‘Lakini kuna kitu
muhimu,....mhasibu nakupa muda mwingine, nataka uniambie ukweli, maana mimi
bado nina mashaka nanyi,...’
‘Una
mashaka gani na sisi...?’ nikauliza
‘Ni
kuhusu wewe kujivika ndevu, mimi nina uhakika na hilo kuwa wewe ulijivika ndevu...’akasema
na mimi nikaanza kuhisi uwoga fulani, moyoni nikijilaumu kwanini sikuweza
kumuambia ukweli toka mwanzo, lakini hapo hapo nikakumbuka onyo la mdada.
‘
Mimi ninachotaka kujua kutoka kwako,... kutoka kwenu ni kwanini mlifanya hivyo, kama sio mlikuwa na
mpango fulani dhidi ya mtoza ushuru, mlipanga pamoja kuwa uvae hizo ndevu, ili
huyo mtoza ushuru sikutambue wewe ili kufanikisha lengo fulani, ambalo
lilifikia hadi kuuwawa kwa mtoza ushuru....’akasema huku akitaka kuondoka,
‘Lakini
mimi sijafanya hivyo, na ukisema una uhakika una maana gani, mimi sijavaa ndevu
za bandia una ushahidi gani wa kusema hivyo ina maana huniamini tena ndugu
yangu?’ nikamuuliza.
Kwanza
akaniangalia kwa uso wa kunionea huruma, halafu akatikisa kichwa kuashiria
kusikinisikitikia, akasema;
‘Nimejaribu
sana kukuamini, lakini naona nina beba mzigo ambao haubebeki, na nionavyo hata
kama nitajitahidi vipi, sitaweza kuujua ukweli wote kutoka kwako, sasa mimi sina
budi kutimiza wajibu wangu, nilijua wewe utanisaidia,ili na mimi nikusaidie,
...lakini nionavyo mmi huenda sivyo ninavyokufikiria wewe....’akasema
‘Kwanini
mpelelezi?’ nikamuuliza
‘Kwasababu
wewe sio mkweli, ...niambie ni kwanini unafanya hivyo, ni kwasababu ya
mdada,...?’ akaniuliza.
‘Lakini
mimi nimekuambia ukweli wote, wewe unataka ukweli gani zaidi ya huo....na hilo
la kuvaa ndevu, nahisi ni ...mlinzi katunga tu, halipo, hakuna mtu kama huyo...’nikasema
Mpelelezi
akaniangalia kwa makini, halafu akafungua mkoba wake,na mara akatoa mfuko wa
plastiki na ndani ya huo mfuko wa plastiki kulikuwa na ndevu za bandia...akanionyesha
na kusema;
‘Unataka
ushahidi sio, ushahidi huu hapa....haya niambie, lakini kwa vile muda
umekwisha, na muda wangu wa kukuamini wewe pia umekwisha, inabidi mimi nifanye
kazi yangu, ni ukweli usiopingika wewe na mdada mnahusika kwa namna moja au
nyingine na kifo cha mtoza ushuru, ....’akasema na kabla sijasema
kitu,akaondoka kwa haraka....
Tuendelee na kisa chetu
‘Unataka ushahidi
sio, ushahidi huu hapa …’
Haya yalikuwa maneno ya mpelelezi ambayo yalinifanya nikose raha, na hasa pale
nilipoangalia sura yake iliyobainisha kuwa mimi siomkweli kwake,kwahiyo hawezi
kuniamini tena na hapo nikahisi mwili wangu ukinisisimuka kwa woga,nikawa naendesha
gari huku nikiwa sijaamini,nikihisi kuwa kwa muda wowote sasa ninaweza
kukamatwa kwani polisi wanaamini kuwa huyo mtu mwenye ndevu ndiye muuaji au
ndiye mshirika wa mauaji
‘Lakini...kama huo ushahidi alikuwa nao mpelelezi muda
wote huo, kwa nini hakuweza kuufikisha kwa
polisi?’ nikajiuliza huku nikiendesha gari,na nilijitahidi kuendesha kwa mwendo
wa kawaida kwani kwa hali ile ya mawazo ningeendesha kwa mwendo kasi
ningeliweza kusababisha ajali, akili haikuwepo hapo kabisa.
‘Au ni kwa vile hana uhakika kamili kuwa mimi ndiye
niliyekuwa nimevaa hizo ndevu,...lakini atakuwa kachunguza alama za
vidole,...sasa ni kwanini bado anataka ukweli, wakati ukweli anao yeye, ...oh,
ataka kujua sababu ya sisi ufanya hivyo, mimi nahisi anvuta muda ili apate
ushahidi mwingine wa kutosha kunikabidhi mimi kwa polisi kuwa mimi na mdada
ndio tuliokuwa na njama za kumuua mtoza ushuru….kweli mtu huyu mjanja...sasa
tumekwisha, hatuna ujanja...ni lazima tuseme ukweli....’nikaendelea kujiuliza
‘Lakini haya yote kayasababisha mdada,…..huyu mwanamke
hana mema kwangu, nisipoangalia atanipeleka kubaya, lakini kwanini moyowangu
hautaki kuachana na huyu mtu…sijui kanipa nini huyu mwanamke,sijui …mmh,lakini siwezi
kujidanganya mbele yake, ….’nikasema nikimuwaza mdada
‘Hata hivyo ni lazima niongee naye ili afahamu kuwa
mpelelezi anafahamu kila kitu, …ni lazima nimkanye asishindane na mpelelezi
kama kweli hataki kuingia matatani, na hiyo tabia yake ya kunitumia mimi kama
chambo ni lazima aiche,...kama kweli ananipenda kidhati, basi na yeye
anisikilize mimi…..vinginevyo, oh,sijui nifanye nini, ina maana nitafungwa tena
kwa ajili yake, haiwezekani…
‘Safari hii ni lazima nimueleze,ni lazima niongee naye,
ni lazima tukubaliane…’nikasema na kuchukua simu yangu kumpigia mdada, na simu ikawa
inaita bil kupokelewa, nikahisi labda mdada kafanya hivyo kwa vile bado
anaongea na baba mkwe.
‘Ni lazima nionane naye kwa haraka zaidi, maana sijui
mpelelezi ana mipango gani dhidi yangu kwa sura aliyonionyesha pale inaonyesha
wazi haniamini tena na ile hali ya kuondoka kwake kwa haraka akisema
keshagundua jambo ni lazima kuna kitu kingine kakigundua cha kuwezesha
kuunganisha ushahidi wake ‘ Na kwanini wanamtafuta sana huyo mtu mwenye ndevu ambaye ni mimi…’nikajiuliza
‘Haya yote bila kuonana na mdada, sitaweza kupata
uhakika wa kutosha, ….ni lazima nionane na mdada nione yeye kajipanga vipi, na
safari hii siwezi kukubali kufungwa…wakati hayo yote kayapabga yeye….’nikasema.
Kwa vile muda wangu wa kuonana na mzee ullikuwa haujafika,
kwani kila mmoja alipangiwa muda wake wa kuonana na huyo mgonjwa, nikaona ni
vyema kwanza nipitie hotelini kwangu kubadili nguo, na kujimwagia maji kidogo,
na pia kwa vile nilihisi ninaweza kukamatwa tena nikaona ni vyema nijipange
vyema.
Nikafika hotelini kwangu na kuingia kwenye chumba changu
moja kwa moja, niliona ni bora nijimwagie maji kidogo, na wakati naoga
nikasikia simu yangu inalia,nilikuwa nimeiacha kitanani, haikuchukua muda mrefu
ikanyamaza, nikahisi huyo mpigaji anaweza kuwa ni mdada,ndiye mwenye kawaida ya
kunipigia simu hivyo. Yeye anapiga simu kwa muda mfupi tu usipopokea anakata
simu.
Nikaharakisha kuoga na kukukimbilia chumbani kwangu na
nikachukua simu yangu,kuangalia huyo aliyenipigia simu ni nani, namba niliyoiona
hapo ilikuwa ni ngeni kwenye simu yangu, nikaipiga hiyo namba, lakini simu
ilisema mtu unayempigia hapatikani kwa sasa, basi nikajiandaa na kuvalia vizuri
kwa safari ya kwenda kwa baba mkwe.
Wakati natoka chumbani kwangu, nilihisi mwili ukinisisimuka,
hiyo hali iliniashiria kuwa kuna kitu hakipo sawa, sijui ni kwanini ....nikatulia
kidogo kuhakikisha kama kila kitu kipo sawa, na mara akili ikanituma niende
kwenye ofisi yangu, nikachapuka, kuelekea huko, na mara nikawaona wale jamaa
wawili waheshimiwa, wakielekea kule ofisini kwangu,nikajificha ili wasinione.
Wale jamaaa walikuwa na mwendo wa haraka, na
hawakuonyesha wasiwasi wa kuangalia huku na kule,walikuwa kimiya hawaongei,
walikuwa briefcase mikononi mwao,na walipofika kwenye mlango wa ofisi
wakaangalia huku na kule na walipohakiki, wanachokiangalia, wakapeana ishara ,
na wote wakavaa kinga za mkononi mwao, halafu wakafungua mlango na kuingia
ndani.
Mimi nikajiuliza kuna nini kinaendelea kwa hawa watu
wawili, na kwanini watumie kinga ya mikononi iliwasiache alama za vidole,
nikashindwa kuvumilia nikatembea kuelekea pale mlangoni,nilipofika niliona
mlango upo nusu wazi,nikasikia sauti zao kwa mbali
‘Fungua hilo kabati na uweke pale pale ilipokuwa awali….’nikasikia
mmoja akisema, na baadaye mwingine akasema
‘Mbona hili kabati leo halifunguki..’sauti nyingine ikasema
‘Haiwezekani! labda hebu jaribu tena, au umebadili
ufunguo...’sauti nyingine iasema na mwenzake akajibu
‘Hapana sijabadili, ufunguo ni ule ule,...nahisi huyu
mtu kaamua kubadilisha vitasa vya kabati,huoni, hivi ni vipya kabisa,,….’akasema.
Ni kweli, baada ya wao kunikabidhi dhamana za humo ndani, nilichofanya mimi ni
kubadili vitasa vyote vya zile kabati,na hili nililifanya bila kumwambia mtu,
hata mdada mwenyewe alikuwa halifahamu hilo.
‘Sasa tufanyeje…’mmoja akauliza
‘Tutafuta sehemu nyingine yoyote tuweke,..maana hapa
tunahitajika tuondoke haraka iwezekanavyo, muda umekwisha ,polisi wanaweza
kufika hapa muda wowote kuanzia sasa,hali sio shwari kabisa, unaona hali
ilivyo, wakubwa wote wapo roho juu kuhusu hii kesi, …’akasema
‘Na huyu mhasibu mwenyewe atakuwa wapi, huenda yupo
chumbani kwake,mimi naona twende tuonane naye,na tumuambie kuna vitu tunavitafuta
ofisini kwake, halafu akitupa huo ufungua itakuwa rahisi kwetu kuviweka hivi
vitu bila ya yeye kufahamu...’akasema
‘Tukienda kuonana naye, italeta shaka zaidi,hatutakiwi
kueleweka kuwa tulifika hapa, hasa yeye asilijue kabisa hilo, na mbaya zaidi
akigundua kuwa tumeingia ofisini kwake, usije kugusia kabisa kuwa tumegundua
vitasa vya kabati vimebadilishwa, unakumbuka tulivyomwambia muhudumu , kuwa
kuna mtu tunamtfauta huko juu, hatujasema tunakwenda kuingia kwenye hiyo
ofisi...’akasema mwenzake
‘Kwahiyo sasa tufanye nini?’ akauliza mwenzake.
‘Ngoja nifikiri, cha muhimu tuhakikishe kama hayupo
chumbani kwake, kama hayupo sisi tunaweza kuviweka huko huko chumbani kwake,, …..’akasema
na nahisi alichukua simu na kuanza kunipigia mimi na mimi kwa haraka na kwa
vile simu ilikuwa mononi mwangu, nikaizima wakati mlio wa kwanza ulishaanza
kusikika, na kwa haraka nikaondoka maeneo hayo kushuka chini, sikutaka kuonana
tena na hao watu.
Nilipofika chini cha kwanza kufanya ni kumpigia simu
mpelelezi, lakini cha ajabu hakupokea, iliita mpaka ikakatika, nikaone niandike
ujumbe wa maneno, nikaandika hivi;
‘Wale jamaa wawili
wamefika ofisini kwangu wakiwa na vitu, nimewasikia wakisema ni vitu
vinavyotafutwa na polisi, wamekuta nimeshabadili vitasa vya kabati, na
wamepanga kwenda kuviweka vitu hivyo chumbani kwangu...’nikautuma huo
ujumbe, lakini haukwenda ukawa hewani, kumbe simu iliisha salio.
Muda ukawa anakimbia kweli, nikakopa salio, na kuutuma
tena huo ujumbe, mara simu ikazima, ....oh, haukuwa na chaji, ...oh leo mambo
vipi, ndio kifo cha nyani nini..., sikutaka kupoteza tena muda, sikutaka kurudi
kuchaji hiyo simu, muda ulikuwa hautoshi;
‘Nitachajia kwenye gari langu...’nikasema huku nikatoka
nje, hadi sehemu nilipoweka gari langu.
Niliendesha gari na kutoka nje ya eneo la hiyo hoteli hadi
sehemu nyingine mbali kidogo na hiyo hotelini. Nilipofika hapo nikaangalia kama
simu imeongezea kidogo, lakini haikuingiza chaji. Nilitoka na kuongea na jamaa
yangu mmoja ninayemfahamu kuwa anisaidie kunichajia simu yangu angalau ipate
chaji kidogo, na aniangalizie gari langu kwani nimesahau kitu hotelini.
‘Sawa bosi najua ukirudi nitapata pesa ya soda...’akasema
‘Usijali ...’nikamwambia na kuondoka.
Nilirudi tena pale hotelini, lakini safari hii kwa
tahadhari, nilijilaumu kwanini nilitoka haraka, kwanini nisingelihakikisha kuwa
wale jamaa wameweka hivyo vitu chumbani kwangu, huenda wanaweza wakaweka sehemu
nyingine na kama wameweka humo, nitafanya nini.....
Haikupita muda wale jamaa wawili wakatoka nje na kuelekea
kwenye gari lao, waliendesha taratibu hadi bara bara kuu, mimi nikawa
nawafuatilia kwa macho, niliwaona wakiangalia huku na kule wakiwa ndani ya gari
lao, nafikiri walikuwa wakitafuta gari langu,na walipohakikisha kuwa sipo
maeneo hayo wakaondoka.
Mimi kwa haraka nikarudi tena kule kwenye gari langu na
kuwasha simu yangu na mara nikakutana na simu zilizopigwa na zote zilikuwa
namba ngeni , na moja ilikuwa imejirudia, nahisi ni hao hao jamaa
walinionipigia nikataka kuzipiga, lakini nikaona haina haja kwa muda ule,
nikautuma ule ujumbe wa maneno kwa mpelelezi.
Halafu kwa haraka nikarudi hotelini lakini wakati
nakaribia pale hotelini kwa mbali nikasikia king’ora cha polisi kikika kuelekea
hapo hotelini, nikajua ni polisi hao wanakuja kunikamata tena, .....
NB: Ni nini kitatokea kwa mhasibu, tutaona sehemu ijayo
WAZO
LA LEO: Wema mara nyingi haulipiki, ukitendewa wema, huwezi
kusema nitaulipa huo wema ulionitendea. Ukitaka kuhakiki hilo, hebu, angalia
muda wa wema uliotendewa, huwezi kuurudisha huo muda nyuma ukaulipa kwa muda
ule, pia huwezi kujua, jinsi gani huyu mtenda wema alivyojitolea kwako, na
hujui nafsini mwake alikuwa anajisikiaje, je wewe unaweza kubuni yote hayo,
haiwezekani,
Kwahiyo wema haulipiki, cha muhimu ni kumshukuru mtenda
wema, na kujitahidi na kuitakidi kimoyo kuwa utajitahidi na wewe kumtendea huyo
mtu wema kama huo, na zaidi mshukuru yule aliyemuwezesha huyo aliyekutendea huo
wema, kwani hata huyo aliyekutendea huo wema, sio kwa uwezo wake, hayo yote ni
kwa uwezo wa ,muumba wa kila kitu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment