Ikabidi nimpigie simu tena rafiki yangu ili kuhakikisha kuwa
hajatoka, maana hospitali nyingine ukijifungua kama huna tatizo, unaruhusiwa
mapema tu, na mazungumzo yetu yakawa hivi;
‘Samahani rafiki yangu, simu ilikatika, mzee aliingilia kati,
unajua tena, mume ni mumw inabidi umpe kipaumbele au sio, nisamehe tu kwa hilo,
…hebu niambie kwanza unaendeleaje?’ nikamuuliza
‘Kiukweli, ni maumivu tu…hapa yananitesa kweli, wamenipa dawa za
maumivu lakini bado,…oh, ….ila sikupata taabu kujifungua, sio ile kama
ninavyohadithiwa, namshukuru sana mungu….ooooh, , nimejifungua salama,
iliyobakia ni jinsi…lakini nitajitahidi kama ulivyonishauri …’akasema
‘Yaani siamini ina maana miezi tisa tayari… hivi urafiki wetu
umekuwaje, ndio ..lakini ndio maisha au sio…kweli, kweli siku zinakwenda na
maisha yanabadilika, umesema ..upo hospitali gani vile maana mimi nimebahatisha
tu?’ nikamuuliza.
‘Hilo swali gani tena rafiki yangu…, mimi siendi kwenye hospitali
tofauti na ile hospitali yangu niliyozoea kutibiwa na ndipo nilipojifungulia, wewe
kama upo bize, haina haja…utanikuta nyumbani,..nilikuwa nakufahamisha
tu...’akasema rafiki yangu huyo na mimi huwa naifahamu hiyo hospitali yake
anayopenda kwenda mara kwa mara akiumwa.., sikutaka kumuuliza zaidi, nikasema;
‘Eti kama nipo bize, hilo usithubutu kusema, mimi na wewe tena,
ninakuja hivi sasa nipo njiani,…maana taarifa hiyo kwanza ilinishtua, na furaha
ikawa kama mshtuko fulani, sijui kwanini…’nikasema
‘Oh, unakuja….mbona unasumbuka hivyo, kuna mtu ….’akasema akiwa
kama anauma uma maneno
‘Ninakuja usiwe na shaka, kama ni kukuchukua nitakuchukua
mimi,…oh, nimefurahi kweli, ....nakuja sasa hivi, nataka niwe wa kwanza baada
ya manesi kumshika huyo mtoto na kumpa huduma stahiki, mimi ndiye wa kuendelea
kutokea hapo, sijali kazi hilo ni muhimu kwangu kwa sasa...’nikasema na kukata
simu.
Kiukweli nilikuwa na mambo muhimu sana lakini niliamua kuyasitisha
kwa kuona umuhimu wa jambo hilo, nilimthamini sana rafiki yangu na, haraka nikaingia kwenye gari kuelekea huko
hospitalini. Sikukumbuka kumpigia tena mume wangu kumuarifu mimi ninakwenda
hospitali gani!
Tuendelee na kisa chetu
****************
'Rafiki yangu nimejifungua, mtoto wa
kiume...bado nipo hospitalini...' nilijikuta maneno hayo yakijirudia rudia kichwani, hasa nikikazia
hilo la ‘mtoto wa kiume…’
‘Mtoto wa kiume…mmh,….ana bahati kweli…’nikasema nikakumbuka mume
wangu jana alivyokuwa akiongelea kuhusu watoto na alitamka neno kuwa hivi sasa anatamani
kumpata mtoto wa kiume, akishampata huyo hasumbuki tena, nikamwambia
‘Kupata mtoto wa kiume ni majaliwa ya mungu, ..’nilisema hivyo,
tukaishia kuongea maneno mengine.
Nikiwa kati kati ya bara bara ndio nikakumbuka kuwa mume wangu
alitaka nimuambie naelekea hospitali gani, nikampigia simu , lakini kila
nilipojaribu namba yake inasema
inatumika, sikujali sana, nikijua mwenzangu katingwa na majukumu, yake ya
kikazi.
Mimi nikaongeza mwendo, na kuelekea hospitalini hapo alipolazwa
huyo rafiki yangu, na wakati naendesha nikaona nimpigie tena huyo rafiki yangu,
nia ni kujua kinachoendelea kama nahitajika kumchukulia chochote cha kula.
Lakini badala ya kuliongelea hilo kwanza tukajikuta tunaongea mambo mengine.
'Oh, hongera sana mambo si hayo, ..wewe ulikuwa unapoteza muda
bure, uzee ndio huo. Ulikuwa unasubiri mtoto aje akuite bibi,..’nikaanza kwa
utani na akawa anacheka, na kusema.
‘Usinitanie mbona sijazeeka kiasi hicho cha kuitwa bibi…ni kweli
ukiangalia wenzangu wenye umri kama wangu, unaweza kuwasalamia lakini mimi bado
naonekana kijana tu…sasa naogopa nisije kuelekea huko’akaniambia na mimi
nikasema;
‘Ni kwasababu ulikwepa majukumu ya kuolewa na kuogopa kuzaa
mapema, ndio maana bado unaonekana bado kijana, ngoja upate mtoto wa pili, na
upate shemeji anayejua mfumo dume, kama hutabadilika sasa hivi na kuitwa
bibi...’nikaendelea kumtania.
‘Nani azae tena, …mimi...subutu yake..na kwa vile sina mume, …hilo
limepita.., hii kasheshe niliyoipata siwezi tena kubeba mimba, kwanza uone
ilivyo, nimezaa nikiwa mzazi peke yangu, nawaza huko mbele, mtoto akikuwa,
anaweza kuanza kudai baba yake ni nani….na ole wake akiniuliza , nitampa jibu
hatakumbuka kuniuliza tena….’akasema.
‘Oh, kwanini useme hivyo mpendwa, siumesema huyo shemeji anajua
una mimba, na kwahiyo nahisi utakuwa umeshamwambia kuwa umeshajifungua,
japokuwa kiukweli hayo uliyoyafanya hayanihusu , umekwenda kinyume na
makubaliano yetu, ni hatari, nahofia ndoa za watu, ….’nikasema.
‘Ukifika tutaongea bwana, ….pamoja na mengine niliwazia sana
ushauri wako, kuwa nimtafute mwanaume ambaye sitakuja kupatishwa taabu na
mkewe, na..laki ni stutakuja kuyaongea, nataka nije kuyaweka wazi mapema tu….’akasema
‘Kwahiyo unataka kusema nini, kuwa utamuhusisha na huyo mzazi
mwenzako je mke wake itakuwaje…?’ nikamuuliza
‘Nitajitahidi sana …unajua, sizani kama ni tatizo, hata hivyo,
ifike muda tuongee, tuone tutafanyaje, na huyo mwanaume …sihitajii sana
kumueleza, japokuwa ananiganda sana, unajua awali kabla sijajifungua nilikuwa
natamani sana awepo, kuna hali ilikuwa inanivuta awepo,..mpaka nakereka,…lakini
sasa nimeshajifungua, sitaki hata kumuona, sijui kwanini ....’akasema
‘Haya tutakuja kuongea tu, na kuhakikisha kila kitu tunakiweka
sawa, mtoto wako ni wangu, hilo halina shida, usijali kabisa....’nikasema huku
nikimuwazia huyo rafiki yangu na mtoto wake, nikikumbuka ushauri nilio mpa, na
kujisifia moyoni kuwa nimefanya jambo moja kubwa kwa rafiki yangu, nikasema.
‘Ninakuja na zawadi kibao kuonyesha jinsi gani nilivyofurahi, na
shemeji nilimuambia kuwa ninakwenda hospitalini kumuona mzazi, unajua
alichoniambia,….eti na yeye kuna hospitali anakwenda kumuona mzazi pia…’nikasema
‘Oh, ndivyo kasema hivyo, …..’akasema hivyo.
‘Nahisi ni mfanyakazi wao ….sijamuulizia sana, lakini anaweza
akaja kukuona, ingelikuwa ni bora tungelifika sote,…wanaume hawajui zawadi gani
kwa mtoto ningemshauri zawadi gani tuje nayo,…’nikasema
‘Ok….sawa, nimekuelewa, …ukija tutaongea….’akasema na mimi
nikaendelea kuongea;
‘Unajua hizi kazi zetu tena,
mimi na yeye siku hizi tumekuwa kila mtu bize-bize, yeye na shunguli
zake, na kazi zake za kuajiriwa, na bado anahitajika kusimamia, kwenye ofisi
yake aliyoifungua, kwahiyo kazi zinamuendesha mbio mbio, kama ilivyo mimi,…mimi
tu, nina ofisi yangu mwenyewe bado
nasumbuka hivyo, na wafanyakazi, je yeye mwenye majukumu mawili itakuwaje…kwenye
ajira ya kuajiriwa na kwenye ofisi yake ya kujiajiri, sio mchezo. …’nikasema
‘Hongera zenu mlioweza kujiajiri na sasa mnaajiri wafanyakazi,
hata mimi natamani niwe hivyo, natamani sana maisha yenu, yaani sijui kwanini,
nataka niwe kama nyie…’akasema
‘Unajua …nilitaka nimwambieje shemeji yako, aje tukutane mahali
ili tukakununulie kila kitu sitaki ugharimie chochote, cha mtoto hadi wewe
mwenyewe…mimi ninataka kila kitu nitoe mimi, unasikia, wewe ni rafki yangu,
hilo halina mjadala…’nikasema.
‘Mhh, rafiki yangu, utanifanya nilemae bure…hapana… mimi nataka
niwajibike kama mzazi, kuanzia mwanzo hadi mwisho, nataka nifaidi kile
nilichokikosa miaka yote hiyo, nataka niwe mzazi,… sio mlezi,….’akasema
‘Hili usiniambie, bado utaendelea kuwa mzazi,…najua tutanyaje….Hivi
nikuulize maana tumeongea sana, vipi kuhusu chakula ….ngoja kwanza
nikakununulie supu ya nguvu, napitia kwenye hoteli, .. nitakuja nayo hiyo supu
sijapika mwenyewe, nitakuwa nakupikia …lakini kwa leo, kwa dharura, ngoja
tununue hotelini…, sitaki mtu mwingine alete unasikia….najua ndio chakula chako
kwa hivi sasa…’nikasema
‘Haya usichelewe maana huenda wakaturuhusu leo hii…, kwa hivi sasa
docta hajapita bado, …..na mimi sipendi kuendelea kukaa hapa ndani, madawa na
harufu za kihospitali sizipendi ....we acha tu..hata hiyo supu sizani kama
nitaweza kuinywa,…mimi naona ususumbuke kuinunua,..labda kama utainywa wewe…’akasema
‘Ina bidi uanze kuzizoea hali za namna hiyo, maana kuna kiliniki
ya mtoto, laaima ufike hospitalini, na huwezi jua, ...akiumwa unatakiwa kuja
kumuona docta, tena docta wa watoto…’nikasema
‘Najua najua..hayo baadae…’akasema
‘Sio unajua sikiliza, hayo ni muhimu sana, mtoto mchanga akiumwa
uhakikishe unampeleka kwa docta bingwa wa watoto,..sio unaitisha madocta
mitaani, au nyumbani,..na usimpeleke mtoto kwa docta wa kawaida, unaweza ukamkomaza
mtoto kwa madawa yasiyomsaidia.....’nikamwambia.
‘Haya bwana, wajifanya wewe ni mzoefu sana nakusikiliza, kwani upo
wapi, maana nakusubiria, mshauri wangu, na…hebu kwanza,…ok, … nakata simu,
maana naona kama docta anakuja....’akasema na mimi nikakata simu.
************
Nilifika kwenye hiyo hospitali mapema, maana kulikuwa hakuna
foleni kama nilivyotarajia, nikampigia simu katibu muhutasi wangu abadilishe
ratiba zangu za siku, ofisi yangu ya kujiajiri ni kubwa, ina kila kitu
kinachohitajika kama kampuni inayojitegemea.
Nilipofika hospitalini, nikapitia njia tofauti ya kuingilia,
nilipitia njia wanayotumia wafanyakazi wa hapo maana wao wanasehemu yao,
nikaenda kulisimamisha gari langu sehemu wanayosimamisha magari yao, kama mfanyakazi
wa hapo, nikaongea na mlinzi alilalamika, lakini nikampa pesa ya soda, akanyamaza.
Nikaenda moja kwa moja kwenye wodi ya wazazi, nikamuona rafiki
yangu, akiwa amekaa kwenye kitanda, huku akiwa na mkoba wake pembeni,
nikashangaa, na kumuuliza.
‘Vipi tena, mbona umekaa mkao wakuondoka…?’ nikamuuliza nikimkagua
akiwa kambeba kichanga chake na mimi nikasogea na kumpokea.
‘Yaani ulipomaliza kuongea na mimi kwenye simu , akaja docta, na
akaniambia sina haja ya kuendelea kukaa zaidi hospitalini, nilishukuru kitu,
alisema kwa vile mimi sina tatizo lolote, ninaweza kuondoka tu…, basi, nikaona
nifungashe-fungashe vitu vyangu, nimempigia simu ndugu yangu aje kunichukua,
japokuwa....’akatulia kidogo akimwangalia mtoto.
Wakati anaongea akili yangu ilishazama kwenye mtoto, nikawa
namkagua,unajue tena sisi akina mama, macho yetu yameumbwa hivyo kudadisi,
sura, umevaa nini upoje…kwahiyo kwa muda mfupi nilikuwa nimeshamkagua mtoto ,
usoni, ..na sikutaka kumuuliza kwanini kakatisha kuendelea kuongea, nikasema;
'Mhh, mtoto mnzuri kweli, halafu,ana kila ngapi, mnzito…….umegundua
kitu, kwanini watoto wachanga wote huwa wanafanana, maana namuona mtoto
wako anafanana sana na watoto wangu, walipokuwa wachanga...’nikasema na yeye akaniangalia kwa haraka, halafu akageuka
kumwangalia mtoto wake, huku akitabasamu, hakusema kitu akawa anamweka vizuri.
‘Naona kweli ndoto yako imetimia, maana ule usemi wako wa kuwa
unatamani mtoto wako afanane na watoto wangu, umekamilika…’nikasema
‘Mhh, nashukuru kwa hilo,ahsante sana rafiki yangu, bila wema wako
sijui ingelikuwaje, .….’akasema akitabasamu.
‘Ni kweli, unajua rafiki yangu…ni kweli sasa kile tulichokitaka kimetimia,
kweli mungu kasikia kilio chako…yaani nikimuangalia huyu mtoto wako, nakumbuka
watoto wangu walivyokuwa wachanga,…’nikasema nikiendelea kumkagua mtoto.
‘Kwanza angalia vimdomo
vyake, na…na, macho yake japokuwa kalala.....yaani kama ungelimuweka na watoto
wangu enzi hizo wakiwa wachanga, ungelisema ni mapacha na watoto wangu….’nikasema
huku nikiendelea kumchunguza yule kachanga.
'Kweli,...japokuwa nilitaka wasichana kama wa kwako, na wawe
mapacha kama wakwako, …unajua nilitakamani kuzaa mapacha kama wewe…lakini mungu
kanipa mvulana, na kweli eeh,…kumbe … wanafanana na watoto wako, oh…’akasema
‘Unajua watoto wangu wanafanana zaidi na baba yao kisura , na
kirangi wanafanana na mimi, watu wengi wanasema hivyo, hata wewe uliwahi
kuniambia hivyo…’nikasema
‘Hivi eeeh, ni kweli, …anafanana shemeji…unajua nilikuwa
sijaligundua hilo…akili yote ni kwenye furaha kuwa nimempata mtoto…'akasema na
akawa kama anaonyesha uso wa haya, hata kuniangalia machoni inakuwa ni ngumu
mimi sikuwa na mwazo yoyote zaidi ya kujua ni kufanana tu;
‘Mhh, nina hamu sana ya kumuona huyo shemeji, maana sipati picha,
kama umeamua kumuhusisha basi hata mimi nastahiki kumuona, au sio,..kwani nikuulize
huyo shemeji yangu ni nani, nahisi kama
anafanana sana na watoto wangu, je ameshafika kukuona?’ nikamuuliza
‘Bwanaeeh, hayo tuyaache kwanza, tutaongea vizuri tukifika
nyumbani, najua una hamu kujua mambo mengi kwa wakati mmoja,…kila kitu
nitakuambia,.. lakini kila kitu na wakati wake au sio, tukianza kuongea hapa,
huoni watu watatusikia,a au….’akasema
‘Mhh, leo twaanza kufichana, haya bwana, lakini kama umeamua
kumuhusisha huyo shemeji,…kiukweli sikupendezewa na hilo, halikuwa kwenye
makubaliano yetu, mimi ni mwanamke…,
nipo kwenye ndoa, nafahamu ndoa ilivyo…hili lilitakiwa liwe siri yako mimi na
wewe, sasa umeshaanza kuharibu mapema, sijui una lengo gani, sijapendezewa na
hilo, kwanini ukamwambia huyo mwanaume…’nikasema
‘Lakini …sikupenda iwe hivyo,…nilijitahidi sana rafiki yangu… hata
hivyo…sizani kama itakuwa na matatizo, sizani..’akasema
‘Najua haitakuwa na matatizo,…nitajitahidi kukusaidia, na
kukushauri inavyotakiwa, ila nakuonyesha hatari yake,…ndoa ni kitu kingine,…na
kwa hili, mimi nataka nionane na huyo shemeji nimsomeshe mwenyewe, ili aelewe…,
sitaki uje kupata matatizo, sitaki nikuone unakuja kuishi maisha ya kujihami,
maana hujui wanawake wa ndoa walivyo…’nikasema
Nikamuuliza huku akilini
nikimuwazia huyo shemeji, ambaye nahisi atakuwa akifanana na mume wangu, kwani kiukweli
watoto wangu wanafanana na baba yao, na kiukweli, ukimuangalia huyu kichanga, anafanana sana na watoto wangu.
‘Mwambie kuanzia sasa hatakiwi kabisa…na wala asije hapa kukuona…’nikasema
‘Mbona keshafika, alikuwa wa kwanza kufika hapa, na ,na
hukumuona huko nje, au aliniambia anasubiria nikiruhusiwa mapema, kama ndugu
yangu hajafika atanichukua yeye,… yupo huko nje, ila mimi nimemkatalia kama
ulivyonishauri,nimemuambia aondoke, sasa kama bado yupo huko nje shauri lake…’akasema
‘Ina maana alishafika…tatizo sikuingilia mlango wa kawaida,
nimeingialia mlango wa mastafu…unajua rafiki yangu unafanya visivyo kabisa…’nikasema
‘Sikutaka kabisa yeye aje nilimuelezea yote hayo, kuwa kuanzia
sasa sitaki anifuate fuate, lakini akasema na yeye atachukua tahadhari, hata
hivyo hawezi kuniacha, …ndio maana alikuja mapema ili anichukue , halafu arudi
nyumbani kwake…hata yeye hapendi…lakini unajua tena…hata hivyo nilimuambia huu
ni ushauri wako …’akasema
‘Masikini…mmh, unajua naanza kuwazia mbali, huyo mke wa huyo
mwanaume, unajua inauma sana....lakini tutaona la kufanya, ila nataka nionane
naye huyo mwanaume kwanza ni muhimu nikutane naye nimsomeshe mimi mwenyewe..,
kama ni lazima vitu vyote vipitie kwangu, na mimi nitajua jinsi gani ya kufanya…’nikasema
‘Usijali rafiki yangu, …mimi nataka hili jambo niliweke wazi
kwako, ndio maana nataka tukaliongelee huko nyumbani, wewe ni rafiki yangu,
najua hutanilamu kwa lolote lile, nilifuata ushauri wako tu…’akasema
‘Siwezi kukulaumu kabisa, kwanini nikulaumu..ushauri nimeutoa mimi
mwenyewe, sasa itakuwa ni ajabu nianze kukulaumu, ila ni lazima tuchukua
tahadhari, maana utu, ubinadamu,…kuna kuumia hapo, mwenye mume, akijua ni
lazima ataumia, ndio hilo silitaki kabisa…’nikasema na rafiki yangu akawa kama
ananywea fulani hivi.
‘Umefanya makosa sana…’nikasema
‘Usinilaumu rafiki yangu, maana nilifanya juhudi zote,….lakini
ikashindikana…hata sijui alijuaje kuwa nimejifungua, sikutaka kabisa
kumfahamisha hilo maana nilikuja kutoka Zanzibari kwa siri, na sikuwahi
kumpigia simu, …’akasema
‘Sasa alijuaje…?’ nikauliza
‘Hata sijui, kaniambia … kumbe alikuwa akinifuatilia kila siku
alipogundua kuwa nimefikia muda wa kujifungua, akawa anafuatulia nitakwenda
hospitali gani, sijui kwanini …nashangaa nimejifungua, sina hili wala lile huyu
hapa , akawa yeye ndiye wa kwanza kuja kunipa
hongera, na alipogundua kuwa nimejifungua mtoto wa kiume, amefurahi kweli
kweli, nikampa onyo, kuwa huyo sio mtoto wake...’akasema
‘Kwahiyo kumbe mlikuwa mnaelewana sana na huyo shemeji, mlikuwa
karibu sana kihivyo usinidanganye rafiki yangu, umefanya makosa ambayo utakuja
kujijutia, nakueleza ukweli ulivyo…, inatakiwa tuwe makini kuanzia hivi sasa,
utakuja kupata lawama kubwa sana.
‘Kuelewana kwa vipi, si tuliliongea hili kuwa nimetafute yule
ambaye namuelewa sana,….na unajua,… nikuambie kitu, shemeji alinibana
sana...mwanzoni nilimficha, lakini wanaume bwana, akawa akinidadisi mara kwa
mara hasa alipoona mabadiliko, najuta kwanini nilishindwa kumdanganya, ...na
tatizo kama nilivyokuambia awali , nilikuwa natamani sana awepo karibu yangu
mara kwa mara..na…kila mara nataka angalau nisikie sauti yake, angalau, …mimba
ina matatizo jamani….’akasema
‘Nayafahamu sana, ukiwa na mimba unaweza ukampenda sana mume wako
au ukamchukia sana, inatokea hivyo, lakini mimi naangalia kote kote, kwa vile
mimi ni mzazi, mimi nipo kwenye ndoa, nayafahamu hayo zaidi, jinsi gani mtu
unavyoumia ukiibiwa mume wako…’nikasema
‘Usitake kunitia kwenye lawama tena, ushauri wako ndio umeifanya
hii kazi, na najua wewe hutaweza kunilaumu kwa hili…’akasema kidogo akionyesha
hasira.
‘Sio kwamba nakualaumu, ..unasikia kwa vile ni mimi nimeutoa
ushauri, nataka ushauri uende ilivyo, isje ukapata matatizo, tunahitajika
kuchukua tahadhari zote, unielewe hapo…’nikasema
‘Sawa basi tuondoke, maana dawa ndio hizo hap anazileta nesi, kila
kitu sasa kipo sawa sawa….’akasema
‘Kwahiyo mimi nashauri ni bora twende nyumbani kwangu ili niweze
kukusaidia vizuri, sitaweza kujigawa, mimi nilikuja na wazo hilo japokuwa
sijaongea na mume wangu, lakini hili sio lazima nimuambie anakufahamu wewe kama
ndugu yangu…’nikasema.
NB: Ngoja tuishie hapa kwa leo
WAZO LA LEO: Urafiki wa kweli hujengwa na
kuaminiana,..kama mtakuwa manafichana mambo yenu, ujue urafiki huo una
walakini. Lakini pamoja na hayo, tusiwe tunafanya mambo kama kufurahishana tu,
unamshauri rafiki yako, ili tu afurahi, bila kujali athari zake mbeleni.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment