‘Kuna tatizo limetokea....’
‘Tatizo gani...?’
‘Mlinzi kakutwa kwenye chumba chake akiwa hajiwezi, na
akakimbizwa hospitalini, lakini hakufika hospitalini, akafia njiani, na docta
alipomchunguza alisema huyo mlinzi kafa kwa sumu, alikuwa kanywa
sumu....’
‘Na huyo wakili wake yupo wapi?
‘Alikuwepo hapa, hajaondoka, nimetoka kuongea naye muda
mfupi uliopita,
‘Nataka kuonana na huyo wakili ni muhimu sana.....
‘Nipo hapa mkuu...’
Tuendelee na kisa chetu
*************
Mpelelezi alimgeukia yule wakili, na mimi kwa taratibu
nikageuka kuwaangalia, kuona ni nini
kitatokea na katika hisia zangu nikajua sasa ni ugomvi, mafahali wawili
wamekutana, na ukiangalia maumbo yao yanafanana, wote wamejazia kifua...niliona
pingu ikiwa mfukoni mwa mpelelezi, niliona ajabu ya yeye kutembea na kitu kama
hicho.
Mpelelezi ni mwepesi kweli, alivyogeuka utajua huyo mtu
ni wa mazoezi, na mwenzake alikuwa keshajiandaa, akawa kasimama kimtego, tayari kwa lolote, na wakati huo
mkuu wa lile gereza alikuwa naye keshajiandaa kuamulia, kwani nilimuona
akiwaangalai kwa tahadhari
Mimi nikawa nasubiria, nikipiga chabo la kujiiba, moyoni
nikisema cha kwanza atakachofanya mpelelezi ni kutupa ngumi, na itatua kwenye
shavu la huyo wakili, na wakili ataenda chini, akisimama , atakuwa na hasira
nay eye atamrukia ile ya dume la ngombe lililokasirika, na hapo mpelelezi kwa
vile ni mwepesi atampisha, na wakili ataenda moja kwa moja kugonga ukuta,....nashukuru mdada hayupo na kilini mwangu nikawa namuona akiangalia tukio hili huku akitabasamu
Akili bwana, ilikuwa ikiwazia kitu ambacho
hakijatendekea, na huenda kisitendeke, pale nilimuona mpelelezi akimsogelea
wakili kwa tambo, na alipomkaribia huyo wakili alisimama, na wakawa wanaangalia
usoni kwa muda hivi, halafu mpelelezi
akasema;
‘Nataka uniambie ukweli wote,...najua unafahamu
mengi, sizani kama hujui
kilichosababisha kifo cha huyo mlinzi, sizani kama hujui ni jambo gani huyo
mlinzi alitaka kuniambia na mkaamua kumuwahi kabla hajakutana na mimi, sasa ili
kupoteza muda nataka uniambie yote, sasa hivi….’akasema mpelelezi
‘Mlinzi alitaka kukuambia jambo mbona mimi sifahamu
hilo?’ akauliza yule wakili akionyesha uso wa kushangaa. Na mara simu ya
mpelelezi iliita, mpelelezi akaichukua na kuangalia mpigaji, akasema
‘Samahani kidogo, usiondoke, nataka kuongea na
wewe.....’akasema na kuanza kusikiliza ile simu, alisikiliza kwa makini kwa
muda mrefu, hadi yule wakili akawa anaangalia saa yake, na karibu kutaka
kuondoka, ndipo mpelelezi akakata simu na kuanza kuongea na huyo wakili
‘Haya tuongee, nataka uniambie ukweli....’akasema
‘Ukweli upi, kama ni kuhusu kifo cha mteja wangu mimi
sijui zaidi, ndio nafuatilia kujua ukweli, ....’akasema
‘Sio kweli, ...haya niambie ulipofika uliongea na mkuu
wa kituoa hiki, na uligundua nini au utakwenda kuwaambia nini wanafamilia wa
huyu marehemu?’akauliza
‘Kama alivyoniambia mkuu, kuwa marehemu kafa kwa sumu,
na inaonekana amejiua, na uchunguzi bado unaendelea,...hakuna zaidi...’akasema
‘Wewe unafahamu kuwa mteja wako alitaka kuongea na mimi
hii leo?’ akaulizwa
‘Ndio nakusikia wewe, ukisema hivyo...’akasema kwa kauli
ya kutokujiamini
‘Ndio maana siamini hiyo kauli ya kuwa aliamua kujiua,…ni
nyie mliamua kumuua kabla hajaniambia hicho alichotaka kuniambia, na mkafanya
hivyo ili ionekana kajiua, yule sio mtu wa kujiua, namfahamu sana…’akasema
mpelelezi
‘Mimi sijui ...nimepata taarifa hizo ndio nikaja hapa,
na hata mimi siamini hilo la yeye kujiua, lakini ni mpaka uchunguzi ufanyike,
ndio tutagundua ukweli, hata hivyo mimi ninakushangaa kwa wewe kunihusisha mimi
na hayo, mimi ningeliwezaje kumuua mteja wangu, ambaye ni tajiri wangu ,
nafanya kazi kwake ili baadaye nipate pesa, halafu nimuue, hebu tumia akili
yako vyema, halikuingii akilini….’akasema huyo wakili kwa kujiamini.
‘Unaweza kufanya hivyo, kama umepata fedha zaidi, na
ndivyo nyie watu mlivyo, lakini
nikuambie ukweli, fedha kama hizo hazina faida, utatumia zitaisha, lakini
dhambi ya hicho kifo haitaisha abadani, damu yake itakuandama hadi unaingia
kaburini, na ukifika kwa mungu utachomwa moto….’akasema mpelelezi
‘Kwanza naomba tuelewane, chunga sana kauli yako, hizo
shutuma mimi sizikubali, na kwa kauli yako hiyo ninaweza kukuchukulia hatua za
kisheria, wewe ni mtaalamu na unafahamu hayo, huwezi kumshuku mtu tu
....’akasema
‘Fanya utakalo, nenda kachukue hizo hatua, tutakutana
mahakamani na utaona jinsi gani nitakavyokufanya, nitaweka machafu yenu yote
hadharani, unafikiri mimi siwajui, nazungumza haya nikiwa na
ushahidi...’akasema mpelelezi na kumfanya yule wakili amuangalia wa macho
makali.
‘Una ushahidi gani wewe..msipende kuchukulia mambo juu
kwa juu, mimi sijui lolote, na kifo cha mteja wangu ni changamoto kwangu, ikizingatia kuwa mimi ndiye niliyekuwa
mtetezi wangu...’akasema kwa uchungu. Mimi nafahamu hasira inayokuandama, lakini
hata mimi nina hali kama hiyo hiyomoyoni, naumia, na kuwalaani wote waliofanya
hivyo,…na sitatulia mpaka hao watu wafikishwe mbele ya sheria, wewe utaona
tu…’akasemana mpelelezi akamshika huyo wakili begani na kusema;
‘Sikiliza wewe, watu kama nyie nawafahamu sana, kwa
jinsi gani mnavyoweza kuigiza,nawafahamu sana hata kwenye msiba mtafika mkilia,
mkiigiza kuwa mna majozi, lakino moyoni mna malengo yenu, kwenye nyie mali ni
muhiimu kuliko uhai wa mtu, mpo tayari kuua, kama mtu huyu anaziba nafasi zenu za
kunufaika,lakini mimi nawaahidi kuwa siku zenu zimeshafika ukingoni…’akasema
mpelelezi
‘Naona hapa hatutaelewana, kwani wewe hapa nakuona una
hasira na unachofanya ni kumshuku kila mtu na hiyo ni hatari, maana unakiuka
maadili yako ya kazi,mimi nimekusamehe, kwani najua hapa unalolifanya sio
kusudio lako, hata hivyo, sioni kwanini wewe ujione unamhusu sana huyu marehemu
wakati wewe ulikuwa msitari wa mbele kumuona kuwa ana hatia,...’akasema
‘Kushikwa kwake ni utaratibu wa kisheria, na sio kuwa
hakuwa na haki, ...nyie mnanyima hata haki ya kuishi, huo ni utetezi
gani,...mtaniambia ukweli, naahidi kuwa sasa sirudi nyuma, ni lazima nipambane
na nyie hadi nione kundi lenu lote limesambaratika.....’akasema mpelelezi kwa
hasira
‘Hata mimi nakuunga mkono kama nia yako ni njema ya
kuliondoa hilo kundi, kama lipo, lakini fuata utaratibu unaokubalika,
usichukulie jaziba, jaziba hazitakusaidia
kabisa...’akasema.
‘Natumai familia hiyo ya marehemu itagundua ukweli kuwa
wewe ni ndumila kuwili, kuwa wewe
unahusika moja kwa moja kwenye kifo hicho….na mimi nitaongea nao kuwa
wasikuamini tena…’ akasema mpelelezi na na yule wakili akatikisa kichwa kama kusitikia, na kuanza kuondoka
‘Unaenda wapi, hutajamalizana, nimekuambia uniambie
ukweli kuhusu marehemu, je alitaka kuniambia nini?’ akauliza mpelelezi
‘Mimi siwezi kujua, kwasababuhakuwahi kuniambia kuwa
anataka kuongea na wewe, na tulishakubaliana naye kuwa hataongea na mtu
mwingine mpaka mimi niwepo, naona ajabu kuniambia kuwa mlipanga mje mkutane
naye, hapo na mimi nakutilia mashaka,..’akasema
‘Mlipoongea naye kwa mara ya mwisho alikuambia nini?’
akaulizwa
‘Alisema amechoka kukaa jela,na anahitajia kutoka nje,
kwani yeye hana hatia, na alisema nifanye haraka kumtafutia dhamana yake,na pia
akasema anahitajia kusimamishwa mahakamani ili aeleze ukweli kuwa hahusiki na
kifo cha mtoza ushuru..’akasema
‘Na kwanini wewe ukawa kikwaza cha maombi yake hayo,mtu
alitaka kusema ukweli mahakamani , lakini wewe kwa ujanja wako ukawa
unamzuia…?’akauliza
‘Mimi ni mwanasheria nafahamu athari za maombi yake hayo, yeye alitaka kusimama
mahakamani na kuongea mambo ambayo yangelimtia matatani na kuonekana kuwa kweli
alihusika, ndio maana nikawa na mzuia kwa nia njema maana nilijua athari
zake…’akasema
‘Hivi kumzuia kusema ukweli ndio kumsaidia, nini maana
ya mahakama, ..mahakama ipo hapo kwa kusikiliza ukweli, na yenyewe itajua
ukweli upo wapi,..huoni kuwa kwa kufanya hivyo umasababisha ukweli aliokuwa nao
huyo marehemu usitambulikane tena,na mumemzuia na mlipoona bado anataka kuongea
ukweli, mkaona mumunyamazishe kabisa...’akasema mpelelezi
‘Aliyotaka kuyaongea kama yangesikika mahakamani yangeli
mtia mteja wangu matatani mimi nafahamu sana sheria kuliko wewe, kwahiyo nafahamu nini cha
kufanya, nilifanya vile kwa masilahi ya mteja wangu, kwa nia njema kabisa ya kumsaidia mteja wangu, sasa wewe elewa unavyojua wewe, haijalishi, …’akasema.
‘Ukweli upi, ambaoalitaka kuusema,ambao unahisi
ungelimuingiza matatani...kama sio ujanja ujanja wako?’ akauliza mpelelezi.
‘Kwa mfano huyo mlinzi alitaka kukiri kuwa ni kweli yeye
hakuingia kwa kupitia mlangoni,kama ilivyoelezewa awali, japokuwa baadaye ilikuja
kubainika hivyo,kuwa yeye alipitia dirishani….’akasema wakili
‘Na huoni jinsi gani ulivyomzuia kusema ukweli huo hadi
nilipoleta ushahidi wa kubainisha kuwa kweli hakupitia mlangoni alipitia
dirishani, hivi ndivyo sheria zako zinavyokuelekeza kuwa mtu afiche ukweli,
wakati huo ukweli ndio unaohitajika?’akauliza.
‘Ukweli unahitajika kwa wakati maalumu, kwa masilahi ya
mteja wangu, na ukiona ukweli huo upo, na unamuathiri mteja wangu, ni lazima
nimshauri kwa manufaa yake...’akasema
‘Huo sio uadilifu na huo sio uwakili wenye manufaa kwa
taifa, nyie ndio watu mnaofanya kazi kwa ajili ya matumbo yenu, na sio kwa
ajili ya kutafuta haki na ukweli...’akasema mpelelezi
‘Wewe sema unavyotaka, lakini hujui misingi ya kazi
zetu, na mimi ninajua ni nini cha kufanya kwa waati gani kwa masilahi ya mteja
wangu, jiulize ni nini maana ya wakili mtetezi, nitakuwa mtu wa ajabu kama
nitafanya kazi ya muendesha mashitaka kwa mteja wangu badala ay kumtetea, wewe
vipi bwana....’akasema
‘Haya niambie jambo gani ambalo lilikufanya usimsimamishe
marehemu na ambalo angelisema lingemtia matatani..?’ akauliza mpelelezi
‘Sio lazima nikuambie yote, hayo ni mambo yangu na mteja
wangu, hata hivyo nitakuambia hili la bastola, najua unataka kulifahamu kuwa
yeye aliwahi kuchukua bastola ya mdada,japokuwa bastola hiyo haijahusishwa na
kifo cha mtoza ushuru…hayo na mengine kama angeliyaongea mahamakani unafikiri
hakimu angelihukumu vipi, ni moja kwa moja ingeonekana mlinzi ana hatia, ndio
maana nikamzuia kwa manufaa ya mteja wangu,..…’akasema.
‘Unasema jana mliongea na mteja wako, ukaondoka, na kuelekea kwa mdada, maliongea nini na mdada?’
akauliza
‘Mdada ni bosi wa mteja wangu, kuna malipo yanahitajika
, aliyokuwa akidai mteja wangu na alihitajia hizo pesa kwa ajili ya familia
yake, ndio maana nilikwenda kuonana na mdada...’akasema
‘Na ulipotoka hapo ulikwenda wapi?’ akauliza mpelelezi
‘Nilirudi ofisini kwangu, ..’akasema
‘Muda wa saa mbili za usiku ulionekana maeneo ya hapa
gerezani, niambie huku ulifuata nini ?’ akauliza
‘Mimi nina uhuru wa kwenda popote, na ndio nilikuja
maeneo haya lakini sio kuja huku gerezani, nina fundi wangu wa gari yupo maeneo
ya huku, nilikuwa kuonana naye, kwa ajili ya gari langu..’akasema
‘Ulipomaliza kuongea na huyo fundi, ulimpigia simu mteja
wako, mliongea nini...?’ akaulizwa na hapo akawa kama kashituka halafu akasema
‘Nilikuwa namjulia hali....ni wajibu wangu kuongea naye
kujua anaendeleaje...’akasema
‘Ulimuambia kuwa awe makini na mimi, ...wewe ulijuaje
kuwa mimi nataka kuongea na yeye...?’ akaulizwa
‘Yoye hayo umeyapatia wapi, ...usizue mambo, mimi ni
kweli niliongea naye, na ni wajibu wangu kumkanya kwa lolote lile...’akasema
‘Ujue siku hizi dunia ni kijiji, usione kuwa wewe ni
mjanja,...nakuambia ukweli, sitatulia mpaka wote niwaweke ndani,...wewe
ulimtisha mteja wako kuwa akiongea na mimi na kufanya nitakavyo mimi, itakuwa
mwisho wake..na huoni kuwa kauli yako ndio imatimiliza...’akasema mpelelezi
‘Niliongea naye kwa kumkanya, nawafahamu sana nyie watu,
mtamdanganya halafu mwisho wa siku mnamuhukumu...ndio maana
nilimkanya...’akasema
‘Ulipotoka hapa gerezani ulikwenda wapi?’ akaulizwa
‘Nilirudi ofisini kwangu..’akasema
‘Ulimpigia nani simu kwa muda huo?’ akaulizwa
‘Niliwapigia watu wengi sana, siwezi kukuambia wote
maana ni maswala ya kikazi, na wateja wangu mbali mbali, na wewe huna haki ya
kuwajua..’akasema
‘Wewe mwanzoni ulijifanya kuwa hujui kama mteja wako
alitaka kuonana na mimi, na sasa hivi nimekubana hadi umekiri kuwa ulionngea
naye ukamkanya kuwa asiongee na mimi, ...huoni hapo unaficha jambo, hebu niambie
na uliporudi ofisini kwako, uliongea na askari mmoja wa hapa gerezani kuwa
ahakikishe mimi sipati nafasi ya kuongea na mimi kweli au si kweli.....’akasema
mpelelezi
‘Sasa nakuona unazua mambo, mimi siwezi kuendelea
kuongea na wewe hapa, kama unaona mimi ninahatia nishitaki, na tutapambana
mahakamani....’akasema
‘Jibu maswali yangu kama wewe ni wakili unayejiamni,
...kama huna hatia mbona unaogopa, ..’akasema mpelelezi
‘Nimeshakujibu yale ninayostahili kukujibu zaidi ya hayo
nione ofisini kwangu, au kama unaona nina kosa nishitake, mimi nitakuja
kujieleza kituo chochote cha polisi,...’akasema na kuanza kuondoka, na
mpelelezi akamuendea na kumshika begani
‘Usiondoke mimi sijamalizana na wewe...’akasema
mpelelezi na yule wakili akageuka na kusogeza mkono wa mpelelezi pembeni na
kusema;
‘Naona sasa unataka kunipanda kichwani, nimeshakuambia
kuwa kama unataka kuongea na mimi kisheria, na ili nijibu maswali yako
kisheria, njoo ofisini kwangu au nifungulieni mashitaka, na mimi nitafika
kituoni, na kujajibu maswali yenu kisheria, lakini hapa tunaongea kama wapiti
njia tu...’akasema
‘Sasa mimi ninakushika kwa kosa la kuhusika na mauaji ya
mlinzi...’akasema na mara nikamuona mpelelezi akitoa pingu aliyokuwa kaiweka
nyuma,...
‘Eti nini.....’akasema wakili sasa akibadilika na kuwa
mkali na muda huo mkuu wa hapo gerezani akawa anawasogelea akijua sasa hali sio
shwari tena...
NB: Ni kweli kuwa huyu wakili anahusika na kifo cha huyo
mlinzi, tutaona sehemu ijayo
WAZO
LA LEO: Katika maisha yako ya kikazi, (waajiriwa) kamwe usifanye kazi kwa
ajili ya bosi, fanya kazi kwa mujibu wa kazi yako inavyotakiwa iwe- kitaaluma. Kuna baadhi ya wafanyakazi maofisini wana tabia hiyo, ya kuvizia bosi akiwepo ndio
wanawajibika, au kuwahi kazini kama bosi yupo kama huyupo wanachelewa au kama hayupo wanaongea tu,....huu ni utumwa,
huu sio uwajibikaji na huo sio utawala bora, jaribu kuwa muadilifu wakati wowote....
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment