‘Kwahiyo wewe una wasiwasi gani?’ akaniuliza mdada, sasa
akiwa ananiangalia moja kwa moja usoni.
‘Ina maana wewe huoni kuwa polisi walichokuwa
wakikitafuta wameshakipata…’nikasema
‘Polisi walikuwa wakitafuta nini?’ akaniuliza mdada,
kama vile hayo yote niliyomuelezea awali hakuyasikia, na mimi kwa vile
nilishamjulia nikaona niende naye hivyo hivyo,nikasema;
‘Walikuwa wakimtafuta huyo mtu aliyekuwa na ndevu ambaye
aliongea na mlinzi,na kama ujuavyo wao wanaamini kuwa huyo mtu ndiye wanayehisi
kuwa ndiye muuaji..’nikasema
‘Kama ni hivyo kwanini walimkamata mlinzi wangu, na
wakasema wana ushahidi wa kutosha kuwa huyo mlinzi ndiye aliyefanya hayo yote,
si kila siku unasikia yanayoendelea huko mahakamani...?’ akaniuliza
‘Wanasema mlinzi hakuwa peke yake kulikamilisha hilo,
.....’nikasema
‘Na hao polisi wanasema wamepata ushahidi, na
wameshamfahamu huyo mto aliyekuwa na ndevu wanasema huyo mtu ni nani?’
akaniuliza na mimi kwanza nikamuangalia mdada, kwa hali ya kutahayari kwani
niliona kama hayupo na mimi, nikijitahidi kuwaza nini lengo lake la swali hilo
mimi nikasema;
‘Wewe unafahamu fika kuwa huyu ni nani, unafahamu fika
kuwa huyo mtu ni mimi, …’nikasema na yeye kwanza akashikilia ile laptop akitaka
kuifunga, halafu akaangalia kitu alichokuwa akikiandika, na baadaye akainua
kichwa kuangalia pembeni, hauniangalia moja kwa moja sasa akatabasamu huku
akiwa anajikuna kichwani, alikuwa kaweka nywele zake ovyo ovyo, nahisi alikuwa
na mpango wa kwenda saloon,akasema;
‘Unaonaeeh, kumbe polisi wanamtafuta huyo mtu ambaye
alikuwa na ndevu si ndio, na hii ni kutokana na maelezo ya mlinzi, kuwa huyo
mtu ndiye aliyeongea na mlinzi, au sio...na yeye, ndiye wanayemshuku kuwa
huenda kahusika na hayo mauaji...’akatulia kidogo na kupitisha mkono wake
kichwani, na akasema
‘Kwa maana nyingine, polisi sasa wanaamini maelezo ya mlinzi
kwa vile wamepata ushahidi wa hizo ndevu au sio, na kwahiyo wanaanza kuamini kuwa alichosema huyo mlinzi kumbe ni sahihi, ...kwa hali hiyo sasa polisi sasa wanaanza
kuyafanyia kazi maelezo ya mlinzi, ni muhimu kuyaangalia maelezo yake kwa kina, je sisi yanatugusa vipi, unaona point yangu hapo...’akatulia kidogo.
‘Na kutokana na maelezo yako wewe, huyo mtu aliyekuwa na
ndevu ni wewe, na kwahiyo polisi wanakutafuta wewe, au sio? Sasa nikuulize
swali mimi nahusika vipi hapo, na kwanini kama ni hivyo maana wewe
unajifanya mwaminifu kwanini hujajipeleka polisi, ukawaambia jamani ulimi uliteleza, niliyosema awali sio sahihi mimi ni yule mtu mwenye ndevu.....’akasema mdada na kuniangalia
mimi moja kwa moja usoni
‘Mdada una maana gani kusema hivyo, `wewe unahusika vipi
hapo, mbona sikuelewi, unataka kusema nini hapo, kuwa wewe huhusiki na hayo
yote, wakati unafahamu fika kuwa wewe ndiye uliyenishauri kufanya hayo yote,
wewe ndiye uliyenivalisha hizo ndevu bandia kwa mikono yako mwenyewe, halafu unanisema kwanini nisiende polisi,….’nikasema
‘Nikuulize, je polisi wataamini hayo maneno yako,je kuna kitu gani
cha kuthibitisha hiyo kauli yako, kuwa mimi ndiye niliyakuvalisha hizo ndevu
bandia,...je kwenye hizo ndevu bandia kuna alama zozote za kwangu, kwa mfano labda
kuna alama zangu za vidole,...mmmh, hebu fikiria hilo, ....’akasema mdada huku
kainama chini kama anatunga sheria.
Mimi nilijaribu kukumbuka ile siku, ni kweli sikue ile
mdada alikuwa na tahadhari zote yeye hakubanduka na kinga za mkononi, na nikajua
kayasema hayo kwa akiaminisha hivyo kuwa yeye alikuwa amevaa kinga za mikononi,
na alama zilizoonekana kwenye hizo ndevu bandia ni za kwangu, maana nakumbuka wakati nakimbia, nikiwa
nazivua hizo ndevu sikuwa na kinga yoyote mononi....
‘Mdada unataka kusema nini hapo....’nikamuuliza nikianza
kuingiwa na mashaka.
‘Nikuulize wewe kwanza, je polisi wanamtafuta huyu mtu
aliyemvalisha huyo mtu aliyekuwa na ndevu au wanamtafuta huyo mtu mwenye
ndevu?’ akaniuliza mdada akiniangalia kwa macho ya udadisi.
‘Wanamtafuta huyo mtu mwenye ndevu , lakini nijuavyo
mimi hawataishia hapo ni lazima watataka kujua ni kwanini alifanya hivyo, na
hapo ndipo na wewe utaingia nikikutaja kuwa wewe ndiye aliyevalisha hizo ndevu,
unaona hapo, mimi kila nitakachofanya ni lazima niangalia na athari zake
kwako...’nikasema
‘Mhasibu kuwa makini hapo...’akasema huku akiwa kama
anawaza jambo
‘Mdada kama lengo lako ni kuniruka, huwezi kabisa kufanikiwa,na
polisi wanahisi kuwa huyo mtu mwenye ndevu alikuwa akishirikiana na wewe, na
huyo mtu ndiye aliyemuua mtoza ushuru…’nikasema
‘Wanahisi au wanaamini hivyo, kwa ushahidi gani, …na
hiyo hoja ya kushirikiana na mimi imetoka wapi, walitamka polisi au umeitunga
wewe mwenyewe kichwani mwako, hiyo hoja naiona ni ngeni kwangu, usitunge hoja
zako mwenyewe, sema polisi wanachokisema wao, hebu niambie hiyo hoja umeitoa
wapi ?’ akauliza
‘Wanahisi hivyo,..ndio maana wanakusanya ushahidi, kama
hizo ndevu, na hata kama hawatatoa kauli ya moja kwa moja kuhusiana na huyo mtu
kushirikiana na wewe, lakini ipo wazi, ….’nikasema
‘Ipo wazi kwa vipi, acha kuzua mambo, usitunge kauli,
tuangalia kauli zao na ushaidi uliopo, ukijitungia mambo yako mwenyewe unajidanganya,
nikuulize swali, kwanini unakuwa na wasiwasi sana kuhusu hizo ndevu kuonekana,…?’
akaniuliza na mimi nikakaa kimiya nikianza kuhisi uwoga wa kusalitiwa, moyoni
nilianza kumuhisi mdada kuwa hana nia njema na mimi, na sikujua nimwambie nini
kwa muda huo.
‘Mhasibu unatakiwa ujue jinsi gani ya kujitetea pale
unapokumbwa na matatizo kama hayo, na ujue jinsi gani ya kujielezea wewe
mwenyewe...’akasema akinionyeshea kidole.
‘Kamwe, usitegemee kuwa mimi nitakubeba wakati wote,...leo
nipo kesho sipo...mimi ni mjanja nafahamu jinsi gani ya kupambana na majanga
kama haya...’akasema kwa kujiamini na mimi nikamwangalia kwa macho
yakutokuamini, na mdada aliponiona nipo hivyo, akasema;
‘Mimi, nimekuuliza maswali hayo yote kutaka kukuweka
katika hali ya kujiamini zaidi, …nikuambie jambo la ujasiri, kamwe usiwaogope
polisi, polisi ni watu kama sisi, wao kama wao ni fani yao hiyo, na watafanya
kila namna kutimiza wajibu wao, na wakati mwingine ili wafanikiwe ni lazima
wakutishe wewe raia, kuona uthibiti wako,
cha muhimu ni kuwa tayari kukabiliana nao,….’akasema
‘Lakini mdada, kwanini unafanya hivyo, mimi kuja kwangu
hapa ni ili tuweze kujipanga, ili tuwe kitu kimoja nitakachoongea mimi na wewe
iwe hivyo hivyo , na kama unavyoona hilo swala la ndevu linatuweka pabaya, je
tutasema nini sasa, ...tuendeele kuongopa, ndio maana nikaja kwako
tuongee..’nikasema
‘Ni sawa hujafanya vibaya, ndio maana nikawa nakuhoji
kujua jinsi gani utakavyojieleza mbele ya polisi, nikuambie kitu,
unapokabiliana na hao watu jieleze kivyako, usiongee ukiwa na lengo la kumkinga
mtu, hapo ni wewe na pilato...’akasema akitabasamu.
‘Ukiongea kumkinga mtu huku ukijua ni makosa, ujue
unafanya kosa juu ya kosa, na ujue jinsi gani ya kuyafuta hayo makosa mawili,
uliyojitakia...ongea ukiwa na lengo moja, kama ni kujihami ujue jinsi gani ya
kuja kupambana...unanisikia
‘Na kama ni kujitetea, basi na ujue jinsi gani ya kujiweka
sawa kwa hatua inayofuata, kama ni kukimbia au kujitoa muhanga, yote yanatakiwa
yajipanga kichwani mwako,hata siku moja usitegee ukimtegemea mtu fulani, atakuja
kukusaidia, kama hayupo, ama keshauwawa kwenye uwanja wa mapambano,...ni vyema
ujipange....’akasema mdada na kunifanya nimuangalia mara mbili tatu na yeye
akaendelea kusema;
‘Usipende kusema yeye aliniambia nifanye hivyo,sijui
yeye ndiye, yeye , yeye inaonyesha hujiamini, kwanza hao watu, watakuona wewe
una kili za kitoto,utaonekana mjinga,
hujiamini,…unanisikia…’akasema
‘Lakini kwa kuhusu swala la ndevu huo ndio ukweli
wenyewe…’nikasema
‘Ukweli gani hapo…?’ akaniuliza akiniangalia kwa mashaka
na kwa udadisi
‘Kuwa wewe ndiye uliniambia nifanye hivyo na wewe ndiye
uliyenivalisha hizo ndevu, ..’nikasema
‘Nilikushika kwa nguvu nikakuvalisha kweli si kweli?’
akauliza
‘Hukunishika kwa nguvu…’nikasema lakini kwa hali kama
ile haina tofauti na kunishika kwa nguvu maana sikuwa nafahamu lengo
lako..’nikasema na yeye akacheka na kusema;
‘Masikini mhasibu, ...wewe sio mtoto mdogo bwana, upo
zaidi ya miaka mingapi sijui,muhitimu wa chuo.., wewe hukuwa mfungwa kwangu,...nilikufunga...’akawa
kama ananiuliza.
‘Wewe ni mwanaume bwana, si ndivyo mnavyojinadi nyie
wanaume,na kusema mimi mwanaume, mimi najiamini, mimi kiongozi wa familia, ndio
hivyo eeh,..., hivi kweli utawaambia polisi kuwa mimi nilikuvalisha ndevu, kwa
nguvu, au kwa hiari, na wao wakubaliane na hiyo kauli yako….hebu fikiria hilo
kwa makini…’akasem
‘Lakini mdada ni kweli kuwa ulinivalisha hizo ndevu na
mbele ya sheria hapo natakiwa kusema nini, natakiwa niseme ukweli au
nidanganye, je ni kweli hukunivalisha hizo ndevu,...na kiukweli , mimi sikujua
ni nini kusudio lako,…ningelijua kusudio lako nisingelikubali kufanya hivyo’nikasema
‘Sikiliza wewe mwanaume hebu jiamini, kwanza jua lipi la
kusema kwa nani, hapo polisi sio mbele ya sheria, wao wanakusanya ushahidi tu,
na utakavyojikanyaga kwako, ndivyo watakavyolichulia hilo tukio hata kama sio
sahihi, ukweli halisi utajulikana sasa mbele ya sheria, kwenye kiapo, na kwa
wakati muafaka….’akasema na mimi nikawa najilaumu kwanini sikusema ukweli pale
niliposimamishwa kutoa ushahidi, mdada akasema;
‘Sawa haya tuseme mimi nilikuvalisha hizo ndevu baada ya
hapo ukafanya nini?’ akaniuliza
‘Nikaenda kuonana na huyo mgeni ambaye alikuwa na huo mzigo wako…’nikasema
‘Halafu…?’ akauliza sasa akiendelea kuandika mambo yake
kwenye laptop, ilionekana kama
nampotezea muda wake, nikaanza kuhisi vibaya, nilitaka kukasirika, lakini kila
akinitupia jicho tukiangaliana tu, inakuwa kama ufuto umepita kwenye nafsi
yangu na kuifuta ile hasira na kuingia kitu kingine.
‘Mdada mimi naona tunapoteza muda hapa, mimi nakuona
kama wewe una lengo jingine kabisa, na lengo hilo ni kuniruka ili mimi
nionekane ndiye niliyefanya hayo kwa matakwa yangu binafsi, sasa niambie
ukweli,…’nikasema na kabla sijamaliza akafunga laptop yake na kushusha miguu yake chini, ni kama vile kawaza jambo
la kutisha, akasimama na kusema;
‘Wewe ndio unanipotezea muda wangu najaribu kukusaidia,
nikijipanga wa kugawa muda wangu, huku nafanya mambo yangu, huku
nakusaidia...lakini mmh,...’akasema kuonyesha kukerwa.
‘Ujue muda ni mali,kesho mimi natakiwa kusimama
kizimbani kutoa ushahidi ni lazima nijiandae,wewe umekuja na porojo zako zisizo
na kichwa, wala miguu, najaribu kukusaidia kwa kupanga muda wangu, lakini wewe
hunielewi, unataka mimi nifanye nini…..’akasema kwa hasira
‘Unasema kesho unasimama kutoa ushahidi una uhakika na
hilo, …?!’ nikauliza sasa nikiwa na mshangao sikuwa nimelithibitisha hilo kuwa
kweli mdada ataweza kusimama kizimbani na kutoa ushahidi, kwani mdada
alishasema siku akisimamishwa mahakama hali ya hewa inaweza ikabadilika
kabisa...
‘Nimeshapata barua rasimi kuwa kesho ni zamu yangu ya
kutoa ushahidi, na dakitari wangu kathibitisha kuwa ninaweza kufanya hivyo,
sina jinsi nyingine ya kukataa kwahiyo hapa nilipo nina mambo mengi ya kuweka
sawa, na wewe unakuja na shida zako unahitajia msaada wangu, sawa siwezi kukukatalia
ni lazima nikusaidie....’akasema na mimi nikatulia.
‘Sasa niambie unataka nini kwangu, unataka mimi
nikusaidie vipi?’ akaniuliza akiwa kashika kidevu kuonyesha kutafakari, huku
akiwa haniangalii mimi moja kwa moja na mimi hapo nikashindwa kabisa kumuelewa
mdada
‘Hivi mdada hapa
ni swala la kunisaidia mimi au ni swala la sisi tutasaidiana vipi,….hivi
unahisi polisi wakinikamata mimi sasa hivi unafikiri mimi nitasema tena uwongo,
nakuambia ukweli safari hii sitakubali kusema uwongo tena,nitawaambia kila
kitu, toka mwanzo nilivyokutana na wewe hadi hatua ilipofikia ili niwe huru ...…’nikasema
na mdada akanigeukia na kuniangalia akasema;
‘Mhasibu kwanini hukuwaambia hayo toka awali ukawa huru
kama ndivyo unavyojidanganya hivyo,...hujui sasa hivi upo nje kwa dhamana kwa
sababu ya hayo uliyoyaelezea, kama ingelikuwa hivyo unavyofikiria wewe, ....’akasema
huku akitabasamu, halafu akasema kwa sauti ya utani.
‘Ungelishaolewa huko jela, na kwa jinsi ulivyo wewe handsome boy....mmmh, sijui, masikini
mhasibu, jeribu kuamuka, jaribu ujiamini...hata hivyo, mimi sikuwahi kukuzuia
kusema ulivyotaka wewe, nikuulize , niliwahi kukuambia usiwaambie polisi hayo
yote? Hayo ulisema kwa hiyari yako bwana,....’akasema
‘Sawa mimi nimejipanga kuja kusema uweli wote, ili
nisiwe msaliti wa haki na ukweli..’nikasema
‘Mhasibu, nimekufahamu udhaifu wako, kweli wewe hujiamini,
...nikuambie ukweli usione mimi nakuuliza maswali hayo yote ukafikiri miimi
nimekusaliti…hapana nia yangu ni kukuweka wewe sawa...uweze kujiamini,..lakini
naona kama namsaidia mtoto mdogo anayeanza kusimama....’akasema na kutembea
tembea mbele na kurudi tena hatua mbili nyuma.
‘Hivi hadi sasa wewe mtu hjanielewa, hivi wewe unanionaje
mimi, unahisi kuwa hayo yote niliyokuuliza
nilikuwa na lengo la kukuruka, ndivyo akili yako inavyokutuma au sio...hahaha,
masikini mhasibu...’akasema huku akitikisa kichwa.
‘Ndio hivyo..’nikasema
‘Mhasibu hebu kuwa na ujasiri wa nafsi,...unajua nafsi
ni kitu kidogo tu, lakini kinaweza kukutawala na kukuyumbusha, lakini sivyo
inavyotakiwa, ...sisi kama wanadamu tunatakiwa tuweze kuitawala nafsi,
usipoweza kufanya hivyo, utakuwa muoga, utakuwa hujiamini na mwisho wake utakufa
kwa shinikizo la damu...’akasema mdada.
‘Mdada sizani kama nitakuja kukuelewa, sikuelewi kabisa,...mara
nyingi wewe hueleweki, leo upo hivi kesho upo vile, na nakuona kama unanitumia
tu kwa malengo yako binafsi....’nikajitetea
‘Jamani mhasibu yaani ndio imekuwa hivyo...’akasema huku
kashika shavu, akiniangalia kama ananisikitikia, na mimi nikawa simuangalii
nimeangalia mbele huku napitisha mkono wangu kichwani, sikusema kitu, yeye
akasema kwa utulivu;
‘Kwanza elewa kuwa polisi bado hawajamfahamu huyo muuaji
ni nani hilo nina uhakika nalo, hata huyo mlinzi waliyemkamata hawana uhakika kuwa
kweli ndiye aliyafanya hivyo, hata hivyo ni lazima mtu awajibike, ni lazima
waonekane wanafanya kazi,....’akasema na kuanza kutembea tena hatua kadhaa
mbele, halafu anageuka na kutembea hatu nyingine , akawa anarudia hivyo hivyo
na mimi nikainua kichwa na kumuangalia, nikasema
‘Kweli eeh, ...wewe umejuaje?’nikamuuliza
‘Ndivyo ilivyo, polisi ili wafanikiwe, ...sisemi kuwa
hawawezi, wanaweza sana, lakini ili wafanikiwe katika kazi yao, wanategemea
ushahidi na maelezo ya watu walishuhudia au kuwepo kwenye tukio.....mimi na
wewe ndio wahusika wakuu, au sio...je umetoa msaada gani kwako ili waweze
kufanya kazi yao..?’ akaniuliza
‘Nimewaambia yale niliyoweza kuwaambia....’nikasema
‘Kwahiyo basi kwa jinsi tukio lilivyokuwa, wao
hawajapata ushahidi wa kutosha kuweza kumfunga mtu,wao hadi sasa wanategemea
huo ushahidi kidogo walioupata, hata hivyo ni lazima mtu akamatwe hasa linapotokea
jambo kama hilo...’akasema akiwa kasimama lakini sasa alikuwa akiangalia nje
kupitia dirishani.
‘Nikuambie ukweli, huyo waliyemkamata mpaka sasa hawana
uhakika wa mia kwa mia kuwa ndiye aliyehusika na hayo mauaji...ushahidi wa raia
wema ndio utakaowasaidia wafanikiwe kwa hilo,..., sasa raia wema ndio wewe na
mimi, ndio maana nakuuliza wewe kama raia mwema umewasaidia vipi hao polisi ili
haki itendeke...? ’akaniuliza.
‘Hapo sikuelewi...’nikasema
‘Kwanza ujue kuwa muda umepita sana, tangu tukio lile
litokee, kuna watu walifanya kazi yao vyema...polisi wakupima wakuangalia hiki
na kile, wakawakisliha ripoti zao, lakini zilipofika kwa wakubwa, hao
waheshimiwa, wakazifutika kibindoni kwa masilahi yao, na hapo ushahidi wa awali
ukachakachuliwa...’akasema mdada
‘Kwanini?’ nikauliza
‘Kwanini, unaniuliza mimi kwanini...kawaulize
wao...inawezekana hili lilifanyika kwa mipango maalumu, maana kama wewe ulikuwa
ni mwenzetu, sasa umeamua kutusaliti, unafikiri wenzako watakufanya nini, na
wakati wanafahamu fika wewe unafahamu kila kitu, dawa ni kukuziba mdomo...sina
uhakika na hilo usije kuninakili vibaya.....’akasema
‘Huko kwa wakubwa kunawaka moto, kuna wakubwa wengine
hawalikubali hilo sasa wenyewe kwa wenyewe wanazungukana,..ndivyo ilivyo kwenye
mzunguko huu wa dunia, kama dunia inavyozunguka na mambo yake yanazunguka,...na
yote yanawezekana, swali la kujiuliza ni kwa masilahi ya nani, mimi hapo sijui
….’akasema mdada
‘Mdada hayo yote mimi sielewi, wasiwasi wangu ni sisi
tunaochukuliwa kama chambo, hujui linachoendelea , wewe unatumbukizwa tu, wewe
huoni katika hali kama hiyo mimi nitafungwa kama mshukuwa, kama
niliyeshirikiana na huyo mlinzi na hiyo ina maana kuwa mimi nitaenda kuteseka
jela kabla huyo muuaji wa kweli hajapatikana, kama kweli akipatika, kama
unavyodai, nikuambie ukweli mdada,jela sio mchezo, wewe unaisikia tu….’nikasema.
‘Masikini mhasibu kumbe wewe ni muogo kihivyo, na kama
una hisia hizo za kwenda jela, usipoangalia vyema hao watu watakufunga kweli,
mara nyingine simba akikosa nyama hula nyasi,sasa uwe makini na tabia hiyo, wakimkosa
huyo muuaji wa kweli, kwa kutaka watoto wao waende choo, watawakamata wote
wanaowashuku na kuwaweka ndani,....’akasema
‘Ndio wasiwasi wangu huo....’nikasema
‘Mhh, pole sana, maana baba mkwe sasa hayupo upande
wako, ambaye ndiye aliyekuwa akikubeba, na nikuambie ukweli safari hii wakikumata
ujue wanakupeleka jela, sio huko kwenye vituo vyao vidogo,..’akasema mdada.
‘Usiseme hivyo mdada, uliwahi kusikia habari za huko,
jamaa mmoja alipelekwa huko mwezi mmoja aliporudi alikuwa kama kachanganyikiwa,
anajikuna mwili mnzima, anakohoa kupita kiasi, masikini hakuchkua muda....’nikasema
na kuinama kwa huzuni.
‘Ndio hivyo ndio jela zetu hizo, lakini zimewekwa
kwasababu gani,...?’ akaniuliza na mimi nilikuwa abdo nimezama kwenye mawazo ya
kumkumbuka huyo jamaa aliyewahi kufungwa kwa kushukiwa tu na mdada aliponiona
nipo kimiya akasema;
‘Haya hebu niambie kuhusu hao jamaa wawili ...’akasema
akinisogelea na kunishika begani
‘Jamaa gani ...?’ nikauliza nikishituka pale
aliponishika begani, na hali ile ilimfanya mdada aniangalie kwa mashaka,
akasema;
‘Upo sawa wewe..?’ akauliza
‘Unauliza jamaa gani....?’ nikamuuliza tena, na yeye
akatabasamu na kushika kidevu, halafu akasema;
‘Hao jamaa wawili uliosema walifika huko hotelini kwako,
wakaweka au waliotaka kuweka vitu ofisini kwako,hebu niambie walisema wanataka
kuweka vitu gani, hapo ofisi kwako au chumba kwako…?’ akaniuliza
‘Kiukweli sikusikia wakitaja ni kitu gani?’ nikasema.
‘Lakini walikuwa wameshika nini?’ nikauliza
‘Walikuwa na na hii mikoba ya safari, ....briefcase,...’nikasema
‘Ukiuona huo mkoba, au briefcase unaweza kuutambua..?’
akaniuliza
‘Kwanini nisiutambue, ulikuwa wa rangi, na sio hizi
briefcase za bei mbaya,...ni kama mkoba wa safari....nitautambua sana....’nikasema.
Kwanza mdada aliniangalia kwa makini, kama ana wasiwasi
na mimi, halafu akageuka na kuanza kutembea kwa mwendo wa kiaskari ule wa
mwendo-pole, hadi kwenye kabati,akatoa ufunguo na kutoa mfuko mkubwa wa nailoni
ndani yake kulikuwa na brifcase za kawaida tu, nikakumbuka ile briefcase, ....
‘Hivi vitu nimevichukua chumbani kwako,…..kabla polisi
hawajafika kukagua chumbani kwako…’akasema mdada nilibakia nimeduwaa huku
nikimkodelea macho mdada, baadaye nikasema;
‘Haiwezekani….’nikasema nikiuangalia ule mfuko wa
plastiki na ndani yake kuna hiyo briefcase ambayo nili-iona akiwa nayo mmoja wa
wale jamaa wawili...
NB: JE ITAKUAJE...TUZIDI KUWEPO
WAZO
LA LEO: Kunapotokea tatizo, kupotea kwa kitu, kuharibika kwa
kitu, kuibiwa kwa kitu, au jambo lenye kuleta hasara, hasa kwenye utendaji wetu
wa kazi, kuna tabia ya watu kusingiziana ubaya, hata kama hawana uhakika na
shutuma hizo, watakimbilia kusema ni huyu au yule ndiye anahusika.
No comments :
Post a Comment