Kama nilivyokwisha kusema awali, rafiki yangu tulishibana sana, na
tulijaliana sana, na hakuna angelipenda kufanya jambo kwa mwenzake ila liwe la
heri na lisiwe la kumkwanza mwingine, tulichunga sana hilo, tokea tulipokuwa na
akili…kwa hali hiyo tulichunga mipaka yetu kuhakikisha hatukwazani.
Na kwa upande wa mume wangu alikuwa mpole sana, hakupenda makuu,
hakuwa na tabia mbaya , hakuwa mlevi, kuvuta sigara, au tabia za uhuni-uhuni,
na alinijali sana na kuijali ndoa yake. Sikuwa na wasiwasi kabisa na mume wangu, na
usingeliweza kunidanganya kitu kuhusu mume wangu…na yeye hakupenda kufanya
jambo linaloweza kunikera mimi au familia yake, alichunga sana hilo, ni mume wa
pekee..ndio maana hata rafiki yangu alimuheshimu sana
‘Mume wako namuheshimu kama mkwe, nampenda sana kwa tabia yake, yaonyesha kabisa
hana tamaa, au tabia mbaya, na wanaume wa namna hii ni wachache saa,..unajua nikimuona
mahali natamani asinione, sipendi, hali ya kuwa naye faragha, japokuwa
ananisalimia vyema tu…na kuna kipindi ananialika chakula cha mchana, namkatalia
‘Kwanini unafanya hivyo, huoni atakufikiria vibaya, huyo ni
shemeji yako, si zani kama mnaweza kufanya lolote baya…?’ nikamuliza rafiki
yangu siku moja kipindi hicho nina uja uzito.
‘Hapana sitaki watu waje kusema lolote dhidi yetu, najua watu
wanaweza kujenga fitina na urafiki wetu ukaja kuleta madoa, nachunga sana hilo…sisi
tumetoka mbali,..na kama tulivyowahi kuambizana, muhimu ni kuchunga yale yote yanayoweza kuvuruga urafiki wetu,
sitakufanyia chochote kibaya, nikijua kitakuja kukuumiza, ni bora nikafanye kwa
wengine na sio kwako…’akasema
‘Usijali, mimi na wewe..sina shaka kwa hilo….mimi nafahamu hata
kama itatokea mkalala chumba kimoja na mume wangu bado nina imani kuwa hutawezi
kunisaliti, hahaha.’nikasema tukacheka.
‘Ni kweli…hahaha eti tulale chumba kimoja ina maana vyumba vya
wageni havipo, tusifikie huko ..pa kujaribiana…’akasema
Mimi na rafiki yangu ilikuwa hivyo…
Nayaweka haya bayana kwanza,
ili uone tulivyokuwa tumeshibana na huyo rafiki yangu, kwahiyo kwa kutoa kwangu
ushauri kama ule.., sikuwa nina mashaka yoyote na yeye, maana wengine watasema
kwanini, ukamshauri mwenzako hivyo, wakati una mume, kwanini sikumshuku vibaya…na
najua itakuwa hivyo…. aah, nilimshauri
rafiki yangu nikijua atafanya kile ambacho hakiwezi kuniumiza na atafanikiwa na
hatimaye na yeye atakuwa na furaha,…
‘Sasa nilimshauri nini, hebu sikia ushauri wangu….
Tuendelee na kisa chetu…
*************
‘Kama ni hivyo, mimi sioni kwamba kuna tatizo, kwanza wewe tayari
ni mzoefu wa wanaume,…mimi sijawahi kuwa na mahusiano yoyote zaidi ya huyo mume
wangu, kwahiyo kwako, sioni kama ni tatizo, au…?’ nikamuuliza, baada ya mume
wangu kuondoka,…
Mume wangu alipofika tulikatisha mazungumzo, hakukaa sana, alisema
alikuja mara moja, kuna sehemu anakwenda mara moja…
‘Ugumu unakujaje …nataka mtoto ambaye ana sura ninayoitamani mimi,
..yaani ninachowazia, sio ilimradi tu kupata mtoto, ukichagua nyama, chagua
iliyonona, au sio, ….unajua sitaki kukufuru, ila kwa vile nimeamua hivyo, basi
kiwe kile kitakachonisuuza moyo wangu….’akasema.
‘Wewe cha muhimu si ni kupata mtoto, hujali tena cha ndoa, au sio..hapo
uwe na uhakika,..usije kusema aaha rafiki yangu, kanichuuza…kama ni hivyo, …,
basi zaa kwanza na mwanaume yoyote…ningependa kukushauri hivyo…’nikasema na
kumkagua usoni.
‘Hapana ….sio hivyo…’akasema.
‘Sio hivyo kwa vipi tena, kwani unataka akuoe,….au wewe
watakaje…mimi nilionea hivyo, wewe uzae kwanza na yoyote yule… , huku
ukiendelea kusubiria kama utapata mwanaume chagua lako ambaye ataweza kukuoa, lakini
huku ushapata mtoto wako ili kutokuingia kwenye umri hatari hujazaa..…unaona
hapo, hata akiolewa umeshafikia huo umri, huna haja ya kuzaa tena maana unaye mtoto
tayari unaona hilo wazo langu lilivyokaa...’nikamwambia na yeye akaniangalia sasa
kwa uso uliojaa hamasa.
‘Hapo sasa nimekuelewa, hivi kweli hilo inawezekana kirahisi hivyo…?’ akauliza
‘Kwanini isiwezekane, hahaha, wewe ni mjanja bwana, usitake
kunifanya kwua mimi sikufahamu, …’nikasema.
‘Mhh, kunifahamu unanifahamu lakini sivyo kama nitakavyo
mimi….’akasema
‘Unatakaje…?’ nikamuuliza
‘Kwanza niambie, kwa vipi hapo, maana nilitaka nizae ndani ya
ndoa,..huo ndio ukweli wangu, sasa ndoa imegoma, hivi sasa tunashauriana
kuwa ni zae tu hata nje ya ndoa…si hivyo…?’
akaniuliza
‘Hilo ni jibu lipigie mstari, au…?’ nikasema na kumuuliza
‘Mmhh, hapo kwangu bado pagumu kweli kweli,…isingelikuwa hoja hiyo
ya kuchelewa kwa umri, nsingelijali sana, isingelikuwa ….aah, hapana mimi
nataka mtoto, kwa vyovyote vile…lakini sipendi maana hapo nitakuwa
nimekiuka kiapo changu,…nitakuwa msaliti wa ahadi yengu mwenyewe..unajua , niliapa
mimi sitazaa nje ya ndoa, sasa nifanyeje mungu wangu,..?’ akaniuliza.
‘Hili si unalifanya kwasababu, hii tuichukue kama dharura, maana ….
umri umekwenda, au sio, unaogopa utafikia kikomo kabla hujapata mtoto, hiyo si
dharura, au sio…. basi wewe cha kufanya ni kutembea na mwanaume yoyote, …mimi
hapo nasema ‘yo-yo-te’ sijui kwako
wewe….maana mtoto ni mtoto au sio, kwa mzazi kama mimi…’nikasema
‘Ha-pa-na sio kwa yoyote, hilo hapo natofautiana na wewe kidogo,
tuliweke sawa hilo, ..maana yoyote atanizalia mtoto yoyote, hapana, mimi nataka
yule atakayenipatia nikitakacho, moyo unapenda, unaona hapo, tuliangalia
kihivyo, mimi naona hapo turekebishe kidogo....’akasema.
‘Mpaka hapo tunakwenda sawa, siwezi kukukatilia hivyo uakavyo, ila
wasiwasi ni kuwa ukianza kumtafuta umtakaye inaweza ikachukua muda tena,…na
hujui ya kesho au sio….’nikasema
'Mhhh…hapo sasa, unaleta ugumu , mimi kama nimeamua kula haramu,
basi acaha nile haramu haswaa…unielewe hapo, sitaki nile haramu halafu nisikie
kichefu chefu, hapama, nataka mume anipatie mtoto ninayempenda….’akasema
‘Wewe ndio unaleta ugumu, unarudi kule pa kuchagua
chagua..mwishowe siku zinakwenda, …’nikasema
‘Hapana si ndio tunawekana sawa, tukishakubaliana hilo, kuwa
nataka mume atakaye nizalia mtoto ni nimpendaye,…hapo tutaingia kuangalia ni
nani…unajua pamoja na yote mimi najali sana mtoto wangu aweje, naanza kuangalia
sasa…nisije kujitia baadaye…mtoto awe na sura , tabia, maumbile…ninayoyatamani
mimi, eeh, hapo hapo tufanyeje ..’akawa kama anaota au kujenga taswira fulani
akilini
‘Aaah, unajua kwangu mimi kama mzazi mtoto ni mtoto tu…hayo ya
sura, sijui nini, hayo ni wewe ambaye hujabahatika kuzaa, …mmh, na wewe kwa
kuchagua, unachagua mpaka maumbile ya mwenyezimungu, usikufuru kihivyo,….’nikasema
‘We-we..unasema mtoto ni mtoto tu, ina maana mimi kuchukua dhima
hiyo basi nijizalie tu,… hapana..ni lazima nifanye jambo nije kulifurahia
mwenyewe, sitaki nije kujutia baadae,.. najua nimetenda dhambi, tena ya
kudhamiria,…sasa nije kupata adhabu hivi hivi tu, mungu anisamehe tu, sipendi
hili jamani,…sasa mimi nitakavyo nikipate nikitakacho,..nizae mtoto nikimuangalia
hivi eeh , moyo unasuuzika na wala nisije
kujijutia…’akasema
‘Oh, mungu wangu , hapo sio dharura tena,..ni dhamira mbaya,..hebu
niambie kwahiyo wewe unatakaje…?’ nikamuuliza
‘Ninataka huyu mwanaume akinipa mimba, nizae mtoto mwenye sura
nzuri, umbo nzuri, maana na mtoto anarithi tabia, basi awe na tabia nzuri
kutoka kwa baba yake,…na hata mimi nikimuona huyo mtoto ninafurahi mwenyewe…’akasema akitabasamu sio kama
alivyokuwa awali, sasa uso umeshaanza kunawiri na urembo wake ukawa bayana,
kiukweli rafki yangu ni mrembo, sijui kwanini kapata bahati hiyo mbaya ya
kutokuelewa.
‘Mhh, ….haya, kama utakavyo ni hivyo, basi twende hivyo hivyo,
nikubaliane na wewe, na lile wazo langu la mwanaume yoyoete tuliondoe, sawa,
twende sasa,…kwahiyo inabidi hapo uchague mwanaume sasa kama ni hivyo mbona
ulikosa wa kukuoa, maana usione ni rahisi kumpata atakayekidhi viwango vyote,
ndoa inajengwa na wawili na ndiyo inazaa chema..’nikasema
‘Ndio hapo unisaidie, wewe ushaingia kwenye ndoa, ..na najua
vyovyote iwavyo, mtoto huwa anatokana na damu ya wazazi wake, hata tabia,
uziri, umbile ndio basi tena…nisaidie kwa hapo…’akasema
‘Unajua wewe unanitwika mzigo ambao mimi sina tabia nao…mimi sijui
kuchagua chagua kihivyo, najua chema ukimuomba mungu atakupatia, sio mpaka
nianza kuchagua tu..kama nguo,..hapa hatuzungumizii nguo, tunazungumzia mtu, na
mtu huletwa na utashi, wa muumbaji, ..sio kweli kuwa unaweza kumpata mume
akakupatia hichoukitakacho…’nikasema
‘Rafiki yangu tuangalia uhalisia, hili ulilonishauri, la kuzaa
eeh, hata nje ndoa, ni uhalisia, pia linaendana na maumbile, ..tusikwepe ukweli
hapa…’akasema
‘Ok, sawa nimekuelewa…..’nikasema
‘Sasa tuseme tumeshakubaliana huyo mwanaume aweje, ..eeh,awe
nitakavyo mimi, kazi inakuja , nitamuanzaje, kuwa nataka unipe mimba, au nataka…inakuwa
kama nauza mwili wangu..huoni hapo najizalilisha…’akasema
‘Hilo rafiki yangu utaanzaje, mimi siwezi kujua, najua wanaume
wakiona ishara fulani wanajua huyo mwanamke anataka kitu..kapenda, tatizo ni
huyo mwanaume uliyemchagua je…ana tabia hiyo,…’nikasema
‘Unajua kuna kitu nikuambia ukweli rafiki yangu, pamoja na ya kuwa
hawataki kunioa,..lakini nimegundua kitu, wanaume wengi wananiangalia kwa
matamanio,..wengine wananitongoza, tatizo ni hilo wengi wao, wanachotaka ni
mwili wangu, na wengi wao sijawapenda…sasa hapo, nifanyeje….?' akasema.
‘Unajua pamoja nakushauri hivyo, bado mimi silipendi hilo
wazo,…lakini pia nakuona kweli umri umekwenda, na wanaume ndio hao, …mikosi,
sijui tuite hivyo, au ndio huko kuchagua kwako kumefikia…’nikasema
‘Tusirudi huko, tutashindwa kufikia muafaka,…najua mungu
anakuadhibu, kwa kasumba yangu hiyo, sawa….’akasema
‘Hapana usifikirie hivyo….mimi bado nilikuwa na imani kuwa muda
bado upo,…lakini mtoto kweli ana umuhimu wake, cha kufanya mtafaute huyo
unayempenda, mengine utajua mwenyewe cha kufanya, usitake mimi nikutanue kila
kitu...’ nikasema na hapo akanikazia macho kwa kushangaa.
‘Nimtafute yoyote ninaye mpenda, bila kujali,…aah ina maana
unanishauri hivyo, yoyote ninayempenda, …mmh, hapo sasa ndio naanza kuogopa,
maana,….sijui sijui..nifanyeje rafiki yangu…?’ akaniuliza
' Wewe wazo lako si kuzaa tu na mwanaume yeyote unayeona
atakuwezesha kupata mtoto mwenye sura unayoipenda wewe, si ndio hivyo naona
hata `wadhungu’ wanafanya hivyo, wanaingia kwenye mitandao, wanaandika
wakitakacho kuna mawakala wanakutafutia, sasa huku hakuna, ila wewe unaweza
kutafuta mwenyewe,....na kwako wewe sizani kama itakuwa ni ngumu kihivyo, wewe
mwenyewe unajifanya u mzungu, unaishi kizungu-zungu, matawi ya juu, kwanini
kitu kidogo kama hicho kikushinde, haikuwa na haja ya kuja kuniuliza hayo
yote.., au sio, mtafute unayempenda uzae naye...kwa siri…unielewe hapo…'hatimaye
nikamshauri hivyo rafiki yangu.
‘Sasa nikufuchulia ukweli,..sikuwa na wazo hilo kabisa, maana
naogopa sana, ila uliponishauri hivyo wewe rafiki yangu kuwa naweza ..sas
anikuambie ukweli, wengi ninaowapenda, kama mungu angenijalia, …wengi ninao ona
wanaweza kunipatia mtoto nimtakaje ni waume za watu, ndio hapo naogopa sana.…’nikasema
‘Oh waume za watu ina maana hakuna mwanaume mwingine ambaye hajaoa,
hapo uanishangaza, waume wapo wengi, wana umbile, sura nzuri, kwanini ushindwe
kuwapata, mimi hapo sioni kuwa ni tatizo …’nikasema
‘Ni tatizo,..maana ni waume za watu, ndio sana nawapenda, ndio
sana nikiangalia watoto wao nasema hata mimi nataka mtoto kama yule, nina
ushahidi wa kizazi chao, hawa ambao hawajazaa, sina ushahidi nao, ndio maana
naingiwa na mashaka nao, uone wazo langu lilivyo, hao, nawa-penda, sio
kuwa….unielewe, sio kwamba nina nia mbaya nao, lakini ndio najua wataweza
kunizalia kile nikitakacho na nina uhakika nacho..…’akasema
‘Mhh, rafiki yangu utavuruga ndoa za watu, ….’nikasema
‘Sasa mbona unaharibu, unanitisha, basi tuache….’akasema
‘Sio nakutisha, nawazia mbali unajua…’nikasema
‘Kiukweli mimi sipendi
kuvuruga ndoa za watu…yaani sijui kwanini, sijawahi kumuona wa kumpenda ninayevutika
naye, ambaye nahisi nikizaa naye nitapata mtoto mwenye sura na umbile
nilipendalo ambaye hajaoa,…huo ndio ukweli..nakuambia ukweli kwa vile wewe ni
rafiki yangu,… sijawahi kumuona, nimezunguka nimeangaza huku na kule hakuna,....ninao
waona na kuwapenda wengi ni waume za
watu...sijui kwanini inanitokea hivyo,…’akaniambia.
‘Sawa mimi nimekuelewa sana, mimi sioni tatizo, kwa vile hutarajii
kuishi na huyo mwanaume, ..nikuuliza hapo, kwani wewe najali nini sasa maana
sasa unataka nikufundishe kila kitu, kwanza ninataka unihakikishie kuwa lengo
lako sio kuvunja ndoa ya watu, ni kuzaa tu, na kuzaa huko kuwe ni siri
yako…usije kuniingiza kwenye lawama ya kuvunja ndoa za watu, mimi sipo….’ nikasema
‘Ndio hivyo….’akasema
‘Na pili wewe unataka mwanaume salama asiye kuwa na tatizo, nahisi
nimekuelewa hivyo…na unahisi kuwa wao watakuwa na tabia nzuri, sasa kama
anakubali kutembea nje ya ndoa, mimi naingiwa na walakini na tabia hiyo, lakini
wewe utakua jinsi gani ya kumshawishi , maana wanaume hata aweje, ukimfikisha
mahali sizani kama anaweza kurudi nyuma….’ nikamwambia.
‘Mhh, hapo kuna mawili, nimuambia lengo langu au nimfiche lengo
langu, mimi sitaki iwe hivyo, unaona hapo, nataka iwe siri ili sije kuvuruga
ndoa au sio, nionavyo mimi,…haaah…. unajua umenitia hamasa kwa wazo lako,
nimelipenda, japokuwa sipendi kutembea na mume wa mtu,…kwani nitakuwa nimevunja
ahadi yangu nyingine kubwa , tena kubwa sana…’akasema
‘Ahadi gani…?’ nikamuuliza
‘Ahadi ya kuwa sitatembea na mume wa mtu, vinginevyo aje kunioa…’akasema
‘Nimeshakuambia uichukulie hiyo kama dharura tu, ikipita basi
isahau kabisa, msahau huyo mwanaume na usahau kile kitu, usije kunogewa ikawa
ndio basi tena…’nikasema
‘Mhh, hapo nipagumu, kutembea na waume za watu na huenda awe ni
mume wa rafiki yangu, hapana mimi nawaheshimu
sana marafiki zangu....hilo mimi naliona tuliache tu, sio wazo zuri, na kumpata ...ambaye atanipatia
mtoto nimtakaye inakuwa ngumu, ninaowapenda zaidi ni waume za marafiki zangu,
mmh, mimi naona mungu kapanga iwe hivyo, tuliache …..’akasema.
‘Wewe usijali, ukimpata huyo mwanaume, hata kama ni mume wa mtu, tembea
naye bila kumwambia kitu, hakikisha umelenga zile tarehe…., nia na lengo ni akupe
uja uzito, mkishamalizana, unaachana naye kabisa…., na fanya hivyo ukiona kweli
mimba imeingia,…maana yawezekana ukajaribu mara ya kwanza isiingie…’nikasema
‘Hapo sasa si ndio nitaanza kujenga mazoea…’akasema
‘Hapana, akili yako iswe kumchukua mume wa mtu,…mimi nina imani
hiyo mara ya kwanza inaweza kuleta matunda,..ukishamalizana naye, achana naye, usiwe na mawasiliano naye tena, achana naye
kabisa mpige marufuku kukufuata fuata tena….mimi naona iwe hivyo.,…’nikamsahauri
hivyo.
‘Hiyo ni kazi kubwa, maana hapo natakiwa nitongoze mwanaume wa
matu, wakati siku zote natongozwa mimi, nitamuanzaje huyo mwanaume, tena
mwanaume wa mtu tena labda awe ni mume wa marafiki zangu,…’akaangalia juu
akiwanza.
‘Mwanaume ukimuonyeshea ishara tu wao wanajua, na wewe bado mrembo
unavutia, sizani kama hilo litakuwa tatizo kwako, mimi sioni kama ni tatizo,
ndio inauma, na sijui, jitahidi umalizane na hilo usahau, mimi naona ufanye
hivyo. Maana sasa unaniingiza kwenye kuchagua chagua……’nikasema
‘ Sio hivyo, ..hapa tunapanga kitu chenye uhakika,….maana hapo unazungumzia mume wa mtu ninayemfahamu ,maana
ili niwe na uhakika inabidi awe ni mwanaume ninayemfahamu, si ndio hivyo,..ambaye
natamani anizalie watoto kama ….unaona inakuwa ngumu, nitakuja kumuangaliaje
huyo rafiki yangu, ndio maana nikasema hili wazo sio zuri, naona tuliache tu...’akatulia
kidogo.
‘Wewe unajali nini kwani unaondoka na huyo bwana..hahaha, naona
unanifanya na mimi niwazie mambo niliyokuwa sinayo kichwani mwangu, wewe kama
lengo lako ni mtoto na ni kweli umri ndio huo,… fanya hivyo, na iwe siri yetu
wawili tu..,usije kumuambia mtu kuwa mimi nilikushauri hivyo….sitaki..’nikasema
huku nikicheka.
‘Mhh, unajua ni rahisi kusema, lakini kwenye kutenda ni kugumu,
maana ni kweli watoto wa marafiki zangu nawapenda sana, na natamani
niwapate kama hao hao....hapo ndipo naona ugumu, kuwasaliti marafiki zangu,
wewe huoni hapo inaweza kuleta shida baadaye, wanaweza wakaja kugundua, urafiki
utageuka kuwa ni uadui, sipendi kukosana na marafiki zangu....mmh, ngoja
nifikirie huo ushauri wako…’akaniambia.
‘Sio swala la kufikiria sasa rafiki yangu, …hapo ni swala la kulifanyia
kazi, sizani kama itakuwa ni ngumu kwako, wewe ni mrembo bwana, nashangaa kwanini
hujaolewa, kila mtu anakushangaa mrembo kama wewe huna mume...’nikamwambia.
‘Kila mtu ananishangaa, basi anipatie mume wake,, waache wafikiria
watakavyo, mimi hilo sijali kabisa..maisha yangu hayawahusu....kwangu mimi hilo
la watu kiukweli ninachohofia kwasasa, nisije nikafikia umri ambao hautakiwi
kuzaa tena, sijapata mtoto, yaani hilo
ndilo tatizo kwangu si vinginevyo....’akaniambia.
‘Kama ni hivyo , basi fuata ushauri wangu, na wala usipoteze muda,
kama waume za watu ndio unaowatamani, ndio watakao kupatia mtoto unayemtamani,
basi hao wapo wengi, ila chunga sana, ....’nikamwambia
‘Nichunge nini tena, unanikatisha tamaa…?’ akauliza akiniangalia
kwa mshangao.
‘Kuna waume wana wake zao ni wakorofi, wakija kugundua wanaweza
kukuharibu hiyo sura yako, tafuta waume ambao wake zao ni wastaarabu, ...na iwe
siri yako, usimwambia yoyote...haya,usipoteze muda tena kalifanyie kazii hilo…’nikamshauri.
‘Sawa rafiki yangu, maana umenipa wazo ambalo sikuwa nalo kichwani
kabisa...kiukweli naogopa sana, waume za watu...bado naogopa....kutembea na
mume wa mtu, na mbaya zaidi awe ni mume wa rafiki ninamyemuheshimu sana
..naogopa sana... hapana hiyo sio tabia yangu, itakuwa ni mara ya kwanza
kutembea na mume wa mtu...’akasema.
Rafiki yangu alitulia kwa muda, nadhani alikuwa akiwaza
jinsi gani atakavyotembea na huyo mume wa mtu, na wakishamaliza, jinsi
gani atakavyojisikia vibaya, na kama kweli huyo mwanaume ni muungwana na yeye
atabakia akiwa anajutia....nikamtoa kwenye mawazo hayo na kusema;
‘Shauri lako kama na hilo nalo ni mpaka uchague chague kama nazi
endelea kufanya hivyo, hilo halina kuchagua tena hapo, maana mwenyewe
umeshasema kuwa waume za watu wapo wengi unaowapenda, na umeshaona watoto wao
au sio, sasa watakaje, nikuchagulie mimi au..?’ nikamuuliza
‘Hapana, umeshanipa njia inatosha…na kiukweli marafiki zangu wote
nawafahamu watoto wao, nafahamu yupi ni yupi anafaa, nitachagua mmojawapo, au
sio..?’ akaniuliza
‘Ndio hivyo, chagua yoyote
atakayekukidhi matakwa yako, sizani kama hilo ni tatizo kwako, au…?’
nikamuuliza
‘Sijui kama ni tatizo, maana sio kawaida yangu, lakini nitajaribu,
maana wengi, nawaoana wakinitizama kwa jicho la kunitamani, kwahiyo..sawa,
natumai sitaharibu kitu, ngoja nione itakavyokuwa, nashukuru sana rafiki yangu,
kwa kunijali,..wewe ndiye rafiki wa kweli, hilo wazo limekaa vyema japokuwa
..mmh…’akasema
‘Usijali,..sasa kazi ni kwako wewe ushawajua ni nani anakuvutia
zaidi, mweka kwenye anga zako, tembea
naye,hakuna atakayejua...wewe mjanja bwana, hilo lifanyie kazi, haraka
iwezekanavyo, kabla mambo hayajabanika..’nikamwambia na yeye akataka kuondoka
‘Mbona huwaagi watoto , …naona wazo hilo limekuhamasisha
sana…’nikasema
‘Oh, yaani we acha tu,….’akasema na kuwafuata watoto kule
wanapojisomea, na kuwa-aga…wakamsindikiza hadi mlangoni… , na alipofika mbele
kidogo, akageuka na kuwaangalia ,
akatabasamu na kuwapungia mkono na huyoo, akaondoka zake….
‘Mlikuwa mnajadili nini….?’ Ilikuwa sauti ya mume wangu ilinishtua
kwakweli… sikujua bado yupo, maana aliaga kuwa anaondoka!
Nb, mkuki ukachongwa, tayari kwa kumchoma nguruwe......
WAZO LA LEO:
Wengi twachukulia rahisi tu kuongea, kutamka neno, vyovyote akili zetu
zitakavyotutuma, tukumbuke kuwa kila neno lina thamani yake inaweza kuwa mbaya
au nzuri... Neno dogo tu laweza kuzua sintofahamu, likajenga chuki, likaumiza,
na hata kubomoa kile ulichoanza kujenga…rafiki wa leo anaweza kuwa adui mkubwa
wa kesho, sababu tu ya kauli.. , kauli zaweza hata kuua.
Wachamungu wa kweli
wametuasa kuwa ni bora kufunga mdomo wako, ukauzuia ulimi wako, ili kujiepusha
na mtihani wa ulimi.
Najiusia mimi mwenyewe na kuwausia wenzangu, tuweni makini sana na
kauli zetu, tuchunge sana ndimi zetu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment