Haya
tuje kwenye kesi yetu moja kwa moja, ni kwanini huyu mtoza ushuru aliuwawa, na
aliuliwa na nani na kundi au...?’
‘Kabla
sijajibu swali lako, kwanza ni vyema tukamtambua huyu marehemu, mtoza ushuru,
alikuwa nani hadi kifo chake
‘Marehemu
ni vijana wa mwanzo walioandaliwa na hilo kundi, na alipewa hiyo kazi mwanzoni
kabisa, na hadi anafariki, alikuwa ameshafikia kiwango cha u-mwenzetu,...U-mwenzetu
ni kiwango cha juu katika kundi, wana vyeo vyao wenyewe, na hadi anafariki, alishafikia
hatua hiyo na akawa anaandaliwa kupewa cheo kikubwa...’
‘Huenda
cheo hicho ndicho chanzo cha kifo chake, kwasababu migogoro ndani ya kundi,
ilianzia ipindi hicho, wakati wanataka kumpata kiongozi muwakilishi wa kundi
kwa hapa nchini, ukumbuke kundo hilo sasa ni la kimataifa,...’akasema
‘Katika
kugombea vyeo, kila mtu akimtaa mtu wake,kukatokea mgongani, wenyewe kwa
wenyewe wakaanza kupigana vita, na marehemu akaanza kushutumiwa kwa makosa
mbali mbali, makosa ambayo hata wao wenyewe walikuwa nayo, lakini kwa mtizamo
tofauti marehemu akaonekana kuwa anajijali mwenyewe, na hata baadaye kufikia
kumshuku kuwa anasaliti kundi..na hi ilitokea kipindi akiwa na mahusiano na
mdada...’akasema.....
Tuendelee na kisa chetu
******
Ni wakati wakili mtetezi anataka kuanza kuuliza maswali
, na ndipo kukatokea kitu muelekeo wa mlangoni, na hapo, kukatokea kama sauti
ya watu kuhangaika, na kuanza kugeuka kuangalia muelekeo wa mlangoni...
Watu wote waligeuka kuangalia kule mlangoni,na hata mimi
nikageuka kuangalia, na hakimu naye halikadhalika akawa anafanya hivyo hivyo,
nikajiuliza kuna nini, ...na mimi nikageuka, lakini sikuona cha ajabu huenda
aliyekuwa akiangaliwa alikuwa ameshapita, nikazidi kuangalia kama nitamuona
aliyeingia au kitu gani cha ajabu lakini sikuweza kabisa kumuona,au kuona tukio
lolote la ajabu,..
Watu sasa wakawa wananong’onezana hata yule ambaye hata
hakuwahi kuona hicho kichotokea huko muelekeo wa mlangoni, naye akawa na lake
jambo, ilimradi mdomo ufunguke, na mnongono wa watu wengi hugeuka kuwa ngurumo,
na mimi nafsini nikawa najiuliza kuna nini, kumetokea jambo gani..lakini
sikupata jibu
‘Utulivu, tunataka utulivu...’akasema hakimu akigonga
kirungu chake mezani
‘Wakili mtetezi unaweza kuendelea kumuuliza shahidi
maswali…’akasema hakimu, na wakili mtetezi akiwa kama kapigwa na butwaa, kwanza
akatulia kama anawaza jambo na bado akiwa anaangalia muelekeo ule wa mlangoni,
na baadaye akamgeukia hakimu na kusema;
‘Samahani sana Muheshimiwa hakimu, kwa sasa sina maswali,
na hata wenzangu, hawana maswali kwa sasa, nilitaka kuliweka hili wazi tu
muheshimiwa…’akasema na hakimu alionyesha mshangao, na alitaka kusema kitu
lakini akawa kama anafikiria jambo, baadaye akamgeukia wakili muendesha
mashitaka na kusema;
‘Wakili muendesha mashitaka unaweza kuendelea na mtu
wako, maana naona upande wa utetezi wanaonekana kukosa maswali ya kuuliza,
sijui ni kuelewa au bado wanatafakari,..tuendelee muendesha mashitaka ,maana
naona muda hautusubiri...’
Wakili muendesha mashitaka naye akiwa kama haamini,
maana alijua kunaweza kutokea maswali mengi upande wa utetezi, lakini aliona
ajabu kwa watu hao kuwa kimiya, naye akageuka upande ule wa muelekeo wa
mlangoni, akawa kama anaangalia jambo, huku uso wake ukimemeta kwa tabasamu,
tofauti na uso wa wakili mtetezi, aliyekuweo hapo muda mfupi, wakili huyu akasema;
‘Ukweli umedhihiri muheshimiwa hakimu, ndio maana
wenzetu wameshindwa hata kuuliza swali moja, sisi tunachotaka hapa ni haki
itendeke....’akasema huku akiangalai upande ule wa utetezi, halafu akamgeukiwa
shahidi wake, na kusema;
‘Sasa tutaendelea na shahidi wetu, tukumbuke kuwa huyu
ni mtaalamu, kwahiyo yote anayoyaongea hapa kayafanyia kazi na tafiti yakinifu,
na kila jambo lina ushahidi wake, hatuongea kwa maneno tu, tutakuja kuonyesha
shahidi zote na mashahidi wengine kuthibitisha haya wapo,....’akasema na
kuangalia kule muelekeo wa mlangoni, huku akitabasamu, na baadaye akamgeukiwa
mpelelezi na kusema;
‘Shahidi wetu, mpelelezi, mtaalamu, sasa ni wakati wa kutuelezea jinsi mtoza
ushuru alivyouwawa kutokana na uchunguzi wako na jinsi kifo chake
kinavyohusiana na hilo kundi….’akasema muendesha mashitaka
‘Kwanza hebu tueleze siku ile ya tukio , siku ile ambayo
mtoza ushuru aliuwawa, wewe ulikuwa wapi?’ akaulizwa
‘Siku ile ya tukio, siku ambayo mtoza ushuru aliuwawa, mimi
nilikuwepo hapo hapo kwenye eneo la nyumba ya mdada...’akasema na watu
wakaguna, na kuanza kunongong’ona, na hata hakimu naye akaonyesha uso wa
mshangao na kuuliza hilo swali tena
‘Ina maana ulikuwepo eneo hilo, kwa ndani au kwa nje...?’
hakimu akauliza hilo swali akiwa kama hajaelewa na alionyesha kushangaa kidogo.
‘Nilikuwepo ndani ya eneo la hiyo nyumba, yaani
nilishaingia getini na kuwa kwenye sehemu ya nje ya nyumba, lakini sio ndani ya
jengo la nyumba yenyewe,....’akasema shahidi
‘Ukisema ndani ya eneo, ina maana ni kwenye viwanja,
inawezekana ni sehemu ya bustani, au sehemu yoyote ya nje, lakini sio ndani ya
nyumba wanapoishi watu au sio?’ akauliza muendesha mahistaka
‘Ndio hivyo muheshimiwa,....’akasema
‘Ehe, hebu sasa endelea na maelezo yako sitaki
kukuongoza natumai unajua jinsi gani ya
kuyaweka maelezo yako sawa ili
yaeleweke kwa muheshimiwa hakimu na mbele ya mahakama hii tukufu...’akasema
wakili muendesha mashitaka.
‘Siku hiyo mimi nilikuwa na ahadi ya kukutana na mdada,
ni ahadi isiyo rasimi, yaani yeye hakuwa na taarifa ya ujio wangu, na
nilipofika karibu na eneo la makazi yake,nikaona kuna mishughuliko isiyo ya
kawaida, baadaye niliona gari likija na mtu mmoja akatoka ndani ya gari, mtu
huyo alikwenda kuongea na mlinzi....’akatulia kidogo
‘Mimi nikajongea hadi eneo la getini, nikawa nawaona mlinzi
na huyo mtu wakiongea, na kwa muda huo gari alililokuja nalo huyo mtu lilishaondoka,
mimi nikapata nafasi ya kuweza kusogea zaidi na niliona geti likiwa nusu wazi,
na muda huo mlinzi akatoka kwenye lindo lake, na kumuacha yule mtu aliyefika
hapo kwenye lindo...’akasema
‘Alitoka kwenye lindo kwa vipi, kutoka nje, au kuelekea
wapi?’ akaulizwa
‘Alitoka kwenye kibanda chake cha ulinzi na kuelekea
kwenye nyumba, na kumuacha yule mtu akiwa kasimama nje ya hicho kibanda cha
huyo mlinzi,alikuwa kasimama kwa nje ya hicho kibanda huku akiwa anaongea na
simu ya mkononi...’akasema
‘Nilimchunguza yule mtu kwa haraka nikagundua kuwa kwa
muda huo huyo mtu mawazo yake yalionekana kumuangalia zaidi yule mlinzi, na huku
anaongea na simu...’akatulia
‘Na kwa akili za kawaida, mtu huyu asingeliweza kuwa
makini na kitu kinachotokea nyuma yake, na hapo mimi nikautumia hiyo nafasi,
nikasukuma mlango wa pale getini , na kwa mwendo wa haraka wa kujificha, nikaambaa-ambaa,
sambamba na michongoma, kuelekea sehemu ya maegesho ya magari, bila ya huyo mtu
kuniona...’akasema
‘Na wakati huo mlinzi alikuwa ameshafika maeneo ya
maegesho ya magari, hakuelekea mlangoni kama nilivyohisi , kuwa labda alitumwa
ndani na huyo mtu,kuongea na bosi wake, lakini cha ajabu huyo mlinzi akaelekea
maeneo ya maegesho ya magari, na kwa haraka akaingia kwenye gari la madada, na kwa
muda huo mimi nilikuwa nimeshafika maeneo yale kwa kujificha, nikatulia sehemu
huku nikiwa na simu yangu nikichukua matukio yote hayo...
‘Nilimuona akiingia kwenye gari la mdada, na hakukaa
sana akatoka kwenye gari hilo akiwa kashika Nyundo mkononi...’alipotaja nyundo
watu wakaguna, na hata hakimu akawa anaandika kitu huku akipitia pitia
makabrasha yake...
‘Ilikuwa ni nyundo na pisipisi, akaelekea sehemu ya
dirisha la nyuma, ...nilikuwa na nilijitahidi sana kuchukua matukio hayo kwenye
simu yangu mkononi ambayo ina nguvu ya hali ya juu kuchukua matukio, kwahiyo
hayo yote ninayoyaongea hapa yapo kwenye vielelezo vya ushahidi kama mnataka
kuyaona kama ushahidi...’akasema
Wakili muendesha mashitaka akasogea na kuinua juu mfuko
uliokuwa na kanda za video, na kusema
‘Ushahidi wote upo hapa....hamna shaka...’akasema
‘Endelea mtaalamu wetu...’akasema muendesha mashitaka
‘Kwahiyo mlinzi alipochukua nyundo na ile pisipisi, akatembea
hadi kwenye dirisha la nyumba ya mdada, na nikamuona akitoa ile pisipisi
akatumbukiza kwenye kona za dirisha na kuanza kufanya jambo, kumbe alikuwa akipachua
dirisha, kwani baadaye niliona akilisukuma kwa mkono likafunguka na kwa haraka
akaingia ndani kwa kupitia dirishani....’akasema na muendesha mashitaka
akasema;
‘Hadi hapo tumeelewa, kuwa mlinzi aliingia ndani kwa
kupitia dirishani sio mlangoni kama ilivyoelezewa awali, je wenzetu upande wa
utetezi mna swali, ....?’ akauliza na upande ule ulikuwa kimiya
‘Sasa nikuulize mpelelezi, kabla hujaendelea nataka hili
liwe wazi, wewe ulimuona mlinzi akiingia ndani kwa kupitia dirishani na je
ulimuona wakati anatoka?’ akauliza
‘Ndio nilimuona wakati anatoka...’akasema
‘Wakati anaingia alikuwaje na wakati anatoka
alitokaje...?’ akaulizwa
‘Wakati anaingia alikuwa hakuvaa gloves mikononi, yaani kinga za kuzuia alama za mikononi, ila
wakati anatoka alikuwa amevalia hizo kinga za mikononi na akiwa kashikilia ile
nyundo, pisipisi na mfuko wa bahasha kubwa, nahisi ndani kulikuwa na kitu...’akasema.
‘Bahasha hiyo ni kubwa, na ilionekana kuwa na vitu ndani
yake, ni kubwa za kuweza kuweka faili hizo kubwa za kiofisi...mkiangalia kwenye
hizo kanda, mtaona vyema...’akasema
‘Yule mlinzi alipotoka alitoka kwa haraka sana na kukimbilia
muelekeo wa kuelekea huko getini....’akasema
‘Una uhakika kuwa kweli alielekea getini?’ akaulizwa
‘Nina uhakika maana nilitoka pale nilipojificha na kuangalia
upande wa maelekeo huo japokuwa sikuweza kuona vyema kwa mbele,lakini kwa jinsi
alivyokimbia alionekena kuelekea huko...’akasema.
‘Haya hebu tuambie wakati upo hapo nje, uliona nini
kingine au kusikia kitu gani kingine?’ akaulizwa
‘Nilisikia mlio wa risasi...lakini haukuwa na nguvu
sana, kwasababu ukiwa nje, huwezi kusikia sauti ya kutoka ndani kwa ukamlifu
wake, na mimi nilitambua moja kwa moja kuwa huo ni mlio wa bastola, kwa vile
nina uzoefu na vitu hivyo,lakini kwa mtu asiye na uzoefu wa milio kama hiyo
asingeliweza kugundua hilo....’akasema
‘Ulifanya nini, uliposikia hivyo?’ nikamuuliza
‘Hakukuwa na muda wa kufanya lolote, zaidi ya kutafuta
njia za kuondoka hapo kwani kwa muda huo mfupi polisi walishafika,...polisi
walifika muda ule ule wakati mtu mmoja niliyemuona akitokea ndani akiwa anakuja
muelekeo wa pale nilipokuwa nimejificha.
Mimi niliona kuendelea kukaa pale nistashindwa kuendelea
na uchunguzi wangu ambao sikutaka kuingiliwa na polisi,...nilichofanya ni
kutafuta njia ya kutoka ndio nikamuona yule mtu yupo mikononi mwa polisi, na
muda huo nilishafika maeneo ya getini ...’akasema
‘Huyu uliyemuona akiwa mikononi mwa polisi ni nani, ni
yule wa mwanzo au ni huyu aliyetokea ndani?’ akauliza
‘Ni huyu wa pili...’akasema
‘Okey, huyo wa mwanzo tutakuja kumuongelea baadaye,
nataka kumjua huyu wa pili ni nani?’ akauliza
‘Huyu wa pili ni mhasibu,....’akasema na watu wakaguna
na kuanza kunong’ona...hadi hakimu akasema
‘Utulivu....endelea na maelezo yako’ akasema hakimu
‘Huyu mtu alivyotoka mimi sikumuona kuwa ametokea wapi,
ila alikuwa anakimbia kuja muelekeo huo wa maegesho ya magari, nilimuona wakati
anakaribia maeneo hayo ndio polisi wakamuona maana muda huo polisi walishafika,
na hapo hapo mimi nikatafuta muelekeo wa kutoka nje, sikutaka kukutana na
askari polisi kwa muda huo.
‘Huyu mtu ulivyomuona kwa muda huo mfupi kabla hajaingia
mikononi mwa polisi, alikuwa vipi, na je hukuona mtu mwingine aliyekuwa na
ndevu..akitokea ndani kwa muda wote uliokuwepo hapo?’ akaulizwa
‘Huyu mtu aliyetokea ndani alikuwa na wasiwasi sana, na
kitu nilichokigundua ni kuwa alikuwa akijipangusa kwenye kidevu,na ghafla
akavamiwa na maaskari, akanyosha mikono juu na huku akionyesha kwa mikono kwa
wasiwasi kuelekea mlangoni, lakini polisi hawakumpa muda wakawa wamemshika na
kumuweka pingu.
‘Na muda huo nilikuwa nimeshapata upenyo nikawa sambamba
na mlinzi,na mlinzi aliniona lakini yeye alijua kuwa mimi ni sehemu ya maaskari
waliofika hapo, mimi nikamnyoshea mkono
kama kumsalimia, nikamsogelea na kumuuliza
‘Kumetokea nini hasa?’ nikamuuliza
‘Kumetokea kitu kama mlio wa bastola...ni, bastola, kimetokea
huko ndani, ndio polisi wameshafika,
nashangaa kwa jinsi walivyofika kwa haraka , sijui zaidi...’akasema
‘Wakati wanafika wewe ulikuwa hapa getini?’ nikamuuliza na
yeye akaniangalia kwa wasiwasi, halafu akasema
‘Nilikuwa nimekwenda kujisaidia na wakati narudi, ndio
nikasikia huo mlio na polisi wakaanza kuingia....’akasema
‘Kwahiyo wakati wanaingia hukuwepo kwenye lindi lako...?’
nikamuuliza
‘Ndio.nilikwenda kujisaidia....’akasema sasa akionyesha
wasiwasi uliodhahiri.
‘Na mwenzako kaenda wapi?’ nikamuuliza
‘Mwenzangu!, Mwenzangu gani, mimi nipo peke yangu....’akasema
akionyesha kushangaa, huku akiniangalia kwa wasiwasi, na hapo nikapata picha
kuwa mlinzi hataki huyo mtu mwingine aliyekuwepo hapo afahamike,...’akasema
shahidi na wakili muendesha mashitaka akaingilia na kuuliza
‘Je wakati unatoka , ukitafuta upenyo wa kutoka nje,
hukumuona huyo mtu mwingine aliyekuwa kaachwa hapo getini?’ akaulizwa
‘Sikumuona kabisa, inaonekana huyo mtu aliondoka haraka
na mapema sana, na hata ile bahasha aliyokuwa nayo mlinzi sikuweza kuiona
popote maana niliingia ndani na kuanza kufanya upekuzi sikuona kitu, kwahiyo
hiyo bahasha ndicho alichokuwa kakifuata huyo mtu mwingine,alipokipata
aliondoka...’akasema mpelelezi.
‘Na wakati unasikia mlio wa risasi ulikuwa bado sehemu
ya nyuma, kwahiyo hukuona mtu mwingine yoyote akitoka?’ akaulizwa
‘Kwa muda huo hadi mlio wa risasi unasikika, nilikuwa
upande wa nyuma, sehemu ya uficho ambayo huwezi kuona mbele ya nyumba hiyo,
kwahiyo kwa huko mbele kama kulitoka au kuingia mtu nisingeliweza kuona, na
hadi mlio wa risasi unasikika, bado nilikuwa sehemu ile ile, ila nilishaanza
kusogea sehemu ninayoweza kuona kule dirishani alipoingilia huyo mlinzi.
‘Mlinzi alipotoka alionekana vipi?’ akaulizwa
‘Alionekana mwingi wa wasiwasi, nilimuona akihangaika
hata kufunga dirisha ilikuwa ni kwa kuhangaika sana alionekana kutetemeka, hadi
kuangisha ile pisipisi, ambayo hakukumbuka hata kuiokota, mimi niliwahi
kuikota, ...’
‘Kwahiyo mlio wa risasi ulisikika mlinzi akiwa ndani ya
hilo jengo?’ akaulizwa
‘Ndio alikuwa bado yupo ndani ya hilo jengo...’akasema
‘Na hukuona mtu mwingine kutoka zaidi ya mlinzi
aliyetokea dirishani na mhasibu aliyetoka na kukamatwa na askari, je huyu
mhasibu alitoka baada ya risasi au kabla ya mlio wa risasi kwa jinsi
ulivyoona...’akaulizwa
‘Huyu mhasibu muda anatoka na ndio mlio
unatokea....sizani kama alikuwa ndani, haingewezekana, ni muda anatoka, na mlio
unasikika, nasema sizani, maana huyu mtu nilimuona akija muelekea wa maegesho
muda mfupi sana baada ya huo mlio, ...’akasema
‘Haiwezekani kuwa alikuwa ndani wakati mlio unatokea na
ndio akakimbia?’ akaulizwa
‘Hapana haiwezekani, ..kwa mpangilio wa muda, ni lazima mlio
ulitokea wakati anatoka ukiangalia maheabu ya muda....’akasema
‘Na kule getini, ulisema kuliachwa mtu, je wewe wakati
unatoka,hukumuona huyo mtu..?’ akaulizwa hilo swali tena
‘Sikumuona huyo mtu tena,..walikuwa wameshafika
maaskari, ni muda mfupi sana,hao maaskari walifika mapema sana, ni kama vile
walikuwa hapo nje wakisubiria tukio..’akasema mpelelezi
‘Sasa hebu tuambie kuhusu huyu mtu wa kwanza, huyu mtu
uliyemuona akiongea na mlinzi akaachiwa ulinzi hebu tumfahamu alivyo, kabla
hujatuambia jinsi gani kifo cha mtoza ushuru kinavyohusiana na hili kundi, je huyu
mtu wa kwanza uliyemuacha getini ni nani,alionekana vipi?’ akaulizwa, na mara
kukatokea ghasia upande wa nyuma, ilionekana kuna mtu alikuwa kaingia, na
kusukuma watu...
‘Utulivu, kuna nini hapo maeneo ya mlangoni, ...walinzi
hebu hakikisheni utulivu upo...’akasema hakimu na kukaonekana bado kuna mtu
anataka kupita mbele, na walinzi sasa wakawa wanawaondoa watu ili kupatikane
njia....
NB: Kuna nini zaidi, tuzidi kuwepo sehemu ijayo?
WAZO
LA LEO:Ustaarabu wa mtu huonekana katika kauli na mateno. Kauli
inaweza ikamfanya mtu aonekane jinsi alivyo...kwa,jisni gani anavyoweza kuongea
na watu mbali mbali, wakubwa na wadogo, au jinsi gani anavyoweza kuelekeza
jambo, au jinsi gani unavyoweza kutoa hoja mbele za watu.
Kuna watu hawana huo ustaarabu, hawajui waongee kauli
gani kwa wakati gani, au waonyeshe adabu gani kwa watu wa iana gani. Ni muhimu
sana watu tukajichunga kwa tabia hizi kwani vitu vidogo vidogo kama hivi
vinaweza kusababisha mzozano, chuki, na hata maumivu kwa watu wengine, kwa kauli tu, tunazozitoa mdomoni.
Tukumbuke kuwa hulka na tabia njema, sio matendo tu bali
ni pamoja na kauli zako kwa wenzako, na kwa jamii.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
kazi nzuri sana yaani..nasubiri mwendelezo wake
Post a Comment