Kwanza mdada aliniangalia kwa makini, kama ana
wasiwasi na mimi, halafu akageuka na kuanza kutembea ule mwendo wa kiaskari
ujulikanao kama mwendo-pole, alitembea hivyo hadi kwenye kabati kubwa
lililokuwa hapo varandani
Akatoa
ufunguo na kufungua hilo kabati, akawa anavuta kitu, na mara akatoa mfuko
mkubwa wa nailoni
Aligeuka
na huku ameushikilia ule mfuko wenye kitu ndani yake akanisogelea na kuja hadi
pale nilipokaa, akauinua huo ule mfuko, na nilipoangalia vyema ndani ya huo
mfuko nikaona mkoba,(briefcase), lakini ni hizi briefcase za kawaida tu, na akili yangu kwa haraka
ikakumbuka kuuona huko mkoba mahali, ....
‘Ule
mkoba (briefcase),
niliiona wapi vile...ooh, ndio...’nikawa nasema kimoyo moyo, na mdada alipoinua
juu ule mfuko wa nailoni, ili nione kilichope ndani yake, alisema;
‘Huu
mfuko nimeuchukua chumbani kwako,…..kabla polisi hawajafika, mimi nilikuwepo
chumbani kwako....’akasema
‘Ulifika
saa ngapi?’ nikamuuliza
‘Nilifika
muda ule ule uliofika wewe...’akasema
‘Hao
polisi, walikuwa wakivitafuta hivi vitu vilivyopo humu ndani…’akasema mdada
nilibakia nimeduwaa huku nikimkodelea macho mdada, kwa kutoamini maneno yake
kuwa alifika muda nilipofika mimi, na kwanini sikumuona, baadaye nikasema;
‘Haiwezekani….’nikasema
sasa nikiuangalia ule mfuko wa plastiki na ndani yake ule moba ulionekana
dhahiri, na sikuwa na shaka, utakuwa ni ule mkoba aliokuwa nao mmoja wa wale
jamaa wawili waliofika hotelini kutaka kuweka kitu ofisini kwangu...
Tuendelee
na kisa chetu
**********
`Unasema haiwezekani,hahaha masikini mhasibu, mimi sio
mwenzako....’akasema mdada akiinua ule mfuko , halafu akauweka ule mfuko sakafuni
mbele yangu akasema;
‘Kama haiwezekani, hivi vitu nimevipata wapi, na wewe
jiulize kwanini polisi hawakuvipata vitu walivyokuwa wakivitafuta wakati wewe
mwenyewe uliona wale jamaa wakiviweka au wakitaka kuviweka kwenye chumba
chako....’ akasema sasa alikuaj kukaa karibu yangu, na mimi nilibakia kimiya
nikiendelea kuangalia ule mfuko uliokuwa umewekwa huo mkoba.
‘Wewe niulize ilikuwaje....’akasema mdada na mimi nikahema,
na nikasogea nyuma na kukaa vyema kwenye sofa nikiwa kama naogopa kabisa
kukaribia huo mfuko na mdada akaendelea kusema;
‘Mimi nilifika
kwako hotelini pale wakati unaoga, nilikuwa nyuma yako, sikuwa na shaka ya
kujificha sana, nikijua utaniona ukigeuka, lakini haikuwa hivyo......ulipoingia
ndani, ukafunga mlango. Hukufunga kwa ndani, niliponyonga kitasa mlango
ukafunguka, nikaingia ndani, na ili kujua wapi upo, nikaipiga simu yako, nikaisikia ikiita
chumbani kwako,nikaingia na kumbe ulikuwa bafuni....’akasema.
‘Unakumbuka wakati unaoga,simu yako iliita ,….mimi ndiye
niliyepiga, kujua utachukua hatua gani, na
hakutoka haraka bafuni, ....mimi nikachukua nafasi hiyo kujificha sehemu ambayo
hata ukirudi usingeliniona kirahisi, nilitaka kuona unataka kufanya nini.
‘Cha ajabu, kukuthibitishia kuwa wewe haupo makini, hata
ulipotoka bafuni hukutaka hata kukagua kagua chumba chako, ulichokimbilia
kuangalia ni simu yako,...’akasema
‘Na nilikuona ukiwa na mwazo sana, labda ulikuwa ukiwaza
jinsi gani ya kuongea na baba mkwe wako, ...ningeweza kukuambia usihangaike
kwenda huko, lakini akili yangu ilinituma nisikushitue....’akasema
‘Wakati nataka kujitokea ili unione, wewe ukawa unavaa kwa haraka, nikaona nikupe muda, nikijua
utageuka kuangalia upande ule nilipokuwa nimejificha, simu yangu nilikuwa
nimezuia sauti kusikika, ila nilihisi kuna ujumbe umeingia, nikawa nausoma na
wewe ukawa umeshatoka nje ya chumba chako...’akasema
‘Wewe ni mtu wa ajabu sana, kiukweli mimi ukiingia ndani
na kujificha, kuna hali inanionya, nahisi kitu mwilini, nywele sinasisimuka
lakini wewe, mmmh, inatisha.Lakini mhasibu mimi ninakupa ushauri wa bure, siku
zote ukifika sehemu hata kama ni nyumbani kwako, hebu jaribu kuwa makini
sana….utakuja kuwawa kirahisi tu…’akasema
‘Mpaka sasa siamini….ina maana muda wote ulikuwa mle
ndani?’nikauliza kwa mshangao.
‘Ulipotoka hapo chumbani kwako ulionekana kuwa na
mashaka,nikajua utaweza kunigundua, lakini hukuwa makini kuangalia tena ndani
hukutaka kuitumia vyema hisia yako ya sita, hisia inayokuashiria jambo, ni
hisia ambayo ukiitumia vyema unaweza kuhisi kama kuna hatari karibu. Ulipotoka tu nikajiweka sawa na mimi kukufuata
ili nikuambie kuwa hutaweza kuongea tena na baba mkwe wako umeshachelewa,
lakini nikarudi nyuma haraka baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa wangu…’akatulia
kidogo
‘Nikiwa hapo nikapata taarifa kwa ujumbe wa maneno kuwa kuna
hao jamaa wawili wamekuja huku juu, na wamebeba mkoba, tofauti na ile mikoba
yao, ya kikubwa,na watu wangu wakautilia mashaka, wakawa wanawasilia na askari waliopo
kwenye kundi langu....’akasema
‘Ina maana una kundi lako lenye maaskari?’ nikamuuliza na
yeye akanitupia jicho, na hakujali swali langu akaendelea kusema;
‘Mtu wetu upande wa polisi akasema kuna taarifa kuwa
kuna vitu muhimu vilivyokuwa vikitafutwa na polisi kama ushahidi vimebainika
kuwa vipo ofisini kwako, kwahiyo kuna watu wanaandaliwa kuja huko....’akatulia
‘Hapo machale yakanicheza, nikaona kwa ahli ilivyo ni
bora nisikutane nawe wanza, nikawaambia watu walifuatilie hilo jambo, na wanipe
taarifa haraka iwezekanavyo...mimi nina vijana wanaojua kazi, ukiwaambai jambo,
wanajua umuhimu wake, wakanipa taarifa kuwa hao jamaa wawili walionekana kuja
huku juu, walikuwa na huo ushaidi, inaonekana wanataka kuuweka huko ofisini....
Vijana wangu wakawasiliana na mtu wetu aliyekuwa upande
wa utawala wanakofanya kazi hao watu, tukapata taarifa kuwa kuna mpango wa
kuhakikisha kuwa wewe unakamatwa, na hicho cheo kinahtajika kwa mtu mwingine, kwahiyo
wewe unaandaliwa uonekane kuwa ndiwe uliyemuua, mtoza ushuru, na ushahidi
kamili umeshatayarishwa....’akasema
‘Niliposikia hivyo nikajiandaa kufanya lolote, maana
ukikamatwa wewe, na kwa jinsi ninavyokufahamu unaweza kuropoka ovyo,..na pili
nilitaka kujua huo ushaidi ni kitu gani, nikataka kukukimbilia kukuonya, lakini nilikuwa
nimehachelewa,nikavuta subira, baadaye nikatoka kuangalia ni nini kinachoendelea
na wakati natoka nikakuona ukikimbilia kwenda chini...nikawasiliana na watu
wangu wakufuatilie..’akatulia
Mimi nikahisi kuna jambo unalikimbia, nikasubiri,
...nikaona sehemu nzuri ya kusubiria ni chumbani kwako, huku nikiwasiliana na
vijana wangu, nikiwa nawaza nifanye nini, mara nikasikia mtu akifungua mlango
wa chumbani kwako,kwa haraka nikajificha
pembeni mwa kabati la nguo. Nilijua ni wewe umerudi,...kumbe ni wao.
Nilifanya vyema kujificha humo chumbani kwako, kwani
walipoingia humo, hao jamaa, wakiwa na huo mkoba, waliangaza huku na kule,
sikujua kwa muda huo wanatafuta nini, na mmoja akasema;
‘Tuuweke chini ya kitanda, ionekane alikuwa
anauficha....’akasema mmojawapo Na wakakubaliana hivyo,wakaelekea chumbani
kwako, na kuuweka huko huo mkoba chini ya kitanda, na kwa haraka wakatoka mbio.
Na niliwasikia wakisema polisi wanakuja, na lengo lao litakamilika walipotoka
mimi kwa haraka,nikawasiliana na watu wangu wakanipa habari ya kinachoendelea.
Nikawaambia wanilinde,kwani nilihitajia muda ili niweze
kuuchukua huo mzigo, nikaangaza huku na kule na bahati nzuri, nikaona huo mfuko
wa plastiki,na sikupoteza muda nikainua godoro na kuuona huo mkoba nikauweka
ndani ya huu mfuko, nikiwa na tahadhari zote nisiuguse kitu bila kinga ya
mkononi, nikauweka huo mkoba kwenye mfuko na nailoni, nikatoka nao.
Sikutaka kutoka na kuteremka chini na huo mzigo kwa muda huo, kwani nilijua ningelionekana, japokuwa
vijana wangu walikuwa chini wakifuatilia, na ningeweza kuwaelekeza nikajua wapi
pa kutokea, lakini nilichofanya kwa muda huo ni kutoka kwenye chumba chako na
kuingia chumba cha jirani....’akasema
‘Chumba cha jirani cha nani?’ nikauliza na moyoni
nilihisi kitu kama wivu, sijui ni kwanini na mdada akatabasamu na kuangalia
pembeni halafu akasema;
‘Kuna chumba nilikichukua karibuni kwa kazi zangu…’akasema
na mimi nikamuangalia mdada bila kummaliza na yeye akaendelea na maelezo yake
kwa kusema;
‘Nilipofika kwenye hicho chumba nikasubiri, vijana wangu
wakiwa wananipa kila kinachoendelea, na polisi walipopanda juu, wakielekea
ofisini kwako, nilikuwa nafahamu. Ila sikujua kwa jinsi gani walifahamu kuwa
huo mzigo unaweza kuwa kwako, hii inaonyesha kuwa kuna mpango uliopangwa na hao
jamaa wawili na hao polisi,....’ akasema
‘Baadaye wakaja chumbani kwako, nafikiri walikuwa
wameshaelekezwa wapi wakakague, hapo nilisubiri hadii polisi walipomaliza msako
wao,na walipokosa hicho walichokuwa wakikitafuta walitoka nje, na wakawa wanapigiana
simu na wenzao, kwa muda huo nilikuwa nimesimama mlangoni nikiwa wachungulia
kwenye upenyo wa mlango.
‘Nilisikia wakisema; twendeni, hakuna kitu hapa..muda wa
zoezi hili umekwisha...naona zoezi hilo lilikuwa na muda maalumu, wakaondoka na
kurudi huko walipotoka,na mimi nikarudi kwenye hicho chumba changu na kitu
nilichofanya ni kukagua ni kitu gani kipo humo ndan, nikimaliza niurudishe huo
mzigo hapo nilipouchukua..’akasema
‘Niliufungua huo mkoba na nilifanya zoezi hilo kwa
haraka na kitu kilichonishutka sana, ni kuona humo ndani kuna bastola, na zile
nyaraka zilizoluwa zikitafutwa na nyaraka nyingine nilizokuwa nazo mimi ambazo
ndizo marehemu alikuwa akizitafuta...’akatulia akionyesha hisia ya mshangao
usoni.
‘Kulikuwa na bastola, oh, hiyo bastola ilikuwa ya nani?’ nikauliza na yeye akaangalia ule
mkoba pale chini, akausogelea na akiwa amevalia kinga mkononi mwake, akautoa
ule mkoba, na kuufungua na dani yake kulionekana bastola, mimi nilihisi mwili
ukiisha nguvu.
‘Mungu wangu, ina maana walitaka kunibambikia kesi ya
mauaji, mimi sijawahi kumilii bastola, hiyo bastola ni ya nani, na kwanini
watake kuniwekea mimi....?’ nikawa nauliza maswali mengi, na mdada akawa
anaufunga ule mkoba na kuurudisha kwenye ule mfuko wa nailoni akaubeba na
kuuweka kabatini kwake na kulifunga lile kabati, akasema;
Hiyo bastola ni ya kwangu....’akasema na kuniangalia
machoni, na mimi nikabakia mdomo wazi.
NB: Mambo hayo...nawamegea tu kidogo, kutokana na muda,
na diary yangu inataka kutoa tukio la wiki lilitokea karibuni huko maeneo
fulani.
WAZO
LA LEO: Ubinadamu sasa umekwisha, wiki hii kulitokea kisanga
huko eneo la Kipunguni Moshi Bar. Ni tukio la namna yake, la kuokota mamilioni
kadhaa ya pesa,zilizodondoshwa na gari moja likiwa kwenye shughuli za
kibiashara. Nahisi walidondisha kwa bahati mbaya, na sijui watakuja kusema nini
kwa muajiri wao.
‘Tuliliona lile gari, likgeuza baada ya kumaliza kazi
waliyokuwa wakifanya, na wakati linageza tukaona mfuko ukidondoka toka kwenye
hilo gari, na kwa muda huo hakuna aliyehisi kuwa ule mfuko una pesa, na mara likapita
gari jingine na kuukanyaga ule mfuko, ukapasuka....
Pale karibu yake klikuwa na mtoto anacheza, akauona ule
mfuko, na sisi tuliokuwa mbali tukaona jinsi gani yule mtoto alivyoshangaa, kashika
mdomo na mkono kama aliyeona kitu cha kutisha au cha ajabu, na alipouliza kaona
nini akisema;
‘Pesa....’ na hapo wote tuliokuwepo pale macho yetu
yakafunguka kuangalia ule mfuko uliokuwa barabarani ukiwa sasa umepasuka, na
rangi nyeundu za pesa zikanasa macho yetu,..jamani pesa ni shetani...
Kila mwenye shughuli yake akaacha, na mioyo yetu ikaanza
kupiga, na kila mmoja akifirikia jinsi ya kuruka pale tulipokuwa hadi pale penye
hizo pesa. Hakuna aliyefikiria jinsi gani ya kumpata mwenye lile gari, ili
azipate dhamana zake.
Kwa vile pale ni barabarani, wanapita watu wengi, na
muda ule kulikuwa na vijana wanapita wakikimbilia maeneo ya Moshi Bar, kwenye
mishemishe zao, na wao wakaziona zile pesa, na sisi tuliokuwa mbali,tulishaanza
kujongea pale, na kulaani kwanini hatukufanya haraka, na mmoja wetu nafikiri ni
yule mzazi wa yule mtoto akawa anamuita yule mtoto aziokote zile pesa haraka,
akachelewa, mmoja wa wale vijana wapiga debe, akaziwahi...
Purukushani zikaanza hapo, kwanza kwa wao wenyewe kwa
wenyewe, hakuna ati yao aliyeweza hata kuuliza hizi pesa ni za nani, wao
walichofikiria ni kuzichukua hizp pesa na kukimbi nazo.
‘Ni zangu, nimeziona mimi...’ waaanza kugombana wao
wenyewe kwa wenyewe, na yule aliyeziwahi mkononi, akatoa kiasi cha pesa na
kuwapa wenzake, wenzake wakasema;
‘Hapana sisi tunataka hizo pesa tugawane sawa kwa sawa,
huwezi kutupa kiasi hicho kidogo,..hali ile litufanya na sisi tuliokuwa mbali
tukimbilie pale, na yule kijana, ni hawa wapiga debe, alipoona hivyo akaanza
kutimua mbio na zile pesa..
Watu tukaanza kumkimbiza, utafikiri mnakimbiza mwizi,
watu wakazidi kuongezeka, kila aliyepata taarifa hiyo akawa anafukuzia huko, na
kila aliyemkaribia huyo mpiga debe, alipewa kiasi, akikipokea anaona hakitoshi,
anaendelea kumfukuza huyo jamaaa..jamaa alikimbia utafikiri mwizi...akawa
anakatisha kwenye majengo ya watu akiruka ukuta, na kila aliyemkaribia alipewa
kidogo.....
Sijui aliishia wapi , na sijui kama yeye atasalamika,
maana wale wenzake walishageuka wanyama wanataka hata kumdhuru ili tu azitoe
hizo pesa zote...
Jamani ubinadamu umekwisha...badala ya watu kusema
tumeona hizo pesa ni za nani, au ni nani kazidondosha tuzihifadhi na tuweze
kumuwakilishia mwenyewe, kila mmoja anawazia kuwa ni zake, anataka kuzipata ,
tunagombea jasho la wengine...’akamalizia kusema
‘Hivi kweli ukipoteza kitu kama pesa, unatarajia
kuzipata, siku hizi simu ukidondosha mwenzako akiwa nyuma yako akaiona,
akiipata mkononi imeshakuwa yake....hilo la ubinadamu wa namna hiyo sasa sahau...’akasema
mwenzake.
Jamani hali ngumu za kimaisha, umasikini uliokithiri,
kupungua maadili ya dini kunamgeuza mwanadamu kuwa mwingine kabisa,ni heri ukutane na mnyama sasa hivi kuliko kukutana na mwanadamu aliyekengeukiwa. Hivi sasa utu, huruma
upendo hakuna tena, watu wanatumia nyumba za ibada, wanajivika vazi la ucha mungu, lakini moyoni mwake anawaza mali,jinsi ya kupata pesa,jinsi ya kuhadaa watu ili achume zaidi na zaidi
....utu sasa umeyeyuka, ..kinachotawala kwenye nyoyo za binadamu hisia za changu, hata kama sio chako....
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Kweli kaka Mira dunia imelewalewa mpk walimwengu tumelewalewa
Post a Comment