vile umeshataja kuwa ni matatizo, ina maana yapo akilini mwako, na yanakusmbua
akilini, na yanaweza kukupa matatizo, ukadondoka kwa shinikizo la damu, huwa
inatokea, sasa isje kufika huko,…’akasema na nilikuwa sijamueleza kuwa
nilipoteza fahamu.
‘Mhh, hata sikuelewi, …kwanini lakini, au kuna kitu unakijua mimi
sikijui, kwanini usiniambie tu, kuliko tuzunguke zunguke…’nikasema
‘Kuna kitu nahisi kuwa kipo kati yako wewe na mume wako
hujaniambia…, na kuna tatizo kati yako wewe na rafiki yako, nataka kulijua hilo,
kuna kitu ambacho ungeniambia, ningeliweza
kuhitimisha hilo ninalolifikiria mimi na tukaangalia njia sahihi ya kulitatua…,
lakini kawaida yangu kama unijuavyo,…sipendeleo haya, nimekusihi uniambie wewe
kwa vile ni rafiki yangu tu, la sivyo
nisingelihangaika kabisa…’akasema
‘Ndio maana nakushangaa naona kama umebadilika siku hizi…, sio
kawaida yako, kwanini uyatake haya ya watu, kuyafahamu,… na mwenyewe mara kwa
mara umekuwa ukinikanya kuwa nisiwe na tabia ya kufuatilia mambo ya watu
wengine.., na nisiwe mtu wa dhana mbaya kwa watu, au sio wewe…’nikasema
‘Hili sio la dhana mbaya…, ila mimi nataka nikusaidie ili baadae
usije kunilauamu, najua kabisa baadae unaweza kunilaumu, kuwa huenda, nahusika,
huenda nilijua, nataka nijitoe kabisa, lakini ni muhimu kwangu kulitatua hili
kadri inavyowezekana…sasa hebu niambie…huyo rafiki yako, ana kukwanza nini, ni
kuhusu ndoa yako…?’ akaniuliza tena
‘Ananikwanza,…!!! Sijasema hivyo… Nani kazungumzia kukwazana
kwenye ndoa hapo!!!…nikuambie ukweli, huyo rafiki yangu hahusiani kabisa na
lolote katika ndoa yangu,...nakuomba usije ukamuhusisha rafiki yangu na haya
maswala yangu,..hahusiki na lolote lile..hilo nakuthibitishia...hayo matatizo
niliyosema kuhusu mimi na yeye, ni
matatizo ya kawaida tu kati yangu mimi na yeye, hata mume wangu hajui...’nikasema.
‘Nikuulize kitu, unakubaliana na mimi kuwa mume wako yupo karibu
sana na huyo rafiki yako..?’ nikauliza
‘Ndio hilo halina siri..ila kwa vipi sasa …kwa jinsi unavyofikiria
wewe unakosea, sivyo hivyo, acha hilo…’nikasema
‘Nisawa nitaliacha, ila…, nataka kuwa na uhakika tu kuwa hilo
umeliridhia, kuwa mume wako yupo karibu na rafiki yako, wanakula pamoja,
wanatoka wakati mwingine pamoja…na imekuwa sipo karibu sana na yeye kwa vile
wanakuwa na huyo rafiki yako,.utasema labda nawaonea wivu, hapa…sasa ,.je hilo
halina wivu kwako wewe, na sio sababu ya
matatizo yako na rafiki yako, …wivu labda..?’ akauliza.
‘Karibu sana kwa vipi…ndio, kama umewaona wanaongea, au wanakula
chakula pamoja, ni kawaida tu, tumezoea hivyo, wala usiwafikirie vibaya, siwezi
kabisa kuona wivu kwa rafiki yangu, kuwa na mume wangu hivyo, na sizani kama
inaweza kwenda zaidi ya hivyo, mengine ni dhana zako potofu, na ni wivu wako
unakusumbua….’nikasema
‘Kama ni hivyo, sawa, kama umeliridhia hilo, sawa…na sio kwamba
nawachimba, au wivu kama unavyodai, hapana, ndio maana nilitaka uhakika kutoka kwako,
nilijua hayo matatizo na rafiki yako huenda ni maswala ya wivu, ok sasa…ili tusaidiane,
na mimi nirizike, eeh, ..maana kuna kitu kinanitia mashaka…’akasema
‘Kipi hicho kinachokutia mashaka, kuhusu rafiki yangu na mume
wangu au…?’ nikauliza
‘Rafiki yako naona kakimbilia kuzaa kwa kuchelea umri, au sio, ni
sawa maana aliwahi kuongea na mimi, kuhusu hilo, na mimi kama dakitari
nikamshauri kuwa ni bora aolewe mapema, maana umri umekwenda, akasema yupo
mbioni kulitatua hilo, nikajua keshapata mume , sasa naona kazaa, simuoni huyo
mume…’akasema
‘Ndio hivyo hakuna shida, au ulitakaje wewe,…?’ nikamuuliza
‘Nilimuambia awe lakini awe makini sana na mawazo hayo…maana
yanaweza kumpelekea akataka kuzaa tu, kwasababu ya kukimbizana na umri…lakini
hakutaka kuongea na mimi zaidi, ni kweli kuna muda alikuwa karibu sana na mimi,
mpaka watu wakatushuku vibaya, hata mke wangu, nikaona aah, tukakosana...’akasema
‘Ndio niliwaona mkiwa sambamba, lakini mimi nilijua mumarafiki tu
kama alivyo karibu na mume wangu, japokuwa …alikuja kuniambia ulimtaka kweli si
kweli…’nikasema
‘Hahaha, hayo yaache, sasa ni hivi, maana wewe ndiye rafiki yake,
kwanini akaamua kuzaa bila kufunga ndoa, ulimshauri wewe hivyo, na je baba wa
mtoto wake ni nani?’ akaniuliza huku
akiniangalia kwa macho ya udadisi, na mimi kwanza nikaguna, halafu nikaangalia
pembeni na kusema;
‘Hilo hata mimi sijui..labda baba wa mtoto ni wewe,maana mlikuwa
marafiki au sio, sasa sijui ,.. au ndio maana unataka kuchunguza kuhakiki kama
mtoto ni wako au ni wa matu mwingine…’nikasema.
‘Aaah, sio wangu bwana.. .kama angelikuwa ni wa kwangu
angelifanana na mimi, sura yangu haijifichi..na wewe ungelishaniambia , na
nafahamu wewe unafahamu mwenzako katembea na nani , kweli si kweli...?'
akaniuliza lakini kabla sijamjibu akasema
'Hivi wewe una uhakika kuwa mume wako hajawahi kutongoza wanawake
wengine...hata kiutani tu, hayo yanatokea tu,...lakini baadaye unajirudi,...
lakini hayo tuyaache maana ilikuwa zilipendwa, sasa niambie ukweli, unamfahamu
aliyezaaa na rafiki yako, maana mimi naulizwa na wazazi wake...’akasema.
‘Mimi simfahamu....’nikasema .
‘Ok. Sio shida, nimewaambi ahivyo hivyo, lakini kuna mambo mengi
wameniuliza, hasa kuhus urafiki wako na mwenzako…mmh, unajua mambo mengine
unaweza ukayaficha, lakini wazee ni wepesi sana kuyagundua…’akasema.
‘Walisemaje…?’ nikauliza.
‘Hebu nikuulize kwanza, una
uhakika kuwa kweli mume wako hakuwa ametokea huko kwa huyo rafiki yako?’
akaniuliza swali hilo na kunifanya
nishtuke kidogo. Akilini nikajiwa na kumbukumbu, kuwa kuna muda niliona gari
kama la mume wangu, pili, yule kijana wa kuosha magari, alisema ‘shemeji
alikuwepo, huyu naye anasisitiza hilo hilo, na sijui anataka kuthibitisha nini…
‘Mimi nilikuwa huko kwa
rafiki yangu...kama mume wangu angelikuwa huko si ningelimuona jamani…, labda
alipita njia hiyo, sijui akitokea wapi, na sina uhakika na hilo, maana nijuavyo
mimi alikuwa kwenye kikao…sasa alitokea wapi akapitia njia hiyo mimi sijui..’nikasema.
‘Kwahiyo mkiwa huko hukumuona mtu, aliyefika kwa rafiki yako,
au….?’ Akauliza
‘Labda mdogo wake, nahisi hivyo tu…’nikasema
‘Mdogo wake!!!’ akasema kwa mshangao
‘Nahisi hivyo tu…sina uhakika…’nikasema
‘Kwanini unahisi hivyo…?’ nikaulizwa
‘Nimekuambia sina uhakika, tuliachie hapo tu, maana unanichimba
sijui unatafuta nini…’nikasema hivyo maana nilijua hilo linaweza kuendelezwa
mpaka nikasema yasiyotakiwa kusemwa.
‘Mbona mdogo wake, nilikuwa naye, alikuja kwangu kuna mambo fulani
ya mkewe aliyafuatilia kwangu, ya kiafya..tukawa naye hapa tukiangalia mpira
kwenye runinga,na niliachana naye muda mfupi, kabla sijapigiwa hiyo simu ya
ajali....sizani kwamba aliweza kuja huko kwa muda huo mfupi,...’akasema
‘Mlikuwa naye nyumbani kwako…?’ nikauliza kwa mshangao
‘Ndio…sasa sizani, kam ni yeye, hata hivyo, yeye aliniomba gari
langu kuwa anafuatilia mzigo wake, ndio maana nilishindwa kumchukua mume wako
kwa haraka, kwani sikuwa na gari...ndio maana pia tukaamua kuagiza gari la
wagonjwa....’akasema.
‘Ina maana gari lako mpaka sasa analo mdogo wa mume wangu?’
nikamuuliza.
‘Ndio maana yake, aliniazima gari langu , kwa vile gari la mumeo
alikuwa nalo kikazi, au sio, na anasema alipiga simu kwa mumeo akawa
hapatikani, ..haiwezekani akawa ndio yeye, labda yule mdogo wake mwingine, na
yule hayupo hapa dar, alisafiri jana kama si kosei kwenda mikoani....’akasema.
‘Basi kama sio yeye, kuna mtu mwingine anafanana na
….huyo….’nikasema
‘Kwanini unasema hivyo…?’ akauliza
‘Hapana, tuyaache tu, sioni kama kuna lolote baya,
nitamgudnua tu kuwa ni nani yangu, ninachotaka kusema, ni kuwa mimi nilihisi
kuwa yeye alifika huko kwa rafiki yangu wakati mimi nipo huko, kama sio
yeye.basi kuna mtu mwingine anayefafana naye....ni hivyo tu basi...’nikasema
nikiwa sina uhakika.
‘Mhh..nisamehe tu..akilini mwangu nahisi kuna tatizo
hapo,…’akasema
‘Tatizo gani…?’ nikauliza
‘Hebu niambie ukweli....unasema wakati upo huko, alifika mtu
anayefanana na mdogo wa mume wako si ndio hivyo, nyie muda huo mlikuwa ndani,
au nje…?’ akauliza
‘Tulikuwa ndani…’nikasema
‘Sasa ulimuonaje kuwa anafanana na shemeji yako…?’ akauliza
‘Mhh..nilihisi tu hivyo, kwa vile mtoto anafanana na shemeji, na
huyo aliyekuja alikuwa ….eeh, sasa unataka niongee yale ambayo sikutakiwa
niyaongee…’nikasema
‘Nimekuelewa kuwa hisia zako kuwa huyo aliyezaa na rafiki yako,
anafanana na mtoto wake, na huyo mtoto anafanana na shemeji yako, … sawa, lakin
huna uhakika maana hukutoka ukamuona sawa, na kwahiyo ..eeh, …inawezekana
hakuwa huyo shemeji yako, kama unavyofikiria wewe, labda alikuwa ni mtu
mwingine au sio, ?’akasema na kuniuliza
‘Ni hivyo lakini rafiki yangu alisema ni shemeji ..akiwa na maana
shemeji yangu ndivyo nilivyo muelewa…’nikasema na docta kacheka kiddogo
‘Ah, shemeji..ok…kwa maana nyingine wewe ulifananisha huyo mtu na
shemeji yako wewe…, kwa kuhisi tu, kwa kupitia kwa mtoto,….na hakutaka wewe umuone,
au sio, kwahiyo yeye…shemeji,…alipogundua kuwa upo hapo, ...akaondoka kwa haraka…au sio.., hamkuonana
naye, uso kwa uso…au sio…?’ akauliza
‘Ndio, kwahiyo unataka kujenga hoja gani hapo…?’ nikamuuliza
‘Nijibu kwanza , …kuna kitu nataka kukipata hapo, ..kwa leo sitaki
unielewe vibaya..’akasema
‘Sawa, …ndio, lakini sikuonana na yeye maana alikimbia,..’nikasema
‘Alikimbia!!!..alikimbia,.., kwanini akimbie hapo kuna ulizo,
majibu ya haraka ni ili usimuone, labda, kwa vile alitaka iwe siri, lakini
anajua kabisa wewe ni rafiki yake au sio..ila wewe ulitaka kuonana naye, ili
muweze kuliweka sawa, au sio, kwa nia njema, lakini akakimbia..au sio?’
akaniuliza
‘Mimi nilitaka niongee na yeye, lakini rafiki yangu hakutaka
nikutane naye, na hata yeye alimuonya rafiki yake kuwa hataki yeye kujulikana,…nikaona
ananiwekea uzito, ndio nikatoka nje , …sikumuona kwa wakati huo, kumbe alikuwa
kajificha, sasa wakati nipo ndani ndio nikasikia akikimbia huko nje…’nikasema.
‘Mpaka hapo inaashiria kuwa huyo mtu , ni mtu wako wa karibu
hakutaka kabisa umuone, umeona hapo..na hadi kukimbia hivyo, ina maana kubwa,
hakutarajia kukuta wewe hapo, ndio maana akakimbia, na huenda alipofika kwenye
gari lake, akalichukua na kuendesha kwa kasi sana, sasa wewe huoni ni nani huyo
mtu…?’ akauliza
‘Sioni kuwa ni nani….hapana…sijaona kuwa ni nani zaidi ya shemeji
yangu, ..lakini sina uhakika , maana sikuonana naye……’nikasema
‘Nje kulikuwa hakuna gari, gari lake alikuwa kaliweka wapi..?’
akaniuliza
‘Sikuliona gari lake hapo nje…na sijui alikuwa kaliacha wapi....’nikasema
‘Je ana gari, rafiki yako hakukuambia hilo?’ akaniuliza
‘Ndio analo, lakini hakuliacha hapo nyumbani,…na rafiki yangu
hawezi kujua aliliacha wapi, maana alikuwa hajaingia wakaongea…’nikasema
‘Kwahiyo huyo mtu alipotoka hapo, alipogundua kuwa ni wewe,
akaogopa akihisi kuwa atamfuatiliwa, utakuja kumgundua kuwa ni yeye, akatoka
akalifuata gari lake akaondoka kwa mwendo kasi, au sio….?’ Akasema
‘Unataka kusema nini hapo mbona unarudia rudia hilo la ‘mwendo
kasi’
Najua dhana yako…, kuwa labda anaweza akawa ni mume wangu au si
ndio hivyo...?’nikamuuliza.
‘Mimi sijafikia kuhitimisha hivyo, ninachotaka ni kukuweka katika
hali ya kuyakubali yote, kwasababu nijuavyo mimi, mume wako hawezi kukuficha
kitu, au sio.. na kama kuna kitu kakifanya, atakuwa na wakati mgumu wa kutafuta
ni namna gani atakuambia …hiyo ajali yake sio ya kawaida, kuna kitu hapo, ndio
maana najaribu kutafuta hilo, ili umsaidie yeye, apone haraka…’akasema
‘Sio mume wangu, kwani kama angelikuwa ni yeye, kwanini alifika
kwa haraka, halafu anikimbie, si alikuja kwa nia njema kumsalimia shemeji yake...kuna
tatizo gani la kunikimbia mimi…, ndio maana nasema sio yeye, hilo sikubaliani
nalo...mume wangu hana tabia kama hiyo...’nikasema nikijaribu kumuwazia huyo
mtu aliyefika na kukimbia anaweza kuwa ni nani.
‘Kwani huyo mtu aliyefika, mkiwa huko ndani na rafiki yako alifikafikaje,
kuna kitu gani cha tofauti unaweza kusema huyo mtu alikuwa nacho, cha kuweza
kumkumbuka,,..?’ akaniuliza.
‘Viatu vyake vilikuwa vikitoa sauti,….’nikasema.
‘Mume wako alikuwa kavaa viatu vya kutoa sauti asubuhi ..?’
akaniuliza
‘Mhh.. ndio alivaa viatu vya kutoa sauti, lakini huo sio ushahidi
tosha, au sio…’nikasema
‘Ok…hebu nirejee nyuma kidogo…, samahani lakini, rafiki yako
alisema huyo aliyekuja wakati ukiwa kwake ndiye aliyezaa naye, sawa si sawa…?’
akaniuliza
‘Ndio, na alimpigia simu nikiwa pale…’nikasema
‘Una uhakika na hilo…’akasema akiniangalia kwa makini.
‘Uhakika wa nini sasa…, si yeye kaniambia hivyo, nitakuwa na
uhakika gani zaidi ya kauli yake, au…’nikasema
‘Na ukiwa ndani, ukasikia akikimbia, lengo ni ili wewe usimuone,
ulisikia viatu vyenye sauti…?’ akauliza
‘Itakuwa hivyo, ndio…’akasema
‘Kwahiyo hiyo kwa vyovyote huyo mtu aliyekimbia ni huyo huyo
aliyefika awali,…sio kwamba huyo ni mwingine alikuwa kajificha, nataka uwe na
uhakika hapo,…na kwa hiyo ndio huyo baba wa huyo mtoto, kutokana na kauli ya
rafiki yako, na wewe ulikuwa na hamu sana ya kukutana na yeye au sio….?’
Akauliza
‘Ndio, lakini mimi nilishahisi kuwa ni huyo mdogo wa mume wangu,
sasa ukisema mlikuwa naye hapa,…hapo sijui atakuwa ni nani mwingine…’nikasema.
‘Je tusaidiane kumtafuta huyo mtu…, kama ni muhimu sana kwako, na
kama itasaidia kuondoka hiyo hali ya wewe na rafiki yako…ili usiwe na wakati
mgumu,..?’ akauliza
‘Haina haja, sihitaji msaada wako kwa hilo….’nikasema
‘Sijui lakini…hata hivyo mimi nitaongea na rafiki yangu nitaujua
ukweli wote, sio muhimu kwangu sana, lakini sitaki ije kuleta mtafaruku kwenye
ndoa yenu,. Hata hivyo mimi…, sitaki sana kuingilia mahusiano yenu, …na usije
ukaniona labda nayaongea haya kwa nia ya kukuharibia ndoa yako, ila mimi nataka
nikuweke tayari, usije kusema mimi kama rafiki yako sikuwahi kukuambia hili,
ukanioana mbaya baadae, nakufahamu sana wewe…’akasema docta
‘Una maana gani kusema hivyo..?’ nikamuuliza
‘Je ikitokea kuwa huyo aliyefika wakati upo hapo kwa rafiki yako
ni mume wako utasemaje…’akasema
‘Unasema nini, kwanini unafikiria hivyo, najua wewe unawaza nini,
na hata wengine watawaza hivyo hivyo ,lakini wewe hujui mimi na rafiki yangu
tulikubaliana nini, na mimi nipo tayari kwa lolote lile..kwasababu ni mimi
nilimshauri, ila wewe unataka kuharibu kuwa yeye labda katembea na mume wangu ,
hawezi kufany ahivyo abadani, atakuwa ni mwehu basi, na mimi sitakubaliana na
hilo…?’ nikamuuliza kwa hamaki.
‘Ndio hapo…nawajibika kuingilia kati, ili kuwasaidia wewe na mume
wako…najua kwa vyovyote vile mimi ndiye nitakuwa mtu kati…na nakuelewa sana
wewe ulivyo….kuliko unavyojielewa wewe mwenyewe….ndio maana nataka kukusaidia
hili. Inawezekana ulim-mshauri mwenzako kitu na yeye akakichukulia juu kwa juu,
bila kuelewa lengo lako, …na akijua wewe ni rafiki unaweza kumtunzia siri
kuliko mtu yoyote yule, kwahiyo …’mimi hapo nikamkatisha na kusema;
‘Mhh, sikiliza, unajua najiuliza kama alikuwa ni mume wangu kama
unavyodai wewe, kuwa huenda alikuwa ni mume wangu basi kwanini, aogope kiasi hicho,mimi namfahamu sana mume
wangu..hanificho kitu akikosea, atanipigia magoti kutubu,.., na rafiki yangu
alisema huyo ndiye baba wa mtoto wake, …sasa atakuwaje ni mume wangu, hebu na
wewe lifikirie hilo, mume wangu ndio aje kutembea na mdogo wangu haiji akilini,…’nikasema.
‘Nimekuuliza tu, …kama ikitokea ndio hivyo, ndio yeye, bado
utakubali kuwa ndiye baba wa huyo mtoto, …’akasema
‘Haiwezekani, akawa ndio yeye bwana, sitakubali kabisa,, ...mume
wangu hawezi kutembea na rafiki yangu, na rafiki yangu ambaye nimemchukulia sawa na
ndugu yangu, rafiki yangu hawezi kunisaliti, hilo halina maana, na wala
tusiliongelee zaidi maana linaweza kujenga dhana mbaya,,...kabisa
haiwezekani...kwanini,,,.’ nakasema nikionyesha kukereka.
‘Je ikiwa na kweli, utafanya nini..?’ akaniuliza
‘Haaah, weee, tuliache hilo, sitaki hata kufikiri, ndio maana
nasema sio yeye, rafiki yangu pamoja na yote ananifaham nilivyo…labda ahame
nchi, ..mungu wangu, sio yeye, sio mume wangu…’nikasema nikiwa na kitu moyoni
kinaniwasha.
‘Unajua nilipomuona mtoto,…na yote yanayoendelea hivi sasa
nimekuwa nikiliwazia hilo, nakuelewa wewe sana,…je wewe au mume wako,
itakuwaje,… na sijui, kwanini nilimshauri rafiki yako ajitahidi kuzaa kwani
umri umepitiliza, nahisi alilichukulia ushauri wangu huo kwa pupa …kiukweli
mimi nilimshauri hivyo na sitaki kujilaumu maana sikumshauri akatembee na waume
za watu…’akasema
‘Mbona hata mimi nilimshauri hivyo…’ nikasema
‘Ndio kama ulishauri hivyo kuwa aolewe, ili azae, ulikuwa ushauri
mnzuri, kiukweli, kiumri na …rika lake, alitakiwa aolewe, na mimi nilimshauri
mengi tu, na hakutaka kuwa muwazi kwangu, kuwa ana mipango gani,…na labda
alishanichukulia vibaya, kwasababu tulishakorofishana…kwahiyo nikajua ni lazima
atakuwa kaja kwako,….’akasema
‘Ndio alikuja kwangu, nikamshauri hivyo,… mengine ni siri yangu
mimi na yeye…’nikasema
‘Umeona eeh , hapo unanificha, na hapo nahisi kuna siri kubwa,
ambayo inaweza kutengua hiki kitendawili…kwahiyo wewe ulimshauri hivyo kuwa ni
bora azae kwanza, kwa vipi sasa, maana hilo hakutaka mimi nimuingilie, alisema
atalifanyia kazi…’akasema
‘Kwahiyo kumbe wewe unanitega ili ujue niliongea nini na rafiki
yangu, kuwa labda nimemshauri akatembee na mume wangu, hivi ukiwazia hivyo,
unanifanya mimi ni juha au…’nikasema kwa hamaki
‘Nakuuliza hivi nikiwa na maana, unielewe sana hapo,…mpaka nakuuliza haya
nimeyatafakari sana, nakupenda, na kukujali, nawapenda wewe na mume wako,
sitafurahi ndoa yenu ikija kuvunjika, ubaya unaweza kutendwa, kwa bahati mbaya,
na hatujui hadi sasa ni kipi kilitendeka,..mimi kuna muda nilikuambia urafiki
wako na mwenzako, ni sawa..siukatai…, lakini usifikikie kumuamini sana
kihivyo.., ukasema ni kwa vile mimi eti nilimtongaza huiyo rafiki yako
akanikataa…’akasema
‘Ndio hivyo..nawafahamu sana nyie wanaume mlivyo…’nikasema
‘Sasa nikuulize tena ulimshauri vipi maana nijuavyo, yeye hakutaka
kuolewa kwa sababu zake za kumtafuta mume ambaye hajazaliwa, kawakataa wanaume
wengi tu, mimi mwenyewe niliwahi kumwambia kuna rafiki yangu anataka kumuoa,
akamkataa, anasema haendani na yeye, na hilo ndilo lilifanya mim na yeye
tukosane dio hivyo mnavyofiria nyie, kuwa nilimtongaza akanikataa,….’akasema
‘Ndio tatizo lake yeye, kuwakataa wanaume,..ndio nikamshauri
hivyo, kuwa bora atafute mume azae naye....lakini hayo yameshapita , kazaa
basi, haina haja ya kulijadili hilo saana…, nahisi tukilijadili hilo, tutafikia
sehemu sisi wenyewe hatutaelewana, na sitaki tufikie huko…’nikasema
‘Una uhakika na hilo kweli, halikuumizi akilini kweli, na baada ya
kuyaongea haya nahisi litazidi kukuumiza kichwa, je ..ni kweli kuwa hutaki kumtambua baba wa huyo mtoto wa rafiki
yako,…?’ docta akauliza
‘Nitamfahamu tu,….mimi mwenyewe, au yeye mama wa mtoto ataniambia,
maana tulishakubaliana hilo, hawezi kunificha mimi rafiki yake,…’nikasema
‘Hataweza kukuambia, hilo nakumbia ukweli, kwa jinsi
ninavyokufahamu wewe ulivyo, lazima atakuwa kaagopa, huenda alivyofikiria yeye
awali, sivyo ulivyokuja kukusikia ukilipokea, na kiukweli,…, sasa naomba
tusaidiane kwa hili, ili wewe uwe na amani, leo na baadae …’akasema
‘Kwanini unasema hivyo…?’ nikamuuliza
‘Nina uhakika kwa hali hii ilivyo, kama rafiki yako atakuja
kukuambia ukweli, kitu ambacho sizani kama atakifanya …kwani nina uhakika kuwa mtakuja kukosana na yeye kabisa…’akasema docta
‘Docta, docta….docta, najua wewe umeshajenga dhana fulani, na wewe
kila mara umekuwa ukinikanya kuhusu hilo, kwanini sasa wataka kuliendekeza
hilo, na kumbuka kama ndivyo hivyo, unavyodhania wewe utakuja kukosana na
rafiki yako…je kama akisikia hivyo, na nina uhakika sio kweli…itakuwaje…’nikasema
‘Wewe ni rafiki yangu
hatufichani, au sio, na tumekuwa hivyo, nikiwa na tatizo nakuambia wewe
hata likimuhusu mke wangu, unanishauri, na mambo yanakuwa sawa…nashukuru sana
kwa hilo,…na halikadhalika mimi umekuwa
ukiniuliza maswala mengi haya yanayomuhusu mume wako…nakushauri
unayamaliza…’akasema
‘Ndio hivyo nikikwama huwa nakuuliza lakini ukiona sijakuuliza
ujue sijakwama, na kwa hili sijakwama..ndio maana ….’nikakatisha
‘Hapana, sema kwa vile ..unahisi wewe ulifanya makosa …sawa, ila
nakuuliza tena, je una uhakika hutaki kumfahamu huyo mwanaume aliyezaa na
rafiki yako…?’ akaniuliza
‘Nimeshakuambia nitamfahamu mimi mwenyewe…’nikasema
‘Sawa kama hutaki, siwezi kukulazimisha, lakini kama unataka nikusaidie
hilo, nipo tayari, ila uniahidi kuwa hutalichukulia vibaya, ...nia ni muhimu umfahamu
na ujue ni nini utafanya kwa masilahi ya ndoa yako na maisha yako, basi
tulimalize hivyo, mana muda umekwenda…’akasema
‘Nikuulize kitu, wewe una uhakika na unachokidhania…?’ nikamuuliza
Na yeye akaangalia saa halafu akatabasamu, …simu yake ikaita, akaniangalia
usoni, halafu akasema
‘Ngoja nipokee hii simu…ni rafiki yako, kanipigia…’akasema
‘Rafiki yangu…!!!’ nikajikuta nasema hivyo kwa hamaki, sijui
kwanini naanza kuhamaki, labda ni kwa vile docta kajenga hizo dhana mbaya, au
labda..hata sijui, nikasubiria kusikia docta anaongea nini na rafiki yangu..
WAZO LA LEO: Je ukiwa unaufahamu ukweli kuhusu rafiki
yako, na unaogopa ukimwambia ukweli huyo rafiki yako inaweza kuleta mtafaruku
na mkewe, utafanya nini…?’ ni swali niliulizwa, na jibu langu likawa hivi… ‘ukwel
wakati wote ni silaha ya ushindi, lakini hekima yake ni ngao, inatakiwa tuwe makini sana kwenye baadhi ya mambo,
maana ukweli unaweza ukaumiza, japokuwa ni kwa muda mfupi…na uwongo, ni hatari,
unaweza ukasaidia kwa muda mfupi lakini ukaja kuumiza kwa kipindi kirefu, na
kuharibu kabisa…sasa ni wewe mtoaji ushauri upime mwenyewe.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment