‘Ajali….’ Ilikuwa kauli yangu ya awali pale nilipozindukana, sijui
kwanini hali hiyo ilinitokea,..kupoteza fahamu,…mmh.. nilijiuliza pale bila
kujua sababu ni nini,.. labda ni kuchoka tu, mambo yamekuwa mengi kupitiliza…,
niliinua uso na kuwaangalia watu , maana walishafika kuangalia kuna tatizo
gani, …haikuchukua muda mrafu hiyo hali.
Bahati nzuri, nahisi ni dakitari, alikuja kutokea hapo kwenye hilo
jengo la soko-duka, alikuwa kavalia nguo za kidakitari, hilo jengo ni kubwa
lina ofisi nyingi na mojawapo ni dispensary. Na kuwa huo alikuwa kachuchumaa karibu yangu, na akawa ananiangalia
tu, huenda alishanichunguza nikiwa nimepoteza fahamu
Mimi kwa haraka nikajaribu kusimama,…nikajikuta narudi chini,..
nilihisi kizungu zungu kidogo, huyo docta akanishika mkono, kunisaidia, nikaa
vyema, nikawa najifunika vizuri, kushusha gauni vyema….
‘Upo ok.., unajisikiaje sasa..?’ akaniuliza na mimi nikawa kimia,
nikitafakari, kuvuta fikra.
‘I hope so, nipo ok…’nikasema
‘Mhh, unahitajika kutulia kwanza, naona hali yako bado haijawa
sawa, unahitajika mapumziko kidogo, sijaona tatizo lolote kubwa kwako, lakini
ni vyema, ukafika hospitali kwa uchunguzi zaidi, hapo ndani kuna zanahati,
nahudumia hapo, kama hutojali unakaribishwa...’akasema huyo docta?’ akaniuliza
‘Nipo ok…nahisi hivyo, natumai, hunidai kitu…’nikasema
‘Hamna…sijafanya lolote, nilikukagua tu Je utaweza kuendesha gari mwenyewe…, au
tumpigie mume wako simu,au jamaa yako, simu yako hii hapa, tukusaidie kumpigia…?’
akauliza huku akiwa kashikilia simu yangu, nahisi waliichukua wakitafuta namba
ya jamaa yangu yoyote.
‘Hapana….niko ok..’ Ni alipotaja kuhusu mume wangu, ndio akili
ikafunguka, nikakumbuka ile simu niliyopigiwa na hapo hapo kwa haraka nikaingia kwenye gari…
‘Ahsante sana kwa huduma yako,….’nikasema
‘Hamna shida, uwe mwangalifu tu, na nazidi kukushauri fika
hopsitali, usizarau hilo laweza kuwa chanzo cha tatizo , na huwezi kulijua
mpaka ukapimwe…’akasema huyo docta na mimi nikawasha gari na kuanza kuondoka.
Niliendesha gari langu kutoka eneo hilo, na muda huo sikuwa na
wazo la kuangalia vitu vyangu kama vipo salama,..sikuwa na wazo la kuangalia
simu yangu ambayo, alinikabidhi huyo docta niliweka pembeni ya kitu,..kumbe
simu yangu …ilikuwa imezima..watu wananipigia wanipati.
Nilipokaribia eneo la nyumbani kwangu ndio nikakumbuka kuwa
dakitari alisema nipitie kwake,… lakini niliona haina umuhimu kwa muda huo, kwanza nifike nyumbani kwangu, nijue
kinachoendelea,…maana mpigaji simu, nakumbuka alisema,..
‘Kuna ajali, gari la mume wako limepata
ajali, lakini hayupo….haonekani…. , tunahisi huenda kaimbilia nyumbani kwake…
watu wanamtafuta haonekani sijui wapi alipo….’nilikumbuka hiyo sauti.
‘Ajali halafu yupo nyumbani, haonekani wapi alipo…?’ nikajiuliza
tu, hata sijui nifanyeje, lakini muhimu nikaona nifike nyumba kwangu kwanza,
nianzie hapo.
Ndio nikakumbuka simu yangu, nikaichukua na kuiwasha sijui kwanini
ilizimika, maana chaji ipo ya kutosha, nia yangu nikujaribu kumpigia mume wangu…
lakini ujumbe nyingi zikaanza kuingia, kuashiria kuwa watu wengi walikuwa
wakinitafuta, nikapokea simu iliyokuwa inaita kwa muda huo.
Alikuwa ni docta jirani yangu….
‘Upo wapi…’ akaniuliza kwa
haraka hivyo
‘Nipo , ndio nafika kwangu…’nikasema,
‘Ok sasa ni hivi, fika hapa kwangu mara moja ni muhimu sana, mume
wako yupo hapa,…’akasema
‘Yupo salama lakini…?’ nikauliza
‘Ndio…anaendelea vizuri…mengine utayajua ukifika hapa….’akasema.
‘Haya…nakuja…’nikasema
Nikarudisha gari nyuma, maana sio mbali na kwangu, tunatenganishwa
na bara bara na ukuta…
‘Umeshafika…’akanipigia tena docta, nilishangaa kwanini kapiga
tena kwa haraka, nikaanza kuhisi kuna tatizo kubwa.
‘Nimeshafika eneo la getii ya nyumba yako....vipi kuna maendeleo
gani…maana huyo mtu aliyenipigia simu, alisema kaona kama gari la mume wangu
limepatwa na ajali, …lakini sizani kama ni yeye, kwani ninafahamu yupo kazini,
yupoje mume wangu, ni yeye, kaumia, …’nikasema.
‘Sawa ingia ndani, tutaongea ukifika, hajambo….’akasema.
‘Nataka kujua ni kweli docta, niambie yupoje..?’ nikauliza.
‘Mume wako ni kweli kapatwa na ajali..…, na yupo hapa nyumbani kwangu,
...’akasema
‘Kwanini hajaenda hospitali, …?’ nikauliza
‘Ukifika tutaongea, kama ni kwenda hospitali..au la…wewe ukifika
unaweza kusaidia hilo, maana mwenyewe hajataka kwenda hospitalini ...’akasema
‘Mhh..haya nakuja…’nikawa najiuliza imekuwaje, nijuavyo mume wangu
alikuwa kazini, sasa hiyo ajali ilitokeaje, na wapi…nikawa najiuliza.
Basi nikaingia nyumbani kwa docta
************
‘Oh, shemeji bora umewahi kufika, naona uliendesha kwa mwendo usio
wa kawaida, msifanye hivyo....’akasema jirani yetu huyo mmoja, ambaye nahisi
aliniona wakati naingia na gari kwa mwendo wa kasi.
‘Mumeo ni kama unavyomuona kapatwa na ajali mbaya sana, kwa jinsi
nilivyoambiwa na watu, …na ameponea kwenye tundu la sindano,hapa tumempatia
huduma ya kwanza , hata hivyo alitakiwa awepo hospitalini kwa hali jinsi
ilivyo...cha ajabu mumeo amekataa kata kata tusimpeleke hospitalini,…’akasema
‘Kwanini jamani, hili sio swala la kuhitaji yeye kukubali au la,
docta, rafiki yako huyo, unambembeleza kwa hilo…?’ nikauliza
‘Yeye alisema afikishwe hapa nimpatie huduma ya kwanza, anahisi hana
tatizo,..’akasema
‘Kwahiyo..?’ nikauliza
‘Muhimu afikishwe hospitalini haraka iwezekanavyo, ...’akasema docta.
Mimi sikuelewa, kwanini mtu apatwe na ajali ya gari, watu badala
ya kumpeleka hospitali, wanamleta huku nyumbani kwa docta,...labda, au sijui
alikuwa na maana gani kutibiwa nyumbani.
‘Shemeji kwa hali ilivyo, tunahitajika tumuwahishe hospitalini,
hatuwezi kumsikiliza tena yeye, na kwa vile wewe upo, utawezesha hili,
tulishapigia simu gari la wagonjwa linakuja,,....’akasema docta.
‘Haya, mimi sioni kwanini tusubiria hilo gari la wagonjwa, si
tunaweza kumbeba hadi kwenye gari langu,au…?’ nikauliza
‘Gari la wagonjwa linakuja na kitanda cha kumlaza, …isije kuleta
matatizo mengina lakini kwa vile limechelewa, basi tumbebe tu, awahishwe
hospitalini…’
Nilimuangalia pale alipolala, shati ni vipande vipande…uso
umevimba, na michubuko…
‘Sasa hivi kapatwa na usingizi kwa dawa nilizompa…’akasema docta
‘Basi abebwe hivyo hivyo, afikishwe hospitalini…’nikasema
‘Ni kweli, lakini lazima atazindukana, na ataweza kuhisi maumivu
kwa sasa , alikuwa kama kachanganyikiwa alivyoletwa hapa…’akasema
‘Kwahiyo aliletwa kumbe…?’ nikauliza
‘Kuna mtu alikuwa anamsaidia, alikuja naye, wakati mimi nataka
kutoka nje..kiukweli alikuwa akitembea kwa shida sana, na muda huo hajaanza
kusikia maumivu bado, nahisi sasa ataanza kuyasikia, nimempa dawa za kutuliza
maumivu zitasaidia kidogo…’akasema
‘Mhh, ...huyu mtu ana hatari kweli…angelifika hospitalini kwanza,
kwa hali hii jamani anakuja kutibiwa nyumbani kama mhalifu…’nikasema,
‘Hayo hayana maana kwa sasa, hakuna haja ya kusubiria hilo gari la
wagonjwa, tulionelea kama gari la wagonjwa
lingelifika mapema, tungeliweza kumfikisha hospitalini bila kukwazika na foleni,
na kuzidi kulete athari mwilini.’akasema docta.
Docta akatoa kitanda chake
ca kukunja, wakasaidiana kumweka mume wangu kwenye hicho kitanda, sasa alikuwa
kilalamika maumivu., wakamtoa nje na kumlaza kwenye kiti cha nyuma cha gari
langu, na tukaanza safari ya kuelekea hospitalini.
Ndani ya gari pamoja na docta alikuwepo mtu mwingine na jirani
mmoja, na hapo ndio nikaanza kusikia jinsi ilivyokuwa, lakini akili haikuwa
sawa kusikiliza wanachoongea….
‘Nimeambiwa hiyo ajali ni ya aina yake, ukiambiwa kuna mtu katoka
hapo huwezi kuamini…’akasema
‘Kwahiyo ilikuwaje, uliona ilivyotokea…?’ akaulizwa
‘Hapana , mimi nililiona hilo gari, halina thamani tena…’akasema
Sikutaka kusikia wanachoongea, kwani wanavyozidi kuongea hivyo,
ndio nazidi kuogopa, nilitamani kuwaambia wanyamaze..sijui ilikuwa, wakanyamaza
hadi tunafika hopsitalini.
Kila nilipokuwa nikimtupia macho mume wangu, wakati sasa anatolewa
kwenye gari kuweka kwenye vitanda maalumu vya wagonjwa, ndivyo nilivyoanza
kuona kuwa kweli mume wangu yupo kwenye haali mbaya, hali yake ilishaanza
kubadilika, alionekana kama anazidiwa, na hapo wasiwasi wangu ukazidi, na hadi anaingizwa
hospitalini,sikuwa na amani, nilimuona
kama kapoteza fahamu..
Mwili uliniisha nguvu
kabisa, lakini nikajitahidi kutembea hadi sehemu ya kusubiria…nilijiuliza
tatizo ni nini hasa, ..maana docta
alisema mume wangu hajaumia sana. Hapo sikuwa na sababu za kuvumilia,
nikamuendea docta, muda huo alikuwa akiongea na simu.
‘Docta kuna nini tena kwa mume wangu....?’ nikamuuliza, na yeye
akaniangalia machoni, na hakusema kitu hapo hapo, lakini baadaye akasema;
‘Tutajua baada ya uchunguzi, hivi sasa siwezi kusema lolote,
lakini kila kitu kitakuwa sawa....ngoja wakamchunguze na kumpiga x-ray. Na utra
sound, tutakuja kufahamu hilo…’akasema, sasa hakusubiria akaelekea huko
alipopelekwa mume wangu, chumba cha wagonjwa mahututi.
‘Docta…’nikamuita, nilitaka kumuambia asichelewe kunipa taarifa,
sijui kama alinielewa, yeye alinionyeshea ishara kuwa nitulie, nisijali kwa
mkono,
**********
Dakitari huyu pamoja ya kuwa ni jirani yetu,pia ni rafiki mkubwa
wa mume wangu na alikuwa mpenzi wangu wa awali kabisa ,kabla sijakutana na huyu
mume wangu na wazazi wangu walitaka sana niolewe na yeye, lakini mimi
nilipingana nao kwani hakuwa ndio chagua langu. Wazazi wangu waliona yeye ndio
hadhi yangu, kiuchumi na kielimu.
Kuna sababu za msingi, zilinifanya nisioelewe na yeye, mojawapo ni kuwa mimi nilikuwa nimempenda huyu
mume wangu bila kujali hali yake ya kiuchumi. Nilikuwa na sababu zingine tu
ambazo hazina umuhimu wa kuzitaja hapa kwa sasa.
Tulikuwa nje sasa
tukisubiria,..mimi pale sina amani kabisa…na haraka nikataka nipate angalau mtu
wa kuongea naye angalau niwe na amani, ndio nikampigia rafiki yangu simu,
nikamwelezea kuhusu ajali iliyompata mume wangu..
‘Unasema nini kapatwa na ajali saa ngapi…?’ akauliza, kama vile
haamini, na mimi nikamuelezea jinsi nilivyosikia.
‘Oh, labda…ilitokea muda ule, na kumbe ndio hiyo watu
wanaiongelea, kuwa hajapona mtu kwenye hilo gari, ..nahisi sio hiyo maana
wanasema hawezi mtu kupona kwa jinsi gari lilivyo…oh, kwanini aliendesha kwa
mwendo kasi, kiasi hicho…’akasema
‘Hata sijui, maana mimi najua alikuwa kazini, na muda ule ni wa
kikao, kwasababu niliongea na mtu mmoja alikuwa kwenye hicho kikao chao, hata
mpaka natoka pale kwako, najua yupo kwenye kikao, sasa …alitoka saa ngapi..hapo sijui…’nikasema
‘Oh ..na ile kona ni mbaya…’akasema
‘Kona gani…?’ nikamuuliza
‘Acha ile kona ya kutoka kwangu , unaipita hadi ile kona ya bara
bara inayokwenda kuelelea kwenu…ndio nimesikia hiyo ajali imetokea hapo, lakini
sizani kama ndio hiyo ya she- , …ya mume wako…’akasema, nilisikia mtoto analia,
akawa anakat akata maneno.
‘Oh, mungu wangu wakati napita hapo niliona watu wamekusanyika,
sikutaka kuangalia, maana nilikuwa na haraka, ina maana…sasa huko alitokea
wapi, …mbona kupo kinyume na barabara ya kutokea kazini kwao…?’ nikauliza
‘Labda…alipotoka….hata sijui…hilo tuliache tu…’akasema
‘Hapana,..tuliache kwa vipi, …yaani, muhimu ni kujiuliza huko
alifuata nini, na….oh, mungu, ….mungu amjalie apone tu..,..maana hali
ilibadilika ghafla tulipofika hapa hospitalini, naogopa kweli rafiki yangu…’nikasema
‘Mhh…muhimu ni hali yake,…hiki kitoto kinasumbua, nakiogesha hapa,…basi,
usijali rafiki yangu, mengine hayana tija, atapona tu kwa uwezo wa muumba, …’akasema
‘Ni kweli,…mengine sijui yapi hayo…haya, ndio hivyo rafiki yangu, ni siku ambayo sitaisahau kabisa, maana njiani napo
nilikutwa na mikasa, nikiwa soko-duka, nilipoteza fahamu ghafla..’nikasema
‘Ulipoteza fahamu…!!!, ilikuwaje tena jamani… pole, na wewe
umezidi kujiongezea mawazo, mengine yaache yatajipa yenyewe, ukitaka kufahamu
kila kitu unaweza kuathiri ubongo wako…Haya utanipa taarifa
kinachoendelea…’akasema
‘Sawa nitakujulisha..’nikasema na kukata simu.
*************
Baadae docta mmoja akaja, akasema wameshaondoa ile hali mbaya,
hakuna matatizo tena, hakuna athari za ndani, kwahiyo mume wangu atapelekwa
chumba cha kulazwa wagonjwa wa kawaida, baadae kweli akatolewa huko ICU,
‘Hii ina maana kuwa hana tatizo kubwa…’akasema docta jirani yangu,
aliyekuja baadae
‘Kwahiyo tunaweza kwenda kumuona….?’ Nikauliza
‘Ndio..sizani kama kuna kikwazo…’akasema
Tulipofika kwenye hicho chumba alicholazwa mume wangu, tulimkuta
kama kalala, kafumba macho, kalala kaangalia juu, nilimkagua kichwani kafungwa
fungwa, umebakia uso,..na shingoni kavaliwa dude kuashiria huenda kuna hitilafu
shingoni….hiyo ni dalili kuwa kweli alikuwa kaumia, japokuwa alijikaza
kuonekana kinyume chake..
Baadae akafungua macho, nikamsogelea nilimuangalia mume wangu pale
alipolala, nikahisi machozi yanataka kunitoka…kalala huku kaangalia juu,
hakutaka hata kugeuza kichwa kuniangalia, labda hawezi kugeuza shingo,..nikamsogelea
pale kitandani, na hapo akajitahidi kuniangalia, kwa kugeuza macho, nikaona
machozi yanamtoka…akasema
‘Pole sana mume wangu, mungu ni mwema utapona tu…’nikasema
‘Nisamehe sana mke wangu, ni-sa-sa- mehe…’akasema huku machozi
yakiendelea kumtoka, nikachukua leso yangu na kumfuta, sikuelewa, nahsi ni hiyo
hali,…hata mimi pale machozi yakawa yananilenga lenga, nampenda sana mume
wangu, na kumuona kwenye hiyo hali, niliumia sana, mawazo yalinipeleka mbali
sana.
‘Usijali utapona, tu…mume wangu…’nikajitahidi kusema hivyo.
Sasa akafumba macho, akawa
anahema taratibu, na hilo lilinipa moyo, kuwa kufumba macho huko sio kwa ubaya,
nikasema
‘Mume wangu utapona tu..tuzidi kumuomba mola…, umenielewa eeh,
docta amesema hakuna tatizo kubwa…’nikasema, lakini akilini nikawa najiuliza ni
kwanini kakimbilia kusema; nimsamehe…labda,…kawaida mtu akiumwa hujua hatapona
ndio anaomba msamaha kwa watu, labda…
‘Atapona tu…’nikasema hivyo
‘Ndio atapona docta kasema ni athari ndogo za kuteguka …na ngoja
tusubiria vipimo halisi havijatoka kwanza…’akasema docta huyo jirani yangu.
Baadae mume wangu akapitiwa na usingizi, na tuliambiwa tumuache
alale, sisi tutoke nja, tukafanya hivyo.
Na wakati tupo nje, ndio nikajaribu kuwauliza watu walikuja nasi,
yupo docta , na jirani mwingine na mfanyabiashara aliyenipigia simu, yeye alishafika,
wengine yule mwingine tuliyekuja naye alishaondoka, huyu mfanyabiashara anasema
yeye alishuhudia hiyo ajali,…
‘Kwani ajali hiyo imetokeaje..?’ nikauliza
‘Imetokea ile kona ya kutoka barabara kuu, kuingia barabara ya
mitaa inayoelekea kwako, mume wako alitokea mitaa ya kutokea Uzunguni, mimi
nilikuwa barabara kuu naelekea kwingine, nikasikia huko nyuma paaah, mlio wa
kuogonga, unajua nilikuwa naendesha sikuona ilitokeaje, nikasimamisha gari, na
kutoka nje…’akasema
‘Ina maana ni huu mtaaa wanaouita ‘Uzunguni..’..huko alitokea
wapi, …huko si ndipo anapoishi rafiki yangu, mbona mimi nilikuwa maeneo ya huko…,
sijamuona ….?’ Nikasema na kuuliza
‘Ndio hivyo..yawezekana alikuwa anaendesha kwa mwendo kasi, nahis
alikuwa akiwahi jambo, au angelikuwa mhalifu tungelisema anawakimbia polisi…’akasema
huyo mfanyabiashara
‘Mhh, hata sielewi, na hana tabia ya kuendesha gari kwa mwendo
kasi..sio kawaida yake…’nikasema
‘Mimi nilijua mlikuwa naye labda…akawa anawahi kitu nyumbani,
..kama ulikuwa maeneo ya huko…’akasema jamaa mwingine.
‘Oh, hata sijui…sikumuona kabisa maeneo ya kule…hakuna mtu
aliyemuona,.., labda kwa vile nilikuwa ndani
naongea na rafiki yangu..labda kuna kitu alikuwa akikifuatilia, akapitia njia
hiyo..akitokea wapi sasa…mmh, hata hivyo ni kwanini akimbize gari hivyo…’nikasema.
‘Ni ajali tu…’akasema docta
‘Kiukweli ana bahati sana, maana ukiliona hilo gari, utasena
hakuna mtu aliyetoka humo ndani, halitamaniki, alikuwa kwenye mwendo kasi sana,
..na gari lenyewe baadae liliwaka moto, na hata watu walipouzima, lilikuwa
limeshateketea kabisa…’ akasema jirani.
‘Oh, ...niliona ajali hapo njiani wakati nakuja, lakini sikujua
ndio hilo ya gari la mume wangu,....,’nikasema
‘Sasa mimi nawashangaa huyo mtu aliyemleta hapo nyumbani kwako
docta, badala ya kumkimbiza hospitalini,
alikuambia ni kwanini alifany ahivyo?’ akaulizwa docta.
‘Nahisi alichanganyikiwa, na labda hakutaka ijulikane ajali hiyo
imetokea wapi, labda maana tunajisema wenyewe tu kuhisia,..sabbu kubwa ni kuwa alichanganyikiwa maana haina maana hapo…, gari
si lipo, kama ni wazo hilo, la kuficha kuwa ajali ilitokea wapi…’akasema yule
mfanyabiashara.
‘Unajua watu walipofika kwenye hilo gari, walijua wanafika kutoa
maiti tu..mimi mwenyewe nilishashika kichwa nilipogundua kuwa ni gari la mumeo…lakini
watu walipofika hapo, wanashangaa kuona ndani ya gari hakuna mtu…ina maana huyo
mtu alitoka kabla ya kugongana au alirushwa nje ya gari…’akaelezea
‘Na walipoona hivyo hakuna mtu, wasamaria wema wakaanza kuhangaika
kutafuta dereva yupo wapi, lakini hakuonekana kabisa…mimi mwenye nahangaika
kukupigia, simu inatumika, mara hupatikani mara…baadae ikawa haipatikani kabisa….’akasema
huyo mfanyabiashara.
‘Mimi hata sijui….mume wangu jamani, apone tu,..sikujua kuwa ni
gari lake wakati napita pale, nilikuwa na mawazo mengi, na kama ni ajali
nilitegemea kwingine kabisa sio njia hiyo...’nikasema
‘Gari halithaminiki, hakuna kumbukumbu yoyote ndani,..maana
lilikuwa bado haliingiliki, baadae mimi kwa vile nalifahamu ni la nani,
taratibu bila kuwaambia watu lolote, nikaanza kufuatilia, kukupigia simu ukawa
hupokei, baadae mimi wazo likanijia...
Nikaamua kwenda nyumbani kwanu, na nimefika pale haupo, na mumeo
hayupo,,…nikaona hapa, isije ikawa mtu kaungulia ndani ya gari hatukuona vyema,
nikataka kurudi tena kuhakikisha,…sasa wakati natoka pale kwenu, ndio nikakutana na jamaa mmoja rafiki yangu, akaniambia,
kuwa kakutana na mumeo, yupo kwenye hali mbaya, …kaingia nyumbani kwa docta.
‘Mhh, hapo kwa haraka nikahisi aliruka alipohisi ajali, lakini
mmh, yatakiwa uwe mzoefu kweli kama askari, sijui…yaani hapo ni kitendawili
mpaka mwenyewe ajae kutuambia…’akasema
‘Hata hatujui alifikaje kwa docta,…..rafiki yangu mmoja alikuwa
anapita na gari lake, ndio akamuona yupo nje ya mlango wa docta akiwa kasimama,
kashikilia mlango, ..yupo hoi,..kama aliyepatwa na ajali, ana damu, shati
limechanika,..ikabidi asimamishe gari kuja kuangalia kuna tatizo gani, ndio
akamuona yupo kwenye hali mbaya,… akamsaidia kuingia naye ndani,kwani aliadai
aingizwe humo ndani kwa docta.
‘Nikamuuliza alimuachaje …hali
yake vipi, maana siamini, mtu katokaje kwenye hilo gari…’akasema.
‘Akasema kumbe docta huyu jirani yenu yupo likizo, walimkuta yupo
hapo ndani, basi ikabidi aanze huduma ya kwanza, akaniambia kuwa kamuacha huko
ndani akimuhudumia, lakini anaonekana hayupo vibaya, ila ni kama
kachanganyikiwa…’akasema
‘ Mhh… mungu mkubwa…’nikasema hivyo. Na mimi ndio nikaingia na
kumkuta docta akimuhudumia na kwa muda huo hata docta hakujua kilichotokea,
ndio nikamuelezea, nilichokiona huko nilipotoka, na ndio akajaribu kukupigia,
naona simu yako ina matatizo,…simu yako haina matatizo kweli…?’ akauliza huyo
mfanyabiashara.
‘Haina matatizo, lakini kuna muda ilizima…’nikasema hivyo,
sikutaka kuongea zaidi, pale nilikuwa na hamu nirudi ndani nikamuangalia tena
mume wangu.
Nikamsogelea docta kumuomba akaombe ili niweze kuingia ndani, nikamuone
tena mume wangu.
‘Sawa, hamna shida…’akasema na kuniambia tuongezane, basi tukaenda
naye hadi pale alipolazwa mume wangu
Nilipomchungulia mwili wake, nilihisi mwili wangu ukisisimuka
sikujuwa kwanini, kwanini kanyoka tu vile…, na muda ule alikuwa kafungua macho,
sasa hataki hata kuniangalia machoni, mwili wangu hapo ukafa ganzi, nikawa
nasubiria tu hiyo taarifa ya docta nisikie kama ana tatizo au hana...
Pale docta akaongea nilipomuuliza ni kwanini alikuja kwake…
‘Yeye ndiye aliyenipigia simu, na namba tofauti, nahisi alimuomba
mpita njia mmoja, mtu wa bajaji…kwa bahati nzuri nipo likizo, kwahiyo nilikuwa
hapo nyumbani, nikijua ni tatizo dogo, ndio hivyo akaletwa, kiukweli nilimshauri aende
hospitalini, lakini alisema ni muhimu atibiwe hapo nyumbani tu, na nilion
akachanganyikiwa, anasema hataki ijulikane kuwa kapatwa na ajali, ..ni
kuchanganyikiwa tu huko...
‘Kwanini hataki, wakati keshapata ajali, mmh…?’ nikamuuliza
‘Atakuja kukuambia mwenyewe, ndivyo alivyosema…’akasema docta
‘Kiukweli nilipomfanyia uchunguzi wa haraka haraka na kufanya kile
kinachowezekana, sikuona tatizo kubwa la nje, ila…ajali ni ajali, unaweza kwa
nje usione kitu, tatizo likawa lipo kwa ndani, na unaona, kumbe kuna athari
kwenye uti wa mgongo na shingoni, ngoja tusubiria taarifa za madocta,..
’akasema huyo docta jirani yangu
‘Uti wa mgongo…umeathirika..mungu wangu ina maana gani sasa ina
maana hataweza kutembea tena,..’nikasema nikishika kichwa
‘Usiwe na wasiwasi, …yupo kwa wataalamu..ngoja tusubirie uchunguzi
wa mwisho….’akasema docta kunipa faraja
NB: Ndivyo ilivyokuwa hivyo....,
WAZO LA LEO:
Mwili wa binadamu una uvumilivu wake, tunahitajika kuutunza sana, na
unapouzidishie mambo juu ya uwezo wake, ukiulazimisha sana mwili, hasa
kimawazo, tunaweza kujikuta tukipatwa na athari za kiafya. Mazoezi ni muhimu
sana ili kuwezesha miili yetu, na akili zetu kubeba mambo kwa mpangilio. Lakini
pia tusipende kuulazimisha kupita kiasi…hasa mawazo, mawazo yakizidi sana huja
kuleta matatizo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment