Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, February 25, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-17



‘Unalo hilo....’

Sauti ile ilinifanya nisimame, japokuwa nilikuwa tayari nimeshaanza kuondoka na pikipiki langu, Niliposikia sauti ikisema;

Nikageuka kuangalia kule sauti ilipotokea, nikagundua kuwa ni mmoja wa wafanyakazi wa hapo. Walikuwa wale jamaa wawili waliokuwa wakipigana siku ile nilipofika kwa mara ya kwanza, ambao kwa sasa ni marafiki wakubwa, kweli wagombanao ndio wapatanao.

Nikawaangalia, wakija kwa mwendo wa taratibu huku wameweka vifaa vya kusikilizia muziki kwenye masikio yao, na vaa yao ndio ile ile ya kizazi chetu, uruali mlegezo,...japokuwa walikuwa wamevaa kiofizi,...naona, walikuwa wamechelewa kutoka ofisini, na walikuwa wakija kuchukua magari lao.

Jamaa hawa wawili ni miongoni mwa wafanyakazi, wanaotoka kwenye familia zenye uwezo, kwani kila mmoja alikuwa na gari lake, na walilonunuliwa na wazazi wao.Na hapo nikajiuliza kwanini siku ile walipigana, ...Je ni kweli,walikuwa wakipigana kwa ajili ya mapenzi , au ni kutokana na mashinikizo mengine, sikupata jibu, na muda huo walikuwa wameshanifikia.

‘Mhasibu habari za muda...’akasema mmojawapo, akitoa vile vifaa masikioni, na mimi nikamwangalia na kusema;

‘Mimi nawaoenea huruma sana na hivyo vitu mnavyoweka masikioni, kwasasa hamuwezi kuona athari yake, lakini baadaye asilimia kubwa ya watu wanaotumia hivyo vifaa, watakuwa na matatizo ya masikio...’nikasema

‘Wee acha longo longo zako, hivi vimethibitishwa kitaalamu ..hawawezi kuuza vitu kwa watu watumie, bila kuhakiki usalama wake...’akasema huyo mmojawapo,

‘Hata dawa zinahakikiwa, lakini zina madhara au sio cha muhimu ni kufuata masharti ya docta...’akasema mwingine.

‘Kwahiyo mnamaanisha kuwa wakati mnanunua, mliambiwa havina madhara na docta, hasa wa masikio?’ nikamuuliza

‘Usikwepe hoja, ya msingi, maana wewe unaangalia upande wetu, hebu tukuulize wewe na mdada vipi,...maana madhara ya huyo mdada ni makubwa kuliko hivi vifaa, au wewe hilo hulioni...’akasema mmojawapo.

‘Kwani vipi,....?’ nikauliza

‘Naona wewe umeshanaswa na mdada....’akasema mwingine.

‘Nimenaswa kwa vipi, sijawaelewa...?’ nikauliza nikikumbuka kuwa hawa jamaa walipigana kwasababu ya wivu wa mapenzi, kwahiyo huenda wananiambia hivyo kwa vile wameshaona nipo karibu na mdada.

‘Mhasibu sisi tunamfahamu sana huyo dada siku nyingi kabla hujafika hapa, na bahati siku ile ulipofika nakumbuka sana, ulituona tukipigana, yote hayo yalikuwa ni majaribu ya huyo msichana, ....’akasema.

‘Ni ujinga wenu, kwanini mpiganie mtu ambaye wala hakuwa na mapenzi na nyie....wakina dada wapo wengi wazuri na kila siku wanazaliwa, ...ni ujinga kupigana, eti kwasababu ya mapenzi...’nikasema.

‘Hahaha, unamuona mhaibu anajiona mtu wa hekimaaa... hivi tukuulize na wewe ambaye umeingia kwenye mitego naye, una uhakika kuwa kweli kuwa mdada ana mapenzi na wewe...maana yaliyotukuta sisi, tunaona ndio yamekukuta na wewe...’akasema mmojawapo.

‘Mimi sidanganyiki ovyo, mimi hayajanikukuta na mna maana gani kusema hivyo.....?’nikajitetea na kuuliza japokuwa akilini nilifahamu kuwa wanasema kweli.

‘Hata sisi tulijidanganya hivyo hivyo, kila mmoja akijiona kawini, kumbe tulikuwa tunajidanganya wenyewe..huyo dada ni mjanja sana, anaweza kuwagonganisha vichwa, mkachanganyikiwa msijue mbaya wenu ni nani....’akasema mwingine na kunifanya niwe na hamasa ya kujua zaidi.

‘Hebu niambieni kwani huyu msichana aliwafanya nini , mpaka mkagombana, maana kama nijuavyo mimi, huyo mdada hakuwa na mpango na nyie, nyie kwa ulimbukeni wenu, mkahisi anawapenda, mkagombea kitu ambacho hakipo kwa ajili yenu...’nikasema huku nikajribu kuwakoga.

‘Ndivyo alivyokudanganya wewe sio..., kama alivyoniambia mimi kuhusu mwenzangu na kama alivyomwambia mwenzangu kuhusu mimi, na wewe umeambiwa hivyo hivyo....’akasema huyo ambaye alionekana muongeaji sana kuliko mwenzake.

‘Kama angelikuwa na mapenzi na nyie, je mlipogombana yaliishia wapi, mlifukuzwa kazi, je mdada alikuja kuwatetea....na huko mlipokuwa aliwahi kuongea na nyie, angalau kuwapa pole....?’ nikawauliza.

‘Tulishaona ujinga wetu upo wapi, na baada ya lile tukio, tulikutana, ofcourse, wazazi wetu walitukutanisha, tukaongea na busara za wazazi zikatuingia, ndio maana hatukuwa na mazoea naye tena, japokuwa limetuuma sana, na ipo siku...’akasema huyo mwingine, na akakatisha, kwani simu yake ilikuwa ikiita.

‘Hatusemi kuwa huyo mdada anatupenda au anatujali,...inawezekana kweli ikawa hivyo kwa tamaa zake, lakini sisi tunafahamu fika, alitutumia sisi ili kufanikisha malengo yake, na kweli alitupata kilaini,...’akasema huyo mwingine.

‘Ina maana aliwafanyia nini, mpaka mkakubalia kufanya kile alichokitaka?’ nikawauliza

‘Hicho hicho alichokufanyia wewe....tunafahamu kabisa atakuwa kafanya hivyo, ndio mtegeo wake ulipo,..alitutege, kila mmoja kwa wakati wake, akijua kabisa kuwa familia zetu zina uwezo, na zipo kwenye nafasi ambayo, akitoa huo uchafu wake, itakuwa kasheshe....tulitoboka kweli...hilo tunakuambia kama kukuonya ...’akasema.

‘Ubaya wako wewe unatuona sisi ni hatuna subira,...nikuambie ukweli, huyo mdada ni mjanja kweli, kutokana na urembo wake, ni rahisi sana kumnasa yoyote...sio siri,..’akasema huyo mwingine.

‘Naona na wewe umeingia kichwa kichwa, ukaona umepata mrembo, haya endelea naye, sisi hatuna shida naye tena...’akasema huyo mwingine.

‘Hata hivyo, kuna kitu tunajiuliza ni kwanini kakuchagua wewe, maana kiukweli, sizani kama una utajiri huo anaoutaka yeye,...tumjuavyo huyu dada, anapenda pesa sana, dau lake io mchezo, na ni mjanja kweli, anakulia pesa, na hupati chochote kwake, zaidi ya kukurembulia...’akasema huyo mwingine.

‘Au mwenzetu ulibahatika...mmh, sizani, pale hupati kitu, ni mwongo, mjanja, na tapeli wa hali ya juu,...atakuliza, huku anakucheka, na ukiktaa kufanya anavyotaka, kama keshakuingiza kwenye mitego yake, atahakikisha anakuharibia kila kitu..hilo tunakupa kama onyo...’akasema

‘Onyo, onyo...onyo...kwanza nashukuru kwa kunzarau kuwa mimi sina lolote kwake, sina utajiri kama mlio nao nyie..its okey, lakini mimi nina akili zaidi yenu, hamjui nimepanga nini kwenye akili yangu, mimi nawazidi kiumri, nafahamu mengi zaidi yenu...’ nikasema nikajaribu kujiaminisha.

‘Kuna wazee, wenye wake zao, wamelizwa, semebuse wewe, umri sio tija, ...kama ulikosea awali, akakuingiza kwenye mitego yake, hubanduki, kama unabisha kataa anavyokuagiza, ....tunakuhakikisha, hayo machafu yako yote yatafika kwa watu unaowaheshimu,...na kama ulikuwa na mpango wa kuoa huko kijijini, ujua utavurugiwa, sizani kama huyo binti wa kijijini ataona hayo machafu aendelee kuwa na wewe....sijui, maana tusiseme mengi....’akasema mmojawapo.

‘Mimi bado najiuliza mdada, ana kitu gani anatafuta kwa huyu jamaa?’ yule mmojawapo akawa anamuuliza mwenzake.

‘Kwanini unasema hivyo?’ mimi nikauliza.

‘Tuseme ukweli, wewe una nini cha maana, una mali gani za kumfanya mdada akutake wewe, familia yenu ina uwezo huo....hapana, tumekuchunguza tumegundua huan lolote, ndio maana najiuliza huyu mdada anakutakia nini wewe...’akasema na kabla sijaongea kwani niliona wanaanza maneno ya kashifa huyo mwingine akasema;

‘Sio kwamba tunakuzarau mhasibu wetu, ila tujuavyo mdada anatafuta watu wenye uwezo ili kujinufaisha, sasa wewe unayo mali, au ni hicho cheo cha uhasibu...ili akutumie kuhujumu mali ya kampuni...?’ akauliza

‘Mimi hayo siyajui, mnasema nyie...’nikasema huku nikiona hakuna haja ya kuendelea kuongea na wao

‘Aaah, mhaibu tuliongee hilo kwa nia njema, je umeshanawa..kama keshakutega basi, huna jinsi, lakini kama bado hujaingia kwenye mitego yao, chondechode, mkwepe huyo mdada....’akasema huyo mwingine.

‘Huyu keshanaswa bwana, hukusikia tetesi kuwa aliandika hundi bandia kwa ajili yam dada, ...mhasibu mzima anaweza kufanya kitu kama hicho, kama sio kwa shinikizo...mimi nina uhakika mhasibu keshaingia kwenye mtego, na kama ni hivyo huna ujanja...’akasema

‘Hivi mnaniona mimi ni mjinga sana...eeh, kwa taariaf yenu, mimi huyo mdada hanibabaishi, uzuri wake kwangu ni sawa na maua mazuri ya waridi, yanavutia, lakini nafahamu kuwa huo mvuto ni wa muda tu,....’nikasema na huyo jamaa mwingine akacheka na kusema;

‘Kama ulishaingia kwenye mitego yake, jaribu kukataa, hebu jaribu ili uone atafanya nini..mwenzangu hapa alijaribu, ...huko kwao akienda sasa hivi anaingia usiku, mtaa wote wanamfahamu kuwa ana....’kabla hajasema mwenzake akamziba mdomo.

‘Hebu acha upuuzi huo, ..hujui unavyoniumiza....yaani hapa nilipo nina kisasi na huyo mdada, kaniharibia kila kitu, ...nilikuwa na mpenzi wangu nampenda sana, kafanya nikosane anye kabisa...alichonifanyia kilisababisha mimi na wazazi wangu tukosane, ...imechukua muda sana, kwa wazazi wangu kuniamini tena...na sio kama zamani....sijui nitafanya nini ili nilikoshe jina langu,...’akasema

‘Ni ujinga wenu...’nikasema

‘Kama ni ujinga wetu, jaribu kukataa atakavyokuagiza huyo mdada...hebu jaribu, wewe siunajiamini, jaribu...’akasema huku akiniangalia kwa ushahibiki na mwenzake akasema;

‘Kwa mfano, kama leo kakuambia ukafanye jambo fulani, au siku yoyote , ili kuthibitisha maneno yetu, hebu lipinge, usifanye, uone...hahaha, nakuambia ukweli, kampuni yote itaona uchafu wako, ..na huko kijijini, utahama kabisa...hebu jaribu, tuone video ya bure...hahaha mhaibu utaumbuka....’akasema na kucheka kwa kebehi.

‘Achenani na mimi, mimi nina akili zaidi yenu, ...ninafahamu wapi pa kumpatia huyu binti, nyie mtaona, dawa yake ipo jikoni....’nikasema huku nikianza kuondoka.

‘Hahaha, masikini mhaibu, kachoooka...’wakasema na kuangua kicheko, na mimi akilini nikawa nimejawa na hasira,...lakini sikuwa na la kufanya...

********
Usiku nilikuwa nimetarajia kupata simu toka kwa mdada, labda kunihitajia kufanya jambo fulani kama alivyosema, lakini haikuwa hivyo, hadi kunapambazuka, na asubuhi nikawahi kazini,....wakati napita kwa wauza magezeti, nikaona watu wamejazana, wanaanglia magazeti ya udaku.

Nikavutika na kwenda kuangalia, na mbele kabisa niliona picha ya jamaa ikiwa ukurasa wa mbele...akiwa uchi, lakini sehemu ya mbele, akawekea alama ya kizuia, asionekane sehemu zake nyeti, na maandishi yakisema;

Mtu mashuhuri anaswa akifanya uchafu kwenye hoteli, na mwandishi wetu wa mashahuri akamnaa taarifa zake kamili zitakuja hivi punde...nikaona herufi mbili za majina yangu japokuwa jina halikukamilika, kuonyesha kuwa ni alama za huyo mwandishi ili picha hizo zisinakiliwe.

 Mwili mzima uliniisha nguvu, nikabakia nimeduwaa, sikujua nimesimama kwa muda gani pale, ila baadaye simu yangu ikaingia ujumbe, ulikuwa hauna namba ya mtumaji, nikashituka na kuufungua huo ujumbe,...

‘Kazi yako mwandishi imeanza kufanya kazi, jamaa kajifanya mtata, na huo ndio utangulizi wake....kesho tunaweka kubwa lake...vinginevyo afanya nitakavyo mimi, nimemdai pesa kidogo tu, milioni kumi na tano, kwake yeye ni vijisenti, akanitumia milioni tano, hiyo tutagawana vipi....

‘Tunaweka...na nani ...huyu mdada ana maana gani, anafanya mambo yake, halafu ananihusisha mimi...sikubali, sasa hii imevuka mpaka....’nikasema na kukimbilia ofisini.
Nilipofika ofisini, hilo ndilo lilikuwa gumzo, watu wanamuongelea huyo tajiri, mtendaji mkuu wa sehemy nyeti za serikali, kakutwa akifanya uchafu ...na  kila mmoja aliongea leka,...nilikuwa na wasi wasi, kuwa huenda wakanihisi na mimi kuwa ninahusika.

Nilifanya kazi nikiwa na mawazo mengi, nikikumbuka maneno ya wale jamaa wakiniambia;

‘Kwa mfano, kama leo kakuambia ukafanye jambo fulani, au siku yoyote , ili kuthibitisha maneno yetu, hebu lipinge, usifanye, uone...hahaha, nakuambia ukweli, kampuni yote itaona uchafu wako, ..na huko kijijini, utahama kabisa...hebu jaribu, tuone video ya bure...hahaha mhasibu utaumbuka....

`Ina maana hata mimi nikikataa kufanya atakavyo mdada, na mimi nitatundikiwa hadharani....?’ nikajiukuta najiuliza na mara sauti ikasema nyuma yangu.

‘Ndio maana yake, na saa hivi nina usongo na wewe, jana ulikuwa ukiongea nini na wale vibaka?’ ilikuwa sauti akiwa nyuma yangu.

‘Vibaka gani?’ nikauliza

‘Unajifanya hukumbuki...nikukumbushe...’akasema akichukua simu yake, na mimi nikamsogelea na kusema;

‘Mdada hebu tafadhali achana na mambo hayo, sijasema sikumbuki,..kwani nimekufanyia nini mpaka utake kufanya hivyo, wao walikuja na kuanza kuongea na mimi, hatukuwa na nia mbaya na wewe...’nikajitetea.

‘Nina hasira sana leo, naweza kufanya kitu mbaya,..lakini tuone jinsi gani huyu mshamba atakavyofanya nimempa masaa, asipotuma hiyo pesa, namuumbua, yeye,a anjifanya anazo, kuwa atanimaliza, kama alivyodai, ..naafanay atakavyo aone vumbi langu...’akasema na mara bosi akaingia.

‘Kuna nini?’ akauliza

‘Hakuna kitu bosi tunaongea tu...’nikasema na mdada akaondoka.

 Baadaye bosi akaniita ofisini kwake;

‘Mhasibu uwe makini ...sasa hivi dunia imeharibika, siwezi kuamini, yule jamaa wa uhuru wa magari, kakutwa mahotelini akifanya uchafu, nasikia wamemtoa kwenye magazeti ya udaku....’akasema

‘Jamaa gani huyo?’ nikauliza

‘Kuna jamaa mmoja mtu wa heshima zake, ana utajiri sana, na yupo kwenye idara nyeti naona watu wa udaku wamemnasa, nyie wanaume mna nini, kwasababu jamaa ana mke wake mzuri tu, ana pesa,....na ana kazi nzuri,...kwanini ajizalilishe vile,...namsikitikia sana, kwani huenda akaondolewa kwenye hicho kitengo, kama ikigundulikana ni kweli...’akasema bosi.

‘Ina maana kwa ajili hiyo anaweza kuondolewa kazini?’ nikauliza

‘Ile ni kashifa mbaya, na kitengo hicho kinataka watu waadilifu, kama unadiriki kufanya huo uchafu, utaaminikaje,...anaweza haat kufukuzwa kazi...’akasema bosi.

‘Na hao watu waliofanya hivyo, hawaogopi, maana mimi naona ni hatari..’nikasema

‘Ni hatari kweli, jamaa yule anaweza akaua...japokuwa ni kashifa zaidi, lakini tumbe mungu yaishe salama...’akasema bosi

‘Baadaye tutaendelea na simulizi letu...’akasema bosi

Siku hiyo nzima sikuwa na raha, nilikosa amani kabisa, niliogopa, kama huyo jamaa atakuja kunitambua kuwa mimi nilikuwepo siku hiyo ataweza kunimaliza....japokuwa ankumbuka siku ile nilivaa mawani yangu ya kuendeshea pikipiki, ili kuficha sura, lakini kwa wataalamu wa kuangalia sura na amumbile ya watu wanaweza kunigundua...sasa nitaishije, mbona maisha yangu yanakuwa ya mashaka, nifanye nini......

 Baadaye bosi akaniita na kuanza kunisimulia kisa cha maisha yake..

********

Kuna mambo ukiyasikia kwa wenzako unaweza ukayazarau na kusema hayana maana ni mambo ya kuzarau tu, ...unaweza ukasema hivyo kwasababu hayajakukuta wewe,...hata mimi nilipokuwa nisikisia mtu akilalamika kuwa kasingiziwa ubaya, na akawa analalamika, nilimuona ni  wa ajabu sana, na nitamwambia;

‘Kama hujafanya una wasiwasi gani....’

‘Lakini yakukute wewe, unaambiwa wewe umeiba, wakati hujaiba, ...unaambiwa wewe ni mchawi, wakati, huujui hata huo uchawi upoje...hebu fikiri wale wazee , vikongwe, wanaofikiwa hata kuchomwa moto, au kuvunjiwa nyumba zao, kwa kusingiziwa uchawi,..kumbe wengine hawana makosa masikini ya mungu.

‘Hebu fikiria mimi yamenikuta hayo nasingiziwa kuwa mimi ni mchawi, nimefikia hatua ya kumuua mama mkwe,..wakati hata huo uchawi wenyewe nausikia tu watu wakiuongelea, siujui hata upoje, au watu wanafanya nini ili kumloga mwenzake,...watu wameenda huko kwa wanaoitwa wataalamu wamedanganywa kuwa mchawi wao yupo humo humo ndani, yupo hivi ha hivi, anafanana hivi na vile, wakaniona ni mimi

 ‘Usiombe, kusingiziwa mambo kama hayo, yanauma, na yanakufanya usiwe na amani kabisa, ...’akatulia.

‘Shutuma za kuwa mimi nimemfanyia uchawi mume wangu anipende, asiwapende ndugu zake, asiwasikilize wazazi wake,....niliziona ni za kupita tu, lakini, hizi zilizokuja kuwa eti mimi ndiye niliyemuua mama mkwe wangu, zilinichanganya kichwa kabisa nikawa sina furaha wala amani.

‘Nikawa najiuliza mwenyewe iweje watu wanifikirie mimi hivyo, mimi nipoje, ..ina maana mimi nina nguvu za mungu za kumtoa kiumbe roho, sijamtilia sumu, au kumuua kwa silaha, mama huyo kafa kwa ugonjwa, na madocta wamesema hivyo, huo uchawi umetoka wapi...sikuelewa.

Yaani shutuma hizo zilivyoletwa, zilikuja kama shutikizo kwangu, ni kitu ambacho sikukitegemea kabisa,maana kwa ahli ya kawaida, wengi wanasingiziwa mambo hayo ni watu wazima, wazee, lakini mimi....hapana,..sikuelewa,..nikawa nimechanganyikiwa hata sikujua nijitetee vipi...nikawa sijiamini, niliona kama kila mtu ananiangalia kwa jicho la ubaya,....sikuwa na amani kabisa.

Haikupita muda, tetesi hizi zikazagaa, na wanafamilia wakataka kuitisha kikao ili eti  waniweke kitako waniulize kuhusu shutuma hizo, lakini kuna rafiki yake mume wangu akakataa kabisa kufanyika kwa hicho kikao. Akiwaasa kuwa hizo ni shutuma mbaya, hazina ukweli,na wakifanya kama hicho kinaweza kuzua mtafaruku kwenye familia.

‘Jamani kufa ni matakwa ya mungu, mtu siku zake zikifika hata mfanye nini, atakufa tu, hakuna mwanadamu mwenye mamlaka hayo,...msikimbilie shutuma za kushukiana uchawi, mtagombana bure, na kuanzishiana chuki zisizo na ukweli...’akawaambia.

‘Wewe unasema tu kwa vile sio mzazi wako...kama ingelikuwa ni mama yako,ukasikia hivyo usingelikaa kimiya, nina imani ungelihangaika...’akaema mmoja wa shemeji zangu.

‘Jamani hayo mambo yamepitwa na wakati, hivi imani zenu kwa mungu zipo wapi, hivi mnaamini kuwa kweli kuna mtu anaweza kufanya uchawi kumuua mwenzake..kama watu hao wapo wana uwezo wa kufanya hivyo kwanini wasiende benki wakachukua pesa wakawa matajiri?’ akauliza.

‘Wewe wasema tu kwasababu hayajakukuta, ....’akasema wifi

‘Mimi sikubali hilo lazima lifanyiwe kazi...lazima mchawi wetu aumbuliwe, tumkalishe kikao asema ukweli...’akasema wifi mwingine.

‘Jamani hayo yote hayatasaidia kitu, je hilo litasaidia kumrejesha mama duniani, mama yetu ameshafariki, hata tufanye nini hatarudi tena duniani...cha muhimu kwa sasa ni kumuombea mzazi wetu huyo aishi mahala pema peponi sio kugombana...’akasema huyo rafiki wa mume wangu.

Baada ya malumbano ya muda mrefu, watu wakatawanyika bila maafikiano, na mambo yakawa yameisha hivyo kimiya kimiya, kila mtu akiwa na lake moyoni.

Siku zikapita japo kinyongo na kijicho dhidi yangu kiliendelea kuwepo, lakini siku zilivyozidi kwenda, hali hiyo ikawa kama inasahaulika kidogo kidogo. Na maisha yakaendelea.

Pamoja na maisha magumu, lakini nilijitadi sana, kuwa karibu na mume wangu, kumpa matumaini, kuwa hayo yote ni mitihani ya kimaisha, na kumuasa kuwa hayo wanayosema watu sio kweli, cha muhimu ni kumwamini mungu tu.

Sijui ilitokeaje,  maana na hii ilikuwa kama moja ya mashtukizo kwangu, sikutarajia kabisa, ilikuwa kipindi moto wangu anakamilisha mwaka, nikahisi mabadiliko mwilini, nikawa sijiamini, nikaona niende kwa docta,...oh, docta akasema nina mimba,, sikuamini ...

‘Docta sasa mtoto wangu ndio ana mwaka mmoja, nifanyaje...?’ nikamuuliza.

‘Hakuna shida, ni kiai cha kujipanga, ukijua sasa unatakiwa ule vyema, na wakati huo huo usimsahau mtoto...maana bado mdogo...’akasema docta.

‘Na ujitahidi sana kuja kiliniki, ili upate ushauri, ...’akasema docta.

‘Docta hakuna njia nyingine....’nikasema na docta akasema

‘Imeshatokea hakuna jinsi inabidi ulee mimba yako, na uwe makini kumpa mtoto wako huyu mdogo vitu vya kumsaidia..ili akue vyema,....’akasema docta, na kunishauria sana nisije nikafanya makosa eti ya kuitoa hiyo mimba.

Basi kutokana na ushauri wa docta nikaona niendelee kuilea hiyomimba yangu. Na wakati huo bado nilikuwa kwenye kile kile chumba kimoja na hali ilikuwa haijabadilika.Maisha bado yalikwua yanandelea kuwa magumu.

Nilipoona hali inazidi kuwa ngumu, na kama nitaendelea kumtegemea mume wangu tu, nitazidi kuumia, na mimba ndio hiyo inazidi kukua, ndio hapo likanijia wazo la kujishughulisha..hulka za familia yetu ni biashara, na hilo lilikuwa kwenye damu, nikaona kwanini nisijaribu.

Nikaona hiyo ndio njia pekee ya kunisaidia ili niweze kujikimu,..kuanzisha biashara, wazo hilo likanijaa akilini, na nikavutika nalo, nikaanza kujipanga nianze vipi, maana biashara inahitaji mtaji, inahitaji sehemu ya kuanzia, mume wangu hana mbele wala nyumba, sina mtu wa kumkopa,shemeji zangu hawawezi kabisa kufanya hivyo, sasa nitafanyaje hiyo biashara.

Nikawaza sana, na mwisho wake, nikakumbuka, kuwa nina vitu vya dhahabu, nilivyowahi kupewa kama zawadi , nilichofanya ni kanza kuviuza hivyo vitu vyangu vya dhahabu, nikapata pesa kidogo, na ndiyo niliyoanzia biahara ...nikafungua duka kwa kuanzia kwa vifaa kidogo, na nilivyoona nikaanzia kwa nguo.

Kidogo kidogo kwa shida nikaanza kuzoea, na nikaona sitaweza kufanya hivyo nikiwa na mtoto wakati wote, tukatafuta mfanyakazi wa ndani, na hapo nikaweza kutoka kwenda kwenye shughuli huku namuachia mfanyakazi huyo mtoto, mambo yakaanza kuchanganya.

Siku moja, shemeji yangu alifika kwangu, na kwa vile alimzoea mtoto, akamchukua na kwenda naye kwake, mimi siku hiyo nilitakiwa kwenda kiliniki, na sikuwa na wasiwasi na shemeji yangu huyo, kwani sio mara ya kwanza kumchukua mtoto.

 Mimi nikiwa na amani kabisa,  nilijiandaa nikaenda kliniki, nilipotoka huko kiliniki, nikapitia dukani kwangu,kuendelea na kazi za dukani, bila wasiwasi, nikifahamu kuwa mtoto yupo kwa shemeji.

Siku hiyo ikanyesha mvua kubwa sana bila matarajio, sikuweza kutoka pale dukani, na mtoto nafahamu yupo kwa watu wazima watamuangalia, nikawa naendelea na kazi.

Nikiwa naendelea na shughuli huku nafsi ikiwa haina utulivu fulani, kama ujuavyo hisia za mzazi kwa mtoto zinakuwepo, huwi na amani kama mtu yupo kwa mtu mwingine, nilikwua siamini...., nilikuwa kama sina amani fulani, nina wasiwasi....,

Mimi nikaona wale ni watu wazima, na kama nitawatilia mashaka, ndio mambo yale yale ya kuzua mambo yaliyopita, na wakati nawaza hivyo, ghafla akaja mfanyakazi wa shemeji yangu akiwa anahema kweli, nikamuuliza kulikoni

‘Funga duka haraka twende nyumbani....’akasema

‘Kuna nini,...?’ nikamuuliza

NB: Je ilikuwaje...


WAZO LA LEO: Kauli ni kitu muhimu sana cha kuangalia, tunapoongea kwa wenzetu, tukawa tunatoa kauli za kejeli, shutuma, kisingizio,tetesi...tuwe makini nazo, kuna watu wanapenda kushinikiza mambo na kudai ni ya kweli, hata kama hazina uhakika...

Tujue huyo tunayemshutumu ni binadamu kama wewe, ana hisia sawa na wewe, je kama wewe ungelishutumiwa hivyo, au kusingiziwa hivyo ungelifurahi...Tujifunze kuwa na kauli nzuri, kwani kauli njema zenye hekima zinamtoa nyoka pangoni.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Baada ya kuona chapisho kwenye mtandao la Jenna kutoka USA akisema jinsi alivyosaidiwa na Dk. DAWN, niliamua pia kuwasiliana naye kwa msaada kwa sababu sikuwa na chaguo nilichotaka ni kumrudisha mpenzi wangu na furaha. Kwa mshangao mkubwa mpenzi wangu alifika nyumbani akiwa amepiga magoti kwamba nitafute nafasi moyoni mwangu kumsamehe, hakika nilistaajabu na kushtuka mpenzi wangu alipopiga magoti akiomba msamaha na mimi nimkubalie tena. Kweli nimepungukiwa na maneno, na sijui ni kiasi gani cha kukushukuru wewe Dr. DAWN. Wewe ni Mungu aliyetumwa kurejesha uhusiano uliovunjika, Na sasa mimi ni mwanamke mwenye furaha. mawasiliano yake ni Whatsapp +2349046229159
dawnacuna314@gmail.com