‘Kwahiyo mimi naona twende ukaishi kwangu…;’
‘Hapana, hilo sio wazo zuri kabisa, mimi sikubaliani nalo, huwa
nafuata ushauri wako, lakini sio huo…..nataka nikaishi kwangu, sitaweza kuishi
nyumba moja na shemeji, hahaha, unajua mimi nataka nikakae kwangu ili niweze
kumlea mtoto wangu mwenyewe, nataka
niipata ile shida ya mama…’akasema
‘Mhh,..sijakuelewa kwahiyo kinachokukataza kuja kuishi kwangu ni
kumuogopa shemeji yako, hayo yameanzia wapi, …ya kuanza kumuogopa, si unamfahamu
alivyo, hana muda na mtu kabisa, ni simba mwenda pole, ila namuamini sana mume
wangu hana tatizo na mtu, hajawahi kunificha ficha mambo yake, labda kama yapo
mengine siyajui…’nikasema.
‘Ni kweli simba mwendo pole, …hata hivyo, nimesema tu hivyo…’akasema
‘Au wewe una lako jambo,nahisi mumeshapanga na mwenzako kuwa uendelee
kukaa kwako, ili aweze kukutembelea…bila kuwa na kikwazo, si ndio hivyo….’nikamwambia
‘Aaah, hapana..sio hivyo, sijaongea naye kuhusu hilo, ila sio
vizuri,….na.., na kwanza hilo halimuhusu kabisa…ila mimi mwnyewe naona tu
nikakae kwangu, tafadhali nielewe hivyo…, na hilo tusiishie kubishana nalo..,
wewe kama huna muda, …na najua hutakuwa nao, kuna ndugu yangu kasema
atakuja….’akasema
‘Nikuulize swali moja, je huyo mzazi mwenzako unampenda….?’
Nikamuuliza
‘Swali gani hilo jamani, nitampendaje mume wa mtu,…au umesahau
tulichokijadili tokea awali, …yeye kazi yake imekwisha au sio….lakini nataka
tukifika nyumbani tuongee vizuri, hili jambo tuliweke wazi, nataka nikuambia kila kitu au unasemaje,
ili isije kuleta matatizo baadae unaonaje…?’ akaniuliza
‘Sawa, kwani kuna shida kwa hilo, mimi na wewe tena, au sio, hata
mimi nina hamu ya kusikia ikiwezakana kila kitu, usinifiche mimi, sawa hilo
litanipa faraja kuwa unaniamini …’nikasema
'Unajua baada ya hili,..sizani kama nitarudia tena ….maana hata
yeye, amekuwa kwenye wakati mgumu, japokuwa unajua tena wanaume,, sikutaka wazo
la kuwa marafiki wa siri, hilo nimelipinga, japokuwa aliniomba hivyo…unajua
hata kama imetokea hivi, bado msimamo wangu upo pale pale, sitaki mume wa mtu,
hili nimetokea kama dharura basi..kuanzia leo..sitaki tena mwanaume, hasa mume
wa mtu, iliyotokea imetokea, hiyo mara moja na sitarudia tena hili....’akasema.
‘Hahaha, hata sisi tulisema hivyo, kuwa sitazaa tena, lakini
kiukweli, watoto wanaraha zake, ukiona mwenzako ana watoto zaidi ya mmoja,
wanakimbizana, utatamani sana na wewe uwe nao…, kama mimi sasa hivi natamani
nipate mtoto, nipate mtoto wa kiume, kama anavyotamani shemeji yako, ...’nikasema.
‘Mhhh….kweli eeh, labda…’akasema na kutulia kimia kama anawaza
jambo.
‘Unajua kama huyo mwanaume angelikuwa sio mume wa mtu,
ningekushinikiza akuoe, maana naona umempenda kweli,…lakini sasa, kama ni mume
wa mtu achana naye kabisa,…unasikia, ukitaka usalama, na ili hili lisivuje,
achana na huyo mwanaume, ndio maana nilitaka nikutane naye, ili nimkanye, na
mambo yaishie hapa hapa,kwani mlikubalianaje, kuwa atakuwa akikutembelea au,...?’
nikamuuliza.
‘Nitakubaliana vipi bwana…., na mtu mwenyewe sio mtu wa
kunioa...kwanza sipendi kumuongelea tena ...naona hilo tuliache kwanza….’akasema
na niliona kweli hakutaka kumuongelea huyo shemeji, nilifahamu ni kwanini,
lakini moyoni nilikuwa na hamu sana ya kufahamu huyo mwanaume wake.
Kila mara nilipo-muangalia huyo kichanga, nakuwa kama nawatizama
watoto wangu walipokuwa wadogo, na hamu ya kukutana na huyo jamaa ndio inazidi,
kwani nahisi atakuwa anafanana sana na mume wangu. Wakati mwingine niliwazia
huenda ni mmoja wandugu za mume wangu, lakini nani nisiyemfahamu.
Basi taratibu za hospitalini zilipokwisha nikamshauri kuwa mimi
nitampeleka nyumbani, haina haja ya kusubiria gari lake,..kwani aliagiza mtu
aje kumfuata, hakutaka kupelekwa na mtu mwingine,
‘Nimesema mimi ndio nitakufikisha nyumbani,…’nikasema, na hapo
akawa hana ubishi kwa hilo, na muda huo, ….nikawa nataka kumpigia mume wangu
simu, lakini nafasi ikawa hanipi kufanya hivyo, nilitaka nimuarifu kuwa
tumeshaondoka hospitalini kama ananitafuta,..na huenda atakuwa na hamu ya kuja
kumuona mzazi, lakini kama kawaida nilipojaribu kupiga simu yake ikawa inatumika.
‘Huyu shemeji yako bwana…’nikasema
‘Shemeji yangu..nani, mume wako, kwani vipi, kasemaje…?’
akaniuliza akiniangalia kwa hamasa
‘Kila mara simu yake ipo inatumika, yaani nikitaka niwasiliane
naye labda nimtumie ujumbe wa maneno…, ndio baadae anakupigia, siwezi kumlaumu
yupo na shughuli nyingi sana,..’nikasema
‘Hamna shida, usimsumbue tafadhali….’akasema
‘Sio kumsumbua, atakuja kunilaumu kuwa
sijamfahamisha,…..’nikasema, na akaonekana hana raha, akawa kaangalia nje.
‘Mhh, usiseme sasa tunataka kufichana nakuona kama una mawazo sana
badala ya kuwa na furaha, hiki ni kipindi chako cha kufurahi au sio, mimi ndiye rafiki yako, mshauri wako, na lako
ni langu, kama kuna kitu unahisi kinakukwaza, niambie nijue ni jinsi gani ya
kukusaidia, unanielewa hapo….au ni kuhusu huyo shemeji…?’nikamuuliza.
‘Shemeji!….mmh,…’akasema na akawa kama anawaza jambo halafu
akasema;
‘ Ni kweli kama usingelikuwa wewe, nisingelikuwa na wazo hili,
lakini mhh, kuna kitu bado sijakielewa,
na sijui kwanini naogopa,…labda kwa hivi sasa nibadili mawazo….kwanini, nisifuate masharti yako kabisa,
ili kuepusha shari,…’akasema
‘Kuepusha shari…! Ahari gani kwani,…mimi nakushangaa, n kwanini
ulikwenda kinyume na maagizo yetu, ungelifuata nilivyokuambia usingelikuwa kwenye
wakati mgumu wa mawazo ..sasa nakuona huna raha, sijui kwanini….’nikasema
‘Ni lazima iwe hivi, na hujui tu, nilijua ni rahisi kwa vile ni
wewe, lakini mmh, unajua nilijitahidi sana, yaani mpaka nafikia hatua hiyo…niliwazia
sana…kiukweli nimepitia wakati mgumu sana…sijui kwanini niliamua kwa haraka iwe
hivyo, sikuwa na nia na yeye, lakini imeshatokea tena nitafanyaje, nakutegemea
wewe tu…’akasema
‘Ina maana huyo shemeji, ..hukuwa na …sijakuelewa hapo, hebu
nifafanulie kidogo, ni kama ulilazimishwa, au ilikuwaje…?’nikasema na kuumuliza
‘Unaonaje tukafunga huu mjadala wa huyo shemeji,..ili nifikirie
zaidi, tukifika nyumbani nitakuwa na maamuzi kuwa tulijadili na mimi nikuambie
kila kitu au la, ….najua wewe ni mshauri
wangu, lakini…kwa hivi sasa naomba tusimjadili shemeji, unaonaje,…tusubirie
hadi nifikie muafaka fulani kichwani…’akasema
‘Sawa ungeliwazia hilo tokea awali, lisingelileta mashaka,
ingelikuwa ni siri yako tu, lakini sasa umeshaanza kuliweka wazi, na mimi
huwezi kunificha tena, ni wewe umenihamasisha, na sio wewe tu hata mtoto
ananifanya niwe na hamasa ya kumuona huyo baba yake, ni nani huyo shemeji yangu…’nikasema
‘Sio baba yake jamani…, tafadhali, hiyo kauli siitaki kusikia,,…’akasema
‘Naongea nikiwa mimi na wewe,…hata hivyo kwanini,…ndio nafahamu
kwanini unasema hivyo,..lakini wewe mwenyewe umeshamshirikisha huyo mtu au sio,
hata hivyo usijali, kwangu mimi najua kila kitu, ni siri yetu mimi na wewe au
sio…’nikasema
‘Ukisema ni baba yake wakati ni mume wa mtu naumia sana...mimi
sina mpango wa kuolewa na yeye na wala sina mpango wa mahusiano na yeye tena, ilikuwa ni kwa minajili ya hilo zoezi na sasa
limekamilika basi….na kiukweli, sitaki hata kuyakumbukia hayo yaliyopita....’akasema
na mimi nikaingiwa na hamu zaidi ya kujua ilikuwaje siku hizo walipokutana naye
ilikuwaje , lakini sikutaka kushinikiza aniambie jinsi livyokuwa .
‘Ok sawa, lakin kama rafiki yako nahitajia kufahamu mengi ili
nisiumie kichwa changu kuwazia hilo,…usiniweke njia panda tena,… na kama
umeshampa tahadhari huyo mwanaume, ya kuwa
iwe mwanzo na mwisho basi haina shida…’nikasema
‘Nimemwambia shemeji, hili jambo limetokea lakini nataka iwe siri,
kwani hata hivyo tangu awali sikutaka alifahamu hili kuwa ndio yeye aliyemipa
huo uja uzito, ila kwa kunifuata fuata kwake mara kwa mara ndio nikajikuta
nikimwambia hivyo…najua nimefanya kosa kubwa, kinachoniumiza zaidi ni kumuona
jinsi alivyokuwa na furaha alipomuona huyo mtoto, sijui kwanini…’akasema.
‘Eeeh,…alikuwa na furaha, ndivyo wanaume walivyo…na huenda na yeye
alikuwa akihitajia mtoto, hana watoto nini…?’ nikamuuliza
‘Mbona anao,…’akasema
‘Basi huenda, alihitajia mtoto wa kiume, ..ndivyo ilivyo, ni kama
mimi na mume wangu, mfano si kama huyu mume
wangu, anahitajia sana mtoto wa kiume, ila nimemuambia asije akakufuru, akaenda
kutembea nje, sisi tumtegemee mungu tu, na ipo siku atawapata, …tena mapacha wa
kiume kama walivyokuwa mapacha wa kike…hahaha…’nikasema na kucheka.
‘Mapacha tena,!…Unanifanya nikumbuke kuwa hata mimi nilitaka
nipate mapacha, ndio maana nilimuona shemeji ataweza kulifanya hilo, kumbe …sio kwa kila mwanamke inaweza kutokea,
ni mipango ya mungu au sio…’akasema
‘Kwahiyo kumbe na yeye ana watoto mapacha, kama wangu ehe…wewe
naye, kila kitu unataka sawa na mimi, hahaha…lakini ndio uafiki wetu ulivyo,..usingelikuwa
wewe ni kama ndugu yangu, ningelisema…uolewe na mume wangu,…hahaha natania
bwana, wewe, kuolewa uke wenza sio mchezo, ni heri yeye mwenyewe aamua,..hujui mimi nina wivu sana, naweza kuua, hata hivyo,
mume wangu hataki,..na mimi pia sitaweza,….’nikasema na kucheka.
‘Hata mimi sitaki kuolewa uke wenza…..’akasema kwa sauti nzito
‘Mbona umezaa na mume wa mtu…’nikasema kiutani huku nikicheka.
‘Na wewe bwana unaanza kunigeuka, halafu....nimeshampa onyo, kuwa
kazi yake imekwisha, sitaki tena mahusiano na yeye na nimemwambia hii iwe siri,
kwani sijui kama litapokelewaje, maana kusema na kutenda ni vitu viwili tofauti…’akasema
‘Kupokelewa na nani, na huyo mke wake au sio, ni ngumu, halitaweza
kupokelewa vyema, hilo ndivyo ilivyo, najichukulia mwenyewe mimi, ..nisikie
mume wangu kafanya hivyo, mbona kutachimbia, sio rahisi kihivyo, ndio maana
nilitaka hili lifanyike kisiri na iwe siri yako, wewe…’nikasema
‘Mimi nilijua kutokana na ushauri wako, wewe upo radhi..na nilijua
hakutakuwa na matatizo, kwani ushauri wako ulikuwa wa kunitega mimi…’akasema
‘Sio wa kukutega bwana, wewe ndio umeharibu, ..hukufuata kama
nilivyokuagiza,..’nikasema
‘Mhh, kwa kauli hiyo, mimi naanza kuhisi uwoga fulani hivi,..maana
huwezi kujua msimamo wa mtu nafsini mwake,..na mimi ni jambo la mwisho
nililotaka litokee maisha mwangu, mimi sikupenda na sitaki kabisa kuharibu ndoa
za mtu. Nitaumia sana, itanifanya nihame huu mji…’akasema
‘Nio maana nilikutahadharisha kuwa hata hilo tendo, eeh, usije
kumfahamisha kuwa lengo lako ni nini..na mbegu ikiota usije kumwambia huyoo
mkulima…umenielewa hapo…’nikasema
‘Wewe ni rafiki yangu nakuamini sana, na siri hii unaifahamu wewe
tu kwa vile wewe ndiye mshauri wangu,….na kama ulivyonishauri wewe kuwa iwe
hivyo, ndivyo nilivyofanya, na kuanzia sasa itakwua hivyo, nimekosea huko
nyuma, sitaki nikosee tena…,’akasema na kutulia kidogo.
‘Sawa lakini niachosema hapa, eeh, ni wewe hukufanya nilivyotaka
mimi…’nikasema
‘Nasema hivyo wewe ulinishauri kuwa hata kama ni mume wa mtu,
nisijali kwa vile ni jambo la dharura, na nichague kwa marafiki zangu ambao
naona hawataniletea matatizo,..naomba unisikilize hapo kwa makini…’akasema
‘Sawa basi tutaliongea huko mbele, au sio, au unataka tuliongelee
humu kwenye gari nisimamishe kidogo, au
sio…?’ nikamuuliza na kusimamisha gari.
‘Hapana nataka nikuweke wazi tu,…kuwa mimi hata kufikia kulifanya
hilo haikuwa kazi rahisi kama unavyofikiria wewe..na nilijitahidi iwe hivyo,…kuwa
ni dharura tu, lakini ikashindikana maana ilikuwa kama natishwa sasa, usipo..nitamuambia..vitu
kama hivyo..unanielewa hapo…mimi sitaki nikuweke wazi kabisa,…maana nimeshaanza
kuogopa,… ila naomba usinilaumu kwa hili kabisa, nilifanya juhudi zote
ikashindikana…’akasema
‘Ndio maana nasema, kuanzia sasa usifanye jambo bila kuniuliza na
huyo mtu kama ingeliwezekana nilitaka awe anapitia kwangu, maana kwa hali yako
kwa sasa huhitajiki kukutana naye tena, unanielewa hapo, kuna kitu kinaitwa
kubemenda mtoto, uliwahi kusikia kitu kama hicho…, wengi wanakizarau, lakini
kina maana yake kubwa sana…’nikasema
‘Mimi wala sipo huko, huyo mtu ilitokea hivyo, na simtaki tena,
hata kumuona, nikiwa na mimba ndio nilikuwa natamani …sasa hivi, sitaki kabisa,
hata nikimuona naona aibu, nahisi dhambi,....na nitajitahidi kumfukuza
akija…’akasema
‘Lakini, sio nakualamu, haya yote umeyataka wewe, nilikushauri
vizuri tu,...sasa ni hivi, kwa vile keshajua, na amekuwa na kimbelembele chake,
kama atazidi kukufuata fuata, eeh, nina
wazo jingine…, usimwache hivi hivi, maana mtoto akikua anaweza kuanza kudai
baba yake ni nani…’nikasema
‘Unataka kusema nini…?’ akaniuliza akinitolea macho.
‘Naongelea hili nikiwa na maana ya hali halisi, ..mtoto utamficha
wewe kuwa baba yake ni nani, lakini jamii, itakuja kuligundua hilo, na mtoto
atakuja kuambiwa, wakati huo wewe umeshaumia sana,..kulea nk…sasa kama
anajilengesha kihivyo, basi, mbebeshe dhamana…. muwajibishe , sio kwamba
hatuwezi kumtunza, hapana, lakini ili aone kuwa na yeye anathamani fulani, na
ili asije kuharibu mpe bajeti yake..’nikasema.
‘Hapana, hapana,…hilo wazo siliafiki, kwa hilo tutakosana, mimi bado nipo kwenye
makubaliano yetu ya awali,…, naomba tuyalinde kabisa,..ndio nimeshaharibu
kidogo…lakini tusiendelee kuharibu zaidi, na …mimi naona hata kile nilichotaka
tukijadili kiishe tu, tuondoke tu….’akasema
‘Usitake kuniudhi, si umeshamuambia yeye…sasa hapo kuna siri gani
tena eeh, au mimi na yeye unayemthamini na kumuamini zaidi ni nani,…, mimi
nataka tuwe sawa, inachotakiwa kwa vile umeshaharibu , basi na huyo muhusika
naye awajibike kama baba, hutaweza kumtenganisha na huyo mtoto tena, huyo baba
anaweza kujitahidi kuonana na huyo mtoto, unajua kitakuja kutokea nini,…unielewe
hapo, …, hapo kwa hivi sasa hakuna siri,
kama tulivyopanaga awali….’nikasema
‘Mhh, hapana,….mimi sitaki
kumuhusisha huyo mwanaume na mtoto wangu, sitaki anisaidie kwa lolote lile,
mimi mwenyewe nilishajiandaa kwa hilo, nitajua jinsi gani ya kufanya,…na sitaki
mtu yoyote yule kubeba majukumu ya kumlea mwanangu, sitaki lawama na mtu…usije
kunielewe vibaya wewe ni rafiki yangu…’akasema
‘Kwanini unasema hivyo…?’ nikamuuliza
‘Huyu ni mtoto wangu, na lengo lake tulishaliweka bayana tokea
awali,…au sio… hata jina la baba yake nitaandika ukoo wetu, basi, mengine
tuyaache kama yalivyo,.....’akasema
‘Ulitakiwa ulifahamu hilo kabla hujamuhusisha huyo mtu, wewe ndio
umeharibu, nitarudia tena hilo mara nyingi ili uelewe,..na huenda hata sijui
kwanini ulimchagua mtu kama huyo ambaye sasa anakuja kukusumbua, labda kumbe
ungelinishirikisha na hilo, huenda hili lisingelitokea,…’nikasema
‘Ndio nakiri kuwa nimefanya makosa, lakini sitaki kuendelea
kuyafanya makosa zaidi,..na kumchagua huyo, niliangalia mambo mengi tu..urafiki wetu nk…,
na jingine kubwa ni usalama wangu na mtoto wangu,… lakini hata hivyo, yeye ni mume wa mtu, na kwangu mume wa mtu ni
sumu, hili kosa nililolifanya sasa naanza kulijutia,na kamwe sitarudia tena,
namuomba mungu anisamehe, na anisaidie…’akainama kama anajijutia.
‘Kwahiyo unataka kusemaje,…maana hapo ni kama unaniweka pembeni,
kuwa nisijihusishe na mambo yako tena, au…?’ nikamuuliza
‘Hapana sina maana hiyo, najua wewe ni muhusika mkuu wa hili, na
kwako nahitajia msaada mkubwa kwako… bila ya wewe bado nitakuwa kwenye wakati
mgumu, ..nashukuru kwa hilo, kuwa wewe ndiye umeliwezesha hili, kwa upande huo
napata faraja sana, kwani nimepata kile nilichokuwa nikikitaka, kabla sijafikia
miaka ya hatari ya kuzaa, ila mengine eeh, tuyaache kama yalivyo, ..’akatulia
huku akimwangalia mtoto.
‘Ok, japokuwa sijakuelewa….ngoja tufika nyumbani, na …najua hata
shemeji yako akikuona atakuulizia baba yake ni nani…mimi siwezi kumuambia
lolote hata kama ni mume wangu,..najua jinsi gani ya kumweka sawa…’nikasema
‘Nampenda sana mtoto wangu..kinachonisikitisha ni tendo lenyewe,
..sikupenda kutembea na mume wa mtu, sikupenda kabisa....ni mawazo yako
yaliniteka akili yangu, na sio kwamba nakulaumu kwa hilo,…lakini je yataisha
salama,…ninaanza kuingiwa na mashaka,… je hizo lawama hazitaendelea,, hapo ndio
naogopa zaidi…’akasema
‘Mimi sioni kwamba kuna tatizo hapo, nakulaumu tu kwa vile
hukutaka kufanya kama nilivyokuelekeza, na wasiwasi wangu ni kuwa huyo shemeji,
huyo mwanaume anaweza kuwa ndiye tatizo, na lisije kufika hadi kwa mke wake,
ndio hapo naogopa mimi…’nikasema
‘Oh, sijui…lakini kwanini….’akashika kichwa huku akimuangalia
mtoto wake…
‘Kwanini vipi tena, yaishe tutatafuta njia ….tukishirikiana
tutaliweka sawa,…na huenda ukampata mume ..ukimpata mume hili litajifunika
kabisa…’nikasema
‘Kumpata mume, wakati nimeshazaa tayari…mmmh, sijui,.. kuna wakati
mwingine nawazia mbali na kujiuliza, ni
kwanini mimi, na ina maana mimi nilitakiwa iwe hivi, nizae tu bila kuolewa, na
huenda nitaishia kuzalilika hivi…, na sasa naanza kuhisi uwoga ambao sikuwa nao…nilitarajia
hili litakuja kuisha kwa salama tu, na kwa hili nimejifunza kitu, sitarudia
tena makosa haya, huyu anatosha kabisa sitaki tena mwingine...’akasema.
‘Pole sana rafiki yangu, hiyo ndio ujue kwanini watu wanasema ni
nani kama mama,…sisi akina mama wakati mwingine tunabeba mzigo mnzito wa siri…usione
wakina mama wana watoto wengine wanawabebesha waume wao watoto sio wao, lakini
inabakia kuwa siri ya hadi kifo…ni maisha tu…’nikasema
‘Ndio maana, nataka nimlee
mtoto wangu peke yangu….’akasema
‘Hamna shida, lakini mimi nitakusaidia kadri ya uwezo wangu,
nahili litapita tu.., na mambo yatakuwa sawa tu…, kama tutashirikiana na
kuhakikisha huyo mwanaume hakusumbui na kujiweka kimbele mbele, kama ana mke
wake, aendelee kuwa na mkewe, kosa limtendeka, basi liishie hapo hapo….’nikasema
‘Na hapo ndio najikuta kujuta kuwa nimetenda kosa, kwanini
sikuchagua mtu mwingine zaidi ya huyo, nilijua huyo ndiye chagua sahihi, lakini
mmh, lakini `anyway’ cha muhimu ni kuwa kile nilichokitaka
nimekipata, na nashukuru sana kwa ushauri wako huo, wewe ni rafiki yangu mwema
sana, nakushukuru sana, mengine kwa sasa eeh, niachie mimi mwenyewe, usitake
kujua zaidi..’akaniambia.
Nikaangalia saa nikaona tumepoteza muda mwingi tukiongea, na muda
huo tulikuwa tumesimamisha gari, nikasema;
`Haya twende….kwahiyo sasa umeamua kuwa twende kwako, umeanza
kunikimbia rafiki yako kidogo kidogo, naanza kulihisi hivyo,…mimi nilipendelea huyu mtoto ikiwezekana akulie na
kulelewa pale kwangu, ili uwe na nafasi ya kuhangaika na shughuli nyingine ujue
wewe ni baba, na mama pia…’nikasema
‘Hapana….nataka nikakae kwangu…’akasema
‘Unajua niliposikia umejifungua, nikawaza huyo mtoto akiwa kwangu,
na mabinti zangu waanavyopenda watoto, nikajua huyo atakuwa sehemu ya watoto
wetu, sijawaambia na wakisikia, sijui itakuwaje, watafurahi sana, watataka
wakae na kaka yao… , mdogo wao,
anayefanana na wao, kwanini unapinga wazo langu...’ nikamuuliza .
‘Unajua hata huyo shemeji, alipofika hapa alisema hivyo hivyo…’akasema
na akawa kama kasahau kitu akashika mdomo.
‘Alisemaje…?’ nikamuuliza, na akasita kidogo, baadaye akasema
‘Hamna shida …’akasema
‘Mimi sitaki hiyo tabia, ya kuongea jambo, halafu unaghairi, hujui
unaniweka kwenye wakati mgumu wa kuwawa waza, usingelikuwa wewe ni rafiki
yangu, ningelikufikiria vibaya…’nikasema
‘Alisema hivi, kaamua kuacha shughuli zake kwa ajili yangu, kwa
ajili ya mtoto, kwahiyo nisikatae yeye kunichukua hadi nyumbani…..sipendi
kufuatana naye tena, nimemkatalia, na ungelifika mapema mngelikutana naye hapa,
sijui ingekuwaje, na mimi sikulitaka hilo,....nimemuonya kuwa sitaki anifuate
fuate tena, lakini namuona kama kapagawa,hasa alipomuona mtoto utafikiri
hana mke na watoto..’akaniambia..
‘Mhh, kwani yeye ana watoto wangapi…?’ nikamuuliza
‘Anaaaah, mh, ana watoto wawili wa kike…’akasema
‘Kama mimi, wewe una hatari kweli, kwanini ukachagua mwanaume sawa
na mume wangu, hahaha, nimekugundua, wewe unataka kila kitu tuwe sawa, lakini
umezaa wa kiume na sio mapacha, yote ni heri tu au sio….’nikasema
Akatabasamu….na kuangalia
pembeni, halafu akasema;
‘Aaah mimi sijui, nilichotaka ni mtoto, sasa kama kuna mtu
anapenda mtoto wa kike au mtoto wa kiume, mimi sina wazo hilo,…hilo kwangu
halikuwa na sababu niliongea mengine wakati ule kuwa nataka awe hivi na vile
lakini …ilikuwa ni kuonga tu, sasa hivi naona mtoto ni mtoto tu…hayo ya mtoto
gani, wa kiume au wa kike, ni mawazo ya mtu binafsi, na sitaki hata kuyasikia,
...’akasema
Na tukaondoka kuelekea nyumbani kwake, maana alikataa kabisa
niende naye kwangu, sikutaka kumlazimisha zaidi… na mara simu yangu ikalia, alikuwa na mume
wangu, nikapokea,
‘Nimekuwa nikikupigia lakini ukawa hupatikani, simu yako muda wote
inatumika, vipi ulikwenda kumuona mzazi uliyesema unakwenda kumuona..?’
nikamuuliza
Akasema ndio, ameshamuona tayari, ila anaweza akaenda huko
nyumbani kwake, kuna mambo anataka kuyaweka sawa….
‘Kajifungua mtoto gani, mambo gani tena kwani ana udugu na familia yenu….?’ Nikamuuliza, akasema mtoto
wa kiume, hakusema zaidi
‘Oh, nahisi umeona wivu sana kwa vile ni mtoto wa kiume na wewe
unataka mtoto wa kiume nikuambie kitu hata huyu rafiki yangu kajifungua mtoto
wa kiume…yaani we acha tu,..na sisi tukijaliwa tutampata tu, mtoto au watoto wa
kiume hahaha, mume wangu, usiwe na wivu,.. …unasemaje…, sijakusikia vyema…’
nikasema kuna kitu aliongea lakini sikukisikia vyema
Baadae akaniuliza nikitoka huko nitakwenda wapi, au nitarudi
nyumbani muda gani, nikasema;
‘Sijajua, ila nikimfikisha huyu mzazi kwake, naweza kurudi
nyumbani mara moja kuhakikisha shughuli zangu zinakwenda vyema, baadae naweza nikurudi tena
kuhakikisha kuwa mzazi yupo na mtu, au nikusubirie huko kwa mzazi, unasemaje,
utakuja saa ngapi, ?’ nikamuuliza, na hakujibu mara moja nikazidi kumuambia
‘Ni vizuri uwe wa awali awali, njooo bwana kwani upo wapi, kazini…’nikamuuliza,
akasema yupo njiani, barabarani,…
Mara akageuza mazungumzo na
kuanza kuniuliza mambo mengine ya kikazi, na baadae nikamuuliza tena
‘Sasa utakuja huji, …mbona hujanijibu swali langu…’nikamuuliza na yeye
cha ajabu akaniuliza kuja wapi....,
‘Hivi upo sawa wewe, tunajadili kuhusu rafiki yangu, huyu ni mtu
muhimu sana kwangu, kama upo na shughuli zako sawa, lakini nilitaka uje unikute
hapa, kuna mambo nilitaka tuyajadili pamoja …’nikasema akauliza mambo gani
‘Ukifika nitakuambia…kwahiyo unasemaje utakuja, ni muhimu sana
kwangu…kuna kitu nimekigundua, na…ungelikuja …eeh, unasema, …mbona una mumunya
maneno, sikuelewi, …nimefanya makosa gani, hebu uje….kwanini sasa…’nikasema na
yeye akasema kwa hivi sasa hana nafsi, niwahi kurudi nyumbani kwani kuna jambo
muhimu anahitajia tulijadili mimi na yeye, nikamuuliza jambo gani, hakujibu hapo hapo, ….baadae akasema;
‘Njoo haraka nyumbani nakusubiria…’
‘Ok nakuja…’nikasema
NB: Haya mambo yanaanza kujipika
WAZO LA LEO: Tunaweza kupanga mambo yetu, lakini yawe
ya heri, tukipanga mambo yenye ‘shari’ ndani yake, shari hiyo hiyo inaweza ikawa
ni sababu ya kuharibu hayo mambo. Hatutafanikia,na hata tukifanikiwa, shari bado
itatusakama kwenye maisha yetu. Tusisahau kuwa tukiwa wawili, mwenyezimungu
yupo nasi, ..kwahiyo hatuwezi kuficha mambo yetu. Ni bora tujitahidi sana
kukwepa mambo mabaya, na kujadili mambo yenye heri, ambayo yatakuja kuleta
baraka kwenye maisha yetu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment