Docta amekuwa mfariji wangu
mkubwa, tokea enzi hizo, ananifanya nikumbuke mbali sana, maana mara kwa mara nikiwa
sina furaha, basi naweza kumpigia simu,tukaongea akaniliwaza, na hata kunipa
ushauri, na sijui kwa vile ni docta, lakini hata hivyo tumetoka naye mbali
sana, na sehemu katika maisha yangu ndio maana sitaacha kumsimulia kwenye kisa
cha maisha yangu….
Kutokana na huyu docta ndio nilijenga na kuiendeleza tabia yangu
ya kuamini watu, sio kwa kila mtu lakini wale unaoona wanaaminika, wale
marafiki zako wa karibu, waamini, maana na wao watakuamini, yeye ndiye
aliyenifundisha jambo moja, kuwa nisipende kuwadhania watu vibaya, maana
ukifanya hivyo unajijengea hisia mbaya moyoni mwako, na kujitwika mzigo ambao
haujatua kichwani mwako.
Basi wakati nipo hapo hospitalini, docta huyu akawa karibu nami
kunipa faraja ili nisahau maumivu ya kumuwaza mume wangu …na kiukweli nilikuwa
kwenye hali ngumu sana…mawazo, na yote yaliyotokea siku nzima, yangeliweza
kunifanya niathirike kisaikolojia, docta akanipa pambaja, nikahisi sasa nipo na
watu wenye kutumania.
Huyu docta ndiye aliyewahi
kuwa mchumba wangu, sasa kwanini ilitokea nikamuacha na kuolewa na huyu mume
wangu,..ni kisa fulani chenye mazingatio kwa wenye hekima…
Tuendee na kisa hiki
***********
Docta alikuwa pia ni rafiki ya mume wangu, wengi walitarajia
angelikuwa nai adui yake mkubwa, baada ya kunyang’anywa tonge mdomoni, lakini
haikuwa hivyo,…docta amekuwa seehmu ya kuijenga ndoa yangui kila inapolega
lega..
Naweza kusema pia docta ndiye aliyeniingiza kwenye dunia ya
mapenzi, alinitoa kwenye ujana na kuniingiza kwenye usichana, nikafahamu ni
nini maana ya mapenzi, enzi hizo, nikiwa kwa baba na mama yangu…hutaamini,
kinyumbe na walivyotaka wazazi, sikuweza kuolewa naye….
Huyu docta ni nilianza kujuana naye zaidi tukiwa chuoni, huku nyuma,
miaka ya utoto, shuleni, … nilikuwa namuona tu, ..kwa vile walikuwa majirani
zetu, na ni familia yao ni miongoni mwa familia zilizokuwa na uwezo wa mali,
wasomi waliobobea, kwani hata mtoto wao huyu aliweza kusomeshwa nje, kabla hajarudi
hapa nchini,
Pamoja na mengine mengi sitaweza kumsahau kabisa katika maisha
yangu
Ilivyotokea tunaweza kusema ni mipango ya mungu, maana kipindi
nipo na huyu docta , ndio amerudi kutoka ulaya, wakati huo hajawa docta kamili,
ndio alikuwa anachipukia, na kwa vile familia zetu zilishibana, aliporudi tu,
akawa anakuja kwetu, na akija anakaribishwa vizuri, mtoto wa watu, basi
tunakutana naye na kuongea mambo mbali mbali, akanizoea mpaka tukafikia hatua ya kukubalina
kuwa wapenzi.
Basi ikawa ni jambo la furaha kwenye familia zetu, maana tupo
kwenye daraja moja,…ni maisha yalivyo, kila mti na ndege wake. Familia zetu ikawa
imeliidhinisha tamko la kuwa mimi ni mchumba wa docta, kwahiyo yeye aliweza
kuja kwetu kunichukua, …unajua tena wao waliishi kizungu zaidi,..basi akija,
ndio hivyo tena, ila hali ya wazazi kukuchunga kwake inapungua, ananiombea ruhusa tunatoka kutembea sehemu
mbali mbali,…kiukweli mimi sikupenda sana maisha hayo y akujichanganya kwenye
majumba ya starehe nk..lakini utafanyaje
Na kitu ambacho kilinifanya nisipende maisha hayo, ni ile hali ya
kutizamana, nani kavaa nini, na zaidi pombe, tangia utoto nilitokea kukichukia
kinywaji kinachoitwa pombe ya aina yoyote…namshukuru mungu kwa hilo.
Na hata nikiandamana naye kama mpenzi wangu, alifahamu kabisa mimi nipo mbali
na ulevi, yeye kunywa kwake, ilikuwa kama kunywa soda, lakini hakuwa anakunywa
kuelewa, alikuwa na kipimo chake, sijui kwa vile ni docta.
Ikafikia muda akaanza kunishawishi ili nami niwe nakunywa kama
yeye, hapo ndio hisia zetu zilianza kusigishana, na hilo ndilo lilofanya tukaja
kukosana kabisa nay eye, lakini haikutokea hivyo tu kwa vile, hapana mimi
naweza kukiri kuwa ni mipango ya mungu ilipangwa iwe hivyo.
Kiukweli ilibidi afanye juhudi sana kunishawishi kwa kitu ambacho
sikipendi, na sijui kwanini siku hiyo ilitokea nikakubali. Ilitokea siku hiyo,
kulikuwa na shughuli za jirani, mmoja wa watu wenye uwezo, waliandaa tafrija
kwenye hoteli moja kubwa tu, tukawa tumealikuwa…baada ya mambo mbalimbali,
ikawa watu wanakula na kunywa, na hapo mpenzi wangu huyu akaanza kunishawishi,
ninywe
Kwa vile niliona ni siku ya furaha, na sikutaka kumuuzi mpenzi
wangu, siku hiyo nikasema ngoja nijaribu, nione ina ladha gani, ngoja nijaribu
nione hiyo raha wanayoifaidi wenzangu,…ilikuwa ni aibu kwangu na ndio siku
niliapa kuwa sitakunywa tena.
Nilikuwa nimekunywa kidogo, kumrizisha mpenzi wangu ambaye kipindi
hicho alikuwa ni huyu docta, nilikunywa gilasi moja tu tena kwa kujilazimisha,
ilikuwa haipiti kooni, nahisi ni harufu mbaya, nilipomaliza hiyo gilasi moja
tena haikumalizika,..,…
Hapo hapo nikaanza kujisikia vibaya, tofauti na ninavyoona
wenzangu wakichangamka, mimi nilihisi vibaya kupindukia, niliona kama dunia
inageuzwa, inazungushwa, roho imechafuka, tumbo linapanda na kushuka, nataka
kutapika lakini hakitoki kitu
Yaani siku hiyo nilijuta ni kwanini nilikunywa,..nilimuona mpenzi
wangu kama alitaka kuniua, na muda huo huo, nikamwambia mimi naondoka, siwezi
kukaa hapo tena, akanisihi, na kunishawishi, kiukweli anajua kubembeleza, na
unajua tena ni mpenzi wangu ikabidi nikae tu…kumrizisha.., na hata
aliponishawishi ninywe tena sikukubali, nilimuambia kabisa ukiendelea
kunishawishi kunywa hii sumu tutakosana kabisa.
Kwa muda ile nikajitahidi,
lakini hali haikuwa nzuri, bado nilikuwa najisikia vibaya,..ikafika muda,
siwezi kuvumilia tena, kwani roho ilishachafuka kupitiliza, nikakimbilia chooni, (washing-room), nikamuacha docta na
watu wengine wakiendelea kuongea na kunywa, wanajisikia raha zao.., ambazo kwangu
mimi ilikuwa ni kero tu.
Nilipokuwa kule hali ikatulia, kidogo cha ajabu sikutapika, kama
nilivyodhania nitafanya hivyo,..nikaona labda, hali imetulia, ndio wakati nataka
kutoka sasa,natoka chumba hicho cha usafi, nipo mlangoni, nikahisi kizungu
zungu,na kama asingelikuwa huyo jamaa kunidaka ningelidondoka vibaya kwenye
sakafu….
‘Pole sana dada, ....’akanidaka huyo jamaa na kunisaidia kusimama
vyema, lakini sikuweza, mwili ulikuwa hauna nguvu, tumbo linapanda na kushuka,
na sikuweza kuvumilia zaidi nikaanza kutapika, na matapishi ya mwanzo yakaenda
moja kwa moja kwenye nguo za huyo jamaa.
‘Oooh...pole pole, inaonekana umelewa, wewe..oh, ..tulia
kidogo,....’akasema bila kujali kuwa nimemchafua. Na kunisaidia ….
Na hutaamini hakujali kuchafuka kwake, yeye alichojali kwangu ni kunisaidia mimi akanishika vyema,
akichelea nisichafuke na yale matapishi niliyomlowesha nayo mimi, ambayo
yalikuwa kwenye nguo zake,....na akaweza kunisaidia hadi chooni, ilibidi aingie
choo cha wanawake ili niweze kujisafisha,..alipohakikisha nipo sawa, yeye
akakimbilia choo cha wanaume kujisafisha, nilijiskia vibaya sana siku hiyo.
Hali ilipotulia nikatoka, kumbe huyu jamaa alikuwa hapo nje
akinisubiria, alikuwa keshamaliza kujisafisha, na kukausha nguo zake
usingeliweza kujua kuwa nilimchafua, na aliponiona nikitoka akanifuata pale
mlangoni, na kuniuliza.
‘Upo sawa sasa,…?’ akaniuliza
‘Ndio nipo sawa, hamna shida, samahani sana, na nashukuru
sana…’nikasema
‘Usijali, inatokea tu…na samahani nikuulize ,upo na nani maana
naona hiyo hali unahitajia msaada...?’akaniuliza huku akinisogelea, na sikutaka
kuongea na mtu, nilichotaka ni kuondoka, na kwenda nyumbani kulala.
‘Nipo na na...’nikasita kusema
‘Na mume wako, au mpenzi wako, off course....’akamalizia
na mimi nikakubali kwa kutikisa kichwa, ili nitimize ule usemi wa kubali
yaishe, ili aondoke zake, na mimi niende kumuaga docta kuwa narejea nyumbani.
Kiukweli kwa muda ule nilidhamiria kuondoka, sikujali tena
kuendelea kukaa kumrizisha mpenzi wangu, wakati hajui kinachonisumbua, yeye
aliona ni kwa vile ni mara ya kwanza, basi nitazoea,…hapana sikuzoea na
sitaweza kuzoea maishani mwangu.
Nikawa natembea kulekea kule walipo docta na marafiki zake, lakini
nlikuwa nayumba, kizunguzungu, yaonekana kichwani bado nilikuwa sipo vyema,na kumbe
jamaa yupo nyuma akiwa na mashaka kuwa naweza kudondoka tena,…na alipoona sipo
sawa akanijia kwa nyuma na kusema;
‘Basi ni bora nikusaidia hadi kwa huyo mume wako,maana
unavyoonekana hujawa sawa, kwanini unakunywa pombe, wakati unaona
hazikupendi,.....achana na pombe,pombe zinawenyewe bwana, mimi mwenyewe
sinywagi kihivyo, ni kwa dharura tu....’akasema.
‘Sinywi tena...hapana nitaweza mwenyewe…..’nikasema na nikamtupia
jicho huyo mtu, na ilikuwa kama ndio namuona kwa mara ya kwanza, nikahisi hali
fulani, kama mshituko , ni kama kuna kitu nilikihisi, lakini niliona ni sababu
ya pombe, maana mtu mwenyewe simfahamu, lakini nikajiuliza ni kwanini nihisi
kitu kama hicho, nikapotezea, na sikutaka kumwangalia tena machoni.
‘Samahani nikuulize,… inakuwaje mume wako asijitokeze, kwani naona
kama umekaa huku muda mrefu hajashtuka tu…kama ulikuwa na hali hiyo alitakiwa
akujalia, au sio,,? Samahani lakini kama nawaingilia maisha yenu, au....?’akasema
kama kuniuliza, hata mimi nililiona hilo , lakini sikujali, na sikutaka huyo
docta afahamu kilichotokea.
‘Wenyewe wameshalewa, sizani kama hata wanatambua kuwa nimechelewa
huku....na nisingelipenda wanione kuwa nimetapika kwa ajili ya pombe, wala
usije ukawaambia hata hivyo nipo safi, haina haja ya wewe kunisaidia nashukuru
kwa wema wako huo..na sitakunywa tena hiyo mipombe yao, ....’nikasema.
‘Pole sana....mimi kama ningelikuwa na mpenzi kama wewe, ningeshtuka haraka sana,
ulivyochelewa hivyo…sio kwamba namsema vibaya huyo mpenzi wako, lakini kwa hali
hiyo alitakiwa awe karibu yako,…mimi hapa naogopa usije kudondoka tena.. sawa,
basi tembea mimi nitakufuatilia kwa mbali kuhakikisha umefika salama kwa mume
wako, ...’akasema, na kunifanya nifurahie sana wema wake.
‘Hongera ...kama upo hivyo, na mpenzi wako atakuwa na bahati sana…hata
hivyo, ni leo tu, mbina mpenzi wangu ananijali sana, sina shaka naye….’nikasema
na nikatamani kumwangalia tena huyo jamaa usoni, na nilipomuangalia, akili
yangu ikakumbuka kama niliwahi kuiona hiyo sura mahali, lakini sikuweza
kukumbuka vyema ni wapi, na lini, sikutaka kuwaza zaidi , nikapotezea.
‘Ina maana hunikumbuki mimi kabisa...?’ akaniuliza na kunifanya
nisimame wakati huo nilishaanza kuondoka kuelekea kule walipokuwa docta.
‘Kwani wewe ni nani…?’ nikamuuliza , na hapo ndio nikapa ujasiri
wa kumchunguza vyema usoni baada ya kugeuka kumuangalia vyema…hata hivyo
sikuweza kumkumbuka kuwa ni nani, akili ilikuwa haitaki kufikiria sana, na
sikutaka kufanya hivyo nikasema;
‘Samahani kwakweli sikukumbuki kabisa,..zaidi ya kukufahamu hapa
kuwa wewe ni mtu mwema, ...tuliwahi kukutana wapi mimi na wewe, shuleni, au
chuoni, au wapi?’ nikamuuliza ili tu kumuonyesha kuwa namjali kwa fadhila zake
hizo, lakini sikuwa nataka kuongea...
‘Kweli ukiwa mtu wa chini, ..watu hawakukumbuki kabisa, wewe sio
wa kwanza kusema kuwa hunikumbuki, lakini nafahamu ni kwanini...’akasema hivyo.
‘Hapana sio kwa vile wewe ni mtu wa chini, kwanini unasema hivyo,
wewe ni mtu wa kawaida mbona, mimi sipendi watu kujishusha, hakuna mtu wa juu
na chini, hizo ni hisia potofu, na kiukweli sipendi watu kujifanya hivyo…’nikasema,
na nikamwangalia tena kwa makini,japokuwa akili iliona kuwa nilishawahi
kukutana na mtu kama huyo, na sio kukutana tu, lakini moyoni nilikuwa kama
nimeguswa na hamasa, lakini sikuweza kukumbuka kabisa kuwa huyu mtu ni nani.
Muda ulikuwa umekwenda, sikumuona docta akija ..na sikupenda
kumuacha huyu msamaria mwema hivi hivi, nilitaka niondoke akiwa amerizika, sio
niondoke aone nimemdharau..hisia za wema wake ziliuteka ubongo wangu, ule
ukaribu wake , kunijali, nilimuona kama mtu niliyemzoea….sijui kwanini, yaani
kumbe kitu kidogo tu kinaweza kubadili hisia za mtu.
‘Samahani sana, labda kwa vile nipo katika hii hali, ndio maana
akili haifanyi kazi vyema, na nisingelipenda kufikiria zaidi, maana kichwa
kinaniuma, labda unikumbushe tu, kama hutojali...’nikasema na huku nikikwepa
kumwangalia tena moja kwa moja usoni na yeye akaniangalia na kusema;
‘Mimi ni mtoto wa mzee Mchapakazi…’akasema
‘Mchapakazi…?’ nikauliza, sikuweza kukumbuka ni nani anamuongelea
kwa wakati huo..
‘Humkumbuki yule mzee, aliyekuwa mlinzi wa pale nyumbani
kweny, na pia alikuwa akiwalimia mashamba yenu na mimi nilikuwa nafika kumletea
baba chakula, na siku moja ukanisadia pesa za ada ya shule, kipindi mzee
anaomba mkopo kwa baba yako, na baba yako akakataa kumpa hizo
pesa..umeshanisahau ehe...’akasema
‘Mungu wangu ndio wewe..mbo-mbona..hapana sio wewe…’nikasema huku nikainua kichwa kumwangalia na mdomo wangu
ukabakia wazi kuonyesha mshangao.
‘Ndio mimi …huamini eeh…mlifikiri tumejifia au sio…’akasema
‘Oh, …sio…ila kiukwe umebadilika sana..ooh, nimeshakukumbuka, ..oh
jamani , mimi nilikuwa kasichana kadogo kipindi kile,…unajua baada y alile
tukio, nilitokea kuwachukia sana wanaume, na nailijiskia vibaya sana kwa yale
yaliyotokea, hata hivyo nilitamani nikuone tena, lakini hukuja, nilishaahidi
kukusaidia ..kukulipa fadhila ulizonitendea...’nikasema.
‘Kunilipia fadhila , si zilishalipwa na baba yako, au umesahau
yaliyotokea..’akasema
‘Usiseme hivyo, wazazi wangu na wao walipokea taarifa
tu,..nakubali hawakutaka kuzichunguza,..’akasema
‘Unaweza kuwatetea hivyo, sawa, ni wazazi wako ni lazima useme
hivyo…ila kiukweli iliniuma sana kumuona baba yangu anazalilishwa, na sikutaka
kurejea tena kwenu, na nikawa nafanya vibarua tu pale waliponiachia jela, na sijui
ilitokeaje kesi ikafutwa na kuachiliwa, nilihangaika sana...hadi nikapata pesa
za kujisomesha, unakumbuka nilifaulu, na kwasababu ya kufungwa sikuweza kwenda
sekondari,…’akasema
‘Pole jamani…nilisikia, lakini aah, mimi sikuweza kufuatilia,
maana sikuwepo tena yaliyotokea nyuma nilifanya kuhadithiwa, nilijua yameisha,
kumbe..ndio hivyo tusamehe tu, na wazazi wangu…’nikasema
‘Nilipata msamaha, sikufungwa muda mrefu,.. na nilipotoka
nilimuomba baba tuhame hapo kijiji kabisa, tukaenda kuishi kijiji cha mbali,
huko nikaweza kujisomesha kwa kufanya vibarua...Baba yangu aliumwa sana, naweza
kusema ni kutokana na hilo tukio, na kuumwa
huko ndio ikawa sababu ya kufariki kwake...’akasema kwa uchungu.
‘Oh, pole sana, ina maana yule mzee alishafariki...?’nilimuuliza
nikishikwa na huruma, na fadhaa, na nilitamani nimkaribie ni mkumbatie
kumuonyesha jinsi gani nilivyojisikia….kiukweli niliona nina deni kubwa la
kumlipa huyu mtu, maana hii ni mara nyingine ananiokoa na kunifanyia huruma…moyoni
niliahidi kuja kumlipa kwa kadri nitakavyoweza.
‘Alifariki......ndio mapenzi ya mungu, na mapenzi ya mungu ndivyo
yalivyo, na moyoni hatukosi kuwa na sababu..ila kiukweli, baba alinipenda sana,
na hali yake hiyo ya kuumwa, na ilianzia pale mama alipofariki , mama yeye
alifariki mapema tu, tulipohamia huko,…na,… na hutaamini, baba alikuwa haishi
kumkumbuka mama, na hicho ndicho kilichomfanya hali yake izidi kuwa mbayae....na
hakupenda mimi niteseke, aliona ni bora yeye akafungwe, aliwaomba sana wahusika
afungwe badili yangu...’akasema.
‘Oh, jamani, poleni sana, sizani kama wazazi wangu walifahamu
hilo, na ukweli wote wa hayo yaliyotokea…na kwa vile alikuwa mfanyakazi wao kwa
muda mrefu wasingelifikia kumfanyia ubaya huo wote…na hata kufariki huko,
sizani kama walikuwa na taarifa,..wangeliniambia, na hata wao kufika kwenye
msiba, sizani kama wangeshindwa kufanya hivyo, sizani...’nikasema.
‘Baba alikataa kabisa, mama alipofariki, hakutaka kutoa taarifa
kwa watu wa mbali, na hata yeye alisema ikitokea akifariki..sisi tufanye hivyo
hivyo..maana alishaona dunia haina wema..aliniusia kabisa,.., nisije kuja
kuwaambia...na ndivyo ilivyotokea, alizikwa na watu wachache tu…, na wengi
hawakufahamu zaidi ya ndugu na jamaa wa karibu tu .....ndio hivyo, lakini mimi
sikukata tamaa ya maisha, nikasonge mbele, ....’akasema.
‘Sasa hivi unafanya kazi wapi?’ nikamuuliza.
‘Nipo hapa kwenye hii hoteli nabangaizabangaiza, nilipata tenda
ndogo hapa, ndio naifukuzia, ikiisha nakwenda sehemu nyingine, maisha
yanakwenda kidogo ninachokipata kinanisaidia, sitaki ile ya kuajiriwa maoja kwa
moja, mpaka nikamilishe malengo yangu…’akasema
‘Mungu wangu, imeniuma sana…sikutarajia hili , kweli milima
haikutani, ila wanadamu..mmh…sijui nitakulipa nini, sijui nifanye nini ili hayo
machungu yaliyokupata yaishe,..sijui, tusamehe tu, mimi na wazazi wangu..’nikasema
‘Ndio maisha sisi watu wa chini kupata kazi inakuwa shida,
na sipendi kwenda kuwapigia watu magoti kuwa wanipe kazi, sitaki nizalilike
kama alivyozalilika baba yangu, mimi nimeona njia iliyorahisi ni kujiajiri kwa
njia hii...hapa leo, keshi kwingine maisha yanakwenda,…..’akasema na hapo
nikamwangalia na kumbukumbu za nyuma zikanirejea...
‘Maua unafanya nini huku….?’ Ilikuwa sauti ya docta, na nikageuka
haraka na kuanza kutembea kumfuata, nilipomfikia, akaniuliza
‘Ulikuwa na nani muda wote huo…?’ akaniuliza
‘Nilikuwa najisikia vibaya, …sana…’nikasema
‘Utazoea tu,…pombe kidogo tu ndio imekufanya hivyo, ajabu kabisa…
tatizo lako hutaki kujifunza, starehe hiyo unaikosa bure, dunia hii kuna
starehe gani kama oh, upo ok, lakini samahani, sikuja kukuangalia, kuliko na
maongezi nyeti kidogo, nisamahe mpenzi…’akasema akinishika kiunoni kunifanya
nisipepesuke.
‘Nipo sawa, haina haja kunishika hivyo, mimi sipendi…’nikasema
‘Ok, ok…samahani nimesahau…haya twende, na yule aliyekuwa karibu
yako ni nani..?’ akaniuliza
‘Ni mfanyakazi wa hii hoteli, kanisaidia, sana, maana nilizidiwa
kidogo…’nikasema
‘Mhh, ok, sijamshukuru, naona simuoni tena....haya, twende
tukaendelee ..wenzangu ndio kumekucha..’akasema, na docta alikuwa hivyo hana
hisia mbaya na watu, ndio nilimpendea hivyo, ukimuambia kitu atakuamini, na
inaishia hapo.
‘Hapana mimi naondoka…siwezi kurudi tena kule, nahisi harufu za
pombe zitaniua,wewe nenda kaendelee tu na wenzako…’nikasema
‘Oooh,..hapana usifanye hivyo,…utaharibu, nitawaambiaje rafiki
zangu, kuna mambo muhimu tunaongea pale unajua kazi zangu ni watu, na watu ndio
wananiongezea michongo ya maisha..unajua, ...na wale pale ni watu muhimu sana,
ni madocta, wamenitangulia, nikiwa nao, najua nitafika sehemu ninayoitaka sana,
elimu yangu nataka inifikishe mbali kabisa..’akasema
‘Basi ..ndio maana nasema, wewe nenda kaendelee nao, wala sijali
kuhusu mimi, mimi nitarudi nyumbani peke yangu, maana hapa
na nyumbani sio mbali, nitafika bila wasiwasi..’nikasema
‘Siwezi kukuacha uende peke yako, na hii ni shughuli muhimu ya
majirani zetu haitaonekana vyema tukiondoka, hata wazazi wako hawatafurahi,
wakisikia hivyo, hebu lifikirie vyema hili, nikuombe kitu.., vuta vuta muda,
tutaondoka pamoja ..’akasema, niliwaza sana baadae nikasema sawa, basi nikarudi
pale mezani, lakini baadae nikamuomba mpenzi wangu kuwa nataka nikakae kwenye
hewa, nipate upepo,..sijisikii vizuri.
‘Wapi sasa, unaona mambo tunayoyaongea hapa ni muhimu sana, yanaweza
kukusaidia hata wewe , kwenye maswala ya ajira, kujiajiri, kuwekeza, unaona, ni
mambo muhimu kwenye maisha, leo wazazi, kesho ni sisi, tunahitajika kuchukua
hatamu, au sio..umesikia mwenyewe, mimi hatima ya haya ni kuwa ni hospitali yangu
kubwa, ndio ndoto yangu…’akasema
‘Usijali, mimi nitakuwa kule sehemu ya kutokea, ..palee , unaona,
wamekaa akina mama , na wasichana wasiopenda kujichanga huku,…utakuwa unaniona
au sio…’nikasema akakubali, kwa shingo upande, ..kiukweli kwa muda huo,
sikutaka kukaa pale na akili yangu ilishaondoka, yaani kuna kitu kilinibadili
ghafla, na ..hata sijui ni kwanini.
Nikaenda ile sehemu na kukaa , kulikuwa na watu wengine
wasiokunywa wamekaa hapo wanakunywa vinywaji vya kawaida, nikatafuta sehemu
nikaa, na nikanyosha mkono kumuashiria docta, kuwa nipo sehemu hiyo, na
akanipungia mkono kuwa kaniona..
Sasa ni wakati nimetulia, mara akaja mtu pembeni na kukaa,
…sikutaka kugeuka kwa haraka, kumuangalia ni nani, nilikuwa akili yangu
imetekwa na tukio kwenye Tv, kuna tamithiliya nzuri inaonyeshwa, na mara sauti
ikasema;
‘Kumbe yule ndio mume wako, najua hata yeye keshanisahau, …yupo na
akina kaka zetu wa enzi hizo,…mnaoana watu wenye hadhi zenu…’nikashtuka, kumbe
alikuwa yule msamaria mwema, nikahisi moyo ukinienda mbio, maana sasa kakaa
karibu yangu, nikageuka kuangalia kule alipokaa docta, nikawaona wanaongea na
kucheka tu. Hana habari kabisa na mimi…
‘Mhh…sio mume wangu…’nikasema
‘Kwahiyo, kumbe hujaolewa bado…’akauliza
‘Bado ndio tupo mbioni…’nikasema
‘Oh, mungu wangu kwanini hivi lakini…’akasema
‘Kwanini unasema hivyo…?’ nikamuuliza
‘Unakumbuka ahadi yetu lakini…?’ akaniuliza
‘Ahadi, mmmh…na..ndio na…nakumbuka, lakini…hayo yalishapita au sio ni mud asana,
na mambo yamebadilika,…na nishamuahidi docta kuwa ndiye mume wangu mtarajiwa,
samahani sana..’nikasema
‘Najua,hamna shida , nilitaka ukumbuke tu hilo, najua huwezi
kuolewa na mtu kama mimi,….ila nakuuliza tu…je moyo wako bado upo kwangu, au
uliniambia tu kunifurahisha,
utoto..lakini hatukuwa watoto kivile, au sio…samahani sana kukuuliza haya,
najua umeshampata mtu wa hadhi yako…sizani kama nina maana tena kwako…’akasema
‘Usiseme hivyo, wewe hujui tu….niliteseka sana,…sijui kwanini, na
hadi naamua kumkubalia docta, ilikuwa ni baada ya kusikia kuwa wewe haupo hai,
walisema ulifia jela au baada ya kutoka kitu kama hicho….’akasema
‘Eti nini…nilikufa…hahaha.., hayo labda waliyatunga wazazi wako,..ili….lakini
haina haja, najua, hutaweza kuolewa na mtu kama mimi, nafahamu hivyo,… lakini
niliapa kuwa bila wewe sitaweza kuoa tena, ndio maana nikawa napambana ili
niwze kufiki hadhi yenu, na nilitaka siku tukikutana unione tofauti, lakini ya
mungu mengi tuakutana leo bila kutarajia…’akasema
‘Jamani…..’nikasema hivyo nikigeuka kumuangalia kwa macho
yaliyojaa huruma
Na wakati namuangalia, ndio kumbukumbu za nyuma zikaanza
kunirejea, na ikawa ndio sababu ya kunibadili kabisa mawazo yangu, hasa
kutokana na yaliyotokea siku za nyuma kweli kumbukumbu hubadili maisha…na
kutokana na kumbukumbu hizo zikanifanya nimuache docta…haikuwa kazi rahisi,
lakini…
NB: Tutaendelea sehemu ijayo. Ilikuwaje, na ina umuhimu gani
kwenye hiki kisa, tuzidi kuwepo…
WAZO LA LEO:
Tofauti za maisha, tofauti za kipato, tofauti na utawala na wasio kuwa
watawala, isiwe ndio sababau ya kuzarauliana, maana huwezi kujua, ni yupi ni
muhimu kwenye maisha yetu. Unaweza ukawa na kipato lakini ukawa na mapugufu
fulani ambayo yanaweza kujaziliwa na yule unayemuona ni hadhi ya chini, au
akaja kukusaidia yule ambaye hukutarajia kabisa. Mola ni mwingie wa hekima
anajua ni kwanini maisha yapo hivyo,..
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment