Mahakama ilikuwa imejaa watu isivyo kawaida, ilibidi
askari wa usalama wafanye kazi ya ziada kuwazuia watu wasiendelee kuingia
kwenye ukumbi huo wa mahakama, kwani ndani kulishajaa watu na bado watu
walikuwa wakizdi kuja kusikiliza kesi, na kesi iliyovutia wengi ni hiyo ya
mauaji ya mtoza ushuru, japokuwa kulikuwa na kesi nyingine iliyopangwa
kusikilizwa siku hiyo hiyo.
Penye wengi pana mengi, kila mwenye mdomo hapakosi la
kuongea, hata kama halina uhakika, kwani kwa mbali niliwasikia watu wawili
wakiongea kwa sauti ya juu kidogo, bila kujali kuwa wapo mahakamani, mmoja
akasema;
‘Leo tutaona ukweli kama kweli wanasiasa wana nguvu
zaidi ya sheria…’
‘Lakini uonavyo wewe kweli ni hivyo kuwa wanasiasa ndio
wakosaji, mimi naona ni uzembe wa watendaji wenyewe?’ akauliza mtu mwingine
‘Watendaji gani, unaozungumzia wewe, hivi kama bosi
ambaye ni mtu wa siasa akitoa amri, hili lisifanyike, au lifanyike hivi, hao
watendaji watakaidi, hawawezi kumpinga bosi wao hata siku moja, ....wafanye
hivyo kama hawataki kazi,…’akasema jamaa wa kwanza
‘Ndivyo ilivyo, mimi sioni ajabu, maana mengine
tumejitakia wenyewe, hao wanasiasa tumewachagua wenyewe, wapo hapo kwenye
nyadhifa zao kutokana na kura zetu, na sasa wanatuonyesha jeuri yao,wanasema
ukitaka kumjua mtu tabia yake muache apate, akipata tu, utaijua tabia yake
ipoje, lakini wakati hana atanyenyekea utafikiri ni mtu mwema sana....’akasema
‘Kura yako ina thamani pale inapotafutwa, lakini baada
ya kuhesabiwa, haina thamani tena, kwani yule uliyemchagua anakuwa ndiye bosi
wako,…..na hatajali kuwa wewe ndiye uliyempa hicho cheo,ndio mchezo wa siasa
ulivyo….’akasema
‘Lakini hawa watendaji hasa watu wa usalama,kwanini
wawaogope wanasiasa wakati wao ndio walinzi wa dola….?’ Akauliza
‘Kawaulize wenyewe…chunga mdomo wako, mimi sijawataja
hao,...’akasema mwenzake akitaka kumkatisha kwani kesi ilishaanza, na mara watu
wakatulia pale hakimu alipoanza kuitaja hiyo kesi,na baada taratibu zote za
kimahakama, na kuelezea kesi hiyo inavyokwenda ikafikia hatua ya kuitwa shahidi
aliyetakiwa kutoa ushahidi wake siku hiyo, hapo hakimu akasema;
‘Upande wa wanaoshitaki, muiteni shahidi wenu,…’hakimu
akasema na muendesha mashitaka akasema;
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, nitamsimamisha shahidi wangu,
lakini nawaomba upande wa utetezi wawe makini katika uulizaji wao wa maswali,
kama tulivyoongea nao,kwani hatutaki mahakama hii ikageuka sehemu ya kutuliza
fujo…’akasema na kauli hii iliwafanya watu wagune, na wakili mtetezi akasema;
‘Mheshimiwa hakimu,muendesha mashitaka, anataka
kututisha, hiyo kauli yake inaonyesha jinsi wenzetu walivyo, nia na lengo lao
ni kutufanya sisi tusitimize wajibu wetu….’ Na hapo kukatokea malumabano ya
mawakili hao wawili hadi hakimu alipoingilia kati
‘Nimesema shahidi anayestahiki kutoa ushahidi wake aitwe
nasikusema muanze kulumbuana,nawaonya tena ….’akasema hakimu akigonga kirungu
chake na mahakama ikawa kimya,na muendesha mashitaka akasema
‘Shahidi wangu atakayekuja kutoa ushaidi wake ni Mdada
Binti Majivuno…..’akasema na mara minong’ono ya watu ikasikika, na minong’ono ya
kundi la watu hugeuka kuwa mngurumo, na ndipo hakimu akagonga kirungu chake na
kusema;
‘Kama hakutakuwa na utulivu hatutaruhusu tena
wasikilizaji, watu wa usalama hakikisheni sheria za mahakama zinafuatwa na kama
hakuna utulivu tutawatoa wote nje…’akasema hakimu na kukawa kimi wakati huo mdada
alishafika sehemu wanaposimama mashahidi na kuanza kutoa kiapo, na taratibu
nyingine zikafuatwa.
Mimi pale nilipokaa nikiwa na askari usalama nyuma yangu
nilihisi mwili ukinisisimuka, hasa nilipomuona mdada akiwa kasimama pale mbele,
nilianza kuingiwa na wasiwasi hasa hapo wakili mtetezi atakapoanza kumuhoji
mdada.
Akili yangu ilirejea nyuma siku ile nilivyoshuhudia
akimtupa mtu kama katoto, umbile la mtoza ushuru ni kubwa, lakini kwa mdada
ilionekana kama katoto...sikuamini, ni nguvu gani hizo zinazoweza kumuingia mtu
awe na nguvu kama za tembo, ndio hayo mashetani au kuna nini cha
zaidi...nikaendelea kuwaza huku mdada akitoa maelezo yake huku akiongozwa na
msimamizi wa kesi hii.
‘Haiwezekani mtu awe na nguvu za namna hiyo, aweze
kumrusha mtu kama mtu anayerusha gunia lisilo na uzito…’nikasema siku
nilipomuahdithia mpelelezi
‘Hizo ni imani tu,hakuna kitu kama hicho,kitaalamu mdada
anajulikana kaathirika na msongo wa mawazo kutokana na madhila aliyoyapata,
hayo mengine ni uvumi tu wa watu…’akasema mpelelezi.
‘Ipo siku utashuhudia mwenyewe na wewe utakuja kuniambia,….hata
mimi nilikuwa siamini hayo,lakini siku ile niliposhuhudia mwenye kwa macho
yangu,nimeanza kuamini kidogo kuwa kuna mambo yanayozungumzwa mengine yapo…’nikasema.
‘Kwahiyo wewe unasema mdada ana mashetani?’ akaniuliza
mpelelezi, na hapo nikashituka toka kwenye mawazo nilipomuona mdada akiulizwa
swali na muendesha mashitaka;
‘Mdada binti Majivuno hebu tuambie siku ya tarehe ambayo
marehemu aliuwawa wewe ulikuwa wapi?’ akaulizwa mdada.
‘Nilikuwa nyumbani kwangu muheshimiwa…’akasema mdada
‘Ulikuwa ukifanya nini?’ akaulizwa
‘Nilikuwa nipo kwenye mapumziko maana nilikuwa naumwa,…’akasema
mdada
‘Ulikuwa unaumwa nini,unaweza kutuambia tatizo gani lilikuwa
linakusumbua?’ akaulizwa
‘Mimi huwa nina matatizo yanayotokana na msongo wa
mawazo,japokuwa wengine wanasema nimekubwa na mashetani lakini kitaalamu
wanasemani ni tatizo linatokana na mgandamizo wa mawazo yaliyotokana na
matatizo yaliyowahi kunikuta kipindi cha nyuma….’akasema mdada
‘Inatosha haina haja kuelezea zaidi, Muheshimiwa hakimu,
nia ya kumuuliza hivyo ni ili mahakama yako tukufu ielewe tatizo alilo nalo
mdada,ili wenzetu wakianza kumuhoji wawe na tahadhari hiyo,na sikuwa na
makusudio ya kuwatisha….’akasema wakili muendesha mashitaka,na wakili mtetezi
akataka kuweka pingamizi lakini katulia
‘Hebu tuambie siku hiyo ambayo marehemu aliuwawa,
ulikuwa na nani?’ akaulizwa
‘Alikuwepo Mhasibu na kabla ya hapo alikuwepo bosi wa
kampuni yangu niliyokuwa nikifanyia kazi…’akasema
‘Walifika hapo kufanya nini?’ akaulizwa
‘Walifika kuja kunijulia hali,na katika hali
waliyonikuta nayo,ikabidi wapeane zamu ya kunilinda,….’akasema
‘Je kipindi marehemu anafika wewe ulikuwa wapi?’
akaulizwa
‘Mimi nilikuwa ndani chumbani kwangu, kama nilivyosema
nilikuwa naumwa,…’akasema
‘Kwahiyo wakati marehemu anaingia wewe ulimuona?’
akaulizwa
‘Wakati marehemu
anaingia mimi sikumuona, nilimuona wakati nimetokea chooni, na nilipofika pale
alipokuwa amesimama nilishangaa kumuona amemshikia bastola mhasibu,….’akasema
‘Wewe ukafanya nini?’ akaulizwa
‘Kwanza nilishituka sana,pili nikajua kuna
hatari,kwahiyo ni lazima nijihami,na kwa vile mtoza ushuru ambaye ni marehamu
alikuwa hajaniona, nikaona nichukua nafasi hiyo kumgonga mkono wa huyo
marehemu,mkono uliokuwa umeshika silaha, na nilifanya hivyo, na silaha ikamtoka
mononi……’akasema mdada
‘Ehe ikawaje?’ akaulizwa, na mdada akasema;
‘Wakati huo hali ilishaanza kunibadilika, nikawa
sijitambui tena...’akasema
‘Una maana gani kusema ulikuwa hujitambui tena ….?’
Akauliza
‘Akili ya kawaida ilinitoka, nikawa mtu mwingine, sijui
inavyokuwa ila nakuwa sina kumbukumbu zangu za kawaida,…’akasema mdada
‘Kwahiyo wakati unamgonga huyo mtoza ushuru mkono,
ulikuwa bado unajitambua, baada ya hapo hali ikabadilika ukawa hujitambui
tena...?’ akaulizwa
‘Ndio muheshimiwa, ninachokumbua hapo ni kuwa nilimuona
mtoza ushuru akiwa na bastola, nikamgonga mkono na bastola ikamtoka, na wakati
huo mwili wangu ukawa unasisimukwa, kichwa kikawa kinaniuma sana, na mara
nikahisi kama kitu kimeziba aili yangu, nikawa sijitambui tena.....’akasema
‘Ulizindukana
kutoka kwenye hali hiyo wakati gani?’akaulizwa
‘Kipindi polisi wameshafika nilizindukana na kujikuta
nipo sakafuni nimelala….na nilipoamuka dakitari wangu akanituliza na kuniambia
nisiwe na wasiwasi….’akasema
‘Ulpozindukana uliona nini?’ akaulizwa
‘Niliwaona askari wakipima huku na kule,na baadaye macho
yangu yakamuona mtu kalala sakafuni, akiwa kafunikwa,nikamuuliza dakitari wangu
kumetokea nini,akaniambia mtoza ushuru kauwawa….nilishituka sana, na kwa vile
alikuwa mtu wangu wa karibu niliumia sana…..’akasema
‘Hebu niambie ukweli,kabla hujapoteza fahamu, ulimuona
mtoza ushuru akiingia, kwanini aliingia nyumbani kwako?’ akaulizwa
‘Mtoza ushuru alifika kwangu akinilitea kazi
yangu,zilikuwa nyaraka za gari langu ambazo zilikuwa zinahitajia kukamilishwa,
na ilitakiwa nizione mimi kwanza,na niweke sahihi yangu na baadaye nimalizie
malipo yangu niliyokuwa nadaiwa..’akasema
‘Sasa kwanini mtoza ushuru ageuka na kumuwekea silaha
mhasibu,..?’ akaulizwa
‘Mhasibu hana mahusiano na mtoza ushuru, na siku
alipoleta huo mzigo bado nilikuwa naumwa,na sikuweza kupata hizo pesa zote alizokuwa
akizihitajia huyo mtu, nahisi baada ya kupewa kiasi pungufu, akahisi anataka kudhulumiwa
ndio maana akaamua kutumia vitisho….’akasema mdada.
‘Hebu tuambie,unapopoteza fahamu unaweza kujijua baadaye
kuwa ulifanya nini?’ akaulizwa
‘Hapana siwezi kujua kabisa,mengi nafanya kuambiwa…’akasema
na muongoza mashitaka akasema;
‘Panapokuja mgeni kwako utaratibu wako upoje?’ akaulizwa
‘Mlinzi anakuja kunipa taarifa, na mimi namuambia huyo
mgeni aingie au namuelekeza jinsi gani ya kumuambia....’akasema
‘Siku hiyo ya tukio, alipofika huyo mgeni, uliongea na
mlinzi wako , akikupa taarifa kuwa kuna mgeni?’ akaulizwa
‘Hapana kwa vile nilikuwa naumwa, sikuweza kuongea naye,
nilimuomba mhasibu ambaye alikuwepo kwa muda huo, ili aonane na huyo
mtu....’akasema
‘Kwahiyo kazi yote alifanya mhasibu?’ akaulizwa
‘Ndio...’akasema mdada
‘Kwahiyo mhasibu ndiye aliyeonana na mtoza ushuru baada
ya kuongea na mlinzi?’ akauliza hilo swali tena
‘Ndio...’akasema
‘Na huwezi kujua ni kitu gani waliongea hao watu,
hukuweza kusikia walichokuwa wakiongea?’ akaulizwa
‘Hapana, sikuweza kusikia, nilikuwa nimepumzika chumbani
...’akasema
‘Kwa namna hiyo watu waliokuwepo hapo kwa muda huo ni
mlinzi akiwa getini, na ndani akawa yupo mtoza ushuru na mhasibu?’ akaulizwa
‘Ndio....
‘Kwa sasa nawaachia watetezi wamuhoji shahidi
nitaendelea naye sehemu ya pili…..’akasema muongoza mashitaka na wakili wa
utetezi akasogea hadi pale aliposimama mdada, akamuangalia kwa macho makali,na
kusema;
‘Kama wewe una shetani, ushindwe na hilo shetani lishindwe
na liangamie kwa nguvu za mwenyezi mungu….’akasema na watu wakacheka, na hakimu
akasema;
‘Wakili usilete mchezo mahakamani….’akasema hakimu
‘Ndugu muheshimiwa,mimi nilitaka kuliondoa hilo shetani
nililosikia linamsumbua huyo shahidi, na kuondoa wasiwasi kwa watu, samahani
sana, natumai shetani limeondoka,…’akasema na watu wakacheka,
‘Samahami muheshimiwa hakimu, nataka kumuuliza huyu
shahidi anayesema kuwa yeye hakujua kilichoendelea kipindi chote hadi polisi
walipoingia….’akatulia
‘Huyu mtu anadai alipotewa na akili, na tunaweza kusema
kwa muda huo alikuwa mwendawazimu na aliweza kufanya lolote bila
kujitambua…’wakili muongoza mashitaka akaweka pingamizi kwa kauli ya wakili
mtetezi,na maelezo yake na hakimu akakubaliana napingamizi hilo.
‘Mdada,unasema hali hiyo ikikutokea unakuwa hujitambui,
sawa si sawa?’ akaulizwa
‘Sawa..’akasema mdada
‘Kwahiyo unakuwa huna akili za kibinadamu za kawaida?’
akauliza
‘Mimi sijui kwasababu sijitambui..’akasema mdada
‘Kwahiyo unaweza kufanya mambo kinyume na hali halisi ya
kibinadamu..?’ akaulizwa
‘Mimi sijui kwasababu ninakuwa sijitambui…’akasema mdada
‘Kwahiyo kwa vile hujitambui,kwa vile akili ya
kibinadamu haipo,unakuwa wewe sio binadamu wa kawaida, na unaweza kufanya mambo
ambayo hata mnyama anaweza kufanya, au wale waliotindikiwa na akili wanavyofanya….’akasema
na wakili muendesha mashitaka akaweka pingamizi.
‘Muheshmiwa hakimu, mimi namuuliza shahidi anavyokuwa
kipindi hicho, na hali kama hiyo haina tofauti na wale waliotindikiwa na
ubongo, na kwa majina mengine japo hatuyapendi wakiitwa watu, majina kama
vichaa, au wendawazimu, mimi hapo nina kosa gani?’ akauliza wakili mtetezi.
‘Hebu niambie mdada, hali kama hiyo hukutokea wakati
gani?’ akaulizwa
‘Hali kama hiyo hunitokea mara chache sana...’akasema
mdada
‘Hata kama ni mara chache, ieleze mahakama hali hiyo
hukutokea wakati gani, natumai swali langu lipo wazi...’akasema wakili
‘Ni wakati nimetingwa na msongo mkubwa wa mawazo na
kupandwa na hasira,...’akasema
‘Na ni kwa watu wote wanaoweza kukufanya hali hiyo
itokee?’ akaulizwa
‘Hapana, sio kwa watu wote, mara nyingi ni kwa wanaume,
..na ni kutokana na....’ kabla hajaendelea wakili huyo akasema;
‘Kwahiyo ugomvi wako mkubwa ni kwa wanaume....?’
akaulizwa
‘Nahisi hivyo, kutokana na hayo waliyowahi kunifanyia....’akasema
‘Na mtoza ushuru alikuwa mwanaume,...au sio? ’akasema na
muendesha mashitaka akasema wakili anahitimisha kulazimishia hoja yake...’na
hakimu akakubali pingamizi
‘Wakati mtoza ushuru anaingia na bastola wewe ulikuwa
wapi?’ akaulizwa
‘Nilikuwa nimetoka pale nilipolala na kwenda
chooni...’akasema
‘Na wakati huo akili zako zilikuwa sawa?’ akaulizwa
‘Ndio...’akasema
‘Na ulipomuona mtoza ushuru akili zako zikabadilika...?’akasema
‘Hapana, zilibadilika pale nilipomuona kashika bastola,
na nilipomgonga mkononi, na yeye akaanza kuja juu kupambana na mimi na hapo
hasira zikapanda, hali ikaanza kunibadilikia, na fahamu zikawa sio zangu,
sikujua kilichoendelea....’akasema
‘Umesema hali hiyo ikikutoka unakuwa hujitambui, na
kwahiyo unaweza kufanya lolote bila kujijua au sio?’ akauliza na kabla shahidi
hajajibu akaendelea kusema;
‘Na umesema ulipomuona mtoza ushuru, akiwa na bastola, ukamgonga na bastola ikamtoka,
lakini yeye akaja juu kupambana na wewe, na hasira zikakupanda, ukawa
hujitambui tena, na umesema, hasira zako zinakuwa zaidi kwa wanaume, si ndivyo
ulivyosema
‘Ndio...’akasema
‘Ulimgonga mtoza ushuru mkononi, silaha ikamtoka, na
unasema hapo akili ikawa sio yako, na kawaida ukimdhibiti mtu asiye na silaha
na silaha ikimtoka unachofanya ni kuhakikisha kuwa haipati tena hiyo silaha, au
kuichukua hiyo silaha, na kwa vile wewe ulikuwa huna fahamu za kibinadami na
umeshika hiyo silaha, ...kilichofuatia ni nini...’akawa kama anauliza na wakili
akaweka pingamizi kuwa wakili anahitimisha ...
‘Tuendelee sehemu ya pili....’akasema wakili mtetezi na
wakili muendesha mashitaka akafika, na muda huo vielelezi kadhaa vikaletwa
mezani kuonyesha kuwa sehemu hiyo inayofuata inahitajia vielelezi na moja kati
ya vielelezo hivyo ni ule mfuko ukiwa na mkoba uliokuwa na bastola....na kwa
muda huo nikamuona mpelelezi akisogea na kuteta na muendesha mashitaka.
NB : Mambo yameanza kuiva
WAZO
LA LEO: Utu na ubinadamu ni pamoja na kujali afya zao, sasa
hivi Dar, kuna
msongamano mkubwa wa magari, na foleni zinakuwa ndefu sana na
magari yanasimama kwa muda mrefu zaidi ya msaa manne. Humo ndani ya magari
kunakuwa na wagonjwa, watu wasijiweza, watoto, na watu wamebanana.
Kiafya sio salama mtu kusimama ndani ya daladala lililojaa kwa masaa zaidi ya matatu. Najua foleni kwasasa inatokana na matengenezo ya
barabara, lakini wakati mwingine ni kutokana na misafara ya waheshimiwa,
...ratiba za hao wakubwa zinajulikana , kuwa muda fulani watapita barabara fulani, basi ingelifaa magari
yaambiwe mapema, kuwa kuanzia saa fulani kutapita msafara, kwahiyo magari hayo
yapitishwe njia nyingine mbadala, au kwenye barabara zisizo rasimi, ili kupunguza foleni na
watu kuathirika kiafya....
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment