Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, October 6, 2017

MKUKI KWA NGURUWE-2



 Ilipita muda rafiki yangu akawa haonekani, hafiki kwangu na sio kawaida yake na baya zaidi hata kwenye simu yake nikipiga simpati, kwa hali kama hiyo sikuweza kuvumilia, nikafunga safari hadi nyumbani kwake…

Nilipofika nyumbani kwake, sikuweza kumpata, nikauliza majirani wake, wakasema, siku hizi  anatoka asubuhi sana kwenda kazini na anarudi usiku sana,…bado sikurizika na hilo jibu, nikaona nipitia kazini kwake, lakini wakati nataka kufanya hivyo, nikapigiwa simu ya muhimu kwenye shughuli zangu za kibiashara, ikabidi nikatize safari hiyo, moyoni nikijipa matumaini kuwa,.., huenda ana sababu zake za msingi za kufanya hivyo.

Baadaye jioni, nikamuona huyu anakuja, alioneka kuwa mnyonge sana, kama mgonjwa, usoni hana raha, uso umesawajika, kachoka, mpaka nikaingiwa na mashaka, nikahisi kuna tatizo, ni lazima kuna tatizo…!

Kwa muda huo, watoto walikuwa kwenye meza wanajisomea, kipindi hicho walikuwa darasa la tano,…wakubwa, na watoto wakike hukua haraka!

Kama kawaida yao walipomuona mama yao kafika…, maana napenda kumuita hivyo, ‘mama yao’ kwa jinsi walivyomzoea, kwa haraka wakaacha kusoma na kusimama na kumsalimia kwa kumkumbatia, wamezoeana hivyo,  ..na yeye kama kawaida yake japokuwa alikuwa haonyeshi furaha akajitahidi kuongea nao, akawafundisha fundisha hapo mezani, baadae akawaachia kazi za kufanya, halafu…, tukaenda chumba cha maongezi.

‘Haya niambie maana hata bila kukuuliza kila kitu kinaonekana dhahiri, kwanini tunafanyiana hivi, urafiki wetu umekwenda wapi…?’ nikaanza kulalamika.

‘Rafiki yangu sio kwamba nimefanya makusudi, hata mimi nilikuwa na wakatu mgumu, lakini …kila nikitaka kukupigia, nashindwa, nahisi nitaishia kulia kwenye simu, ..nikitaka nije, ooh…lakini leo sijambo, naona naanza kuizoea hiyo hali, maji yameshamwagika hayazoleki..’akasema

‘Mhh..bado, sijakuelewa…’nikasema

‘Jana niliwaza sana…baada hayo kutokea, baada ya kujipa muda wa kutafakari kwa kina,…, unajua ni kweli,…nilifanya makosa, na kiukweli …hata sijui nifanyeje, na…na…umri wa mwanamke una ukomo wa kuzaa, na mimi nahisi naendea huko, baada ya kwuaza hilo, niliogopa sana kuwa sasa nimeshazeeka bila ya kuwa na …na…hata kumbukumbu…’akasema

‘Mhh, wanasema kitaalamu ndio…lakini mbona watu wanazaa tena wazee tu, ni hivyo kiunjumla, lakini sio kwamba wote watakuwa kwenye hatari hiyo,…kuwa ukizee kw umru huo wa utu uzima ni hatari, hata hivyo…mb- mbona wewe bado tu mdogo, hujafikia kwenye hiyo hatari…, au sio…?’ nikamuuliza

‘Mhh…hapo sasa, urafiki wetu ule wa zamani wa kuambizana ukweli naona umepita, kwa vile mimi sasa nimekiri hilo, kuwa…nimeshaze-zeeka, au sio,…naona hutaki kunishauri mambo ya ukweli, kwa ajili tu ya kunipa matumaini, au sio,….’akasema

‘Mbona nilishakuambia sana hilo…, nikakushauri sana tu…, nikaona basi nijinyamazie tu, maana nakuelewa sana, wewe sio wa jana kwangu, ukiwa na maamuzi yako huingiliki, hata kama mimi ni rafiki yako, huwezi kubadilika mpaka mwenyewe upende…’nikasema

‘Yaani rafiki yangu hilo ndilo limekuwa nikijiuliza akilini mwangu, baada ya kutafakari sana nikaona nije nikuone,...nimegundua kuwa sasa hivi natakiwa nichukue hatua nyingine kabla sijachelewa zaidi…na kiukweli baada ya kutoka hayo, nahisi kipaumbele changu kwa hivi sasa sio mwanaume, ..sio kuolewa, …huu sio muda wa kuwazia kuolewa tena…na baada ya yote hayo, naona ili kuepusha shari zaidi, bora niishi peke yangu, ..kwa kifupi mimi sitaki tena kujiingiza kwenye mawazo ya kuolewa…, nimeshajizoelea kuishi kihivi hivi, kivyangu-vyangu,  kuwa na uhuru wa kufanya nipendavyo…’akasema

‘Sizani kama hilo ni sahihi, …hayo sio maisha ya kibina-adamu, lazima kuolewa, ili uweze kupata familia yako, au hutaki watoto,…?’ nikamuuliza

‘Watoto…., watoto….mmh, ….yaani umeshanigusa, hilo….ooh, hata sijui nifanyeje…’akasema akiangalia mlangoni, nahis alitaka kuangali akitu ambacho hakioni.

‘Ndio, sisi ni wanadamu umri wetu una …mipaka na hatujui lini mtu anaondoka duniani, na ubora wa mtu, uzae utoe mbegu na mbegu zije kuotesha mti mwingine, kizazi kinakua,…au sio, usipozaa hutakumbukwa tena hapa duniani…’nikasema

‘Sawa kabisa, hilo ….ndilo lililoniumia jana,…lakini kwa vipi,…na mimi sipendi kuwa mtumwa wa kujipendekeza, eti nikajiangushe kwa mwanaume kuwa yamepita basi, nimekusamehe, hapana, na hata hivyo haiwezekani, siwezi kuingie kwenye mashindani ya kugombea mwanaume…’akasema

‘Kuna kitu unanificha au..?’ nikamuliza

‘Unajua rafiki yangu,  nikuambie ukweli, ninachotamani kwa sasa ni kupata mrithi,…kuhakikisha na mimi nabakia ni kizazi cha huko mbeleni, hata kama…hilo,…ndilo naliwazia….’akasema

‘Ni kweli, ni lazima upate kizazi chako, ni lazima upate mtoto, na utapataje, bila kuingia kwenye ndoa,..hilo …labda ndilo la kuwazia,…’nikasema

‘Hapana siwazii, ndoa…mimi nawazia kupata mtoto, ninajua  nikipata mtoto basi, maisha yangu yatakuwa na furaha sana…’akasema

‘Hahaha, sasa leo umekuja na jipya, unataka mtoto bila ndoa,…leo umeshabadilika au,sijakusikia vyema,…kuwa unataka uzae nje ya ndoa, au mimi sijakuelewa, au hebu niambie vyema....utapataje mtoto bila ya mwanaume au unataka mtoto wa kurithi, sijakuelewa hapo..?’ nikamuuliza

‘Ninataka mtoto wa kwangu wa kuzaa mimi mwenyewe, lakini nataka iwe halali, isiwe nafanya vibaya, …ndio maana nimekuja kwako tulijadili hilo, kama huko kuolewa hakupo, maana nimesubiri sana sijampata mume wa kunioa, wengi wanataka kuuchezea huu mwili wangu tu,…kwa vile hajatokea mume wa kunioa, basi, nipate angalau hata huyo mtoto, …’akasema.

‘Unataka kusema nini sasa…?’ nikamuuliza na alikuwa kama kaichokoza fikra fulani niliyokuwa nayo akilini, lakini sikupenda kabisa kumshauri rafiki yangu nilijua ni makosa, lakini sasa naona anaelekea huko-huko, ila sikutaka kuianzisha mimi, nikasubiria.

‘Natamani mtoto rafiki yangu, lakini kwa vipi, kama ulivyosema sijaolewa, na mtoto akizaliwa, najua hata kuwa na muonekano mnzuri kwa jamii, atapewa ‘majina mapya…’ akasema kama anaimba

‘Na mbaya zaidi,..hilo mimi silitaki,..eti aje kuitwa mtoto aliyepatikana kwa njia za haramu, mimi nitaonekana muhuni…ooh, kwanini mimi..unajua najishia vibaya sana…kwanini lakini…, silipendi, ndio maana nimejitahidi kujizuia sana nisije kwanza hapa, maana ningelifika kwa muda huo ningeliishia kulia,..sitaki huo unyonge,..’akasema

‘Sasa ina maana unatakaje sasa rafiki yangu..au kwani imekuwaje tena, maana sisi tulishajua sasa mambo yanaelekea kwema, au..?’ nikamuuliza

‘Hapo sasa, ndio maana nimewaza sana hilo…mpaka kichwa kinauma, nimekuja kwako tushauriane, nilikuwa nimejitenga kidogo kuja huku nikiwazia hili jambo kwa makini sana, nimeshindwa namna, nifanyeje…mimi nataka mtoto, natamani nipate na mimi mtoto wangu…., nilitamani ndoa, ndoa haijatokea, sasa hata mtoto jamani…’akasema kwa sauti ya huzuni.

‘Nikushauri rafiki yangu, ukianza mtindo huo, utazalishwa na waume tofauti tofauti, na kuwa na watoto wa kila mmoja na baba yake, huoni hiyo itakuja kukuletea mawazo mengine uzeeni kwako,…maana sawa, utakutana na mwanaume ilimradi mwanaume upate mtoto, utazaa wa kike, ..kesho utataka wa kiume, utaenda kutembea na bwana mwingine atakuzalisha,kumbe anakuja tena wa kike…kesho kutwa utataka mwingine…huoni itakuleta sifa mbaya…?’ nikamwambia

‘Aaah, hayo ya huko mbele anayajua mungu peke yake, tugange haya  yaliyopo sasa,,, kwani wewe unajua kesho itakuwaje, nikifa hapa si ndio mtanisahau kabisa, sina hata kumbukumbu huku nyuma, au sio, hiyo ndio ajenda yetu, tuijadili …’akasema hivyo , na kwa vile namfahamu sana rafiki yangu sikutaka kumchukulia kwa haraka.

‘Unajua rafiki yangu nilikushauri sana awali, ukanipuuzia, sasa umri ndio huo umekwenda, na tabia yako haibadiliki, wanaume wameshakusoma wameshakugundua ulivyo,…kuwa wewe ni mtu wa matumizi tu,..dharau, msomi sana,… mtoto wa bei mbaya, mtu wa matumizi makubwa, wanaume hawapendi hayo maisha,…wanmeshakuogopa, na maisha yenyewe yalivyo,..oh, angalia sana…’nikasema

‘Sasa ndio imekuwa hivyo, mimi ndio nipo hivyo, sina mbadala, na hata nijitahidi vipi kwasasa ni nani ataniamini kuwa nimebadilika,..labda niende ulaya nikamtafute mnzungu mzee…hahaha, …nacheka utafikiri nina raha, naumia mwenzako,…ni nani atakayenipenda hivi sasa, hakuna…, lakini sitaki kuzalilika…, nataka maisha ya hapa hapa kwetu, nataka mtoto wa damu ya kiafrika, nataka mtoto kihalali, sasa kwa vipi….’akasema


‘Vipi yule shemeji , kawaje kwani, mbona naona anakupenda sana imekuwaje, sisi tulitaka tuonane na nyie wawili tunishinikize ndoa…kwanini yeye asikuoe, ili upate huyo mtoto, mimi nakushauri hivyo…’nikamshauri.

‘Mhh, ungelijua,..yule ..hahaha sitaki hata kumsikia tena, sitai simtaki, na hata hivyo ipo wazi, sio wangu tena…’akasema

‘Kwanini…niambie..’nikasema

‘Siku kadhaa , alisita kuja kwangu, sikujua ni kwanini, nikasubiria wee, niaona kwanini nisjiumize kwa mawazo, nikasema ngoja niende kwake…labda anaumwa, sikutaka kumpigia simu, maana tulishazoeana kihivyo…basi, nikaenda kwake,.., ile nafika eneo la nyumba yake,…nikahisi mwili unasisimuka ajabu…, nikahisi kuna tatizo…lakini nikajipa moyo, nikafika nikagonga geti…kumbe lipo wazi, nikafungua hadi kwenye mlango wa nyumba,…’ hapo akatulia kidogo.

‘Unajua kabla sijagonga mlango, ukafunguliwa,…, mara anatokea mdada  half cast, si unajue waniga fulani,..kijamika jamaika fulani, alivyo sio….kavaa khanga moja, ile ya khanga moja hakuna kitu kingine ndani, mhh, kuashiria nini hapo, kuwa katokea wapi sio.. utajaza mwenyewe……’akatulia akikunja uso kwa hasira

‘Mhh, kwahiyo ina maana gani hapo…?’ nikamuuliza

‘Ndio hapo nakuambia, mimi nina gundu…nina mkosi gani sijui, na uelewe baada y aule ushauri wenu na shemeji, nilipanga niende nimwambie sasa tufunge ndoa, nimekukubali, na sitaki kupoteza muda tena, na hilo alikuwa akilisubiria, niliwahi kumwambia akasita, akawa haniamini, sasa nilitaka nimuhakikishie kuwa nipo tayari,… siku hiyo nilipanga iwe hivyo,..hebu jiweke kwenye nafasi yangu uone nilivyoumia,… sasa sijiu kwanini alinifanya hivyo, hata sijui muda wote huo, kwanini hakuaniambia ana mchumba wake anasoma huko marekani…leo hii, inatokea hivyo…’akasema

‘Ulimuuliza baada ya hapo…?’ nikamuuliza

‘Mimi tena, ..mimi, weeh, unanijua nilivyo, wee…mimi  nikamuuliza,hahaha, sikuwa na muda huo,… hapana,…nilipojua kuwa huyo ni mchumba wake, nikaondoka zangu na hata aliponipigia simu sikutaka kabisa kupokea, na hali hiyo ilinitesa sana, sikutaka hata kuja kuongea na nyie, na ningelikutana na yeye, angelinijua mimi ni paka mwenye makucha makali…’akatulia

‘Sasa ulijuaje kuwa ni mchumba wake..sijakuelewa hapo?’ nikamuuliza

‘Nilimuuliza, ilibidi amuite kwani alikuwa ndani, na mara huyu, ti-ti-ti…katoka na taulo na likitambi-tambi lake, unajua kajiachia sana, na likitambi lake,.. sipendi hali hiyo, lakini nilishafikia sehemu nikaanza kumpenda tu, alivyo, kubembeleza, hakati tamaa..kumbe alikuwa na lengo lake…’akatulia

‘Nikamuuliza huyo kinyago ni nani…?’

‘Kinyago, hahaha huyu ni mchumba wangu….’akasema na huyo binti, akasimama pemebni yake na kumwekea mikono hivi, kimahaba, kuninyaa…nikihisi ile hali natamani irejee niwe na gun, niwashoot…lakini yamepita…’akatulia

‘Pole sana…’nikasema

‘Kiukweli…niliumia sana, unajua kuumia, mtu nilishasema huyu sasa ndiye wangu, leo hii inatokea hivyo, ni mara ya ngapi yanatokea haya, hapana siwezi tena,siwezi kuyabeba haya tena…sitaki mwanaume tena,…’akageuka akizuia machozi.

‘Pole sana sikujua,…na kwanini hukunipigia angalau simu…?’ nikamuuliza

‘Hayo tuyaache, mimi nimekuja na wazo hilo unisaidie kwa ushauri nifanyeje sasa ili na mimi nimpate mtoto, maana …nimeshafika sehemu sitaki kupenda mwanaume tena…, nataka nimpate mtoto wa kuniliwaza tu..basi…’akasema


‘Kwahiyo upo thabiti na msimao huo, are sure about it ….umedhamiria kufanya hivyo, au unatakaje, maana mtoto sio wa kupata hivi hivi tu kama kuku, au sio..kuwa upite hivi jogoo akupande, au sio…?’ Nikamuuliza

‘Mimi kwa hivi sasa sitaki mwanaume, na kama yupo,  yupi tena, hao wakunitesa, hakuna tena mwanaume mwanifu, hawapo..wote ni waongo , wahuni, wana hadaa, wema wazuri, waaminifu wameshaoa, nina imani hiyo, hakuna…sasa nifanyeje nife bila hata ya  mtoto…’akasema

‘Sijakuelewa hapo ina maana unataka mtoto kwa vipi hapo,…?’ nikamuuliza kwa mshangao kidogo.

‘Vyovyote iwavyo,…kwani kama ingelikuwepo ndoa, angelikuwepo wa kunioa ningelihangaika hivi, kwanini nihangaike…ndoa siioni tena, siwaoni kabisa wa ndoa hapa, wengi wao nimeshawajua ni tamaa zao za mwili wangu tu,na hilo ndio sasa silitaki tena, nimechoka kuchezewa-chezewa, wakunioa simuoni tena, …’akasema


‘Hapo sasa pagumu, ..maana wewe ni rafiki yangu, siwezi kukushauri jambo ambalo hata mimi silipendi,…’nikasema

‘Rafiki yangu, wewe ndiye umenishinikiza na mawazo haya, sikuwa na mawazo kabisa ya kuolewa…unajua, nilijionea sawa tu…,sikuwa na mawazo ya maisha ya famalia, lakini wewe nikija hapa tukiongea unakuja na kauli zako hizo, olewa, olewa…mtoto , mtoto, na zidi nikikuona una watoto wako,  na mimi navutika, naingiwa na hamasa hiyo….’akasema

‘Basi tafuta mume mwingine aku-oe, hata kama humpendi kihivyo, mtakuja kupendana mbele kwa mbele…’nikasema

‘Hahaha..mume , ilimradi mume, mimi….haya tuseme hilo sawa, haya yupo wapi huyo mwanaume…’akasema

‘Kwahiyo wewe kwa hivi sasa hufikirii kupata mwanaume wa kukupenda tena, mbona wewe ni mnzuri, wanume wanakutamani, mimi hilo siamini kuwa hakuna mwanaume anayekutaka tena..’nikasema

‘Wewe unasema tu, kwa vile unaye,..sio rahisi kihivyo,..na siwezi, kujiuza, kujizalilisha,…ila wazo langu ni hilo, nishauri, kama huna ushauri niondoke zangu…’akasema

‘Mhh kifupi nimekuelewa umefikia hapa kwa maamuzi hayo baada ya kutendwa,…chuki ikajitokeza dhidi ya wanaume au sio , achana na huyo piga moyo konde utapata mwingine au kwanini hadi ukate tamaaa kihivyo…?’ nikamuuliza.

‘Ingewezekana akapatikana wa kunioa, ambaye pia namkubali, ..na asije kunitenda hivyo tena, ningekuwa na uhakika huo, sawa, lakini huyo mwanaume wa ngapi, watano wote wananifanyia hivyo hivyo…mimi, nina mkosi gani,…sitaki tena nimesha kata tamaa …licha ya tabia yangu ya kuchagua-chagua, lakini ilishafikia muda nikasema haya, si kuna kuolewa, haya nioeni,..anatokea huyu tukifikia mahali pa kufanikisha linatokea la kutokea..

‘Ni bahati mbaya tu…’nikasema

‘Huyu wa mwisho ndio akanimaliza kabisa…hapana,…nimechoka, kwanini mimi, ina maana adhabu za kuwakataa waume nikiwa binti ndio zinaendelea mpaka sasa, ina maana mimi nina madhambi makubwa kiaisi hicho…’akageuka kuangalia pembeni akificha machozi.

‘Hapana sio sababu hizo, ila wanaume nao wana chaguzi zao, wana mitizamo yao, wengi wao akili zako ni moja, wao wanataka wenye tabia fulani, tabia nzuri, ..nk.. hata kama wao hawana tabia hizo,…hawajui kuwa na wewe ulikuwa na mtizamo wako…’nikwambia

‘Tusipoteze muda …mimi sasa nataka mtoto tu inatosha, lakini mtoto….aweje, …kwa vipi, nitampataje, nataka ushauri wako, nisaidie rafiki yangu…

‘Mhh, unaniweka pagumu,..unajua rafiki yangu, ukizaa mtoto bila ya mume, huyo- huyo mtoto atakuja kumuhitajia baba yake, utafanyeje huko mbele, …maana sawa, nitakushauri kapachikwe mimba sijui kama utakavyo, kwani kupata mimba ni ngumu, kama una kizazi…’nikasema

‘Kwahiyo…?’ akauliza akikuna kuna kichwa.

‘Au labda ukarithi, wapo watoto mayatima kwanini usiende kumchukua mmoja ukafuata taratibu za kurithi,…’nikamwambia hapo akaniangalia kwa jicho baya, halafu akasema kwa hasira.

‘Nimekuambia mimi  nataka wa kumzaa mimi mwenyewe, aje kunyonya ziwa langu aje kupitia taratibu zote za mtoto wangu …na zaidi ya hapo awe mtoto atakayekidhi viwango vyangu, unajua, ...’akasema akiwaangalia watoto wangu, mbao walifika kuna kitu walihitajia, nikawasikilia halafu wakaondoka.

‘Kama ni hivyo mbona ni kazi rahisi sana....’nikasema hapo akaniangalia kwa hamasa, sijui alitaka niseme hivyo, nilivyosema au kwanini aliniangalia machoni kwa hamasa kubwa.

‘Ni kazi rahisi eeh, sasa niambie nifanyeje….maana wewe ni rafiki yangu, na kwenye dini wanasemaje, mpendelee rafiki yako, au sio..umpe kile unachokipenda, name natarajia utanifanyia hivyo..nishauri, nisiendelee kuteseka, maana baada ya hapo, unaweza ukasikia mengine, naweza hata kujiua,..sikutanii, nimeshafikia kubaya…’akasema

‘Oh, imekuwa hayo…’nikasema

‘Sitanii, niambie sasa, nifanyeje, …wewe ndiye rafiki yangu wa pekee nikishindwa hapa, basi, dunia, hainitaki tena, tumeshirikiana mengi tokea utotoni, hili nalo nahisi utanisaidia,...maana wewe ni mimi, japokuwa kwa hili  huwezi kujua ninavyoumia kichwani,…unajua … nilipowaona watoto wako wakiingia hapa, nikahisi ni wangu..nawapenda sana watoto wako….’akasema

‘Basi kama umedhamiria hivyo,,…japokuwa sio sahihi, mimi nitakupa ushauri wangu ila..ninaona tena sana iwe siri, kati yako mimi na wewe….sawa….?...’mara mlango ukagongwa, mume wangu akafika….

NB: Msiseme ninazunguka, ..hii ni tamithlya, inajiongeza, ngoja huo ushauri sehem ijayo.

WAZO LA LEO: Udhaifi wetu kibinadamu unaweza kutufanya tufikie kufanya yale ambayo hata hatukukusudia, …uhimili wetu unafikia kikomo, hasa ukiwa huna imani thabiti ya kumjua mola muweza, kuwa yeye ndiye mpaji. Na imani hii haianzi ghafla tu, imani hii huanzia utotoni. Nawausia wenzangu na kujihusia mimi mwenyewe, tuwajenge watoto wetu mapema kwenye imani sahihi za dini. Ulimwengu hivi sasa unashuhudia mambo ya ajabu , yanayotokea hivi sasa, na zaidi ya yaliyoandikwa kwenye vitabu vya imani, yamepitiliza, …iliyobakia ni mungu mwenyewe anajua.


Tumuombe mola wetu avilinde vizazi vyetu, kwenye mitihani hii , ambayo huko zama ilitokea gharika, ..watu wakaangamia, je hivi sasa itatokea nini…Ewe mola tunakuomba utusamehe, utuongoze kwenye njia sahihi tusije kuangamia kama hao, waliowahi kuangamia.
Ni mimi: emu-three

No comments :