Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, February 24, 2014

BAADA YA DHIKI NI FARAJA-16



 Kama wiki moja hivi, hali ya mdada ilikuwa tofauti, alikuwa hana habari na mtu, akifika ofisini yeye na kazi, na akitoka kidogo, yupo na gari lake, mpaka nikaanza kujiona mpweke, maana ndiye mtu aliyekuwa karibu yangu na kunifanyia via vya hapa na pale, bosi mara nyingi nakutana naye kikazi zaidi na akipata nafasi ndio ananihadithis visa vya maisha yake.

Mdada alikuwa anaingia ofisini kwangu, akiwa na maswala ya kikazi alikuwa akifika na kunikabidhi stakabadhi za malipo, na san asana ataniuliza;
‘Kuna cha zaidi, kuna lolote kuhusu mimi,...’
‘Hapana hakuna bosi....’nitamwambia na yeye atabenua mdomo kama anacheka , anageuka na kuondoka.

‘Naona mdada kabadilika kweli, yeye na kazi hana utani na mtu, ...’nikamwambia bosi.

‘Ni vyema, kama kaamua kufanya hivyo, ila nahisi gari limenmfanya ahisi tofauti, na hali yake ya kipato sio mbaya, nafurahi kuona wafanyaakzi wangu wanajituma...’akasema bosi.
‘Najisikia mpweke sana maana yeye ndiye aliyekuwa akinichangamsha,pamoja na utukutu wake ....’nikasema kwa utani na bosi akaniangalia nay eye akatabasamu na kusema;

‘Usijali, nafahamu kwanini unajisikia hivyo, pindi ukioa utamsahau kabisa mdada, labda akukoroge kichwa, uingie kwenye mitego yake, ....hata hivyo, na yeye anahitajia kuolewa, ili atulie, ndoa ina siri kubwa sana kwa wenye kuelewa, hebu nikuulize mipango yako ya ndoa bado ipo ..?’ akaniuliza na mimi nikawa kimiya kama nawaza jambo, na kabla sijamjibu akasema;

'Nimekuuliza hivyo, maana sioni maandalizi yoyote, au ni ya kimiya kimiya...?' akaniuliza tena.

'Bado sijajipanga, ni mpaka nifike huko nyumbani....'nikasema

‘Sawa yote ni mipangilioa, na hilo ni muhimu sana katika maisha yetu, ni vyema tukawa na melengo ya karibuni na ya muda mrefu,....mara nyingi tunapoteza muda kwa jambo ambalo halina maana kabisa na ambalo huenda likawa ni hatari kwetu, mimi nakushauri, ....fikria maisha yako ya baadaye acha kumuwazia mdada, mdada ana mambo yake, vinginevyo usema unataka kumuoa yeye.....’akasema na mimi nikamwangalia kwa muda huku nikishindwa hata nimuambie nini.

'Mhh, bosi, nimuoe yeye...?' baadaye nikamuuliza

'Mimi sijui nasema tu...'akasema bosi.

'Bosi, hilo nitakuja kuwaambia, kwasasa nataka nijiweke sawa, mambo yangu mengi hayajawa sawa...'nikasema.

‘Sawa, panga mambo yako ukijua kuwa umri haukungoji, ....umri ni kitu cha ajabu sana, huwa hauna muda wa kumsubiri mtu, kuwa kwa vile hajafanikisha hili basi ukusubiri, hilo halipo, ...umri unapita kama unavyoona saa inavyokwenda, kawaida ya mishale ya saa kama ni nzima huenda mbele, hairudi nyuma, na ndivyo umri wetu ulivyo,  jana tu ulikuwa ukiitwa mtoto, leo wanakuita kaka, kesho baba,kesho kutwa babu,...’akasema bosi.

Boi aliposema hivyo, nilibakia kimiya, nikiwazia, maisha yangu, lini nitaweza kupata angalau kibanda, kodi ya nyumba ndio imepanda, na nilitaka niongee na bosi anifikirie....lakini niliona huo sio muda muafaka, nikatulia nikisubiria bosi atasema nini.

‘Leo sina muda,wa kukusimulia kisa changu,  kesho asubuhi,tutaendelea na kisa chetu, sasa hivi nina kazi nazimalizia, ...’akasema bosi.

‘Sawa bosi maana tumekaa siku sijasikia simulizi la maisha yako, huwa ninapata mafunzo mengi sana,...’nikasema.

‘Ndio hivyo maajabu ya dunia, mambo ya kufanya yapo mengi sana, nawashangaa wale wanaokaa saa nzima wanaongea mambo yasiyo na tija, au wanakalia masaa wakiwateta wenzao, hawajui umri, pumzi, vyote vinakwisha bure...’akasema.

'Haya tutaonana kesho...'akasema bosi na mimi nikaondoka, ....

*****

Jioni hiyo wakati tunaondoka,tukiwa tunatoka ofisini, ikatokea tumeongozana na mdada, alikuwa mbele yangu, na alipofika kwenye gari lake akasimama na kugeuka kuniangalia, alitaka kusema kitu, lakini bado nilikuwa mbali, akapunguza mwendo hadi nikamkaribia, akageuka kuniangalia, akatabasamu, mimi sikusema kitu.

Tulitembea hivyo hivyo hadi akalifikia gari lake, nilimuona kama ana mawazo, na hakutaka kusema kitu, na sio kawaida yake, mara nyingi yeye ndiye huanza kunisemesha, lao alitulia kama sio yeye.

Alipofikia gari lake, akalishutua na remote, halafu akatulia kama kasahau na mimi nikawa nimeshalichukua pikipiki langu nalikokota, kuelekea nje ya maegesho, nilipomkaribia , alikuwa tayari ameshafungua mlango wa gari lake,akiwa hajaingia kwenye gari lake na mimi nikiwa ninampita na pikipiki langu, nikitaka  kuliwaha, mara akakohoa kile kikohozi ya uchokozi.

Nikageuka kumwangalia, akaniangalia, lakini usoni alikuwa kama sio yeye, hatabasamu, hacheki, yupo kimafikara zaidi, na mara akasema;

‘Vipi ile pesa umeifanyia nini?’ akaniuliza, huku akiwa haniangalii, alikuwa sasa anaingia ndani ya gari lake na mimi nikasimama kama mtu aliyeshitukiziwa sikuwa nimelitegemea hilo swali, ...nilisimama huku nikiwa bado nimeshikilia pikipiki langu nikamuuliza;
.
‘Pesa ipi?’ nikauliza nikionyesha mshangao, nilishahisi,  anauliza kuhusu pesa gani, japokuwa sikutarajia kuwa ataniuliza swali kama hilo mahali hapo.

Yeye akawa kimiya akiwa anaweka mkoba wake kwenye gari, na alipomaliza kuuweka mkoba wake kwenye viti vya nyuma kwenye gari lake, alikaa vyema kwenye kiti cha gari lake, na huku akiwa kashikilia usukani wa gari lake,akageuza kichwa kuniangalia, akatabasamu.

Mimi bado nilikuwa nimesimama huku nimehikilia pikipiki langu, nilikuwa bado sijalipanda nikawa nimeangalia mbele, huku nikiwaza, itakuwaje, akianza kuidai ile pesa, hata hivyo, yeye mwenyewe ndiye aliyenipa,..nilikuja kugundua kuwa kaweka pesa hiyo kwenye lile koti langu  bila hata ya mimi kufahamu.

Yeye bila wasiwasi akiwa tayari ameingia ndani ya gari lake, lakini alikuwa hajafunga mlango wa gari lake, alitulia huku akiwa kauinamia ule usukani huku akionyesha tabasamu, akageuza kichwa kuangalia mbele, halafu akageuka kuniangalia tena na akawa sasa analiangalia pikipiki langu.

Mimi, nikaliangalia pikipiki langu, nikijiuliza kwanini analiangalia hivyo, pikipiki langu ambalo nilikuwa nalipenda sana, kwani lilikuwa likinirahisishia safari zangu, nilikuwa sipendi kabisa kupanda magari, kwani ukiwa na pikipiki, huchelewi kwenye safari zako.
Mdada, alipopata hilo gari, alinisihi sana niachane na hilo pikipiki tuwe tunatumia gari lake,  kwenda na kurudi kazini, nilimkatalia.

‘Mimi sitaki kuachana na pikipiki langu,...nashukuru...’nikamwambia.

‘Tatizo lako wewe bado mshamba, kuwa na pikipiki unajiona umefika,...mhh, nahisi ni kwa vile ndio usafri wako uliowahi kuupata kwa mara ya kwanza...’akaniambia, na mimi sikumjibu, nikabakia kimiya,nikiwazaia mbali..........

‘Ok, hamna shiida, ila ukijisikia kupanda gari wewe niambie tu , wewe wangu,...’akasema na mimi sikutaka kuongea naye siku hiyo, kwani zilikuwa ni zile siku ambazo nilikuwa bado na wasiwasi baada ya tukio alilolifanya kwa yule mtu kwa ajili ya kumshinikiza atoe gari lake.

Akiwa bado katulia akiliangalia pikipiki langu mimi nikaanza kulisukuma tayari kuondoka, na yeye akasema;


‘Nimekuuliza swali, hujanijibu unaondoka, una maana gani?’ akauliza kwa sauti ya hasira.

‘Na mimi nimekuuliza swali kutaka ufafanuzi,...maana mimi ni mhasibu ninashughulika na pesa nyingi, sijui unaulizia pesa ipi,.....’nikasema.

‘Una uhakika...?’ akauliza akiwasha vile vidude vya kusafisha kiyoo cha gari.

‘Sasa kwanini usinifafanulie, kuna ubaya gani?’ nikamuuliza

‘Unataka kila kitu niongee kiuwazi upo tayari kwa hilo, mimi siogopi kuongea, usione nipo kimiya, ...nakustahi wewe mgeni wa mambo haya...kama unataka ufafanuzili, naweza kukufafanulia..ndivyo unavyotaka sio?' akaniuliza

'Ndio ili nielewe, nitakujibu kitu ambacho huenda sio...'nikasema

'Ok, kama ndivyo unavyotaka, haya,..nilikuwa nakuuliza hivi, zile pesa ulizochukua kwa ajili ya ile kazi ya usiku umezitumiaje....'akatulia akiniangalia, na aliongea maneno hayo kwa sauti mpaka, nikashituka, na kunifanya niangalia huku na kule, kuhakikisha kuwa hakuna watu wengine.

'Unataka niendelee kufafanua...’akasema kwa sauti, na mimi hapo nikaogopa, nikawa nataka kumwambia nimelewa, lakini nikasema

'Kwanini unafanya hivyo?’ nikamuuliza nikionyesha mshangao

‘Unataka nikuulize tena...?’ akasema akiniangalia kwa uso wa kunisanifu

‘Ina maana kila pesa nitakayopata natakiwa kutoa maelezo kwako kuwa nimeifanyia nini?’ nikamuuliza

‘Mimi nilijua umeitupa au umeitolea sadaka, maana wewe uli-iita pesa chafu,....’akasema

‘Mhh, ni kweli, ...lakini niliwaza sana, nikaona kuwa ni haki yangu kwa vile nilifanya jambo la hatari bila ya mimi kupenda,.....’nikasema kwa sauti ndogo.

‘Unaonaeeh, ..sasa kidogo unaanza kuelewa, usione watu wanadai pesa nyingi ukaona ni wajinga au wanatamaa, ...ni kutokana na hatari ya kazi zenyewe,....sasa basi, natumai pesa ile haikukutosheleza, kufanya hicho ulichokifanya, nina uhakika huo...kweli si kweli...’akasema

'Mhh...'nikaguna

 Ni kweli zile pesa nilishazituma kijijini kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, ...ziliweza kununua kiwanja na kufyatulia matofali,...nakuweka msingi, na hilo lilinifanya nipande chati huko kijijini hasa kwa wakwe zangu. Na hapo nilipo nilikuwa na mawazo jinsi gani ya kupata pesa nyingine, ili niweze kuendeleza hiyo nyumba...kumbe pesa chafu zinaweza kufanya jambo, lakini ...mmh, hapana, sizitaki tena...nikwa najisemea kimoyo moyo

‘Unataka kusema nini?’ nikamuuliza

‘Na kusikiliza wewe, kama una hitaji nyingine useme, ukumbuke yule jamaa hatujamshtua tena,....alichofanya ni kulitoa gari langu, lakini bado hajalipa yale aliyonifanyia,...nataka tumkamue mpaka anione kuwa mimi ni nani, ...watu hawanijui mimi. Mimi ni mtu mnzuri sana, ukiwa huna ubaya na mimi, lakini ukiniingilia anga zangu, ukanichokoza, hutaamini...’akasema na mimi nikabakia kimiya.

‘Kwa ujumla wewe bado hujafanya kazi niliyotaka uifanye, umepokea pesa ambayo hujaifanyia kazi, ...muda sasa umefika wa kuifanyia kazi hiyo pesa, usiona zinaingia tu, ukafikiri ni bure bure,...’akasema huku akitikisa kichwa.

‘Kwahiyo...’ nikataka kusema na yeye akanikatiza kwa kusema;

‘Unakumbuka pale kwenye tukio wewe uliigiza kama mwandishi wa habari, sasa ndio wakati wa kuufanyia kazi huo uandishi wako wa habari, ilikuwa sio njia ya kumtishia tu, bali pia ilikuwa ni akiba ya baadaye, na muda huo sasa umefika, unatakiwa kuufanyia kazi huo uandishi wako wa habari....’akasema

‘Lakini mimi sikupenda iwe hivyo, wewe ndiye uliyeshinikiza mimi nifanye hivyo, na wala ikujua una maana gani, kwahiyo saa unataka mimi nifanye nini?’ nikamuuliza nikiwa na wasiwasi...

‘Usijali, nitakuambia ni nini cha kufanya, uwe tayari kwa hilo,....’akasema huku akiwasha gari lake na kuanza kuondoka, nikabakia pale nimeduwaa, sina hata nguvu ya kuendesha pikipiki, nikajikuta nikijiuliza kwa sauati..

‘Huyu mdada anataka nifanye nini tena..?’ nikajiuliza.

‘Unalo hilo...’sauti ikasika nyuma yangu nikageuka kumwangalia ni nani huyo...

**********


 Mama mkwe alikuwa kanisingizia mimi kuwa eti nimemloga mtoto wake ndio maana mtoto wake siku hizi hamsikii yeye, na mtoto wake hakuwa na tabia hiyo huko nyuma;

‘Mtoto wangu alikuwa na tabia nzuri, nikimwambia kitu ananisikia, lakini alipokuoa wewe tu kabadilika,...nilishamwambia kuwa wewe humfai, kaacha kuoa wasichana wazuri huku kijijini akakimbilia kuku-oa wewe, angalia sasa anavyopata taabu...’akasema mama mkwe.

‘Lakini mama hayo yote ni maisha, mimi sijamfanya lolote mume wangu, na hata mimi ipendi tuihi hivi, lakini nina imani kuwa ipo siku hali itakuwa nzuri....’nikasema.

‘Hali itakuwa lini nzuri, wakati wewe una gubu, ...kabla hajakuoa alikuwa na shughuli yake, alikuwa akitujali, anatusikiliza, sasa hivi kipo wapi,  hata kazi hawezi kupata tena, hana mbele wala nyuma...’akadakia wifi.

‘Lakini sio yeye tu asiye na kazi,mbona wapo wengi wanahangaika, ...’nikajitetea

‘Kwahiyo umemfanya hivyo ili awe sawa na hao wengine wasiokuwa na kazi, ili azidi kuzalilika, ili awe anakusikiliza wewe....’akasema mama mkwe.

‘Jamani hiyo ni hali ya mapito tu, maisha ndivyo yalivyo kuna kupata na kukosa, na kwanini nimfanyie hivyo, wakati ninayeteseka ni mimi na mtoto ...jamani tuacheni imani hizo, sio za kweli, ni uwongo...’nikasema.

‘Wewe ndiye chanzo cha yote haya, umemloga mwanagu,..usiniite mimi ni mwongo, huna adabu kabisa, mimi na utu uzima huu niseme uwongo,...ni kweli wewe umemfanyia kitu kibaya mtoto wangu, sio bure....’akasema mama mkwe .

Kauli yake hiyo ilinikera, hata nilipojaribu tena na tena kuwaelimisha kuwa hayo ni maisha ya kawaida, kuwa katika maisha kuna kupata na kukosa wao hawakinielewa, wanasema wao wamefanya utafiti na kugundua kuwa mimi ndiye chanzo cha matatizo cha mtoto wake.

‘Na ulipokwenda huko kwenu kujifungua, ukaenda kuongezea uchawi wenu, ndio maana mtoto wangu anakuwa kama mjinga, hana kazi, wenzake wanapata kazi, lakini yeye hapati, huoni sababu kubwa ni wewe, angalia sasa nikiongea naye, hanisikii, muda wote anakuwazia wewe, kuna kitu umemfanyia mtoto wangu sio bure...’akasema mama mkwe.

 Niliposikia kauli ile, iliniuma sana, nikaona hilo halitavumilika, mwanzoni nilipanga nikae kimiya kwasababu sio kweli ni fikira zao potofu, na niliogopa kumwambia mume wangu, ili kutomzidishia mawazo ya zaidi. Nilimuonea huruma mume wangu, kwani alikuwa akihangaika kutafuat kazi, ili tupate riziki, nikaona nikimwambia hayo, atazidi kuchanganyikiwa, lakini kauli za mama mkwe zilipozidi, na kufikia kusema hataki kutuona kwenye nyumba kuu, nikaona hilo inabidi tulijadili na mume wangu.

Basi siku hiyo nikapanga kuongea na mume wangu akirudi kwenye mihangaiko yake, kwani hata hivyo kwa kauli ya mama, hatukutakiwa kukaa tena kwenye nyuma ya familia,sasa tutaenda wapi, nilitaka na mimi nifahamu.

Aliporudi mume wangu akahisi kuna jambo, ila mimi sikutaka kumchukulia haraka, nikajifanya hakuna kitu hadi ikafika muda wa usiku wa kulala, ndio nikamwambia mume wangu;

‘Mume wangu eti mimi ni mchawi nimekufanyizia madawa, ndio maana humsikii mama yako...’nikamwambia.
‘Kwahiyo ni kweli umenifanyia hivyo?’ akaniuliza na kunifanya nishituke

‘Wewe unaamini hayo, kuwa nimekufanyia hivyo?’ nikamuuliza

‘Ningaliamini hayo, ningelishakosana na wewe mapema tu, kwasababu hayo nilishaambiwa mapema, hayakuanza leo, lakini kwa vile najua ni uwongo, nimeyapuuzia...’akasema.

‘Wewe unanifikiria mimi nitajisikiaje kuambiwa eti mimi ni mchawi,nimekuloga wewe, hebu fikiria kwa makini kama ungelikuwa wewe ni mimi, ukaambiwa hivyo wakati hujafanya hayo mambo, na hata siyajui yakoje, utajisikiaje?’ nikamuuliza

‘Kama sijafanya nitapuuzia, maana ukihangaika, kulalamika, utaonekana kuwa unaamini mambo hayo,...’akasema.

‘Mimi nimekuwa mvumilivu sana, na nipo tayari kuvumilia mabaya yote ninayofanyiwa na familia yako, ..lakini swala la kuisingizia familia yangu kuwa ni wachawi, hilo limefika mbali, nashindwa kuvumilia...’nikasema.

‘Sasa unataka mimi nifanye nini, na hali yenyewe unaiona, ndio maana mimi nikayapuuzia, maana hayana maana, wewe vumilia tu, yote hayo yana mwisho, ni kwa vile sijafanikiwa kuwa na sehemu yetu...’akasema

‘Wewe unasema nitulie, nivumilie, wakati mama keshasema mimi sitakiwi kukaa kwenye nyumba kubwa, hebu niambie, tutakwenda kuishi wapi..?’nikamuuliza

‘Hilo ni jukumu langu, wapi tutakwenda kuishi, ...kwa hivi sasa hakuna, ila nalifanyai kazi, usijali...’akasema akionyesha kutokujiamini, na mimi nikaona nitulie tu, nione itaakvyokuwa.

Kwa,bahati nzuri kulikua na chumba kimoja cha nje ndio tukahamia mimi na mume wangu, na kuanza maisha mapya humo nikawa nakaa humo na pikia humo nafulia humo yaani kila kitu nilikuwa nakifanyia humo humo, kwenye hicho chumba kimoja, hatukutakiwa kuchangia maeneo mengine.

Ukumbuke kwa kipindi hicho mume wangu hakuwa na kazi yoyote, lakini sikuonyesha tabia ya kulalamika, niliweza kumudu maisha hayo yote, nikavumilia nikijua kuwa mimi ni mkewe, natakiwa kuwa naye bega kwa bega kwa shida na raha. Lakini kwa ujumla maisha yalikuwa kupita kiasi, hatukuwa na chochote cha kupika,na ndani tulikuwa na jiko moja la koili na sufuria moja tu.

Hali hiyo ilikuja kuwa ngumu bila kutarajia kwani ilifikia hatua mie na mume wangu tulishindia vipande vya mkate na maji ya kunywa, zaidi ya mwezi tulikuwa tunakula hivyo hivyo, na ukumbuke mimi bado nilikuwa nahitajika nile vizuri ili nipate maziwa ya kumnyonyesha mtoto. Lakini ningelipata wapi chakula...njaa inauma jamani, isikieni kwa watu....

 Ikaja taarifa kuwa mama mkwe anaumwa, alishaanza kuumwa umwa kidogo kidogo kabla, na nilikuwa nakwenda kumuangalia, na kumjulia hali, lakini hakutaka hata kuongea na mimi, nikajua ni hiyo hiyo kauli yao kuwa mimi ni mchawi, na hata kama kuna kazawadi kadogo  nilipata kama matunda, nikimpelekea, mawifi walipokea nikiondoka kinatupwa nje. Nikavumilia tu, nikijua kuwa yote ni maisha ya ndoa.

Mama mkwe hali yake ilizidi kuwa mbaya, na kila siku ilikuwa ikiongezeka, baada ya mwezi na nusu mama mkwe akafariki na mimi kama miongoni mwa wanafamilia, nikajumuika kwenye shughuli zote za msiba. Lakini kwenye msiba, japokuwa hawakunionyesha moja kwa moja, lakini niliona dalili za kunitenga, hata hivyo sikujali, nikawa najishughulisha kwa kila jambo.

Baada ya shughuli za msiba, kukawa na kikao cha familia, sio kikao rasmi ilikuwa kama sehemu ya kuangalia msiba na mambo mengine, na hapo ndio kukatokea kauli iliyonivunja nguvu kabisa, sikuamini kuwa hata watu wazima, waliolemika kidogo wangelifikia hatua hiyo;

‘Kaka mimi nina uhakika, mchawi wa mama yetu yumo humu humu ndani,...’akasema wifi, wakiongea pembeni.

‘Hayo yaache, tutayaongea baada ya msiba kuisha...’ akasema shemeji yangu mmojawapo.

‘Lakini nyie mna uhakika gani na hilo...?’ akauliza shemeji mwingine alipoambiwa na wifi huyo ambaye ndiye aliyekuwa akiendesha hiyo kampeni.

‘Tumeenda kuangalizia kwa wataalamu, ni tumemgundua mchawi wa mama yetu, yumo humuhumu ndani, mimi sikubali kabisa, mama yetu afe tukae kimiya, kama hamna uchungu na mama mimi nitahangaika peke yangu...’akasema wifi. Wakawa wanaongea hivyo hivyo wao kwa wao, na hadi shemeji zangu hao wakaamini hivyo.

Maneno haya yalienda chini kwa chini hadi yakanifikia,..nikaja kuambiwa wazi kuwa eti mimi ndiye niliyemuuwa mama yao....!

NB: Haya mpendwa anazidi kukabiliwa na majanga, je itakuwaje

WAZO LA LEO: Umasikini ukizidi, hali ngumu za maisha zikizidi, jamii haiwi na amani, na matokea yake, hisia mbaya miongoni mwa jamii hujengeka, watu badala ya kuhangaika na kupambana na adui huyu mkubwa, umasikini,kwa kufanya tafiti sa kisayansi, wakajikita  kwenye kuzalisha mali...kufanya kazi kwa bidii...


Jamii iliyogubikwa na umasikini, kutokana na upeo mdogo wa kuona mbali, watapoteza muda, kuhisiana vibaya, na mara nyingi wengine hukimbilia kwenye hisia za kishirikina, kudhaniana uchawi. Ushirikiana, ni moja ya adui mkubwa wa maendeleo na chanzo chake kikubwa ni adui ujinga. Elimu bora , ndio suluhisho la hili tatizo, ukielemika, utajua chanzo cha tatizo fulani ni nini na jinsi ya kulitatua..
Ni mimi: emu-three

No comments :