Baadaye ilibidi niondoke pale hospitalini na kumuacha
mpelelezi akiendelea na uchunguzi wake,wakishirikiana na polisi, na msako wao
ukamlenga kumtafuta yule nesi aliyekuwa akimuhudumia mzee, ambaye kwa muda huo
hakuonekana tena maeneo ya hapo hospitalini, na hiyo ikazidi kutia shaka kuwa
huenda anahusika na na hujuma hiyo.
‘Kinachonipa mashaka ni huku kutoweka kwake ghafla,
japokuwa hatuna uhakika wa moja kwa moja kuwa sumu hiyo kaiweka yeye, au ndiye
aliyempa mzee hiyo sumu, lakini yeye ndiye aliyempa maji mzee, na inavyoonekana
sumu hiyo kainywa mzee kupitia kwenye maji,...na mtu ambaye alipewa kazi ya
kuhakikisha usalama wa kitu anachokula mzee, ilikuwa mikononi mwa huyo nesi.
‘Hata hivyo ile gilasi alikunywia maji mzee haikuonekana....’akasema
‘Docta anasema sumu , japokuwa wamewahi kumpa mzee dawa
ya kuituliza hiyo sumu, lakini ni vyema upasuaji wa haraka ukafanyika kwani
sumu hiyo hula mwili taratibu, ...’akasema
‘Baada ya mabadiliko ya hali ya mzee na kufikishwa
kwenye vipimo, na kugundulikana hilo tatizo, watu wa usalama walimtafuta huyo
nesi lakini hakupatikana,...alishaondoka
hata kabla ya muda wake wa kazi....unaona hapo...’akasema
‘Kwani huyo nesi ni wa siku nyingi hapa hospitalini?’
niauliza
‘Kwa maelezo yao, huyo nesi sio wa siku nyingi hapa
hospitalini, yeye alifika hapo akitokea hospitali ya jirani akija kutoa msaada,
na alikuwa na vyeti na barua rasmi za kumhamishia hapa kwa muda, kwa vile barua
hizo ni halali, hakuna aliyekuwa na shaka naye na kwa vile kweli hospitali hiyo
ilikuwa na uhaba wa wafanyakazi, ilimpokea
nesi huyo kwa mikono miwili.
‘Inaonekana ni jambo lililopangwa kwa umakini wa hali ya
juu, na ni kama vile walijua mzee huyo atazidiwa na kuletwa hapo, ni jambo la
aina yake kutabiri kuwa mtu ataumwa na hospitali yake ya matibabu ni hapo,na
kama walivyokuwa wamejipanga huyo nesi akapangiwa kuwa mmoja wa watu waliokuwa
wakimsaidia dakitari na moja ya kazi yake ni kuhakikisha usalama wa vyakula na
vinywaji anavyotumia mzee, kwani watu walishashuku uwa hayo yanaweza kutokea.
Watu wa usalama walikwenda hadi huko alipotokea huyu
nesi, na wengine wakaenda nyumbani kwake, kote hakuonekana, na walipojaribu kuchunguza
habari zake huko alipokuwa kifanyia awali,ikibainika kuwa na hapo alihamishiwa
kutoka hospitalini nyingine za mikoani,…na hauko alipotokea walikubali kuwa ni
mmoja wa wafanyakazi wao aliyekuwa akitokea chuo cha wauguzi, na alikuwa
mtendaji mzuri wa kazi,na akapata uhamisho
‘Ni nani alimpa huo uhamisho?’ akauliza
‘Ni mkurugenzi anayehusika na kazi ya uahamisho, na
uhamisho huo hakufanyika kwake peke yake, ililkuwa ni kampeni rasimi ya
kuwatawanya wafanyakazi kwenye hospitali mbali mbali ili kuweka uwiano ulio
sawa, kwani baadhi ya hospitalini zilikuwa na mapungufu ya wafanyakazi ,
‘Mimi namshuku huyo mkurugenzi pia, kuwa anaweza
kuhusika...’nikasema
‘Mkurugenzi ana ushahidi wa kuweza kumlinda hata kama
unamshuku,...hili ni kundi lililojipanga vyema na kila mahali kuna watu wao,
...anaweza akahusika au kundi hilo lilitumia mwanya huo kupandikiza watu wao...’akasema
‘Kwahiyo sasa?’ nikauliza
‘Uchunguzi bado unafanyika na hiyo kazi ni ya polisi,
...mimi nitaingiza mguu wangu kwa mambo yangu, lakini sitalifuatilia sana hilo
tukio, ..’akasema mpelelezi
‘Huoni kuwa tukio hili linaweza kukupeleka ahdi kwa hao
watu?’ nikamuuliza
‘Hiyo sio muhimu sana kwa sasa, kiujumla watu hao wapo
wengi, na mimi nilitaka nichimbe kundi hilo hadi mzizi mkuu, wapi tatizo hili
lilianzia, na japokuwa mzee kanipa ushahidi mkubwa wa wapi kundi hili lilianzia,
lakini mimi mwenyewe nilishajua mengi kabla, na kuwagundua baaadhi ya wahusika
wakuu, iliyokuwa imebakia ni ushahidi wa kuwafikisha hao watu kwenye sheria...’akasema
‘Mzee yeye alikupa ushahidi wa maneno, je kuna ushahidi
wowote unaoweza kuufikisha mahakamani ukasaidia kisheria...?’ nikauliza
‘Kwanza kuna kitu muhimu sana natakiwa nikipate, na
hicho mzee alisisiiza sana kuwa nikipate kwani kina kila kitu, i...’akasema
‘Kitu gani hicho?’ nikauliza
‘Hizo nyaraka nyeti, zipo kumbukumbu na ushahidi mbali
mbali ...’akasema
‘Sasa unazo wewe?’ nikamuuliza
‘Sijazipata zote, nilzopata ni kumbukumbu tu za kikasi,
bado kuna nyaraka nyeti ambazo ndizo mzee alizifanyia kazi, na kuweka kila kitu
wazi,....’akasema
‘Sasa utazipatia wapi hizo nyaraka nyeti...?’ nikauliza
‘Kwa mdada, nina uhakika nyaraka hizo anazo mdada....’akasema
*****
Nilipomaliza kuongea na mpelelezi, akili yangu haikuwa
na utulivu niliona ni bora nikaonane na mdada mwenyewe, na sehemu ya kumpata
kwa muda huo ilikuwa ni nyumbani kwake, sikupoteza muda nikaelekea nyumbani kwa
mdada, nikiwa na uhakika nitaonana naye huko maana nilipopiga simu yake haikuwa
hewani.
Nilipofika eneo la nyumba anapoishi mdada, nikakutana na
mlinzi, alikuwa akisoma gazeti na aliponiona akaliweka chini na kuja pale
getini, na aliponiona ni mimi akasema
‘Oh, bosi wangu, karibu sana....pole na majanga, maana
nilisikia walikushikilai tena, kumbe wamekuachia...’akasema na mimi sikutaka
kuongea naye sana nikamwambia;
‘Nataka kuonana na mdada...’nikasema
‘Mhh, huyo mtu kaondoka mapema kabisa alifika na hakukaa
sana, akatoka akiwa na mizigo kuonyesha kuwa anasafiri, na sizani kama ni
safari ya hapa karibuni...’akasema
‘Kwanini unasema hivyo?’ nikamuuliza
‘Kwasababu aliondoka na vitu vingi, ni kama vile mtu
anahama, na haikuchukua muda akaja mpangaji mwingine kwenye hii nyumba...’akasema
‘Ina maana hii nyuma sio mali ya mdada?’ nikauliza
‘Nijuavyo mimi ni nyumba ya familia yao...na aliyeingia
kwasasa ni mmoja wa ndugu zake...mrembo kama yeye, kwahiyo usijali, unakata mti
na kupanda mwingine, kazi kwako...’akasema huku akitabasamu, na mimi nikasema;
‘Oh, naweza kumuona huyo ndugu yake, huenda akanisaidia
kujua wapi alipo mdada..’nikasema na huyo mlinzi akasema;
‘Wewe tena, ..usijali ngoja nikakuunganishie, najua
ukifanikiwa hutanisahau....’akasema na kuelekea kwenye hiyo nyumba, baadaye
akarudi.
Aliporudi aliniambia huyo mdada ananisubiria kwani na
yeye alikuwa anataka kutoka kwenye shughuli zake, na mimi nikaingia ndani,
nilikuwa nimeliacha gari langu sehemu niliyozoea kuliacha, kwahiyo niliingia
hapo bila gari.
Niliingia ndani nakukutana na huyo binti, ni kweli ni
ndugu yake hata ukiangalia sura yake wanafanana sana na kama alivyodai mlinzi
kweli dada huyo alikuwa mrembo kama mdada mwenyewe, tukasalimiana na
nikajitambulisha na yeye akasema aliwahi
kusikia mdada akinitaja mara kwa mara
‘Akinataja kwa mema au mbaya?’ nikamuuliza na yule binti
akatabasamu , tabasamu lile lile la mdada linalonipoteza akili yangu aasema
akionyesha aibu;
‘Mhh, kwa mema,...alisema wewe ndiye mtarajiwa wake...’akasema
na safari hii akawa kaangalia chini
‘Ndio maana nataka kuongea naye , naweza kumpata wapi,
maana simu zake zote hazipatikani...?’ nikamuuliza na huyo mdada akasema;
‘Mhh,sijui kwakweli, kwani alivyoondoka, kasema anakwenda
kikazi, na huko anapokwenda hatarajii kurudi hivi karibuni, na hakutaka kutaja
ni wapi, ....tumeshamzoea, akipata kazi zake huwa ndio hivyo, anaaga kuwa
anaondoka na hasemi anakwenda wapi...’akasema
‘Kwani mdada ana kazi gani nyingine hasa?’ nikamuuliza na
yeye atakaniangalia kwa haraka akionyesha kushangaa akasema;
‘Ina maana wewe hujui,...nilijua labda wewe unaweza
kujua zaidi, maana Mdada mwenyewe hasemi ana kazi gani, na hakai sehemu moja,
mara leo ana kazi hii , kesho anakuwa na kazi nyingine, ukimuuliza mara nyingi
anasema yeye kasomea uwakala, mtu kati, kama una biashara , au kama una kazi
yoyote ya kufuatilia, unampa yeye anajua jinsi gani ya kuonana na wahusika,
hadi kazi yako inakamilika...ndivyo tunavyojua sisi, na ndivyo alivyotuambia ,
....’akasema
‘Oh, kwahiyo nitampataje?’ nikauliza
‘Kwakweli hapo siwezi kukusaidia maana anapotuaga,
hasemi anakwenda wapi, sana sana atakuambia anakwenda kikazi, wapi hakuambii, na
mawasiliano yake yanasitishwa hadi hapo atakapokupigia yeye mwenyewe,..siwezi kabisa kujua wapi pa
kumpata, sisi mwanzoni tulikuwa tukiumiza kichwa sana kumfuatilia, lakini
baadaye tukamzoea, ndivyo maisha yake yalivyo, na hakuna anayeweza
kumuingilia...’akasema
‘Oh,na hii nyumba ni mali ya nani?’ nikamuuliza
‘Hii ni nyumba ya familia, na nilitakiwa mimi nije
kuishi hapa mapema tu, lakini nilikuwa bado nasoma, na nilipomaliza shule,
ikapangwa kuwa mimi nije kuanzia maisha yangu hapa na mdada ataenda kuishi
kwenye nyumba zake...’akasema
‘Na nyumba zake zipo maeneo gani na wapi, maana huenda naweza
kumpata huko..’nikamuuliza na yeye bila hiana akanipa ramani ya wapi nyumba
zake zilipo, na kusema;
‘Sizani kama unaweza kumpata huko , nyumba zote
zimepangishwa...’akasema lakini mimi nikaona nikajaribu tu
‘Sawa hamna shida, nitazidi kuja kuonana na wewe kama
nikikwama, huenda akakupigia simu...’nikasema na yeye akasema;
‘Hamna shida, unakaribishwa wakati wowote...’akasema na
mimi nikaondoka hapo
Nilikwenda hadi huko kwenye nyumba zake, lakini zote
nilikuta zina wapangaji kama
alivyoniambia mdogo wake mdada, na wapangaji hao hawakujua wapi alipo mdada,
walisema wao ikifikia muda wa malipo, wanawasaliana na mdada, na mara nyingi
yeye ndiye anapiga simu na kuwaelekeza wapi pa kuzililipa hizo pesa, na hawana
tabia ya kunana naye mara kwa mara...
Nilirudi hotelini kwangu nikiwa sijui la kufanya, nikampigia
simu mpelelezi kumuelezea hayo yam dada na mpelelezi akasema, hata yeye hawezi
kujua wapi alipo mdada, na mawasiliano yake yote hayafanyi kazi, na kwa vile hana umhimu sana kwake,
hajajiangaisha kumtafuta.
‘Simu zake zote hazipo hewani....’akamalizia kusema
mpelelezi
‘Sasa nitampataje?’ nikauliza
‘Kwakweli mimi hapo sijui, na siwezi kuhangaika naye kwa
sasa, najiandaa kutoa ushahidi wangu kesho ambao utahitimisha hili tatizo...’akasema
‘Kwani umeshazipata zile nyaraka nyeti?’ nikamuulza
‘Sijazipata, kama nilivyokuambia mdada ndiye inawezekana
anazo,..lakini ndio haonekani, lakini hazitanifanya nishindwe kutoa maelezo
yangu, ambayo yatathibitisha mambo mengi tu, na mlinzi atakuwa shahidi yangu
mkuu, na kama atakubali kushirikiana nami, nitaweza kujua mengi ambayo yataweza
kumaliza hoja muhimu ya kifo cha mtoza ushuru....’akasema
‘Na inavyoonekana mlinzi anaweza kukutwa na hatia ya
kuua vinginevyo amtaje aliyemtuma, kwani inavyoonekana yeye alitumwa, na
muhusika hajaweza kutambuliakana, je huyo aliyemtuma ni nani....?’ nikamuuliza
‘Mpaka nione naye, kabla sijaweza kulijibu hilo swali
lako, sasa hivi naelekea huko kuonana
naye, sijafika bado ,nikiongea naye naweza kujibu hilo swali, na pia nitakuwa
na uhakika wa mambo fulani fulani,..tatizo kubwa ni kuwa wakili wake hataki
kumpa nafasi hiyo, lakini mwenyewe mlinzi kanipigia simu kuwa niende tuonane
naye kwa haraka, bila ya wakili wake
kufahamu, alisema ana jambo muhimu sana la kuniambia;....’akasema na
niliposikia hivyo nikavutika kujua kinachoendelea, nikasema;
‘Naweza kuja kuungana na wewe..’nikasema
‘Kwanini bwana, usijiingize kwenye haya
matatizo...lakini kama upo tayari unaweza kuja, utanikuta nje ya gereza alipo
huyo mlinzi, ila hutakuwepo wakati naongea naye, nikimaliza kuongea naye,
utaweza kumsalimia, na nitakuambia kila kitu atakachoniambia...’akasema
‘Sawa nakuja mkuu...’nikasema nikiwa na shauku, hata
kama sitakuwepo wakati wanaongea, lakini nitaweza kupata maelezo ya awali
kutoka kwa mpelelezi akimaliza kuongea naye.
Niliondoka na gari hadi kwenye gereza hilo, na
nilipofika nilimkuta mpelelezi akisubiri, na tulisalimiana kidogo, baadaye
akaja mkuu wa gereza hilo, akasema;
‘Mpelelezi hebu tuongee kidogo,......’akasema na
wakasogea pembeni na wakawa wanaongea kwa sauti ya chini, niliweza kusikia
wanachokiongea kwa shida,
‘Kuna tatizo limetokea....’akasema huyo mkuu wa gereza
‘Tatizo gani...?’ akauliza mpelelezi
‘Mlinzi kakutwa kwenye chumba chake akiwa haijiwezi, na
akakimbizwa hospitalini, lakini hakufika hospitalini, akafia njia, na docta
alipomchunguza alisema huyo mlinzi kafa kwa sumu, alikuwa kanywa sumu....’akasema
‘Haiwezekani.....’akasema mpelelezi kwa hasira
‘Ndio hivyo mpelelezi, nimezipata hizi taarifa kwa
machungu makubwa sana, na upelelezi wa haraka unafanyika, na inavyoonekana ni
kama aliamua kujiua mwenyewe...’akasema
‘Sizani kama alifanya hivyo, hilo la kujiua halipo,
atakuwa kauwawa...’akasema mpelelezi
‘Tutaliona hilo baada ya uchunguzi,....’akasema huyo
mkuu, na mpelelezi akauliza
‘Na huyo wakili wake yupo wapi? Akauliza mpelelezi
‘Alikuwepo hapa, hajaondoka, nimetoka kuongea naye muda
mfupi uliopita, yeye alifika mapema tu alipopewa hizo taarifa, alifika kujua
ilivyotokea, na kama wakili wake,amesisitiza upelelezi wa hali ya juu ufanyike,
....’akasema mkuu huyo.
‘Nataka kuonana na huyo wakili ni muhimu sana nikutane naye aniambie ukweli,
haiwezekani hili litokee, na kwanini mara nyingi alikuwa akinizuia nisiongee na
huyo mtu, huyo wakili, yupo wapi, ana jambo analifahamu...?’ akauliza mpelelezi kwa sauti ya hasira.
‘Nipo hapa mkuu...’sauti nzito ikatoka nyuma yetu,
NB: Haya mzee, kapewa sumu, yupo chumba cha upasuaji,
mlinzi mtuhumiwa mkuu keshamalizwa, ni nini kitatokea.
WAZO
LA LEO: Ubinafsi ni hulka ya kibinadamu, kila mmoja anapenda
apate yeye, na ikiwezekana apate yeye zaidi ya wengine. Upendo wa kweli , imani ya
kweli ya kiroho, inatokana na jinsi gani mtu atakavyoweze kuishinda hiyo hali ya ubinafsi, ikakufanya ukapambana na tabia hiyo ya ubinasfi.
Ili ujione umeshinda, ni pale utapokeweza kumjali mwenzake kuliko wewe,...awe tayari
kukosa kwa ajili ya mwenzake, uwe tayari kuona mwenzako anapata kabla yako...na
ukifikia kwenye hilo daraja basi wewe ni muumini wa kweli, wewe una upendo wa kweli,
wewe ni mcha mungu wa kweli.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment