Halafu
kwa haraka nikarudi hotelini lakini wakati nakaribia pale hotelini kwa mbali
nikasikia king’ora cha polisi kikija kuelekea hapo hotelini, nikajua ni polisi
hao wanakuja kunikamata, hapo hapo kwa haraka nikarudi kinyume nyume hadi nje
ya hiyo hoteli, nikasubiri, nilihakikisha sehemu niliyokuwepo hakuna mtu
anayeniona.....
Gari la polisi lilipofika pale waliingia moja kwa moja hadi
ndani na kshi kasha zao, huku wakiwa wamevalia nguo zao rasimi na pingu zimening’inia
kiunoni, wakaingia hadi ndani ya hoteli, sikujua huko ndani kinaendelea
nini...nikasubiri, na jambo la kusuibri linachukua muda, lakini baada ya nusu
saa hivi nikawaona wale polisi wakitoka.
Na walipotoka kwenye eneo la wazi la ile hoteli, wakawa
wanaangalia huku na kule, kulizunguka hilo jengo, walipita kwenye eneo la
kuegesha magari, nahisi walikuwa wakitafuta gari langu,
Baadaye nilimuona polisi mmojawapo akiwasiliana na simu
na wenzako nahisi ni huko ofisini kwao, haikupita muda, wote wakaingia kwenye
gari lao, nahisi waliambiwa waondoke tu, wakatoka nje kabisa na kuingia
barabara kuu, wakatoweka.
Niliangaza sehemu zote kuhakikisha kuwa hakuna
aliyebakia kwenye eneo la hiyo hoteli, ndipo namimi nikajitoa pale mafichoni,
sijui kama kuna watu waliniona , sikutaka kukaa pale zaidi nikaondoka kwenyeeneo
la hiyo hoteli,
Nilitembea kwa tahadhari hadi kule nilipoweka gari
langu, nikamuuliza yule jamaa kama kuna mtu yoyote alikuja kuniulizia, akasema
hakuna mtu aliyefika kuniulizia, akasema;
‘Ile nimesikia polisi wamevamia hiyo hoteli kubwa hapo
mbele, sijui wanatafuta nini hapo hotelini, umetokea huko?’ akaniuliza
‘Nimewaona, lakini sijui wanatafuta nini, walifika
wakaingia ndani na baadaye wakatoka, nahisi ni katika misako yao ya kutafuta
wahalifu...ndio kazi yao’nikasema
‘Mhh, na hiyo hoteli siku hizi inakumbwa na majanga,
sijui imekuwa ni chaka la wahalfu, siku za nyuma ilikuwa hoteli tulivu, lakini
waliiongeza na kuifanya iwe na huduma nyingi, naona mambo yamebadilika...’akasema
‘Sizani kama ni chaka la wahalifu, mimi nahisi ni moja
ya majukumu ya polisi kufika sehemu mbali mbali kukagua usalama ....’nikasema huku
nikiingia ndani ya gari langu na kabla sijaondoka yule jamaa akasema;
‘Sasa bosi wangu vipi, huniachii hata pesa kidogo ya soda....’akasema
na hapo nikakumbuka, nikatoa chochote mfukoni na kumkabidhi, alinishukuru sana
akidai kuwa siku ile hali yake sio nzuri sana, kwani tokea asubuhi alikuwa hajapata
hata tone la maji, moyoni nikasema;
Hayo
ndio maisha ya walio wengi hapa kwetu, mtu unaamuka asubuhi hujui hata utakula
nini, wakati huo huo kuna wengine wanajiuliza wakale kwenye hoteli gani ya
kifahari, lakini yote ni maisha.
Nilipotoka pale niliendesha gari kwa tahadhari mpaka
nilipokaribia eneo karibu na nyumba ambayo nimeambiwa baba mkwe huyo anaishi
hapo kwa ajili ya matibabu , ni nyumba aliyojenga baba mkwe huyo kwa ajili ya
dada yake, ni nyumba kubwa ya kifahari.
Mimi sikutaka watu wajue kuwa nimefika hapo nikapita
hadi mbele, ambapo huko kuna gereji, na huyo jamaa mwenye hiyo gereji
ninafahamiana sana na yeye, huwa wakati pikipiki langu likisumbua nampelekea
yeye, namuamini sana kwa kazi za ufundi wa magari na pikipiki
Nilipofika tu, jamaa akajua nina tatizo la gari,
akanipokea kwa shangwe, na huku akishanglia kwa kuita, bosi,bosi....
bosi,...sikupenda sana kuitwa jina hilo, lakini wakati mwingine sina jinsi kila
mtu anatumia jina alipendalo kwa malengo yake.
‘Karibu sana bosi, lisogeze hili gari lako ndani kabisa,
kwa maaliwatani, ....wewe ni mtu mashuhuri ni lazima nikupe kipaumbele,
...’akasema na mimi nikaliingiza gari moja kwa moja hadi ndani nikateremka
kwenye hilo gari na jamaa alishasogea tayari kusikia shida yangu.
‘Sijafia hapa kwa tatizo kubwa sana, ni ushauri tu,...muhimu
hebu likague hili gari uniambie tu kama kila kitu kipo sahihi, maana natarajia
kusafiri masafa...natumai unanielewa, nitaliacha hapa kwa muda, nakuaminia
mtaalamu wangu...’nikamwambia na yeye kwanza akaliangalia kwa kulipitia kwa
haraka halafu akasema;
‘Hili gari bado jipya kabisa...sizani kama lina matatizo
ni bora umefika hapa kwangu , kwani ungeliwapelekea mafundi wa njaa kali,
wangelichakachua na usingizia maosa ambayo hayapo, lakini sijaingia ndani
zaidi, huko kama una muda tunaweza kuangalai wote...’akasema
‘Sina muda huo kuna sehemu na kwenda kwa miguu, nikirudi
utaniambia...’nikasema
‘Ok, ni uamuzi wako,.....’akasema na mara moja akaanza
kazi mimi nikaondoka hapo ndani na kuelekea kwa baba mkwe, ni hatua chache kutoka
hapo kwenye hiyo gereji, nikatembea wa tahadhari hadi kwenye eneo la hiyo
nyumba, ni nyumba anapoishi shangazi yake mchumba wangu, sijawahi kufika hapo
kabla, ninapita tu, lakini sikujua kuwa ni sehemu anapoishi huyo shangazi.
nilihakikisha gari hilo lipo ndani kabisa sehemu
isiyoonekana kirahisi
‘Mtaalamu wangu, gari langu hilo hapa sio bovu,
nimelihifadhi kwa muda,...’nikasema
‘Hamna shaka tajiri wangu, ilimradi ukitoka unikumbuke,
siunajua tena siku hizi kazi hakuna, tunaganga njaa tu...’akasema
‘Hamna shida, ....’nikasema na kuanza kutembea kuelekea
kwa baba mkwe
**********
‘Baba mkwe wako haruhusiwi kuonana na mtu kwa sasa,
kaongea vya kutosha…’aliniambia dakitari niliyekutana naye mlangoni akiwa
anatoka na gari lake.
‘Oh, lakini alipanga kuongea na watu watatu, na mimi ni
mojawapo…’nikasema huku nikiangalia saa na muda ulishapita sana.
‘Ndio hivyo, muda niliopanga wa yeye kuongea na watu
umeshapita, na hata hivyo kutokana na hali yake kwa leo haitawezekana tena
aongee na mtu mwingine nimeshampa dawa maalumu za kumsaidia kupumzika,…’akasema
docta na mimi nikawa sina namna nyingine nikageuka kuondoka, na wakati nataka
kuvuka bara bara mara nikamuona shangazi,akija kwa mwendo kasi, alikuwa katika
mishe mishe zake.
‘Wewe mtu umefuata nini hapa nyumbani kwangu?’
akaniuliza aliponiona, nikaona sasa nimelikoroga, nikajinyenyekeza kwa
kumsalimia;
‘Shikamoo shangazi...’nikasema
‘Kamshike huyo shangazi yako dada yake huyo hawara
wako,nimekuuliza swali umefuata nini hapa kwangu, sitaki wanga hapa kwangu,
mnataka kuniuliza ndugu yangu, nahangaika huku na kule ili apone, bado mnakuja
kuwanga mchana, niambai umefuta nini hapa kwangu.....’akasema hayo maneno
makali mpaka nikashangaa, sikutaka kusema lolote baya nikasema;
‘Niliitwa kuja kuongea na baba mkwe..’nikasema
‘Ni nani amekuita na ni nani baba yako mkwe?’ akaniuliza
na mimi nikabakia kimya
‘Nikuambie tena na tena, sitaki kusikia hilo neno kutoka
kwako, ukilitaja katika hii familia, kama ni baba mkwe wako nenda kwa baba wa
huyo hawara wako, natumai na yeye ana baba sisi wewe kwetu ni kama mfu tu,
unasikia, sisi tumeshakuzika zamani, hatukutambui tena, ulishawahi kuongea na
binti hivi karibuni…?’akasema na kuniuliza
‘Hapana sijawahi kuongea naye, nikimpigia simu hapokei
kabisa, sijui kuna nini kinachoendelea,...hata hivyo shangazi…’nikaanza
kujitetea na akanisogelea na kuwa karibu na mimi akaniangalai usoni na kusema
‘Unaona nilivyofanya, hivi katika mile zetu kuna mkwe wako
anaweza kufanya hivyo, akakusogeela hivyo, hii ni kuonyesha kuwa mimi sio mkwe wako tena,kwahiyo, geuka na
sahau kama uliwahi kuchumbia kwenye familia yetu...unasikia eeh,
mpedwa...’akasema na kunisha na mkono wake shavuni
Kwakweli nilikereka kwani hata kama ni shangazi katika
mila zetu mtu kama huyo anajitahidia sana kuwa mbali na mkwe wake, na tendo
alilofanya hapo ni kuashiria kabisa kuwa mimi sio mkwe wake tena.
‘Shangazi hebu jaribu kunielewa, hivi mimi nina kosa
gani, ...’nikasema
‘Huna kosa mpendwa,..nikushauri kitu, tafuta mwanamke wa
kuoa, huyo hawara wao sijui anaitwa nani vile....eeh, mdada, hivi kuna jina
kama hilo uliwahi kulisikia, sisi tunafahamu majina kama Tausi, Rose, na
mengine lakini mtu anaitwa mdada, huoni kuwa ni majina ya kihuni....’akasema
‘Hapana hilo jina alilipendelea kutokana na maisha yake
aliyoyapitia, hataki kulitumia jina lake hasa, maana linamkumbusha madhila
hayo...’nikasema
‘Unaona eeh, jinsi gani unavyompenda, mpaka ukajua
historia yake yote,kweli ukipenda sana chongo utaita kengeza, masikini kijana
wewe, hapo umeingia choo cha kike, hapo eeh,
umeingia mkenge, utakuja
kuniambia....’akasema
‘Lakini shangazi ...’nikasema
‘Mpendwa,...niite mpendwa, kama umenipenda, lakini
shangazi kwa maana kuwa ni shangazi wa binti, hilo lifute akilini mwako,
umenisikia....’akasema na kunisogelea akitaka kunishika na mimi nikasogea
nyuma, akacheka kicheko cha dharau, na kugeuka kutaka kuondoka.
‘Shangazi tafadhali nipo chini ya miguu yako...’nikasema
nikijitahidi hata kupiga miguu, na aliposikia hiyo kauli akageuka na
kuniangalia huku kashika kiuno, akasema
‘Nimessahau, niliongea na kaka, akanipa maelezo yako
yote, na moja ya jambo tuliloliongelea ni kuhusu mkataba mliwahi kuandikisha
kati yako na binti yangu, sasa kama mkataba unavyosema ukikiuka masharti ina
maana nyumba na kila kitu chako ni mali ya mtoto, ambayo itakuwa chini ya binti
yangu…unanielewa, kwa vile wewe ndiye umevunja mkataba, usahau kabisa kama
ulikuwa na nyumba kule kijijini hilo ni la kukusaidia tu…’akasema
‘Una maana gani kusema hivyo shangazi kwani mimi
nimevunja mkataba gani, mbona hamnipi nafasi ay kujitetea?’ nikauliza
‘Kwenye mkataba wenu mlisema kuwa,kwa yoyote ambaye
atakiuka masharti ya uchumba wenu, akachepuka,...japokuwa mlikuwa hamjafunga
ndoa, sawa, lakini kwa vile ulimzalisha mwenzako tena kwa kubaka, basi, kila
kitu chako kitachukuliwa na mtoto,na mama yake akiwa msamamizi
wake….mliandikisha hayo wenyewe, siku ulipokwenda huko kijijini na
kujinadi
kuwa una nyumba na nyumba hiyo ni mali yako na familia yako yaani mke na mtoto au
sio, na kwa kujitamba ukasema upo tayari kuandikisha mkataba, ili kuhakikisha
kuwa kweli upon a binti yetu...’akasema
‘Ni kweli niliyafanya hayo kwa nia njema kabisa, hadi
sasa nina imani hiyo, binti yule ni mchumab wangu na tulikuwa tunasubiri
tufunge ndoa....’nikasema
‘Mtafunga ndoa na hawara yako nimeshakuchunguza sana,
...nikuambie ukweli, mapenzi hayalazimishwi, nimekugundua kuwa unampenda sana
huyo mdada, na binti yetu ulimtaka kwa tamaa zako za kimwili tu, ukambaka na
kumpa mimba....’akasema.
‘Shangazi ile ilikuwa ni bahati mbaya, lakini tangu
awali tulikuwa tunapendana na binti, ulishawahi kumuuliza hilo...’nikasema
‘Hayo yote nimeyafanya, nimafuatilia hatua kwa hatua
kuhakikisha hilo, wewe humpendi binti yangu, usijidanganye, usije ukamuoa binti
yanagu, ikawa ndoa ndoana...tumakubali hasara, lakini angalau umefidia kidogo
na hiyo nyumba....’akasema
‘Shangazi hiyo sio haki kabisa,....ile ni nyumba
niliyojenga kwa nia njema ili niweze kuja kuishi na familia yangu mimi na huyo
binti na mtoto wetu, mkifanay hivyo itakuwa sio halali kabisa…’nikasema
‘Hilo liwe fundisho kwako na wenzako wenye tabia kama
hiyo, manojifanya vijogoo, kwa tamaa zenu za kimwili,...kama mnajiona mna
midadi kwanini hamuendi huko mitaani, wanawake wa namna hiyo wapo wengi....wanajiuza,
wanajua jinsi zote ....’akasema akiwa hacheki kuonyesha kuwa hatanii.
‘Hao wanawake wamesomea hizo kazi, hawana haya kabisa,
kwanini hukuwaendea, ukamaliza hizo tamaa zako, kwanini mnawaharibu mabinti wa
wenzenu, wazazi wako wamehangaika, hawalali, nyie mnavizia kama fisi,
wanahaarmu wakubwa nyie....’akafyonza na kutema chini.
‘Nikuambie ukweli, mimi nilichukia sana niliposia hivyo
ulivyomfanyia binti yetu, mimi yule niliwahi kuishi naye nikamfunza na kumfunda
tabia njema, kwa tendo hilo ulinizalilisha sana, nilionekana kama sijui
kulea,...na hata hivyo binti hana kaosa wewe ulimbaka na ulikiri kufanya
hivyo...’akasema
‘Shangazi ilikuwa ni bahati mbaya tu...’nikajitetea.
‘Unajua sijui kwanini naendelea kuongea na wewe hapa,
nimekustahi sana, hebu uliza hapa mitaani, watu kama nyie nawafanya nini,
nilimshangaa sana kaka yangu kwanini kaka hakukufunga wewe, anakudekeza, hadi
anakutafutia kazi nzuri, na bado huna shukurani, unaona uliyoyafanya, mumeua,
mishirikiana na mdada, bado mnabebwa tu, ngoja sasa jamaa wamecharuka huko juu,
utakwenda kuozea jela kwasababu ya tamaa zako,..’akasema
‘Shangazi sisi hatujaua, huo ndio ukweli wa mungu, mungu
ni shahidi wetu..na hayo ya binti naomba tukae tuyaongee nina imani kuwa
tutafikia muafaka, nipeni nafasi ya kujieleza,...’nikasema
‘Nikuambie ukweli, ondoka mbele yangu nisije kukutukana,
...hunielewi eeh, hebu uliza hapa mitaani mimi naitwa nani, ...hilo sasa
limefika kwangu, ujue hapo ni mwanzo tu, sijamalizana na wewe, utaukimbia huu
mji...uliza wenzako, kesi ikiisha salama hakikisha unaondoka huu mji,
nitakuharibu uonekane choo, kilichotapishwa, hilo nakuahidi, kama unabisha
subiri...’akasema na kuanza kuondoka.
Niligeuka na kuona kundi la watu lilishaanza kuja
kusikiliza, taratibu nikaondoka nikiwa na aibu tele usoni, nilijiona mtu wa
balaa, maana kila ninapogeuka nakutana na matatizo, nikajiuliza nimekosa nini
‘Yote haya kayasababisha mdada, ni lazima niende
kwake,..’nikasema na kuelekea pale nilipoweka gari langu nilipofika jamaa
akaniuliza
‘Nimesikia kwa mama shughuli kuna mtu alikuwa akipashwa
vipande vyake...’akasema
‘Mama shughuli ni nani, ..?’ nikauliza
‘Mama mipasho, mama yule ni hatari, akikuamulia
utakimbia mji, ...anaongea,ana matusi, anaweza akakuzalilisha hivi hivi, na
usimfanye lolote, yule mama ni balaa, halafu ana nguvu, aliwahi kupigana na
midume miwili akaipiga kama watoto wadogo na kuwavua nguo hazarani...usicheze
na yule mama, wanaume wanamuogopa....’akasema
‘Unasema kweli....?’ nikauliza nikionyesha wasiwasi
‘Hayo ni kwa nje, na kwa ndani, watu wanaamini kuwa huyo
mama ana amini sana mambo ya kishirikiana, anaweza kukushusha mzigo....’akasema
‘Kunishusha mzigo una maana gani...?’ nikauliza
‘Unaweza kuota busha, na hata kupoteza kabisa sehemu
zako za siri, ukawa sio mwanaume tena, wapo waliofanyiwa hivyo, ilibidi
wahangaike sana na huyo mama ndiye aliyewasaidia kuwarejesha katika hali yake
tena...mimi nilishudia kwa rafiki yangu mmoja, sasa hivi kahama kabisa huu
mji....’akasema
‘Lakini hayo yana maana gani, anapata faida gani...?’
nikauliza
‘Cha msingi asichokitaka yeye ni kuingilia mambo yake,
kuwaharibu mabinti wadogo, na wanaume wanaowatesa wake zao, ...hayo kayafungia
kazi na amefanikiwa sana hapa mjini, kila mwanamke akionewa anakimbilia kwa
huyo mama, kama kuna binti kabakwa huyo mama anatafutwa....ole wao umbake binti
wa shule, huyo mama atalifungia njuga hadi mbakaji apatikane na akipatikana cha
moto atakiona...na ni lazima atafungwa, na akitoka huu mji
ataukimbia....’akasema
‘Oh, mbona balaa...’nikasema
‘Kwani humfahamu huyo mama,...?’ akaniuliza
‘Namfahamu lakini sio kwa mambo hayo...’nikasema
‘Sasa kama humfahamu kwa mambo hayo, jihadhari sana na
mabinti wadogo, jiepushe sana kuwaonea wanawake...na akikunyoshea kidole,
kimbia, hama kabisa huu mji,...vinginevyo ni mama mzuri tu, watu wanampenda
sana kwenye shughuli, hasa akina mama maana anajua kutoa mipasho, ndio maana
wanamuita mama shughuli., au mama mipasho.
‘Oh, sasa nimekupata, sijui hata nifanya
nini.....nitakimbilia wapi mimi...’nikasema
‘Kwani umefanya nini?’ aakniuliza
‘Mdada....’nikasema
‘Oh, kafanya nini yule binti mzuri...?’akauliza
‘Nataka kwenda kwake, hajafanya kitu kibaya....’nikasema
ili kupoteza lengo
‘Uwe makini naye, yule binti mjanja sana,...akikuweka
kwenye kona zake, atakuumiza huku anacheka....hebu jiulize mtoto mzuri kama
yule kwanini haolewi, kila aliyejaribu kumuoa sasa ni marehemu, angalia huyo
mtoza ushuru, yupo wapi...chunga sana kujuana na huyo binti...’akasema na mimi
nikasema
‘Mhh, haya sasa majanga, sijui nikimbie huu mji...lakini
ni lazima nimuone huyu mdada kwanza,...’nikasema na kuingia ndani ya garii
langu, huku akili yangu ikimuwa mdada, na nilipofika barabara kuu, nikakutana
na gari la polisi , likanisimamisha...
NB:Haya mambo
ndio hayo yanaiva mhasibu bado anakumbana na mitihani je ataishinda
WAZO
LA LEO:Ukikutana na mitihani mbali mbali ya kimaisha, majanga,
shida, magonjwa, fitina, umasikini nk, usikate tamaa, jitahidi uwezavyo kwa
kufuata njia iliyosahihi, kamwe usikimbilie kwenye ushirikina ukamkufuru mola
wako. Kumbuka mitihani mingine ni kwa ajili ya kukupima imani yako, ni kwa
ajili ya kukukomoza wewe ili uwe na uzoefu wa maisha,
Unapopatwa na mitihani ukakikimbilia kwenye
shiriki, ukadanganywa, ujue hapo haupo na mola wako tena upon a shetani, adui
mkubwa wa imani sahihi. Na ukifanya hivyo ukamtii shetani utakuwa umeshindwa
katika mitihani ya maisha, na hata kama utajiona umefanikiwa kwa kufuata njia
ya shetani, ujue mafanikio hayo ni kwa
muda tu,
Hebu jiulize wapo wapi waliofanikiwa kwa njia hizo za
kishetani, mbona hawakuweza kupambana na umauti...ujue raha za dunia ni kwa
muda tu.
Muhimu,
pambana kwa namna iliyo sahihi, jijenge kwenye imani iliyo sahihi, yashinde
majaribu kwa kujitahidi kufanya kazi kwa bidii kwa misingi ya haki na ukweli, huku
ukimuomba mungu wako akusaidie, na hayo utayweza vyema kama utasoma, ujue kuwa elimu ndio taa ya kukumulikia njia
iliyo sahihi.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment