Kesi ikaahirishwa na wakati huo askari wa fanya fujo
uone walishatanda kuzunguka hiyo mahakama, eti kuja kukabilia na vurugu zilizosababishwa na mdada, nahisi
taarifa zilienda vibaya kuwa kuna watu wameleat vurugu mahakamani,...nikajiuliza
hivi kweli hao askari wangeliingia humo ndani kipindi kile wangeliweza
kumkamata mdada, kwa jinsi alivyokuwa, labda wangempiga risasi..
Nikawa najiuliza jinsi gani mdada alivyoweza kuniinua
hewani na wakati keshajiandaa kunirusha, akaishiwa nguvu na kudondoka, na mimi
akili ilishanipaa nilijua kuwa nimesharushwa, kumbe, ni kwa vile mdada
aliniachia wakati yeye anadondoka.
Aliponiachia nilimdondokea , nikawa nimelala kichwa changu
kikiwa tumboni kwa mdada, na wakati huo docta alikuwa ameshifika akiwa na sindani
yake mononi tayari kumdunga mdada, lakini lipoona mdada katulia pale sakafuni,
akasubiri, kidogo na mimi nikawa nimajiinua na kujikagua kama nipo sawa,
nikasimama na docta akasema;
‘Haina haja ya kumpiga sindani,....’akasema na mimi
nilipoona sina tatizo, nikawa nimesogea mbali na mdada, nikionyesha wasiwasi
tayari kukimbia na docta alipoona nipo vile akaniambia;
‘Usiwe na wasiwasi hawezi kufanya kitu tena...’akasema
huyo dakitari, na mara polisi wawili wa fanya fujo uone wakawa wameingia na
vifaa vyao, dakitari akawaambia
‘Ni vyema mkaondoka tu, hawezi kufanya lolote, akiwaona mlivyo
hivyo inaweza hali yake ikamrudi tena...’akasema na kiongozi wao akawa kama
anakaidi akaja kumkabili mdada, akisema
‘Hivi kweli mtu huyu mmoja anaweza kuleta hizo vurugu,
..haiwezekani...’ akasema huyu askari, na wakati huo mdada akaanza kupata
fahamu, akajiinua na kukaa vyema.
‘Waulize wenzako...’akasema docta akimaanisha awaulize
askari polisi walioumia , wengine walishakimbizwa hospitalini, na yule askari
wa fanya fujo uone akamuangalia mdada kwa dharau, akasema;
‘Huyu ni lazima twende naye mahabusu , hawezi
kuizalilisha mahakama, huoni kuwa kafanya kitendo kisichokubalika, au kulikuwa
na watu wengine wametumia mwanya huo kuleta vurugu…?’akasema kama anauliza
‘Hujafanya hayo kwa akili yake,amefanya hayo bila kujua
alichokifanya, mimi ni dakitari bingwa wa mambo haya, ni vyema ukanisikiliza
kuliko kutumia jaziba, na ni vyema tukafanya haya kwa ajili ya afya ya huyu
binti, aliyoyapitia sio kusudio lake, anahitaji kupumzika, na nashauri sio
vyema kumpeleka huko mahabusu, haitamsaidia yeye, mtazidi kumuumiza
kisaikolojia…’akasema huyo dakitari.
Yula askari akamuangalia tena mdada halafu akageuka
kuwaangalia wenzake, akawatolea ishara ya kuondoka, na kweli wakaondoka na
kumuacha mdada akiwa na dakitari wake…
‘Kwani nimefanya nini docta..?’ akauliza mdada akiwa
bado yupo kwenye mshangao, huku akiangalia huku na kule.
‘Naona walikushitua ubongo ukawa umechanganyikiwa
tena,lakini nakuhakikishia kuwa haitatokea tena, kwani mara nyingi mshituko
kama huu hutokea mara mbili ya tatu, inakuwa kubwa,…na inakuwa ndio ya mwisho,
nina uzoefu na hilo, utapona kabisa sasa, na itafuta hatua nyingine uonane na
dakitari wa maswala ya uzazi…’akasema
‘Hata sielewi,ina maana watu wametoka wote, kesi
imeisha…’akauliza akageuka kuniangalia mimi
‘Mhh,imeahirishwa…’nikasema
‘Oh,hata sielewi,…nakumbuka nilikuwa natoa
ushahidi,…halafu yule wakili akaanza kunifokea, oooh,sijui,kilichotokea
baadaye, kichwa kilianza kuniuma, na ghafla akili sikujitambua tena,...mm huyo
wakili yupo wapi, au nimemuumiza, mbona siwaoni, mawakili wengine, mmh, jamani
hebu niambieni ukweli kumetokea nini…’akauliza
‘Mdada nafikiri ni bora ukapumzike kwanza, ili upate
nguvu,hizi dawa ukizinywa zitakufanya ulale sana, na ukiamuka, utakuwa
umetuliza kichwa chako,cha muhimu ni kukwepa mambo ya hasira…’akasema
‘Lakini mambo mengine yanaletwa na watu unaweza
ukajizuia, lakini watu wasiojua tatizo lako ni nini wakakuchokoza..yule wakili
aliambiwa hakusikia…’nikamtetea mdada
‘Kama alikuwa anabisha natumai sasa wamejionea wenyewe,
sijui hakimu atasemaje,maana nilivyomuona sijui kama ataweza kusema usimame
tena mahakamani kutoa ushahidi..’nikasema huku nikicheka
Mdada aliniangalia huku akikunja uso,nafikiri alikuwa
akijaribu kuwaza jambo, au kujaribu kukumbuka hicho kilichotokea,halafu akasema;
‘Mimi nataka nisimamishwe tena kutoa ushahidi nataka
niseme,ukweli wote bila kuficha, naona ndio wakati muafaka kila mmoja asema
kila anachokijua ili hili tatizo lifikie mwisho,nimechoka na hili tukio,
….’akasema
‘Mimi nafikiriumeshasema kila kitu,kwani kuna ukweli
gani uliobakia?’ nikauliza
‘Kuna mambo mengi yamejificha hapa, kufa kwa mtoza
ushuru ni sehemu ndogo tu, lakini mara nyingi kunapotokea mauji kinachoangalia
ni kile kifo, ni nani kamuua, …basi,lakini chanzo mpaka ikafikia…’akatulia
kidogo, halafu akauliza
‘Mpelelezi yupo wapi, …ni muhimu ule ushahidi wote
uwepo, nafahamu yeye anajua mengi sana, mimi naona ni muda muafaka mimi na yeye
tukaweza kuungana na kulimaliza hili tatizo…’akasema mdada na kunifanya
nimuangalia kwa mashaka.
‘Mdada unayaongea hayo kwa dhati kweli, au ….?’
Nikauliza
‘Unakumbuka tulipoitwa na mzee, baba mkwe wako, kuna
jambo alilisema,kwakweli sikumuelewa huyo mzee, inaonekana kuwa huyo mzee
anafahamu mambo mengi sana, mimi nimekuwa simuamini….’akasema
‘Kwanini…?’ nikauliza
‘Nataka nione naye kwanza, …..ni muhimu sana niongee
naye na nikiongea naye, nataka nisimame tena kutoa ushahidi wangu, nataka
nipambane na huyo wakili wao kwa hoja…yeye aliniandama kwa vitisho na kunishuku
kuwa mimi ndiye niliyemuua mtoza ushuru,…ni lazima hili liwekwe wazi mbele ya
mahakama…’akasema
‘Huwezi kuzidiwa tena, ukaleta fujo?’ nikauliza
‘Kwani mimi nilileta fujo…?’ akauliza akionyesha
mshangao, na docta wake, alikuwa akimuangalia mdada kwa makini, akasema;
‘Mdada ni bora kwanza ukapumzike,…nataka kukupa dawa na
hizo dawa ukizitumia, unatakiwa kulala, zitakusaidia sana….’akasema
‘Hapana docta, hili ninalotaka kulifanya halitakiwi
kusubiri, nisipoliweka hili wazi mapema,jamii itanishuku mimi vibaya…nyie
hamulioni hili,kuwa sasa hivi mlinzi haonekani tena muuaji, hiyo hatia
imesukumwa kwangu...’akasema
‘Lakini…’nikasema na mdada akanikatisha.
‘Wewe huijui jamaii ilivyo,mara watu wengi wanapenda
kuyachukulia mambo juu kwa juu bila kufanaya utafiti,na sijui huyu hakimu
atakuwa na maamuzi gani, hebu niwaulize je hakimu alisema nini,…?’ akauliza
‘Alisema kesi imeahirishwa, hadii takapotajwa
tena…’nikasema
‘Mhh, kwahiyo kauli hiyo aliitoa baada ya vurugu, …ina
maana mimi nilisababisha kesi kusimama…hapana, lakini kwanini hawakumsimamisha
yule wakili kuniandama kwa maswali yasiyo na ukweli…kuna nini hapa..?’ akauliza
‘Pale nahisi wengi walihisi wewe una mashetani, na yule
wakili alikuwa akiyakemea,ili yakutoke,kwahiyo kukawa na kitu kama
imani,wanavyoamini watu wengine….hata mimi niliona ajabu kwanini wakili yule
alipokuwa akikiuliza maswali, na akaambiwa aache,hakuacha,akawa anaendelea tu,
na hakukuwa na jitihada za kumsimamisha…’nikasema
‘Ngoja nionane na hawa watu wawili, hasa huyo
mzee,aliyekuwa baba mkwe wako….’akasema na kuniangalia huku akionyesha tabasamu
la kulazimisha pale alipotamka neno hilo `aliyekuwa..’, nahisi alikuwa na maana
yake, nikasema;
‘Sizani kama watakuruhusu kumuona, shangazi hawezi
kukupa nafasi hiyo..’nikasema
‘Hana ubavu wa kunizuia mimi, wewe utaona, mimi sio wewe….’akasema
na akageuka kumuangalia docta na kusema
‘Tafadhali docta hili tatizo nataka liishe haraka
iwezekanavyo,na likiisha nitakuwa mgonjwa wako kamili,ili nipone kabisa…sizani
kama nitakuwa na kazi nyingine baada ya hii,nataka kupumzika, na mimi natamani
kuwa mama wa nyumbani, hata kama siwezi kupata mtoto…’akasema na docta
akatabasamu
‘Mhasibu, …’akasema mdada akiniangalia mimi machoni,
mimi nikamuangalia, nay eye akasema;
‘Unakumbuka niliwahi kukuuliza swali, uje kunipa jibu
baadaye, natumai sasac umeshapata jibu, kama una majibu yake natumai muda wa
kuniambia umefika, kabla mimi sijachukua maamuzi mengine,…’akasema na mimi
nilitaka kumuuliza swali gani, lakini yeye akaendelea kuongea, kwa kusema;
‘Mimi nafahamu henda hata wewe utakuwa na uwoga wa
kuishi na mimi,baada ya kushuhudia yote yalitokea, kuwa labda mimi nina
mashetani, nitakuwa nakusumbua, lakini kiukweli, mimi sina mashetani, docta
huyu hapa anafahamu tatizo langu ni nini, na kaniahidi kuwa litakwisha….’akasema
na docta akasema;
‘Hayo sio mashetani,…ni ugonjwa unaotokana na mashinikizo
ya ubongo, kutokana na madhila aliyopambana nayo, ambayo yameanzia utotoni, na
baadaye akaja kukabiliwa na mjanga ya kudhalilishwa, hadi kuharibiwa kizazi, …yote
hayo yakajenga kitu kwenye ubongo wake, chuki, na kutaka kulipiza kisasi…’akasema
docta
‘Docta ndio awe na nguvu za namna hiyo , aweze kuongea
kama….mwanaume,ananguruma kama simba…hapana docta, mimi nahisi hayo ni mashetani…’akasema
‘Wewe utaona tu, hili ni swala la muda, tatizo ni kuwa tangu
nianze kumuhudumia mdada ,sijapata nafasi ya kukaa naye kwa karibu kama
nilivyomshauri, nilitaka yeye afuatilie masharti yangu,...nilitaka
atulie...aachane na kazi za kumvuruga akili yake, lakini hakutaka, sasa inakuwa
vigumu sana…’akasema docta
‘Au kuna watu wanataka iwe hivyo ili wakamilishe mambo
yao kwa kukutumia hayo matatizo yake aliyo nayo….?’ Nikauliza na mdada akawa
kama anawaza jambo na mara simu yake ikalia, ilikuwa kwenye mlio wa kunguruma
tu, akaangalia na kusema;
‘Mzee anapiga sijui anataka nini….’akasema na kuipokea
alisikiliza kwa makini bila kusema neno baadaye akasema;
‘Sawa mzee nitakuja kuonana na wewe…lakini iwe mara ya
mwisho, nimeshakuelezea msimamo wangu, na nataka usiyahusishe haya na mambo
binafsi,binti yako anatakiwa kukubali ukweli, yaliyotokea kwake ni bahati mbaya,….’akasema
na kusikiliza kwa makini halafu akasema;
‘Kama ni hivyo sawa tutakuwa pamoja,na nikija hapo,
sitaki kukutana na huyo shangazi,maana tutaishia kubaya mimi na yeye hatuivani,
kama ni mambo ya uchawi,yeye ndiye mchawi,mimi sijui chochote kuhusu uchawi…’akasema
na kutulia kusikiliza, halafu akasema
‘Yeye ndiye
anasema hivyo nakutangaza kwa watu hivyo,na mimi sina mashetani…hizo ni dhana
za watu wenye imani hizo za kishirikina, mimi nina tatizo linalotambulikana
kitaalmu na litakiwsha tu….’akasema
‘Sawa nitakuja mzee, muda sio mrefu, nipe dakika kumi,
mimi sijambo, usiwe na wasiwasi na mimi, yah, yupo hapa, anasubiri kauli ya
mahakama,...ndio yupo docta wangu, kutokana na yaliyotokea , natumai umeambiwa,
…’akatulia kusikiliza halafu akasema
‘Ndio, nitakuja, nije na yeye, kwani yeye anahusikana
vipi na hayo,sitaki kuwahusisha watu wengine, yeye na mimi ni maswala binafsi,…kwanini
unataka nije na yeye?, hapana mzee ,kwanza ni lazima tuongee wawili, tukimaliza
anaweza kuja mkaongea naye, hutakufa mzee, kwanini unasema hivyo, wewe sio
mungu, na kuumwa sio kufa, haya mzee nakuja…’akasema mdada na kusikiliza kwa
muda, halafu akakata simu na kusema;
‘Huyu mzee kachanganyikiwa, anasema anataka kusema
ukweli wote, na hana muda mrefu wa kusubiri eti siku zake za kuishi
zimekwisha,…naona keshakata tamaa ya maisha, …’akasema mdada na kunifanya mimi
nianze kujilaumu, kwani huyo mzee kanisaidia sana, na kama kafikia hiyo hali ni
muhimu niweze kuongea naye, ili angalau niweze kuonyesha huruma na fadhila
zake,nikasema;
‘Ni muhimu nionane na huyo mzee…’nikasema
‘Ndivyo anavyotaka yeye hakujua kuwa umekamatwa tena,
anataka mimi na wewe tuonane naye pamoja, lakini nijuavyo mimi ataanza kuingiza
mashinikizo yake kwako kuhusu binti yake, yeye anampenda sana binti yake, hatakubali
wewe utoe kauli ya kumkataa mbele yake,..’akasema mdada kwa sauti ya utulivu.
‘Na kwa hali aliyo nayo ukitoa kauli knyume na matarajio
yake huenda itamuumiza sana, japokuwa shangazi yeye keshatoa maamuzi, sijui kwa
huyo mzee, yeye ana kauli gani, sasa maamuzi ni yako...ila ,nikujuavyo wewe
hutaweza kusema ukweli,…utakubali tu kumrizisha huyo mzee, na hilo mimi sitaweza
kuvumilia, ni bora uje utoe kauli yako wakati mimi sipo,....’akasema kwa sauti
ya huruma na sio kama yule mdada niliyemfahamu kabla.
‘Niliwahi kukuuliza kabla kuwa je upo radhi kuoa, na
kuishi ukiwa huna mapenzi moyoni...uoe,kwa sababu tu ya baba mkwe, hukuwa na
jibu la kujiamini, ukawa unasema eti kwa vile, ulifanya hayo makosa,
kwahiyo...ooh, ...’akawa anatikisa kicha halafu akasema
‘Kiukweli,mimi sasa nimechoka, huenda ni vyema na mimi
nikawa na maamuzi magumu, japokuwa nakupenda, japokuwa nilitarajia mengi kutoka
kwako, lakini je mwenzagu unaweza kujiamini ukatoa maamuzi ya kutoka moyoni
kwako kwa ujiamini japokuwa yataumiza wengine, sasa upo tayari kuyatoa majibu
hayo kwa baba mkwe...'akasema
'Ila mimi sitaki uyatoe hayo nikiwepo, ili isije ikawa mimi ni
sababu, hata hivyo, nikuonavyo huenda ukajibebesha zigo usilioweza kujitwika,
ni bora mimi nianze, tukijaliwa basi au unasemaje…?’ akaniuliza
‘Mdada nilishakuelezea kwanini nimeamua kufanya hivyo,
na ni vyema kwanza nikaongea na mzee nikajua msimamo wao....napenda sana niwe
na wewe, kwani kiukweli moyo wangu kila mara unakuwaza wewe, sijui nitaishije
bila ya wewe....’nikasema na mdada akawa kama analazimisha kutabasamu,
‘Mdada kiukweli mimi nataka wewe uwe karibu yangu wakati
wote, kwa kipindi nilichojuana na wewe nakuona kama sehemu ya mwili wangu,
lakini nitafanyaje sasa, sijui kwakweli mdada...’nikasema na nilijaribu
kumuangalia docta kama anatusikiliza , lakini nilimuona akihangaika na mambo
yake, na mimi nikaendelea kusema;
‘Mdada, hivi wewe huoni kuwa nitakuwa nimefanya unyama, nikitoa
kauli ya kukataa mbele ya baba mkwe, na hali aliyo nayo kwasasa, wewe hujui niliyoyafanya
kwa huyo binti yake huko nyuma, ni kweli ulikuwa ni ujana, unanisumbua, lakini
nilifanya vibaya, na nikajifunga kwa kuahidi mbele ya wazazi wake kuwa
nitamuoa...’nikatulia
‘Sasa naanza kujuta, najuta sana mdada kwa hayo
niliyoyafanya , lakini nifanye nini kwa sasa,..nashindwa , na sijui kama
nitaweza kumsaliti huyo mzee, kwa mambo mengi aliyonifanyia,...pia huyo binti
yake ana mtoto wangu, hebu niambie mdada kama wewe ungelikuwa katika nafasi
yangu au wewe ungelikuwa huyo binti ukafanyiwa hivyo ungelifurahi…’nikasema
mdada alikunja sura na kusema;
‘Lakini wao wenyewe kwa kauli yao wamesema hawakutaki
tena umchukue binti yao, wewe umekuwa chanzo cha matatizo kwa binti yao, na
wameshataifisha mali zako, kutokana na mkataba mliowekeana...sasa ukiendelea
kung’ang’ania sijui watakuelewa vipi, ...je ni kwamba unampenda huyo binti, au
unataka tu kulipa fadhila...?’ akawa kama ananiuliza halafu akasema
‘Ok, mimi sijui, sasa hayo utajua wewe mwenyewe, kwasasa
mimi nina mambo muhimu ya kufanya, nikiyamaliza kama hujanipa jibu, huenda tusionane
tena...’akasema mdada
‘Una...’nikataka kusema kitu lakini nikashikwa na
kigugumizi, na wakati huo mdada alikuwa amemgeukia docta, na docta akawa
anafunga funga vitu vyake kuondoka, na alipoona mdada anamuangalia yeye akasema;
‘Hayo ni mambo yenu binafsi, nisingelipenda kuyaingilia,
ila eeh, samahani kwa nitakalosema, kwani mimi kwenu ni mkubwa , na licha ya
utaalamu wa udakitari lakini pia nina uzoefu wa maswala ya ndoa, kwahiyo sio
vibaya nikachangia jambo hasa kwako wewe mhasibu, niyasema haya kwa nia njema, mhasibu,
jaribu kuwa makini, hasa katika swala la ndoa...’akasema docta.
‘Mimi nimeshaoa, na kama ingeliwezekana kurudia nyuma,
huenda ningelikuwa makini sana katika kuchagua mwenza wa maisha,
nisingeliharakisha, sasa mimi nisingelipenda na wewe mhasibu ukaja kujijutia,
kaa chini, panga,jiulize na ujipime, … ‘akasema docta
‘’Nikuambie
kitu kufunga ndoa ni pa-pa, utashangiliwa,
sherehe nk, ...lakini maisha ya ndoa na wewe na mwenza wako, wenzako watakuwa
hawapo tena, na hayo maisha ni safari ndefu,...’akasema huku akiweka mkoba wake
begani.
‘Mimi nakumbuka wakati naoa,niliambiwa ndoa ni nusu ya
imani yako,...kwa muda ule sikuelewa, maana akili ilikuwa na hamu ya kuingia
kwenye chumba hicho cha ndoa, nikijua ni maisha rahisi tu, na kama nimekosea, nitamfunda
mwenzangu maisha yataendelea ikishindikana si basi bwana nitaacha nitaoa
mwingine,...ilikuwa hivyo, lakini sio rahisi kihivyo....’akasema docta
‘Kwanini walisema ndoa ni nusu ya imani,..ukiangalia kwa
makini ndoa ni imani, maana unaoa, na unatakiwa ufuate masharti ya ndoa, kwa
siri na kwa dhahiri, hiyo ni imani. Ni imani iliyokunga na hapo huna ujanja,..ukiiba
uachepuka moyo unakusuta, mwenyewe unajihisi umefanya dhambi,..unaona hapo, imani . Na ndio maana hapo unatakiwa ujipime,...
‘Unatakiwa ujipime kwasababu maisha ya sasa sio yale ya
kale, ya akina baba,au babu zetu , hayo yalikuwa enzi zao, watu wanaoa, hata
kama hawajuani, kinachohitajika kwa kipindi kile ni mwenza wa maisha, na maar
nyingi wao walikuwa wakiangalia vigezo vya kijamii, ....lakini sio sasa, maisha
ya sasa yana mitihani mingi, ndio maana kabla ya kuoa, unatakiwa ujipme
kiukweli kama kweli unaweza kuishi ndani ya ndoa, ...usifuate mkumbo tu
baba...’akasema na kutulia
‘Kwani hapo ukifanya makosa, ujue nusu hiyo ya imani ya
maisha yako ambayo ni moja ya mihimili ya maisha ya ndoa itakuwa imevurugika,
utakuja kujuta maisha yako yote …kwahiyo ni muhimu ukajiuliza wewe mwenyewe; je nipo tayari kuoa, na kama nipo tayari
ni nani anafaa kuwa mke wangu,..’akatulia
na huku mdada akiwa kashika shavu sijui alikuwa akimsikiliza docta au alikuwa
akiwaza yake.
‘Nikuambie ukweli, kila mmoja ana mapendeleo yake,
wengine wanaangalia sura, wengine wanaangalia mali, wengine hiki na wengine kile,.
...ukiambiwa uorozeshe hayo mapendeleo ya watu kuhusu mke au mume gani anayefaa
kwake, huwezi kuyamaliza, lakini muhimu sana ni upendo wa kutoka moyoni...’akasema na kushika kifuani
‘Usifanye kosa hapo ukasema unaoa tu, eti wengine
wanafanya hivyo kwasababu ya yale yaliyotokea nyuma kwa mfano unaoa kwa vile baba
na rafiki yake wameshibana,au mlisoma wote, au...mwingine kwa vile baba mkwe
alimfadhili, mwingine...’akatulia akionyesha mikono kwa ishara.
‘Hayo ninayokuambia yapo, lakini ukumbuke ndoa sio maisha
ya muda mfupi, ndoa sio sehemu ya majaribio....itafika muda utakumbana na
mitihani, vishawishi, utashindwa kuvumilia, na wakati huo mna watoto, unafikiri
utafanya nini hapo...je kama ulioa kwa ajili ya fadhila, ndio basi tena, na
sijui kama fadhila zinalipwa hivyo, ..hapana jaribu kufikiri zaidi….’ akasema
‘Mimi nakushauri, kabla hujatoa maamuzi ya nani umuoe,
hebu chuja moyo wangu, hebu weka maisha yako mbele zaidi na ujaribu kuhisi kuwa
upo na mke wako, anakufanyia hivi na vile, ...unaweza kuangalia maisha ya
majirani zako,ndugu zako , hata wazazi wako,waliowahi kuoa, ikawa ni shule
kwako....’akatulia
‘Kama nilivyokuambia wengine huwa wanaoa kwababu ya
upendo,...hili ni muhimu sana katika ndoa, lakini upendo wa namna gani, mtu anaweza kupenda maumbile, mwingine sura,
mwingine sauti..je hivyo vitu ni vitu vya kudumu,kama sio vya kudumu vikiisha
utafanya nini, mtaachana?, ....angalia hapo kwa makini,...kwahiyo upendo nao
una sura nyingi tu....’akaangalia saa yake na kumtupia jicho mdada, na mdada
naye akawa anaangalia simu yake nafikiri alikuwa akisome kitu kwenye simu yake.
‘Sasa ndugu, sikutaka kukuingilia sana, ila kwa vile
nimesikia mkiongea maswala ya ndoa,nikaona niwasaidie kwa hilo, kuwa kabla
hujaoa au kuolewa fikirieni kwanza, kabla hujachagua mke au mume, angalia nafsi
yako kwanza, inapenda nini, na huko mbeleni hicho unachokipenda kitakusaidia
nini, lakini la muhimu ni upendo wa kweli, wa kutoka moyoni..’akashika tena
kifuani.
‘Ukiwa hivyo ukawa unampenda mwenza wako na yeye akawa
anakupenda mtafurahia sana ndoa yenu,kwani amani na upendo vitatawala ndani ya
nyumba yenu, na mtapata kizazi bora, hata neema za riziki
zitaongezeka....kumbuka ndoa ni sehemu ya kutuliza kichwa, ndoa ni sehemu ya
kupendana , ndoa ni raha, na kamwe
ndoa haikupangwa iwe ni karaha, kwahiyo ni muhimu umuoe mtu wa chaguo lako, mtu
unayempenda, usichukue maamuzi kwa shinikizo fulani……’akasema
Mdada akawa katulia tu, na mimi nikawa naangalia chini
nikishindwa la kusema chochote, halafu mdada akasema;
‘Docta naona kama niwaache, maana muda umetaradadi, ila
ni muhimu nikamuone mzee, halafu baadaye nitakuwa na kikao na mpelelezi, naona
kanitumia ujumbe wa kukubali kukutana na yeye, na kama mambo yatakwenda vyema,
basi nitakuambia wapi nitakuwa tayari kwa matibabu yangu, nina imani kuwa
safari hii nitatulia…’akasema na kuanza kuandoka, hakuniangalia..nikajihisi
mpweke, nilitaka kumuita lakini sikuweza...
‘Hata mimi naondoka, sijui kama watakurudisha huko
rumande au ndio dhamana imepita,....lakini mimi nakutakia kila laheri, usikate
tamaa, na mimi nisingelipenda ukawa na pupa ya kuoa haraka kama hujajiweka
sawa..usifuate shinikizo, acha haya yanayokukabili yapite, halafu ukitulia,
mambo yatajileta...’akasema na kunishika mkono akawa kama ananikumbatia kidogo,
alafu akawa anaondoka, nikasema;
‘Ahsante sana docta, ...’nikasema na sikuweza kusema
zaidi nilihisi machozi yakinilenga lenga sijui kwanini,...
Nilibakia pale mahakamani nikiwa nimeduwaa,baadaye
nikatoka, nikitarajia nitakumkuta mdada hapo nje, ili tuongozane, lakini
sikuona gari lake, nikajua ameshaondoka, nikaingia kwenye gari langu na kuanza
kuondoka ,moyoni nikiwa nawaza maneno ya docta;
..Ujue
ndoa ni safari ndefu, na ndoa inakuwa nusu ya imani yako, ina maana ukikosea
hapo tu, ujue nusu hiyo ya imani ya maisha yako ambayo ni muhimili muhimu wa
ndoa yako utakuwa umeharibika, …kwahiyo ni muhimu ukajiuliza wewe mwenyewe je
unaoa, kwasababu ya yaliyotokea huko nyuma, kama vile kulipa fadhila, au….’
‘
Au
unaoa kwa sababu ya upendo, na amani katika maisha yako ya baadaye, jiulize kwa
makini maana ndoa ni upendo, ndoa ni ya raha, ndoa sio karaha, na ili uyapate
hayo ni muhimu umuoe mtu wa chaguo lako, mtu unayempenda, usichukue hayo
maamuzi kwa shinikizo fulani…
NB: Darasa la
ndoa kidogo,
WAZO
LA LEO: Ni msimu mwingine wa ndoa, na wale waliojaliwa wapo
mbioni au wanafunga ndoa.Ni muhimu sana, watu kabla ya kuingia kwenye kitengo
hicho muhimu cha maisha,wakapitia darasa la ndoa, angalau mtu kujua ni nini
maana ya ndoa, na ndani ya ndoa kuna nini, na natakiwa nifenye nini.
Ndoa nyingi sasa
ni maumivu, na hii ni kutokana na kuamua kabla ya kujifunza. Elimu ya ndoa ni
muhimu sana, tujue, na tuwe na maamuzi ya uhakika, ili tukioa au kuolewa tuwe
tumechagua mke au mume mwema, kwa ajili ya matunda mema.Tukumbuke ndoa ni raha,
na haikutakiwa iwe ni karaha
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment