Mpelelezi akawa ameshapita kwenye kizimba cha kusimama
watu wanaotoa ushahidi, baada ya kukamilisha taratibu zote kwa mujibu wa
sheria, baadaye akaanza kutoa maelezo yake akiongozwa na muendesha mashitaka.Mimi niliwatupia macho kundi la washitakiwa niliwaona wengine wakificha nyuso zao.
‘Hebu
tuambie wewe ni nani.....?’ akaulizwa
‘Mimi
ni askari mpelelezi wa kesi mbali mbali kwa mujibu wa sheria....’akasema
‘Kwahiyo
wewe ni askari kanzu kama wanavyoita watu....’akasema muendesha mashitaka
‘Ndio
hivyo kama wanavyoita watu...’akasema
‘Hebu
tuambie utaalamu wa kazi hii uliupatia wapi?’ akaulizwa
‘Mimi
baada ya kujiunga na jeshi la polisi, nikitokea chuo kikuu, nilipelekwa nje
kusoma, nikisomea mafunzo hayo hayo ya upelelezi, lakini katika kitengo cha maswala
ya ujasusi, yaani makosa yanayotokana na makundi haramu, ambayo yanafanywa
kitaalamu zaidi, na hasa katika uhalifu mkubwa wa kimataifa.
‘Lakini
sisi tujuavyo askari kanzu wanajificha huwezi kuwatambua, mbona wewe hujifichi,
na wakati mwingine unaonekana ukiwa rasmi na mavazi ya kipolisi..?’ akaulizwa
‘Ndio
wapo askari wa namna hiyo lakini pia wapo askari wapelelezi wa namna yangu
ambao hawajifichi, ambao tupo wazi kwa raia, na raia wenyewe wanafahamu kabisa
kuwa huyu ni askari mpelelezi....ni mgawanyo wetu wa kazi....’akasema
‘Kwasababu
wewe ni mtaalamu, hebu sasa tuelezee, elezea mahakama hii kwa makini jinsi
ulivyoweza kuifanya hii kazi hadi kuligundua hili kundi haramu,hatua kwa hatua...’akasema
muendesha mashitaka
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, baada ya kutokea wizi mkubwa
na upotevu wa mara kwa mara wa nyaraka za serikali, serikali iliona kuwa kuna
umuhimu wa kufanya uchunguzi wa kina, kwahiyo kwa vile walikuwa na watu tayari
wameandaliwa kwa kazi hizo wakawatuma watu wao kufanya hiyo kazi...
‘Kiukweli mwanzoni, ilifanyika kazi nzuri, na
kukabainika kuwa kuna kundi limejijenga kwa mbinu na linafanya kazi yake kimiya
kimiya likiwa limejificha ....wao wakatoa taarifa yao, lakini utekelezaji wake,
ukaishia kimiya kimiya. Na mwanzilishi wake hakubainika moja kwa moja...
Hali ikatulia kidogo, lakini kumbe watu hawa walikuwa
wakijipanga upya, ilikuwa kama wamegundua kosa lao lipo wapi, serikali ikaliona
hilo, na wao wakajipanga kinamna ambayo inaweza kulimaliza abisa hilo kundi,
ndio wakanipa hiyo kazi maalumu ya kuchunguza hili kundi kiundani zaidi.
Kwa ujumla hili ni moja ya makundi haramu, ni kundi la
kijasusi lenye mbinu za hali ya juu, kiasi kwamba huwezi kufahamu kuwa
wanajishughulisha au wana nia mbaya katika jamii. Kwa nje wataonekana ni watu
wema sana, wanatoa misaada , wanajenga mashule, na kila aina ya huduma
wanakuwepo...
Muanzilishi wake, aligundua kuwa ili uweze kuwateka
wanajamii kirahisi, ni vyema ukajikita kwenye shida zao, udhaifu wao,...hasa
kwenye maadui wakubwa wa binadamu, ujinga , umasikini na maradhi,...huko ndipo
walipowekeza, kitaalamu kabisa...
Wakaanzisha mashule, mahospitali, majumba ya ibada, na
hata mabenki, na vitega uchumi, na hivyo vyote vilitoka humo humo kwenye kodi
ya wanajamiii, na misaada toka nje, kwa mbinu, na utaalamu wa hali ya juu...
‘Watu hawa ni wazawa, wamesomeshwa na kodi ya serikali,
na sasa wanakuja kulipa hizo fadhila, na hizo ndizo fadhila zao,...wananchi
hawajui, wanachojua ni kuwa hao watu wamekuja na elimu yao ya kuweza kuwasaidia
, maana kweli wamejenga mashule, wamejenga, mahospitali,...yote hayo ni muhimu
kwa jamii....’akatulia kidogo pale wakili alipoonyesha kumzuia asiendelee, na
wakili akasema;
‘Hebu hapo tufafanulie, jinsi hawa watu walivyoweza
kuwekeza, walipatia wapi hizo pesa, na jinsi gani walikubalika, elezea kwa
undani, kuhusu kundi hilo , jinsi lilivyoanzishwa hadi kuanza kuleta matatizo
katika jamiii....’akasema muendesha mashitaka.
‘Kundi hili lilianzishwa na jamaa moja aliyekuwa na
ndoto ya kuja kuwa mtu mkubwa sana duniani, na ndoto yake hiyo ilianza wakati
akiwa anasoma huko nchi za nje..na alijengwa na tamaa hiyo kwa vile alikuwa
msomaji mnzuri wa vitabu vyenye maelezo ya kijasusi, akavutika, na watu kama
akina Carlos, na wengineo.
Siku moja akakutana na marafiki zake ambao walipenda
sana kusoma hivi vitabu vya hadithi, wakawa wanahadithiana, na mmoja wao
akasema;
‘Hivi kweli hivi vitabu tunavyovisoma, ni kwa ajili tu
ya kujifurahisha, hivi humu ndani hakuna cha kujifunza zaidi ya kujifurahisha, hamuoni
kuwa kuna mambo tunaweza kuyafanya, tukawa kama wao, mimi nimekuwa nikivisoma
katikakati ya mistari hamjaliona hilo hata nyie...?’ akawa anauliza
‘Mhh, ni hadithi, tu bwana, lakini kwa mwenye akili
anaweza kujifunza jambo...ila mimi ninavyoona wengine wametunga kinjia ya
propaganda, watunzi wengi wanatumia sana hii mbinu, kushawishi watu kwa ujanja,
ili waamini kile wanachokitaka wao, au wanachokitaka watu fulani, au kundi
fulani, hilo ndilo nililoliona mimi....’akasema mwenzao.
‘Mimi nina wazo, sisi sote ni wasomi, na akili zetu
zinatambuliakana, sisi ni wale waliojaliwa akili za hali ya juu,...tulikuja
huku kusomea mambo ya kisayansi, lakini kwa bahati mbaya, tukajikuta tunasomea
mambo ya kijamii,...hebu tuiangalia hii jamii na haya tuliyoyasomea tuyaweke
kisayansi zaidi, hapa hatuwezi kugundua jambo linaloweza kutusaidia baadaye....’akasema
mmojawapo
‘Sasa unataka tufanye nini?’ akauliza mwingine ambaye
aliingiwa na hamasa.
‘Tutengeneze tofauti, angalia watu walioweza kufanya
maajabu, walikuwa ni watu kama sisi, wakabuni mambo, wakaweza kujenga jamii kwa
namna moja na katika namna nyingine wakawa wanafaidika...hebu angalia watu kama
eeeh...
‘Watu hawa waliibuka kutoka chini kwenye jamii, kwa
ajili ya akili zao wakavumbua mambo, wakaweza kuunda jambo likakubalika katika jamii,
lakini kisiri wana ajenda zao, wakatajirika, na kuanza kuogopwa.....’akasema
‘Nahisi wewe kuna kitu umekigundua huenda ndio hicho
hicho nilichokuwa nikikiwaza mimi, hebu tuwekane sawa maana tunakaribia kurudi
nyumbani...’akasema mwingine
‘Wewe kwanza umegundua kitu
gani... tuambieni wewe kwanza...’akasema mwingine
‘Nataka tuanzishe kitu
ambacho tunaweza tukaitawala dunia....’akasema
‘Kuitawala dunia kwa vipi,
unaota...’akasema mwingine kwa kumaka
‘Kuitawala dunia sio lazima
uwe mfalme, sio lazima uwe kiongozi mkubwa wa kisiasa, unaweza kuitawala
kiuchumi, na hilo ndilo la msingi, na kuitawala kiuchumi sio lazima uanza na
miradi mikubwa mikubwa, hapana...’akasema
‘Sisi tukirudi nyumbani
tutakwenda kuwa viongozi kwenye mashirika mbali mbali, cha muhimu kwanza
tuhakikishe kitu ujamaa kinasahaulika, na yale makampuni yenye mlengo huo
yanakuja kumilikiwa kibinafsi, na wamiliki wake wanakuja kuwa sisi au watu
wetu...tutaanzia hapo...’akasema
‘Muhimu sana tuwe na akiba
zetu nje...ili lolote likitokea, tunajua wapi pa kukimbilia...’akasema mwingine
‘Oh, hilo wazo jema,
...tupeani nafsi ya kulifanyia kazi, lakini ni lazima tuwe na kitu kama chama,
au kundi, na tupate jina zuri tu...’akasema mwingine
‘Mimi napendekeza tuliite
kundi letu....`dunia yangu...’
‘Mimi bado hapo
sijawakubalia hiyo ni ndoto, hiyo dunia yenu mnayotaka kuianzisha labda
mkaianzishe kwenye sayari nyingine...’mmojawapo akawa mpinzani mkubwa, lakini
baadaye alikuja kukubali baada ya kuwa wanakutana mara kwa mara kulipangilia
vyema, wakaja kukubaliana na hilo wazo, na wakaanza kulifanyia kazi
‘Ujue hawa watu wana akili
sana, wao wangelipata nafasi ya kusomea masomo waliyoyaendea ya kisayansi
huenda tungelikuwa na wataalamu, lakini walipofika huko kwasababu mbalimbali
wakajikuta wanasomea masomo ya kijaamii, na hili ni tatizo sana....’akasema
mpelelezi.
‘Wenzetu hawataki tuwe na
watalaamu wa namna hiyo, au sisi wenyewe tunavutika na mambo mengine ya kupata
utajiri...sasa hawa watu walikuwa na akili ambazo tungezitumia kwa masilahi ya
nchi, lakini wao wakaja kuzitumia kibinafsi zaidi,...
‘Walichokuja kukubaliana ni
kuwa wakirudi cha kwanza ni kuhakikisha kuwa katika kila taasisi kuna watu wao,
katika kila idara wana watu wao, hata kwenye makampuni binafasi wanapandikiza
watu wao, lakini je hilo lingefanikiwa vipi...
‘Wakajipanga kwanza kwa
kupata wafuasi wakiwa huko huko....’akasema
‘Watu hawa waliendelea
kusoma huko nje, huku wakilifanyia kazi hilo wazo walilolibuni, kwahiyo wenyewe
wakagawana malengo, kila mmoja akasomea fani fulani kwa undani zaidi,...na somo
la ziada ni la kiujasusi wa kimataifa, ili waweze kutamba kokote kule...
Huyu muanzili wa wazo hilo
akamaliza masomo yake kwanza na kurudi hapa nchini, na wenzake wakabakia huko
wakimalizia masomo yao,na wakawa wanarudi mmoja mmoja, lakini kila mmoja akiwa
na lengo walilokubaliana na hata walipokamilika, wakaitana.
Kikao hicho kilifanyika kwa
siri sana, kilianza kama sherehe ya kukutana kwa wale waliosomea nje, na baada
ya shamra shamra jamaa wakaitana na kukumbushana malengo yao...
‘Waliwachukua watu , na
kuanza kuwafundisha kinamna, wao kama wadhamni, wakawaambia watu hao waanzishe
taasisi za kijamii, wao watawatafutia wadhamini, na misaada kutoka nje...
‘Taasisi zikaanzishwa
nyingi tu...za wasio jiweza, mashule, nakadhalika, na kila taasisi jamaa hao
wana mikono yao, walifanya hivyo kwani ili kujenga ukaribu wao na wananchi,
wakawa wanapata misaada toka nje, walipojiona wamepata sana, wakaanzisha
mashule yao, ambayo humo ndipo wapopata watu wao wanaowataka, na waliwalenga
sana watoto wenye vipaji maalumu, nia na lengo ni kupata vichwa, au majembe...
Na hao vijana walioweza kusomeshwa
na kuchaguliwa na wao wenyewe kwa uchunguzi maalumu, vijana hao kwa siri wakawa
wakapata mafunzo maalumu, ambayo waliyalenga kwenye mikakati yao, na vijana hao
walipomaliza hayo mafunzo wakasambazwa kwenye maidara, maofisi na kila sehemu
kutegemeana na kile walichokisomea..
Kazi sasa ikaanza, kila
mmoja alipewa majukumu, na majukumu hayo ni kuhakikisha, kila mmoja anaingiza
kiasi fulani kwenye mfuko wa kundi,dunia ikaanza kujengwa, maana ili dunia
iweze kuzunguka, ni lazima iwe na mali, na mali hiyo itapatikana wapi, ni
kwenye shughuli zetu, kodi zetu,mali asili yetu....wakaanza kujijenga
Kila sehemu nyeti walihakikisha
wana watu wao na kila sehemu zenye masilahi walihakikisha kuwa kuna mirija
yao...wakahakikisha pia sehemu za kuingizia mizigo zinakuwa na watu wao, ili
waweze kufanya biashara zao haramu bila kujulikana, ...kundi likazidi kukua, na
uimara wa kipesa, utajiri, ukawajengea kiburi, utaenda wapi usiwakuta....
Katika hali halisi watu
hawa walijulikana kama kundi la kusaidia jamii, na kila walipopata nafasi
walifanya hivyo, ila walifanya pia kwa msilahi, ingiza rupia upate dola, nini kama dola bwana, watu wakawa
wanajiunga bila hata wao kujijua, na wanajikuta wakikaribishwe kwenye shughuli
za kupongezana, na humo wakifika wanaulizana, nani mwenzetu, wao wenyewe `uwenzetu...’
una maana yao.
Kwasababu ya pesa,
kwasababu ya utajiri, kwasababu ya kuwa wao sasa wameshika kila eneo nyeti
wakaanza kuonyesha kiburi,..ile hali ya kujificha sana ikawa inaanza kufutika,
wakaanza kuonyesha makucha yao, kila aliyeingia akawa sasa anapewa amri kuwa
ukiingia hutakiwi kutoka unatoka ukiwa maiti, na kama ni mwenzetu ukiwa kwenye
sehemu nyeti ni lazima utii masharti ya kuwezesha wengine au kuwezesha kundi....
Kipindi cha nyuma kundi
hili liliingia matatani, kuna watu wa usalama waliwashutukia, na upelelezi
ukaenda hadi kugundua kuwa kuna kundi kama hilo, na kuonekana wanafanya mambo
kinyume na sheria ya nchi, na viongozi wao waanzilishi wengi wakakimbilia nje....
Hata hivyo hakukuwa na haja
ya kuwafuatilia kwani bado walikuwa hawajafanya jambo la kuwatia hatiani, na
wenyewe walipofika huko wakiwa wawekezaji maana walishawekeza huko, na
walishajipanga mapema kuwa kitu kama hicho kitatokea, na wafanye nini, na huko wakajifanya
hawahusiki tena,...lakini baada ya uchunguzi wangu nimegundua kuwa bado wapo
wanatoa amri, wanaelekeza, na wanafaidi matunda ya mambo yao..
Katika kila kitengo nyeti
wana watu wao, na wanajuana na kusaidiana, ...huku wakijifanya wanazalisha,
huku wakitoa misaada huku wakifanya mambo yao kinyume cha sheria, kama biashara
haramu, kukwepa kodi, na kuingiza bidhaa kutoka nje bila kufuata taratibu,na
zaidi wakawa wanafanya biashara ya madawa ya kulevya, ili kuzidi kuangamiza
vijana wetu....’akasema
‘Kama nilivyotangulia
kusema hawa jamaa walishaandaa watu wao, ambao wamesoma kwa taratibu zote,
lakini wakiwa wanafadhiliwa na kundi, wakiwa wamepitia mafunzo maalumu, na
wanajua ni ni wanachokifanya, na wakati mwingine wanapewa maelekezo kuwa
wafanye jambo fulani, liwe la heri au baya,...
‘Kama nia yao ingekuwa
nzuri, maana taasisi hizi za jamii zipo nyingi na zina malengo maalumu, ya
kusaidia jamii, na zinakubalika, lakini hawa jamaa walianzisha taasisi zao
ikiwa na malengo ya nje mazuri lakini ya ndani kuna mipango ya kuwanufaisha,
kwa migongo ya wengine...’akaendelea kutoa maelezo na wakili muendesha
mashitaka akamwambia.
‘Kuna silaha kubwa wanayoitumia
wao, nayo ni propaganda potofu, kila wakitaka kugundulikana wanageuza maneno,
wanageuza ajenda kinamna ambayo hali halisi inasahaulika, na ajenda zao
zinapenyenzwa kinamna....kuna miradi kama mahoteli ya kitalii, humo kuna mambo
yao, kuhakikisha jamii inazama kwenye anasa zaidi na kujisahau...
‘Watoto wetu wanajikuta
wakizama kwenye starehe zaidi, elimu inakuwa ni lugha tu, lakini elimu yenye
mlengo wa kisayansi, yenye kuelimisha kiuzalishaji zaidi wanakuwa nayo wao na
watoto wao...kwahiyo wao wanakuwa wamiliki, viongozi na wazalishaji, wengine ni
bendera fuata upepo...’alipofika hapo wakili muendesha mashitaka akasema;
‘Sasa hebu tuingie moja kwa
moja kwenye kesi yetu, tumeona kuwa kundi hili lilianzishwa kama makundi
mengine ya kijamii, likasajiliwa, na wanachama wake ni watu mashuhuri tu,
wanajitolea kusaidia jamii, je imekuwaje liwe na mafungamao mabaya, ya hata
kuua?’ akaulizwa na wakili
‘Nia ya kundi ni kuunda
kitu kama dola, lakini sio dola ya utawala, kuwa washike nchi hapana, wao
walilenga mbali zaidi, dola la kiuchumi... , ya kuwa hataka kama kutakuwepo
mtawala, basi awe anafuata amri zao, kwasababu kila sehemu wameshikilia wao..na
kama atatokea mtawala mtu wao basi itakuwa bora zaidi, lakini hawakutaka sana
kuonekana kwenye majukwaa...’akasema
‘Haya tuje kwenye kesi yetu
moja kwa moja, ni kwanini huyu mtoza ushuru aliuwawa...?’ akaulizwa
‘Kabla sijajibu swali lako,
kwanza ni vyema tukamtambua huyu marehemu, alikuwa nani hadi kifo chake, ...’akasema
na wakili mtetezi akaweka pingamizi kwa kusema hayo ni kumsema marehemu wakati
hayupo, hakimu akapinga hilo pingamizi akasema shahidi aendelee.
‘Marehemu ni vijana wa
mwanzo walioandaliwa na hilo kundi, na alipewa hiyo kazi mwanzoni kabisa, na
hadi anafariki, alikuwa ameshafikia kiwango cha u-mwenzetu,...mwenzetu ni kiwango cha juu katika kundi, wana vyeo
vyao wenyewe, na hadi anafariki, alikuwa katika maandalizi ya kupewa cheo
kikubwa...’akatulia
‘Kwasababu ya kugombea vyeo
kukatokea mgongani, wenyewe kwa wenyewe wakaanza kupigana vita, na marehemu akashutumiwa
kwa kujijali mwenyewe, na baadaye wakamshuku kuwa anasaliti kundi..na hi
ilitokea kipindi akiwa na mahusiano na mdada...’akasema.
‘Hebu sasa tuingia moja kwa
moja kwenye hoja ya mauaji, najua sasa kundi au chanzo cha kundi
kimeshajulikana, lakini nimeona kuwa wenzetu wana dukuduku, naona tuwape nafasi
wamuulize mtaalamu, mpelelezi wetu...’akasema wakili muendesha mashitaka.
Wakili mtetezi mmojawapo
akasimama na kumsogelea shahidi akitaka kuanza kuuliza maswali, yule wakili
akasita kidogo pale alipoona mtu akiingia mlangoni, na mara watu wakasikika
wakisemeshana na hata shingo zao kugeuka nyuma kuangalia ni nani aliyeingia...
NB: Haya mambo hayo....jana
hatukuweza kuwakilisha sehemu hii maana ni sehemu nyeti kidogo, ilibidi ipitiwe
kwa makini.
WAZO
LA LEO: Utajiri ni mnzuri, na kila mtu anatamani kuwa hivyo,
lakini utajiri huo usitokane na dhuluma, usitokane na jasho la wanyonge, ukafaidika
wewe , huku watu wanakufa njaa, watoto wao wanakosa elimu, mayatima, wajane
wanaongezeka kutokana na utajiri wako, huu ni unyama.
Na kwanini unafanya hivi,
kuwa wewe utaishi milele, kuwa wewe jamii na familia yako itaendelea kuneemeka,
tusijidanganye, dhuluma kamwe haidumu, na ikiendelea ujua amani haitakuwepo
kamwe..
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment