‘Mdada hebu tuambie baada ya tukio la kuuwawa kwa mtoza
ushuru uligundua nini ndani ya nyumba yako,kulikuwa na mabadiliko yoyote?’
akaulizwa
‘Moja ya dirisha langu lilionekana halipo sawa, kuna mtu
alilinasua na kufyatua vidude vya kuliwezesha kubana na kufunga vyema…’akasema
‘Kwa namna nyingine lilivunjwa …?’akasema wakili
‘Ndio….muheshimiwa’akasema mdada
‘Je dirisha hilo lilikuwa na matatizo kama hayo kabla’
akaulizwa
‘Ndio kabla ya hapo niligundua kuwa halifungii
vyema,tofauti na ilivyokuwa awali, nikalirekebisha mwenyewe, kwa kuvinyosha
vidude vilivyokuwa vimejipinda, …’akasema mdada
‘Kwahiyo dirisha hili sio mara ya kwanza kuvunjwa,
kulazimishwa kufunguliwa?’ akauliza
‘Ndio..’akasema mdada
‘Uliwahi kumuuliza mlinzi wako kuhusu hilo tukio,maana
kama ni mtu alifanya hivyo, ni lazima aliingia kupitia getini, …?’ akaulizwa
‘Niliwahi kumuuliza na yeye akasema hawezi kujua, na
hakuna mtu aliyewahi kuingia, akasema huenda ni tatizo lilijitokeza wakati wa
kufunga kwa nguvu, lakini mimi niliingiwa na wasiwasi kwani hayo madirisha
wakati wa kufunga hayatumii nguvu, ila likishajifunga, ukiwa nje huwezi
kufungua mpaka utumie pisipisi kukwanyua na hapo unaharibu uimara wake
…’akasema mdada
‘Na ulivyoona ndivyo ilivyofanyika kuwa mtu alitumia
pisipisi kulazimisha kulifungua kutoka nje?’ akaulizwa
‘Ndio, hata ukiangalia utaona michirizi ya kitu kama
pisipisi imeacha alama, ipo dhahiri kabisa...’akasema
‘Hiyo michirizi uliigundua lini?’akaulizwa
‘Kwa mara ya kwanza sikutulia maanani sana, ila hii
safari ya pili ilinifanya nichunguze kwa makini ndio nikaona hiyo
michirizi...’akasema
‘Je ulipooa hivyo kwa hii mara ya pili na kugundua pia
dirisha halifungi, ulifanya nini?’ akaulizwa
‘Nilipoona dirisha halifungi, nikaanza kuingiwa na
wasiwasi, nikaanza uchunguza mle ndani, kama kuna kitu kimeibiwa, ni wazi
ikitokea kitu kama hicho hisia za kwanza ni kuwa umeibiwa. Nilifanya utafiti
kujua kama kuna kitu kimeibiwa, na nikagundua kuwa moja ya kabati langu
ninapoweka vitu vyangu muhimu lilikuwa limevunjwa, mara nyingi silifungui hilo
kabati…’akasema mdada
‘Ulifanya nini baada ya hapo?’akaulizwa
‘Nilifanya uchunguzi wa kitaalamu zaidi,mimi nina vifaa
vya kuchunguza alama za vidole,kwahiyo nilijaribu kuangalia kama kuna alama
zozote za vidole zilibakia hapo dirishani…’akasema
‘Uligundua alama gani au za nani?’akauliza na wakili
mtetezi akaweka pingamizi lakini hakimu akasema swali hilo lijibiwe
‘Niligundua alama za vidole ni za mlinzi wangu…’akasema
mdada
‘Mlinzi wako ndio huyo mshitakiwa namba moja kwenye kesi
hii?’ akaulizwa
‘Ndio muheshimiwa…’akasema mdada na mimi nilijaribu
kumuangalia huyo mlinzi,na nilimuona kama akitikisha kichwa kusikitika.
‘Je wewe unamuamini sana mlinzi wako?’ akaulizwa
‘Kwakweli namuamini sana mlinzi wangu, na hata baada ya
kugundua hivyo, bado moyoni nilihisi huenda ni katika kuhakikisha kuwa dirisha
limefungwa vyema, ndio maana alama hizo zilibakia, yeye kama mlinzi anaweza
kufanya hivyo kuhakiki kama madirisha yote yamefungwa vyema...’akasema mdada
Msimamizi wa mashitaka hayo akasogea hadi pale pilipowea
vielelezo, na kutoa kielelezo kimoja wapo, na kumuuliza mdada kama anakitambua
na mdada akasema ni alama za vidole alizozichukua yeye tarehe imejionyesha na
saa, kwani wakati unafanya hivyo vipimo, kila kitu kinajiandika, muda, na
tareha ya tukio la kufanya uchunguzi huo.
‘Nawakilisha alama za vidolezilichokuliwa na mdada
zikionekana wazi kwenye dirisha la mdada, na alama ya dole gumba lilipatikana
kwenye mshikio wa kabati la mdada lililovunjwa,…..’akasema wakili na wakili
mtetezi akatoa pingamizi na kusema;
‘Hvyo vielelezo vilichukuliwa na mtu ambaye hatuwezi
kumkubalia, maana yeye sio ofisa usalama au mtaalamu wa kazi hiyo
aliyetambulikana, na alifanya hivyo kwa utashi wake, na sio kwa utashi wa
polisi waliopewa jukumu hilo….’akasema na muendesha mashitaka akasema;
‘Hajalishi ushahidi umechukuliwa na nani,kama ushahidi
huo unakubalika kitaalamu, kutegemeana na muda, mahali na ukiangalia chombo cha
kunasia hizo alama za vidole ni cha kitaalamu zaidi kinaonyesha hadi muda wa
alama hizo za vidole kuwepo hapo,…na upo sahihi, mimi sioni kwanini uweke
pingamizi hapo, mimi nawakilisha kama vidhibiti vya kimahakama…’akasema
muendesha mashitaka na hapo kukatokea mlolongo wa ubishi hadi hakimu akaingilia
kati na kusema
‘Ushahidi huo utapokelewa na kama utakuwa na ushawishi
zaidi ,hatutasita kuutumia, na kama hauna vigezo au ushawishi mwingine
utatupiwa mbali, hiyo sio kazi yenu mawakili, tuendelee…’akasema hakimu.
‘Mdada,hebu tuambie wewe unamiliki bastola?’ akaulizwa
na mdada akainua uso bila kusita akasema.
‘Ndio muheshimiwa….lakini katika vitu nilivyoona kupotea
siku hiyo ni pamoja na bastola yangu..’akasema na mimi nikashangaa kauli yam
dada.
‘Ulipogundua hivyo ulichukua hatua gani?’ akaulizwa
‘Kwanza nilifanya uchunguzi wangu kama nilivyofanya
kwenye kabati langu,na katika kuangalia alama za vidole niligundua alama ya
dole gumba la mlinzi wangu, ….’akasema mdada na hapo hata mimi nilianza kumshuku mlinzi wa mdada
kuwa anahusika sana na hayo mauaji.
‘Ndugu muheshimiwa hakimu,nawakilisha ushahidi wa
bastola ya mdada iliyokuja kugundulikana baadaye,ambayo ilichukuliwa kwenye
kabati la mdada…’akasema muendesha mashitaka
‘Je kuna kitu gani zaidi uligundua kupotea?’akaulizwa
‘Kulikuwa na nyaraka za siri ambazo nilipewa na marehemu
nimuhifadhie…’akasema mdada
‘Kwanini marehemu alikupa wewe nyaraka kama hizo
uhifadhi wewe, kwani wewe ni mfanyakazi wa idara hiyo?’ akauliza
‘Yeye mwenyewe aliniambia kuwa hizo ni nyaraka muhimu
sana, na anaogopa kuwa zinaweza kupotea, na ni ushaidi wake wa mambo yake, mimi
sikutaka kumkatilia, nikazichukua, na alisema pia hakuna sehemu anayoiamini
kwasasa akiipata atakuja kuzichukua ,kwahiyo mimi sikuona sababu ya kumkatalia,
ilimradi ni kwa muda….’akasema mdada na wakili huyo akawa amemuangalia hakimu,
ambaye alikuwa akindika jambo, na alipogeuka kumuangalia shahidi wake, akasema;
‘Endelea…kutoa maelezo...’
‘Na nilikuja kugundua kuwa hizo nyaraka ni moya ya vitu
vilivyokosekana kwenye kabati
langu….’akasema mdada.
‘Ina maana viliibiwa na huyo aliyeiba ndio huyo huyo
aliyevunja dirisha, na kuvunja kabati, na uiba hivyo vitu ikiwemo bastola,...na
huenda bastola hiyo ilitumika kwenye uhalifu ikiwemo mauji’akasema wakili
Wakili wa utetezi akasimama na kutoa pingamizi akasema;
‘Ndugu muheshimiwa hakimu,kesi hii ilipoanza tulisikia
kuwa bastola iliyotumika kumuua mtoza ushuri ni bastola yake mwenyewe
aliyoingia nayo,hii bastola nyingine haina umuhimu kwenye hii kesi...na ni wapi
imeonyesha kuwa ilitumika kwenye
uhalfu,...’akasema wakili huyo na hakimu akakubali pingamizi hilo.
‘Naishia hapa kwa sehemu hii, wakili mtetezi unaweza
kuendelea...’akasema wakili muendesha mashitaka
*********
Wakili mtetezi hakuacha mbwembwe zake, akamsogelea mdada
na kuonyesha alama za imani yake na kusema;
‘Kama kuna shetani na dalili zake zishindwe, niweze
kuitafuta haki, shetani ushindwe kabisa.....’watu wakacheka, na yeye akiogopa
hakimu atamkemea akasema
‘Katika imani za dini kabla hujaanza jambo ni vyema
kujikinga na mabaya ikiwemo imani za mashetani, sio kwamba nafanya haya kwa
kuwafurahisha watu....’akasema
‘Uliza maswali wakili, usipoteze muda....’akasema hakimu
‘Mdada, wewe unasema ulitumia utaalamu kuchunguza alama
za vidole, huo utaalamu umeupatia wapi?’ akauliza, na wakili muendesha
mashitaka akaweka pingamizi kuwa swali hilo halina msingi kwani hayo ni mambo binafsi
hayafungamani na hiyo kesi...
‘Nimeuliza hivi kwasababu vielelezo alivyovichukua
vimewakilishwa kama ushahidi, tutaamini vipi kuwa huyu mtu hakugushi hivyo
vielelezo, au kwenda kwa mtaalamu akavitengeneza...’akasema na hakimu aktulia
kidogo, akasema hilo swali lijibiwe
‘Nimewahi kuhudhuria mafunzo ya vitu kama hivyo katika
vyuo vinavyotambulikana, na kama unahitaji ushahidi ninaweza kuleta vyeti
vyangu ,....’akasema
‘Kwahiyo kumbe wewe ni mtaalamu wa kuchunguza alama za
vidole, kwanini ulichukua mafunzo hayo..?’ akauliza na wakili msimamizi akaweka
pingamizi, lakini hakimu akasema lijibiwe, na mimi hapo nikaona kuna kitu
hakimu anakitafuta.
‘Ni katika kuendeleza kipaji changu, mimi huwa napenda
sana kuchunguza mambo kitaalamu zaidi..’akasema
‘Ulisema unapotokewa na ile hali, mmh, ya kibinadamu na
ukatawalia na shetani, shetani ushindwe kabisa...’akasema kunyosha mkono kwa
mdada, na watu wakacheka
‘Hebu niambie sio kwasababu uliogopa kuwa ulijuwa kuwa
wewe ndiye uliyefanya hayo mauaji wakati umepoteza akili za kibanadamu ndio
ukaanza kufanya huo uchunguzi ili uweze kumsingizia mtu mwingine...na ukijua
kuwa mlinzi anaweza akaacha alama za vidole kutokana na kazi yake, ukaona huyo ndiye
anayefaa kusingiziwa....’akasema na wakili muendesha mashitaka akaweka
pingamizi na hakimu akakubali hilo pingamizi.
‘Naomba nimjibu huyu muheshimiwa hilo swali kuwa mimi
nina matatizo na hayo matatizo yanatambulikana kitaalamu, na nina dakitari
bingwa anaweza kulithibitisha hilo, siwezi kusingizia kitu kama hicho, na ni
kitu kinachonisumbua sana, usifikiri mimi naifurahia hiyo hali...’akasema mdada
kwa sauti ya kuonyesha uchungu, lakini hakutaka kuonyesha unyonge.
‘Sijasema umesingizia huo ugonjwa, nimesema ugonjwa huo
upo, na kweli unao na unakubalika sawa kutokana na dakitari wako bingwa,...na
kama ulivyosema ugonjwa huo ukikutokea unakutoa kabisa katika hali ya kawaida
ya kibinadamu si ndivyo ulivyosema...’akawa kama nauliza na mdada akawa
anamuangalia tu.
‘Ndivyo ulivyosema wewe mwenyewe kuwa hali hiyo
ikikuingia unaweza kufanya jambo usilikumbuke, na unaweza hata kuua, kama
ulivyomua mtoza ushuru, usikumbuke kabisa si ndio hivyo....?’akasema wakili
huyo na wakili muendesha mashitaka akaweka pingamizi kuwa wakili huyo anazidi
kuliongelea jambo ambalo limeshawekewa pingamizi, na kufanya hivyo anataka
kuvuruga utaratibu...’
Wakili mtetezi akasema huku akimuangalia hakimu;
‘Mimi nilikuwa namjibu shahidi wake, kumfafanulia kile alichokisema,
sikuwa nauliza swali, sijavuruga utaratibu hapo...’akasema na alipomuona hakimu
yupo imiya akamgeukia mdada, huku akisema;
‘Unasema kati ya vitu vilivyoibiwa ni pamoja na nyaraka
za siri, ambazo ulipewa na marehemu, sijui ni siri kinamna gani, ....lakini kuna
tetesi kuwa wewe na marehemu mlikuwa marafiki kabla, bila kujali huyo ni mume
wa mtu,...’akasema na wakili muendesha mashitaka akatoa pingamizi, lakini
wakili huyu akaendelea kuongea
‘Urafiki wenu baadaye ukaanza kulega lega, kama kama
kawaida yak oleo huyu kesh yule hayo yapo wazi huna haja ya kuyakubali,
nazungumza kwani mimi ni mwanajami na namfahamu mdada....’akasema na wakili
muendesha mashitaka akaweka pingamzi kuwa wakili huyo anaingilia mambo binafsi,
ambayo hayana msingi kwenye hiyo kesi, na hakimu akamuonya huyu wakili, na
wakili huyo akasema
‘Samhani muheshimiwa hakimu, lakini mimi nilikua
najaribu kuelezea hali halisi iliyosababisha hayo yote, hayo yaliyotokea hapo
yana historia pana...’akasema na bila kujali, akaendelea kuongea
‘Kutokana na kukorofishana kwenu, kukosana kwenu, wewe
hukutaka kumrejeshea marehemu nyaraka zake ndio maana akaja juu, siku hiyo mauti
yalipomkuta, alishasema basi liwalo na liwe, ndio maana alikuja na bastola...’akasema
wakili huyo na wakili muendesha mashitaka akasema
‘Muheshimiwa hakimu, wakili mtetezi anatoa maelezo,
badala ya kuuliza maswali, je huo ndio utaratibu na wakili akamuonya tena huyo
wakili na wakili bila kujali onyo hilo akasema
‘Mdada, sema ukweli, hayo niliyozungumza nakusingizia
...?’akasema kama anauliza na wakili muendesha mashitaka akaweka pingamizi kuwa
wakili anatoa maelezo yasiyo na msingi wa hoja na ushahidi, na anamshinikiza
shahidi kujibu maelezo aliyoyatoa mwenyewe huyo wakili na hakimi akakubali hilo
pingamizi, na kusema;
‘Wakili mtetezi, nakuonya tena, fuata utaratibu wa
kiuwakili,....’akasema hakimu na wakili huyo akasema;
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, haya ninayoeleza naweza kuja
kuyatolea ushahid kama yakihitajika, lakini kwa hivi sasa ninachotaka mahakama
yako tukufu ifahamu ni kuhusu tabia ya
huyu mdada, yeye anachofanya hapa ni kujaribu kuficha ukweli, kwa vile marehemu
sasa hivi hayupo hapa, ndio maana anasema kuwa
alichokuwa amekifuata marehemu ni nyaraka za gari lake, kitu ambacho sio
kweli, ...’akasema na wakili muendesha mashitaka akasema;
‘Thibitisha kauli yako kwa ushahidi na vielelezo, sio
kwa hisia zako...’ wakili muendesha
mashitaka akasema
‘Ninaweza kuthibitisha hilo kwa majibu kutoka kwa huyu shahidi
yako mwenyewe, mpe nafasi ajibu...’akasema na hakimu akaingilia kati na
kumwambia wakili mtetezi aulize maswali na sio kutoa maelezo yake binafasi.
‘Unadai kuwa nyaraka za siri ulizokuwa nazo zilikuwa
kati ya vitu vilivyoonekana kutoweka kwenye kabati lako , na wakati huo umedai
kuwa marehemu alikuwa kuchukua nyaraka za gari lako, kwanini aje nyumbani
kwako, wakati kazi kama hiyo ni ya kiofisi...?’ akauliza na wakili muendesha
mashitaka akaweka pingamzi, na hakimu akalikubali hilo pingamizi.
‘Ndugu muhehimiwa hakimu, nahitaji mdada ayajibu maswali
yangu ili kuthibitisha kuwa marehemu hakuwa amefuata nyaraka za gari, marehemu
alikwua amefuata hizo nyaraka za siri, na hizo nyaraka za siri, mdada
alishaziondoa hapo, na alichofanya yeye ni kuvunja hilo kabati, ili ije
ionekane kuwa mtu mwingine aliingia akafanya hivyo...’akasema wakili na wakili
muendesha mashitaka akaweka pingamzi kuwa wakili huyo anatoa maelezo yake
anavyohisi yeye, hayana msingi na hitimisho la hoja.
‘Mdada kwanini unamiliki silaha?’ akauliza swali
‘Kwasababu raia yoyote anaweza kufanya hivyo,..na nina
kibali cha kufanya hivyo...’akasema
‘Kwahiyo wewe ni mtaalamu wa kutumia silaha...?’
akaulizwa
‘Ndio nafahamu kutumia silaha, nisingeliichukua kama
pambo..’akasema mdada
‘Na hata
ukipotewa na fahamu zako unaweza kuitumia hiyo silaha..’akasema na mdada
akacheka na kusema
‘Nikipotewa na fahamu sijui kinachoendelea, ...na
nimeshakuambia ili ujue vyema kuhusu tatizo langu dakitari wangu yupo anaweza
kuja kutoa maelezo, ya kuwa mimi nikiwa katika hiyo hali sihitaji
silaha,...’akasema
‘Utajuaje kuwa huhitaji silaha, wakati
hujitambui...huoni kuwa unaidanganya mahakama, wewe ulipopotewa na fahamu ya
kibinadamu uliweza kufanya lolote ikiwemo kuua,...’akasema wakili huyu akiongea
kwa haraka haraka, bila kujali pingamizi la hakimu.
‘Nna hutaki kukubali tu kuwa wewe ndiye uliyemuua mtoza
ushuru, kwasababu ulikuwa na hasira naye,na yeye alikuwa mwanaume, na yeye
mlishakorofishana kwenye mambo yenu, na kwa vile alikuja kufuatilia hizo
nyaraka ambazo wewe ulizichukua kwa lengo la kuzitumia kum-black maili, ili akutolee gari lako bure...na hiyo ndio tabia
yako, ya kuwarubuni watu, kwa kutoa mapicha mabaya, na baadaye kuwadai pesa ili
upate unachokihitajia,..naweza kutoa ushahidi wa hili, ninao ushahidi...nasema
ninao ushahidi...’akawa anasema kwa jaziba
‘Sio kweli....’akasema mdada kwa sauti na ilikuwa sauti
nzito kidogo, mimi pale nilipokuwa nimekaa nikaanza kusimama, na wakati huo wakili
muendesha mashitaka aliuwa akiweka pingamizi lakini wakili huyu akaendelea
kuongea, na akimu akawa anamuangalia kwa mshangao....
‘Hata huyo mhasibu umemtumia kwa njia hiyo hiyo,
ulimchukua picha mbaya ili aweze kuingia kwenye anga zako, kubali hayo ili haki
itendeke usitake, kumsingizia mlinzi wako kwa kosa ambalo hakulifanya, kubali
kuwa wewe ndiye uliyeua...kubali ili damu uliyoimwanga isifukiwe hivi hivi,
kubali haki itendeke, kubali kubali...’akaendelea kuongea kama wahubiri
wanavyofanya bila kujali pingamizi huku akimnyoshea mdada mkono juu chini...
‘Stop...’akasema mdada kwa sauti nzito, sauti iliyofanya
chumba kizima cha mahakama kuwa kimiya, na wakili mtetezi naye akatulia ghafla
kumuangalia mdada, na walipokutanisha macho yao, wakili huyo akaanza kurudi
kinyume nyume, na nilipomuangalia mdada nikamuona akianza kutikiswa, na mara
akaanza kutoa mngurumo kama wa simba....
NB: Jamni tuendelee kidogo hapo?,.....mmm samahani
kidole kinauma...
WAZO
LA LEO: Kila mtu ana mapungufu yake na wengine wanajijua kuwa
wana mapungufu hayo , na mbora wa hayo ni yule anayekubali na kutubu, lakini
kuna wengine wanajijua, lakini hawataki kukubali kuwa wana mapungufu hayo. Hawa
ni wale wenye tabia za uwongo, wanafiki, mafisadi.
Kuna watu wana
tabia za uwongo na uzushi kwao ni
starehe, na hawajali athari za uzushi huo kwa wengine. Uwongo, uzushi,
propaganda potofu,utesi ni tabia za hawa
watu. Na watu hao, ni wanafiki kwani hawaaminiki, wanapenda kusema uwongo,
kuwazulia wenzao mambo wasiyoyafanya, ili tu kukidhi matakwa yao,na watu hao
hawatekelezi amana walizokabidhiwa hasa wakipewa madaraka.
Jamani mkiwa na tabia hii mukajijua ni bora kutubu,
kwani ni dhambi , na unapowafanyia wengine wanaumia, kama ungeliumia wewe
ukifanyiwa hivyo hivyo, huo ni ufisadi, huo ni unafiki, tuuache.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment