Ikapita wiki, kutokana na shughuli za kazi nyingi, nikawa kama
nimeshamsahau rafiki yangu huyo, na nikawa na migongano ya hapa na pale ya
kifamilia, ni kawaida, lakini safari hi ilizidi, maana mume wangu ratiba zake
zikawa hazieleweki sio kama ilivyokuwa awali, tukawa tunabishana, lakini kwangu
nilichukulia ni mambo na kawaida tu.
Basi siku moja nikapokea
simu kutoka kwa huyo rafiki yangu, akaniambia kuwa anajiandaa kuondoka kwenda
Zanzibar, kuna mambo muhimu anatakiwa kuyafuatilia
‘Mambo gani mbona mapema hivyo…?’ nikamuuliza
‘Kuna jambo natakiwa kwenda kulifanya, natakiwa kukabidhi kabidhi ofisi,
kwani inawezekana nikasafiri kwenda kusoma
nje ya nchi…niliwahi kukuambia kipindi fulani kuwa niliomba kwenda kusoma, sasa
imetokea kipindi hiki na mimi siwezi kuachia hiyo nafasi,…’akasema nilitaka
kumuuliza na mtoto vipi, nikasita yeye akasema
‘Na uzuri..haitakuwa muda wote, nitaweza kulea na kusoma, mfadhili
wangu kasema hilo halina shida..kwahiyo sitakuwa na muda wa kukabidhi, nikimaliza
likizo yangu ya maternity, yawezekana nikaondokea huku….’akasema
Ilinisthua kidogo, ikizingatiwa kuwa mtoto bado mdogo,
sikumuulizia sana kuhus mtoto,…. kwasababu hapa kati kati tulifikia sehemu
hatuelewani na yeye kabisa, alichoka na maswali yangu na hata kufikia kusema niache kumfuta fuata
masiha yake na mtoto wake.., kauli hiyo ikaniudhi sana, ikabidi kweli nimuache
na maisha yake. Hata hivyo kiukweli, sio kwasababu hiyo, ila sikuwa na muda wa
kukutana naye mara kwa mara, majukumu yalizidi sana.
Tuliongea kidogo kwenye simu …tukamaliza hivyo tu, na sikuweza
kumpigia tena , na siku mbili baadae akapiga yeye, nahisi ni pale aliponiona
nipo kimia, akasema;
‘Rafiki yangu vipi, nilijua utakuja, kabla sijaondoka, si
nilikupigia simu jamani, sawa najua labda, bado umenikasirikia,… lakini utakuja
kuelewa tu, baadae, …ila nilikuwa na ombi moja kwako, kwa vile wewe nyumba yako
ina nafasi naomba baadhi ya vitu vyangu nije kuviweka kwako maana hizi nyumba
za kupanga nikiondoka, vitakuwa havina usalama kabisa....’akasema
Kiukweli mimi sikuwa na hasira kihivyo, hasira zangu ni za hapo
kwa hapo..na ukiniudhi naweza kufanya jambo kubwa hapo hapo…baada ya hapo,
mambo yamekwisha, ila …kiukweli naweza kufany ajambo baya huwezi amini,..mimi
kwa hilo nilishaliondoa nafsini kwangu sikuwa na kinyongo na yeye,..nikasema
hakuna shida, nyumbani kwangu ni kwake, nikazidi kumsisitizia kwa kusema;
‘Wewe ni rafiki yangu bwana, hakuna haja ya kuniomba, hapa ni nyumbani
kwako pia, watoto wanakuulizia kila siku, wewe lete vitu vyako na wewe kama
mkataba umekwisha kwenye hiyo nyumba haina haja ya kulipia tena, njoo ukae
hapa, mapak siku ukiondoka, ...’nikamwambia.
‘Hapana, sina maana hiyo, na sitaweza kufanya hivyo, urafiki wangu
usiwe mzigo kwako, umeshanisaidia mengi sana, kiasi kwamba najihisi vibaya, na
..hata sijui nitawezaje kulipia hayo,…. ninachokuomba kwa sasa ni hilo
tu....’akasema.
‘Sawa hamna shida, wewe vilete wakati wowote utakapopata nafasi,
au nikipta nafasi, hata kama wewe haupo ninaweza kuja au kutuma gari likaja
kuvichukua haina haja ya kusumbuka sana, ila nitajitahidi nije kabla hujaondoka..’nikasema,
nikiwa na mambo yangu mengi shughuli zangu, na sikutaka kuongea naye zaidi,
hasa kuhusu maisha yake alishasema hataki nikikutana naye tuyaongelee maisha
yake, hasa kuhusu mtoto na aliyezaa naye.
Kesho yake nikapata nafsi nikaona nimpitie kidogom, nijua
kinachoendelea, na kama vitu hivyo sio vingi, na kaviandaa, basi ninaweza
kuondoka navyo, kwa kukodi gari, sikutaka kumpigia simu, mimi mwenyewe nikaenda
nyumbani kwake…kwa mbali niliona gari kama ya mume wangu, lakini sikuwa na
uhakika kama ilitokea kwake, au ilikuwa inapita tu, na mume wangu alikuwa
kwenye mkutano.
‘Hivi mkutano ulishamalizika,..au kuna mtu kamtuma na gari lake…?’
nikajiuliza, nikataka kupiga simu kwake, lakini ikaingia simu ya mteja wangu
muhimu, nikajikuta naipokea kwanza, na nilipomaliza kuongea naye , nikiwa
nimesimamisha gari nyumbani kwa rafiki yangu,..nikawa nimeshaua kumpigia simu
mume wangu
Rafiki yangu alikuwa kasimama mlangoni kwake kunikaribisha,
nikamsogelea tukasalimiana kama ada yetu, nikaingia ndani na swali la kwanza
likawa hili.
‘Mtoto kalala…?’ nikamuuliza
‘Ndio….’ Akasema ile ya kulazimishwa, sio sauti kama ile niliyo-izoea,
halafu akauliza
‘Hujakutana na….’akasita,kwani simu yake iliita, akaisikiliza
kwanza kwa muda, akasema
‘Nimekuelewa hamna shida, lakini niache kwanza, sitaki, sikiliza,
nilikuelezea, msimamo wangu basi…’akasema na kukata simu.
Alionekana kama ana hasira na hataki kuongea, akawa kama anataka
kuniambia jambo lakini anasita, nilihisi hivyo, ila na mimi nikasimamia kwenye
msimamo wangu kuwa sitamuuliza tena kuhusu maisha yake na mtoto, …kwa jinsi
alivyo nilijua ana tatizo.
Baadae mtoto akawa analia, kwahiyo akaenda kumchukua, na
kumnyonyesha alipomaliza, akanipa nimpakate ili aniandalie kinywaji, ndivyo tulivyozoeana
, nilitaka kujiandalia mimi mwenyewe, maana anajua mimi ni mpenzi wa sharubati
ya baridi,… lakini akasema hapana
‘Wewe mpakate mtoto ..hujamshika tokea siku ile….’akasema na mimi
sikukataa nikamchukua mtoto.
Unajua mtoto wa mwenzako hakawii, sasa anageuza macho, anangalia,
na sura halisi inaanza kuonekana, sura haikujificha alikuwa akifanana kila kitu
na watoto wangu, maana watoto wangu wanafanana, ni wale mapacha wanaofanana kwa
kila kitu, mimi akilini nikaweza hitimisho kuwa rafiki yangu atakuwa atakuwa
katembea na mdogo wa mume wangu. Hata hivyo sikuweza kuvumilia nikamwambia;
‘Hapa sasa haijifichi kitu, lakini tuyaache hayo, lini unaleta
hiyo mizigo, au nitafute mtu tupakie, kukurahisishia kazi…’nikasema
‘Haijifichi nini, usianze yale mazungumzo tena, nimefikiria kwa
makini nimeona, ni bora iwe hivyo, libakie kama tulivyokuliana basi… sasa
ibakie utakavyofikiria wewe inatosha,..’akasema.
‘Hamna shida, isiwe taabu, sasa unasemaje…?’ nikamuuliza
‘Nilitamtafuta ,mtu, kuna mambo sijayaweka sawa, kuna mtu
ananisumbua akili yangu, sipo sawa, ila nimeshukuru kuwa umafika….’akasema
‘Ok, sawa mimi naondoka…’nikasema
‘Kuna kitu nilitaka kukuambia, lakini bado sijawa na uhakika,
nataka nipate ushahidi halafu tutaongea….’akasema
‘Kuhusu nini….?’ Nikauliza
‘Nataka uwe na amani na hili jambo tulimaliza kabisa….’akasema
‘Jambo gani…?’ nikamuuliza
‘Kuhusu huyo mtu niliyezaa naye….’akasema
‘Sijakuelewa bado…na usiumize kichwa chako kabisa,..kama hutaki
nijue haina shida, ..mimi nakujali sana, sitaki uumie, uwe na wakati mgumu kwa
ajili yangu,…mimi nina amani kabisa, sina kinyongo na wewe, naahamu una sababu
yako muhimu tu y akufany ahivyo….’nikasema
‘Unajua mimi linanisumbua sana, nimejaribu kuliwazia tukio zima la
siku ile sijaweza kulithibitisha,…sijawa na uhakika ilikuwaje…’akasema
‘Tukio gani…?’ nikamuuliza
‘La kuipata hiyo mimba….’akasema
‘Mhh..sikuelewi, ...usinidanganye rafiki yangu..wewe sio mtu wa
kubakwa, wewe sio mtu wa kufanyiwa tendo bila rizaa yako, nakufahamu sana, kwa
hilo usinidanganya....’nikamwambia, ni kweli rafiki yangu ni mbabe, mjasiri na
anajiamini, anaweza kupambana na midume, hata kama ni kwa kupigana ngumi.
‘Kwakweli siku ile, nilizidiwa, na sijui kwa vile nilitaka iwe
hivyo, ndio maana sikujali, hata hivyo nikuambie ukweli, sikuwa nimepanga
itokee hivyo, sio siku ambayo nilisema leo nataka nikafanye hivyo, hapana,
...ilitokea tu , na huenda ilipangwa iwe hivyo, kwa kifupi siwezi kukumbuka
siku ile nililewa...’akasema.
‘Ulilewa, ulianza lini kunywa…?’ nikamuuliza
‘Siku hiyo hiyo…na nilijuta …na mara pili, nikarudia tena, ..na
kilichotokea ndio nikasema sitakunywa tena,…najuta…’akasema
‘Wewe mtu…..ina maana ukinywa pombe…na wewe uliwahi kuapa kuwa
katika vitu ambavyo hutaweza kuvitumia kimojawapo ni pombe…?’ nikamuuliza
‘Nimevunja miiko mingi sana ya kwangu, na kila nilichokifanya kwa
kuvunja miiko yangu nimekuja kupata matatizo makubwa..hadi sasa sina amani…’akasema
‘Ilikuwaje maana wewe mwenyewe ndio umenichokoza, nilipanga
nisikuulize tena, lakini umelianzisha wewe mwenyewe, utanieleza au niondoke, na
nikiondoka sitaki tena kuniambia kuhusu maswala yak ohayo…’nikasema
‘Sawa kama umeamua hivyo,
mimi nitakuambia ilivyokuwa siku ile, na wewe mwenyewe utajaza,…na naomba usije
ukanilaumu,....maana wewe mwenyewe ndiye uliyenishauri...’akasema na mimi
nikafurahi tukakaa na kuanza kuongea, na yeye alianza kusema hivi;
Siku uliponipa ushauri wako, moyo wangu ulianza kuwa na shauku,
…nikawa na hamu sana ya mtoto kuliko siku zote,….nikawa nawaza sana kupitiliza
mpaka watu wakanifahamu kuwa nina mawazo…niliwazia nikiwa nimempakata mtoto
wangu, na hasa wawe mapacha….nilipata shida sana....’akatulia kidogo.
‘Unakumbuka ulivyoniashauri, nimtafute yoyote hata awe mume wa mtu
nifanye naye tendo kwa minajili ya kupata mtoto, na nilijiuliza nitamuendeaje
mwanaume bila..unajua mume ndiye anakutongoza, au sio..sasa nitakuwaje na uso
usio na aibu….haraka nikasema kwanza labda nitafuta kitu cha kuniondoa aibu,…’akasema.
‘Ndio ukaenda kulewa…kwenye mabar, au ilikuwaje…nashindwa hata
kukuelewa, kwanini usingeliniomba ushauri nikakuelekeza jinsi gani ya
kufanya…’nikasema
‘Unajua rafiki yangu, kinachonishinda kwa hivi sasa ni kuhusu
shemeji…’akasema
‘Nani, huyo bwana mliyezaa naye…?’ nikamuuliza
‘Ndio.....’akasema.
‘Kasemaje…? Nikamuuliza.
‘Ndio, kaniomba sana, tena sana hata kulia, hata kunipiga magoti,
kuwa nisimwambie yoyote kwa sasa iwe siri kubwa kwani kuna mambo kayagundua
yanaweza kumleta matatizo kwenye familia yake….’akasema
‘Ni sawa,…hata mimi nilikushauri hivyo, je labda mkewe keshamuhisi
vibaya au….?’ Nikamuuliza
‘Anasema…kuna mambo yake ya kifamilia, ambayo hataki yaharibike,
na ikigundulikana kuwa ana …mtoto nje, atayaharibu..ok, mimi nilion ni jambo la maana, kama na yeye kakubali iwe
hivyo itakuwa ni heri kwangu…ila kwa masharti kuwa anataka mtoto atambulikane
kuwa ni kwake kwa siri..hapo ndio tukaanza kukorofishana,...’akasema.
‘Unakubali nini na unakataa nini, kosa umelifanya wewe mwenyewe,
kwanini toka mwanza usingelimdanganya kuwa mimba sio yake,..hii inaonyesha kuwa
ulitaka afahamu, na huenda ulifanya hivyo kwa dhamira fulani ambayo unaogopa
kuniambia...’nikasema na yeye akainama chini kuashiria kuwa kauli yangu
umemgusa moyoni.
‘Kwa hali kama hiyo nimeona nisimwambae yoyote ....shemeji
kaniomba na mimi nikamuahidi iwe hivyo, kwa masharti kuwa na yeye asinifuate
fuate tena..lakini naona yeye kaanza kuvunja ahadi, kila siku hodi, na mbaya
zaidi ananunua vifaa vya mtoto..sipendi, na ndio maana ilipotokea nafasi hiyo
ya kusoma mimi nikaikubali kwa haraka sana, na sijamwambia kuwa mimi nakwenda kusoma
nje....’akasema.
‘Kwahiyo eeh, unajua mimi unaniweka kubaya, …mimi naona nikuache
na mambo yako, kwani kila hatua unanitamanisha intake kumfahamu huyo shemeji,
na hutaki kuniambia ni nani…tuyaache kama ulivyosema au…?’ nikamuuliza nikiwa
nimekunja uso kwa hasira.
‘Mimi nitakuambia jinsi ilivyotokea siku ile...au niache maana
wewe unakimbilia kumjua huyo shemeji lakini hutaki kujua ilitokea vipi, nataka
ufahamu ilivyotokea, ili uone kuwa sikuwa nimekusudia siku ile,…japokuwa
tulipanga iwe hivyo, lakini sio kwa huyo na …hata sijui, nisemeje ndio maana
nataka nikuelezee ilivyo kuwa na sio alzima nikutajie kwua ni nani...’akasema
‘Sawa hebu elezea, uonavyo wewe… maana na wewe sasa unajifanya
mtunga tamithiliya, wengine hawapendi vitu virefu, sawa mimi sijali ila unipe
kitu cha ukweli, sio hadithi za kubuni...’nikasema kutoka moyoni hadi hapo sikuwa
na dhamira yoyote mbaya dhidi yake, sikua na wazo kuw ahuyu mtu anaweza
kunifanya chochote kibaya, yaani sijui kwanini ilitokea hivyo, maana pamoja ya
kuwa ni rafiki kwangu mimi nilishamweka kuwa ni ndugu yangu…moyo wangu
umejengwa hivyo kuamini watu.
‘Baada ya ule ushauri wako, nikajikuta nakutana na wanaume wale
ambao wana watoto ninaowapenda, nilijipangia kama karatiba fulani, ..ni ngumu
lakini…kwahiyo ikawa inatokea awali, kwa huyo na yule lakini ghafla ikaja
kubakia kwa huyo mtu mmoja, bila hata kukusudia,…
Cha ajabu sio kama awali wengi wakinialika kwenye chakuala cha
jioni, inaishia kula na kunywa kidogo basi, tunaagana imekwisha, nahisi walishanisoma,
na wengi hawakutaka kuniomba tufanye lolote zaidi ya hapo, ni ile raha ya kukaa
na mimi kula kuongea, inaishia hapo tu,…na mimi sikuweza kushinikiza ili lifanyike hilo tendo,
siwezi, ningalianzaje..na hata kwenye
akili yangu bado nilikuwa na shaka...’akatulia.
‘Kwahiyo baadae ndio akabakia huyo mmoja ambaye hutaki kumsema,
japokuwa mimi nimeshamfahamu kuwa ni nani, au sio… shemeji yangu wa ukweli.. au
sio..?’ nikamuuliza huku nikicheka.
‘Ndio, sijui ilitokeaje, …ilikuwa kila nikienda kupoteza mawazo, shemeji
yumo..ni kama ananifuatilia nyuma, utafikiri alikuwa ananilinda, au hata sijua
ni kwanini alikwua akifanya hivyo, na ndiye niliyekuwa nikijaribu kumkwepa
kuliko wengine, lakini haikuwa rahisi, kila nikitaka kutoka shemeji yupo nyuma,
akiona sina mtu, anakuja kunipa pambaja,…nikaanza hata kuogopa, nikifahamu
ukaribu wangu na mkewe, na familia kwa ujumla....’akasema.
‘Ok,…tuendelee..’nikasema.
‘Lakini mimi naona tuache tu kuyaongelea haya,…’akasema
‘Umeshaanza, siwezi kuondoka mpaka uelezee, hapo utaniuzi,
hatutaelewana…’nikasema
‘Sawa, ngoja niendelee, maana hata mimi sijawa na uhakika, ni kwanini litokea hivyo na je ni yeye
kweli,..nachanganyikwia ndio maana sina raha na kwanini ilitokea siku zote
mbili, ilikuwa kama….haa, hata sijui nisemeje,....’akasema.
‘Sawa endelea ilikuwaje, ...kwani naiona hiyo sasa ni tamithilya
fulani , kuna kitu unanificha na nitakigundua tu,...’nikasema.
‘Ofisini kwangu kupo karibu sana na ofisi za shemeji..’akasema.
‘Ok…ni sawa, ...ndio maana ilikuwa ni rahisi sana, kwako
wewe ..mmh najaribu kujiuliza ni nani pale anafanana na mume wangu, mbona wengi
wanaofanya kazi pale nawafahamu hata huyo mdogo wa mume wangu yupo karibu
sana…ok..na upande huo wa pili yupo mume wangu,…, sasa naanza kuelewa,
tuendelee..’nikasema na yeye akaniangalia huku akijaribu kutabasamu lakini uso
ulikuwa umejaa huzuni.
‘Ndio ni kweli ndio maana ilikuwa ni rahisi sana kwake.., kuniona
nikitoka, na niliona kama kadhamiria kufanya hivyo, na mimi hata nilivyojaribu
kumkwepa ikawa haisadii, nikaona isiwe shida, kwanza ni mtu ninayemwamini
hawezi kunifanyia lolote baya na anafahamu kabisa kuwa mkewe ni mtu
tunayefahamiana sana naye...’akasema.
‘Mhh, ndio nafahamu si mlikuwa mashoga kipindi fulani na mkewe..,
nikafikia kukukanya kuwa huyo mwanamke haaminiki, anajaribu tu kuficha ule
ubaya wake , ili uone ni kawaida tu…maana kama angelikuwa rafiki wa ukweli,
asingelikuibia mchumba wako, …mara nyingi marafiki wanaweza kuwa hivyo,
unatakiwa rafiki awe kweli rafiki mnayeaminiana, ambaye huwezi hata kumdhania
ubaya, au sio..?’ nikamuuliza na yeye akatikisa kichwa kukubali, hakusema neno
‘Ni kama mimi na wewe, mtu hawezi kuniambia kitu kibaya kuhusu
wewe, najua huwezi kamwe kunifanyia mabaya, kama mimi nisivyoweza kukufanyia
mabaya, mtu kama humfanyii mwenzako ubaya, huwezi kufanyiwa ubaya, au sio..itakuwa
ni ajabu sana wewe ukinifanyia ubaya, au sio…....’nikasema na yeye akatabsamu
na kusema.
‘Mhh, mabaya kama yepi tena rafiki yangu, wakati mengi
tunafanyiana baada ya kushauriana…?’ akaniuliza
‘Kama aliyokufanyia yule rafiki yako, mtu unamuamini, halafu
anakuja kukuibia mchumba wako…kiukweli inauma, kuibiwa mume au mke, unajua
inatokea kama nilivyokushauri,au sio, na huwezi kumfanyia rafiki yako,
mpendwa,, ni lazima utafanya mbali kabisa,…maana kama ni rafiki yako,
mtaumizana sana…’nikasema
‘Mhh…hapo sasa…’akasema, akijikuna kichwa, halafu akajaribu
kutabasamu na kusema;
‘Nimewaza sana hili…..naona bora ….nikuambie tu, ilivyotokea…’akasema
‘Ikawaje hebu endelea bwana, acha kusua sua, usinipe ugonjwa wa
moyo….’nikasema
‘Basi kutokana na hali hiyo, kuwa mke wake namfahamu, ni mtu
tunaheshimiana, nikaona nisimzalilishe, maana kama unavyonifahamu, huwa
simkopeshi mtu, huwa siogopi mtu, kama sitaki sitaki...naweza nikamtolea nje
mbele za watu akabakia kuzalilika na nisingeliweza kufanya hivyo kwa
shemeji....’akasema.
‘Ni kweli mimi nakuaminia,ndio maana hilo lililotokea siwezi
kuamini kuwa lilitokea bila ya ridhaa yako, wewe utakuwa ulikubaliana nalo,
vinginevyo kuna kitu unanificha, na sipendi unifiche kitu, maana nikigundua,
haaa..weee, si unanijua nilivyo, mume wangu mwenyewe ananiheshimu kwa hilo,
ananiogopa, ndio maana anajitahidi kuwa mkweli kwangu, kama nilivyo kwake...’nikasema.
Hapo akatulia kidogo kama anawaza jambo, baadae akaendelea
kunihadithia…
‘Ikawa kila nikitoka kwenda kula jamaa huyu hapa, nikitoka kwenda
kazini, jamaa huyu hapa, ikawa kila siku nakutana naye, nikajikuta sina raha,
na hata yeye akaliona hilo,…lakini akaniambia niwe na amani, atajitahidi
kuhakikisha hatuvunji heshima yetu, …kiukweli hata lile wazo likafutika,
sikutaka tena,… lakini moyoni...nilikuwa unanijia ule ushauri wako,na nikawa
natamani ufanye kazi, lakini sio kwa huyo mtu, mume wa mtu, siku zinasogea...’akatulia
kidogo.
‘Endelea…nina muda kidogo…ila najiuliza kwanini ulipoteze muda kwa
huyo mtu, maana hapo ulikuwa unajichora kwa watu, walikuona, wanakuona au sio,
kwahiyo hadi hapo wana ushahidi bayana ….hapo
eeh, uliharibu…’nikasema
‘Kwa vile ni jamaa, ambaye…ni..ni .. shemeji yangu, sikuona
tatizo, na ..unajua nisingeli…mkatalia hata chakula, japokuwa awali nilikuwa nafanya
hivyo….’akasema
‘Ok nimekuelewa, sasa nikuulize katika wanaume wote wewe uliona
huyo ndiye anakufaa au kwa vile ulihisi atakuzaliwa watoto sawa na wakwangu au…?’nikauliza
‘Kiukweli ndio hivyo, kama ungelianiambia nichague ni nani wa
kunipa mimba, kama hakuna kikwazi, mimi kutoka moyoni, ningelimchagua
yeye....lakini kutokana na ukaribu ulivyo hapana, sikupenda litokee kwake, lakini ndio hivyo,
watu husema litokee ili liwe fundisho,...kwakweli hadi sasa siwezi kuamini,
sikujua kabisa kuwa nitakuja kuzidiwa kiasi hicho…ni pombe, sitarudia tena…’akasema.
‘Hebu kwanza nikuulize yule jamaa anakunywa, unajua mimi
simpafahamu vyema maisha yake, na unijuavyo huwa sifuatilii maisha ya watu
wengine hata mke wake hatupo karibu kihivyo, japokuwa ni mke wa shemeji yangu…?’
nikamuuliza
‘Anakunywa lakini sio kihivyo….’akasema
‘Mhh, hawa wanaume jameni…. unajua nilikuambia hata mume wangu
anakunywa, lakini akiwa na wazee, watu wa heshima wa dini, anajifanya mtu wa
dini sana, na kupinga ulevi,....mimi nafahamu siri yake, uzuri wake hata
akinywa huwezi kufahamu, anajitahidi sana kujificha…, nimemkanya sana tabia
hiyo ya kunywa pombe…, yeye anasema anakunywa kwa dharura, na kidogo sana…’nikasema
‘Wanaume wengi wapo hivyo….sioni ajabu kwake,…’akasema.
‘Ilikuwa sio sana kama ilivyotokea baada ya kunipa huo ushauri,
mwanzoni nilikuwa nakutana naye, anaiomba tukale chakula pamoja, tunaongea,…ananishauri
kuhusu maisha, ni nani angelipenda awe mume wangu,…nikawa nimezoeana naye sana,
nikiwa sina raha, yeye anipa ushauri , lakini sikuwa na wazo jingine lolote
dhidi yake, na yeye alilitambua hilo...’akasema.
‘Mambo ya shemeji hayo , nafahamu sana ulichompendea, ni kw vile
kwanza ni mtanashati,…. mrembo kama mume wangu, wanafanana sana, na mume wangu,
kwahiyo nahisi ndio sababu ulimpendea hivyo au sio..?’ nikamuuliza..
Kwanza akaniangalia kwa makini, halafu akawa kama anasita kunijibu
baadae kwa shingo upande, akiwa kainamisha kichwa akasema…..
Nb….naona inazidi kuwa ndefu na muda umekwisha, ngoja niishie hapa
kwa leo
WAZO LA LEO: Urafiki
wa kweli ni ule wa kuangalia athari za kila jambo kuwa unalolifanya
halitamkwanza mwenzako,... ni hilo litafanikiwa pale utakapojiuliza je, kama
nitafanyiwa mimi jambo kama hilo nitafurahia au nitachukia. Tukiwa na
tabia hiyo ya kuchuja matendo yetu kwa wenzetu nina imani kuwa hatutachukiana,
tukumbuke kuwa ubaya kwe wenzetu unauma kama vile tungelifanyiwa sisis, kwani
mkuki sio nguruwe tu, na kwa binadamu mchungu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment