Sikutaka kuondoka kabisa siku hiyo hapo hospitalini, lakini baada
ya ushawishi mkubwa wa madocta ilibidi niondoke, maana walisema hata nikikaa
hawataniruhusu nionane naye kwani hawajui ni kwanini ilitokea hivyo baada ya
kuniona mimi.
Basi baada ya kurejea nyumbani, nikapiga simu kwa rafiki yangu,
kabla hata sijamuuliza yeye akatangulia kusema kuwa ile kazi hajaikamilika,
kuna vitu bado hajaweza kuvipata kwahiyo nimpe muda zaidi, na mimi sikuwa na
cha kumwambia maana mawazo yangu kwa wakati huo yalikuwa mume wangu.
‘Mume wangu hali yake sio nzuri…kwahiyo sawa,…kama wahitaji muda,
..sijui wataka mpaka lini,… ila jitahidi, nakupa siku moja ya ziada, ufanye haraka iwezekanavyo, maana huo
uchunguzi ni moja ya mambo ya kumsaidia yeye mgonjwa..’nikasema
‘Kwani kazidiwa tena zaidi, si ndio hiyo hali ya kutafuta
kumbukumbu au…?’ akauliza
‘Hivyo hivyo tu, unasema kumbukumbu, ulipata wapi taarifa hizo…?’nikasema
na kuuliza
‘Atapona tu…ilimradi yupo na madakitari…’akasema bila kujibu swali
langu, na sikutaka kumuuliza tena.
‘Ndio hivyo, ila kuna kitu kinamsumbua, mimi sijajua anasumbuliwa
na nini hasa, hata madocta hawajui tatizo ni nini hasa…walitarajia mimi
nitaweza kusaidia..hata sijui nifanye nini,…, ndio maana nilitaka hiyo kazi
uimalize kwa haraka iwezekanavyo, unielewe hapo rafiki yangu ni muhimu sana
kwangu na kwa mume wangu, nashindwa mimi nifanye nini sasa…’nikasema
‘Sawa nimekuelewa,…ila kiushauri wangu, hata ikikamilika hii
taarifa ni bora ukasubiria apone kabisa, kuna mambo mengi, yatamsumbua kichwa
ukianza kumhoji ni kwanini, ni kwanini..unanielewa hapo lakini.., hasa ya
kazini kwake, na mengine ni wewe na yeye, hakuna zaidi ya hapo, mengine ndio
haya sijapata uhakika nayo…’akasema
‘Mimi nikiipata hiyo taarifa nitajua kipi ni kipi cha kuongea
naye..je huyo mzazi aliyekuwa akimfuatilia umeweza kumtambua ni nani, maana
siku hiyo ya ajali nasikia aliondoka kwenye kikao, akiaga kwenda kumuona mzazi,
…sasa ni nani..?’ nikamuuliza
‘Mhh, nani kuambia hayo..ok,…hapo kuna utata, ndio kuna mzazi alijifungua
siku hiyo, siku ambayo na mimi nilijifungua, lakini sio mfanyakazi mwenzao,
sasa hakuna uhakika wa moja kwa moja kuwa ndio yeye,..unaona hapo, na ni kweli,
kuna kipindi cha nyumba mume wako alikuwa karbu na huyo mama,…sasa huwezi
kuchukulia hilo kama kigezo, ndio maaana nasema kuna mambo kidogo
hayajakamilika hapo
‘ Ni nani huyo…Je huyo mzazi anaweza kuwa mpenzi wa mume wangu ,
ndio huyo shetani ninayemtafuta mimi au, nataka majibu hayo haraka
iwezekanavyo, umenisikia, ..?’ nikauliza kwa ukali kidogo
‘Bado sijaweza kupata uhakika, maana kama nilivyosema sio
mfanyakazi mwenzao…lakini sasa, huyo mwanamke ana mchumba wake,…nilitaka...niende
kwake,..lakini nimesikia kasafiri jana….ooh, hebu subiria kidogo,..’akasema na
kutuli baadae akasema
‘Kuna kitu nafuatilia, ….ujumbe uliingia, lakini sio muhimu,…sasa
ni hivi subiria kidogo,leo nahis nitafikia sehemu, nitakuambia …mambo mengine naogopa
kutumia watu, kwasababu za kiusalma na siri zetu, unanielewa hapo…’akasema
‘Ok….sawa, nimekuelewa,…mimi nakusubiria wewe…maana leo nilitakiwa kuonana
na baba, kuna mambo ya kuongea naye, muhimu sana..na nilipomueleza hayo
mabadiliko ya afya ya mume wangu, akaona tuahirishe hicho kikao, ..na kasema
kuna mambo zaidi kayagundua, sasa sijui ni mambo gani…’akasema
‘Kagundua nini, hakusema ni mambo gani hayo, mmh…?’ akauliza
‘Mimi kwa hivi sasa akili haipo sawa, siwezi kujua, hakusema….labda
yanaweza kuwa ya kazini kwa mume wangu au hata sijui, nahisi anaona namficha
jambo, kawa mkali sana..’nikasema.
‘Unajua baba yako nilionana naye, bahati nzuri sikuwa na mtoto, na
kukutana kwetu ilikuwa ni bahati mbaya tu, sio kwa kupanga ilitokea tu, nikiwa
nafuatilia jambo fulani nikiwa na haraka kurudi nyumbani, na hakutaka hata
kunisalimia, akakimbilia kuniuliza maswali ….’akasema
‘Maswali gani…?’ nikauliza
‘Kwanza alisema kwanini nimeamua kuzaa bila kuolewa,…nikamwambia
ni bahati mbaya tu,…akaniuliza haya baba wa mtoto ni nani, ..nikamwambia hilo
ni siri yangu,..akaniuliza mambo mengi-mengu tu mfululizo…, nahisi anajua
kitu….sijui kajulia wapi mambo mengi ambayo hata sikutagemea kuwa atayafahamu,…rafiki
yangu…, tusipokuwa makini, baba yako anaweza kuchukua hatua ambayo hukutarajia,
maana keshafahamu kila kitu…’akasema
‘Ndio maana nilikuambia ufanye juhudu za haraka, ili uwahi kuziba
sehemu zote nyeti, lakini wewe ukalichukulia taratibu, sijui ulijiamini nini,
ujue mimi nina mipaka yangu, na kama kuwajibika kama baya likitokea, sawa, nitawajibika kama
mtendaji, lakini huyo ni baba yangu hawezi kunitupa moja kwa moja lakini nyie
je nitawasaidiaje, na ina maana juhudi yangu yote ndio ifike hivyo, inaniumiza
sana, kama watu niliowategemea, na lakini sawa....’nikasema
‘Nimejitahidi nilivyoweza, nikaziba sehemu nyingi tu…lakini baba
yako kama umjuavyo anaweza kufika kokote bila vikwazo, hata
hivyo,..hawajafanikiwa kuupata uhakika wa baadhi ya mambo, ndio maana aliniuliza
maswali mengi, kuashiria kuwa hana uhakika,…unajua …mimi nimeshaamua, liwalo na
liwe, sasa nitafanyaje .…’akasema
‘Una maana kusema hivyo, liwalo na liwe…?’ nikauliza
‘Sasa rafiki yangu yaliyotendeka, yameshatendeka, utafanyaje sasa
hapo…eeh, hebu niambie, wakati mwingine tuangalie mbele, tukirudi kinyume nyume
kwa kujiuliza, tutajikuta tupo kwenye lawama sote …na lawama hizo zinaweza
kutufikisha kubaya, kama tutajiangalai nafsi zetu tu…na kumbe ilikuwa ni
dhamira nzuri tu..lakini sawa, mimi nitakukamilishai huo uchunguzi na uamuzi
utakuwa mikononi mwako…’akasema
‘Nataka kufahamu tu, je wao wameshagundua lolote kuhusu baba wa
mtoto, maana hilo linaweza kuleta picha mbaya kwangu,..kama..lisemwalo lipo
sijui nitauweka wapi uso wangu, lakini kama sio kweli..nataka kumkosha mume
wangu..awe huru na shutuma hizi..’nikasema
‘Kwani …mmh, mume wako si yupo, waache apone atasema mwenyewe,
kwanini ulaumiwe wewe…’akasema
‘Baba anasema kagundua mambo mengi ambayo kama angelifuatlia awali
yasingelitokea na hili limempa fundisho…sasa mimi sipendi hiyo hali ya kuingilia
mambo ya mume wangu, …ndio maana nilitaka ukweli kutoka kwako…na hilo la baba
wa mtoto wako, lisiwe kama wasemavyo, itakuwa heri sana kwangu, na kwa mume
wangu, vinginevyo, sijui baba atachukua hatua gani…’nikasema
‘Unajua hizo shuku shuku zao kuhusu mtoto kama nimezaa na nani…nimemwambia
baba yako wazi wazi hayo ni maisha yangu, hayawezi kuingiliana na biashara
zake, akifanya hivyo anakosea sana..kwani vyovyote iwavyo hakuna
nitakayemwambia baba wa mtoto wangu, na sina lawama na mtu, kuwa labda nitambebesha
yoyote majukumu ya ulezi, kwahiyo sipendi watu kuniuliza-uliza hayo maswali …’akasema
‘Sawa , kwa baba unaweza kuongea hivyo, lakini kila kauli yako
anaichukulia kwa uzito wake, maana naye sasa hivi keshasikia mengi, …mimi
nakupa angalizo tu, uwe makini sana ukiongea na baba, usimchukulie juu-juu, ana
lengo lake, unaweza ukajikuta kubaya sana, na anajua ni nini anachokifanya,
hawezi kuingilia mambo ya watu bila sababu maalumu…’nikasema
‘Namafahamu sana…najua ni vipi niongee naye, na wapi ikibidi na
mimi niwe mkali, maana na mimi nina haki zangu,kiukweli ndio baba yako ni
mkali, lakini mimi siwezi kumuogopa tu, ..ninachoogopa ni hatua zake, kuwa labda
anaweza kuchukua hatua mbaya zikaumiza wengine bila kujali, na visingizio vije
kwangu, hapana kama ni langu aniumize mimi mwenyewe….’akasema
‘Baba anachoangalia ni heshima yake, pili bishara zake, maana
heshima ndio inamletea wateja na biashara, na mambo ya kisiasa, hataki kashfa
mbaya …Na hilo litakuwa ndio ajenda kubwa kwenye hicho kikao, watakuwepo
wakurugenzi wote wa vitega uchumi ambavyo ana hisa navyo,…kwahiyo sio kikao
kidogo, ni kikao cha maamuzi,..sasa haya mambo ni mengi na yanatokea kipindi
hiki, na wewe ulikuwa msaada wangu mkubwa, sijui, umekuwaje sasa…’nikasema
‘Niliponana na baba yako, alikuwa na mdogo wa mume wako…’akasema
‘Oh yupo yule aliyesafiri au huyu mwingine….kwahiyo wameshaongea,
huenda kabanwa na kusema ukweli wote au…?’ nikauliza
‘Ndio, lakini huyo mtu nilishaongea naye kabla na kumuweka sawa,
sizani kama anaweza kufungua bakuli lake, nina mambo mengi yake mabaya
ninayoyafahamu, anajua kabisa akinisaliti nitamuumbua kwa mkewe.., kaahidi
hatasema loloye baya dhidi yangu, usiwe na wasiwasi na huyo mtu….’akasema
‘Una uhakika hataweza kusema ukweli, maana nilipanga kuonana na
mke wake…?’ nikauliza
‘Hawezi kusema chochote, …mambo yangu yatabakia kuwa yangu, nina
uhakika, hilo litabakia sirini kwangu, hakuna nitayakemuambia nimeshaamua
hivyo, mpaka hapo muda muafaka ukifika, , kama ikibid kusema, nitasema…, lakini
sizani kama kuna mtu atafahamu siri hiyo,..na unasema unataka kuongea na mke
wake unataka kuongea naye nini, …usije ukaharibu…’akasema
‘Hapana…kuna mambo yangu mengine na huyo mwanamke..mambo ya akina
mama, unajua nimewekeza huko pia, kwa akina mama, sasa yeye ni mmoja wa
wahusika wakuu, na nilitaka nijue yeye anasemaje kuhusu haya yanayoendelea hasa
kuhusu huyo mtoto wako,je hamshuku mumewe …’nikasema
‘Hata sijui….lakini kwangu nimehakikisha kila kitu kipo sawa,
…mimi nakushauri wewe hangaika na mume wako, haya mengine yaache kama
yalivyo,..hiyo taarifa itakusaidia kidogo tu…sizani kama ina lolote
jipya…’akasema
‘Unajua nilipokuwa naongea na docta, docta alisema mume wangu anaonekana
kama anataka kuonana na wewe…?’ nikasema,
nikahis kama kashtuka na akahema kidogo na kusema
‘Kuonan na mimi, aliongea hivyo au…?’ akauliza
‘Docta, rafiki wa mume wangu ndiye anahisi hivyo…’nikasema
‘Mhh, kuna nini kilitokea mpaka ahisi hivyo, lakini eeh, hata
hivyo ni wajibu wangu kumuona au sio , nyie ni kama ndugu zangu, tumeishi
nanyi, tumeleleana, shemeji namuona kama ndugu yangu pia, japo,…haya
yanayotokea sasa yanaleta kigugumizi, ila …sijui nitafikaje na mtoto,. Si
unajua tena, …’akasema
‘Wewe fanya mpango uje uonane na yeye, kama itasaidia,..huyo mtoto
isiwe kisingizio, huyo unaweza kuja naye…maana kutokana na docta kuna muda akiwa
anaweweseka, alitaja mtoto, kama ingelikuwa ni watoto wake, angelisema watoto,
lakini katamka ‘mtoto’…hizi ni hisia zinajengeka, na kumfanya docta ahisi
kitu…’nikasema
‘Mtoto, katamka hivyo mtoto, mtoto wa nini, hapana, labda kamsikia
vibaya, na hiyo sio sababu ya kuhisi mtoto wangu…sema kwa vile kuna kitu
kinatakiwa hapo, lakini hilo lisikusumbue kichwa, ni langu, najua jinsi gani ya
kupambana nalo…’akasema
‘Docta analifuatilia hilo kwa karibu na anajaribu kuwa karibu na
mume wangu, kusikia kama atapata chochote kutoka kwake…je hamjawahi kuonana na
docta ukiwa na mtoto wako…?’ nikamuuliza
‘Hajawahi, labda, ..sina uhakia maana huyu ndugu yangu anayekaa na
mtoto angeliniambia…kama aliwahi kuja nikiwa sipo, na mimi sijamuacha mtoto
wangu kwa muda mrefu na huyo msaidizi wangu…’akasema.
‘Unajua kila hatua, naanza kuingiwa na mashaka..anyway, mimi nina imani hujanificha
kitu,..sijui, maana, umeshasema huwezi kumuambia mtu kuhusu baba wa huyo mtoto
wako.., ikiwemo mimi, na kauli hiyo inanifanya nianza kuwaza mengi, ni kwanini
hadi mimi unifiche, najiuliza sana…’nikasema
‘Ndio maana naona bora iwe hivyo,…kama mwenyewe umeshaanza
kubadili imani yako kwangu, unaanza kupinga hata kauli zako, basi hata mimi
naingiwa na mashaka, je mimi rafiki yako naweza kufanya jambo kinyume na kauli
zako, aah, kwa hali hiyo, hata safari, sijui itakuwaje….na huenda nikaondoka
haraka iwezekanavyo…’akasema
‘Huwezi kuondoka kabla sijaufahamu ukweli. Ujue hiyo safari
nimeidhamini mimi mwenyewe, sasa usije kuharibu kila kitu…Hilo la kuujua ukweli,
nitalijua tu, nimeahidi hivyo…, umesikia, kupitia kwako au kwa njia nyingine,
nitamfahamu baba wa huyo mtoto, umesikia, na nina maana yangu kufanya hivyo…’nikasema.
‘Haah , sawa…lakini ….hebu kidogo…’ na simu ikakatika, nilishtuka
kwa kitendo hicho cha kukata simu kabla sijamalizana naye…, sio kawaida yake
kukata simu, kihivyo
Kwa vile nilikuwa na haraka, sikutaka kumpigia tena simu, …lakini
kitendo icho kilinikwanza kweli kweli….
***********
Nilifika hospitalini, na
nilihitajika kuonana na docta kwanza kama naruhusiwa kuonana na mume wangu.
‘Sawa unaweza kuonana naye, ila docta, jirani yako, yupo huko
anaongea naye… NA kumpatia mazoezi kuna huduma nyingine tunataka kumfanyia
kidogo huenda ikasaidia..’akasema
‘Kwahiyo sasa anaongea vizuri…?’ nikauliza
‘Ndio ila, kumbukumbu hazijakaa vyema kabisa…kuna muda
anajichanganya, na siku ya leo amekuwa akikuulizia wewe, ni mnyonge sana,
nahisi wewe utaweza kumsaidia, jaribu sana kuwa naye karibu…’akasema
‘Haya ngoja nikaonane naye, kwahiyo unahisi ana tatizo jingine
kubwa…’nikauliza nikiwa na hamasa ya kwenda kuonana na mume wangu.
‘Hakuna zaidi ni hilo, …mengine hatuwezi kuyafahamu kwa sasa,
maana hatua kwa hatua anaanza kuimarika, usiwe na wasiwasi kabisa…’akasema
Basi nikaondoka na kuelelea
huko alipolazwa mgonjwa, nilipoingia nilimkuta docta akimfanyia mume wangu
mazoezi, nilishangaa kuona hata ile kukaa kama kwanza hawezi, …sikutaka
kuwashtua kwanza nikatulia kuwaangalia.
‘Sasa naona upo tayari,…unajua ni muhimu ukajitahidi mwenyewe
ungelifanya kama ulivyojitahid kipindi kile ungelipona haraka tu…’akasema docta
‘Hata sijui ilikuwaje, kwani nilijitahidi vipi…?’ akaliza suti
yake ilikuwa ya kinyonge ya mgonjwa aliyekata tamaa.
‘Uliweza kukaa mwenyewe kitandani…’akasema
‘Mimi, nilikaa mwenyewe, ….sikumbuki. maana hata mwili siuhisi ni
kama vile sina mwili kabisa….’akasema
‘Utakumbuka tu kidogo kidogo,…’akasema docta
‘Hivi unasema kweli ..kuwa Mke wangu aliwahi kuja kuniona, mbona
mimi sikumbuki kumuona…’akasema
‘Mbona kila siku anakuja kukuona…’akasema docta
‘Mmhh, kweli nahisi hataki kuja kuniona kwa hayo niliyomtendea,
nimemkosea sana, sijui kwanini, nahisi mimi ni mtu mbaya sana, na huyo rafiki
yake mhh…’akasema hapo akatulia hakuendeleza neno
‘Usijali,..kosa ni kosa, na ukikosa, ukatubu basi kosa linafutika,
ila ukirudia kosa, ujue wewe ni mkosaji…’docta akasema
‘Nimerudia kosa mara nyingi sana..ndio maana nipo hivi…sijui
atanisamehe kabla hajchelewa… unahisi atanisamehe, nataka nafsi yangu iwe huru,
nina imani akinisamehe, basi, nitapumzika kwa amani, atakuja leo…?’ akauliza
‘Atakusamehe, kwani hujafanya kosa kubwa la yeye kushindwa
kukusamehe, makosa ni kawaida ya mwanadamu au sio…’akasema docta
‘Wewe hujui tu…nahisi moyo mwake ananichukia sana, tena sana,
sijui kwanini ilitokea hivyo, lakini, hata sijui, nilifanya nini…’akasema
‘Kwani anafahamu kosa ulilomtendea, ni kosa gani kubwa hivyo..?’
akaulizwa
‘Ndio maana hataki kuja kuniona, nahisi keshafahamu, ni kosa kubwa
sana, tena sana, lakini sikumbuki, tatizo, nahisi nimekosa, lakini haaa, mbona
sikumbuki kitu…’akasema
‘Kosa gani…lakini utakumbuka tu usijali…si hukumbuki, basi ni kosa
dogo tu, au sio..au unalikumbuka, ni kosa gani…?’ akauliza na hapo akageuka,
wakaniona, na kimia kikatawala.
Mume wangu aliponiona
akaonekana kutokuwa na raha, akawa katulia, nikamsalimia, akaitikia kwa unyonge
sana, nikamuuliza anaendeleaje akasema sasa hajambo.
‘Sasa ni kujitahidi kula na mazoezi, na nitajitahid kuja
kukufanyisha mazoezi mwenyewe, maana walinikataza awali, sasa najua upo tayari,
au sio..?’ nikamuuliza
‘Sawa, lakini ..ulishanisamehe…’akasema hivyo
‘Kukusamehe, mume wangu usiwe na wasiwasi mimi ni mke wako,
tunakoseana sana, au sio, kwani wewe si ulishasamehe au sio..’nikasema
‘Lakini wewe hujanikosea kitu mke wangu, wewe ni mke mwema,
nimeliona hilo, wewe ni mwema,…’akasema
‘Mh, mume wangu nimeshakusamehe kabisa…’nikasema, nikimtupia jicho
docta na docta akaashiria kukubaliana na kauli yangu japokuwa sikufahamu ni
kosa gani analolisemea mume wangu.
‘Najua hujanisamehe, niona nafsi yako…unanichukia sana, nakuomba
uondoke tu, kama hutaki kunisamehe…’akasema na kunifanya nishtuke na kugeuka
kumuangalia rafiki yake.
Docta..alipoona vile..kwanza alitulia, kama ananisubiria mimi niseme
neno la kumsihi au kitu kama hicho, na aliponiona nipo kimiya
yeye akamsogelea mume wangu pale alipolala, akamwiinamia na akawa
anamsemesha sauti ya chini-chini
‘Rafiki yangu nimeshakuambia, ukitaka usipone haraka, uendelee
kujitesa na hayo mawazo yako, mke wako hana kinyongo na wewe kabisa,….
anafahamu kuwa kila binadamu anakosea, na kutenda kosa sio kosa, bali kurejea
kosa, wewe kama uliteleza, uliteleza tu kama binadamu wengine,..na umeshafahamu
kosa lako, umetubu, au sio ...hiyo inatosha kabisa..mimi nimeshaongea na mke
wako, yeye kasema ameshakusamehe.....’akasema.
‘Wewe huelewi tu, .....ninachotaka ni kauli ya mke wangu kuwa
amekubali kunisamehe, kutoka moyoni mwake, nafsi yake bado haijanisamehe,
naiona kabisa, usimsemee…’akasema
‘Nafsi yake umeuonaje wewe…’akasema docta
‘Naiona,…naiona, naiona. Naiona…’akawa anaongea hivyo mfulululiza
mpaka docta akamgusa begani ndio akanyamyaza
‘Mimi najua tu, mimi ni mtu wa kuangamia tu, maana hajanisamehe,
ninajua mimi sio mtu kuishi tena, nimepewa muda wa toba, kabla sijafa, niwe
nimesamahewa, na mke wangu, lakini mke wangu, hajanisamehe, anaongea tu
mdomoni, yeye na baba yake ni kitu kimoja, wanataka niangamie tu,, ....’akasema
na kauli hiyo ikanishitua, nikajikuta nikisema.
‘Wewe mume wangu unakazania nikusamehe, nikusamehe, kwa kosa gani,mume wangu mbona hujanikosea
kitu, kama ni yale ya nyumba nimeshakusamehe, lakini sijui kama una makosa
mengine,labda uniambia makosa gani hayo,na hilo la baba yangu linatoka wapi,,,.?’
nikauliza na rafiki yake akasema.
‘Tulishaongea hilo na mke wako, kwake sio kosa kubwa sana, ni
mambo yanatokea, hasa kwa wanadamu, baba yake alikuja hapa akasema yeye yupo
tayari kuangalia unapona haraka, na kama kuna lolote limekwama aambiwe, sasa
unataka nini tena..’akasema docta
‘Baba yake au mwingine….hahaha, na akisikia hayo madhambi, si
ndio, atanifukuza kabisa,…najua keshayafahamu ila anasubiria kuwa nitapona ili
aje kuniumbua, hatawahi kabisa, ila mke wangu, nisamahe jamani, naangamia mwenzako…’akasema
kwa sauti ya uchungu kama anataka kulia.
‘Kiukweli pale nilitaka kuongea kwa ghadhabu, maana sijui ni kosa
gani, na nimetamka kuwa nimeshamsamehe bado ananisihi, …docta akaingilia kati
na kusema
‘Mkeo anakupenda sana, muda wote yupo na wewe, kaacha kila kitu
kwa ajili yako, sasa unataka nini tena hapo, keshakuelewa, muhimi ni wewe
kupona hayo ya kufikiria kufa , kila mtu atakufa hata akiwa mnzima au sio....’akasema
docta na kunigeuka akaniambia kwa sauti chini chini
‘Toa kauli yenye udhabito kuwa umemsamehe, umeshafahamu kila
kitu,..tusipoteze muda, kwani hali yake, itaboreka haraka akiwa na moyo wa
matumaini,..vinginevyo,…huyu mtu atachanganyikiwa… ‘akatulia kwani dakitari
wawili na nesi waliingia wakiwa na vifaa, vikiwemo vyuma, nikashangaa hivyo
vyuma vya nini tena .
NB: Mambo ndio hayo, msichoke, maana hapo hospitali ndio
tutagundua mengi.
WAZO LA LEO:Fadhila , baraka na rhema kutoka kwa mola
wetu ni nyingi sana, je tunazikumbuka, je tunamshukuru, au tunasubiria mpaka
tuanza kuwa na hali mbaya ndio tuanze kusema ‘ooh mungu wangu…. tumkumbuke mola
wetu tukiwa wazima, tukiwa na uwezo wetu, tukiwa vijana, ..naye atatukumbuka
tukiwa na shida.
Tumuombe mola wetu tuwe na imani hiyo, Aamin.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment