Yaliyotokea kwa mdada
yalifanya nimuonee huruma sana, japokuwa sikuwa nafahamu undani wa yaliyomkuta,
lakini nilihisi kuwa yatakuwa ni mabaya sana. Na hali hiyo ya kujiuliza ni kitu
gani kilimpata, ilinifanya niingiwe na hamu sana ya kukutana na mdada,
ikiwezekana anisimulie yeye mwenyewe aliyokutana nayo utotoni, ..nahisi ni utotoni, lakini hilo nahisi halitawezekana
‘Sasa ni nani
atanisimulia kuhusu masahibu yake,...au nimuulize bosi...’nikajikuta najiuliza mwenyewe.
`Kitu cha ajabu, ukimuuliza ni nini kiliwahi kumtokea, au kwanini anawachukia wanaume, anaghadhika sana,.....na sasa huyo, anakuwa kama mtu aliyepagawa au mtu aliyepandisha
mashetani,...mhh, nahisi kuna tatizo, sasa nifanye nini...?’ nikajiuliza.
Wakati naendelea kujiuliza, kumbukumbu za yaliyotokea muda uliopita zikaanza kunirejea akilini,....
**********
Baada ya mwanadada
kutoka na ule mnyororo, aliniambia nimfunge, na kitu kilichokuwa kikinishangaza
ni ile hali ya kubadilika kwa sauti, yeye ana sauti nzuri ya kuvutia ya kike,
lakini muda ule akawa kama mwanamke anayeigiza sauti ya kiume.
Ninasema kuigiza,
kwasababu mimi naifahamu vyema sauti mdada, kwahiyo akiongea sauti nyingine,
nitajua anaigiza, na hususani kuongea sauti ya kiume..lakini sauti iliyotoka
kwa mdada, kama humjui, utasema ni mwanaume anaongea, kwani ilikuwa sauti nzito
na ya kutetemeka ya mwanaume haswa.
‘Nifunge huu mnyororo
haraka...’sauti nzito ikatoka na wakati huo mdada alikuwa haniangalii usoni
‘Eti
nini,.....’nikauliza nikionyesha mshangao, ule mnyororo ni mnzito, lakini kwa
jinsi alivyokuwa kaushika mkononi mwake, ulionekana kama kitu kidogo
kwake..kitu ambacho kilinifanya nione ajabu sana, kwani namfahamu mdada, pamoja
na ujasiri wake, lakini mikono yake haijashupaa kubeba vitu vizito.
‘Nimesema unifunge
hunielewi, kwanza wewe ni nani....?’ akaniuliza na kunikabidhi ule mnyororo, ni
kama mtu anakutupia na kwa vile ikujiandaa nao nikajikuta napepesuka, na kabla
sijaushike vema akaninyoshea mikono yake, huku akiangalia pembeni.
‘Mimi sikuelewi,
mdada...’nikasema bado nikiwa sina uhakika, akilini mwangu bado nilijua ni ule
utani wake, na alipoona nimeduwaa akauchukua ule mnyororo na kunichapa nao...ni
mnyororo mrefu wenye nguvu, na jinsi alivyouinua ule mnyororo na kunichapa nao,
ni kama mtu kashika kitu kidogo,lakini kwangu mimi niliipata pata ..
Nilijikuta naserereka,
...na kwenda kujigonga kwenye ukuta, na kabla sijakaa sawa akanijia, na ule
mnyororo ukiwa hewani,...alikuwa akitoa sauti ya mngurumo kama ya simba,
nilipoona hivyo, niliinuka haraka pale nilipokuwa nimelala nikigugumia maumivu,
nikajizoa zoa, na kuangalia mlango upo wapi,, kilichofuata hapo ni mbio,...
Na kwa vile nilikuwa
nakimbia huku nageuka kumwangalia, siamini ninachokiona na kutokea, huku nina
wasiwasi, woga umenijaa,nikajikuta najigonga kwenye kizingiti cha mlango,
nikadondoka, haraka nikainuka, nikashika kitasa na kuufungua huo mlango,
nikatoka, huku nyuma nikasikia sauti ya kicheko cha kukera.
‘Hahahahaha....halafu
mnajiita wanaume...bahati yako....’ ilikuwa sauti ya kukwaruza ya mauzi, na
mimi sikuangalia nyuma, nikawa nimeshatoka nje, ...na kwa jinsi nilivyokuwa
naogopa, sikuweza hata kuongea na mlinzi, nililiendea pikipiki langu na kumkuta
yule mlinzi akiwa kasimama karibu nalo, huku akiwa kalishikilia.
‘Pikipiki lako zuri,
siku naomba uniazime kidogo, nikumbukie enzi zangu, unajua nilishawahi kuwa na
pikipiki......’akasema na mimi sikumsemesha nikampiga kikumbo, akaserereka
pembeni, nikalidandia pikipiki langu na kwa haraka nikaliwasha na kuondoka kwa
mwendo wa kasi sana uliomfanya huyo mlinzi abakie akiniangalia kwa mshangao.
‘Vipi wewe ni adabu
gani hiyo ...mbona unanisukuma, halafu unaondoka bila kuaga...kuna nini,
weweeeh,....’akawa anaongea lakini mimi sikusubiria, nikawa nimeshalisukuma geti
kwa ile pikipiki,na kwa vile alikuwa hajalifunga vyema, likafunguka na kwa
haraka nikatika nje ya jengo hilo, na kunifanya kidogo niwe amani,nikaendesha
pikipiki langi kwa mwendo wa kasi hadi nyumbani.
‘Huyu mdada ana
mashetani nini, mmh, au kachanganyikiwa na madawa, lakini haiwezekani, ina
maana kapata wapi zile nguvu, siamini, sasa...duuh, ...’ndivyo nilivyosema, na
sikutaka hata kuwaliwazia zaidi maana kwa muda huo kichwa kilishaanza makeke
yake.
‘Dawa ya hiki kichwa
ni kulala....’nikasema, huku nikawazia nimpigie simu bosi, lakini nikaona ni
bora ni nyamaze tu, nikapanda kitandani, na kujiegemeza huku nikijaribu kuvuta
subira, huku nikijizuia kwenda kutafuta kinywaji.
‘Ukianza kusikia
maumivu ya kichwa, kunywa maji mengi, jitahidi kutafuta usingizi...’nikakumbuka
ushauri wa dakitari, na mimi nikainuka na kuchukua gilasi ya maji, nikayanywa,
nikaongeza tena na tena...halfi kidogo kwa mbali nikasikia unafuu fulani.
‘Kitapona
tu....’nikasema huku nikijizuia kukumbuka yaliyotokea, lakini kwa upande mwingine
wa akili, kuna hali inaniuliza nifanya nini, maana huyo ni mfanyakazi mwenzetu
nahitajika kumsaidia,...na wakati nawaza hivyo, kwa ajabu kabisa nikashikwa na
usingizi. Usingizi ulionishika sio wa kawaida, ....
‘Nilikuambia
nikusaidie nikupe dawa ya huyu mtu anayekusumbua, hukutaka,sasa unaona, na bado
...’sauti ikasema.
‘Dawa gani?’ nikauliza
nikisikia sauti ikiniambia, sikumuona huyo mtu zaidi ya sauti
‘Yakuondokana na hayo unayopambana
nayo..’sauti ikasema
‘Mimi sihitaji dawa,
na kama unaona nahitaji dawa bai nipe hiyo dawa, kama unayo...’nikasema
‘Dawa yenyewe ina
masharti....’ile sauti ikasema
‘Masharti gani?’
nikauliza
‘Unatakiwa uchague
mawili, umuoe au umuue huyo...’sauti ikasema
‘Nimuoe,au nimuue
nani?’ nikauliza kwa mashaka, na ile sauti ikawa kama inaguna , halafu ikasema.
‘Huyo anayekusumbua..’
sauti ikasema
‘Ni nani huyo
anayenisumbua....?’ nikauliza na mara ...
Moyo ukawa unanienda
mbio, na kuhisi kitu kikigonga kichwani kwangu, na mlio kama wa mtu anayegonga
mlango, lakini ule mlio ulikuwa mkubwa wa kunifanya kichwa kiume, nikashituka,
kumbe nilikuwa naota, nikasimama haraka kutoka kitandani, nikatulia nikwaza
nilikuwa naota nini.
Mlango ukagongwa kwa
haraka haraka, ...kumbe kulikuwa na mtu anagonga mlango, ndiye aliyenifanay nizindukane
kwenye ndoto hiyo ya ajabu;
‘Nani wewe
unayegonga...’nikauliza.
‘Ni mimi mtu wa
usalama ....’sauti ikasema na sikutaka kuuliza zaidi, nikaenda kwenye mlango na
kufungua mlango,maana nilifunga na funguo.
Nilipofungua mlango
nikakutana na jamaa alikuwa mrefu, na mwili wake ulionekana shupavu, nahisi
atakuwa mtu wa mazoezi,, nikamwangalai usoni, na yeye akawa akaniakzia macho,
nikasema;
‘Habari yako ndugu...nikusaidie
nini...?’nikamsalimia, na kumuuliza swali, maana sikutaka maongezi na mtu, nilikuwa
na mambo yangu mengi kichwani. Mara yule mtu akatoa kitamblisho na kuema;
‘Mimi ni askari
usalama nilikuwa na maongezi na wewe kidogo...’akasema huyo mtu.
‘Kuhusu nini?’
nikauliza nikiwa na mashaka, na akili yangu linituma kuwa huenda mdada, kapatwa
na madhara.
‘Kuhusu mashitaka
yaliyoletwa kwetu, kuwa kuna kundi limejitokeza, kundi hilo linatishia
amani....’akasema na kunifanya nipumue kidogo, kuwa sio swala la mdada.
‘Kwahiyo umeona mimi
ni mmoja wa hilo kundi?’nikamuuliza
‘Tunajaribu kuwahoji watu
mbali mbali, ili tupate ushirikiano, wa raia wema, huenda katika maongezi yetu
tunaweza kuligundua hilo kundi...ni kwa usalama wetu sote..’akasema na mimi
sikutaka kubishana naye zaidi nikasema;
‘Sawa karibu ndani,
lakini mimi sijui lolote kuhusu kundi lolote....’nikasema na kumpisha aingie
ndani, na yeye kwanza aliangalia kushoto, halfu kulia kwa haraka sana, halafu
akaingia ndani.
‘Nakumbuka tulishawahi
kukutana kabla...’akasema
‘Wapi?’ nikauliza huku
nikijaribu kukumbuka kama kweli sura hiyo nimewahi kuiona mahali, lakini sikuwa
na kumbukumbu yoyote kuhusu yeye, kwangu alionekana mgani kabisa.
‘Kwenye hoteli ya Kajificheni,
ukiwa mdada mmoja..’akasema na hata hivyo, sikuweza kumkumbuka, nikasema;
‘Inawezekana, lakini
mimi sikukumbuki kabisa..’nikasema.
‘Unaweza usinikumbuke,
maana ile siku ulikuwa umelewa sana, na nilitaka kuingilia kati, nihakikishe
umefika nyumbani kwako salama, lakini ulikataa, ukasema huyo dada ni mchumba
wako....’akasema na kujaribu kukumbuka kama kweli nilifanya hivyo, lakini
sikukumbuka kabisa.
‘Nilisema hivyo mmh,
sikumbuki kabisa, na hata hivyo, sizani kama ni mimi nahisi kama umekosea,
labda alikuwa mtu mwingine....!?’ nikauliza kwa mshangao.
‘Inawezekana usikumbuke
kwa vile ulilewa sana...kulewa kwa namna ile sio kuzuri, maana watu wabaya
wanaweza kuchukulia nafasi hiyo kukufanyia lolote baya, na sikupenda
walivyokuwa wakikifanyia wale watu...’akasema na mimi nikaona huyu mtu anaweza
kuniletea matatizo nikasema;
‘Samahani kuna
jingine, maana najiandaa kutoka, ...kuna jingine la kuniula mkuu...?’
nikamuuliza huku nikipiga miayo ya kulazimisha.
‘Nimeanzia hapo kama
kukuweka sawa, sijakuuliza maswala ya msingi, ...’akasema
‘Maswali gani ya
msingi, unataka kuniuliza..?’ nikamuuliza
‘Kwanza, nikuulize
wewe una mahusiano gani na mdada...’akaniuliza na kunifanya nianza kuona
mashaka, nikahisi kuna kitu kimemtokea mdada, huyu mtu alitaka kunianzia mbali.
‘Hayo ni maswala
binafsi, nafikiri sitaweza kukuambia lolote kuhusu hilo...’nikasema.
‘Ndio ni maswala
binafsi lakini yanaweza yakatusaidia sisi, unafahamu sisi lengo letu ni jema
kabisa na tunafahamu lipi ni jambo binafsi, na tukiambiwa tnafahamu jinsi gani
ya kuliweka ili liwe siri, ...nikuondoe wasiwasi kuwa mahusiano yenu ya ndani
hatuna maana nayo sana, cha msingi ni kunijibu, ili niweze kuendelea na maswali
mengine.
‘Yule ni mfanyakazi
mwenzangu,...’nikasema.
‘Sawa hilo nafahamu,
zaidi ya ufanyakazi, ...nikuambie ukweli, kuna jamaa wawili nilikuja kuwauliza
hivyo hivyo, wakanijibu hivyo hivyo, lakini baadaye nikawaona wpo mitaani,
wanalalamika kuwa huyo mdada, kasababisha wao kusimamishwa kazi kwa muda, hata
hivyo, bado waliendelea kuficha siri, siri ambayo tunaifahamu, tunachotaka tu
ni ushahidi...’akasema.
‘Ushahidi gani
mnautaka, kuna mtu kauwawa, kuna jambo limetokea,..?’ nikauliza.
‘Kama nilivyokuambia,
kuna kundi, lenye nia mbaya, kwa jamii, na lenyewe inavyoonekana, linawalenga
watu wenye uwezo, wakidai kuwa watu hao ni mafisadi,...sasa kama ni mafisadi,
kama wanavyodai, kwanini wasishitaki...kinachofanyika na kuwasumbua raia
wema,...nafikiri hapo kidogo nimekuweka sawa, ili uelewe lengo langu...’akasema
‘Kwahiyo unahisi mdada
anahusika na hilo?’nikauliza
‘Hapana, sijasema
hivyo, ndio maana natafuta ukweli, wa tetesi za watu...’akasema.
‘Tetesi za watu....ina
maana watu wanasema hivyo?’ nikauliza.
‘Wanashindwa kusema
hivyo moja kwa moja, maana wanaogopa, na hawajasema moja kwa moja kuwa ni
mdada, na lengo letu ni kutafuta ukweli, ..’akasema.
‘Kwahiyo wewe
unachunguza maneno ya mitaani, ...nilifikiri kuna mtu kashitakia, na ndio
unafanay uchunguzi....’nikasema.
‘Sikiliza ndugu yangu,
ikuulizi kwa ajili ya maneno ya mitaani, kuna hilo tatizo, lipo kwenye jamii
yetu, limeshawakuta watu wengi,...na kila ninamuhoji, huwa anaweza keshakutwa
na hayo matatizo, au anakuja kukutwa na hayo matatizo, cha msingi ni kutoa
ushirikiano ili hili tatizo liishe...’akasema
‘Tatizo gani, mbona
hujalisema...mimi sikuelewi, sijaliona tatizo hapo, na kwanini mimi ?’
nikauuliza.
‘Kama nilivyokuambia,
kuna kundi limezuka, la watu kujifanya waandishi wa habari, au madalali, watu
hawa wapo kila sehemu maalumu, wamejipanga, ...na kwa vile wamejikita kila
nyanja, wanakuwa ni wepesi kuchota taarifa za watu, hasa wageni,kwa minajili ya
kuwatisha na kuwaibia....wanachofanya wao ni kubuni kashfa, na kuipandikiza kwa
watu wanaowalenga, na kuitumia hiyo kashfa kujiingizia kipato kisicho halali,
wanadai pesa,...au chochote....’akasema.
‘Mna uhakika na hilo?’
nikauliza
‘Tuna uhakika nalo
ndio maana tunafanya uchunguzi, ili tupate ushahidi, tatizo ni kuwa wahanga wa
hayo yote hawataki kusema ukweli,kwa jinsi walivyofungwa, na hapo inatuwia sisi
vigumu, kulisambaratisha hilo kundi, hakuna ushahidi wa moja kwa
moja...’akasema
‘Sasa hiyo ni kazi
yenu, ...fanyeni kazi yenu, lakini mimi siwezi kuwasaidia kwa hilo maana sijui
lolote...’nikasema.
‘Una uhakika na
hilo...?’ akaniuliza
‘Una maana gani kusema
nina uhakika?’ nikamuuliza.
‘Wewe uandishi wa
habari, ndio fani yako?’ akaniuliza na kunifanya nishituke, akawa analikunjua
gazeti na mimi sikumpa muda nikasema
‘Uandishi wa
habari..mimi sio mwandishi wa habari, mimi ni mhasibu...tafadhali naomba
uondoke...’nikasema na yeye akatabasamu na kusema
‘Nitaondoka, hapo
utakaponiambia ukweli, ....wewe kazi ya undishi wa habari, umeupatia wapi....?’
akasema akibadilika sura.
*********
Bosi alipofika alisema mdada anaendelea vyema,
na atakuwa na siku mbili zaidi za mapumziko, kabla ya kuweza kuja kazini,...
‘Oh, kwahiyo mliweza
kuongea?’ nikamuuliza
‘Yah, of course , mimi na mdada tunaongea
vyema kabisa kuachia maswala ya kikazi, lakini mambo yake ya nje, alipotokea ,
ananisimulia sana, kwahiyo namfahamu kuliko mtu yoyote...’akasema bosi.
‘Kwahiyo kumbe
unafahamu mambo yake ya siri, anayoyafanya...’nikajikuta nimesema.
‘Inawezekana mengine
asiniambie, maana sio kila kitu unaweza kumwambia kila mtu, kuna mambo unaweza
kumwambia huyu au yule hata kama ni rafiki yako, bado utakuwa na mipaka ya
mambo yako ya siri...’akasema.
‘Nilikuwa na hamu ya
kusikia kuhusu maisha yake ya huko nyuma, ilitokeaje mapaka akawachukua
wanaume..’nikasema
‘Ipo siku
nitakusimulia, kama yeye mwenyewe akitaka nifanye hivyo, vinginevyo kwasasa
ninalokuomba ni kutokumuulizia hayo...kwa ajili ya usalama wako...’akasema
‘Mhh, kwa hali hiyo
utanifanya nimuogope sana mdada..japokuwa...mmh...’nikatulia
‘Japokuwa mhhhh, nini
tena, sema ukweli, japokuwa umetokea kumpenda ...au?’ akauliza bosi huku
akitabasamu.
‘Siwezi kusema hivyo
bosi, ukumbuke mimi nina mchumba wangu, siwezi kumsaliti mchumba wangu,...,ila
tu,...mhhh, kiukweli, nimetokea kumzoea sana mdada,...sio kawaida yangu
kuzoeana na akina dada, kama nilivyomzoea mdada, moyoni kwangu namuona kama
eeh,tuseme, dada yangu...’nikasema.
‘Nimekuelewa, uipate
shida,...hata yeye kasema hivyo...’akasema bosi na kucheka kidogo.
‘Unasema hata yeye
kasema hivyo, ina maana mlikuwa mnaniongelea mimi?’ nikauliza nikiwa na
mashaka.
‘Ilitokea hivyo, tukakuongelea
kwani aliuliza kuwa upo salama, umeweza kufika kazini, na nilipomuuliza kwa
vipi awe na wasiwasi na wewe, akasema huenda alipochanganyikiwa, aliweza
kukuumiza...nikamuuliza ina maana wakati anachanganyikiwa ulikuwepo, akasema
ndio, ulikuja wakati yupo kwenye wakati mgumu, kama angelijua
unakuja,angekuzuia...’akasema bosi
‘Hivyo tu....?’
nikauliza nikimwangalia bosi.
‘Hivyo tu una maana
gani,..ulitarajia tuongee nini zaidi, kama kuna mengine ambayo unahisi ulitaka tuyaongee,
haikutokea hivyo, ila alichoniotuma kwako wewe ni kuwa ujitahidi sana upitie
kwake leo hii ukitoka kazini,...’akasema na mimi moyo ukaanza kunienda mbio, na
kwa wasiwasi nikasema;
‘Lakini bosi umesema
yeye hataki wanaume wamkaribie..sasa huoni najipeleka kwenye tatizo...?’nikasema.
‘Cha msingi ni wewe
kuchunga ulimi wako, ongea mengine, lakini usimuulize maswali yaliyomtokea
akiwa mdogo...ndilo la msingi, mengine ni maswala yenu binafsi mimi siwezi
kuwaingilia, ila...kama kuna lolote, unahisi unahitajia msaada wangu kimawazo,
mlango upo wazi,...na mapema ni bora zaidi, kabla hali haijawa mbaya...’akasema
bosi
‘Kwanini unasema hivyo
bosi, ....?’ nikauliza
‘Kusema hivyo kwa vipi
tena, ni ushauri wangu kwako...ulitaka nikushauri vipi?’ akaniuliza
‘Nafikiria hiyo kauli
uliyosema kuwa, kabla hali haijawa mbaya...’nikasema
‘Ni hisia zangu tu,
maana kila siku naona kama vile wewe unajiiingiza kwenye matatizo, na akilini mwangu,
ninahisi kuna jambo linakukabili, lakini hutaki kuwa muwazi kwangu..ni hisia
tu, sio zaidi, ...’ akasema bosi.
‘Mhh, hapana bosi,
hakuna kitu....’nikasema kwa sauti ya kutokujiamini.
‘Unaikia, nikuambie
ukweli, ilivyo, na kawaida, ukiona upo kwenye hatari, unahisi hali sio nzuri,
ni bora ukamuona dakitari haraka iwezekanavyo,..ili ujikinge, sio usubiri
tatizo litokee ndio uende kutibiwa...’akasema bosi.
‘Lakini mimi
siumwi...’nikasema.
‘Yah, kuumwa sio
lazima ugonjwa, kuna matatizo ya kijamii, yenye mlengo mbaya, kuna vikwazo vya
kimaisha, kuna majaribu ya hapa na pale, unaweza ukajikuta upo kwenye hatari,
au unahisi hatari inaweza kutoke,....kwa majambo kama hayo, kuna watu wazuri wa
kusaidia..mfano kama ni makosa ya kisheria, kuna watabibu ambao ni wanasheria,
hao ndio madakitari wa hayo matatizo....sisi tuna mwanasheria wetu, wa
kampuni,kwa sasa, hana kazi nyingi, tunaweza kumtumia...’akasema bosi.
‘Kwanini
mwanasheria,...mimi sijafanya makosa yoyote ya umhitajia mwanasheria..’nikaanza
kujitetea.
‘Sijasema una
makosa...ila kama unahisia kuna tatizo linaweza kutokea au upo njia panda, ya
kisheria, au kuna vitisho, vinavyoweza kukutumbukiza kwenye mattizo ya
kisheria, ni bora ukajihami...’akasema bosi
‘Sawa nimekuelewa
bosi,...kama nitakuwa na matatizo, sitasita kufanya hivyo,..’nikasema
‘The sooner the better.. wahi mapema kabla
mambo hayajaharibika...’akasema na kuingia ofisini kwake.
Siku hiyo ilikwenda
haraka sana, maana nilikuwa na kazi nyingi za kimahesabu, na wakati napeleka taarifa za mahesebu kwa
bosi, bosi akaniambia.
‘Ngoja nikusimulie
kidodo, nakumbuka sehemu iliyopita tuliikatisha, na ni vyema tukamalizia sehemu
hiyo muhimu kabla hatujaingia kwenye ehemu nyingine ya masiha yangu
yalivyokuwa, au una kazi nikuache, tukutane kesho,...?’ akaniuliza
‘Nimeshamaliza kazi bosi,
....nipo tayari.kusikiliza.’nikasema
‘Na tukimaliza, usisahau
kumpitia mdada....’akasema bosi akiangalia saa yake.
‘Mhh, nitaangalia,
kama ni lazima nitakwenda kumuona, hamna shida....’nikasema
‘Kama una wasiwasi
tutaongozana...’akasema
‘Hapana sina wasiwasi bosi, , nitakwenda tu kumuona,
kama ananihatajia..’nikasema
********
‘Kwanini mumemchelewesha huyu mtu....?’ aliuliza dakitari
akionyesha wasiwasi kwani alisema kichwa cha mtoto kilishaanza kujitokeza, na
hiyo ni hatari.
Hakuna aliyeweza kumpa jibu, na mume wangu akagizwa beseni na
vifaa vingine, na mimi nikawekwa kwenye hilo beseni na kunikimbiza leba na hapo
kiakili nikawa mimi na mungu wangu , kipindi hicho mume wangu alikuwa katumwa
kwenda kununua baadhi ya vifaa vilivyohitajika kwenye duka lao, japokuwa
alikuwa anaumwa lakini kutokana na hali yangu ilibidi kuumwa kwake
akusahau.....
Tuendelee kuanzia hapo......
Namshukuru mungu, alinipa
subira na kunisimamia kwani licha ya hatari iliyokuwepo kuwa huenda tukampoteza
mtoto, lakini kwa uwezo wa muumba, baada ya dakika tano nikajifungua kichanga,
....nilitulia na kumshukuru mungu pale niliposikia kilio cha mtoto.
‘Hongera umejaliwa
mtoto wa kiume...’ilikuwa sauti ya mkunga, na akaniletea kitoto hicho usoni,..nikakiangalia
huku nikiwa sina nguvu hata ya kuinua mkono. Mkunga akakiondoa kichanga kile
kwa ajili ya kukihudumia.
Baadaye ,mume wangu
ambaye alitumwa baadhi ya vifaa alirejea, na mkunga akamwambia;
‘Wewe muda wote
ulikuwa wapi, umeshachelewa...’akasema na kumfanya mume wangu abakie mdomo
wazi,akihisi kuna hatari, docta aliyekuwa akimuhudumia mtoto, akamwangalia mume
wngu, na ili kumuondoa wasiwasi, akakinua kile kichanga, na kumuonyesha,
akisema
‘Hongera mzee,
mumepata mtoto wa kiume, hana matatizo yoyote...’akasema huyo dakitari, na mkunga
akacheka na kusema;
‘Mwanaume alishaanza
kuabdilika....hongera bwana...unaruhusiwa kumkaribia mke wako...’akasema
Mume wangu kwa furaha akasogea kwa dakitari na
kumpokea yule mtoto, lakini dakitari akasema asubiri kidogo, kuna huduma
anafanyiwa huyo mtoto kwanza, basi mume wangu alikaa karibu yangu akiwa
anamwangalia mtoto anavyokuwa akihudumiwa na dakitari.
Baadaye tulikabidhiwa
mtoto wetu, na mume wangu akawa habanduki karibu yangu akionyesha uso wenye
furaha, na huku tukisubiria chakula, tukitarajia chakula cha mzazi kitaletwa
kutoka huko nyumbani, lakini hadi inafika jioni, hakukuonekana dalili ya mtu
kuleta chakula.
‘Mke wangu hapa naona
hakuna dalili ya mtu kuleta chakula..’akasema
‘Sasa utafanya nini?’
nikamuuliza
‘Inabidi nikanunue chakula
cha gengeni, hakuna jinsi hapa....’akasema
‘Pesa unazo...maana ?’
nikamuuliza na yeye bika kusubiria maelezo yangu akaondoka, nilimuonea huruma
maana nafahamu kabisa anaumwa, lakini anajikaza tu.
Baadaye alirudi akiwa
kabeba chakula cha gengeni na kwa mara ya kwanza nilikula chakula bila kujua
kilitoka wapi,nikamshukuru mume wangu, na kujiathidi kula, ili maziwa ya mtoto
yapatikane, kwani kichanga kilishaaza kudai haki yake .
Na ilipofika saa moja za
usiku ndio wifi yangu akaja na chupa ya uji, akiwa kanuna, inavyoonekana
hakupenda kufanya hivyo, ilikuwa kama kalazimishwa, akafika na kuitoa ile chupa
iliyokuwa na uji, akaiweka juu ya meza, akaanza kuondoka, na alipofika mlangoni
akawa kama kasahau kitu akageuka na kuniangalia, akasema
‘Hongera mzazi,
umeleta mtoto gani?’ akauliza, nafikiri aliuliza hilo swali kwani alijua kuwa
akifika nyumbani ataulizwa swali kama hilo na atakuwa hana majibu sahihi,
japokuwa nina uhakika huenda kaka yao, yaani mume wangu atakuwa keshawaambia,
na nahisi ndiye aliyemlazimisha kuleta huo uji.
‘Mtoto wa
kiume...’nikasema
‘Mtu wewe una bahati
kweli...unaujulia sana utaalamu wenu, maana wa kwanza jike, wa pili dume,
unatupangilia eeh,..mmh, kweli mumechanjia, lakini usifikiria mimi bado nina
furaha na wewe...nina usongo na wewe, kwa jinsi ulivyomfanyia mama yangu, mimi
bado nawazia jinsi gani ya kukufanya...’akasema
‘Wifi hayo yametoka
wapi tena...’nikasema
‘Ngoja urudi nyumbani,
...utajua yametoka wapi tena...ninahangaika usiku na mchana kutafuta dawa
yako....labda nife, lakini nikiwa hai hivi hivi tutapambana....’akasema na kufungua
mlango, akaondoka, hakutaka hata kumuangalia mtoto.sikujali, nilishaanza
kuwazoea.
Nililala hapo
hospitali siku hiyo na kesho yake, tukaruhusiwa kurejea nyumbani, na akilini
mwangu nikisema, narudi kwenye uwanja wa vita...
NB: Itakuwaje
WAZO LA LEO:
Kuna majanga yakitokea kwa mwanadamu, huleta athari kubwa kwenye ubongo wa
mwanadamu, na matokea yake yanaweza yakaharibu mfumo mzima wa akili, mwili na
utashi wa kufikiri. Kuna vyanzo vya matatizo hayo, na vingi vinaanzia utotoni,
kwenye ajali, kubakwa na vitu kama hivyo.
Jamii sasa
zinaharibika, na ukichunguza sana, chanzo kikubwa ni malezi, ukiukwaji wa haki
za watoto, watoto wanakosa elimu, wanakosa malezi bora. Elimu sasa ni kwa wenye
kipato,kuna tofauti kubwa inayoanzia hapa, hili haliangaliwi sana, ....jamii
kubwa inakosa haki hizi, ...Tusipoangalia vyanzo vya matatizo haya,
tukakimbilia kutibu, itakuwa hatujafanya lolote.
Ni vyema tukaangalia
chimbuka la mmonyoko wa maadili, tukaangalia tatizo hili linaanzia wapi, na ni
ukweli usiopingika kuwa tatizo hili linaanzia kwa watoto wetu wanaokosa haki
zao za masingi. Tusipoziba ufa, tusipomkunja samakini akiwa mbichi,...tujue
kuwa yanayotoea kwa wenzetu ipo siku yatakuja kutokea hapa kwetu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment