Ni kisa na mkasa, chenye mafunzo ndani yake, kinachotokana na
ushauri wa kirafiki kati ya marafiki wawili. Ushauri uliokuja kuzaa mtafaruku
hadi marafiki hawa wawili wakaja kuwa maadui makubwa wakutaka hata kuuana.
Ulikuwa ushauri wenye nia njema kwa mlengwa, lakini ….athari zake
kwa wengine zinaumiza,…je hao wengine wakiwa ni wewe mshauri itakuwaje….
Hutapenda kuona rafiki yako akiteseka, utafanya kila hali ili
aondokane na shida hiyo, njia mbadala zilishindikana, ikabakia wazo hilo...lililokujia
akilini na kumshauri mwenzako, afanye tu, bila kuangalia upande mwingine wa
athari zake….
Kisa hiki ni kumbukumbu za wale wanaoteseka, wenye shida mbali
mbali, wenye mitihani ya maisha, wengine wakihitajia kuolewa lakini hawajapata
wa kuoa au kuolewa, hawa wanahitajia ushauri, je tuwape ushauri gani…
Wapo wengine wakihitajia watoto, lakini mola hajawajalia,..au wapo
wengine walitendwa na wenza wao, wakaachika, au kuachwa kwa namna moja au
nyingine. Wapo waliovumilia..wapo walioshindwa kuvumilia,…, na wapo waliojikuta
kwenye njia panda…je tuwapatia ushauri gani…
Kisa hiki hiki ni maalumu kwako wewe mtoa ushauri, na wewe
mshauriwa…tuweni makini sana kwa dhamana hii ya ushauri! Ushauri sio kuongea tu
kwa vile…sio wewe utayefanyiwa, sio wewe …hapana shauri ukijiweka kwenye hiyo
nafasi , kama ingelikuwa ni wewe..ingelikuwaje…
Japokuwa unaweza ukatoa wazo hilo kwa nia njema kabisa, ukitaka
kumsaidia mwenzako, lakini jiulize huyo atakayetendewa hataumia,…au kama
ungelitendewa wewe ungakubali kutendewa, ….maana isije ikawa MKUKI NI KWA
NGURUWE TU.
*************
Ilikuwa vigelegele vya shangwe, pale nilipofunga harusi yangu,
kiukweli ilikuwa harusi kubwa, kutokana na hali zetu, na aliyesaidia
kuhakikisha kila kitu kimekwenda sawa, alikuwa rafiki yangu kipenzi…
‘Rafiki yangu, mume wako ni bonge la handsome…hapo sitii kasoro, na nikuambie kitu, wewe usisumbuke kwa lolote
lile, mwili wako na wangu kila kitu
niachie mimi, muhimu ni gharama, nipatie fungu, na wewe kaa, tulia, kama
ningelikuwa na pesa, nisingelipenda wewe utoe hata senti moja, lakini
nitajitahidi…’akasema
‘Ujitahidi kwa vipi, usije kutoa hata senti yako moja, pesa ya
harusi hii ilishaandaliwa kwa kila kitu, wewe isimamie tu, na kila kitu
nitakukabidhi wewe, nashukuru sana rafiki yangu, wewe ni mimi na mimi ni wewe,
…wewe ni rafiki yangu tunajuana, kwa kila hali, nisingelipenda wewe kujiingiza kwenye
madeni,… unasikia, ukifanya hivyo utaniudhi…’nikasema
Basi yeye akasimamia kila kitu, nikaja nikafunga ndoa na mume
wangu..na maisha na rafiki yangu yakawa ni pale pale, ila alichojitahidi kwa
hivi sasa yeye akawa hafiki mara kwa mara nyumbani kwangu, kama ilivyokuwa
awali, yeye alifika akiwa na uhakika mimi nipo nyumbani…nilimuelewa, na sio
kwamba nilimshuku vibaya hapana ni yeye tu, aliona isje ikajenga fitina…’akaendelea
kusimulia.
Masiku, miezi, miaka,
ikaenda mimi nikajaliwa watoto, lakini rafiki yangu bado akawa hajaolewa , sio kwasababu
kuwa hakupata wachumba, hapana, wachumba ni wengi waliotaka kumuoa, lakini yeye
akawa hawakubali kutokana na sababu hii na ile, aliyoiona yeye. Na awali
sikupenda kumuingilia sana kwa maamuzi yake hayo, maana ninamfahamu alivyo…ana
msimamo wake.
Lakini siku zilivyozidi kwenda mbele ikabidi mimi niingilie kati,
nakuumuliza yeye anataka mume wa namna gani, ..japokuwa nafahamu kwa jinsi
tulivyokuwa tukiongea awali kabla ya kuolewa, kuwa yeye angelipenda mume wa
namna hii na ile, na mimi nikawa namuelezea hivyo, lakini mimi nilipoolewa
nikaja kugundua kuwa ndoto za akilini za kuwa utampata mume mwenye kila kitu
unachokitaka ni ndoto tu, aghalabu kuwa kweli…
‘Nikuambie rafiki yangu ukweli, huyo mwanaume unayemtaka wewe hajazaliwa, huwezi
kumpata mume wa kila kitu unachokitaka wewe, vingine vitakuja huko mbele kwa
mbele, na vingine hutaweza kuvipata hadi kufa kwako, ndivyo maisha yalivyo…’nikamshauri
siku za mwanzoni,…
‘Usijali rafiki yangu, ipo siku nitaolewa tu, na mume ninayemtaka
mimi, hilo la kuwa hajazaliwa halipo,..wapo, ninajua wapo…nitasubiri, ipo siku
nitampata , hata hivyo, kuolewa, ni kuolewa, …mimi mwenyewe bado nina malengo
yangu..nisingelipnda kukimbilia kuolewa kwanza…’akasema
Maisha yakaenda hivyo, na umri ukakimbia, umri hausemi, …unashangaa
sura inabadilika, na majina yababadilika, kijana inageuka mtu mnzima, dada,
inageuka kuwa mdada, baadaye…, mama,…mama bila mtoto, baba bila mtoto, mawazo
yanaanza kuingia akilini, mawazo..
***************
‘Rafiki yangu nilimpenda sana, tulianza urafiki tukiwa shuleni, na
hata tulipoanza kazi, ninafahamu kuwa mimi nina uwezo kuliko yeye kihali,
maisha ya familia yangu yalikuwa juu, mwenzangu alitokea familia ya chini,
ninaweza kusema hivyo…’ akaendelea kusimulia
‘Mimi nilijitolea kwa kila niwezavyo, rafiki yangu awe kama mimi,
kila nilipoweza, akiniambia au hata kama hajaniambia, nilijikuta namsaidia
mwenzangu, ilifikia muda kila ninachonunua namnunulia na mwenzangu, kwahiyo
tulikuwa kama mapacha..
‘Unajua ilikuwa sifanyi jambo mpaka nishauriane na yeye kabla
sijafunga ndoa, na baada ya ndoa, ikaendelea hivyo, japokuwa mengine ya ndani
ya ndoa ilibidi nisimuhusishe sana,….kama ujuavyo sheria za ndoa zilivyo.
‘Lakini hata nilipoolewa, sikuacha hiyo tabia, ya kusaidiana na
yeye..ila ikafika muda natakiwa kuwa na familia yangu na mume wangu zaidi, hii
hali iliniuma pale rafiki yangu anapokuja ananikuta mimi nipo na mume wangu,
yeye hana…iliniuma sana, nilitamani huyo mume awe wetu sote, lakini mmh…hapo
pagumu.
Baada ya ndoa mambo mengine
yalijiweka yenyewe rafiki yangu, alianza kupanga muda wake, ni lini aje kwangu,
au lini tukutane naye, hakupenda kuja nyumbani kwangu kama mimi sipo,…sio
kwamba sikumiani kwa hilo…au hakupenda wakutane na mume wangu kupata chakula
cha mchana bila ya mimi kuwepo, hadi mume wangu akaja kuniuliza ni kwanini;
‘Huyo rafiki yako, ni mwaminifu sana, unajua kuna siku nakutana
naye, namuomba nimpeleke lunch,
hataki, eti kisa hapendi ije kulete fitina , mkaja kukosana wewe na rafiki
yako…, sasa mimi ni shemeji yake nitamfanya nini , eti hivi kweli inaweza mimi
nikakusaliti wewe mke wangu, kwa rafiki yako kipenzi…’akasema.
‘Lakini nyie wanaume hamuaminiki,….mimi namuunga mkono kwa
hilo,..hata hivyo mimi sina wasiwasi kamwe na rafiki yangu…’nikasema.
‘Ina maana mke wangu kwa kusema hivyo huniamini…?’ mke akamuuliza
mke wake.
‘Sio swala la kuaminiana hapo, shetani ana mbinu nyingi, …na
kwanini ujiweke kwenye rehani ya mitihani, kama unaweza kuikwepa ni bora
kufanya hivyo, kuliko kujitwika mitihani hiyo,….’akasema mke
‘Ok, nimekuelewa sana mke wangu, lakini nikuulize kitu ni kwanini
rafiki yako hakubali kuolewa, yeye ni mnzuri ana umbo la mvuto, anataka nini na
umri unakwenda…?’ akaniuliza mume wangu.
‘Hata sijui, hajajaliwa bado, siku itafika, ataolewa, ni kweli
umri umekwenda, na hata sijui nifanye nini ili ampate mume anayemtaka,…hata
sijui…’nikasema.
‘Japokuwa yeye ni mnzuri, lakini umri unakwenda mshauri sana
rafiki yako, leo anapendeza hivyo, kila mwanaume anamtaka, lakini itafika
sehemu hatavutia tena, hayo ndiyo maumbile yaliovyo, atakuja kujijutia muda
umeshakwenda…’akasema.
‘Najitahidi sana,…hata sijui nimfanyeje tena…’nikasema.
Kiukweli rafiki yangu huyo sikuwa na shaka naye hata kama
ningelimkuta yupo na mume wangu, ninamfahamu sana kwa msimamo wake…anaogopa sana
waume za watu, ….huwa akiahidi kitu kaahidi, na kwangu nilimuona kama sehemu ya
ndugu zangu, na hata watu walimfahamu hivyo kwa msimamo wake huo, wa
kutokujihusisha na rafiki ambaye ni mume wa mtu. Wanaume wengi walimjaribu
wakashindwa kwa msimamo wke huo.
***************
Kuna kipindi alimpata
mwanaume mmoja wakawa wanakutana mara kwa mara nikajua huyo atamuoa, lakini
baadaye nilipomuulizia, akanipa jibu la kukatisha tamaa.
‘Yule jamaa sitamkia tena,…hanifai, nilijua ni mtu mwenye msimamo,
..mtu wa matumizi, …lakini kumbe ni nguvu za soda, eti anakuja kunilalamikia
kuwa anadaiwa hiki na kile, kwani nilimuambia akope….aah, nimeachana
naye…’akasema
‘Hilo tu…?’ nikamuuliza
‘Wewe unaliona dogo hilo, achana naye, ..mengine sio lazima
nikuambie,.hata kama wewe ni rafiki yangu, huyo nimeshambwaga…’akasema na
sikutaka kumuingilia zaidi,..nafahamu msimamo wake ulivyo.
Kiukweli urafiki wetu ulikuwa ni dhati, na kila mmoja alijua
msimamo wa mwingine na hilo ndilo litufanya tuwe hatuyumbi,…lakini ikatokea la
kutokea, urafiki ukageuka kuwa shubiri, ukagubikwa na uadui wa kutaka hata
kuuana….’akasema
‘Kwanini sasa, mimi nilijua marafiki kama nyie, mliojuana,
hamtaweza kuachana…?’ nikauliza
‘Hapana, yule simtaki tena, hata kumuona simtaki hata aje nyumbani
kwangu…,’ akasema wka hasira….kwa kauli hiyo nikawa na hamasa ya kutaka kujua
kilichoajiri kati yao wawili,
Awali hakutaka kunisimulia undani wa maisha yao, hasa
kilichosababisha hadi urafiki wako ukafa na kujenga chuki za kutaka kuuana,
lakini baadae akaanza kunisimulia…kilichowafanya marafiki waliojulikana kuwa ni
mrafiki wa kweli, marafiki ambao kila mtu alikuwa akitolea mfano kwao, lakini
sasa ni maadui wakubwa….
***********
Miaka ikapita na mimi nikajaliwa kuwa na watoto wawili mapacha wa
kike na rafiki yangu akawa akitoka kazini anakuja tunakuwa naye, ananisaidia
kuwalea, kiasi kwamba watoto hawa walimuona kama mama yao. Na kwa ukaribu huo,
watoto wangu walimpenda sana.
‘Nawapenda sana watoto wako, natamani niwe na watoto kama hawa,
kwa sura, …natamani mume wangu anizalie kama watoto hawa…’akasema
‘Utawapata tu usijali…lakini muhimu uolewe, umri unakwenda, urembo
wa msichana una kikono chake…’nikamwambia tukiwa tunaongea…
Kuna kitu ambacho anacho rafiki yangu, alipenda sana kuchagua wanaume…sio kwa wanaume
tu, hata vitu vyake akitaka kununua, yeye anachukua muda mrefu sana kufikia
maamuzi, atachagua wee, atatoa kasoro wee….mpaka aridhike, itachukukua muda
sana..kilichoniumiza ni kuona rafiki yangu haolewi, na umri unakwenda, yeye hakulijali
hilo mapema na siku zikazidi kusonga mbele.
‘Rafiki yangu ukumbuke umri na urembo wa mwanamke, una kikomo,
jinsi unavyozidi kukua, na urembo nao unapungua, ..na ujue mwenyezimungu
anakupatia neema zake uzitumie, ukizipuuza, itafika muda atakunyang’anya, na
hapo utaaanza kulalamika…’nikamwambia.
‘Usijali…ipo sku nitakuambia kusudio langu ni nini…unajua rafiki
yangu sipendi nije kuumia,…sipendi nije kujutia,..muda utafika na wewe
hutaamini…’akasema
‘Hapo sikuelewi, ina maana kuna kitu unanificha…?’ nikamuuliza
‘Hapana…wewe niamini tu, siwezi kukuficha kitu , wewe ni mimi na
mimi ni wewe,lakini siwezi kukuambia kitu ambacho hata mimi sina uhakika nacho
, bado sijawa na uhakika wowote kwa hivi sasa, ni nani na nani wa kunioa,
nimtakaye hajaonekana na kila ninayempenda, nakuta keshawahiwa, nashindwa
kuelewa ni kwanini…’akasema
**************
Siku zikaenda watoto wangu wakawa wakubwa, na wanaanza shule, hebu
fikiria, miaka mingapi, kama kumi hivi, bado rafiki yangu hajaolewa,…
Siku moja mwenzangu huyu alikuja nyumbani kwangu, akanikuta mimi
nipo na watoto wangu, huwa nikiwa nyumbani kama nimemaliza kazi zangu , huwa
napenda kucheza na watoto wangu, najishusha nakuwa kama mtoto mdogo, tunacheza
ile michezo niliyokuwa nikicheza nikiwa mdogo, basi ni faraja kwa watoto wangu.
Rafiki yangu akaingia na
akawa ananiangalia nikicheza na watoto, aliniangalia kwa makini sana,..nikahisi
kama anataka kulia, siku zote huwa ana ujasiri fulani, akija kwa vile watoto
wamemzoe kama mama yao, basi watamkimbilia, wataanza kucheza naye, na huku
kucheza na watoto yeye ndio kanifundisha…
Lakini siku hiyo, haikuwa hivyo, alikuwa akiwa kanywea, hana raha
kabisa, ule uso uliojaa ujasiri haupo tena,, watoto kama kawaida yao
walipomuona wakamkimbilia, na akasalimiana nao, kiukweli watoto wangu
walimpenda sana rafiki yangu huyu, hata yeye, na hakuchoka kuwasifia kuwa ni
watoto wazuri, anapenda kuwa na watoto kama hao.
Siku hiyo hakuwa mchangamfu kabisa, nikajua kuna jambo, awali
nilihisi labda anaumwa, lakini nilipomuuliza akasema haumwi,..nikaona kuna
jambo jingine kubwa limemtokea, labda…, ikabidi niwatoe watoto ili nipate muda
wa kuongea naye
‘Ok.. rafiki yangu vipi leo,…sio kawaida yako, hutaki hata
kujiunga tukacheze na watoto kama kawaida yako.., unajua watoto wangu wakikuona
wanahisi furaha sana, wanakuona wewe ni mama yao wa ukweli, kuliko hata mimi,
vipi leo kulikoni…?’ nikamuuliza
‘Oh rafiki yangu jana sikulala, mawazo,….nahisi sio mimi tena,…sikuwa
hivi kabla,….’ Nikaona machozi yakimlenga lenga.
‘Mhh, usilie bwana, niambie kuna tatizo gani…?’ nikamuuliza.
‘Unajua rafiki yangu mara nyingi huwa najipa matumaini, lakini kipindi
hiki cha siku mbili tatu, nimekuwa nikiumia sana, nawaza kupitiliza, na hata
kujiuliza, ni kwanini, unajua alipo…nitenda yule mwanaume, kunikasaliti wakati
nilishapanga yeye ndiye wa kunioa, namkuta na mwanamke mwingine ndani, …imenivunja
sana nguvu…’akasema
‘Lakini wapo wengine au sio..keshaoa, achana naye….’nikasema
‘Kwanini sasa inatokea hivyo, kile ninayempenda, tunakwenda
vizuri, baadae hali inageuka, inatokea jambo tunakosana na huyo mwanaume ama
awe msaliti, au awe na imani nyingine ya dini, na siwezi kuacha imani yangu ya
dini, sasa nifanyeje jamani…yaani hata sielewi, inafikia muda siwaamini tena
wanaume, kwanini nisimpate mwanaume kama huyo wako….’akasema
‘Utampata tu rafiki yangu, wewe subiria muda utafika…’nikasema
‘Yaani hata kwenye ndoto nimeota nakuona wewe upo na watoto wako
na mume wako mnafurahi, mimi nipo peke yangu porini, mkiwa, ..oh, mara
nikajiukuta nipo kati kati ya bahari nachukuliwa na maji, napiga ukelele, wa
kuomba msaada, hakuna wakunisaidia, nikawa nawaita nyie, mje kuniokoa lakini mkawa
hamnisikii, nikawa nazama, nikashtuka …’akatulia
‘Hiyo si ndoto tu, au…?’ nikamuuliza
‘Ni ndoto ndio..lakini nahisi imetokea kwa vile jana niliwaza
sana,..mara nyingi najipa matumaini, nikirudi nafanya hiki na kile siwezi sana,
lakini jana, sijui ilikuwaje, hawa watu wamenitibua kweli, ..ndio maana sitaki
kuolewa…’akasema
‘Akina nani tena…?’ nikamuuliza
‘Si hawa wanaume..inafikia sasa wananiringia mimi, …kuna mmoja
kanibwatukia mpaka hamu yake ikaisha, akafikia kusema, nitaishia kuzeeka bila
mwanaume..sawa, labda ana ukweli wake, lakini haya ndio maisha yangu, kama
anataka anioe, anioe basi, yeye anasema anataka kunipima kwanza, kunichezea,
hapana hilo siwezi kabisa…’akasema
‘Kwahiyo, umeshakata tamaa au sio…?’ nikamuuliza
Hapo akakaa kimia akiwa
kashika shavu ile ya kusononeka, kiukweli kama rafiki yake ilinuma sana,
nikamsogelea na kumkumbatia, hapo akalia kweli, hadi alipotulia, nikamwambia
akae , najua sasa ile hasira yake imekwisha
‘Unajua rafiki yangu, ndio maana nilikushauri awali uolewe na yule
mwanaume wa kwanza aliyekuwa rafiki yako, ukamkataa, na hawa wengine ilikuwa
sio bahati yako, ni wao walikusaliti, sio kusidio lako, tumuachie mungu tu…’nikasema
‘Mhh..ni kweli rafiki yangu sasa kweli naona nimechelewa, maana
hata waume nao siwaoni kabisa wanaonifaa, wa umri ninaoutaka mimi hawapo tena,
ninaokutana nao, ndio hao wanaotaka kuuchezea mwili wangu, kitu ambacho
sikitaki,..natamani atokee mume wa kweli, alete posa, simuoni..wale niliowataka
ndio hao wameshaoa…kiujumla kwa sasa sina raha tena…’akasema
‘Sasa unatakaje, maana hata mimi sipati usingizi nikikuwazia wewe.
Tumejadiliana na mume wangu tuone jinsi gani ya kukusaidia, lakini wanaume
tulio-waona wanakufaa, ndio hao wameshaoa, kama ulivyosema, lakini bado wapo
wengine, na wewe huwataki, kwasababu zako…na tulijua yule mliyekuwa naye
angekufaa, sasa unasema hamuelewani tena,…sasa, tukusaidieje..?’ nikamuuliza.
‘Kiukweli, nikikuona hivi, wewe upo na watoto wako, nawazia mbali
kabisa, najua nilishakosea, na umri ndio huu umeshakwenda sana....naona jinsi
gani ulivyo na raha na watoto wako,....nikiwaona watoto wako najisikia kukosa
kitu muhimu sana katika maisha,…’akasema
‘Utawapata tu…’nikampa matumaini hayo, lakini moyoni najiuliza kwa
vipi.
‘Nitawapataje sasa…?’ akauliza
‘Kwanini unasema hivyo rafiki yangu, kuwapata utawapata tu,
ukiolewa au sio, kwanza muhimu ndio hilo,kuolewa, mkubali mmojawapo akuoe, sasa
sio muda wa kuchagua tena…’nikasema hivyo na siku hiyo ikaishia hivyo, na
masiku yakazidi , miezi, miaka, rafiki yangu hajapata mume wa kumuoa.
Na siku nyingine ambayo naikumbuka sana, akafika kwangu, akiwa
hana raha, zaidi ya siku nyingine, nikajua ni yale yale…moyoni nikawa najiuliza
nitamsaidiaje, nifanyeje, ningelikuwa na ndugu yangu wa kiume ningelimshinikiza
amuoe, lakini sina,, ningekuwa sina wivu, ningemshauri aolewe na mume wangu,
lakini nina wivu wa kufa mtu
Hata mume wangu hataki kuoa
wake wawili alishaniambia,…kwani siku moja nilimtania tu, akaniambia niache
kabisa mawazo hayo, yeye hana uwezo wa kuoa mke zaidi ya mmoja, huyo mmoja
kwake, anaona ni kazi…ni mwanaume wangu namfahamu hivyo, kweli hawezi, na
hataki..sina shaka na hilo
Sasa nitamsaidiaje rafiki yangu….na katika maongezi ndio likanijia
wazo….wazo ambalo lilikuwa ni kisu cha kunichoma mimi mwenyewe…
Ni wazo gani hilo
WAZO LA LEO:
Urafiki mwema ni ule wa kujaliana kwa shida na raha, na mkikutana mnashauriana
mambo ya heri, mambo yenye tija, na hakikisha kuwa pale unapotoa ushauri kwa
mwenzako unampatia ushauri ambao hata wewe ungeliweza kuufanya au
kufanyiwa. Usije ukamshauri mwenzako kwenye jambo ambalo kama utakuja kufanyiwa
wewe hutakuja kupendezewa nalo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment