Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, October 27, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-15



 Kumbukumbu za nyuma ziliuteka ubongo wangu,…nikakumbuka yaliyotokea huko nyuma, yaliyompata huyu msamaria mwema, tena kwa ajili yangu, akafikia hadi kufungwa na wazazi wangu, …nikaapa kuwa siku nikikutana naye, nitajitahidi nifanye lolote kumlipa fadhila zake, sasa nitamlipa nini, …na nilishamsahau, nikujua hayupo tena duniani…na siku hiyo, ndio nikakutana naye, nikiwa na docta mtoto wa watu akiwa ni mpenzi wangu…je nilifanya nini, angalia mitihani hii ya maisha…

***********

 Nakurejesha nyuma kipindi nikiwa binti mdogo, wa miaka kumi na tano,…kipindi hicho ndio nilimuona kijana mmoja mara kwa mara akiwa anakuja kuonana na mzee mmoja aliyekuwa mlinzi wa nyumba yetu. Yeye kiumri alikuwa mkubwa kuliko mimi…nikaanza kuzoeana naye tu..
Kuna kipindi baba yake alikuwa akitulimia shamba, basi na yeye anakwenda kumsaidia baba yake mimi, nikawa nafika shamabi kuchukua matunda, nawakuta wakiwa wawili, nawapatia chochote, mwanzoni  sikuwa naongea naye sana, kutokana na hali ilivyokuwa wakati huo. Wazazi walikuwa wakali hawakupenda kabisa nizoeane naye, au kuwa karibu naye,…

Kila huyo mvulana akija, nilimgundua akiniangalia sana, na ikitokea tukikutanisha macho anayakwepesha kwa haraka na kujifanya kama alikuwa haniangalii, ikawa kama mchezo fulani wa utu-rika,.. na tukajikuta tunamezoeana kinamna hiyo, lakini sio ile ya ukaribu ya kukaa pamoja na kuongea.

 Ni ikaja muda hata mimi nikikaa nyumbani, namuwaza yeye, fikiria ni mtoto wa mkulima, mfanyakazi wetu tunaweza kusema wa ndani…lakini mimi sikulijali hilo, nilimuona sawa na wavulana wengine. Sio kwamba nilikuwa na tabia mbaya, ya kuwa na mazoea na wavulana, hapana..ila nilijali sana usawa na utu, hata nikiwa msichna mdogo.

Basi kwa ile hali ya kunyanyapaliwa na wazee, kuwa wakifika wanakuwa na sehemu yao, hawaruhusiwi kuingia ndani, sikulipenda hilo kabisa, nikaona lazima nifanye jambo, la kuwasaidia hawa watu wawili…nilimjali sana huyo baba yake, alikwua na tabia nzuri tu,…huruma na upendo,.

Basi…huyo kijana akifika, ninajua wapi nikae ili aweze kupita na kuniona, kwa haraka nikakuwa na zawadi yoyote ya kumpa, chakula au matunda,…maji ya baridi ili wakinda sahamba wapate kuyatumia yeye na baba yake..na nilijithidi sana wazee wangu wasiweze kuona hayo…

Lakini ikatokea tukio, liloharibu kila kitu, na baada ya tukio hilo, tukaachana na familia hiyo sisi baadaye tukahama na kuja kuishi Dar, ambapo baba yangu alihamishia kampuni yake, na huko kijijini tukawa hatufiki mara moja moja tu. Na sikuweza kuwaona tena. Tukio hilo kwakweli liliniumiza sana kiasi kwamba niliwaona wazazi wangu kama ni watu wasio na utu-wema.

*************


‘Kwanini  hukunitafuta, ulipoachiwa kutoka jela...?’ nikamuuliza, nikikatiza mawazo yangu ya kumbukumbu za huko kijijini….

‘Kwanini nikutafute..ulitaka niendelee kuumia, maana mimi ningelisemaje kwako, ..hebu nijishushe hapo, baada ya tukio lile, ningelionekana na wewe tena,  si ndio ningepeleka tena jela nikafie huko.., nakumbuka niliwahi kuandika barua kuja kwako, lakini sikuwahi kupata majibu...’akasema.

‘Barua,…. hahaha..nani ana mipango ya barua siku hizi, ulindika hiyo barua kuja kwangu ukampa nani..mbona sijawahi kuona barua yako yoyote,...?’nikamuuliza,  niliona kama ananitania tu.

‘Basi nahisi kuna mtu alikuwa akizipokea na kuzichana, mimi niliandika, nyie si mna box la barua, na kuna mtu alisema anakuja huko kwenu , nikampa barua, lakini nikajua umeshatekwa na familia yako, na huenda hata wewe hutaki hata kuniona tena, kwa jinsi watu walivonivumishia ubaya....’akasema akitikisa kichwa kusikitika .

‘Kwanini usingelinipigia, angalau  hata simu...?’ nikamuuliza

‘Nikupigie simu!!! Hahaha…, simu hiyo ningeliipata wapi, huko kijijini, hivi unayafahamu maisha yetu yalivyokuwa...anyway, hayo yameshapita na wewe una mume wako, ...naona nisikupotezee muda, ...’akasema na kutaka kuondoka, mimi nikamshika mkono asiondoke.

‘Nimeshakuambia yule sio mume wangu, ni mchumba wangu, hatujaoana bado…Sikiliza, ..ahadi yangu ipo pale pale…’nikasema na hapo akaniangalia kwa macho yenye kushangaa.

‘Kwahiyo unataka kusema nini…?’ akaniuliza

‘Ahadi yangu ya kufanya lolote ilimradi niwe nimelipa fadhila zako, najua inaweza isikidh haja, lakini angalau na mimi niwe nimfanya jambo kwako la utu wema..sasa mimi nataka tuje tuongee tena nione nitakufanyia nini…’nikasema, na nikaona kama ananywea, hakuridhika na maneno yangu hayo.

‘Hapana, mimi sihitajii msaada wako, sitaki kuwa mfanyakazi wenu, au ….kuwategemea nyie tena, hapana…hilo sitaki, …’akasema

‘Najua ni kwanini unasema hivyo, ila mimi natamani zile siku zirejee tena, kiukweli mimi sijaolewa, na sisemi hivyo kwasababu kuwa nataka uwe ...mpenzi wangu, hapana mapenzi hayalazimishwi, na…mimi na mchumba wangu hatujafikia huko, bado kuna mipango mimi, yeye na mimi pia, lakini mimi ninaweza kufany ajambo la kukusaidia ukafika mahali, usilipuuzie hilo..’nikasema

‘Hilo la kukutana kuongea tena, ni wewe, kama huogopi huyo mpenzi wako, sitaki kuja kuwaharibia mahusiano yenu, ikawa ndio sababu ya kufichua yale yaliyopita, sipendi hilo kabisa,…’akasema

‘Kiukweli unanidai sana, mengi umenifanyia, lakini sijaweza kulipa chochote kwako, kwangu mimi naona ni deni, na nataka uwasamehe wazazi wangu, hata bila ya wao kufahamu, na hilo naweza kufanya nionavyo mimi, niamini tu,…usijali kabisa kuhusu hisia za wazazi wangu, nafahamu ni kwanini wanafanya hivyo,....’nikasema

‘Hahaha, hapana , niliapa kuwa sitaajiriwa kwa watu kama mfanyakazi wa upendeleo, mimi nataka nihangaike kivyangu…sawa nashukuru kwa kuonana nawewe, mengine  tuyaache kama yalivyo, vipi maisha na mchumba wako, katulia siku hizi..?’ akaniuliza

‘Mchumba wangu hana matatizo, ni mzungu kwakweli, muhimu nimuambie ukweli tu, hata akiniona tunaongea, yeye atadai nimuambie wewe ni nani, na ni hivyo, sina shaka naye, ila hayo hayana msingi, wewe sifikiria wako langu la kukuwezesha, unalionaje hilo…’nikasema

‘Mhh…sivyo nitakavyo, najua hutanielewa, ndio maana nasema tuyaache tu, yabakie kama yalivyo, kwa maana mimi nilikufanyia nini kikubwa, ni kawaida tu, na yaliyotokea hadi wazazi wako kufanya hivyo, ni…naweza kusema hata mzazi mwingine huenda angelifanya hivyo…’akasema

‘Hapana lile tukio lilikuwa kubwa, na kiukweli nakiri wazazi wangu walikosea, sana,..maana hawajui ulivyofanya, uliweza kuniokoa mikononi mwa wabakaji, mijitu mikubwa, na wewe ulikuwa sio umbile lako kabisa, ukapigana na wao kufa na kupona, hawakuliona hilo.

Kiukweli mimi..sitalisahau hilo kamwe, nilikuona kama mtu maalumu sana kwenye maisha yangu ndio maa niliahidi siku nikikutana nawe, nitafanya lolote lililondani ya uwezo wangu, ili na wewe uone kuwa nakujali…...’ nikamwambia.

‘Mhh…nilishaipata hiyo zawadi inatosha., wewe wasalimie wazazi wako na mchumba wako, mungu akipenda tutakuwa tunaonana, lakini nisingelipenda wafahamu kuwa tumekutana nafahamu watakavyojisikia, huenda ikaja dhahama kubwa zaidi ya ile…japokuwa sasa nimekuwa mkubwa siogopi, nafahamu haki zangu...’akasema

‘Jamani ina maana hujatusamehe tu…’nikasema

‘Usijali sana ndio ubinadamu ulivyo,..nilishawasamehe mbona…kwa hivi sasa nimeliona hilo, kuwa yale waliyoyafanya wazazi wako walikuwa na maana kwao, kwa ajili ya kulinda heshima ya familia yenu, na walitaka kutoa fundisho kwa jamii, na nasikia familia yenu imekuwa ikiogopewa sana,..ni sahihi, yamepita yapite.

‘Tatizo wewe hufahamu jinsi gani niliumia...lakini ikafika mahali nikasema basi tena, mungu ndiye atakupeni yale yote mliyotutendea wewe na baba yako, na nikatubu sana kwa niaba ya wazazi wangu…kiukweli baba yako nilimuona kama baba yangu mkubwa...sikupenda kumuita babu, kama walivyozoea kumuita wengine, mimi ninajua kuzeeka kwake haraka ni kutokana na hali ya maisha, umri wake haupo mbali na umri wa baba yangu, …mimi nilipenda kumuita baba mkubwa.....’nikasema.

‘Nashukuru kusikia hivyo, ni wewe tu ulikuwa tofauti na wengine, sijui kwanini wazazi wako, walikuja kutuchukia hivyo..niliona kabisa hawakupenda, hata nikukaribie..na nahisi  ilipotokea lile tukio, ndio wakaonyesha hisia zao dhidi yangu. Ni sawa, labda nisiwalaumu sana, maana huenda hata sisi tungelikuwa kwenye hiyo hali tungelifany ahivyo hivyo..hata hivyo nawashukuru wazazi wako, kwani pamoja na hilo tukio lakini walitusaidia sana kimaisha...’akasema.

‘Mimi nilikutafuta sana, lakini sikutaka wazazi wangu walifahamu hilo, nilitaka kukulipa fadhila zako, niliahidi moyoni kuwa nikija kuonana na nawewe, nitafanya  lolote na nimekkuona naomba usilipinge ombi langu....’nikamwambia.

‘Mimi sihitaji msaada wenu, ….’akasema

‘Hapana ni lazima nifanye wema wowote, nakumbuka kama isngelikuwa ni wewe..sijui ingelikuwaje, na….’hapo tena ndio lile tukio likazama kwenye ubongo wangu nikawa naliona lilivyotokea….

**********

Ilionekana wazo hao vijana watukutu, walikuwa wakinivizia siku nyingi, na siku hiyo gari la baba lilichelewa kuja kunichukua shuleni, nikaamua kutembea na wenzangu, na kwa vile shule ilikuwa mbali, wenzangu wakawa wametawanyika kila mmoja na njia yake, ikafikia mahali nimebakia peke yangu, na ghafla ndio nikavamiwa na vijana wanne, na kunibeba juu kwa juu.

Walinibeba juu kwa juu, hadi vichakani, na wakaanza kunivua nguo, na ukumbuke nilikuwa binti mdogo tu, nasoma sekondari..nilikuwa binti, nimeshavunja ungo, lakini sikuwa na mawazo hayo kabisa, na sikujua ni kitu gani kitakuja kunitokea,..japokuwa nilifahamu kuwa wanatka kunifanya kitu kibaya.

Nilijitahidi kupigana lakini sikuweza kufurukuta kwa vijana hawa wenye nguvu zaidi yangu, na kabla hawajafanya lolote mara akatokea mtu, kijana..machozi yalishatanda usoni sikumuone vyema, akawa anapigana nao, akiwa na kigongo hivi kama rungu, alipambana nao kiume mpaka anakuja kuwazidi nguvu, ilikuwa ni kwa msaada wa mungu tu maana wote walikuwa wakibwa zaidi yake…ikafikia muda, ikabidi wakimbie, baada ya kusikia kelele za watu, wakikaribia eneo hilo..na yule kijana akapiga ukelele kuomba msaada. Wale vijana wakakimbia huku wakilaani kuwa watahakikisha wananifanyia hivyo, siku yake...

Sikuweza kuongea nililia hadi nyumbani, nikiwa nimechafuka, nguo zimechanwa, nnipo kama nudu uchi…na huyo kijana alinsiindikiza hadi nyumbani, nikawahadithia wazazi wangu, na wao kwa haraka wakaifahamisha polisi na hawo vijana wakaanza kutafutwa lakini hawakupatikana kwa siku hiyo hata ya pili yake. Walihama kabisa, kijini hapo.

Cha ajabu wazazi wakaongea na polisi wakaja kumshikilia huyo kijana kuwa atakuwa anawafahamu hawo watu, na alitakiwa kuwataja, na aliposhindwa kuwataja, wakamshitakia kuwa ni muhusika wa tukio hilo, ..wanasema walivyomuhoji, alivyojieleza inaonekana kama analifahamu hilo tukio na yeye alikuwa mwenza wao, japokuwa alikana kabisa.

Baadae akafunguliwa mashitaka, na yote hayo wakati yanaendelea mimi nilikuwa sifahamu kinachoendelea kwani ilibidi niondoke hapo kijijini kwa usalama wangu, kwa vile walitishia kuwa ni lazima watanifanyia tena..ikabidi baadae wazazi wangu wanihamishe kabisa kwenda kusomea sehemu nyingine.

 Nilikuja kusikia kuwa kijana huyo kafungwa, na nilikuja kufahamu hilo baada ya muda, mtu alishahukumiwa kufungwa..kwani vijana wale waliofanya hivyo hawakuweza kupatika,ila mmoja wao alipatikana na alipofika mahakamani, akadai kuwa kijana huo alikuwa mmoja wa wenzao, walipanga wote, kulifanikisha hilo, nay eye ndiye alitoa maelekezo jinsi gani wanaweza kumpata huyo bint.

Baba wa huyo kijana akawa anafika mara kwa mara kwa wazazi wangu kuomba kijana wake asamehewe, lakini haikusaidia kitu, na alichoambulia ni kufukuzwa kazi...hayo yote nilikuja kuyafahamu baadaye, na nilipolifahamu hilo nikawaambia wazazi wangu kama hawatamuachia huyo kijana aliyeniokoa basi mimi nitajiua...

Hilo nilidhamiria kweli…

Wazazi wangu awali walifikiri natania, wakaja kunifuma nataka kunywa sumu, na walipoona hivyo,  ndio baadaye wakaenda kuongea na polisi na baadae mahakama, kuwa kijana huyo aachiwe, wao wameshamsamehe..ili ifanyike maongezi, wanayojua wao wenyewe na ndio kijana huyo akaachiwa, hata alipoachiwa sikuweza kuonana naye tena wala baba yake, kumbe waliamua kuhama kabisa hapo kijijini, na baadae hata wazazi wangu wakahamia Dar, ndio ikawa mwisho wa kuonana na huyo jamaa hadi hii leo ndio nakutana naye…

***********.

‘Kwakweli sitaweza kusahau wema wako huo, uliniokoa kwenye janga, huenda ningelikufa, …’nilimuambia siku tulipokutana naye tena.

‘Ile ni kawaida tu, mtu yoyote muadilifu angelifanya hivyo hivyo, na haina haja, kulipwa kwa kitendo kama kile, na sizani kama kuna kitu unaweza kunilipa kikazidi yale ya moyoni kwangu...’akasema na kuinama chini.

‘Una maana gani,ya moyoni mwako, yapi hayo..… ?’ nikamuuliza.

‘Mimi niliahidi siku ile ulipoleta chai na mkate, nilikuambia mimi nitakuja kukuoa, wewe uliona kama utani, nilimuambia hata baba, alinicheka sana,..nakumbuka hata wewe ukasema mungu akipenda,..ukimaanisha kuwa umekubali au sio…’akasema

‘Lakini yale yalikuwa ya ujanani, na niliongea vile kama maongezi tu, ulitaka mimi niseme nini pale, na ni mambo ya ujanani, hayana maana au sio…’nikasema

‘Hayana maana, ndio unasema hivyo, kwangu yalikuwa na maana sana, mimi nilikupenda na …samahani, nikisema hivyo, kuwa siku zote nimekuwa nikikupenda, na kutamani uwe mke wangu, usichukie, ila naelezea hisia zangu, najua ni ndoto za Alinacha, lakini ndio ukweli kutoka moyoni mwangu…’akasema

‘Aaah, hapana,…sawa nashukuru kwa kusikia hivyo, na…hata sijui niseme nini, naogopa, nitakuja kuuumiza , naomba unipe muda..’nikasema

‘Hapana nafahamu, huna haja ya kusema lolote, haiwezekani, mtu kama mimi kukuoa wewe, najua, ila sijui …’akasema

‘Kwanini unasema hivyo…utampata msichana mwingine kwani mimi ni msichana peke yake hapa duniani..’nikasema

‘Sijaona kama wewe, na wewe ndiye uliyeuteka moyo wangu, kama sio wewe basi, mimi naomba mungu nisioe tena, na nitaishi hivi hivi maisha yangu yote…sitaki shida…’akasema sasa akisimama kuondoka. Hapo nilibakia nikiwaza, sikujua kabisa mwenzangu kadhamiria hilo, na..kiukweli moyoni sikupenda kuja kumuudhi mtu kama huyu, ambaye naona kama ananidai …

 Moyo wa huruma uliniingia, nikikumbuka yeye ndiye aliniokoa, vinginevyo sijui ingelikuwaje, na zaidi ya hayo, ananijali sana, kiukweli docta nampenda, na kwa vile pia yupo kwenye hadhi inayoendana na …tusema hivyo..lakini huyo nimetokea kumjali, na labda kuna upendo lakini sio kwa vile…sasa nifanyeje..ilinipa wakati mgumu sana, nikijua kuna wazazi wangu, ambao hawatalisikiliza hilo kabisa

Basi siku hiyo akaondoka, na hatukuweza kukutana kwani nikifika naambiwa katoka, nikimpigia simu hapokei.

************

 Baada kama ya mwezi hivi tukaja kukutana tena, tukaongea mengine , hakupenda kuliongelea hilo tena, nikajua keshakubali ukweli, kwahiyo hilo halipo tena, na huku kwa docta, naye kaanza kunisakama, anataka tuanze michakato ya ndoa..

‘Niambia, lile wazo langu vipi…?’ siku moja akaniuliza sikutarajia hilo swali.

‘Unajua, wewe unachukulia ndoa kama ni kitu rahisi hivyo, ujue mimi nina wazazi, na ndoa inakutanisha familia mbili, wakiwemo wazazi, sasa hebu jiulize, wazazi wangu wataliridhai hili,...je wewe umejiandaaje kuishi na mke, maana usije ukasema unanioa, kwa vile…’nikasema

‘Mimi nimeshajiandaa kwa hilo, sio kwamba nakuambia kwa vile…ninachumba na varanda nimepanga, nina kiwanja kijijini, urithi wa baba, nitauza seehmu nitajenga nyumba,…tutaweza kuishi tu..lakini sikulazimishi, maana kiukweli hutaweza kuishi maisha y akitajiri kihivyo...’ akasema.

Baada ya maongezi hayo, nikawaza sana, nikajiuliza sana, nifanye nini…maana sikuwa nimelichukulia kwa maana hiyo tokea awali,…nikaanza kujenga hisia za kumpenda tu…na huku kwa docta nikawa naharibu, ikawa siivani naye kwa kila anachokifanya.


‘Vipi kwani kumetokea nini, nakuona umebadilika sana siku hizi, kama kuna tatizo lolote niambie mimi nitakuelewa tu mpenzi, sitaki kabisa, kukulazimisha kwa lolote lile, umenielewa, sitaki nikuoe ukiwa hunitaki, unasikia, unieleze mapema…?’ akaniambia

‘Hakuna  tatizo lolote!....’nikawa namwambia hivyo maana bado nilikuwa sijaamua moja kwa moja, nikijua kuwa wazazi wangu hawataweza kunikubalia kumuoa huyo

Nikawa sasa najenga ukaribu sana na huyo jamaa hadi docta akaja kugundua mwenyewe, na aliponiuliza nikamwambia ni rafiki yangu nakutana naye tu na hawezi kunizuia

‘Nimeshakuambia uwe muwazi kwangu, kama hupo na mimi , sawa, mapenzi hayalazimishwi, lakini nataka uwe muwazi, unanielewa, sitaki kupoteza muda wangu na mtu asiye na matarajia na mimi..’akasema

‘Sawa si unataka jibu, sipo na wewe,… nataka kufikiria zaidi, kama una haraka kuoa katafute mwingine....’nikamwambia hivyo, kiukweli ilimuumiza sana, na akavumilia kwa kipindi fulani, baadae akalifikisha kwa wazazi kuona kama wataweza kusaidia

Wazazi wangu waliposikia hivyo, hawakuamini…wakaamua kufanya uchunguzi ni nani kanighilibu, na baadae wakaja kugundua kuwa ni nani huyo ninayekutana naye mara kwa mara, na kipindi hicho nimeshamsaidia huyo jamaa hadi akapata kazi kwenye kampuni kubwa, na akaweza hata kujenga nyumba yake mwenyewe…nilitaka nifanye hivyo baadae…kama atampata mtu mwingine basi.

Lakini kumbe mwenzangu anajua kuwa nayafanya hayo kwa ajili ya maisha yetu ya baadae, kukapita kipindi kirefu hapo,…sio jambo la miezi, hapana ilichukua karibu miaka miwili hadi docta akakata tamaa na mimi....
.
Siku moja wazazi wangu wakanikalisha kikao,  walikuwa wamekasirika kweli kweli..

‘Hivi wewe una akili kweli,..hivi wewe hujaona mwanaume, hadi umchague huyo mtu,..kama kweli nia yako ni kupata mwanaume mwingine zaidi ya docta, huyo hakufai, yule ni mlalahoi, mtoto wa mlinzi wetu...bwana shamba, asiye fanana kabisa na hadhi yako, mbona unataka kutuaibisha....kwanini unamkataa docta, msomi , familia yao ni ya kiheshima, matajiri.....’akasema baba.

‘Baba mimi sio mtoto mdogo, na sina lengo la kuwaabisha, mnakumbuka nilitaka kubakwa nikiwa kule kijijini, niliwaambia ni nani aliyeniokoa, ....mlifanya nini kwa huyo aliyeniokoa, ..badala yake mlikimbilia kumshika yeye ati alikuwa anawafahamu hawo watu waliotaka kunibaka, mkamfunga hata bila ya mimi kujua, kwa vile tu ni mtoto wa masikini..iliniuma sana na niliahidi kuwa ipo siku nikipata nafasi nitamsadia ili kulipa fadhila zangu kwake, na kutubu madhambi mliyoyafanya...’nikasema.

‘Kwahiyo malipo yake ndio hayo, kutudhalilisha sisi au sio...sikiliza, kama sisi ni wazazi wako, tunasema achana na huyo mtu, sisi ni wazazi wako tulijua ni nini tulichokifanya, wewe hukuona kilichotokea, baada ya kumshika yeye na kumfunga, kijiji pale tuliogopewa sana…, hakuna hata mtu aliyewahi kuichezea familia yetu tena....sisi tulifahamu ni nini tulichokifanya, kutoa fundisho kwa wengine....’akasema baba

‘Mtoe fundisho kwa mtu asiye na hatia,...kunikoa kwake ndio imekuwa taabu, kama asingelifanya hivyo nikabakwa, huenda ningelifikia kupoteza maisha au kuambukizwa magonjwa, mngelisemaje, ndio fadhila zeni hizo,  wema wao ndio malipo yake hayo,hapana mlifanyavibaya sana…’ nikasema

‘Je na sisi tusingelifanya hilo, ikatokea tena, maana walidhamiria kweli kulifanya tena kukukomesha , na wale waliotoroka, walikamatwa wakiwa na mipango hiyo …walitaka hata kuja kuchoma nyumba na maeneo yetu..hujui kabisa yaliyokuwa yamepangwa …’akasema

‘Wazazi wangu hamuwezi kujua ubaya huo unaweza ukawageukia nyie wenyewe siku moja, …au ubaya huo uje utendwe kwa watoto wenu, ili iwe fundisho, ...hamjui kibao kinaweza kuwageukia  nyie siku moja kwa tatizo jingine, hujafa hujaumbika...msijione kuwa nyie ni matajiri hamtaweza kupata shida, mung anaweza kuibadili hali bila kujua, kisa ni haya mnayoyaona ni madogo tu...’nikasema kwa sauti ya huzuni na mama akanionea huruma na kuniuliza

‘Kwahiyo ewe ulikuwa unatakaje, tukae kimiya tu, wakati wahuni walishaanza kuiingilia familia yetu, tulifanya vile kwa ajili ya kuilinda famila yetu, na tulipofanya hivyo ilisaidia. Na baadaye tulimtoa, na tukampa pesa za pole,...japokuwa mzazi wake alizikataa lakini baadaye akazichukua hali ilipozidi kuwa mbaya....ile ni kawaida kwa mzazi yoyote anayetaka kulinda familia yake...’akasema mama.

‘Mimi sitawaelewa kamwe, na mimi najua nafanya nini, itafikia mahali, nikiona kampata mtu wake, basi..lakini kwa hivi sasa sitaki kuolewa na docta…’nikasema,

‘Sasa unataka nini, maana huyo kijana keshasema anataka kukuoa,..lakini sisi kamwe hatutakubaliana na ndoa hiyo,…’wakasema

‘Baba mimi naona hatutafika popote kwa hili, ila nawaomba, ..kwa vile mimi ndiye niliyefanyiwa hilo, na namfahamu ni nani aliyenifanyia wema kwa kuniokoa, mniache tu, najua ni nini ninachokifanya, maana kwangu, alilonifanyia ni deni kubwa sana,..na.niliahidi kuwa nitamlipa fadhila zake, ....’nikasema.

‘Kwahiyo unataka kumlipa fadhila gani...?’ akauliza mama.

‘Hilo niachieni mwenyewe....sijaja kuwaomba chochote kwenu kwa ajili yake....’nikasema.

‘Achana na huyo mtu, kama unataka kumuona akiendelea na maisha yake, achana naye, na kama unataka akaishie jela, endelea naye....hatuwezi kukuona ukituzalilisha ....atapotea kama alivyopotea baba yake....’akasema baba.

‘Ina maana mnafahamu kuwa baba yake alifariki,,...?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Tumeshakuambia achana na hiyo familia, vinginevyo utajua kwanini hukutusikiliza....’akasema baba, na mimi moyoni nikasema

‘Kama ni hivyo basi, nitakubali anioe, ili kuondoa kabisa hiyo dhana ya madaraja..najua wazazi wangu wamekosea, na hawataki kutubu, basi mimi nitatubu kwa niaba yao,na njia pekee ni kukubali kuolewa na huyu mtu basi…’nikapanga hivyo…

NB: Kisa ndani ya kisa….ndivyo kisa hiki kilikuwa …kama nawachosha mniambie..


WAZO LA LEO: Utofauti wetu wa hali za kiuchumi usiwe ni tija ya kutokujali utu wa mtu, utu wa mtu haununuliwi kwa pesa au mali, utajiri wako usiwe tiketi ya kudharau wengine, na kuwaoana hawana thamani, ukifanya hivyo,hutakuwa na amani katika maisha yako, kwani kilio cha hawo unaowatendea hivyo kitakuandama.



Ni mimi: emu-three

No comments :