Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, October 11, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-4



 Baada ya kuutoa ushauri kwa rafiki yangu, kukapita kipindi cha pilika pilika nyingi, mambo yakawa mengi ya kupambana na maisha, kiasi kwamba hatukuwa na muda wa kukutana na rafiki yangu , hata tukikutana ni ile ya haraka haraka kila mtu anakimbilia kwenye shughuli zake, na mara rafiki yangu akanipa taarifa kuwa anahamishiwa Zanzibar kikazi,

‘Hamna shida kazi ni kasi, na popote uwapo tutazidi kuwasiliana…’nikamwambia aliponipigia simu na wakati ananipigia yupo tayari anaelekea kupanda express bot, kwani taarifa ilikuwa ya haraka, na alitakiwa haraka akawasili kwenye hicho kituo kipya, na huko atapata maelekezo zaidi…basi, tukawa tunawasiliana kwa simu tu, kuulizana hali na siku, na masiki yakapita.

 Ikawa akija Dar, hakai sana, na mimi nikawa na mishughuliko mingi ya shughuli zangu, wakati mwingine anakuja mimi nipo mikoani, kazi ni kazi, hakuna kulala, ilimradi afya zipo,…na kipindi chote hicho, tunapigiana simu au tunakutana kwa haraka, hutaamini sikuwa na hata na akili ya kumuulizia lile zoezi letu lilikwendaje…

Miezi mingi ikapita, na siku moja akaja kunitembelea nyumbani kwangu, alifika mara moja kikazi, basi tukaanza kuongea hili na lile, alikuwa kavaa Madera yake mapana tu, mimi nilijuwa kwa vile kahamsihiwa huko Zanzibar, basi kajifunza asili za huko, za kujisitiri mwili mnzima,….ila nilihisi kuna mabadiliko, ukimuangalia usoni kazidi kuwa mweupe, na unene kidogo, sijui kwasababu ya hizo nguo alizovaa, japokuwa nilikuwa na haraka kama alivyo yeye, nikamuuliza.

‘Vipi mwenzangu, toka lini ukavaa nguo hivyo, maana wewe ulikuwa ni mdhungu, haahaha, naona  sasa ushakumwa mnzaibari tena, na nahisi huko ushampata shemeji au sio, kwa hilo umbo na sura yako, sizani waname watakuacha upite hivi hivi tu, halafu hebu niambie, nahisi mmh,…na nakuona kama mambo tayari au, ..?’ nikaanza kumtania.

‘Acha utani wako bwana, nimpate wapi mume mie, umri ushaenda, ..naona wengi wameamua kunikimbia, lakini sijali, ..na wala hilo haliniumizi kichwa,… kabisa, kabisa,….mimi  nimeamua kula, kuishi  kivyangu, yaani sitaki tena usuhuba na hao watu, huwezi amini, nimeamua hivyo na imewezekana....’akasema.

Hapo ndio nikaumbuka kile nilichomshauri , ikabidi nimuulize

‘Vipi lile swala letu uliweza kulifanyia kazi?’ nikamuuliza.

‘Hahaha..unajua niliwazia sana hilo, nakumbuka tuliongea kuwa kama …unajua iwe siri, na..aah, …’akasita kuongea

‘Aaah, mbona unasita kuongea, au ulizarau…?’ nikamuuliza

‘Mhh, hapana sikuzarau, ..sio maana hiyo ya kuzarau,..unajua niliwaza sana huo ushauri,…, nikaona nisiende mbali…..lakini  wewe ni rafiki yangu, na hili tulilijadili pamoja, niliogopa ule usemi wako kuwa niwe makini maana wanawake wengine ni vichaa….’akatulia , sikuwa nimemuelewa hadi hapo ana maana gani.

‘Kifupi ulifanya au hukufanikiwa…?’ nikamuuliza

‘Ndio maana nimekuja kwako hivi leo, sina muda, hapa unaona meseji zimeshaanza kuingia natafutwa huko ...’akasema akitabasamu,…usoni ulionyesha furaha ya kweli, japokuwa kuna kiwingu cha kuonyesha ana mawazo fulani.

‘Kwahiyo kifupi tuseme tayari…?’ nikamuuliza nikiwa na hamasa ya kutaka kujua

'Mhh,…rafiki yangu, wewe na mimi ni marafiki, usingeliweza kunishauri kitu nikipinge bure bure…. ushauri wako nimeufuata na sasa hivi unavyoniona hapa nina uja uzito…hapa nilipo sitamani hata kula…kichefu chefu..yaani taabu kweli kweli..hivi mimba ndivyo zilivyo hivyo…, hapana nikizaa huyu mmoja, sizai tena, sitaki tena kuzaa.....’akaniambia.

'Mambo si hayo, ....umefanya jambo la maana sana, ....ulikuwa unapoteza muda tu,.. na umri ndio huo, na kama ulivyosema waume wanakuona sasa umeshakuwa mtu mzima, huna ujana tena, ..na ukiachia mwili hivyo,…mmh,…’nikasema

‘Sijaachia mwili, nachoka tu, halafu …sijisiki vyema,…’akasema

‘Ni kawaida, hali kama hiyo ni kawaida, muhimu ni kufuata masharti ya dakitari, hakikisha huharibu ulichokitaka, sawa….usije kujipilikisha na kazi, mimba ikaja kuharibika…’nikasema.

‘Hutaamini, nafuatilia masharti yote, naingia kwenye mitandao…nauliza madocta, sitaki kufanya makosa, na mungu anisaidie…’akasema

‘Hongera sana…’nikasogea na kumkumbatia rafiki yangu huyo…lakini sijui kwanini kuna kitu nilihisi akilini mwangu,..hata siwezi kukielewa, hata hivyo furaha iliweza kukimeza hicho kitu, ni kama mashaka,…’

‘Mhh,…hongera wakati hata sijafikia ….unipe nikishajifungua, au sio…na kiukweli, nashukuru sana rafiki yangu, umenishauri, na najua utaendelea kuwa name, hata siwezi kuelezea ninavyojisikia, japokuwa moyoni, kuna muda nawaza sana…’akasema

‘Unawaza nini sasa, hayo yameshapita muhimu ganga hili lililope mbele yako, jinsi ya kupambana na ujauzito maana nao sio mchezo, mengine yasahau kabisa,…unanielewa, wala usifikirie kuwa umekosea, ..hayo muachie mungu atakusamehe..’nikasema

‘Mhh…kweli wewe ni rafiki wa kweli..tatizo ndio hilo,… hapa nilipo, najisikia vibaya, sitaki kuongea saaana, mate yanajaa mdomoni…’akasema akitoa leso yake na kuweka mdomoni

‘Pole ndio uuke huo…’nikasema

‘Mungu anisamehe tu, na mnisamehe kwakweli….’akasema

‘Hamna shida wewe tema mate yako tu…ilimradi uteme sakafuni…’nikasema

‘Unajua  haya yote ni kutokana na ushauri wako, wakati mwingine najilaumu kwanini, niliamua kuvunja nadhiri yangu,  lakini sawa, kwa vile ni wewe sina shaka....’akasema.

‘Usijali kabisa…..mimi nilikupatia ushauri huo nikiwa najua wewe ni rafiki yangu, nikupe ushauri wenye tija,…usiwe na shaka na hilo..na sioni tatizo lipo wapi, …muhimu kama ulifuata kama  nilivyokuambia, sizani kama itakuwa na tatizo,…kwani huyo mwanaume, uliwahi kumwambia baada ya kuhisi kuwa una ujauzito unaotokana na yeye?’ nikamuuliza.

‘Mhh, …aah, …unajua wanaume walivyo, baada ya lile tendo,…nisikufiche, ili kuwa na uhakika zaidi,…nilikutana nae mara mbili, mara mbili tu….sasa ikawa ni taabu, unajua wanaume walivyo, na..na…nilipohamishiwa huko Zanzibar, nikashukuru sana, maana huko mpaka aje sio kazi rahisi…na, nilimkanya kabisa kuwa mimi, sitaki tena urafiki na yeye, ndio hivyo, na sitaki kuyaongelea hayo tena tuyaache tu, ila nilitaka ni…niwe muwazi kwako…’akasema

‘Safi kabisa, lakini je baada ya kujihisi una mimba uliwahi kumuambia…?’ nikamuuliza

‘Unajua.hapana sitaki tuliongelee zaidi…nataka kukuambia…hapana, naogopa…’akasema

‘Unaogopa nini sasa, nimekuuliza hivi umemwambia…?’ nikamuuliza

‘Kama nilivyokuambia, wanaume hawana dogo, na hata siku ile, ya kwanza nilimuambia nimfenya hivyo kwa vile nimeshindwa kuvumilia, ila naheshimu ndoa yake, kwahiyo iwe ni mwanzo na mwisho…’akasema

‘Safi kabisa, inatosha ulivyomuambia…’nikasema

‘Lakini bado akawa ananifuatilia, japokuwa nilijitahdii sana kumficha,...na nikajitahidi sana kuwa mbali naye, lakini sijui kwanini, imekuwa kama nimemuonjesha asali , ….yaani nipo kwenye wakati mgumu sana, ndio maana nakuambia nimekosea sana….sijui nifanye nini sasa…kwani hata nafsi inamtaka najizuia napata shida sana….’akasema.

‘Lakini nilikuambia kuwa kama ni mume wa mtu, ukishahakikisha kuwa keshakupachika mimba, achana naye kabisa, nilikushauri kuwa usimwambie hata huyo mwanaume kuwa una mimba yake, utasumbuliwa sana…, unajua waume wengine walivyo, hawatakubali damu yao ipotee hivi hivi, na hujui hatima yake itakuwa…na kumbuka kama ni mume wa mtu , ….utakuja hatarisha ndoa ya watu, kuwa makini sana kwa hilo…’nikasema

‘Hata sijiu nifanye nini, ndio maana nikaja kwako tena, nipata ushauri, au sijui niitoe maana najuta, na inanipa wakati mgumu, namtaka aje awe karibu nami, unaona ilivyo, hata sijui nifanye nini, ndio maana nafikia kujuta, najiona kama nimebeba dhambi mwilini mwangu…?’ akasema sasa akikwepa kabisa kuniangalia machoni

‘Kwani , hebu niambie ukweli huyo shemeji ni nani, maana sasa unanivutia intake kumfahamu, inaonekana umempenda sana…., hebu niambie ni nani ili niweza kukupa njia nyingine ya kumfanya asikusumbue tena..?’ nikamuuliza,  nikiwa na shauku kubwa sana.

'Na wewe bwana, ina maana hapana…. sasa, itakuwa wewe ni  wa kwanza kuvunja ushauri wako, mwenyewe ulianiambia nikishatembea na huyo mwanaume, nisimwambia yoyote hata wewe mwenyewe, sasa wewe unataka niseme, unajua hilo limekuwa likiniumiza kichwa, nawaza nikuambie tu, au ..hapana mimi naona nifanye kama ulivyonishauri, au sio…maana hakuna siri ya watu wawili..’akaniambia.

‘Lakini mimi ndiye niliyekushauri,…sasa , anyway,….fanya ilivyo sahihi, ni kweli ni bora iwe siri yako, ..hata hivyo ukiona ni lazima kuniambia ni nani, usisite kuniambia, kwangu usiwe na shaka kabisa, maana hatufichanai au..’nikamwambia

‘Lakini pia wewe ndiye uliyenishauri kuwa nikishahakikisha nina mimba nisije kusema au kumtaja huyo mtu,  kwa yoyote vile…, unakumbuka eeh, basi tufanye hivyo, najua utanisamehe…. tusubiri nizae kwanza, ....’akasema

‘Usijali kabisa, kunificha ni sawa,….hiyo inanipa uhakika kuwa hutasema lolotekwa yoyote, kama umeshindwa kuniambia mimi, nina uhakika hutaweza kusema lolote kwa mwinginewe, au sio…’nikasema

‘Ni kweli, basi,…haina haja kukuambia, ..na hapa nilipo najisikia vibaya,...ngoja niondoke, hapa nisije nikakutapikia bure, na na..nashindwa, natamani niku—ooh, najisikia vibaya sasa...’akasema na haraka akimbilia nje.

‘Kama mambo yenyewe ni hivyo , hicho kinaweza kikawa ni kidume, na ukija safari nyingine  ni lazima uniambie huyo shemeji ni nani, ...au nitakuja nyumbani kwako, upo mpaka lini...’nikamwambia na yeye akawa ameshatoka nje, …nilipomfuata nilimkuta ameshaingia kwenye gari lake na kuondoka.

                               *********

 Miezi mingi ikapita, ... kwasababu ya kikazi na mambo ya hapa na pale, na kwa vile sasa yeye yupo huko Zanzibar, hatukuweza kuonana na rafiki yangu huyo, na siku moja nikapokea simu, namba ilikuwa ngeni kwenye simu yangu, nikapokea nikijua yawezekana ni wateja wangu.

‘Habari nani mwenzangu..?’ nikauliza

Sauti ya kinyongea kama mtu mgonjwa ikasikika,..kwanza sikujua ni nani..hata kufikiri,…mambo mengi kichwani,…

‘Oh, …ni mimi, yaani …’akasema akitoa sauti ya kinyonge

‘Ni, ni …wewe ni nani maana namba hii ni ngeni kabisa…?’ nikauliza nikjaribu kuwaza ni mteja gani huyo. Na kwanini anaonekana mgonjwa akilini nikahisi inawezekana akawa mmoja wa wateja ninaye mdai.

‘Hii namba ni..simu ya rafiki yangu , ya kwangu imezima haina chaji,…’akasema

‘Ok,….pole..nani mwenzangu, nikusaidie nini…’nikasema

‘Nilikutumia ujumbe nilipofika juzi, lakini ukawa kimia,…..’akasema

‘Ujumbe…ujumbe gani, kwani wewe ni nani…?’ nikauliza kikazi zaidi.

‘Ni mimi…nilikutumia ujumbe nikitokea Zanzabar,….nikajua utakuwa wa kwanza kuja kuniona…nikaona kimia, nikakupigia , lakini kila nikipiga simu yako ipo inatumika, na bahati mbaya nilikuwa natumia namba nyingine, ambayo nilikuwa sijakupatia, ya Zantel…’akasema

‘Oh, ina maana ni wewe..mbona sauti ipo hivyo…?’ nikamuuliza baada ya kugundua kuwa ni huyo rafiki yangu.

‘Ni mimi …sipo vizuri ..aaah , maumivu…’akasema na kabla hajaongea zaidi  ni kasema;

‘Ujumbe wako niliupata,nilipanga nije kwako nikiwa na uhakika kuwa umeshafika…, ulisema umechoka…punguza kazi, pata muda wa kupumzika, ikibidi chukua likiza usije kupata matatizo…’nikasema


‘Unajua nilitaka niende kijijini kwa wazazi…, ili kukwepa yale uliyonishauri, lakini nikaogopa, unajua tena kijijini, nitaulizwa maswali mengi, nikaona bora nipambane kivyangu….’akasema

‘Vizuri, usijali, mimi si nipo, kama utakuwa hapa Dar, usijali kabisa, ..hata ikibidi unaweza kuja kukaa hapa mpaka muda wa kujifungua…’nikasema,


‘Kujifungua…hahaha…. nimekupigia kukufahamisha kuwa mimi nipo hospitali…’akasema na kukawa na ukimia, na nikasikia kama sauti ya kichanga kinalia.

‘Umelazwa,….ina maana…?’ nikauliza

‘Ndio nimeshajifungua mtoto wa kiume...’akasema na nikajikuta nashikwa na mshituko, kama vile nimeambiwa jambo baya, badala ya kufurahi, sijui kwanini…nikajikuta nimetulia kidogo.

Mara simu ikawa inataka kuingia, …na  nakumbuka kulikuwa na mteja muhimu nilitakiwa niongee naye, na hapa rafiki yangu kanipatia jambo muhimu sana…sijui ilikuwaje nikajikuta nimekata simu ya rafiki yangu na simu nyingine ikaingia…alikuwa ni mume wangu.

‘Oh, ni wewe…nilikuwa naongea na rafiki yangu, ….’nikasema na yeye akasema, alinipigia kuniarifu kuwa atachelewa, kuna sehemu atapitia…

‘Wapi huko, maana hata mimi nataka kutoka, ….’nikasema

‘Napitia hospitalini…..’akasema

‘Unaumwa…?’ nikamuuliza

‘Hapana kuna mtu nakwenda kumuona…’akasema

‘Basi hata mimi nakwenda hospitalini, kuna mtu nataka kumuona…’nikasema

‘Hospitali gani…..?’ akaniuliza…na hapo nikashindwa kumjibu maana nilikuwa sijamaliza kuongea na rafiki yangu, nikasema

‘Subiri kidogo nitakujibu, wewe unakwenda hospitalini gani…?’ nikamuuliza

NB: Haya mambo ndio hayo yameanza kujitokeza mkuki ulishafanya kazi yake, sasa tuone matokea yake


WAZO LA LEO:  Kwa watu wengi, ulimi huwa ni mgumu sana kuuzia, mnaweza kupanga kuwa hilo utakaloambiwa liwe siri, lakini kwa wepesi wa ulimi ulivyo, au kutokana na tabia zetu zilivyo, hatuwezi kuhimili, twatamani kuongea sana, ukaja kuliongea hata lile la siri, …siri ikavuja, na siri sio ya watu wawili. Tujifunze sana kutunza kile tulichoahidiana na wenzetu, kama uliambiwa iwe siri, basi na iwe siri kweli,..tukikumbuka kuwa ahadi ni dhamana. 
Ni mimi: emu-three

No comments :