‘Unalo hilo....’
Sauti ile ilinifanya
nisimame, japokuwa nilikuwa tayari nimeshaanza kuondoka na pikipiki langu, Niliposikia
sauti ikisema;
Nikageuka kuangalia
kule sauti ilipotokea, nikagundua kuwa ni mmoja wa wafanyakazi wa hapo.
Walikuwa wale jamaa wawili waliokuwa wakipigana siku ile nilipofika kwa mara ya
kwanza, ambao kwa sasa ni marafiki wakubwa, kweli wagombanao ndio wapatanao.
Nikawaangalia, wakija
kwa mwendo wa taratibu huku wameweka vifaa vya kusikilizia muziki kwenye
masikio yao, na vaa yao ndio ile ile ya kizazi chetu, uruali
mlegezo,...japokuwa walikuwa wamevaa kiofizi,...naona, walikuwa wamechelewa
kutoka ofisini, na walikuwa wakija kuchukua magari lao.
Jamaa hawa wawili ni
miongoni mwa wafanyakazi, wanaotoka kwenye familia zenye uwezo, kwani kila
mmoja alikuwa na gari lake, na walilonunuliwa na wazazi wao.Na hapo nikajiuliza
kwanini siku ile walipigana, ...Je ni kweli,walikuwa wakipigana kwa ajili ya
mapenzi , au ni kutokana na mashinikizo mengine, sikupata jibu, na muda huo
walikuwa wameshanifikia.
‘Mhasibu habari za
muda...’akasema mmojawapo, akitoa vile vifaa masikioni, na mimi nikamwangalia
na kusema;
‘Mimi nawaoenea huruma
sana na hivyo vitu mnavyoweka masikioni, kwasasa hamuwezi kuona athari yake,
lakini baadaye asilimia kubwa ya watu wanaotumia hivyo vifaa, watakuwa na
matatizo ya masikio...’nikasema
‘Wee acha longo longo
zako, hivi vimethibitishwa kitaalamu ..hawawezi kuuza vitu kwa watu watumie,
bila kuhakiki usalama wake...’akasema huyo mmojawapo,
‘Hata dawa
zinahakikiwa, lakini zina madhara au sio cha muhimu ni kufuata masharti ya
docta...’akasema mwingine.
‘Kwahiyo mnamaanisha
kuwa wakati mnanunua, mliambiwa havina madhara na docta, hasa wa masikio?’
nikamuuliza
‘Usikwepe hoja, ya
msingi, maana wewe unaangalia upande wetu, hebu tukuulize wewe na mdada
vipi,...maana madhara ya huyo mdada ni makubwa kuliko hivi vifaa, au wewe hilo
hulioni...’akasema mmojawapo.
‘Kwani vipi,....?’
nikauliza
‘Naona wewe
umeshanaswa na mdada....’akasema mwingine.
‘Nimenaswa kwa vipi,
sijawaelewa...?’ nikauliza nikikumbuka kuwa hawa jamaa walipigana kwasababu ya
wivu wa mapenzi, kwahiyo huenda wananiambia hivyo kwa vile wameshaona nipo
karibu na mdada.
‘Mhasibu sisi
tunamfahamu sana huyo dada siku nyingi kabla hujafika hapa, na bahati siku ile
ulipofika nakumbuka sana, ulituona tukipigana, yote hayo yalikuwa ni majaribu
ya huyo msichana, ....’akasema.
‘Ni ujinga wenu,
kwanini mpiganie mtu ambaye wala hakuwa na mapenzi na nyie....wakina dada wapo
wengi wazuri na kila siku wanazaliwa, ...ni ujinga kupigana, eti kwasababu ya
mapenzi...’nikasema.
‘Hahaha, unamuona
mhaibu anajiona mtu wa hekimaaa... hivi tukuulize na wewe ambaye umeingia
kwenye mitego naye, una uhakika kuwa kweli kuwa mdada ana mapenzi na
wewe...maana yaliyotukuta sisi, tunaona ndio yamekukuta na wewe...’akasema
mmojawapo.
‘Mimi sidanganyiki
ovyo, mimi hayajanikukuta na mna maana gani kusema hivyo.....?’nikajitetea na
kuuliza japokuwa akilini nilifahamu kuwa wanasema kweli.
‘Hata sisi
tulijidanganya hivyo hivyo, kila mmoja akijiona kawini, kumbe tulikuwa
tunajidanganya wenyewe..huyo dada ni mjanja sana, anaweza kuwagonganisha
vichwa, mkachanganyikiwa msijue mbaya wenu ni nani....’akasema mwingine na
kunifanya niwe na hamasa ya kujua zaidi.
‘Hebu niambieni kwani huyu
msichana aliwafanya nini , mpaka mkagombana, maana kama nijuavyo mimi, huyo
mdada hakuwa na mpango na nyie, nyie kwa ulimbukeni wenu, mkahisi anawapenda,
mkagombea kitu ambacho hakipo kwa ajili yenu...’nikasema huku nikajribu
kuwakoga.
‘Ndivyo
alivyokudanganya wewe sio..., kama alivyoniambia mimi kuhusu mwenzangu na kama
alivyomwambia mwenzangu kuhusu mimi, na wewe umeambiwa hivyo hivyo....’akasema
huyo ambaye alionekana muongeaji sana kuliko mwenzake.
‘Kama angelikuwa na
mapenzi na nyie, je mlipogombana yaliishia wapi, mlifukuzwa kazi, je mdada
alikuja kuwatetea....na huko mlipokuwa aliwahi kuongea na nyie, angalau kuwapa
pole....?’ nikawauliza.
‘Tulishaona ujinga
wetu upo wapi, na baada ya lile tukio, tulikutana, ofcourse, wazazi wetu
walitukutanisha, tukaongea na busara za wazazi zikatuingia, ndio maana hatukuwa
na mazoea naye tena, japokuwa limetuuma sana, na ipo siku...’akasema huyo
mwingine, na akakatisha, kwani simu yake ilikuwa ikiita.
‘Hatusemi kuwa huyo
mdada anatupenda au anatujali,...inawezekana kweli ikawa hivyo kwa tamaa zake,
lakini sisi tunafahamu fika, alitutumia sisi ili kufanikisha malengo yake, na
kweli alitupata kilaini,...’akasema huyo mwingine.
‘Ina maana aliwafanyia
nini, mpaka mkakubalia kufanya kile alichokitaka?’ nikawauliza
‘Hicho hicho
alichokufanyia wewe....tunafahamu kabisa atakuwa kafanya hivyo, ndio mtegeo
wake ulipo,..alitutege, kila mmoja kwa wakati wake, akijua kabisa kuwa familia
zetu zina uwezo, na zipo kwenye nafasi ambayo, akitoa huo uchafu wake, itakuwa
kasheshe....tulitoboka kweli...hilo tunakuambia kama kukuonya ...’akasema.
‘Ubaya wako wewe
unatuona sisi ni hatuna subira,...nikuambie ukweli, huyo mdada ni mjanja kweli,
kutokana na urembo wake, ni rahisi sana kumnasa yoyote...sio siri,..’akasema
huyo mwingine.
‘Naona na wewe
umeingia kichwa kichwa, ukaona umepata mrembo, haya endelea naye, sisi hatuna
shida naye tena...’akasema huyo mwingine.
‘Hata hivyo, kuna kitu
tunajiuliza ni kwanini kakuchagua wewe, maana kiukweli, sizani kama una utajiri
huo anaoutaka yeye,...tumjuavyo huyu dada, anapenda pesa sana, dau lake io
mchezo, na ni mjanja kweli, anakulia pesa, na hupati chochote kwake, zaidi ya
kukurembulia...’akasema huyo mwingine.
‘Au mwenzetu
ulibahatika...mmh, sizani, pale hupati kitu, ni mwongo, mjanja, na tapeli wa
hali ya juu,...atakuliza, huku anakucheka, na ukiktaa kufanya anavyotaka, kama
keshakuingiza kwenye mitego yake, atahakikisha anakuharibia kila kitu..hilo
tunakupa kama onyo...’akasema
‘Onyo, onyo...onyo...kwanza
nashukuru kwa kunzarau kuwa mimi sina lolote kwake, sina utajiri kama mlio nao
nyie..its okey, lakini mimi nina akili zaidi yenu, hamjui nimepanga nini kwenye
akili yangu, mimi nawazidi kiumri, nafahamu mengi zaidi yenu...’ nikasema
nikajaribu kujiaminisha.
‘Kuna wazee, wenye
wake zao, wamelizwa, semebuse wewe, umri sio tija, ...kama ulikosea awali,
akakuingiza kwenye mitego yake, hubanduki, kama unabisha kataa anavyokuagiza,
....tunakuhakikisha, hayo machafu yako yote yatafika kwa watu
unaowaheshimu,...na kama ulikuwa na mpango wa kuoa huko kijijini, ujua
utavurugiwa, sizani kama huyo binti wa kijijini ataona hayo machafu aendelee
kuwa na wewe....sijui, maana tusiseme mengi....’akasema mmojawapo.
‘Mimi bado najiuliza
mdada, ana kitu gani anatafuta kwa huyu jamaa?’ yule mmojawapo akawa anamuuliza
mwenzake.
‘Kwanini unasema
hivyo?’ mimi nikauliza.
‘Tuseme ukweli, wewe una
nini cha maana, una mali gani za kumfanya mdada akutake wewe, familia yenu ina
uwezo huo....hapana, tumekuchunguza tumegundua huan lolote, ndio maana
najiuliza huyu mdada anakutakia nini wewe...’akasema na kabla sijaongea kwani
niliona wanaanza maneno ya kashifa huyo mwingine akasema;
‘Sio kwamba
tunakuzarau mhasibu wetu, ila tujuavyo mdada anatafuta watu wenye uwezo ili
kujinufaisha, sasa wewe unayo mali, au ni hicho cheo cha uhasibu...ili akutumie
kuhujumu mali ya kampuni...?’ akauliza
‘Mimi hayo siyajui,
mnasema nyie...’nikasema huku nikiona hakuna haja ya kuendelea kuongea na wao
‘Aaah, mhaibu
tuliongee hilo kwa nia njema, je umeshanawa..kama keshakutega basi, huna jinsi,
lakini kama bado hujaingia kwenye mitego yao, chondechode, mkwepe huyo
mdada....’akasema huyo mwingine.
‘Huyu keshanaswa
bwana, hukusikia tetesi kuwa aliandika hundi bandia kwa ajili yam dada,
...mhasibu mzima anaweza kufanya kitu kama hicho, kama sio kwa shinikizo...mimi
nina uhakika mhasibu keshaingia kwenye mtego, na kama ni hivyo huna ujanja...’akasema
‘Hivi mnaniona mimi ni
mjinga sana...eeh, kwa taariaf yenu, mimi huyo mdada hanibabaishi, uzuri wake
kwangu ni sawa na maua mazuri ya waridi, yanavutia, lakini nafahamu kuwa huo
mvuto ni wa muda tu,....’nikasema na huyo jamaa mwingine akacheka na kusema;
‘Kama ulishaingia
kwenye mitego yake, jaribu kukataa, hebu jaribu ili uone atafanya
nini..mwenzangu hapa alijaribu, ...huko kwao akienda sasa hivi anaingia usiku,
mtaa wote wanamfahamu kuwa ana....’kabla hajasema mwenzake akamziba mdomo.
‘Hebu acha upuuzi huo,
..hujui unavyoniumiza....yaani hapa nilipo nina kisasi na huyo mdada,
kaniharibia kila kitu, ...nilikuwa na mpenzi wangu nampenda sana, kafanya
nikosane anye kabisa...alichonifanyia kilisababisha mimi na wazazi wangu tukosane,
...imechukua muda sana, kwa wazazi wangu kuniamini tena...na sio kama
zamani....sijui nitafanya nini ili nilikoshe jina langu,...’akasema
‘Ni ujinga wenu...’nikasema
‘Kama ni ujinga wetu,
jaribu kukataa atakavyokuagiza huyo mdada...hebu jaribu, wewe siunajiamini,
jaribu...’akasema huku akiniangalia kwa ushahibiki na mwenzake akasema;
‘Kwa mfano, kama leo
kakuambia ukafanye jambo fulani, au siku yoyote , ili kuthibitisha maneno yetu,
hebu lipinge, usifanye, uone...hahaha, nakuambia ukweli, kampuni yote itaona
uchafu wako, ..na huko kijijini, utahama kabisa...hebu jaribu, tuone video ya
bure...hahaha mhaibu utaumbuka....’akasema na kucheka kwa kebehi.
‘Achenani na mimi,
mimi nina akili zaidi yenu, ...ninafahamu wapi pa kumpatia huyu binti, nyie
mtaona, dawa yake ipo jikoni....’nikasema huku nikianza kuondoka.
‘Hahaha, masikini
mhaibu, kachoooka...’wakasema na kuangua kicheko, na mimi akilini nikawa
nimejawa na hasira,...lakini sikuwa na la kufanya...
********
Usiku nilikuwa
nimetarajia kupata simu toka kwa mdada, labda kunihitajia kufanya jambo fulani
kama alivyosema, lakini haikuwa hivyo, hadi kunapambazuka, na asubuhi nikawahi
kazini,....wakati napita kwa wauza magezeti, nikaona watu wamejazana,
wanaanglia magazeti ya udaku.
Nikavutika na kwenda
kuangalia, na mbele kabisa niliona picha ya jamaa ikiwa ukurasa wa
mbele...akiwa uchi, lakini sehemu ya mbele, akawekea alama ya kizuia,
asionekane sehemu zake nyeti, na maandishi yakisema;
Mtu mashuhuri anaswa
akifanya uchafu kwenye hoteli, na mwandishi wetu wa mashahuri akamnaa taarifa
zake kamili zitakuja hivi punde...nikaona herufi mbili za majina yangu japokuwa
jina halikukamilika, kuonyesha kuwa ni alama za huyo mwandishi ili picha hizo
zisinakiliwe.
Mwili mzima uliniisha nguvu, nikabakia
nimeduwaa, sikujua nimesimama kwa muda gani pale, ila baadaye simu yangu
ikaingia ujumbe, ulikuwa hauna namba ya mtumaji, nikashituka na kuufungua huo
ujumbe,...
‘Kazi yako mwandishi
imeanza kufanya kazi, jamaa kajifanya mtata, na huo ndio utangulizi
wake....kesho tunaweka kubwa lake...vinginevyo afanya nitakavyo mimi, nimemdai
pesa kidogo tu, milioni kumi na tano, kwake yeye ni vijisenti, akanitumia
milioni tano, hiyo tutagawana vipi....
‘Tunaweka...na nani
...huyu mdada ana maana gani, anafanya mambo yake, halafu ananihusisha
mimi...sikubali, sasa hii imevuka mpaka....’nikasema na kukimbilia ofisini.
Nilipofika ofisini,
hilo ndilo lilikuwa gumzo, watu wanamuongelea huyo tajiri, mtendaji mkuu wa
sehemy nyeti za serikali, kakutwa akifanya uchafu ...na kila mmoja aliongea leka,...nilikuwa na wasi
wasi, kuwa huenda wakanihisi na mimi kuwa ninahusika.
Nilifanya kazi nikiwa
na mawazo mengi, nikikumbuka maneno ya wale jamaa wakiniambia;
‘Kwa mfano, kama leo kakuambia ukafanye jambo fulani, au siku
yoyote , ili kuthibitisha maneno yetu, hebu lipinge, usifanye, uone...hahaha,
nakuambia ukweli, kampuni yote itaona uchafu wako, ..na huko kijijini, utahama
kabisa...hebu jaribu, tuone video ya bure...hahaha mhasibu utaumbuka....
`Ina maana hata mimi
nikikataa kufanya atakavyo mdada, na mimi nitatundikiwa hadharani....?’
nikajiukuta najiuliza na mara sauti ikasema nyuma yangu.
‘Ndio maana yake, na
saa hivi nina usongo na wewe, jana ulikuwa ukiongea nini na wale vibaka?’
ilikuwa sauti akiwa nyuma yangu.
‘Vibaka gani?’
nikauliza
‘Unajifanya
hukumbuki...nikukumbushe...’akasema akichukua simu yake, na mimi nikamsogelea
na kusema;
‘Mdada hebu tafadhali
achana na mambo hayo, sijasema sikumbuki,..kwani nimekufanyia nini mpaka utake
kufanya hivyo, wao walikuja na kuanza kuongea na mimi, hatukuwa na nia mbaya na
wewe...’nikajitetea.
‘Nina hasira sana leo,
naweza kufanya kitu mbaya,..lakini tuone jinsi gani huyu mshamba atakavyofanya
nimempa masaa, asipotuma hiyo pesa, namuumbua, yeye,a anjifanya anazo, kuwa
atanimaliza, kama alivyodai, ..naafanay atakavyo aone vumbi langu...’akasema na
mara bosi akaingia.
‘Kuna nini?’ akauliza
‘Hakuna kitu bosi
tunaongea tu...’nikasema na mdada akaondoka.
Baadaye bosi akaniita ofisini kwake;
‘Mhasibu uwe makini
...sasa hivi dunia imeharibika, siwezi kuamini, yule jamaa wa uhuru wa magari,
kakutwa mahotelini akifanya uchafu, nasikia wamemtoa kwenye magazeti ya
udaku....’akasema
‘Jamaa gani huyo?’
nikauliza
‘Kuna jamaa mmoja mtu
wa heshima zake, ana utajiri sana, na yupo kwenye idara nyeti naona watu wa
udaku wamemnasa, nyie wanaume mna nini, kwasababu jamaa ana mke wake mzuri tu,
ana pesa,....na ana kazi nzuri,...kwanini ajizalilishe vile,...namsikitikia
sana, kwani huenda akaondolewa kwenye hicho kitengo, kama ikigundulikana ni
kweli...’akasema bosi.
‘Ina maana kwa ajili
hiyo anaweza kuondolewa kazini?’ nikauliza
‘Ile ni kashifa mbaya,
na kitengo hicho kinataka watu waadilifu, kama unadiriki kufanya huo uchafu,
utaaminikaje,...anaweza haat kufukuzwa kazi...’akasema bosi.
‘Na hao watu
waliofanya hivyo, hawaogopi, maana mimi naona ni hatari..’nikasema
‘Ni hatari kweli,
jamaa yule anaweza akaua...japokuwa ni kashifa zaidi, lakini tumbe mungu yaishe
salama...’akasema bosi
‘Baadaye tutaendelea
na simulizi letu...’akasema bosi
Siku hiyo nzima sikuwa
na raha, nilikosa amani kabisa, niliogopa, kama huyo jamaa atakuja kunitambua
kuwa mimi nilikuwepo siku hiyo ataweza kunimaliza....japokuwa ankumbuka siku
ile nilivaa mawani yangu ya kuendeshea pikipiki, ili kuficha sura, lakini kwa
wataalamu wa kuangalia sura na amumbile ya watu wanaweza kunigundua...sasa
nitaishije, mbona maisha yangu yanakuwa ya mashaka, nifanye nini......
Baadaye bosi akaniita na kuanza kunisimulia
kisa cha maisha yake..
********
Kuna mambo ukiyasikia
kwa wenzako unaweza ukayazarau na kusema hayana maana ni mambo ya kuzarau tu,
...unaweza ukasema hivyo kwasababu hayajakukuta wewe,...hata mimi nilipokuwa
nisikisia mtu akilalamika kuwa kasingiziwa ubaya, na akawa analalamika,
nilimuona ni wa ajabu sana, na
nitamwambia;
‘Kama hujafanya una
wasiwasi gani....’
‘Lakini yakukute wewe,
unaambiwa wewe umeiba, wakati hujaiba, ...unaambiwa wewe ni mchawi, wakati,
huujui hata huo uchawi upoje...hebu fikiri wale wazee , vikongwe, wanaofikiwa
hata kuchomwa moto, au kuvunjiwa nyumba zao, kwa kusingiziwa uchawi,..kumbe
wengine hawana makosa masikini ya mungu.
‘Hebu fikiria mimi
yamenikuta hayo nasingiziwa kuwa mimi ni mchawi, nimefikia hatua ya kumuua mama
mkwe,..wakati hata huo uchawi wenyewe nausikia tu watu wakiuongelea, siujui
hata upoje, au watu wanafanya nini ili kumloga mwenzake,...watu wameenda huko
kwa wanaoitwa wataalamu wamedanganywa kuwa mchawi wao yupo humo humo ndani,
yupo hivi ha hivi, anafanana hivi na vile, wakaniona ni mimi
‘Usiombe, kusingiziwa mambo kama hayo,
yanauma, na yanakufanya usiwe na amani kabisa, ...’akatulia.
‘Shutuma za kuwa mimi
nimemfanyia uchawi mume wangu anipende, asiwapende ndugu zake, asiwasikilize
wazazi wake,....niliziona ni za kupita tu, lakini, hizi zilizokuja kuwa eti
mimi ndiye niliyemuua mama mkwe wangu, zilinichanganya kichwa kabisa nikawa
sina furaha wala amani.
‘Nikawa najiuliza
mwenyewe iweje watu wanifikirie mimi hivyo, mimi nipoje, ..ina maana mimi nina
nguvu za mungu za kumtoa kiumbe roho, sijamtilia sumu, au kumuua kwa silaha,
mama huyo kafa kwa ugonjwa, na madocta wamesema hivyo, huo uchawi umetoka wapi...sikuelewa.
Yaani shutuma hizo
zilivyoletwa, zilikuja kama shutikizo kwangu, ni kitu ambacho sikukitegemea
kabisa,maana kwa ahli ya kawaida, wengi wanasingiziwa mambo hayo ni watu
wazima, wazee, lakini mimi....hapana,..sikuelewa,..nikawa nimechanganyikiwa
hata sikujua nijitetee vipi...nikawa sijiamini, niliona kama kila mtu
ananiangalia kwa jicho la ubaya,....sikuwa na amani kabisa.
Haikupita muda, tetesi
hizi zikazagaa, na wanafamilia wakataka kuitisha kikao ili eti waniweke kitako waniulize kuhusu shutuma hizo,
lakini kuna rafiki yake mume wangu akakataa kabisa kufanyika kwa hicho kikao. Akiwaasa
kuwa hizo ni shutuma mbaya, hazina ukweli,na wakifanya kama hicho kinaweza
kuzua mtafaruku kwenye familia.
‘Jamani kufa ni
matakwa ya mungu, mtu siku zake zikifika hata mfanye nini, atakufa tu, hakuna
mwanadamu mwenye mamlaka hayo,...msikimbilie shutuma za kushukiana uchawi,
mtagombana bure, na kuanzishiana chuki zisizo na ukweli...’akawaambia.
‘Wewe unasema tu kwa
vile sio mzazi wako...kama ingelikuwa ni mama yako,ukasikia hivyo usingelikaa
kimiya, nina imani ungelihangaika...’akaema mmoja wa shemeji zangu.
‘Jamani hayo mambo
yamepitwa na wakati, hivi imani zenu kwa mungu zipo wapi, hivi mnaamini kuwa kweli
kuna mtu anaweza kufanya uchawi kumuua mwenzake..kama watu hao wapo wana uwezo
wa kufanya hivyo kwanini wasiende benki wakachukua pesa wakawa matajiri?’
akauliza.
‘Wewe wasema tu
kwasababu hayajakukuta, ....’akasema wifi
‘Mimi sikubali hilo
lazima lifanyiwe kazi...lazima mchawi wetu aumbuliwe, tumkalishe kikao asema
ukweli...’akasema wifi mwingine.
‘Jamani hayo yote
hayatasaidia kitu, je hilo litasaidia kumrejesha mama duniani, mama yetu
ameshafariki, hata tufanye nini hatarudi tena duniani...cha muhimu kwa sasa ni
kumuombea mzazi wetu huyo aishi mahala pema peponi sio kugombana...’akasema
huyo rafiki wa mume wangu.
Baada ya malumbano ya
muda mrefu, watu wakatawanyika bila maafikiano, na mambo yakawa yameisha hivyo
kimiya kimiya, kila mtu akiwa na lake moyoni.
Siku zikapita japo
kinyongo na kijicho dhidi yangu kiliendelea kuwepo, lakini siku zilivyozidi
kwenda, hali hiyo ikawa kama inasahaulika kidogo kidogo. Na maisha yakaendelea.
Pamoja na maisha
magumu, lakini nilijitadi sana, kuwa karibu na mume wangu, kumpa matumaini,
kuwa hayo yote ni mitihani ya kimaisha, na kumuasa kuwa hayo wanayosema watu
sio kweli, cha muhimu ni kumwamini mungu tu.
Sijui ilitokeaje, maana na hii ilikuwa kama moja ya mashtukizo
kwangu, sikutarajia kabisa, ilikuwa kipindi moto wangu anakamilisha mwaka,
nikahisi mabadiliko mwilini, nikawa sijiamini, nikaona niende kwa docta,...oh,
docta akasema nina mimba,, sikuamini ...
‘Docta sasa mtoto
wangu ndio ana mwaka mmoja, nifanyaje...?’ nikamuuliza.
‘Hakuna shida, ni kiai
cha kujipanga, ukijua sasa unatakiwa ule vyema, na wakati huo huo usimsahau
mtoto...maana bado mdogo...’akasema docta.
‘Na ujitahidi sana
kuja kiliniki, ili upate ushauri, ...’akasema docta.
‘Docta hakuna njia
nyingine....’nikasema na docta akasema
‘Imeshatokea hakuna jinsi
inabidi ulee mimba yako, na uwe makini kumpa mtoto wako huyu mdogo vitu vya
kumsaidia..ili akue vyema,....’akasema docta, na kunishauria sana nisije
nikafanya makosa eti ya kuitoa hiyo mimba.
Basi kutokana na
ushauri wa docta nikaona niendelee kuilea hiyomimba yangu. Na wakati huo bado
nilikuwa kwenye kile kile chumba kimoja na hali ilikuwa haijabadilika.Maisha
bado yalikwua yanandelea kuwa magumu.
Nilipoona hali inazidi
kuwa ngumu, na kama nitaendelea kumtegemea mume wangu tu, nitazidi kuumia, na
mimba ndio hiyo inazidi kukua, ndio hapo likanijia wazo la kujishughulisha..hulka
za familia yetu ni biashara, na hilo lilikuwa kwenye damu, nikaona kwanini
nisijaribu.
Nikaona hiyo ndio njia
pekee ya kunisaidia ili niweze kujikimu,..kuanzisha biashara, wazo hilo
likanijaa akilini, na nikavutika nalo, nikaanza kujipanga nianze vipi, maana
biashara inahitaji mtaji, inahitaji sehemu ya kuanzia, mume wangu hana mbele
wala nyumba, sina mtu wa kumkopa,shemeji zangu hawawezi kabisa kufanya hivyo,
sasa nitafanyaje hiyo biashara.
Nikawaza sana, na
mwisho wake, nikakumbuka, kuwa nina vitu vya dhahabu, nilivyowahi kupewa kama
zawadi , nilichofanya ni kanza kuviuza hivyo vitu vyangu vya dhahabu, nikapata
pesa kidogo, na ndiyo niliyoanzia biahara ...nikafungua duka kwa kuanzia kwa
vifaa kidogo, na nilivyoona nikaanzia kwa nguo.
Kidogo kidogo kwa
shida nikaanza kuzoea, na nikaona sitaweza kufanya hivyo nikiwa na mtoto wakati
wote, tukatafuta mfanyakazi wa ndani, na hapo nikaweza kutoka kwenda kwenye
shughuli huku namuachia mfanyakazi huyo mtoto, mambo yakaanza kuchanganya.
Siku moja, shemeji
yangu alifika kwangu, na kwa vile alimzoea mtoto, akamchukua na kwenda naye kwake,
mimi siku hiyo nilitakiwa kwenda kiliniki, na sikuwa na wasiwasi na shemeji
yangu huyo, kwani sio mara ya kwanza kumchukua mtoto.
Mimi nikiwa na amani kabisa, nilijiandaa nikaenda kliniki, nilipotoka huko
kiliniki, nikapitia dukani kwangu,kuendelea na kazi za dukani, bila wasiwasi,
nikifahamu kuwa mtoto yupo kwa shemeji.
Siku hiyo ikanyesha
mvua kubwa sana bila matarajio, sikuweza kutoka pale dukani, na mtoto nafahamu
yupo kwa watu wazima watamuangalia, nikawa naendelea na kazi.
Nikiwa naendelea na
shughuli huku nafsi ikiwa haina utulivu fulani, kama ujuavyo hisia za mzazi kwa
mtoto zinakuwepo, huwi na amani kama mtu yupo kwa mtu mwingine, nilikwua
siamini...., nilikuwa kama sina amani fulani, nina wasiwasi....,
Mimi nikaona wale ni
watu wazima, na kama nitawatilia mashaka, ndio mambo yale yale ya kuzua mambo
yaliyopita, na wakati nawaza hivyo, ghafla akaja mfanyakazi wa shemeji yangu akiwa
anahema kweli, nikamuuliza kulikoni
‘Funga duka haraka
twende nyumbani....’akasema
‘Kuna nini,...?’
nikamuuliza
NB: Je ilikuwaje...
WAZO LA LEO:
Kauli ni kitu muhimu sana cha kuangalia, tunapoongea kwa wenzetu, tukawa
tunatoa kauli za kejeli, shutuma, kisingizio,tetesi...tuwe makini nazo, kuna
watu wanapenda kushinikiza mambo na kudai ni ya kweli, hata kama hazina
uhakika...
Tujue huyo tunayemshutumu ni binadamu kama wewe, ana hisia sawa na
wewe, je kama wewe ungelishutumiwa hivyo, au kusingiziwa hivyo ungelifurahi...Tujifunze
kuwa na kauli nzuri, kwani kauli njema zenye hekima zinamtoa nyoka pangoni.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Baada ya kuona chapisho kwenye mtandao la Jenna kutoka USA akisema jinsi alivyosaidiwa na Dk. DAWN, niliamua pia kuwasiliana naye kwa msaada kwa sababu sikuwa na chaguo nilichotaka ni kumrudisha mpenzi wangu na furaha. Kwa mshangao mkubwa mpenzi wangu alifika nyumbani akiwa amepiga magoti kwamba nitafute nafasi moyoni mwangu kumsamehe, hakika nilistaajabu na kushtuka mpenzi wangu alipopiga magoti akiomba msamaha na mimi nimkubalie tena. Kweli nimepungukiwa na maneno, na sijui ni kiasi gani cha kukushukuru wewe Dr. DAWN. Wewe ni Mungu aliyetumwa kurejesha uhusiano uliovunjika, Na sasa mimi ni mwanamke mwenye furaha. mawasiliano yake ni Whatsapp +2349046229159
dawnacuna314@gmail.com
Post a Comment