Mume wangu aliponiambia yupo barabarani, nikakumbuka kitu, wakati
tunatoka pale hospitalini, ..japokuwa sina uhakika sana, niliona kama gari la
mume wangu likitoka,..unajua gari langu niliegesha sehemu ya nyuma ya jengo la
hospitali…
Hapo nikawaza jambo, huenda mume wangu alikwenda kumuona mzazi
hapo hapo hospitalini, ..sikuweza kukumbuka kumuuliza huyo mzazi alilazwa
hospitalini gani, kama ningelijua kumbe ingelikuwa ni rahisi tu, ningelimuita
aje tumuone rafiki yangu.
Lakini haikuwa na umuhimu kwa muda huo…
Tuendelee na kisa chetu…
**********
‘Mhh, aisee, mtoto wako anafanana sana na watoto wangu, sasa
nimemwangalia kwa makini, mwanzoni nilijua ni kwa vile watoto wachanga huwa
wanafanana sana wanapozaliwa…, lakini kwa huyu, nimehakikisha, anafanana sana
na watoto wangu, isingelikuwa wewe ni rafiki yangu,… ndugu yengu, ningelifikiria
vibaya, lakini sizani kama wewe unaweza kufanya hivyo hahaha, sina mawazo hayo
mabaya, samahani…’nikasema
‘Kufanyaje…?’ akauliza akikwepa kuniangalia
‘Hebu tuyaache hayo, haya niambie ilikuwaje, ni nani huyo shemeji
, maana umekuwa ukisema tu shemeji, shemeji, unajia nikuambie kitu, kila hatua
navutika kufahamu ukweli, niambie nisibakie hewani, maana kiukweli umeweza…,
hujafanya makosa, na umekipata kile ulichokitaka, mimi nakuaminia, sikufanya
makosa kukushauri…’nikasema
‘Nikuambie nini tena rafiki yangu nimeshakuambia,… kosa la awali
sitaki kulirudia tena, kuna kauli zako zimenitisha amani…, naona hata ushauri
wako, haukuwa na usawa kivile…, ulinishauri tu, kwa kunifurahisha…’akasema
akinikwepa kuniangalia machoni.
‘Mhh, sijakuelewa, hapo una maana gani, ina maana mimi nilifanya
makosa kukushauri hivyo au….rafiki yangu hapo sasa wanifanya nitake uniambie
ukweli,…sasa niambie ukweli, tusije kuudhiana bure…unanifahamu nilivyo, subira
yangu ni kubwa lakini ikifikia mahali …inakuwa siwezi tena,.., unanifanya
nianze kuvuta hisia ambazo hazipo na mimi sio mtu wa namna hiyo , hasa kwako..’nikasema
Rafiki yangu akabakia kimia, halafu akamuangalia mtoto wake, kwa
muda huo nilikuwa naye mimi, ….akasogea na kumchukua, na mimi nikajiweka sawa,
kusubiria maelezo,, namfahamu rafiki yangu huyo, akiamua jambo lake , kaamua,
lakini pia ananifahamumimi nilivyo, nikisisitiza kitu ujue kweli ninakitaka,
sio kawaida yangu kusisitiza kitu, kama hakina umuhimu,
Alitulia kidogo huku akimuangalia mtoto wake,…ilikuwa kama yupo
kwenye wakatimgumu sana, nilitaka kumuambia basi, asiumize kichwa, lakini mimi
nitakuwa sina amani, sio amani ya kutokumuamini, mimi namuamini sana rafiki
yangu huyo,..ila hali ile ilinifanya intake nimfahamu tu huyo mwanaume aliyempa
mimba sijui kwanini,
Baadae rafiki yangu akainua uso na kuniangalia,….uso ulikuwa
kwenye hisia, ni kama mtu anayehisi maumivu, na kiukweli sikutaka mjadala huo
uendelee, naona namtesa, lakini yeye baadae akasema;
‘Kwanini unataka niendelee kuharibu, si wewe ulishaanza kunilaumu
kuwa nimeharibu, sasa kwanini tuendelee kufany ahivyo tena…?’ akaniuliza
‘Hapana…hata mimi sikulitaka hilo, ila hizo kauli zako, kauli zako
zenyewe zinakusuta, zinavuta hisia nyingine kabisa,....nahisi kuna jambo
unanificha, … isije ukawa kweli umetembea na mdogo wa mume wangu, hapana kama
ulifnaya hivyo, sio vizuri, sijui lakini...!'nikasema na yeye hapo akacheka
kidogo, na kilikuwa sio kicheko kile cha furaha ni kama kulazimisha hivi, yeye baadaye
akasema;
'Hapana sijatembea naye, na kwanini…hahaha, hapana…bwana, na wewe
mawazo yako ….katika wote, …huyo sikuwa na mpango naye kabisa, unajua aliwahi
kunitongoza kipindi fulani, unakumbuka nilikuambia…na tulivyokosana naye pale,
ikawa basi tena tatizo lake…, hajui kubembeleza, analazimisha, alihisi mimi ni
muhuni, tokea kipindi kile sijawahi kuwa na uhusiano naye wa karibu,
nikusalimiana tu kama tukikutana,…kiukweli, siwezi kuficha, awali nilitamani
sana awe rafiki yangu, sasa alipokuja kuoa ndio ikawa basi, nikamtoa kabisa
akilini mwangu...’akasema sasa kwa kujiamini.
‘Ulimtoa sasa ukamtafuta …hahaha, wewe bwana, nakufahamu ulivyo,
ukitaka jambo lako hushindwi…au uniambie ukweli, ulimpata wapi mwanaume
anayefanana na mume wangu,…na ni nani huyo, hapo ….sikuachii,… kama sio huyo
basi ni nani mwingine,…niambie ukweli rafiki yangu..usiniache njia panda…’nikasema
‘Unajua …hadi hapa nakuona kama huna amani na mimi, na ndio maana
najiuliza ule ushauri wako ulikuwa wa nini hasa, kweli ulitoka moyoni,….sasa nafikia
kuogopa,..ni kweli, wewe ni rafiki yangu mkubwa sana, na mara nyingi tumekuwa
tukishauriana mambo mengi, na mara nyingi wazo lako huwa nalichukulia kwa uzito
mkubwa sana, …sikutaka nikufiche kwa hili, kabisa, nilipanga nikuambie kila
kitu, lakini naona bora tuyaache tu, kwa usawa wa urafiki wetu..’akaniambia na
mimi hapo nikasimama.
‘Hapana wewe niambie tu, ….usiponiambia moyo wangu utakuwa hauna
amani….kiukweli ndio hivyo, sio kwamba nakudhania vibaya, katu wewe siwezi
kukuweka huko huwezi na hutaweza, ila nataka kumfahamu huyo mtu tu..basi, ili
niweze kukusaidia….’nikasema
‘Unakumbuka, niliwahi kukuambia kuwa nawapenda sana watoto
wako, na ningelifurahia kupata watoto kama wako…hilo lilitoka ndani ya nafsi
yangu, ni kweli nawapenda sana watoto wako, na mimi nilitamani nipate watoto
wanaofanana na watoto wako…’akamuangalia mtoto wake.
‘Na…, na uliponishauri hivyo, ..mimi nikaona nifanye juhudi za
kumpata mtu atakayenizalia mtoto kama wako, na muda huo nilikuwa natamani nipate
mapacha, kama wa kwako, ....’akasema na mimi nikamuitikia kwa kichwa na yeye
akaendelea kuongea kwa kusema;
‘Nililiwazia sana hilo,…sasa nifanyeje,…ndio nikaanza kuwachuja
watu ninao watamani, maana sio kupenda…siwezi kusema nilimtafuta nimpendaye, …hivi
utampandaje mume wa mtu,nikaona nisicheze mbali,…kiukweli, sisi ni
marafiki wa kweli na tunaweza kufichiana siri...au sio rafiki yangu…?’
akaniuliza na mimi nikatikisa kichwa, .
‘Wewe na mimi ni kama pete na kidole….au sio…na umkuwa ukinipa
kila ulicho nacho, na mimi halikadhalika, ilimradi tuchangiane kwa …urafiki
wetu, hilo lipo wazi, wapo waliowahi kusema urafiki wa namna hiyo hawautaki…eti
haufai, lakini mimi sioni kama kuna ubaya, au sio …?'akasema huku akisimama na kumlaza
huyo mtoto kwenye kitanda chake chenye chandarua,
Unajua kiukweli, wengi watashangaa kwa hili, lakini kwangu mimi akili
ilifungwa kabisa kumdhania vibaya rafiki
yangu..kabisa kabisa, rafiki yangu nilimchukulia kama mdogo wangu, kwahiyo
nisingeliweza kumfikiria chochote kile,…, hata alipotoa kauli hiyo sikuwa na
mawazo yoyote mabaya, mimi akili yangu ilifikiria kwingine kabisa,…nikasema
‘Sasa kwanini inanificha, unanificha hata mimi rafiki yako,
nilijua tu..’nikasema hivyo, na yeye akanitupia jicho kidogo, na kusema;
‘Unajua sikutaka kukuambia moja kwa moja, kutokana na kauli yako
uliyoitoa awali, nikaona bora nisiseme ukweli, hata hivyo….’akasema hivyo na
kukatisha, huko kukatisha katisha maneno kwake, ndio kulikuwa kunanipa hamasa
ambayo haikuwepo kichwani kwangu kabisa. Hata hivyo sio hamsa ya kumdhania
ubaya, hivi ndugi yako anaweza kutembea na mume wako,..kiuhalisia…hasa awe ni
ndugu unayemuamini….huwezi kufikiria hilo kabisa.
‘Lakini yule ni mdogo wa mume wangu huoni italeta picha mbaya…’nikasema ,
na yeye akanitupia jicho kwa sura ya kushangaa, akasema;
‘Hahaha… rafiki yangu, mbona hivi…mimi siwezi kukuficha, na …hebu
tuyaache hayo jamani,…’akasema akionyesha ile ishara ya mikono ya kuupia jambo.
'Ni kweli kabisa sisi ni marafiki wa kweli...na hatuwezi
kuangushana, lako ni langu na langu ni lako..nakubaliana na wewe, na wala usiwe
na shaka na mimi, …mimi naona ajabu wewe kuogopa kuniambia ukweli, ….sasa
nimeshaujua, hata kama, japokuwa bado nahitajia uhakiki wako,…mimi kama mimi nakuahidi kabisa, hilo litaishia moyoni, na
hakuna mwingine anayeweza kufalifahamu hilo zaidi yako na mimi,..na huyu
uliyemuambia ukaharibu, hilo nakuthibitishia...'nikasema huku nikiweka kidole
mdomo kama ishara ya kuahidi
‘Hahaha kweli rafiki yangu, mmh, mbona nitashukuru, ila sio huyo jamani,
unayemfikiria wewe, haaah, mimi hapo siwezi kuelewa, nilijua una..umeshafahamu,
maana ..aah, sasa hata sijui nisemeji,…kwanini huelewi….’akasema
‘Nimeshaelewa, nakushangaa leo ulimi wako unakuwa mnzito tu…imeshapita
hiyo na maji yakimwagika hayazoleki labda yamwagike kwenye udogo wa mfinyazi
uliokauka…hahaha…uliposema tu kuwa hukutaka kucheza mbali, basi hapo imejieleza
kila kitu, usiwe shaka kabisa, mimi nimelipokea kwa moyo mmoja..., na wewe
bwana kwa kupenda stori ndefu, kwanini usiningeliniambia tu moja kwa moja
kwa shemeji ndiye kayafanya hayo, basi, limekwisha, au….’nikasema
‘Tafadhali mimi nakuomba, tuyaache….’akasema
‘Tuyaache mbona unasema hivyo tena, au, …?’ nikauliza kwa
kushangaa maana mpaka hapo nilishaamini kuwa ni mdogo wa mume wangu, ..yeye
akabakia kimia, akiwa kainamisha kichwa chini.
‘Ina maana sio yeye, au…unaogopa nini kuniambia…?’ nikamuuliza
‘Tuyaache jamani…’akasema akitikisa kichwa.
‘Mimi nauliza tu, kama sio mdogo wa mume wangu ni nani mwingine
anayefanana na mume wangu…, maana sasa unaanza kuniweka roho juu, kama tumechangia
kuna ubaya gani, limetokea limetokea, eeh,....kwanini unaogopa kusema huo ukweli
kuwa tumechangia, siwezi kukulaumu zaidi, ..najua wewe ni rafiki yangu,
kuchangia, tunachangia sana, au sio,…sasa itakuwa …, mimi mkubwa na wewe mdogo
mtu au…?’ nikasema na kuuliza.
‘Kama wewe ni rafiki wa kweli sizani kama hili jambo litakukwaza,
ndivyo nilivyokuwa nimefikiria hivyo,…na…na…, na kama kweli ulikuwa na nia
njema na wazo lako natumai hutaniona kuwa mimi ni mtu mbaya, kwani yote niliyafanya kwa
kufuata ushauri wako…. Zaidi ya hayo kuna kukosea, nimekubali nimekosea
kuliweka hili bayana mapema…na kiukweli , hata mimi sikupenda iwe hivyo kwa
hali hiyo, ila ningefanyaje basi, mmh, …’akasema
‘Sijasema, au kukulaumu kwa hili kuwa umekosea kumchagua huyo…sawa lakini picha kwa jamii, ndio maana
nilisisitiza sana usiri..jamii itatuelewaje au sio…, ninachojiuliza ni kwanini
unifiche kitu kama hiki ambacho watu baadae watakuja kujiuliza na wengine
watapa mwanya wa kusema la kusema…sasa ni vyema ningelijua mapema ili tuweze
kuweka, kinga…’nikasema
‘Mimi nilikuamini sana rafiki yangu kwa ushauri wako, nikaona
ngoja nifanye kama ulivyonishauri...sizani kama nimekosea jambo, ni ushauri
wako ndio umefanikisha hili, na...na nitafurahia sana na wewe ukilipokea hili
kwa moyo mkunjufu...ndio maana sitaki nikufiche kitu...’akasema
‘Kiukweli umefanya jambo la maana sana, kwani hivi ndivyo
nilivyotaka,…. Uzae uapate mtoto na wewe…, maana mtoto ana raha zake, wewe
mwenyewe utaona, utakuja kuniambia…sitawezi kukulaumu kwa vyovoye vile, maana
ndivyo nilivyotaka mimi iwe hivyo, na kwanini nikwazike kwa hili ilihali wewe
ni rafiki yangu kipenzi na pia hilo wazo nilikupa mimi. Nikuambie ukweli wazo
hilo nililiwazia sana kabla sijakushauri,na lilitoka ndani ya moyo wangu, nipo
tayari kukusaidia kwa vyovyote vile….’nikasema kwa kujiamini.
‘Basi kwa vile umenihakikishia hilo na wewe ni rafiki yangu
mpenzi, nitakuambia kila kitu bila kukificha, ila nakuomba uwe mkweli wa kauli
yako hiyo,..kuwa utalipokea kwa moyo mkunjufua…na nanomba iendelee kuwa ni siri
kati yangu mimi na wewe, ama kuhusu shemeji, basi, tutaona jinsi ya kufanya au
sio …’akasema
‘Hapo sasa umenena, na …unajua yule haivani sana na kaka yake,
kwahiyo sina mazoea naye sana, usiwe na shaka na hilo, na tutajua jinsi gani ya
kumbana kiasi kwamba hatafunua mdomo wake, anamuogopa sana mke wake yule,
unasikia…’nikasema
‘Tatizo, ….moyo unaniuma, na naingiwa na uwoga, sipendi kabisa urafiki
wetu uje kuharibika kwa hili, nakuomba sana, maana sijui nitauweka wapi uso
wangu kama wewe ukiamua kunisaliti, ukanitangaza vibaya kwa watu, nitavunjika
moyo wangu sana tena san,… kama …oh, kama…wewe utafanya hivyo, lakini zaidi ya
hayo nitaumia sana kama hili litakukwaza na kukuumiza…nakuomba sana, tena sana….for
the sake of this baby…uwe mkweli kwa akuli yako hiyo’akasema akimwangalia
mtoto wake.
‘Kwanini unasema hivyo rafiki yangu kama vile huniamini au mimi
siakuelewa hapo,..kwa hili nakuhakikishia kuwa tupo pamoja…hili nimekushauri
mimi na nitakuwa mtu wa ajabu kama nitakulamu kwa lolote lile…wewe niambie
tu,na nimeshajua ila ni uhakika wako…mimi nakuhakikishia kuwa tutakuwa pamoja
kwa lolote lile, si ndio hivyo…mmh, sasa moyo umetulia...’nikatulia kidogo
Yeye akatulia na mara alipoinu akichwa na kuniangalia nikaona
machozi yanamtoka,…hapo nikashikwa na mshangao kidogo, sio rahisi kwa rafiki
yangu kutoa machozi, akitoa machozi ujue limemfika kweli, kama mwanamke
inatokea…hapo mimi kwa huruma nikamsogelea, na kumshika, tukawa kama
tumekumbatiaana kiupande upande…alitulia kwa muda, halafu akasema;
‘Rafiki yangu,.oooh, naumia, ….mimi ...nakuomba tuliache hili tu,
nakuomba tena na tena, tuliache kama lilivyo, …sitaki,..na … nitaumia sana
ikija kutokea kinyume na …..ulivyosema, ulivyoahidi, naogopa sana, kumbuka
rafiki yangu ahadi ni deni, ulinishauri wewe, kumbuka hilo….’akasema
‘Hili ninakuthibitishia kutoka moyoni mwangu…, sizani kama huyo
mke wa shemeji atalijua hili..zipo namna nyingi ya kulificha…tutashauriana muda
ukifika…huyo hatajua kabisa …maana akijua vumbi lake naye sio mchezo…’nikasema
‘Hapo ndio waanza kuniogopesha…’akasema
‘Hatajua bwana…usiogope kabisa..nani atamuambia…mimi nakuahidi kama
rafiki yako , mimi nipo tayari kupitisha rupia,… ikibidi…japokuwa ni mkali,
lakini namfahamu madhaifu yake,…yule
mwanamke anapenda sana pesa,...usiogope kabisa...mimi na wewe hakitaharibiki
kitu,..na kwanini ulie, hebu nikuulize, niambie ukweli ni nani mwingine analijua
hili….ni mimi na wewe tu au sio, usije kuwaambia hata wazazi wako unasikia,
ukiharibu tena huko shauri lako..’nikasema.
‘Oh, basi …mimi naona unipe muda,… niliwazie hili zaidi,
nitakuambia kila kitu, usijali, sasa hivi akili yangu haipo sawa....nashukuru
sana rafiki yangu…ningeomba nikapumzika, au…sio nakufukuza..jamani…ila kumbuka
tu ahadi ni deni..’akasema
‘Mimi nimeshakuambia hakuna kitu kitaharibika niamini mimi rafiki
yako, kwanini nikuahidi kitu halafu nije kukusaliti, haitatokea kabisa,
nakupenda sana..wewe ni sawa na mdogo wangu kabisa….hata mume wangu namuambiaga
hivyo, na kila nikitaja majina ya wadogo
zangu na wewe nakutaja, uone ninavyokuthamini, najua wewe huwezi kufanya jambo
la kuniumiza mimi au mimi kufanya jambo la kukuumiza wewe….’nikasema
‘Mhh…hapo sasa….’akasema
‘Ndio hivyo…kwahiyo mimi
siwezi kuja kukasirika eti kwa vile umefanya hivyo kwa shemeji…, hapana
na kama wazo nilitoa mimi eeh, kwanini
nije kuumia,…hapana nikifanya hivyo, itakuwa ni ujinga, …siwezi na sitaweza kukusaliti,
unasikia, sawa…kama wahitajia kupumzika basi wewe pumzika, sijui nikufanyie
nini kwa hivi sasa…’nikasema
Na mara simu yake ikaingia ujumbe, akaichukua na kuusoma, halafu
akanitupia jicho, na mimi nikajifanya kama sikumuona, akawa anaandika kitu
kwenye simu yake, nahisi alikuwa akijibu huo ujumbe wa simu, halafu akasema;
‘Mimi naona wewe uende tu, usiwe na shaka na mimi, ndugu yangu
anakuja, na nikikuhitajia nitakuambia, usiache shughuli zako, mimi nafahamu
sana shughuli zako zilivyo, kazi kwanza au sio, hata mimi sizani kama
nitajilaza tu kwa vile nimejifngua, mwili wangu ni kuhangaika sio wa kulala
lala…’akasema
‘Sawa mimi naondoka naona hata mume wangu ananisisitiza kwa ujumbe
wa maneno kuwa niwahi nyumbani …na nikichelewa sitamkuta, sijui ana jambo gani
muhimu kihivyo..ngoja niondoke ..haya ..ooh, baby kalala, hivi jina bado eeh,
..’nikasema
‘Adamu….’akasema
‘Safi kabisa, …ooh,babu Adam…bakia kwa amani eeh, …’nikasema
nikipitisha mkono na kumshika kwa mbali kichwani, na taswira ile ile ya watoto
wangu wakiwa wachanga ikanijia, ..sijui kwanini….na simu ya rafiki yangu ikawa
inaita, ..aliangalia mpigaji, halafu akaniangalia,
Mimi nikasema
‘Haya mimi naondoka, wewe endelea, nitarudi…’nikasema na akawa
kama anataka kunizuia, nisiondoke, nilijua anataka kuniaga huku anataka kuongea
na simu, nikasema
‘Wewe endelea usijali na wala usinisindikize…, nikatoka kwa
haraka, nikiwahi kwenye gari langu, na..kuanza kutoka, na wakati natoka, gari
kama la mume wangu likawa linakuja, …ikanifanya nisimame, nihakikishe kuwa ndio
lenyewe, na linakwenda wapi…
WAZO LA LEO:
Ni rahisi sana kutamka neno, hasa la kuahidi, na hata kuapa kuwa nitaweza
kutimiza malengo au kutimiza jambo fulani vyovyote iwavyo. Ni vyema, tukawa na
uhakika na kauli zetu hizo, na kama hujalifahamu jambo sio vyema kuahidi kuwa
ni lazima ufanya hivyo, `lazima’ sio kauli nzuri. Tukumbuke kuwa Ahadi ni deni,
na ukiahidi jambo ujue unahitajika kulitekeleza, na ukikiuka ujue umehini ahadi
yako, ni hiyo ni tabia ya mnafiki.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment