Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, October 30, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-17


‘Maswali gani hayo docta unayoniuliza, tulishawekeana mipaka kuhusu maswala ya ndoa yangu, na wewe ulishasema hutajaribu hata siku moja kuingilia ndoa yangu zaidi ya kusaidia kuijenga, au sio, sasa nikuulize…hayo maswala yako yanataka nini kwenye ndoa yangu, sipendi na sitaki, unanielewa…?’ nilikuta namuuliza kwa hamaki, lakini kabla docta hajasema lolote ndio akatokea huyo docta ambaye anamshughulikia mume wangu, na wote tukamsogelea.

Mimi nilikuwa sijamuona mapema hadi alipotukaribia…

‘Mpaka sasa hivi vipimo havionyeshi tatizo kubwa sana, matatizo yapo lakini sio ya kutisha,.tatizo ambalo limeonekana lipo kwenye uti wa mgongo, ambalo sio kubwa sana, ila inaweza ikachukua muda, kutegemeana na jinsi itakavyokuwa.., tutakuja kulijadili hili baadae,...'akasema docta

'Ila kwa hivi sasa itakuwa vigumu kwake kutembea, kuna athari hizo, lakini ni kwa muda,…na kuna vipimo vingine bado, havijawa sawa, ila kwa kifupi ndio hivyo…’akasema docta, na kabla hajaondoka docta huyu rafiki wa mume wangu akamsogelea wakawa wananong’ona kidogo.

Baadae yule docta akaondoka, na kutuacha tukitizamana, mimi nikamsogelea docta rafiki , nikamuuliza;

‘Ina maana mume wangu atakuwa hatembei tena, kwa muda gani …?’ nikauliza

‘Atatembea, ..ila kwa awali ni lazima atembelee kigari cha kukokota kwa mkono, hilo ni tatizo la muda, na kupona kwake kwa hivi sasa kwa haraka itategemeana na nyie wawili, hilo uwe makini nalo sana..’akasema

‘Kwa vipi..?’ nikauliza

‘Kwasababu pamoja na hayo, mawazo,…kutulizana kwa nafsi, kumliwaza na kumuondolea hofu, inategemeana na wewe ambaye mtakuwa naye karibu, ina maana hata kazi zako zingine inabidi uziache, ili asije akashikwa na msongo wa mawazo…’akasema

‘Mhh, sawa ni mume wangu hilo nalifahamu hata kabla ya kuambiwa, hata kama ni kuakia nyumbani siku zote mpaka apone nitafanya hivyo,..ila wasiwasi wangu, kama kaathirika utu wa mgongo mhh!!1…hata sijui nilitaka kuuliza nini…’nikasema

 Pale nilizama kwenye mawazo, na wakati huo docta alikuwa akiongea na simu alipomaliza, akanisogelea na kuniangalia machoni kwa makini, halafu akasema;

‘Najua unawaza nini….lakini ndio hali halisi, …muhimu ni kujua huyo ni mwenzako, na kwa hivi sasa anahitajia ukaribu wako sana, kuliko wakati wowote, na nakuomba sana, usije kumkwanza kwa maswali mengi ya kumtia mashaka…’akasema

‘Maswali gani ya kumtia mashaka….mimi siwezi kuwa hivyo, mimi sio mtoto mdogo, najua wajibu wangu..?’ nikamuuliza na kusema;

‘Ndio maana nilitangulia kukuuliza yale maswali yangu ya awali, nilitaka uwe tayari kwa matokeo hayo, na nijue jinsi gani ya kukushauri, ili sije ikaendeleza tatizo…’akasema

‘Lakini kwanza nikuulize hayo matokea ya vipimo vyake yana athari gani zaidi, ok, mnasema atapona, je akipona, atapona kabisa au …?’ nikauliza nikiwazia mbali zaidi.

‘Kabla sijakujibu swali lako nakuomba unijibu yale maswali yangu , maana yana mingi mkubwa wa maisha yenu,…najua, na nilijua utakuja kuniuliza maswali kama hayo, ndio maana nilitaka uniweke wazi, …unelewe hapo,…’akasema

‘Mhh…’nikaguna hivyo

‘Sikiliza, unaniamini sio…mimi ni rafiki yako, na tulikuwa wapenzi, nakufahamu kama ninavyomfahamu rafiki yangu, nataka kusaidia,.. na nisipoweza kulisaidia hili , nitakuwa sijaweza kuwatendea nyie marafiki zangu haki, kwa vile nahisi kuna dalili fulani isiyo ya kawaida ndani yenu…’akasema

Mimi pale nikajikuta nimtulia na kuzama kwenye mawazo…kwanza nikijiuliza ni kwanini docta ameuliza maswali haya, ina maana labda mume wangu aliwahi kulalamika kwake kuhusu maisha yetu ya ndani..na hilo swali la pili,…hayo ni mambo yangu na rafiki yangu je huyu docta inawezekana anayafahamu, na kama anayafahamu kaambiwa na nani…maana mimi sijaongea na mume wangu kuhus hiyo siri yangu na rafiki yangu...

‘Unawaza nini…?’ akaniuliza, na sikumjibu, nikawa nimetulia tu, nikiendelea kuwaza;

 Labda mume wangu aliwahi kuongea na rafiki yake kuhusu jinsi gani anavyotaka mtoto wa kiume, lakini hilo mbona halina msingi, sasa ni kwanini huyu mtu ananiuliza maswali haya… mahusiano ya kitandani yanamuhusu nini docta,..na sio kwamba anataka kuchokonoa ndoa yangu, ili iweje,… ni kweli nakiri kuwa  nimekuwa mvivu wa hilo, lakini sio ....hapana, nahisi docta ana lake jambo, sitamkubalia …


‘Zilipendwa, hayo maswali yako yana jibu moja tu, kuwa hayo hayakuhusu kabisa,  sijui kwanini unataka kuingilia maswala ya ndani ya ndoa ya mtu, unahisi sisi hatujui umuhimu wa ndoa,..au?   au umetuona sisi ni watoto wadogo…au ….nashindwa kukuelewa….na nikuulize labda…huenda, mwenzangu alishawahi kuja kukulalamika lolote kwako,.....?’ nikamuuliza

‘Sikiliza mimi nayafahamu hayo yote kabisa,…’akasema

‘Kwahiyo kumbe alishawahi kukuambia, eeh, si ndio hivyo…?’ nikauliza nikipandisha sauti.

‘Sikiliza…nazungumzia  kuhusu ndoa, na masharti yake ni kweli kuwa siri ya ndoa ni ya wana ndoa wenyewe…, ila mimi nimeuliza hayo maswali, sana sana sio kama docta, lakini pia kama rafiki yenu mpendwa, naweza kuhusika katika kuwasaidia, kwa nia njema kabisa, lakini kama utaona haina haja haya..sawa,lakini mimi sitachoka kuwasaidia…’akasema.

‘Mimi nakuuliza hivi, je rafiki yako aliwahi kuja kukulalamikia kuwa mimi simtimizii haki zake za ndoa, na ..hayo yanahusikanaje na hiyo ajali yake…kuwa alikuwa na mawazo hayo, hahaha, docta mengine naona hayahitajii udocta kuyafikiria, niambie ukweli, …?’ nikamuuliza.

‘Hajawahi kunilalamikia, hilo nikuambie ukweli, siwezi kukuficha , nikijua wewe ulikuwa mpenzi wangu, na sasa ni rafiki yangu, na tuliahidiana kuwa tutasaidiana kwa heri na shari, …mimi nataka kutimiza ahadi yetu hiyo sio zaidi ya hilo, suije kumfikiria mumeo vibaya, hajaniambia ....’akasema docta.

‘Kwahiyo hizo ni hisia zako tu,ambazo nahisi umezijenga tu, kwa vile....’ nikakatiza.

‘Hahaha,..eti kwa vile..malizia basi…! Sikiliza nikuambie..eeh, usiwe na dhana hiyo , narudia tena, nimekuuliza nikitaka kuwasaidia tu, kwasababu mimi siwezi kamwe kuingilia ndoa yenu,…kwanini nifanye hivyo, wakati nina mke tayari, ili iweje… na wakati wote nimekuwa nikiwasaidia,..leo kwanini iwe ni ajabu,… na maswali yangu hayo yamelenga katika kuwasaidia, kuna kitu nataka kukihakiki kwanza…’akasema

‘Zilipendwa, rafiki , mpenzi wa zamani… kiukweli swali lako hilo,  linaingilia mambo yetu ya ndani ya familia siwezi kukujibu, kwani jibu lake lipo wazi...kama kungelikuwa na tatizo juu ya hilo, ningeshakuambia…eeh, na  kama mimi ningelikuwa nimekiuka hayo, na nikawa sitimizi wajibu wangu kwake, yeye kama rafiki yako, angelikuja kwako kulalamika, kuwa nimekuwa mkaidi, je aliwahi kufanya hivyo, mbona unakwepa kunijibu hilo?’ nikamuuliza.

‘Hajawahi kufanya hivyo …hiyo dhana nimeiweka nikiwa na maana ya ujumuisho, kuwa mara nyingi, wanandoa wanaweza wakawa na matatizo kama hilo…, wakanyamaza, na wengine hasa wanaume wakalichukulia hilo kama kisingizio, kwa siri na kuanza kutoka nje ya ndoa, badala ya kulitafutia hilo tatizo ufumbuzi wake....’akasema.

‘Unasema hivyo ukiwa na maana gani, umeona dalili zozote kama hizo kwa mume wangu, kuwa anatoka nje ya ndoa?’ nikaumuuliza.

‘Nimesema kwa ujumla wake, nielewe hapo… sio kwa mume wako tu...nimesema kuna wanandoa wana matatizo kama hayo, na hawataki kuwa wawazi kwa wenza wao, na matokea yake, hasa wanaume, walio wengi, wanajikuta wakitafuta nyumba ndogo, na wengine wanakuwa walevi kupindukia…, na matokeo yake ni kuzaa nje ya ndoa.....’akasema.
  
‘Kwa, …kwa..hiyo…unasema kusema  nini, ku-ku-kuwa mume hapana sio kweli na sitaki kusikia hilo…?’ nikauliza kwa hamaki

‘Hiyo ndio hali halisi kwa wanaume,…sijasema kwa mume wako…na ni kweli wanaume wanakosea kufanya hivyo, swali tujiulize wenyewe wakikosea ni nani anaumia…usipoziba ufa unakuja kujenge nini…na wanawake mnalijua hilo, lakini mnaweza kukutana mkashauriana mambo ya kuumiza ndoa zenu wenyewe..’akasema

‘Eti nini..ni nani kakuambia hilo…zilipendwa,  kama akili zetu zitajikita kwenye maswala hayo ya ndoa, ya mahusiano ndani ya familia,…aah,… mambo ya kindoa, mapenzi ya ndani..sijui…, hatutaweza kabisa kupiga hatua za kimaendeleo, maana hilo sio tatizo, na lini iliniona nikikaa na wenzangu kuongea mambo hayo, unanifahamu nilivyo…’nikasema

‘Sawa nakuelewa sana huna tabia hiyo ya kukaa ndio,  …ila naelezea hali halisi ilivyo yanatotendeka katika jamii, na sisi na wanajamii, au sio, na sioni kwanini  ujishuku , maana mimi sijakushuku wewe bado, nakuulizia tu, kwa nia njema kabisa…’akasema

‘Najua nyie wanaume, kitu muhimu kwenu ni, .. hilo tendo au sio…, jamani…hilo tendo kwenye ndoa ..ni.. ni kitu kidogo tu, kwanini mnakiona ni kitu cha msingi sana,..cha kusingizia,..kwanza mimi sitaki kabisa kulijadili hilo, kama nyie mnaona hilo ni la msingi kwenu, haya shauri lenu,…na, na nikuambie kitu...kama mtu ana tatizo kwa hilo, kwanini haniiambii...’nikasema.

‘Hakumbii nani, una maana mume wako,…sasa sikiliza nikuambie  hilo sio jambo dogo…unaliona hivyo kwa hisia zako, labda kwa vile muda mwingi upo kwenye shughuli zako, na shughuli zako umezifanya ni muhimu sana, kuliko hiyo ndoa, ndio maana hulitiliii maanani, na matokea yake mnajisahau, na kulisahau hilo jukumu la msingi wa ndoa..na nakuambie kitu, usilipuuzie hilo kabisa, maana madhara yake yanakwenda kuleta matatizo mengine makubwa,....’akasema.

‘Tuyaache hayo,..., hata kama wewe ni dakitari, hatujafika kwako kukuambia tuna matatizo kama hayo…na mimi silioni kama lina maana kuliongelea hapa, maana kila mwanandoa anafahamu umuhimu wake, na wajibu wa kila mmoja kuwa muwazi kwa mwenzake,  hilo eeh  ndilo la msingi…, kama mmoja akiwa kimya, akajitwika matatizo yake mwenyewe, utasema nini hapo?’ nikamwambia.

‘Sawa, endelea naona unataka kunielewa…unataka kusema rafiki yangu hayupo muwazi kwako au sio…?’ nikamuuliza.

‘Sijasema hivyo…ila nimekuuliza swali, je rafiki yako kakulalamikia, je alifika kwako akasema kuwa mimi simtimizii hayo mambo…kama kakulalamikia basi, una haki ya kuniuliza lakini kama hajafanya hivyo, na ni wewe unajenga hisia zako tu, unakosea…’nikasema

‘Hajaniambia, ila nahisi hivyo, kwa vile nakufahamu na yeye namfahamu pia,…na unaweza kuona ni tatizo dogo kumbe kwa mwenzako ni tatizo kubwa…’akasema

‘Hakuna kitu kama hicho, kulikuwa na matatizo madogo na hayo  tulishayaongea na mwenzangu, yanahitajia muda, sio lazima niyaseme kwako. Kama ni hayo, japokuwa zizani kama ni hayo, sizani maana ni kitu kidogo cha ndani ya familia…’nikasema hasira.

‘Kwa jinsi ulivyotahayari... shemeji naona kuna tatizo zaidi ya hilo...na hali kama hiyo nijuavyo mimi kwa wanaume wengine wanaweza kuitumia kama mwanya, au kisingizio cha kwenda nje ya ndoa, naomba unielewe hapo...siwezi kusema rafiki yangu yupo hivyo, maana sijawahi kumuona akiwa na tabia hiyo,, ....’akasema huyo dakitari bila kujali jinsi  gani nilivyomjibu kwa hasira.

Sikusema kitu hapo ,nikampa nafasi aendelee kuongea, kwakweli alijaribu kuongea kwa upole, kama ujuavyo madakitari wanaofahamu kazi yao vyema.

‘Ila kiukweli naweza kuliweka wazi hili kuwa yule rafiki yangu, yule niliyemfahamu enzi hizo, sio huyu wa sasa, nahisi kuna tatizo, tena inaonekana sio tatizo dogo kama wewe unavyolichukulia hivyo…, na nahisi kuna chanzo, na wewe unakifahamu ila hutaki kuniambia...’akasema na kuniangalia machoni , mimi nikamkwepa na kuangalia pembeni.

‘Hakuna tatizo bwana, usikuze mambo, …’nikasema

‘Una uhakika na hilo, unasahau awali ulisema siku ya leo imakuamkia vibaya, matatizo nyumbani, kwa rafiki yako, umesahau au ?  …’akasema

‘Si nimeshakuambia hakuna tatizo, ni ya kawaida tu, sio ya kuambizana kwa kila mtu, na hilo la mwenzangu la kutaka …kuzaa..mmh, kama kakuambia hivyo, kuwa anataka tuzae , tupate mtoto wa kiume, kwani mimi ndio napanga hilo, kuzaa tutazaa, na sio lazima awe wa kiume au,..si ndio hivyo ? alikuambia hivyo au…’nikajikuta nasema hivyo, na kumuuliza…

‘Umeona eeh….hilo ulikuwa unanificha, kwahiyo kumbe, wewe umekuwa mbali na yeye labda kwa vile hujawa tayari kuzaa, na mwenzako , kwa kauli yako, anatamani kupata mtoto wa kiume kwa vile sasa hivi mna mabinti, au sio…?’ akaniuliza

‘Mimi naona tuyaache hayo…unaonaje tukaongelea kuhusu hiyo ripoti ya docta, inasemaje je matatizo hayo ya mume wangu yanaweza kuleta athari gani baadae..?’ nikauliza kukwepesha huo mjadala.

‘Siwezi kuyaacha hayo, maana yanaweza kuwa msingi mnzuri wa wewe na mwenzako hata hiyo ripoti ya dokitari ikija, itakuwa ni ahueni kwako, utajua kipi ufanya na kipi ukikwepe unanielewa hapo..?’ akasema

‘Sijakuelewa, na huenda kama ni hivyo unavyofikiria wewe sitakuelewa au unataka nini hasa labda una lako jambo…?’ nikauliza kwa hamaki

‘Majibu ya vipimo vya mgonjwa ni kitu kingine lakini ninachotaka mimi kwasasa eeh, ni wewe uwe tayari kwa vyovyote itakavyokuwa, kwa ajili ya kumsaidia mwenzako,…tunaweza kuongea haya kama akiba tu,  ili kupunguza mawazo yako ,na usisahau kuwa tumekuwa tukiambizana matatizo yetu na kusaidiana kiushauri, sasa iweje hili, unifiche …’akasema

‘Mhh, hapo nahisi wewe waniuliza ukiwa umeguindua jambo,  na sasa unachotaka wewe ni kunichimba ili tu isionekane wewe unajenga fitina, na labda kunifanya mimi nisije kuumia baadae, au wewe kuna kitu unataka kukichimba ndani ya ndoa yangu yangu kutokana na tetesi za watu tu…, unataka kuhakiki kitu gani maana sio tabia yako ninayoifahamu mimi…’nikasema

‘Kawaida yangu sitaki kubuni, na mimi sio mtu wa kusikiliza tetesi, unanielewa nilivyo, katika urafiki wetu, siku zote nimekuwa nikikuasa kuhus hilo, mimi nataka uhakika kutokana na vipimo, na ndio maana nimekuuliza  maswali muhimu yanayoweza kugusa hoja yangu..na nia ni kusaidia hili tatizo la mumeo..lakini msingi wa yote ni kwanini tatizo hili likatokea,..nahisi sio ajali tu,..nahisi kuna chanzo, nahisi kuna tatizo, kati yenu wawili,....’akasema

‘Kama ni hivyo basii nimeshakujibu au, kuwa hakuna kitu kama hicho, tupo sawa, na maisha yetu ni ya kawaida tu, umeridhika sasa...’nikasema

‘Hdi hapo sijaridikika,..sawa, labda nikuulize hili swali la pili, huko kwa rafiki yako kulikuwa na tatizo gani, maana ulisema wewe mwenyewe kuwa kuna matatizo kwenye familia na huko kwa rafiki yako pi… si ulisema hivyo…?’ akaniuliza

‘Yaaah…lakini sio kwa ukubwa huo…’nikasema

‘Hata kama sio kwa ukubwa huo, nakuuliza tu, je huko nako kulikuwa au kuna matatizo gani..?..., hebu niambie ukweli, maana huenda hayo matatizo yakawa na mahausiano fulani…yawezekana…ikawa hivyo.., wewe ukashindwa kutambua kwa vile yule ni rafiki yako…?’ akaniuliza na hapo nikashituka na kumwangalia machoni, na moyo ukaanza kunienda mbio,....ni kama kuna hisia inataka kujijenga na mimi siikubali.

‘Ni ya kawaida tu…’hatimaye nikasema, baada ya kutulia kidogo

‘Je mume wako wakati anapatwa na ajali alikuwa katokea wapi…?’ akaniuliza

‘Sijui…’ nikasema hivyo, maana kiukweli sijui.

‘Una uhakika hakutokea huko kwa rafiki yako…’akasema

‘Kwa rafiki yangu,..hapana bwana…. hilo nina uhakika nalo, maana mimi mwenyewe nilikuwa huko kwa rafiki yangu..’nikasema sasa nikiwa makini na uhakika.

‘Swali ambalo ninataka tusaidiane, najua nitakuja kumuuliza huyo rafiki yangu na nitafahamu kila kitu, ila kwa upande wako ni mhimu zaidi ukaliweka wazi, nakuuliza nikiwa na maana yangu na wala usinielewe vibaya….’akasema

‘Umeshauliza na umeshapata majibu yake unataka nini tena…’nikasema

‘Yule mtoto wa rafiki yako, …baba yake ni nani…?’ akaniuliza na mimi hapo nikageuka kumuangalia machoni, na yeye akanikazia macho, na ikawa mimi ndiye niliyekwepesha macho yangu, na baada ya muda nikasema;

‘Sijajua bado, hajaniambia…na, kwanini umuulize rafiki yako, au una maana utamuliza rafiki yangu..sijakuelewa hapo,…’nikasema kwa upole.

‘Basi, kama hajakuambia, …basi tuliachie hilo hapo, na kama kuna kitu unanificha ni bora uniambie mapema niweze kukusaidia kimawazo…’akasema

‘Kwanini ukaniuliza mimi hilo swali, kwanini, usingelienda kumuuliza mzazi mwenyewe, maana ni kama vile unahisi mimi nahusika na mimba yake au , eeh,..…unataka kuweka fitina gani ndani ya ndoa yangu…’nikasema

‘Fitina,!!!…hahaha, hapana, mimi au mwingine !!!?’ akauliza kwa mshangao

‘Ndio, umeanza kusema mume wangu alitoka kwa rafiki yangu, kiukweli hajatokea huko, maana mimi nilikuwa huko,…hapo ukashindwa kukamilisha fitina yako,..au dhana yako potofu dhidi ya rafiki yako, na rafiki yangu, halafu ..unafikia kuniuliza mtoto wa rafiki yangu baba yake ni nani….huoni hapo unataka kujenga fitina…’nikasema

‘Na ungelijua, usingelisema hivyo, kwasababu wewe ni rafiki yangu kama alivyo mume wako…na nimekuwa karibu sana na rafiki yangu , mambo yake mengi huwa ananiambia, lakini ikafika muda, ikawa nikimuuliza maswali hataki kunijibu…nikajua kuna tatizo..mimi naweza kuligundua hilo hata kabla hamjaniambia,…lakini nitatoa kauli ya uhakika nikipata uthibitsho, ndio maana nikakuuliza, ili kuondoa hisia mbaya…’akasema

‘Kwahiyo umeshaupata ukweli au sio, sasa ondoa hizi hisia mbaya au kuna jingine…?’ nikamuuliza

‘Bado..sijarizika na majibu yako…, maana hujanijibu kwa uhakika kile nilichokuuliza, unakwepa kujibu swali……’akasema

‘Majibu gani unayo-yataka wewe sasa, mbona siku hizi unaanza udukuzi....sasa sikiliza nikuambie , mimi sitaki,…. na nakuomba tena na tena..huko unapokwenda ni kubaya, sana, mtakuja kukosana na rafiki yako kwa mambo yasiyo kuhusu, kwa ushauri wangu, hilo jambo usiliingilie kabisa, na liishie hapa hapa…’nikasema

‘Hilo jambo lipi sasa…?’ akaniuliza

‘Kuhusu sijui mimi naishije na mume wangu, au, mahusiano yangu na rafiki yangu, au mtoto baba yake ni nani, hayo mambo umeyaanza lini , mbona unabadilika sasa, hayo kiufupi ..hayakuhusu ..kabisa, hayo yaache, na sijawahi kufika kwako kuomba msaada…’nikasema

‘Utakuja tu siku yake..ndio maana nataka kabla haijafikia huko,…nijue wapi pa kuanzia, ila nina uhakika ipo siku utakuja kwangu……si tupo…’akasema

‘Kwanini unasema hivyo, nahisi kuina jambo unalijua hutaki kuniambia…’nikasema

‘Kama mimi ninavyokuhisi wewe, kuwa kuna jambo unalijua, linakusumbua wewe na mume wako, lakini  hutaki kuniambia..sasa tukubaliane, uniambie ukweli, ili na mimi niweze kuhitimisha nadharia yangu, kwa nia njema kabisa,…ili tuweze kuweka akili zetu kwenye kumsaidia mwenzetu, hali aliyokuwa nayo inahitajia msaada wetu sote…sawa, utaanza kuniambia au tuache tu..?’akasema kama kuniuliza

Hapo nikawa sina jinsi, …


NB: Choko choko za docta zitasaidia kuuvumbua ukweli, je docta anauliza hivyo akiwa na msingi gani, je huenda anajua ukweli fulani….mkuki kwa nguruwe, kwa binadamu inakuwaje.....?



WAZO LA LEO: Ndoa nyingi zimekuwa na sintofahamu kwasababu ya kuzarau mambo muhimu kwenye ndoa, na mengine yanaonekana ni madogo au tunayaona hayana maana kwetu… , na mengine ni msingi wa ndoa, lakini wengine wanayaona ni ya kawaida tu ..kama wana ndoa, ni vyema mkayaongelea, maana dogo kwako linaweza likawa kubwa kwa mwenzako, na kama hamtayaongelea wenyewe ni nani atawaongelea, kwanza ongeeni wenyewe, mkishindwa ndio mtafute msaada.
Ni mimi: emu-three

No comments :