Kwa mara ya kwanza
nilianza kuingiwa na wasiwasi na mambo ya mdada, nilijiona nimewekwa kama ngao,
na kutumiwa kama mpini wa shoka, ...nikawa kila mara nikiikia simu,naogopa nikijua inatoka kwa mdada, na hata nilipopigwa na watu wengine, nilihisi kuwa ni
yeye, nikawa naogopa kupokea.
Kutokana na hiyo hali
nikaona ni bora niongee naye nione jinsi gani nitaweza kuondokana na hiyo
hali,lakini nitamuanzia vipi, kwani nafahamu kabisa nikijifanya ni mnyoge kwake,
ndio atazidi kuvimba kichwa na kuzidi kunizihaki, na nikijifanya ni mkali kwake, anaweza kuniumbua kwa kuyatuma hayo mapicha mabaya,
.
'Kwahiyo nifanyeje...?' nikajiuliza.
Simu yangu ya mkono ikalia, nikashtuka hadi kuidondosha chini, na nilipoangalia mpigaji nikaona ni matangazo ya biashara ya makampuni ya simu. Kwa hali iliyofikia,
ninaweza kushikwa na ugonjwa wa shinikizo la damu, kwani mawazo, wasiwasi, na kutokujiamini, vilikuwa vimeteka hisia yangu, japokuwa kichwa
kilikuwa hakiumi kama zamani, naona kilishaanza kuniachia.
'Sasa nifanyeje,....?' nikaendelea kujiuliza
'Au nikatae kumtii,
nione kutatokea nini, mhh, hilo siwezi, nafahamu kabisa kwa mdada nikikataa, muda huo huo atayatuma hayo mapicha.
Nikashika kichwa nikiwaza, halafu nikawa naongea peke yangu kwa kusema;,
'Au niongee na baba mkwe wangu nijaribu kumuelezea hali halisi, ili
hata mdada akipeleka hayo mapicha, ajue jinsi gani ya kunisaidia, lakini je ataniamini ...hilo la kuongea na wakwe zangu,
nililiona halifai kabisa ni kujiabisha...namfahamu sana baba mkwe, ataniuliza maswali mengi ambayo yatakuja
kuniumbua.
Wakati nawaza hili na lile mara akilini, nikakumbuka onyo kutoka kwa wale wahanga wawili wa huyu mdada;
‘Kama ulishaingia kwenye mitego yake, jaribu kukataa, hebu
jaribu ili uone atafanya nini..mwenzangu hapa alijaribu, ...huko kwao akienda
sasa hivi anaingia usiku, mtaa wote wanamfahamu kuwa ana.....
‘Mtaani kote
wanamfahamu kuwa ni nani....’ hapa alikuwa na maana gani, kuna nini alifanyiwa
huyu jamaa, ....huenda alifanyiwa mabaya zaidi yangu...'nikawa naongea peke yangu.
'Mhh, hebu niangalie , mfano nikimkatalia, atakachofanya ni kupeleka hizo picha kwa baba mkwe, baba mkwe
kwa vyovyote ataniuliza, nitamuambia nini, nitamuambia ni uwongo, mmh, yale mapicha yalivyo yanaonyesha kila kitu, lakini baya zaidi, nafahamu kwa kunikomoa atayasambaza hayo mapicha kwa kile anayemfahamu kuwa ni mtu muhimu kwangu, hadi kwa mchumba wangu,...oh, nimekwisha, ...
'Mhh, hapa sasa sina ujanja..'nikasema
'Baya zaidi baba mkwe anamtumia mdada kunichunguza nyendo zangu, kwahiyo anaaminika zaidi ya kwangu, kwahiyo kwa mdada ni rahisi kabisa
kuniharibia maisha yangu...haiwezekani, ni lazima nifanye jambo, ni lazima
niyanyamazishe haya mambo,...na ili nifanikiwe, ni mpaka nijua wapi alipoficha
hayo mapicha.
'Ni lazima nitafute dawa ya hili tatizo,...sasa ni dawa gani?' nikajiuliza na kujiuliza swali hilo hadi nikahisi kichwa kinazunguka.
Wazo likanijia kuwa
huenda kayahifadhi hayo mambo yake kwenye simu yake na kwahiyo nimvizie akiwa
ofisini niichukue simu yake bila kujua nifute kila kitu...lakini sizani kama
simu yake hiyo inaweza kuhifadhi hayo madude yote, ni lazima kahifadhi kwenye
mtandao. Kama ni kwenye mtandao itakuwa ni vigumu sana, kwani ni mpaka nijue
anavyoingia. ...simu ilinishitua, ulikuwa ujumbe wa maneno unaingia,
nikaufungua nikiwa na tahadhari, ulikuwa ukisema;
‘Jiandae, jamaa kama
hataleta pesa leo, kama alivyoniahidi, kesho natoa kubwa lake..uwe makini na
nyendo zako..’ujumbe hauna namba, nikafahamu kabisa unatoka kwa mdada, hapo
nikazidi kuchanganyikiwa
‘Sasa nifanyeje,...’nikajiuliza
na baadaye simu yangu ikaita, nikapokea,
‘Ujumbe huo ni muhimu, kuwa makini, ...hata hivyo naona aklainika, nimemtumia kombora moja, kashikwa na kimuhe muhe, .'akasema na mimi nikawa kimiya.
'Sasa sikiliza nataka uje
hapa hotelini haraka, nimepanga kukutana naye huyu mtu, kasema atauleta huo mzigo
wangu hapo, lakini simuamini, .....’akasema
‘Sasa mimi nije
kufanya nini, ....?’ nikauliza nikitamani nizame ardhini.
‘Hivi nilikuambia
nini, ...unatakiwa uifanyie kazi pesa unayoipata, pesa haipatikani kirahisi
kihivyo...uje haraka, sitaki maswali...’akakata na mara ujumbe wa simu
ukaingia, nilipofungua nikakutana na yale mapicha mabaya, kwa haraka
nikajiandaa na kuondoka kuelekea huko hotelini.
‘Sasa naona ili niweze
kufanikiwa kumpata huyu mtu, ni lazima niwe karibu naye, nikigundua tu ni wapi
anaficha siri zake, basi nitahakikisha nazifuta zote, halafu na mimi naanza
kivyangu,..ikibidi ni lazima niwe ninafika nyumbani kwake, kitu ambacho
sikukipenda, siku zote nakwepa sana kuonekana nyumbani kwake.
‘Ni lazima nijenge rafiki
wa uwongo, ...nitagundua ni wapi anaficha huo uchafu wake...’nikasema kimoyo
moyo, huku nikiwa nimeshatoka nje, na kama kawaida nikakutana na mzee mwenye
nyumba.
‘Kama kawaida yako na
leo una dharura...’akasema
‘Ndio mzee...’nikasema
‘Nikuambie ukweli,
kama huyo mtu anakusumbua niambie nitakusaidia,..mimi najua dawa zao watu kama hao....’akasema
‘Mtu gani huyo mzee?’
nikamuuliza
‘Huyo anayekuita muda
kama huu, mimi nafahamu mambo mengi...maana huyo mtu atakufanya usiwe na amani
katika maisha yako, na nahisi ni mwanamke...’akasema
‘Mzee, ni mambo ya
kikazi tu...’nikasema huku naondoka.
‘Mambo ya kikazi eeh, kazi
gani za usiku, unanitaia mahaka wewe mtu, isije nikawa naficha jambazi kwenye nyumba yangu, ...kila siku usiku una dharura,..ni lazima
niwaambie polisi wakufuatilie...’akasema huyo mzee mwenye nyumba lakini
sikumsikia kwani nilishaondoka kuelekea huko aliponiitia mdada.
*********
Kesho yake nilifika
ofisini mapema, nikiwa bado na usingizi, sikutaka hata kukumbuka mambo ya jana,
na nilielekea moja kwa moja kwenye ofisi yangu, na humo nikakaa na kuinamisha
kichwa ili nipunguze usingizi, na kweli usingizi ukanipitia, tena wa nguvu ...
‘Nikuambie dawa ya huyu
mtu..?' nikaulizwa
'Dawa gani ...?' nikauliza
'Ya huyo mtu anayekusumbua ....dawa yake ni ndogo tu,....’sauti ikaniambia nikageuka kumwangalia huyo mtu, kwani alikuwa akiongea akiwa nyuma yangu. Nikageuka ili nimuone huyo mtu, ...lakini nilipogeuka ikuona mtu yoyote, nikasikia tena nyuma yangu, akiuliza swali hilo hilo, na safari hii nikamuuliza
‘Dawa yake ni nini?’
nikamuuliza lakini nilichosikia ni kicheko, kicheko kiliendelea kwa muda kwenye kichwa changu
mpaka nikajisikia vibaya, na ghafla nikashituka,
‘Wewe vipi unalala
ofisini mpaka unaota,..ndoto za mchana mbaya, ndoto kama hizo zinaweza kukuashiria jambo la kweli, ...kwani unatafuta dawa
ya nani?’ akaniuliza bosi.
‘Dawa, dawa gani?’
nikauliza kwa mshangao huku moyo unanienda mbio,
‘Wakati naingia, bahati nilikuwa naongea na simu, kuna mtu alikuwa akinichekesha kwenye simu,...'akasema.
'Anakuchekesha kuhusu nini?' nikauliza huku nikijaribu kuweka akili yangu sawa.
'Anasema kuwa yule jamaa wa mamlaka
ya ushuru, kakosana na mke wake, ndani ya hiyo nyumba, hakukaliki, na huenda
wakaachana, na wakiachana, ina maana huyo jamaa hana kazi, mke wake ndiye
aliye,mpigia debe hadi kupata hiyo kazi....’akasema bosi.
‘Kwasababu gani?’
nikauliza
‘Si kuhusu ile kashfa ya
kuonekana huko kwenye mahoteli akifanya uchafu wake, ...mke wake kasema
atachunguza mpaka ajue ukweli wake...’akasema bosi.
‘Oh, ndio imekuwa
hayo...’nikasema nikimwangalia bosi kwa mshangao.
‘Dunia hii kuna mambo,mhasibu ukioa tulia na mke wako, kwani hao wanawake wengine wana nini cha zaidi, kitu ni kile kile, cha muhimu ni kuambizana ukweli, kufundisha, wewe unafahamu hiki mfundishe mwenzako, wewe unataka hivi muelekeze mwenzako, ni kazi rahisi tu ...h'akasema bosi.
'Kwahiyo unahisi ni hayo tu...?" nikajikuta nimeuliza hivyo.
'Zaidi ya hayo, kuna watu wametumia mwanya huo,kutafuta pesa, kuna watu wajanja, na si ujanja, ni utapeli...'akasema bosi.
'Ina maana akitoa pesa yatakwisha?' nikauliza
'Nijuavyo mimi, pesa za watu kama hao hazitohi, na watu kama hao, wanahitajia pesa nyingi
sana, maana wanamfahamu kuwa ni mtu wa kuchezea pesa, ....’akasema bosi.
‘Ina maana watu
wanafanya hayo kwa ajili ya kupata pesa, hawaogopi, ...?’ nikauliza
‘Wanaogopa,lakini
wamechukua hatari hiyo mikononi mwao, ...wapo tayari kufa, na mara nyingi
wanawatumia watu wengine, wahusika huwa hawajitambulishi, na hata
wakijitambulisha, ni lazima kuwe na mtu kati, anayetumiwa kama mpini wa
shoka...’akasema
‘Mpini wa shoka?’
nikauliza huku nikijaribu kukumbuka hayo maneno nimeyasikia wapi.
‘Eeeh, ili shoka
likate mti, ni lazima liwekewe mti...unaona, ili huyo mtu afanikiwe ni lazima
atumiwe watu...sasa hao watu wanaotumiwa ndio wanakuwa kwenye hatari, mwenzao
anayeneemeka keshajipanga, anajua jinsi gani ya kujilinda, wajinga ndio
waliowao....’akasema bosi.
‘Mhh, sasa hiyo
hatari....sijui watafanya nini kumkwepa mtu kama huyo...’nikasema kama nauliza
‘Tatizo la ammbo hayo
ukihajiingiza kutoka inakuwa ni vigumu, maana ukijitoa, wahusika watakutilia
mashaka, kuwa unaweza kuwauza, kwahiyo kujitoa kwako ni kuuwawa....’akasema
bosi
‘Unasema kweli..mungu
wangu...’nikasema huku nikisimama na bosi akaniangalia kwa mashaka, na
kuniuliza
‘Vipi kwani, mbona
unanitisha...?’ akauliza bosi
‘Hapana bosi nimesahau
flash yangu nyumbani na ina vitu muhimu sana...’nikadanganya, na bosi
akaniangalia bado akiwa na uso wa kunishangaa
‘Haah, yaani...oh, umenishtua kweli kweli,...ulivyotoa hayo
macho,...utafikiri kuna kitu kibaya umesikia, utadhania unahusika na hayo
tuliyoongea, au mhaibu unahusika nini...?’ akaniuliza akiniangalia kwa
wasiwasi.
‘Hapana bosi...
kuhusika kuhusu nini, ...hapana sio hivyo...’nikawa najiuma uma.
‘Sikiliza mhasibu,
usiwe na wasiwasi na kazi, kama ni hiyo flash,
na ina vitu muhimu huhitajii kushituka hivyo,..., baadaye utaiendea, ila kama
kuna kitu kingine ni bora ukaniambia mapema iwezekanavyo, ili tuone jinsi gani
ya kusaidiana,...’akasema.
Kuna wakati moyo wangu
ulitaka nimuambie bosi wangu kila kitu ili nione kama anaweza kunisaidia,
lakini nilichelea, maana sijui bosi na mdada wanajuana vipi zaidi, naona kama
vile, bosi anamlea huyo mdada kama mdogo wake, ...
‘Leo nitajaribu
kumwambia kidogo...’nikasema kimoyo moyo.
‘Sikiliza mhasibu kama
kuna tatizo kubwa, na unaona upo hatarini niambie mapema kabla halijafika
kubaya, maana ukiingia kwenye matatizo makubwa, mimi sitaweza kukusaidia,
wakati ni sasa...’akasema
‘Bosi, nitakuja
kukuambia tu...lakini..sina matatizo, ni kuchoka tu...’nikasita.
‘Huna matatizo kweli wewe, kwanza nimekukuta
umelala, unaota,..unaweweseka, unaonekana haupo sawa, .....sasa tuanongea, ghafla
umebadilika, na kutoa jicho la uwoga, ni kama vile umeona kitu cha kutisha,
niambie ukweli una tatizo gani...?’ akaniuliza na mara mlango ukagongwa,
akaingia mdada.
‘Bosi samahani
nilikuwa anomba ruhusa kidogo, nimesahau flash
yangu nyumbani,...’akasema na bosi akaniangali, na kusema
‘Wote mumesahau flash, mbona mna mambo...’akasema bosi
‘Nani mwingine kasahau
flash...?’ akauliza mdada, na bosi hakusema kitu akageuka kuingia ofisini
kwake, nikabakia na mdada, na mdada, akaniangalia kwa mashaka, akanisogelea na
kunionyeshea kidole, akasema;
‘Ole wako.....uje
kutoa hata kauli moja, ...utaumbuka, na utakuja kujijutia katika maisha yako
yote...’akasema
‘Kwani vipi?’
nikauliza nikionyesha wasiwasi.
‘Nimesikia bosi
akikuambia umweleze una tatizo gani, sasa ropoka, uone ...nafanya haya kwa
kukusaidia, ile pesa itumie haraka, maana pesa kama hizo, hazina muda,...’akasema
na kunifanya nikumbuke zile pesa alizonipa jana
Mara simu yangu ya
mezani ikaita, nikainua kusikiliza alikuwa bosi akaniita ofisini kwake na mdada
akanisogelea na kunifinya, hadi nikasikia maumivu, halafu akaniogelea na
kunishika, akawa kama anataka kunikumbatia, akasogeza mdomo wake karibu yangu, akama
anataka kunibusu, nikawa nimetulia, .hakunigusa, lakini mapigo ya moyo yalikuwa
yanakwenda mbio kupita kiasi, akaniachia ni kunisukuma;
‘Hahahaha....’, akacheka
na kukiweka kidole chake kwenye mdomo wangu na kusema;
‘Masikini mhasibu
anatia huruma....’. akafungua mlango na kuondoka, na mimi nikainuka kuelekea
kwa bosi.
*******
`Vipi umeshakaa sawa,
maana ulikuwa haupo sawa,..’ akasema bosi.
‘Nipo sawa bosi, naona
usingizi umekwisha niliamuka asubuhi sana, na nilipofika hapa nikaona nipunguze
usingizi, na wakati nimelala ndio nikawa naota ndoto mbaya...’nikasema
‘Ina maana ni ndoto
ndio ilikuwa inakusumbua vile....pole sana, maana kuna ndoto nyingine
zinatisha, au kuna jambo umefanya, maana wewe sasa naanza kukutilia mashaka...’akasema
bosi.
Mimi akilini mwangu
kauli ya mdada ikawa inanijia akilini;
‘huku nikikumbuka kauli yam dada ; Ole wako.....uje kutoa hata
kauli moja, ...utaumbuka, na utakuja kujijutia katika maisha yako yote...’
`Hakuna kitu bosi,
niamini,...’nikasema
‘Sawa... kama una
uhakika na hilo mimi siwezi kukushurutisha, ila kumbuka mapema ni bora kuliko
kuchelewa, kama kuna jambo unalohisi linaweza kukuletea majanga uniambie
,...tuna mwanasheria, anaweza kukushauri kama unaona ni la hatari...’akasema
bosi.
‘Bosi mwanasheria wa
nini, hakuna kitu bosi...’nikasema.
‘Haya ngoja
nikusimulie kisa changu huku unafikiria, ....tuanze pale nilipoishia, pale
alipokuja mfanyakazi wa nyumbani na kusema ni funge duka...’akasema..........
‘Dada funga duka
haraka twende nyumbani.....’akasema huku kashikilia kichwa na anaonekana kama
anataka kulia, nikamuuliza kuna tatizo gani
‘Kwani kuna nini?’
nikamuuliza.
Yule mfanyakazi
akasema wifi yangu alimchukua mtoto wangu na kumfungia nje na mvua kubwa ilikuwa
inanyesha...
‘Unasema nini, ooh, sasa
mtoto yupo wapi...?’nikamuuliza huku nahangaika kutafuta ufungua,
nilishachanganyikiwa na nguvu zilikuwa zimeniishia kabisa, miguu yote ilikwua
inatetemeka.
Kwa hali ile,
sikukumbuka hata kufunga duka, nilikuwa nimechanganyikiwa na kujikuta naacha
kila kitu kama kilivyo na kukimbia nyumani na nilipofika nilimkuta mtoto
anatetemeka nje ya mlango huku kalowa kupita maelezo niliumia sana na nililila
kwa uchungu kweli.
‘Mtoto
wangu..jamani...kwanini mnanifanyia hivi, hivi huyu kiumbe wa mungu kawakosea
nini....’nikamshika na kumkumbatia ili mradi apate ujoto, nikawa nimemshika
hivyo hivyo huku nakimbilia ndani. Mtoto hakuweza hata kutoa sauti, huenda
alilia mpaka sauti ikamkauka.
Kibinadamu sikutarajia
kabisa hilo linaweza kutokea,na wala sikutegemea kuwa shangazi mtu, anaweza
kufanya hivyo kwa mtoto wake,maana shangazi anasimama sehemu ya baba, ...kweli
kumbe mwenye kovu usizani kapoa, kumbe abdo wenzangu wana yao moyoni.
Nilimchukua mtoto na
kukimbia naye ndani nilikuwa nimeshajawa na khofu nikijua kuwa sasa nampoteza
mtoto. Nilikuwa mara kwa mara nikimwangalia na kila nikimtupia jicho naona hali
yake ni mbaya mbaya...siwezi hata kuelezea.
Nilimvua zile nguo
zilizolowana na mvua, na kumvalisha nguo zingine na niliona hazitoshi,
nikachukua na sweta, na nikamlaza kitandani, na kumfunika na blanketi nilikaa
mda huku nalia, kama mtoto, niligeuka kumwangalia mtoto wangu nikaona sasa anapumua
kwa shida sana. Nilipoona hivyo, nikasimama, miguu haina nguvu, nikainama kumtikisa,
niliona kama ndio anakata roho,.
Alipanua mdogo kama
anataka kulia lakini sauti ikawa haikutoka, halafu akalegea na kutulia kimiya,
......
‘Oh, mungu wangu,
mtoto wangu anakufa, ...nisaidie mungu wangu, nimekosa nini oh.....’nikasema
huku machozi yananitoka, na kila ninachofanya hakifanyiki, mfukoni sina kitu,
pesa kidogo niliyokuwa nayo nimenunulia vifaa vya dukani, nitafanya nini...na
nilipotoka kule sikuangalia kama kuna akiba yoyote, nikachanganyikiwa, hata
hivyo nikaona hakuna jinsi ni lazima mtoto apalekwe hospitalini...mvua bado nje
inanyesha kumbwa.
Nikamwangalia mtoto,
bado anapumua lakini kwa shida sana..., nikaona nisitapoteza mtoto, nikakimbia
kama mwehu kutoka nje, bila kujali mvua na kuanza kutafuta usafiri wowote, ili
niweze kumpeleka mtoto hospitali baada ya kuhangaika sana baba moja msamaria
mwema aliniona akashangaakuniona ninavyohangaika na mvua ikininyeshea;
‘Wewe mwanamke vipi
mbona unakimbia huku na kule kwenye mvua?’ akaniuliza kwa sauti.
‘Wewe niache tu,
masikini mtoto wangu anakufa..nifanyeje jamani....’nikasema na yeye akaniuliza;
‘Hebu nieleze mtoto
kafanya nini...?’ akaniuliza na mimi kwa haraka nikamuelezea ilivyokuwa.
‘Dada yangu usijali
nitakusaidia....mimi nina usafiri...’akasema na mimi nikageuka kumwangalia kwa
macho ya kushukuru. Na hapo akaingia kwanye
geti la nyumba yake na mara nikaona gari linatoka, kumbe alikuwa na gari,
akatoka nalo, na kuniambia;
‘Haya haraka panda
twende nyumbani kwako...’akasema na mimi bila kujali nilivyolowana nikapanda
kwenye gari, tukaanza kurudi kuelekea kwangu,...maana kwa kuhangaika kutafuta
gari nilishafika mbali.
Tulirudi hadi nyumbani
kwangu na nikamkuta mtoto yupo vile vile, na hali ilikuwa mbaya zaidi,
nikambeba, nikatoka naye nje, tukaingia kwenye gari na tukaelekea huko
hopitalini, mtoto alikuwa anazidi kuwa na hali mbaya......
NB: Je ilikuwaje
WAZO LA LEO:
Kwa vyovyote iwavyo, hasira na chuki zetu zisiguse watoto , watoto hawana
makosa katika mambo yenu ya kimaisha, mtoto hana dhambi, inashangaza watu
wanagombana, na hasira zao wanazipeleka kwa watoto, huo ni unyama, uliokithiri.
Watoto ndio jamii,
ndio kikazi, taifa letu kutokana na wao, tunatarajia kupata viongozi wetu,
tukiwalea vyema, tunaijenga jamii, iliyo na upendo na amani, na kupata viongozi
waadilifu,kinyume chake tutarajie shida, uhasama chuki na vita....tukumbuke kuwa
watoto ni taifa la leo, kesho na siku sijazao.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Hey there! I know this is kind of off topic but I was wondering which blog platform are you using
for this site? I'm getting tired of Wordpress because I've had issues with
hackers and I'm looking at options for another platform.
I would be fantastic if you could point me in the direction of a good platform.
Post a Comment