‘Mhasibu iliyotokea hapa ni kama vile unaangalia sinema
, ni tukio ambalo ninaweza kusema lilipangwa iwe hivyo na limekuwa hivyo,
nashindwa hata kuamini..’akasema mpelelezi akiwa kashika shavu, ilionekana
imemgusa sana, na hata pale alipo alionekana kutokulia kiakili, alikuwa
akimuangalia kila daitari aliyepita.
‘Hebu niambie imekuwaje, maana nimezuiwa kabisa kuingia
kuonana na mzee...?’ nikamuuliza
‘Huwezi kuingia kumuona tena kwa sasa, na nakushauri ni
bora kwa hivi sasa ukawa mbali na hiyo familia...’akasema mpelelezi
‘Kwanini wanifanyie hivyo?’ nikauliza nikiangalia kule
alipolazwa huyo mzee.
‘Kwa kauli ya shangazi wewe na mdada hamtakiwi kabisa
kufika maeneo ya hiyo familia, japokuwa mdada aliweza kuruhusiwa kuongea na
mzee, lakini aliongea naye kwa masharti na masaa maalumu, akisimamiwa na shangazi.
‘Hutaamini baada ya maongezi hayo mdada aliondoka, akisindikizwa
na maneno makali kutoka shangazi kuwa hataki amuone tena kwenye hio familia...
‘Lakini kwanini haya yote, mbona mimi simuelewi huyu mtu,
mimi au mdada kafanya kitu gani kibaya kwenye hiyo familia....?’ nikauliza
‘Mhasibu usilazimishe mambo, haya mambo yaache yatulie
na yataenda hivyo hivyo, na huenda huko baadaye mkaja kuelewana na hiyo familia
lakini kwa sasa nakushauri uwe mbali kabisa na hiyo familia...’akasema
‘Hebu nikuulize wewe umeweza kuongea na mzee, na hata
huyo shangazi kuna tatizo gani, sisi tunahusika na nini na hiyo familia, mimi
ni mkwe wao, kwanini waninyanyapae, au mzee kakuambia nini?’ nikamuuliza
‘Mimi sijui undani zaidi wa matatizo yako na hiyo
familia, nahisi inatokana na wewe kumtelekeza binti yao,..si ndio hivyo?’
akaniuliza mpelelezi.
‘Lakini mimi sijafanya hivyo,
sijamtelekeza...’nikajitetea
‘Mimi sijui, ...nina mambo makubwa zaidi ya hayo ya
kifamilia,...’akasema
‘Wewe na hiyo familia mpoje?’ niamuuliza
‘Mimi sina matatizo na hiyo familia, mzee na familia hiyo
tunaelewana, hata huyo shangazi mara nyingi nakutana naye tunataniana...unajua
yule mama anavyopenda kuongea utani mwingi, mipasho basi ndivyo alivyo na
nimemzoea hivyo hivyo....’akasema
‘Mimi sijawahi kuiona furaha ya huyu shangazi japokuwa
nasikia sifa zake kuwa ni mcheshi, na mtu wa watu...lakini mimi na yeye
hatuivani mara zote nilizokutana naye ni hasira, na kunikaripia tu....sijui
kama nitakuja kuelewana na huyo mama...na alishaniambia nihame huu mji maana
atakachonifanyia sitakisahau...’nikasema
‘Hayo yataisha tu, ukweli upo wazi kwa sasa, tusubiri
mahakama itakavyoamua, lakini ..’akatulia maana nilimuona docta akija kwa kasi,
akatupita, na alionekana kama ana anafuatilia au kuna jambo limetokea, nikamuangalia
mpelelezi, na mpelelezi akasimama na kuelekea kule alipoelekea docta.
Haikupita muda, docta na mpelelezi wakarudi wakiwa
katika mwendo kasi kidogo, na mpelelezi, akawa anaongea na simu;
‘Hakikisheni mnakagua kila chumba, ..ni nesi, alikuwa
kavaa kinesi ....huyo nesi ana umbile la nane, mweupe hivi, na alikuwa kavaa
raba nyeupe, ndio, ....’akasema
‘Kuna nini kwani...?’ nikawasogelea na kuwauliza
‘Invyoonekana mzee kanyweshwa sumu, na hivi sasa madocta
wanajaribu kuokoa maisha ya mzee, haijajulikana ni aina gani ya sumu...’akasema
mpelelezi
‘Kanyweshwa sumu..na nani?’ nikauliza kwa mshangao
‘Ilivyokuwa ni hivi, wakati nimeongea naye kwa muda
mfupi, akinisimulia mambo mengi ambayo mimi nilikuwa siyajui, ilifika muda
akawa na kiu, lakini kuna dawa alipewa aliambiwa asinywe maji kwanza asubiri
kidogo , na tulipoongea kwa muda, yule nesi aliyekuwepo hapo akamwambia asubiri
kama dakika tano hivi, ataweza kumpa maji,...basi tukawa tunaongea na kila mara
mzee alikuwa akiangalia saa yake, na kuniambia;
‘Nina kiu dakika tano hazijaisha tu....’ basi mimi
nikamuambia yule nesi aliyekuwepo hapo, kuwa mgonjwa anahitajia maji,....
‘Sawa ngoja nimchukulie gilasi...’akasema yule nesi, na
mimi nikaangalia pale kwenye meza kuna maji ya kunywa, nikataka kumpa mgonjwa, anywe
na vikombe vilivyokuwepo,lakini moyo wangu ukasita, na shangazi alikwenda
kusafisha vyombo.
Mzee akasema;
‘Hawa watu bwana, kila kitu mpaka wanipe wao, maji si
hayo hapo, wanataka kunipa maji gani...’akasema mzee, na mimi nikamwambia ni
vyema tukafuata maelekezo na masharti yao, wasije kusema kwanini tulifanya hivi
au vile
‘Basi yule nesi akarudi akiwa na gilasi mkononi,
nakumbuka kabisa alikuwa na gloves amevaa, tokea awali, akaichuua ile gilasi na
kumimina maji yale yale yaliyokuwepo pale mezani, akayainua juu, ..mimi pale
akili yangu ikawa inajiuliza mengi, sijui kwanini niliingiwa na shaka
‘Nipe maji bwana, mimi nina kiu, wewe unayafanya hayo
maji kama dawa...’akasema mgonjwa na muda huo shangazi naye alikuwa ameshafika
akiwa kebeba vile vyombo alivyokwenda kusafisha, na shangazi akachukua ile
chupa ya maji, na kuyamimina kwenye gilasi aliyokuwa kaishika yule nesi...yote
hayo nimeyaona kwa macho yangu
‘Basi yule nesi ndiye aliyempa mgonjwa maji, huku
wakitaniana na huyo nesi kuwa mzee akipona yeye anataka awe mke wake wa
pili,...na mzee akayanywa yale maji yote na kataka mengine, wakamuongezea, na
safari hii akawa anamnywesha shangazi...yule nesi akawa anaangalia na baadaye
huyu nesi akaondoka kwenda kwenye chumba chao, kipo karibu na akiwa pale kwenye
chumba chao unamuona.
‘Oh, sasa najisikia safi....sasa nataka kuongea na huyu
mpelelezi,...’mzee akamwambia shangazi na shangazi akasema;
‘Lakini mimi naona umeongea kwa muda mrefu, umeongea na
yule muhuni, kwa muda mrefu, kaondoka, na bado umeongea na huyu mpelelezi, kwa
hivi sasa ni bora upumzike...’akasema dada yake
‘Muda huo haupo, muda wa kupumzika utafika mtu
utapumzika moja kwa moja, lakini sio sasa,...wewe niachie nafasi hayo
ninayotaka kuongea naye ni muhimu na ni mambo nyeti, tupe nafasi kidogo...’akasema
na dada yake akaanza kuweka vitu vyae kwenye kiapu alichokuja nacho huku mzee
akinisimulia mambo:
‘Nimeshakusimuliza chanzo cha madudu yaliyopo kwenye
sehemu nyeti za nchi yetu, kuna watu wamejiona wao wamefika na hii nchi ni
yao...’akasema
‘Maisha yangu ya utendaji wa kazi nikiwa serikalini yalikuwa
ni ya kujituma, nikiishi kwa mshahara wangu tu, hebu fikiria mishahara yetu
ilivyo, lakini sikupenda kabisa kuwa mbadhirifu, na sikuwa na marupurupu mengi,
hata pale nilipokuwa bosi wa kitengo, sikupenda kupata zaidi wakti wengine
hawana kitu...’akasema na kipindi hicho shangazi alikuwa hajatoka, bado alikuwa
akikusanya vyombo, ili aondoke navyo.
‘Nikuambie ukweli, katika maisha haya yetu ya uhalisia,
watendaji kazi wazuri, wenye kujitolea ndio wanaishia katika umasikini baada ya
kustaafu kwao, na wale wanaofanya kazi kiujanja ujana ndio wanakuja kuwa na
maisha mazuri kutokana na ufisadi walioufanya wakiwa makazini, angalia kiukweli
jinisi ilivyo kwa watu unaowafahamu.
Watu wale waliojitolea, wakifikia uzeeni, wakati
mwingine wanakuja kujijutia, hasa wakiangalia yale waliyoyafanya kwa kujitolea
kwa hali na mali, ..na jinsi wanavyosahaulika,...ni lazima kama binadamu
utakuwa uanawaza sana.....na muda huo hawana la kufanya tena, ,matokea yake
wanakufa haraka kwa kihoro,...au wanapatwa na magonjwa ya kuwatesa hadi
wanakwenda kaburini...’akasema
‘Kwa mfano mimi mpaka nafikia kustaafu, nilikuwa sina
hata nyumba ya maana, maana ungelijenga na nini, kipindi hicho, watendaji
tulikuwa tukiangaliwa sana, na pia mshahara wangu ulikuwa wa kawaida tu, na mimi
sikuwa nafahamu kuiba,..wenzangu wakawa wajanja,kisiri wakawa wanafanya vitu
vyao wakajijenga mimi nawaona, na ndio unawaona wana makampuni, vitega uchumi,
na hayo hawakuyafanya kihali,lakini ungelisema nini.....’akatulia
‘Nilipofikia muda wangu wa kustaaafu nikaenda kuishi
kwenye kibanda changu kijijini, huko nilikuwa na shamba langu, maana kipindi
hicho mashamba yapo mengi tu, unapewa na wananchi bure, kwahiyo huko shambani
nilijenga kibanda changu, nikaweka mifugo, basi nilipostaafu nilirudi huko
kujitegemea,..
‘Kiukweli sikuwa na
ujanja, nisingeliweza maisha ya mjini japokuwa nilikuwa nimeshayazoea, na muda
huo nikawa nadanganywa na bima ya uzeeni kuwa itanisaidia, haiwezi , haikuweza,
kwani thamani ya pesa inapungua kila siku, ni pesa wanayotoa ni ndogo tu...maisha
yakaanza kuniendea vibaya, usiombe....’akasema
‘Maisha yalikuwa magumu, na nikawa nikifikiria
nilivyojitolea kwa hali na mali kuitumikia nchi yangu, na sasa ndio nimefikia
fainali, sina mbele wala nyuma, nikaanza kupatwa na maradhi ya ajabu...mawazo
ni kitu kibaya sana, nikatibiwa tibiwa wewe, sasa na miti shamba, hela ya
hospitali ninayo....
Sijui ni nani aliniona akaipeleka hiyo taarifa kwa
wakubwa, ikawagusa, ndio hivyo tena wavumai papa baharini lakini samaki wengine
wapo, na kila penye ubaya kuna na uziri wake, wakatokea watu wenye moyo wa
huruma, wakaenda kuongea na wakubwa, baadaye nikaitwa....’akasema
‘Nilishangaa siku hiyo aliponijia kijana na gari,
akanipa barua kuwa nahitajika wizarani, serikalini, nahitajika kwenda kutoa
ushauri na kusaidia kazi maalumu, katika vitengo nyeti vya serikali,
...sikuamini, nilishajua muda wangu wa kulipa fadhila za kujituma umefikia,
nisubiri kufa na thawabu zangu nitazikuta peponi,...
‘Basi nikafika kwa huyo mkurugenzi, nilimkuta ni kijana mdogo
tu,....tofauti na enzi zetu, nafasi kama hizo walikuwa wakishika watu wazima,
elimu sasa inalipa eeh, haya ndio enzi zake hizi....’akasema
‘Basi yule kijana akaniambia;
‘Mzee nimekuwa nikifuatilia utendaji wako katika makabrasha
yetu, nimevutiwa sana na wewe, na nimeomba kwa wakubwa zangu kuwa tunahitaji
wazee wa siku nyingi ili tupate uzoefu wao, maana kuna mambo ambayo mimi
nayaona sio sawa,...na tumetumia juhudi zetu za kisomi lakini imekuwa ni kazi kubwa sana , imekuwa
kama ile hadithi ya kumtuma mjumbe, na huyu mjumba akifika anapotea huko huko....’akaniambia
‘Unasema kuna mambo hayapo sawa ni mambo gani hayo?’
nikamuuliza
‘Kuna ubadhirifu wa hali ya juu unaoendelea kwenye
viteng vyetu nyeti hasa vile vinashughulika na masilahi, lakini unafanyika
kitaalamu sana, tumefanya uchunguzi lakini hatujaweza kubaini kiicho chake na
nani yupo nyuma ya hayo yote..’akaniambia
‘Mhh, lakini hiyo si kazi ya polisi, mimi nitawezeje
kusaidia, kwanza na huu uzee mimi nitafanya nini, na hata hivyo mimi mwenyewe sipendi
hayo mambo nimeshajichokea, nahitaji kujipumzisha nisubiri umauti wangu, sitaki
tena misuko suko....’nikamwambia
‘Mzee kuna kitu nimejifunza, ...na mimi kama mimi nataka
kulipa fadhila za watu kama nyie ambao mumelitumikia hili taifa kwa moyo mmoja,
na mumefikia hatua hiyo lakini hakuna anayewajali tena, wanachosubiri wakubwa zetu
ni nyie mfe, waje kuwazika kwa mbwembwe za kitaifa,....mimi hali hiyo siipendi,
kwanini wasiwajali muda huu mkiwa hai wakawasaidia....’akasema
‘Kwahiyo unataka mimi nifanya nini?’ nikamuuliza
‘Ni hivi mzee kazi ninayotaka wewe ufanye, ni nyeti
kidogo, mimi naiita ‘uma huku unapuliza..’
yaani wewe utaingia ndani ya jamii inayotenda yasiyofaa, utaishi nao,
...utafanya kila wanachofanya wao, maisha mazuri, starehe, utajikita pia kwenye
huo ubadhirifu, na hapo ina maana utapata kila kitu na utafanya kama wao, ili
tu uwajue ni nani na wanafanya nini, unauma huku unapuuliza, hadi tuone ni nani
yupo nyuma ya haya yote....’akasema
‘Ohi, kwanza nilikataa kabia, lakini baadaye nikafikiri
kwa makini, hivi mimi maisha mazuri nitayapata wapi, nimesoma hadi chuo kikuu,
nikawa bosi, lakini maisha yangu yalikuwa kama yakujitolea kwa jamii, sikuwahi
kuishi kistarehe, hata siku moja, sikuwa na muda wa starehe kwangu mimi kazi
ilikuwa mbele..., nilitaka kila jambo nilifanye mimi kuhakikisha
linafanikiwa,...usinione hivi, mimi nilikuwa nakuwa wa kwanza kuingia ofisini
na wa mwisho kutoka...’akasema
‘Ni nini nimekipata baada ya hayo yote, hakuna,umri wa
kustaafu ulipofika kila mmoja alishukuru niondoke, maana mimi nilikuwa mnoko,
naziba riziki za watu ... hata watani wangu wakawa wananitania, kuwa nilikuwa
najipendekeza sasa faninali uzeeni, wanasubiri kuja kula maharage..ni kweli
nimebakiza nini ...’akasema kwa uchungu.
‘Basi nilipofikiria sana, nikaona ni bora nikubali
kuifanya hiyo kazi, nikajipanga vyema, nikaja kujadiliana na yule mkurugenzi ,
nikapewa ofisi ya kinamna...sikutakiwa niwe na ofisi ya kutilia shaka , kwahiyo
ofisi zangu mara nyingi zilikuwa mahotelini..nikawa natoa ushauri kwa vijana,
jinsi gani ya kuingia huko kusipoingiwa....
‘Nikaanza maisha adimu, maisha ambayo sijawahi kuishi,starehe,
na kula nchi,...watu wengine wakaanza kunong’ona, mmh, mzee yule bhana, uzee
kaucha njia panda, alishindwa kutumia ujanani, kujirusha sasa ndio anakumbuka,,..ndio
ilibidi nifanye hivyo, ili niweze kufanikisha kazi yangu, na vijana wangu
walijua jinsi gani ya kuigiza, huwezi amini walifanya kazi niliyoibuni mimi...’akasema
‘Nikuambie ukweli pamoja na kuwa nilikuwa na usongo wa
kulipiza kuwa na mimi nipate nafasi ya kutumia, lakini moyoni mwangu nilikuwa
na hasira na hawa mafisadi, kwahiyo nikawa najitahidi niweze kujua siri zao kiundani
zaidi...’akasema
‘Nikajitahidi kujionyesha nilivyoweza hadi nikakubalika,
kuwa huyu sasa ni mwenzetu, ...’akatulia
‘Kuitwa mwenzetu sio
mchezo, ...kuna mambo kwenye hii sifa ya uwenzetu, ...na nilikuja kugundua
jambo kumbe haya maneno, hizi sifa usione inatamkwa ukafikiria ni maneno tu,
mara waheshimiwa, mara wenzetu , mara .....yote haya yana maana fulani kwa
wahusika, kwa wengine ni majina tu...’akatulia
‘Ili nifanikiwe hilo nilihitajika kuwa na watu wangu
ninaowaamini, sikuwa na shaka na hilo, kwani katika utendaji wangu wa kazi huko
nyuma kuna watu niliwaona wanafaa sana kulitumikia hili taifa, vijana niliowahi
kuwafundisha mwenyewe, basi nikawapata hao, nikawapika ipasavyo, nikawaonyesha
njia...na kweli walifuata ninavyotaka...’akasema
Na wao wakawatafuta watendaji wao...unaona hapo, ni aina
fulani ya mnyorororo wenye ndoana mwishoni, lakini nia na lengo ni kumnasa
samaki kubwa lao.....
‘Kuna siku moja nilikuambia kuwa kuna kundi lilitokea
kipindi cha nyuma, lenye mlengo mbaya wa taifa, hilo kundi lilianzishwa na
jamaa mmoja aliyetaka kuunda dunia yake, akasema anataka kuwa na ‘dunia yake..’ kama ni mfuatiliaji mnzuri
wa mambo haya yetu utakumbuka kitu kama hicho...’akasema
‘Sasa yaliyotokea, na yataendelea kutokea ni matawi ya
hiyo dunia aliyoianzisha na huyo jamaa, huyo jamaa hayupo hapa nchini kabisa, ila
ni tajiri wa hali ya juu huko nje anapoishi baada ya kufanikiwa kuiba na
kuwekeza...sasa hivi yeye ni mfadhili wa watu wa kundi lake...lakini sio rahisi
kuligundua hilo...ilibidi nipenye kwenye vizingiti vikali sana, mpaka nikafikia
cheo cha uwenzetu..’akasema
‘Mimi niliweza kuifikia hiyo ngazi kwa muda niliopewa
hiyo kazi, na nilifanikiwa baada ya kuniona nimerudi kuhangaika, nikiwa
nimechoka, sina mbele wala nyuma, wakajua huyu hana la kufanya, dawa ni
kumrubuni tu, na kwa vile anajua mengi kwenye system, basi ataufaa, kwahiyo kidogo kidogo wakawa wananiingiza
kwenye anga zao...
‘Mzee sasa naona umekomaa, japokuwa umekwisha, sisi
tunataka na wewe ule hii nchi...’siku moja akaniambia jamaa ambaye huwezi
amini, ni mtu mwenye wadhifa na heshima zake, kumbe ni mmoja wa kinara ya hilo
kundi..
‘Sasa tunataka uwe nasi,..utusaidie mambo fulani, na
sisi tutahakikisha wewe na familia yako mafi njaa....’akasniambia na mimi
sikujivunga, nikakubaliana na yeye, nikawa nauma na kupulizia...
‘Kwanza walianza kunijenga kiimani zao, maana na wao
wana imani zao,...wakanipika kivyao, hadi wakaona nimeiva...hawakujua nina nini
kichwani mwangu, huwezi amini, watu waliopo humo ni watu wa kawaida, tupo nao ,
ni watendaji wa kazi wazuri tu, wengine ni viongozi wa dini, yaani kila idara
wapo...’akasema
‘Hiyo ndio mikakati aliyoifanya yule jamaa aliyeanzisha
dunia yake...kuna makabrasha nimeyaandika kwa kirefu, nilitaka kutoa kitabu,
lakini nilichelea ....na wakati nimefikia hatu ya mwisho, makabrasha yangu
yakaibiwa,...ndio hayo unayosikia wakisema nyaraka
nyeti, ...wajanja wakachukua kazi yangu .....na nilikuja kumgundua
aliyefanya hivyo ni nani..huyo jamaa akaanza kunichongea kwenye kundi kuwa mimi
ni msaliti...’akatulia
‘Sasa kazi ikaanzia hapo...nikawa nawindwa, ili
upatikane ushahidi, ni ukipatikana mimi napotezwa...’akasema
‘Ohh, lakini mimi sikujali, nilijitahidi kujionyesha
kuwa mimi bado ni mwenzao, na wahusika, hawakunitilia shaka moja kwa moja,
wakawa wananiwinda usiku na mchana, lakini mimi nilishajiandaa,...sasa nafikia
sehemu nyeti...’akasema na kumuangalia shangazi aliyekuwa sasa akisikiliza kwa
hamu, mzee akamwambia shangazi
‘Nimekuambia utoke ndugu yangu, haya
hayakuhusu....’akasema mzee
‘Kwani hayo ni siri, kaka naye bwana, mimi nayafahamu
hayo yote, ...’akasema shangazi
‘Wewe si kila kitu unakijua, tatizo lako hujui hatari ya
haya mambo, usipende kujiingiza kwenye maswala kama haya, watakupoteza hao
watu, hao watu hawajali kumpoteza mtu....’akasema.
‘Mimi hawaniwezi...’akasema na kuanza kuondoka, na mzee
akasema;
‘Mimi nataka kukusimulia yote, ambayo nayafahamu mimi,
na hasa kuhusu yaliyotokea siku ile kwa mdada,..lakini muhimu jitahidi sana
upate hizo nyaraka nyeti, kuna membo mengi nimeyafichua hapo...
‘Sasa kuhusu yaliyotokea kwa mdada, ni mlolongo mrefu,
na imechukuliwa juu kwa juu tu,na kwa vile hilo kundi halijulikani, na mambo
yao ndivyo yalivyo, kutokea kitu kiwe na utata fulani, na wao kwa vile wapo
kila mahali, wanalivuruga lile jambo,...’akasema
‘Sasa yaliyotokea pale, yameshaharibiwa kabisa, na watu
wengi hawafahamu hilo, ila yaliyotokea pale ni katika harakati za wenzetu
kuhakikisha wanaondoa wasaliti kwenye kundi lao...japokuwa kifo cha yule jamaa
ni bahati mbaya tu, hata hivyo ilibidi ifanyike vile, kuokoa watu wasio na
hatia.....’akasema
‘Mhh, mbona...’akasema akikohoa, na kukunja uso...
‘Vipi mzee...’nikasema na nilimuona akijitahidi kutafuta
hewa ya kuvuta, na mara nikamuona mzee macho yanamlegea mimi nikajua kachoka kwasababu
aliongea na mimi kwa muda mrefu na kabla ya hapo alitangulia kuongea na
mdada...’akasema mpelelezi
‘Kwani mdada yupo wapi?’ nikamuuliza
‘Mdada alifika mapema, na alipomaliza kuongea na mzee,
alitoka,na kunikuta nipo nje , nikisubiria zamu yangu, alipotoka aliniona akanipungia mkono...alionekana kuwa na haraa
kidogo, na mimi nikaona nimuwahi, ili
nimkumbushe, kuwa nahitajia kuongea naye baadaye...kwahiyo nikamkimbilia kabla
hajaingia kwenye gari lake;
‘Mdada nakukumbusha tukutane ,...na nitakuambia
wapi...’nikamwambia na yeye akatabsamu na kusema;
‘Haina haja ya mimi na wewe kukutana na sioni kama kuna
umuhimu wa mimi kuongea na wewe, natumai ukimalizana na mzee, utanielewa nina
maana gani, ila cha msingi ninachotaka kukuambia ni kuwa uwe makini, ...hali ya
hewa imechafuka,....wenyewe wameshagundua kuwa kuna watu wameingia kwenye anga
zao...’akaniambia hivyo
‘Lakini mdada ni muhimu sana mimi na wewe tuongee...’nikamsisitiza
na yeye akasema;
‘Haina haja, ...ila mimi nakutakia ushahidi mwema,
mahakamani, nasikia wewe utaenda kufunga kazi,...mimi sizani kama nitakuwepo,
na tukujaliwa huenda tunaweza kukutana kwenye anga hizi hizi, ....’akasema na
kuingia kwenye gari lake na kuondoka
‘Ina maana gani kusema hivyo, na anakuaga anakwenda
wapi?’ nikamuuliza
‘Sijui....mdada haeleweki, lakini nilikuja kuyagundua
hayo nilipoongea na mzee, ...’akasema
‘Mzee alisema nini kuhusu yeye?’ nikamuuliza
‘Kuna mengi niliongea naye kabla, ila sehemu muhimu
niliyoitaka kuijua, haikuweza kuongelewa, ...’akasema
‘Kwani ilikuwaje...?’ nikauliza
‘Wakati mzee anasubiri shangazi aondoke, ili anihadithie
hiyo sehemu nyeti kama alivyoiita yeye, mara nikaona mabadiliko kwenye uso
wake, alianza kuhema kusivyo kawaida, nikahisi kuna jambo, nikamuuliza
‘Mzee vipi, au unahitaji kupumzika kidogo, nakuona
unahekam isivyo awaida, ...’nikasema na shangazi aliyekuwa anaondoka, akageuka
kumuangalia kaka yake naye akaiona ile hali, na mzee akasema
‘Mhh, najiona kama nahama duniani,...mmh, naona sasa muda
umefika, ...na mara akatulia kimiya...mimi nikaingiwa na mashaka, nikageuka
kumuangalia yule nesi, aliyekuwa pale sehemu wanayokaa, lakini sikumuona tena,
nikagonga kengele ya kuomba msaada, ...akaja docta, na alipofika akatufukuza
tutoke....
NB: Je ni nini kilitokea
WAZO LA LEO: Siku hizi walio nacho wanataka kupata
zaidi, hata ikibidi kuwanyang’anya wale waliokuwa nacho kidogo, huwezi kusikia
hata siku moja tajiri akisema mimi sasa ni tajiri sitaki zaidi, utamsikia
akisema maisha magumu,hali ngumu,...yeye kipato alicho nacho hakimtoshi,japo
kuwa anacho, je yule ambaye hana kabisa ...ndio maana wanasema ukisema hakitoshi ujue unacho, hebu jiulize
yule ambaye hana kabisa atasemaje...hilo katika dunia hii halipo tena.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Hi! I just want to offer you a big thumbs up for the
great info you've got here on this post. I am returning to your blog
for more soon.
Here is my website: Homepage besuchen ()
Post a Comment