Nilipotoka kazini, sikwenda moja kwa moja
nyumbani, nilielekea mitaa ambayo nafahamu ndipo anapoishi mdada, nikaitafuta
nyumba kama nilivyoelekezwa, na haikuwa vigumu sana kuipata, kwani ilikuwa karibu na barabarani, na nyumba kubwa yenya kila sifa ya nyumba nzuri, ina geti kubwa na mlinzi, nikagonga geti
la hiyo nyumba , na haikuchukua muda nikafunguliwa;
‘Samahani nimemkuta mdada?’ nikauliza
‘Wewe ni nani kwake?’ akauliza mlinzi wa
getini niliyemkuta, akawa analiangalia pikipiki langu.
‘Ni mfanyakazi mwenzake’nikasema.
‘Ohoo, kumbe, eeh, sijawahi kukuona kabla,
wafanyakazi wenzako walikuwa mara kwa mara wanakuja hapa,...Haya hebu subiri
hapa nikamuulize, umesema jina lako nani?’ akaniuliza huku akiendelea
kuliangalia pikipiki langu.
‘Mhasibu wake, wewe mwambie hivyo
ataelewa...’nikasema
‘Mhasibu wake,...mmh, kweli yawezekana kuweka
mhasibu wake, maana mdada huyu anaingiza pesa, sio mchezo, ...kwahiyo umemletea
pesa...?’ akaniuliza na mimi nikacheka kidogo na kusema...
‘Hapana....’nikasema na yeye akatikisa kichwa
na kusema;
‘Niambie bwana, maana najua kama umekuja na
pesa leo ni furaha, dada yangu huyu akiwa na pesa hana hiana..na mimi nina
shida, na njia ya kumuingia ni wakati ana pesa...’akasema.
‘Hapana sijaleta pesa, nimekuja na maswala mengine
ya kazini..’nikasema.
‘Anadaiwa eeh, mmh, maana kama anadaiwa hata
huko ndani siendi, huyu dada akiwa na madeni, ni vyema ukawa mbali kabisa na
yeye,na siku akiwa hana pesa ndio kabisa hata ukimsalimia haitiki,...’akasema.
‘Mimi sijui kama anadaiwa, nimekuja na maswala
mengine usiwe na wasiwasi...’nikasema.
‘Hata hivyo nimemuona leo akiwa na furaha
sana, nahisi kapata bingo, sijui nikachomekee shida zangu huko...’akasema akawa
anajikuna kichwa kama anawaza.
‘Kamwambie basi kuna mgeni wake...’nikasema
‘Ohoo, haya bwana,....lakini nikuulize kitu
kimoja,wewe ni mhasibu wake, eeh, mimi nataka mkopo nifanyeje?’akaniuliza.
‘Wewe ongea naye kwanza, akikubalia
atakupa....’nikasema.
‘Jana alikuja jamaa mmoja, nilimuonea huruma,
huyo jamaa ni mtu mkubwa sana, huwa anatembea na magari ya kifahari, lakini
jana...nikasema kweli wanawake sio mchezo...’akasema na mimi nikaona kuna
jambo, ngoja nimchokonoe.
‘Huyo jamaa ni nani...?’ nikamuuliza
‘Humjui wewe, yule jamaa tajiri, mwenye pesa
kama nchi yake, anapenda kusema milioni ni vijisenti kwake, pesa kwake ni
mabilioni, pesa kwake ni dola, sio madafu, jamaa ana dharau yule...’akasema na
moyo wangu ukaanza kunishituka, ina maana ni huyo jamaa.
‘Yule wa mamlaka ya ushuru wa magari?’
nikauliza
‘Haswa, lakini jana alikuwa mdogo kama
piritoni, alipofika tu, akasimamisha gari na kuniuliza mdada yupo nikamwambia
asubiri, nilipokwenda kwa mdada, mdada akasema ni mwambia kachoka amelala,
....nikarudi kumwambia akaanza kuniomba, nimwambia kaja kwa dharura,
...nikamwambia mdada huwa hana kauli mbili, akisema kasema,...’akatulia kidogo
akiangalia ndani.
‘Ikawaje?’ nikamuuliza
‘Jamaa akawa ananibembeleza, kweli karibu
kunipigia mgoti, sio kawaida ya huyo jamaa, mwisho akatoa nyekundu mbili,
akanihikisha mkononi, akasema nenda kamwambia huyo mgeni ana mzigo wake...’huyo
mlinzi akaruka ruka.
‘Nyekundu mbili shaaah, nikasema hapa ulaji,
nikakimbilia ndani kufika namkuta mdada yupo kwenye dirisha kumbe alikuwa
anatuangalai kwa ndani,nikasinyaa, maana aliona nikipewa hizo pesa, nikaanza
kujiuma uma.
‘Ndio kazi yako siku hizi wakija wageni
wanakuhonga, unakuja kunisumbua...’akasema
‘Hapana mama, ...unajua..unajua..nikawa sina
cha kumwambia, akaniogelea na kusema;
‘Sikiliza kamwambia kama kaja na mzigo wangu
akupe uniletee, sina muda wa maongezi na yeye...’alisema maneno hayo kwa hasira
nikatoka mbio, hadi kwa huyo jamaa.
‘Kasema niende kumuona?’ akaniuliza
‘Kasema unipe mzigo wake kwanza...’nikamwambia
hivyo, na huyo jamaa akaingia kwenye gari alke akatoa bahasha, imetuna, nikajua
ni pesa, akanipa, na mimi kwa haraka nikakimbilia ndani nikamkabidhi
mdada...mdada akaziangalia akaniambia ziweke hapo mezani , nenda mwambie
tutaongea sehemu nyingine sio hapa nyumbani kwake...’akatulia kuniangalia.
‘Umesema una haraka, au?’ akaniuliza.
‘Ikawaje?’ nikamuuliza
‘Hapa koo linawasha kweli kweli, nina kiu kama
ya soda vile..., nikipa soda itakuwa vizuri, sio lazima maji...’akasema na mimi
kwa haraka nikaingiza mkono mfukoni, nikatoa pesa iliyoguswa na mkono wangu na
kumkabidhi bila kuangalia ni shilingi ngapi.
‘Sasa hapa maneno, naweza kuongea mpaka
kesho...’akasema
‘Ikawaje...?’ nikauliza
‘Jamaa hakutaka kuondoka, akasema nimwambia
hawezi kuondoa mpaka waonane, ikabidi nirudi ndani kumwambia, na niliporudi
nilimkuta mdada akiwa kashkilia ule mzigo huku anazunguka huku na kule,
akaniangalia
‘Mama kasema hawezi kuondoka mpaka uonane
naye...’nikasema na mara mdada akachukua simu yake, sijui alifanya nini, mara
kwa nje, nikasikia mtu akitoa kilio, nikakimbilia nje, nilipofika nilimkuta
jamaa kashikilia simu yake huku kapiga magoti....’akatulia .
‘Kwanini alifanya hivyo?’ nikamuuliza
‘Sijui..nilijarinu kumsogelea lakini alisimama
kwa haraka na akaanza kuelekea ndani nikamzuia, lakini hakutaka, baadaye mdada
akatokeza mlangoni na kuniambia nimuache, na huyo jamaa akapiga mgoti mbele yam
dada, akimuomba,...’akasema
‘Alikuwa akimuomba nini?’ nikamuuliza
‘Eti ampe picha..kitu kama picha, anataka
apewe zote na yupo tayari kufanya lolote kwa huyo mdada, na mdada alipoona
ninasikiliza akamshika huyo jamaa tai yake na kumvutia ndani..ilikuwa picha, na
ikaishia hapo, maana jamaa alipotoka alikuwa kakonda, hana raha, akaingia
kwenye gari lake akaondoka...’akatulia,
‘Kwahiyo mdada unafikiri alimfanya nini huyo
jamaaa...?’ nikamuuliza
‘Mimi sijui, kwanza nimeongea sana, huenda
yupo dirishani anatuangalia ngoja nikamuone...’akasema na kutembea huku
akionyesha wasiwasi,...kulipita kitambo kidogo, na baadaye akatoka huku akiwa
kakunja uso, na kuonyesha wasiwasi, akaniangalia halafu akasema;
‘Mhh, mimi nakushauri usiende kumuona, nahisi
mambo yake hayapo sawa...niliwahi kusikia kuwa akiwa katika hali kama hiyo, hutakiwi
kumsogelea,....mimi sijawahi kumuona hivyo, mwenzangu wa mwanzo aliacha kazi,
eti akimuogopa huyo mdada....’akasema
‘Kwanini amuogope..?’ nikamuuliza
‘Hata mimi sijui ni kwanini, mrembo kama
huyo,....mtu unaogopa kufanya kazi naye, cha muhimu ni kumjulia mtu, mimi
nimeshamjulia, akikasirika na kuwa mbalia naye, akiwa na raha, nakuwa akribu
naye, maisha yanakwenda, watoto wanakwenda choo...’akasema.
‘Kwahiyo unasemaje,...?’ nikamuuliza
‘Mhh, hali niliyomkuta nayo..niliogopa hata
kumshitua,...sasa mimi sijui,...uamue mwenyewe, kwa vile wewe ni mhasibu wake,
na huenda umekuja na mambo mazuri, jaribu kwenda...’akasema akionyesha
wasiwasi.
‘Kwani anaumwa, yupoje,..kalala, ...?’
nikauliza
‘Wewe nakushauri rudi, utampigia simu, zaidi
mimi sijui, maana hata hivyo, miomi bado ni mgeni sana kwake, sijamjua vyema...’akasema
akawa anatembea kuelekea sehemu yake ya kukaa, nikasimama nikijiuliza nifanye
nini.
Baadaye sana, nikaona kwanini nisiende
kumuona, kwanza ni mfanyakazi mwenzangu, kama ana tatizo itakuwa vyema
kumsaidia, pili ni mtu ambaye nimejaribu kuwa karibu naye, na tatu, leo
nimeamua kuwa iwe mwisho wa majanga anayotaka kunitumbukiza..
‘Nikaelekea kwenye mlango, sikugonga maana
ulikuwa nusu wazi, nikaingia ndani
********
Asubuhi, nilichelewa kwenda kazini, kwani
ilibidi nifanya mpango wa kuzipeleka hizo pesa za magumashi huko kijijini, kama
alivyoniagiza mdada; na nilipoingia ofisini nikachuku gazeti nikawa nasoma, lakini
akili yangu haikuwe kwenye gazeti, nilikuwa nakumbuka yaliyotokea jana nilipofika
nyumbani kwa mdada bila kutegemea;
‘Unasema nini, huzitaki hizi pesa, na zile
nyingine unataka kuzirudisha, haya nipe na uondoke hapa haraka ...kwanza sijui
kwanini umeingia bila ruhusa yangu,...’akasema kwa hasira.
‘Sijakuja na hizo pesa nyingine, lakini mimi
naona ni heri nifanye hivyo, maana pesa hizo hazina heri kwangu,naona naingia
kwenye machafu yako,...’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho yaliyojaa
hasira halafu akageuka kama anataka kuondoka, baadaye akasema;
‘Unajua mimi nilidhania wewe ni mjanja,..na
huenda ukawa mmoja wa watu watakao weza kubadili maisha yangu...nimekuona
tofauti na wanaume wengine, na...sijui ni kwanini, ...kama nisingelisikia hayo
ya kuwa una mchumba, nahisi......sijui, sijui....’akatulia kidogo na kushika
kichwa chake akainama chini kama anaangalia kitu.
‘Ni hivi katika maisha haya ya bongo tunaweza
kusaidiana ili angalau na sisi tuwe karibu na mafisadi, hivi nikuulize hawa
mafisadi wanakula nchi yetu, wanakupa
angalau pesa ya soda, au kazi yao ni kututimulia vumbi kwa magari yao...au
kusimamishwa kwenye foleni wakipitishwa na ving’ora na magari ya kodi ya walala
hoi....’akasema.
‘Mimi siwajui hao watu, ...’nikasema
‘Sikiliza nikuambie kwanini nafanya hivyo,
..nafanya haya angalau kuchukua hicho kidogo wanachotuibia sisi wavuja jasho,
..hizo pesa kama tusingezichukua kwa huyu jamaa unafikiri zingekwenda wapi,
kama sio kwenda kwenye miradi yao, au kutumiwa kuchezewa kamari, umalaya, na
ufisadi, ... hawa watu, hawa, wanaoitwa wanaume,...hawajali, hawana huruma
kwanini tuwaonee huruma...’akasema
‘Mimi sielewi hayo unayozungumza...’nikasema
na yeye akaniangalia halafu akashusha mikono kama kukata tamaa
‘Leo nimejisikia vibaya sana, nimekumbuka
maisha yangu, ....hata alipoingia mlinzi kanikuta sipo duniani,..tarehe kama
leo, hawa watu wanaoitwa matajiri,mafisadi, wanaume....nyie wanaume,...kama
ningelikuwa na uwezo ningeliwamiminia risasi hadi nihakikishe hakuna mwanaume
aliyebakia hapa dunia...’akasema
‘Kwanini..?’ nikamuuliza
‘Kwanini,...naogoa kukusimulia maana
nikikusimulia, unaweza ukawa marehemu...’akasema
‘Kwanini?’ nikamuuliza
‘Kwasababu wewe ni mwanaume na wanaume wote
hawana tofauti...ni sawa na shilingi, japokuwa ina huku na huku, lakini
shilingi ni hiyo hiyo...’akasema
‘Sijakuelewa...’nikasema
‘We acha, tarehe kama ya leo, ni siku ambayo,
sitaisahau katika maisha, yangu, na ikifika tarehe kama hii ninakuwa kama
mgonjwa...angalau leo, nimeweza kuvumilia, na ssijui kwanini leo nipo hapa
nyumbani, nilitakiwa niwe sehemu itkayonifanya nisiikumbuke kabisa tarahe kama
hiyo...’akasema na kutulia baadaye akauliza
‘Ina maana mlinzi hukuonana naye, sijamuambia
aruhusu mtu....’akasema
‘Aliingia kuja kukuona...’nikasema
‘Huenda alipofika, alinikuta
nimezimia,....’akasema.
‘Umezimia, kwanini uzimie, acha mambo yako
mdada, mbona unanielezea mambo ambayo hayapo...mdada, mimi nimechoka, usiponiambia ukweli, siwezi kukuelewa, kwani
wanaume walikufanyia nini,...ulikuwa unajiuza, ulikuwa....mimi sikuelewi,..hebu
niambia,ilikuwaje mpaka uwachukia wanaume kiai hicho, halafu sasa unajifanya
eti ulipoteza fahamu, kwasababu ya madawa yako ya kulevya au?’ nikamuuliza
nikiwa nimekasirika
Mdada
akainua uso na kuniangalia, aliniangalia kwa makini bila kupepesa macho,...bila
kusema neno kwa muda..halafu akageuka, hakuniangalia kwa muda, badaye akageuka
kuniangalia akahema na akawa kama anahangaika, akashika kichwa, akaniangalia
machoni na kusema;
‘Kama unataka nikusimulie mikasa iliyonipata
labda uchukua kamba unifunge, na si kamba, labda unifunge kwa minyororo wenye
nguvu sana, maana huenda hata huo mnyororo nikaukata, ...kwani nachelea mabaya
yatakayokukuta....
Nikamwangalia na kutabasamu nikicheka kidogo,
halafu nikamwangalia nikiwa nimebadili muonekano, ikutaka utani na yeye niliona
nimbadilikie kabisa, nikamuonyesha uso wa hasira nikasema;
‘Mimi nataka niusikie huo ukweli....maana bila
kuufahamu sitaweza kuvumilia, na hata hivyo nimechoka na mambo yako, imetosha,
na usiponiambia ukweli kwanza kwanini unawachukia wanaume, pili kwanini
unanifanyia hivi, sitakuelewa...’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho
yaliyojaa uchungu, na baadaye akasema
‘Mhh, siwezi,...sitaki,...nakuonea huruma...hapana,
kwanini unaniuliza hivyo, kwanini unataka nikusimulie jambo ambali huenda
utakuja kujijutia, au mimi mwenyewe nitakuja kujijutia,..siwezi na sitakiwi
kabisa...hapana, ....’akawa anashika kichwa kama vile anahisi maumivu.
‘Usiponisimulia, mimi nitakwenda kulipeleka
hili swala polisi, ni bora ni kose yote, lakini ukweli ujulikane, ni bora
nifungwe, ni bora...’nikasema na mara sauti kama ya mwanaume ikasema
‘Upo tayari eeh, ...’sauti litoka kwa mdada,
kwanza nilihisi kuna mtu mwingine kaingia, nikamwangalia mdada, nikahisi
ananifanyia mzaha, maana huyu mdada kwa mzaha humuwezi, na mimi nikasema
‘Nipo tayari..’nikasema na ghafla, mdada
akaondoka, na kuingia kwenye chumba, nahisi ni chumba chake cha kulala, au cha
kuhifadhia vitu, baadaye akatoka na mnyororo kama ule wanaofungia magari, na
kuniambia
‘Nifunge huu mnyororo, haraka....’akasema huku
akiwa ahniangalii usoni, na mimi nikawa nimeshikwa na mshangao, maana sauti
niliyoisikia sio ya mdada, ilikuwa nzito na kukwaruza kwaruza
‘Eti nini...!?’ nikauliza nikionyesha mashaka.
*****
‘Mdada hali yake ni mbaya sana...yupo
hospitalini ....’akasema bosi alipoingia ofisini na kunikuta nimeshikilia
gazeti, mimi nikajifanya sijui lolote, kwani jana nilikimbia mapema, na sikujua
ni kitu gani kimetokea tena huko nyuma.
‘Kafanya nini, kapata ajali?’ nikauliza kwa
mashaka, nikawa sasa nahisi kuna baya limetokea nilipoondoka pale, nilijifanya
sijui chanzo ni nini, au sijui kilichotokea mdada.
‘Huyu binti ana matatizo makubwa sana, na
nilishamkanya siku kama hiyo, tarahe yake ya kuzaliwa, ajifanya kama haipo,
....na hata siku moja asijaribu kumsimulia mtu maisha yake ya huko nyuma...’akasema
bosi na kunifanya nianza kuogopa, kumbe chanzo cha hayo yote ni mimi.
‘Hata dakitari wake alimshauri hivyo, kuna
dakitari , mtaalamu wa mambo ya fahamu, na maswala kama hayo, yeye alishamuasa na
kumwambia ajaribu kabisa kujizuia na mambo yatakayomkumbusha mambo ya nyuma,
....na ndio maana unaona wakati mwingine anakunywa sana, na huko kunywa
alikatazwa pia, lakini tatizo lake ni mbishi,...kwanini umuhadithie mtu mambo
yako, ambayo unahisi ni hatari kwako, watakusaidia nini hao watu.............’akasema
bosi.
Mimi nikawa nimeduwaa, na moyoni nikawa
najalaumu, lakini sikuwa nafahamu hayo yote, mimi niliona akinisimulia huenda
na mimi nitakuwa kwenye nafai nzuri ya kushauriana naye,..ndio maana
nilimuuliza anielezee maisha yake ya huko nyuma.
‘Jana ni siku yake ya kuzaliwa, na siku kama
hiyo, wakati anashrehekea akiwa na miaka tisa, ndipo yalipomkuta mabaya,...ooh,
naogopa hata kuyasimulia,...hata sijui kwanini alitaka kumsimulia huyo mtu
aliyemuuliza, maana hali kama hiyo hutokea akijaribu kumsimulia mtu...na baya
zaidi awe ni mwanaume ...’akasema bosi.
‘Kwani bosi, ...tatizo laki hasa ni nini?’
nikauliza
‘Usije ukamuuliza mdada, kuhusu maisha yake ya
nyuma, ....atakuua,...’akasema bosi na kunifanya nikumbuke yaliyotokea jana,
kama isingelikuwa mlinzi, huenda kama bosi anavyosema ningelikuwa maiti, lakini
sikuamini, ...ina maana mdada angeniua mimi, nikamwangalia bosi na kuuliza.
‘Bosi ina maana wewe mdada aliwahi
kukusimulia?’ nikamuuliza
‘Ndio , na mimi ndiye niliyechukua hatua kubwa
ya kumsaidia maana watu walishamuona kuwa kachanganyikiwa, ...na wengine
wakakimbilia kumuona kuwa eti ana mashetani, yale sio mashetani, ni athari ya
matatizo aliyokumbana nayo akiwa binti mdogo...’akasema bosi.
‘Natamani sana kuyajua hayo.....lakini
sikuweza, ilibidi nikimbie...’nikasema na bosi akawa kama kashituka na
kuniangalia kama mtu aliyesikia jambo ya kulitisha, akasema;
‘Ina maana wewe jana ulikwenda kwake, hujui
ndio siku yake ya kumbukumbu ya kuzaliwa na siku kama hiyo kwake inakumbusha
mengi, na huenda kwa kiherehere chako, ukamuuliza maisha yake ya huko nyuma?’
akauliza bosi, na mimi hapo nikasita baadaye nikasema;
‘Ndio mimi bosi, nahati nzuri jana
nilimtembelea nyumbani kwake, na tukawa tunaongea nikataka kujua ukweli, maana
kila mara anawalaani sana wanaume, na kuonyesha hali ya kuwachukia wanaume,....nikawa
najiuliza sana, wanaume wamemfanyia nini huyo mdada,!’ nikasema.
‘Kwa tahadhari, usije kurudia tena kumuuliza
maswali kama hayo, utakufa, mdada atakuua.....usije ukajidanganya kuwa kwa vile
yeye ni mwanamke utaweza kumzidi nguvu, huwezi na hamtaweza...’akasema na
kutulia kama anatafakari jambo.
‘Nikuambie ukweli, hali kama hiyo ikimuanza,
na akianza makeke yake, hakuna anayeweza kumshika..hata waje wanaume wenye
nguvu kumi, hawamuwezi....na hatakiwi mwanaume kumsogelea...’akasema bosi na kuingia
ofisini kwake,ilionyesha hakupendezewa na kitendo hicho cha mimi kumuuliza
mdada. Baadaye bosi aliniita na mimi
nikaenda ofisini kwake, na kwa vile ikuwa na kazi nyingi siku hiyo, akasema;
‘Tuendelee na kisa chetu kidogo, baadaye
nitakwenda kumuona mdada nione anaendeleaje, ...’akasema bosi akiangalia saa
yake.
‘Au una kazi nyingi...?’ akaniangalia na mimi
nikasema
‘Sina kazi nyingi, ila kama unakwenda kumuona
mgonjwa, kwa vile ni stafu mwenzetu, naona tuongazane na mimi nikamuone
huyo mgonjwa...naona twende huko hospitalini pamoja.....’nikasema
‘Tuongazane mimi na wewe,...?’ akawa
ananiuliza akiniangalia kwa mshangao, na mimi nikawa nashangaa pia, kwani kuna ubaya gani mimi na yeye tukienda
pamoja kumuona mgonjwa,nikawa sielewi, bosi aliniangalia kwa makini kwa muda,
mpaka nikatahayari na kuhisi nimetenda kosa kumwambia hivyo, baadaye akasema;
‘Unasema twende pamoja, ina maana hukunielewa,
..ohooo, wewe sasa unatafuta kifo chako, na na kuonya tena na tena, usifanye
kosa hilo, kwa hivi sasa hatakiwi mtu anayeitwa mwanaume kumsogelea huyo
mgonjwa, labda kama unataka kufa mapema...mimi huko nitakwenda peke yangu,
nitakujulisheni anaendelea vipi...’akasema
Unakumbuka tulipoachia,...
Kuwa nilipata mtu mwenye gari, akajitolea
kumpeleka mtoto hospitalini, na muda huo mvua bado ilikuwa ikinyesha, na sio
mvuo ndogo, ni mvua kubwa....
‘Haya tuendelee na simulize letu...’akasema
bosi
‘Basi kwa msaada wa yule baba alinipeleka hadi
hopitalini, na ukumbuke hospitali iliyokuwepo karibu ni ya kulipia, sina pesa,
na hata kama nitarudi dukani, kuchukua akiba yangu isingelitosha kwa matibabu,
pesa iliyokuwepo nilishanunulia vifaa.
‘Lakini mungu mkubwa kwani kwa msaada wa yule
msamaria mwema, nilifanikiwa kulipia matibabu ya mtoto na daktari alipomwangalia
mtoto jinsi alivyo, akasema;
‘Huyu inabidi alazwe, hali yake io
nzuri...’akasema docta na wakaanza kumchunguza na kumpa ile huduma ya kwanza
kabla hajaanza matibabu, walimuwekea kifaa caha kupumulia, ni cha oksijeni
kwani pumzi zilikua za shida. Na huku
wakiendelea na vipimo vingine.
Nilimshukuru sana mwenyezimungu kwa
kunikutanisha na huyo baba ambaye alikuwa na moyo huo wa huruma anakanisidia bila
kusita nilimshukuru naye akiendelea kuonyesha ubinadamu wake na kunilipa
shilingi 20,000 kama za kunisaidia na baadaye alipohakikisha kuwa tumelezwa
akaniaga.
‘Sijui nikushukuru vipi baba yangu...’nikasema
nikimwangalia bila kuamini, maana katika dunia ya leo watu kama hawa ni adimu
kabisa.
‘Usijali, kwa binadamu yoyote mwenye utu ,
angelifanya hivyo hivyo, hali ya mtoto inasikitisha..’akasema akimwangalia
mtoto, na baadaye akaondoka.
Nilikaa wiki moja nikiuguza mtoto huku na mie
nikiwa na homa kali, ikabidi na mimi muuguzaji niwe mgonjwa, na nianza matibabu
na ukumbuke nilikuwa na mimba na mimba inakua kwa majanga hivyo hivyo.
Baada ya wiki moja ya kulazwa, nilirudi
nyumbani,na uamuzi niliouchukua ni kuwa hata kama nipo dukani, nitaenda na
mtoto wangu,niwe nashinda naye huko huko dukani mpaka hapo jioni , na jioni narudi
naye.
Katika kuhangaika, tukawa pia tunapika
vyakula, na pia kama kuna sherehe tunachukua hiyo tenda ya kuwapikia wageni,
bahati nzuri, mwezi tisa kukawa na harusi harusi, na tukaweza kupata nafasi ya
kuwapikia watu.
Mwezi huo wa tisa ndio mwezi wangu wa
kutazamia, lakini hata hivyo, ilinibidi nihangaike ili kupata riziki, nakumbuka
ilikua ni majira ya saa kumi na moja alfajiri nikahisi uchungu, yakiambatana na
maumivu makali, nikajua muda umefika.
Uchungu ulikuwa mkubwa sana , hata hivyo
ikutaka kumsumbua mume wangu kwenye kwani na yeye alikuwa mgonjwa, alikuwa naye anaumwa, yupo kitandani, nilivumilia mpaka saa nne hali ikazidi kuwa
tete, na mume wangu akaniona nikigugumia maumivu;
‘Mke wangu ni bora uende
hopitalini....’akasema na mimi kwa hali niliyokuwa nayo sikupinga , nikajiandaa kwenda hospitali, huku uchungu
umenikamata kweli kweli hata kusimama siwezi, nasimama huku nimepinda,
nikajitutumua hivyo hivyo, nikujiandaa.
Tukiwa tunasubiria usafiri, akaja mtu
kutuambia gari walilolitegemea limeharibika, limefika njiani na kuzimika,...
‘Oh mungu wangu, mbona hii adhabu...’nikasema
na mume wangu akanipa moyo kuwa nivumilia watajiathidi kutafuta gari jingine.
Gari lilipopatikana lakini hapo nilipokaa, nilikuwa
sijiwezi, nilihisi kama ninaweza kujifungulia hapo hapo nyumbani,
‘Gari limefika haya inuka twende nje...’akasema
mume wangu,
Nikajikakamua na kuinuka kwa shida, yaani zile
hatu hadi kufika mlangoni ilikuwa ni kama mwendo wa maili wa kupanda
mlima,...haya nikatoka nje, kwenye hiyo nyumba tunapokaa kuna ngazi za kushuka kidogo.Sio
ngazi kubwa saana, lakini cha ajabu ngazi sikuweza kuinua mguu ili niteremke,
watu waliokuwa wakiniangalia ambao hawajui uchungu ulivyo, hata kama wanajua,
lakini kwa vile sio wao yaliyowakuta, wakaanza kunicheka.
‘Wifi na wewe bwana...ina maana hata kushuka
hizo ngazi leo hii huwezi...’akaanza kusema wifi yangu na wote wakaangua
kicheko.
‘Anadeka huyo, kwasababu mume wake leo yupo,nani
asiyejua kuzaa ...wewe uliona ni raha eeh...hehehe...’akasema huyo wifi
mwingine ambaye hata kuzaa hajazaa, anajisemea tu, na wote wakaangua
kicheko.Nikajitutumua kwa shida na kwa jinsi nilivyokuwa natembea hao mawifi
zangu na shemeji zangu wakawa wananicheka kweli kweli, hawana mbavu.
Mimi sikutaka hata kuongea nao, kwani hata
hiyo hamu ya kuongea nao ninao,, ila moyoni nilisema kweli duniani hamna
ubinadamu hata huruma hata kuniuliza, au kunisaidia kunishika mkono hakuna.
Nilijitahidi nikashuka zile ngazi, na
nilipofika chini, nikakaa chini, sijiwezi kabisa, maumivun yalikuwa makali sana,
hapo sasa nikawa nalia, siwezi kuinuka kabisa, siwezi kutembea migumu imegoma,
hakuna aliyejitolea hasa akina mama kuja kunisaidia mpaka mume wangu japokuwa
ni mgonja, akaamua kuja kunibeba na kuniingiza kwenye gari.
Nikapelekwa hadi hopitalini, nilivyofika tu
hospitali kitengo cha clinic ya wazazi, daktari alimuambia mume wangu akimbilie
begi na beseni kwani kichwa cha mtoto kilikua kimesha anza kutoka...
‘Kwanini mumemchelewesha huyu mtu
hivi...’akasema yule dakitari akionyesha wasiwasi, na niliposikia docta akisema
hivyo nikajua mambo sasa yamekuwa mabaya, ni yale yale ya kuambiwa ni mimi au
mtoto.
Waliniweka kwenye hilo beseni na kunikimbiza leba na hapo kiakili nikawa mimi na
mungu wangu , kipindi hicho mume wangu alikuwa katumwa kwenda kununua baadhi ya
vifaa vilivyohitajika kwenye duka lao, japokuwa alikuwa anaumwa lakini kutokana
na hali yangu ilibidi kuumwa kwake akusahau.....
NB: Je ilikuwaje
WAZO LA LEO: Usifurahie kupata kitu amabcho sio halali yako, ukijua kabisa
kuwa hujakipata kihali, na kupata kwako ni kumdhulumu mwenzako, ...huenda umekipata kwa ujanja-ujanja na hadaa za namna kwa namna huku ukisema; ‘hii ni
riziki yangu, hii ni halali yangu....’ hiyo sio halali yako, hilo ni deni,
kwani huyo uliyemdhulumu, anaposononeka moyoni, familia yake ikateseka kwa ajili hiyo, huo ni mzigo wa madhambi kwako. Tujitahidi kuchuma na kupata riziki ya halali, chumo linalotokana na juhudi zetu za halali.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment