‘Unasema humo kwenye huo mkoba
kuna bastola, oh, hiyo bastola unahisi ni ya nani?’ nikauliza na yeye
akaangalia ule mkoba pale chini, akausogelea ule mfuko na akiwa amevalia kinga
mkononi mwake, akautoa ule mkoba, akaufungua, mimi nilitaka kumzuia lakini
akawa ameshafungua ule mkoba.
Alipofungua ule mkoba,bastola ilionekana dhahiri ikiwa na
makabrasha mengine, na moja ya jarida hilo kuna maandishi makubwa yaliyoandikwa: `HATI ZA SIRI’
Na mimi nilipoona hayo makabrasha na ile bastola nikajikuta nikisema;
‘Kweli….’
Niliiangalia ile bastola,
kwa wasiwasi, na nilimuona mdada akiitizama ile bastola bila kuigusa, akasema;
‘Hata hivyo, japokuwa sijaikagua
vyema, ...ila inaonekana imetumika, ..’akasema
‘Umejuaje?’ nikamuuliza
‘Mhh, ....kuna risasi
zimepungua...’akasema
Mimi nilipoitizama ile moyoni
niliumia sana, nikikumbuka kuwa kitu kama hichi kimeshatoa uhai wa mtu, moyoni
nikawa naogopa hata kuitizama zaidi, lakini nikajikuta nikisema;
‘Oh, Mungu wangu, ina
maana hawa watu walitaka kunibambikia kesi ya mauaji, kwanini watake kuniwekea
bastola, na hizo hati za vidhibiti vya polisi, kwanini wanataka kufanya hivyo,
wakati wanajua fika kuwa mimi sikumuua mtoza Ushuru, wananitafuta nini hawa
watu, ni kwasababu ya hicho cheo…?’ nikawa namuuliza mdada na mdada akatabasamu
kidogo, na mimi nikaendelea kuongea.
‘Eti Mdada, hebu niambie,
kwanini wafanye hivyo, kwanza mimi sijawahi kumilii bastola, na hata hiyo
bastila sijui ni ya nani....’ nikasema, na mdada akawa anaufunga ule mkoba na
kuurudisha kwenye ule mfuko wa nailoni akaubeba na kuuweka kabatini kwake na
kulifunga lile kabati, akasema;
‘Hiyo bastola ni ya
kwangu....’akasema aliporudi kutoka kuweka vile vitu kwenye kabati,na
kuniangalia machoni, na mimi nikabakia mdomo wazi na nilisimama nikionyesha
mshangao,nilikodoa macho kumuangalia mdada, kama vile nimeona kitu cha kutisha.
Mdada bila wasiwasi akakaa
kwenye sofa dogo lililopo mbele yangu, na kujiegemeza, halafu akakunja nne, mguu
mmoja akauweka juu ya mguu mwingine, na kwa kufanya hivyo sehemu kubwa ya
mapaja ilikuwa wazi.
Mimi bado nikiwa na ile
hali ya mshituo, lakini macho hayana pazia, kwa haraka ikaona ile hali, na
macho hayakutosheka, yakataka kuhakikisha, kwahiyo yakahama kumtizama mdada usoni,
yakawa yanaangalia yale mapaja ya mdada, ibilisi sio mchezo,….
Tuendelee na kisa chetu….
**********
Mdada akiwa hana wasiwasi akainua kichwa kuniangalia,
hakuhangaikakujifunika vyema, akasema;
‘Hiyo bastola uliyoiona
hapo ni yangu, sijawa na uhakika ni kwanini,imewekwa hapo,….’akasema
‘Waliichukua lini, ?’ nikauliza nikipumua kidogo, na
yeye hakujibu swali langu mara moja akaendelea kuongea.
‘Ni lazima kuna sababu muhimu ya kuifanya hivyo
....’akasema
‘Sababu gani , mimi hata sielewi....’nikasema
‘Hivyo ni vidhibiti vya polisi, hayo makabrasha walikuwa
wakiyatafuta polisi kipindi fulani mwanzoni na ikasadikiwa kuwa yamepotea, sasa
kama ni hivyo, hata hiyo bastola itakuwa na jambo muhimu kwa
polisi....’akasema.
‘Itakuwa na jambo gani muhimu maana mimi nijuavyo, na
hata mahakamani walipokuwa wakitoa ushahidi bastola iliyotumika kwa mauaji ni
bastola ya mtoza ushuru mwenyewe...sasa hii bastola yako ina maana gani?’
nikauliza
Mdada akanitizama, na alitaka kusema kitu, lakini
akaghairi, akawa kama anawaza jambo, na akautoa ule mguu juu ya mwingine, na
nahisi aliona jinsi ninavyomtizama, akapandisha vyema nguo yake na kujifunika,
halafu akaiweka miguu yote chini akasema;
‘Lolote lawezekana.....’akasema
‘Wewe unafikiriaje ni kwanini bastola yako iwepo hapo,na
hata wewe mwenyewe usiwe na taarifa, kwani wewe ….’nikataka kuongea zaidi
lakini nikasitai. Mdada akajiweka sawa na akawa kama anachezesha miguu yake, na
kutoa mlio sakafuni, na mimi nikawa naangalia hicho kitendo, akashika kichwa
kama anajikuna, akatabasamu na kusema;
‘Hebu tumia akili kidogo.....’akasema
‘ Kwa vipi mdada, hilo sio fungu langu....’nikasema na
yeye akakunja uso kwa kutafakari, akasema;
‘ Kama unakumbuka vyema,siku ile wakati tunaongea na mpelelezi
, unakumbuka alisema nini kuhusu bastola yangu....?’ akawa kama ananiuliza na
mimi nilipotoka kusema kitu, akanikatiza na kusema;
‘Mpelelezi alitaka kujua kuhusu bastola yangui,mimi pale
pale nilihisi kuna jambo....’akasema
‘Na hapo bado ulikuwa hujajua kuwa bastola yako haipo?’
nikauliza na hakujibu swali langu moja kwa moja, aliendelea kusema;
‘Mimi niliporudi nyumbani nilienda sehemu ninapohifadhi
bastola yangu,nikiwa najiamini kabisa, mhhh, sikuiona…’akatulia kidogo
‘Mhh, ina maana ilichukuliwa siku nyingi au...?’
nikauliza
‘Hapana sio siku nyingi, maana siku kabla ya kifo cha
mtoza ushuru niliiona, nilitaka kuwa nayo tayari, kama mtoza ushuru atakuja na
shari....’akasema
‘Oh, ..sasa....’nikasema
‘Mpelelezi aliposema kuwa anataka kufahamu kuhusu
bastola yangu akilini nilianza kuingiwa na wasiwasi, na kujiuliza kuna nini
kuhusu silaha yangu, na nilitaka wakija hao vijana wake kama hawana kibali,
nisiwape,...’akasema
‘Walipofika uliwaambia nini?’ nikauliza
‘Hawakufika ….’akasema akibenua mdomo kwa tabasamu
lisilo la furaha.
‘Kwanini hawakufika….?’nikauliza kwa mshangao
‘Kwakeli siwezi kujua , lakini ukiangalia kwa
makini,inaonyesha kuwa mpelelezi alikuwa anafahamu kuwa hiyo bastola haipo mikononi
mwangu,na aliniuliza palekunitega,….’akasema
‘Aaah, hapana mpelelezi hawezikufanya hivyo, kwanini
afanye hivyo…?’ nikauliza na mdada akanitizama kwa mashaka, akasema;
‘Acha ushamba wewe, naona mpelelezi keshakuweka sawa,
unamuamini tu….huyu mpelelezi amekuwa akinitafuta sana, amekuwa akinishuku ,
kwanza alihisi mimi na mtoza ushuru tuna biashara ya pamoja, akakosa
ushahidi,....na hata hivyo hakukoma, nahisi kuna jambo ananihisi vibaya, na nia
yake ni kuona mimi naingia matatani, na kwahiyo amekuwa akiniwinda kwa muda
mrefu…’akasema
‘Mhh, lakini
mpelelezi hana nia mbaya na wewe, nijuavyo mimi lengo lake ni
kuhakikisha haki inatendeka, wewe humfahamu vyema huyo mtu, ni muadilifu na
anatimiza wajibu wake tu….’nikasema
‘Wewe ndio humfahamu vyema huyo mtu,…’akasema mdada huku
akiegemeza kichwa kwenye sofa akiangalia juu.
‘Mhh,haya wewe niambie kwanini sasa yeye hashirikiani na
polisi,akakufunga maana ushahidi mwingi anao wa kuonyesha kuwa wewe unahusika…’nikasema
‘Ushahidi upi unaonyesha hivyo, …?’ akauliza na mimi
nikawa kimiya na yeye akainuka pale alipokuwa amekaa na kukaa vyema akainua
mguu kutaa kuweka juu ya mwingine, lakini alipoona nguo yake unamuacha wazi
mapajani, akasimama huku akisema;
‘Mpelelezi ni mjanja sana, ndio maana hataki
kushirikiana na polisi wengine baada ya kubaini kuwa hawala lengo alilonalo
yeye, .....yeye anatafuta sifa, anataka kuwa shujaa, kwa kufanya jambo ambalo
wenzake wameshindwa kulifanya....’akasema
‘Mhh, .....’mimi nikaguna na yeye akaendelea kusema;
‘Hata huu mtego utakuwa umepangwa na huyo mpelelezi, nia
ni kutaka mimi na wewe tusimame kizimbani kwa kosa la kushiriki katika mauaji
ya mtoza ushuru, baada ya kuona kuwa hatuhusiki moja kwa moja…’akasema mdada
‘Lakini sisi hatuhusiki na yeye anafahamu hivyo, ndio
maana hajafikia hatua ya kutuweka ndani, mimi hayo unayoongea wewe, hata
sikuelewi na nikuulize swali, wewe ulipoona kuwa bastola yako haipo ulichukua
hatua gani? nikamuuliza.
‘Mhasibu, mimi najua nini ninachokifanya, sikusema
lolote kwa yoyote, zaidi ya kufanya uchunguzi wangu binafsi…..’akasema
‘Oh,mdada, kwanini, wewe unafahamu hatari iliyopo na vyombo vya
hatari kama hivyo, watu watavitumia vibaya,mwisho wa siku utaonekana ni wewe uliyefanya
hilo tukio…’nikasema
‘Lengo langu ilikuwa kwanza kupoteza muda ili nijue wapi
bastola yangu ipo, sikuwa kimiya tu, nilijitahidi kufanya uchunguzi wangu
binafsi, lakini hata watu wangu hawakuweza kupata lolote kuhusiana na bastola
yangu ….’akasema
‘Watu wako, watu wako, ni akina nani hao watu wako?’
nikamuuliza na mdada hakutaka kusema lolote kuhusu hilo swali langu, akaendelea
kusema;
‘Nilipoona hivyo, bastola yangu haipo, na hata huko
polisi kwenyewe hakuna taarifa yoyote, nikajua watu waliofanay hivyo, ni kundi
lisiloshirikiana moja kwa moja na polisi, na hapo nikajua ni undi la mpelelezi…’akasema
‘Uliwahi kumuuliza?’ nikasema
‘Lini...! wewe unaona mambo yalivyojitokeza kwa haraka,
sijapata muda kabisa wa kuonana na huyu mtu, ....’akasema
‘Ungempigia hata simu, ili uweze kufahamu
zaidi,...’nikasema
‘Mimi ni mtaalamu, najua nifanye nini kwa wakati gani,
ningelionana na mpelelezi kwa muda huo nisingeliweza kupata chochote, nilitaka
kuvuta subira, na subira yangu ndio hii, bastola nimeiona, lakini ndani ya
vidhibiti vya polisi....’akasema
‘Sasa...?’ nikauliza
‘Kuna maswali nataka nipate majibu yake, ni kwanini bastola yangu ichukuliwe, tena kwa
siri,halafu imewekwa pamoja na vidhibiti vya polisi... .ndio maana nafanya
uchunguzi wa haraka’akasema
‘Kwahiyo sasa umeshapata majibu ya uchunguzi wako?’
nikamuuliza
‘Kiujumla bado, nilimtegemea sana mtu wangu anayenisaidia ndani ya polisi,
lakini hata yeye kashindwa kulibaini hilo na sasa kahamishwa, japokuwa hakuwa
peke yake kwenye kazi zangu lakini huyo alikuwa karibu sana na jikoni…..’akasema
‘Haiwezekani, sasa ni polisi wa namna gani, ....sisi
tunajua polisi wote ni kundi moja...’nikasema
‘Polisi ni kundi moja lakini ndani yake kuna idara
tofauti, na kila idara ina namna yake,...ila mwisho wa siku kama ni tukio kama
hili la maujaji, watendaji hukaa pamoja na kujenga hoja ya pamoja, na baada ya
uchunguzi kila mmoja analeta taarifa yake...’akasema
‘Kwahiyo waliofanya hivi ni kundi gani, ni idara gani?’
nikauliza na mdada hakujibu swali langu akaendelea kusema;
‘Sasa natafuta majibu ya maswali yangu, kwanza kwanini
walichukua bastola yangu, pili kwanini watake kukuwekea wewe huo ushahidi, na
kwanini iwekwe kwenye hivyo vidhibiti vya polisi….’akatulia
‘Sasa utayapata wapi majibu ya maswali yako?’nikamuuliza
‘Majibu ya
maswali yangu nitayapata kutoka kwa huyo mpelelezi,yeye anafahamu ukweli wa
hayo yote…lakini kwa hivi sasa nashindwa jinsi gani ya kumuingia, huyu mtu sasa
amekuwa ni adui yangu mkubwa,na sitakii kushirikiana naye kwa lolote lile,
maana atanitumia kujijengea sifa anayoitaka….’akasema
‘Mhh mdada kwanza nikuulize hayo yote unayofanya wewe ni
kwa masilahi ya nani, maana na wewe unajifanya polisi, kwanini unaingilia kazi
za watu?’ nikamuuliza na yeye akaniangalia kwa makini,na badala ya kunijibu
swali langu akasema;
‘Mimi nataka nikupe kazi,....’akasema na mimi
nikashituka na kumuangalia, na bila kunipa nafsi ya kumuuliza swali akasema;
‘Nataka, ili kulikamilisha hilo zoezi, wewe unisaidie kupata majibu ya hayo maswali yangu,
na sio kunisaidia, ni kwa ajili ya kujisaidia wewe mwenyewe….’akasema na mimi
nikamuangalia mdada kwa mashaka, na kichwani nikawa najiuliza huyu mtu
kachanganyikiwa nini, mimi nitayapata wapi hayo majibu,sijui chochote kuhusu
nyanja hizo, mwishowe nikamuuliza;
‘Mdada una uhakika na hicho unachokisema?’ nikamuuliza
na yeye akatabasamu na kuniangalia moja kwa moja usoni, akasema;
‘Hiyo kazi ninakupa wewe, …utafute,ujue ni kwanini
bastola yangu ilichukuliwa kwa siri, na kwanini imewekwa hapo kwenye vitu
vinavyotafutwa na polisi kama ushahidi wa mauaji ya mtoza ushuru,…..’akasema
‘Kwa vipi,mimi nitajuaje hayo maana hiyo sio fani yangu
kabisa, unafahamu fika mimi sio
mpelelezi na hebi niambie nitaanzia wapi kupata taarifa kama hizo, mdada nahisi
umeshaanza kuchanganyikiwa…’nikasema;
‘Hahaha, mhasibu ninataka wewe uongee na mpelelezi, yeye
ni rafiki yako, na anaweza kukuambia, cha muhimu ni kuwa na uhakika, ...tumia
akili ya kuzaliwa sio lazima utumie utaalamu wa kipelelezi.….’akasema na mimi
nikabakia kimiya, na yeye akaendelea kuongea;
‘Huyo rafiki yako, nimegundua kuwa anafahamu mambo mengi
ambayo hata mimi siyafahamu, kama angejikita kwenye mambo yake, nisingelikuwa
na matatizo na yeye, lakini sasa keshafikia hatua ya kunitishia mimi amani,nashindwa
kukutana naye tena uso wa uso, nita….’akasema mdada na kukatisha akionyesha
kukerwa, hadi nikaogopa asije akabadilika.
Ulipita muda kidogo, halafu mimi nikauliza;
‘Oh,mimi nitamuanza vipi huyu mtu…na hivi sasa keshakata
mguu kwangu kasema haniamini tena,kwa vile nimemficha ukweli kuhusu maswala
hayo ya ndevu…’nikasema na mdada akasema;
‘Sasa kamuambie ukweli ulivyokuwa kwanini ilitokea hadi
ukaweka hizo ndevu, lakini kwa ajili ya kupata ukweli kuhusu huu mzigo hasa
kuhusu hiyo bastola, na hili linatakiwa kujulikana haraka iwezekanavyo kabla
sijasimama kesho kutoa ushahidi,…’akasema
‘Nitampataje maana kwa hivi sasa nikimpigia
simu,hapokei…’nikasema
‘Ulimpigia lini simu kwa mara ya mwisho akaacha kupokea
simu yako?’ akaniuliza
‘Wakati nipo hotelini, nilipowaona wale jamaa
wawili...’nikasema
‘Sasa mpigia tena, na usitume ujumbe kuwa unao huo
mzigo, mpigia tena na tena, mpaka atahisi upo kwente tatizo, akipokea usiongee
naye sana, wewe mwambia kwa kifupi, ninao mzigo wanaoutafuta polisi, fika
tuonane, kata simu, yeye mwenyewe atakupigia.’akasema
‘Mdada hapana,..hiyo kazi mimi siiwezi kwanini usiwape
hao vijana wako, huoni kuwa hilo sasa ni bomu,…..’nikasema
‘Sikiliza mhasibu ina maana mimi niliyejitolea kuliondoa
hilo bomu chumbani kwako kukuokoa wewe mimi ni mjinga,….okey, kama unanion mimi
ni mjinga mimi nitaurudisha huu mzigo
huko kwako, wewe mwenyewe utajua jinsi gani ya kufanya,kazi kama hizi hazihtaji
kubembelezana….’akasema mdada
‘Sikiliza mdada,wazo langu ni hili huo mzigo wanautafuta
polisi njia nzuri na sahihi ni kuupeleka huu mzigo huko huko kwa hao polisi,
natumai wao watajua jinsi gani gani ya
kufanya,…au tuuweke sehemu ambayo wenyewe watakuja kuuona’nikasema, na mdada
akacheka na kusema;
‘Kama kuna watu kichwa maji,basi na wewe ni miongoni
mwao, hebu jiulize kwa kutumia akili yako ndogo tu usiumie kichwa ni, kwanini
polisi hao hao walitaka kuuweka huo mzigo hapo kwako….jiulize kwanza hilo
swali, halafu wewe unauchukua na kuwarudishia wao……tumia akili kidogo kuliwazia
hilo…’akasema
‘Kwani ni polisi waliouweka au ni wale jamaa wawili,
kama hatuwaamini hao polisi wengine basi sisi tupeleke kwa mkuu wa polisi wa
kituo, yeye atajua la kufanya….’nikasema
‘Sikiliza kazi kama hizi ukipewa jukumu hutakiwi
kukaidi, ...sasa mimi nitaurudisha huo mzigo chumbani kwako, na nitawaambia
polisi,waje huko kwako watakuja kuuchukua huko kwako,na wewe utajieleza mweneywe,
sasa tuone ni nini kitafuta baadaye….’akasema na mdada kwa sauti ya hasira na hapo
mimi nikaanza kuingiwa na wasiwasi,
‘Sasa unataka mimi nifanye nini?’ nikauliza
‘Nimekupa ushauri wa bure, wa wewe kuonana na mpelelezi,
na nafahamu sasa hivi atakukwepa kuongea na wewe, sasa hivi anahisi mimi na
wewe ni kitu kimoja, lakini tunaweza kumvuta kwa kutafuta jambo zito, na jambo
zito kwa sasa ni huu mzigo,huu mzigo una uzito mkubwa kwa sasa na ni bomu
ambalo hatujui litalipukaje…mtaalamu wa kulitegua hilo bomu ni huyo mpelelezi, ….’akasema
‘Kwahiyo nimpigia simu huyo mpelelezi nimuambie kuwa huo
mzigo ninao hapa kwako,au?’nikauliza
‘Huu mzigo hautakiwa kuwa hapa kwangu, nilichofanya mimi
nikuuondoa pale kwako kwa muda ili polisi wasiuone, mimi nitaurudisha pale
kwako,na wewe muite mpelelezi mkutane
hapo kwako yeye atajua jinsi gani ya kufanya,….unanisikia umenielewa,au
sio, sasa wewe ondoka,huu mzigo utaukuta huko kwako..’akasema
‘Utafikaje huuko kwangu….?’nikauliza
‘Hiyo sio kazi yako,…’akasema na mara tukasikia mlango
ukigongwa, na mdada akasimama na kuelekea pale mlangoni, akawa anaongea na
mlinzi wake, na baadaye nikasikia akisema muite aje, kukawa kimiya kidogo,
halafu nikasikia mdada akiongea na mtu mwingine, waliongea kwa dakika kadhaa,
baadaye madada akatoka pale mlangoni na kuja kukaa name kwenye sofa akasema;
‘Hali sio shwari,...’akasema
‘Kwani vipi...?’ nikauliza nikiwa na wasiwasi
‘Polisi.....’akasema mdada akiangalia kule kwenye kabati
lake.
NB: Polisi wamechachamaa, je bomu litalipukia wapi,
tuwemo kwenye sehemu ijayo.
WAZO
LA LEO: Ucha mungu wa kweli wa mtu unaonekana katika matendo
yake. Siku hizi uchamungu unakuwa kama
maigizo,watu wanakwenda kwenye nyumba za ibada, ili waonekane kuwa wao ni wacha
mungu, hata kujinadi kwa watu, kuwa wao ni wacha mungu, lakini ndani ya mioyo yao na katika matendo
yao, ni afadhali ya shetani, mimi najiuliza tunamdanganya nani, hivi kweli mwenyezimungu anadanganyika, kamwe
mwenyezimungu hadanganyiki, kwani yeye
ni mjuzi wa siri na dhahiri. Tujirekebebishe ili tujenge jamii ya watu waadilifu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment