Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Saturday, October 28, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-16


‘Shemeji samahani nilikuwa nataka kukuuliza maswali kama hutojali...’ sauti hiyo ilinishitua kutoka kwenye dimbwi la mawazo ya maisha yangu yaliyopita.

‘Unaonekana upo kwenye mawazo mazito, pole sana, najua unavyojisikia lakini usijali mumeo atapona tu….lakini baada ya hili, nawashauri kwa nia njema tu mkae muone tatizo lipo wapi ….’Alikuwa ni docta ambaye alizoea kuniita shemeji.

Docta mara nyingi amekuwa mshauri wangu, hakujali yaliyopita kuwa tuliwahi kuwa wapenzi, hakujali, kuwa huyo mume wangu ndiye aliyefanya akanikosa mimi..ndio hapo unapoweza kumuona docta mtu alivyokuwa mtu wa peke yake.

Nikamwangalia machoni kabla ya kumjibu, na yeye kwanza akatabasamu, pili akaonyesha uso wa kushangaa, na kabla hajasema lolote zaidi nikasema.

‘Naomba usiniulize maswali ya kuzidi kuniumiza kichwa changu, maana leo imekuwa siku ya mikasa kwangu, hapa nilipo nina mawazo emngi sana....’nikasema.

‘Lakini, …mmh, naweza kusema haya yote umejitakia mwenyewe, usimlaumu mtu yoyote, wazazi walikuambia kuchia mimi mwenyewe, ..anyway, ...sitaki kurudi nyuma, lakini wewe mwenyewe unalitambua hilo...’akasema .

‘Ndio hayo siyataki kuyasiki, maana hayatanisaidia kitu,..nafahamu sana unamaanisha nini, lakini nikuambie ukweli, haya yanayotokea hayana msingi kabisa na mambo yetu ya nyuma, na unafahamu kabisa kwanini nilichukua uamuzi huo, na sitajutii kwa hilo...’nikasema.

‘Kulipa fadhila...eeh, haya endelea kulipa fadhila, kiukweli, mimi nimekuvulia kofia, upo tayari kuyaweka maisha yako, rehani…kwa sababu ya kulipa fadhila, na nini unakipata sasa, eeh, mimi nitaendelea kukusaidia tu, hilo nakuahidi …’akasema

‘Najua wewe na wazazi wangu mtasema hivyo sana, ..lakini hamjui ni nini kilicho moyoni mwangu, mume wangu nampenda na nilimpenda toka siku ile ya kwanza, nilipomuoana akiwa na hali yake hiyo hiyo ya umasikini..’nikasema

‘Sio kweli…uwadanganye wengine, lakini sio mimi…’akasema

‘Lakini kwanini unasema hivyo, mimi nimefanya kosa gani, kuwa eti kwa vile nimeolewa, mnayemuita wa daraja la chini au masikini,…hahaha,  hebu niambie sasa hivi ana umasikini gani, mbona mpo sambamba kimaisha, ni hali ya kusaidiana na kuinuana,....’nikasema kama namuuliza.

‘Mimi sijakulaumu kwa uamuzi wako huo, lakini tabia za watu hazijifichi, zingine ni za kihistoria, hata ufanyaje ni kama vile wanavyosema, …mmh,  kuwa kunguru hafugiki,.. na ndivyo maisha yetu yalivyo, misingi ya kizalia ni vigumu sana kuigeuza...unajaribu lakini ipo siku itatokea na tabia itajionyesha na kukuathiri...’akasema.

‘Tatizo lako wewe ni dakitari lakini ukifikia kwenye maswala haya unaacha udakitari wako pembeni, hutaki kuutumia hata katika mambo kama haya, kizalia kina nini na maswala ya mapenzi, ..kuacha kuolewa na wewe  imekua ni nongwa, kwani huyo mkeo uliyempata humpendani...mbona mimi sijaingilia maisha yenu..?’ nikamuuliza.

‘Tuyaache hayo nataka kukuuliza mambo ya msingi, maana pamoja na yaliyotokea nyuma, bado nakuona wewe ni rafiki yangu, na mumeo ni rafiki yangu pia, ndio maana nilipogundua kuwa ndio yeye unayemtaka, sikutaka kupambana kwa vyovyote vile, niliona nikuachie tu, kwa vile ulinitamkia mwenyewe kuwa unampenda,..na ukaja kunitamkia kuwa mimi hunipendi tena…, nikaona kwanini ning’ang’anie mtu asiyekupenda,.....’akasema.

‘Uliza maswali yako bwana, sijasema kamwe sikupendi, nilikuambia sababu za uamuzi wangu, na unazifahamu sana ...’nikasema na yeye akaniangalia kwa muda, halafu akasema;

‘Nataka nikuulize maswali ya ndoa yenu,...’akasema

‘Kama ni maswali kuhusu ndoa yangu, ningelifurahi kama ungeyaacha kama yalivyo, kwani akili yangu haijatulia, siku ya leo imekuwa ni ya mitihani, tangia asubuhi, ni matatizo, ofisi matatizo..nyumbani matatizo, huko kwa rafiki yangu matatizo..’nikasema

‘Kwa rafiki yako kuna matatizo gani…?’ akaniuliza

‘Haya hebu niulize, tuyaache hayo, unataka kuniuliza kuhusu nini?’ nikasema nikijua ni yale yale ambayo mara kwa mara ananilaumu eti kwanini nilimkataa yeye nikaamua kuolewa na huyo rafiki yake.

‘Shemeji ...rafiki yangu…mpendwa…hahaha, wakati mwingine naogopa kuongeza maneni hapo..nikuambie kitu, iIli kuondokana na huko kuchanganyikiwa kwako ni bora ukajaribu kuyaongea hayo matatizo uliyo nayo kwa mtu anayeweza kukusaidia,..’akasema.

‘Hapana, mimi nakufahamu bwana, ...wewe na wazazi wangu siku zote mnaombea ndoa yangu ivunjike, hebu nikuulize, kwa mfano ndoa yangu ikivunjika utapata faida gani, maana wewe sasa una mke, utamuacha mkeo ili uje unioe mimi, au ndio mnataka kunikomoa...?’ nikamuuliza.

‘Hahaha..hivi wewe unafikiri mimi nachukia ndoa yenu, kuwa natamani ivunjike eti kwa vile ulinikataa, acha hiyo, mimi mumeo ni rafiki yangu,...unalifahamu hilo fika, na kama asingelikuwa ni rafiki yangu ningelipambana hadi nihakikishe nimekuoa, lakini niliona hakuna haja, kwanza umepata muda wa kumsaidi rafiki yangu ambaye katokea kwenye shida,....sitaki hata kumuongelea kuhusu maisha yake ya huko nyuma, na kwa kupitia kwako, nimeweza kulipa fadhila zangu pia...’akatulia.

‘Najua hilo mtalirudia kila siku...na hamtafanikiwa, maana sasa mnaishia kumuonea wivu, ana kampuni, ana maisha mazuri,..nini tena cha kumsuta , hakuna, iliyobakia sasa ni majungu, nashukuru kwa ushauri wako wa mara kwa mara sikatai, ila nisingelipenda unilaumu kwa uamuzi wangu huo...’nikasema.

‘Haya bwana, ngoja nikuulize hayo niliyotaka kukuuliza ili uone kuwa mimi najali sana ndoa yenu,...’akasema

‘Uliza, na nitakujibu,....lakini kama ni mambo ndani ya familia yangu,sitaki...’nikasema

‘Hebu niambie ukweli, mume wako alikuwa wapi, kwani watu walioona hiyo ajali wanasema mume wako alikuwa akiendesha gari kwa mwendo wa kasi sana...kama vile alikuwa akikimbizwa,au akikimbia jambo?’akaniuliza na mimi hapo nikashituka, nikikumbuka kuwa hata mimi nilifanya hivyo hivyo.

‘Unataka kusema nini hapo, kuwa mume wangu…ni mhalifu au…?’ nikamuuliza.

‘Nataka kujua kama unafahamu wapi mume wako alikuwepo leo hii, kabla ya hiyo ajali…kuna maswali mengi yanaulizwa, na yataulizwa na polisi pia, …?’ nikamuuliza

‘Kwani hawo watu wanasema alikuwa akitokea wapi...!?’ nikamuuliza huku nikiashiria kushangaa na sijui kwanini niliuliza swali hilo badala ya kujibu swali.

‘Shemeji mimi nakuuliza swali na wewe unaniuliza swali, kwani siku ya leo toka asubuhi, ...mliagana vipi,  na mchana kutwa, hamkuwahi kuwasilina, hamkuonana, au kuambizana mnakwenda wapi, mnafanya nini....nafahamu unafahamu wapi alipokuwa akitokea au hufahamu?’ akaniuliza.

‘Sikiliza nikuambie, mimi na mume wangu tuna mishughuliko tofauti, kila mmoja akiamuka asubuhi anakwenda kwenye shughuli zake kivyake vyake, hakuna kufuatana..hayo ndio maisha yetu na sitaki uniulize kwanini maana hata mimi sijakuulizia kuhusu maisha yako wewe na mkeo, au sio…’nikasema.

‘Sio hivyo, ninachotaka hapa ni kuwasaidia, na wala sio kubomoa, na hata kama wewe ungeliona kwenye nyumba yangu kuna matatizo na kwa vile tunafahamiana, ungeliniuliza, ili uone kama unaweza kunisaidia au sio...’akasema.

‘Sijaomba msaada kwako, mimi na mume wangu tuna utaratibu wetu wa maisha na hatuna shida na hilo,, na haikuwa na umuhimu kuliulizia hilo, ni kama simuamini mume wangu..’nikasema.

‘Lakini mwenyewe kwa kauli yako hapa, umesema siku ya leo imekuwa na mitihani mingi,ukasema matatizo nyumba, matatizo kwa rafiki yako....hii inaashiria nini, kama sio mna matatizo wewe na mume wako, kwanini hutaki kusema ukweli nikaweza kusaidia, hata kiushauri tu...?’ akaniuliza.

‘Hatuna matatizo, na kama yapo ni ya kawaida tu , ya mume na mke..hayakuhusu, na kama yangelikuwa makubwa, ningekuuliza, mbona mara nyingi nakuuliza, au kuna jingine...’nikasema.

‘Sawa, bado hujanijibu swali langu, ....’akasema.

‘Swali lipi zilipendwa....?’ nikamuuliza na kucheka, yeye hakucheka, akasema;

‘Hebu niambie utaratibu wenu wa leo ulikuwaje, ..?’ akaniuliza na mimi nikamwangalia kwa makini, nikaona nisibishane naye sana nikamwambia;

‘Sisi utaratibu wetu ni kuwa, kwa vile kila mmoja ana kampuni yake, na ana mambo yake, tukiamuka kila mmoja ana hamsini zake, hatuaingiliani kabisa, wakati mwingine kama ni lazima ndio tunapeana taarifa, ...’nikasema.

‘Hiyo ni kwa ujumla je kwa leo ilikuwaje, ...?’ akaniuliza, na sikumuelewa ana maana gani, kwani maswali yake niliyaona kama ya polisi nikasema.

‘Ama kwa leo, nakumbuka aliniambia kuwa akitoka kazini anaweza kupitia kumona mke wa rafiki yake ambaye kajifungua, ...nakumbuka aliniambia kitu kama hicho, na sikuwa makini sana kumsikiliza maana nilikuwa na mambo mengine ya kikazi yalikuwa yamenitinga...’nikasema.

‘Mke gani wa rafiki yake, aliyejifungua…?..., alikwenda kumuona mzazi, au mume wa huyo mzazi, maana mimi nijuavyo mara nyingi mke akijifungua wanaokuwa karibu na huyo mzazi ni wanawake, kwahiyo ilitakiwa wewe uende naye....au nimekosea?’ akauliza

‘Kwahiyo unataka kusema nini hapo..?’ nikamuuliza

‘Sitaki kusema kitu, ninachotaka ni ukweli ili niweze kusaidia,...kama ningelikuwa nataka kusema kitu, kwanini nikuzunguke, wakati wewe ni rafiki yangu, na mume ni rafiki yangu pia....’akasema.

‘Nakuuliza hivi kwa maelezo yako una maanisha nini kuhusu rafiki yako?’ nikamuuliza

‘Inawezekana  hakuwa katokea kazini,....maana mimi nilimpitia na nikaambiwa kuwa ametoka mapema tu, kikao chao kilivunjika mapema, kuna mambo yalikuwa hayajakamilika, kwahiyo alitoka mapema ofisini kwake,...’akasema docta.

‘Mimi siwezi kujua  mipangilio yake, na siwezi kutabiri kuwa alikuwa wapi, ...kama hakuwepo kazini, basi alikuwa kwenye shughuli nyingine nje ya kazini kwake, hilo linawezekana na hilo la kusema mzazi ni lazima muandamane na mke wako, halina mantiki yoyote kwangu…, wewe unachotaka hapa ni kujenga sababu ya kumuona mume wangu ana tabia mbaya....’nikamwambia.

`Shemeji lakini nakumbuka tulishaliongelea hili kabla, nilishawahi kuwakanya haya maisha yenu mnayokwenda nayo, ...sio mazuri kwa mke na mume, kiukweli kwa wanafamilia hilo sio jambo jema, hata kama mnaona kuwa huo ni usasa, au wengine wanasema ni uzungu...mimi siupendi. Mimi nawajali sana, kuliko unavyofikiria wewe....’akasema.

‘Nashukuru kama unatujali, na ningelishukuru kama unalosema linatoka moyoni na lina ukweli, kwani hata wazazi wangu wanasema hivyo hivyo, wakati walishatamka kuwa,....nikiendelea na mume wangu watahakikisha maisha ya mume wangu yanakuwa ni mashaka, na huenda akaishia jela...nikakumbuka kauli ya wazazi wangu wakisema;


‘Wazazi ni wajibu wao kumlinda mtoto wao, hata wewe ukifikia mahali pako, utasema hivyo hivyo kwa binti zako, hutapenda aende kuishi na mtu ambaye humuamini..’akasema.

‘Haya unatushauri nini Docta...’nikasema kwa dharau.

‘Mimi nasema hivi maisha hayo mnayoishi yana madhara yake hasa katika maisha yetu haya ya kiafrika,...miundo mbinu ni mibaya, hali za barabarani tunazijua wenyewe, usalama hauna uhakika, kwahiyo ni vyema kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na kila mmoja kumjua mwenzake yupo wapi na anafanya nini, kwani simu zina kazi gani?’ akaniuliza.

‘Unanichekesha kweli, ...yaani umefikia hatua ya kutudharau kiasi hicho...’nikasema

‘Lakini mwenyewe umesema kuwa kila mmoja ana mambo yake, na leo hukujua kabisa kuwa mume wako alikuwa na taratibu gani, za nje ya kiofisi....sasa utajuaje mwenzako yupo wapi, kama likitokea tatizo....’akasema huyo docta na mimi sikuwa nimemuelewa sana, nikamsikiliza tu aendelee kuongea.

‘Endelea doct-aah’ nikasema kwa dharau

‘Mimi siwapingi kwa utaratibu wenu huo wa maisha, lakini ni vyema mkajenga tabia ya kuambizana wapi mmoja anakwenda, sio kila mtu akirudi nyumbani yupo kwenye laptop yake ...kila mtu yupo bize, na kazi zake, mnasahau majukumu yenu ya ndoa...’akasema kama mzazi anayemuelezea mtoto wake aliyekosana na mkewe.

‘Umekuwa kungwi siku hizi au mwanandoa mzoefu, ...nyie mnajipa moyo kuwa ndoa yenu ipo safi eehe,  haina matatizo au sio, unaiona ndoa yangu ndiyo yenye matatizo au sio....?’ nikamuuliza.

‘Mimi siwezi kujigamba kuwa ndoa yangu haina matatizo, yapo na kila ndoa ina matatizo yake, lakini yakizidi ni lazima tuambizane, ni mimi nawaasa, kama wewe ungeliniasha mimi ukiona utaratibu fulani sio mnzuri kwenye ndoa, hasa huo mnakwenda nao.’akasema na mimi nikahisi kukerwa na hayo maneno yake, niliona kama ananiingilia maisha yangu ya ndoa, japokuwa sikutaka kumkatiza, nikatulia tu.

‘Mimi kiukweli sifurahishwi na tabia hiyo, halafu rafiki yangu huyu, siku hizi anaonekana kunywa sana pombe, bila mpangilio, naufahamu unywaji wake, huu wa sasa ni ulevi, sio unywaji...’akasema na mimi hapo nikaa kimia tu.

‘Mimi nionavyo, ana tatizo,  ana msongo wa mawazo, ...mimi kwasababu ya safari zangu za hapa na pale, sijaweza kukaa naye tukaliongelea hili kwa kina, ila kila muda nilipopata nafasi kidogo ya kuwa naye, nimemuona sio yule rafiki yule ninayemfahamu..hana raha, anaonekana anakerwa na jambo fulani..nahisi kuna tatizo ndani ya ndoa yenu..’akasema.

‘Wewe unahisi kuna tatizo kwenye ndoa yetu....kwani hiyo kuhisi imeanza leo?’ nikawa kama namuuliza

‘Ndio maana nataka tusaidiane kwa hilo,...kama kuna tatizo lolote niambie shemeji, hiyo dalili aliyo nayo rafiki yangu inatokana na msongo wa mawazo, shemeji jaribuni kukaa na kuliongelea hili nahisi kuna tatizo..ongeeni ambizaneni, ili muwewe kuishi kama wana ndoa, na sio wabia...’akaniambia huyo dakitari nikacheka kwa dharau aliposema `wabia...’

‘Eti eti unasema nini, ndio umefikia huko kuwa tunaishi kama wabia...dharau ya ajabu kabisa...’nikasema na kutulia

Nilitulia kwa muda bila kusema neno..hayo maneno ya mwisho yalinichefua,, hasira zikanikaba, maana sikuona tatizo lipo wapi, na sikupenda mtu aniingilie maisha yangu, hasa huyu, ambye alikuwa ni mpinzani mkubwa, kwa vile alitaka anioe yeye.

 Mara akaja docta kutokea maabara, akapita na kuelekea kwa docta anayemuhudumia mume wangu, hakusema kitu.

‘Rafiki zilipendwa mimi sijui kama kuna tatizo kubwa kihivyo, kama yapo ni mambo ya kawaida ya mume na mke. …’nikasema

‘Una uhakika kweli na hilo unalolisema…?’ akaniuliza

‘Nikuambie kitu, yule ni rafiki yako, kama umeona kuna tatizo nenda ukamuulize yeye mwenyewe, umesikia sana...’nikasema huku nikionyesha kukerwa.

‘Shemeji ni sawa...sio kwamba nataka kuingilia maswala yenu ya ndani, hapana, ...na nafahamu kila tukiliongelea hili wewe unayaunganisha maswala haya na mambo yaliyopita, mimi nakuhakikishia kabisa sipo huko, nipo kwenye kuijali ndoa yenu,...’akasema.

‘Sawa, nimekuelewa…’nikasema, na aliona sitaki kuliongelea hilo, tukaa kimia kidogo baadae akasema;

‘Shemeji samahani nikuulize swali muhimu sana, nililokuwa nataka kukuulizia...usinielewe vibaya, na wala usilipeleke kwenye urafiki wetu wa zamani, ninachotaka kufanya hapa ni kujaribu kuangalia kama kuna tatizo maana nyie mnaweza msilione, lakini mimi kama docta ninaweza kuliona hata kama hujanielezea kwangu, nakuomba nikuulize maswali ya ndani ya ndoa yako, kama hutojali, ...’akasema.

‘Wewe uliza tu, sioni ajabu na maswali yako,..nitakujibu kama ninavyojua, ..lakini mimi siwezi kumjibia rafiki yako, yeye huenda anaweza akawa matatizo yake binafsi, lakini kama hajaniambai siwezi kuyajua,..kweli mimi ni mke wake, lakini kama mmoja atakuwa sio mkweli kwa mwenzake, basi hilo ni tatizo lake, na huwezi kukimbilia kumlaumu mke au mume, bila kujua undani  wa maisha yao....’nikasema.

‘Shemeji sasa mimi nataka nijue undani wa maisha yenu,..niamini mimi, nina nia njema kwenu, kama mlivyoniamini siku ya ndoa yenu, kama rafiki mkubwa wa mume wako, kama rafiki yako mpenzi wa zamani, nataka niingie ndani ya ndoa yenu, nijaribu kuangalia undani wa ndoa yenu, kama kuna tatizo....tusaidiane’akasema.

‘Haya ....Unakaribishwa....ingia maana nimeshachoka kukuambia kuwa hakuna tatizo...sijui nikueleze vipi,..haya uliza hayo maswali ya ndani ya ndoa...’nikasema

‘Shemeji, je katika mambo ya unyumba mnashirkiana kama kawaida?’ akaniuliza swali lililonifanya nishituke na kugeuka kumwangalia usoni…huku uso umeonyesha kutahayari…

Na kabla sijamjibu, akaniuliza swali jingine,…

‘Na huko kwa rafiki yako kuna tatizo gani, je tatizo la huko kwa rafiki yako haliwezi likawa linaingiliana na matatizo mlio nayo nyie wawili,…?’ akaniuliza na mimi hapo nikabakia kimia, nikiendelea kumuangalia kwa uso uliotahayari….

‘Ukinijibu kwa uhakika…tunaweza kulitatua hili tatizo lenu, nina uhakika kuna tatizo, na...usipoangalia, utakuja kuniambia, je upo tayari kunijibu hayo maswali, tukasaidiana au..utaendelea kunificha,...?' akaniuliza

Nikainua uso na kumuangalia, ...na kabla sijamjibu, docta yule anayemuhudumia mume wangu akatokea....

NB: haya, mambo ndio hayo

WAZO LA LEO: Wakati mwingine unaweza ukawa na matatizo, lakini usijue kuwa una matatizo, wakati mwingine ndoa zinaweza zikawa na matatizo, lakini wanandoa wakajifanya hawana matatizo,…kila mtu akimtegea mwenzake, na kuona mwenzake ndiye anayestahiki kusema, au kulalamika…tukumbuke ndoa ni ya watu wawili, na wote wana dhima sawa ya kuona ndoa yao inasimama imara, tusijenge tabia ya kutegeana, kwani kukiharibika jambo, athari zitakuwa kwa wote, na familia yenu.


Ni mimi: emu-three

No comments :