Nikiwa njiani kuelekea
kwa mdada, garo moja dogo lililokuwa likiendeshwa kwa kasi, lilinipita na kuja
kusimamishwa mbele yangu, ikanibidi nifunge breki za haraka, karibu kujigomga
kwenye hilo gari, na mara wakatoka watu wawili, wakanizunguka, na mimi nikawa
nimejiandaa kwa lolote maana siku hizi usalama ni mdogo, nilijua hawawezi
kufanya lolote maana ilikuwa sehemu yenye watu,
‘Ndio pikipiki yenyewe
hii...’mmoja akasema
‘Naona ndio yeye, namba
ni zile zile...’akasema mwingine.
‘Ndugu tunaomba uvue
kofia yako, tunataka utambuliho mdogo...’akasema huyo mwingine.
‘Mimi siwaelewi,
...mnataka nini kwangu?’ nikawauliza
‘Tunataka kuhakikisha
kuwa ndio wewe au ni mtu mwingine...’akasema
‘Mnataka kuhakikisha
nini, mimi siwaelewi, ...’nikasema kwa mshangao
‘Kama hutaki hakuna
shida, ...hapa hatuwezi kukufanya lolote, muda ukifika, kama ni lazima,
hutakuwa na muda wa kujitetea,...maana siku hizi kila mtu anajifanya mwandishi
wa habari,...’akasema
‘Mimi sio mwandishi wa
habari..’nikasema
‘Tunafahamu hilo, kuwa
wewe sio mwandishi wa habari, ila unaiga kazi za watu kwa ajili ya utapeli,....kama
ni wewe uliyefanya hivyo, tunakuonya uwe makini, maana umechezea
kubaya...’akasema
‘Msinitishe kabisa
nyie, mimi sifanyi kazi hiyo, kama mumetumwa, mwambie huyo aliyewatuma kuwa
mimi siogopi kitu....na ole wenu nipate matatizo, nimeshawamaki sura zenu,
nitahakikisha mnaenda jela...’nikasema kwa kujiamini.
‘Hahaha
jela...ohoo,kwa taarifa yako, huko ndipo
nyumbani,...usijali,...jana tu mwenzangu katokea huko, ....’akasema na kumwangalia
mwenzake, na walipoona watu wanakuja kujazana, wakakimbilia kwenye gari lao na
kuondoka.
Tukio hilo lilinifanya nizidi kuwa na
wasiwasi, niliona sasa maisha yangu yapo hatarini, na yote haya ni kutokana na
mdada, na sijui wamejuaje kuwa mimi siku hiyo niliigiza kama mwandishi wa
habari kwa shinikizo la mdada,.....
‘Mdada kanitia
mashakani, sijui nitafanya nini....’nikasema na huku naendelea na safari yangu
hadi nikafika nyumba anapoishi mdada, akanifungulia mlinzi, na mlinzi
aliponiona akasema;
‘Ohooo, mhasibu wa
bosi umerudi tena...’akasema huku akifungua geti, na nilipoingia ndani
nikamuuliza
‘Mdada yupo?’ nikamwangalai
huku naangalia muelekea wa mlango wa ile nyumba, ulikuwa wazi
‘Unamuita kwa jina,
...huna nidhamu, eeh, sema bosi yupo,...simzarau bosi wangu, na ni bosi wako
pia, au sio,...?’akasema huku kashika kiuno, halafu akawa kama kashituka
akashusha mikono na kusimama kama askari, akasema;
‘Yupo, kajaa tele huko
ndani, kaniambia kuna mgeni wangu atafika, sijui ndio wewe..ngoja
nikamuulize...’akasema huku akiliangalia pikipiki langu kwa macho ya hamasa.
‘Mbona unaliangalia
sana pikipiki langu?’ nikamuuliza na yeye akatabamu, na kuendelea kuangalia, na
sasa alikuwa akiangalia namba za hiyo pikipiki,akatikisa kichwa kama kukubali
‘Sikukosea ndio hiyo
hiyo...mimi ni mkali, ikufaulu kwa sababu ya umasikini, ningelikuwa mbali sana...’
akasema sasa akilishika shika na baadaye akasema;
‘Hata hivyo mimi nimelipenda
sana hilo pikipiki,..naona hata watu wanaliulizia, ....’akasema halafu akasita
kuongea
‘Wamekuulizia kuhusu
nini?’ nikamuuliza
‘Mhh, nahisi
wanakutafuta,au wanamtafuta mtu...’akasema
‘Akina nani hao watu?’
nikamuuliza
‘Siwajui
bwana...tatizo lenu hamjui kula na vipofu...mmhh’akasema huku akiweka mikono
mfukoni, akapiga miayo, halafu akageuka na kujifanya anaondoka, na mimi nikakumbuka
safari iliyopita, nikatoa pesa mfukoni, nikamsogelea na kumhika mkono wake,
halafu nikamshikisha ile pesa kwenye mkono wake, akaipokea kwa haraka na
kuifutika mfukoni, akasema;
‘Mhasibu wewe bwana,
unanijulia, maana nyie muda wote mnacheza na pesa, nyie hamlali na
njaa,...unajua leo nilikuwa najiuliza nitakula nini, ...haya niambie,umeniuliza
swali gani vile...?’ akageuka kuniangalia
‘Hao watu walioulizia
pikipiki langu ni akina nani?’ nikauliza
‘Hawa watu bwana kwanza
niliwashitukia, wao walikuja wakaanza kuniongelesha, wakijifanya watu wa
ukaguzi wa mejengo, wakataak kujua mmumiliki, baadaye ikaona wanakuja na
mengine, eti wanataka kufahamu ni mtu gani anafika fika hapa kwa mdada mara kwa
mara, ...sijua lengo lao ni nini....wakanizuga mpaka, nikajikuta nimekutaja
wewe kuwa uliwahi kufika, ...’akatulia
‘Kwanini unitaje,
kwani walitaka kujua nini hasa?’
nikamuuliza
‘Walitaka kujua ni
nani anatembea na bosi mwenye pikipiki...nahisi wana mtu anamtaka bosi,
nikawaambia bosi hahitajii watu wenye mkono mfupi,...wakauliza ni nani alifika
hapa karibuni, nikawaambia bosi ni mtu mkubwa, ana mhasibu wake anakuja na
pikipiki...’akasema
‘Ukawaambia hivyo?’
nikauliza
‘Ndio nilitaka
kuwaonyesha kuwa bosi sio mtu mdogo kama wanavyofikiria wao,...na nilipotamka
pikipiki, nikaona wakipeana ishara,...’akasema
‘Halafu wakasema nini?
‘Wakauliza namba za
pikipiki yako, na mimi nikataka kuwaonyeshe kuwa mimi ni askari wa kweli,
anayeweza kukariri namba kwa dakika chache,...kichwa changu sio mchezo,
nilishaiweka namba ya pikipiki lako kichwani, nikawatajia namba ya pikipiki
lako...baadaye wakaondoka....’akasema na hapo nikakumbuka wale watu
walionisimamisha,..
‘Hao watu wapoje?’
nikamuuliza
‘Ni watu tu hivi,
inaonekana ni wale wapuuzi wa mitaani kazi yao kupewa kazi, na hawaulizi kazi
gani wanaifanya tu....watu wabaya sana hao, hata kuua wanaweza kuua kwasababu
ya pesa...’akasema
‘Kama unafahamu hivyo
kwanini ukaawaambia kuhusu mimi?’ nikamuuliza
‘Mwanzoni nilijua ni
watu tu....lakini nilipofikiria sana na kujaribu kuwakumbuka ndio nikafahamu ni
watu gani....lakini usijali, hawana lolote wale, wanatafuta ujiko kwa mtu wao,
aliyewatuma, nahisi kuna mtu kawatuma kuangalia kama mdada ana
mshikaji,...’akasema
‘Basi naomba ukamwambie
mdada, nimeshafika...’nikasema na haraka akaenda na pindi akarudi na kuniambia
mdada yupo tayari kuniona...
Nikaingia ndani na
kumkuta mdada, akiwa kakaa kwenye sofa, huku kaweka miguu juu ya sofa kubwa, ni
kama mtu aliyelala, na nilipoingia akawa ananiangalia moja kwa moja usoni, bila
kupepesa macho, mpaka nikaingiwa na wasiwasi tena.
Baadaye nikamkaribia
na kusimama nikawa na mimi namwangalia akatabasamu na kuuliza
‘Unaniogopa?’ akauliza
huku akiendelea kuniangalia?
‘Kwanini nikuogope?’
nikamuuliza huku nikjaribu kutabasamu, lakini kiukweli moyoni nilikuwa na wasiwasi
nikikumbuka tukio la siku ile.
‘Mbona huji kukaa
karibu na mimi....njoo ukae hapa karibu na mimi..uiniogope....’akasema na mimi
nikasita kidogo, lakini nikaona nisimfanye ajisikie vibaya nikaenda kukaa
karibu naye, na akainuka na kushusha miguu chini, halafu akapitisha mkono wake
nyuma ya mgongo wangu akawa kama ananiegemea, kama kudekea, akatulia kwa muda,
halafu akaniangalia na kusema;
‘Nilikuwa na wasiwasi
sana...’akasema
‘Wasiwasi wa nini
mdada?’ nikamuuliza
‘Nilikuwa nawaza,
huenda nilikuumiza, au hata kuku...ku..ua...’akasema kwa kusita
‘Kuniua, kwanini unie,
kweli unaweza kuniua...hapana huwezi kufanya hivyo, ...’nikasema nikichelea
kuongea zaidi.
‘Mhh,... ni kweli nahisi
hivyo, ...maana huwa hali ikibibadilika, huwa sijitambui, na wala sijui
yanayotokea muda huo..., lakini ninachojua mimi ni kuwa kuna hali , hasa
nikianza kukumbuka mambo ya nyuma, ninakuwa na hasira mbaya sana, na muda huo
siogopi, naweza hata kuua...’akasema huku akitikisa kichwa kama mtu aliyeguswa
na mdudu nikamwangalia kwa mashaka.
‘Pole sana mdada, cha muhimu
kwasasa ni kuangalia afya yako, kwani unajisikiaje kwa sasa...’nikamuuliza.
‘Najisikia kuwa na
wewe karibu, na natamani kukushika hivi....’akanishikilia na kuwa kama
ananikumbatia, na mimi nikawa najaribu kujitoa kwake, lakini nikakumbuka kuwa
sitakiwi kumkasirisha, nikatulia, halafu yeye akaniachia na kusema;
‘Najua utakuwa
unaniogopa, kuwa huenda hali kama hiyo iliyotokea,inaweza ikarudi tena, ni
kweli bado kichwa hakijakaa sawa, inachukua muda, lakini hata hivyo, nakuomba, usiniogope,
maana kama ungekuwa kama hao wanaume wengine, nahisi leo hii tungeliongea
mengine, akili yangu inanituma kuwa wewe ni wangu...’akasema
‘Mhh, kwani uhisi
hivyo, huwezi kufanya kitu kibaya kwangu...mmh, kwani ulishawahi kufanya hivyo
kabla?’ nikamuuliza na yeye akainama na kushika shavu.
‘Waliniambia mengi, na
sijui, sina uhakika...ila walisema, yule aliyenifanyia hivyo, nikiwa mdogo....hayupo
duniani tena,...walisema siku nilipokutana naye, nilimfanya kitu kibaya sana, hakuna
aliyeamini kuwa ni mimi nilifanya hivyo, ndio maana wakayamaliza kiaina....’akasema
huku akipandisha miguu juu ya sofa akawa kama anajikunyata
‘Mungu wangu ulimfanya
nini huyo mtu...?’ nikamuuliza
‘Nilimuua....nikamkata
kata...’akasema na mara akasimama na kuanza kushikilia kichwa
‘Mdada, upo safi...?’
nikamuuliza
Na yeye akanionyeshea
kwa mkono kama ishara ya kuniambia nitoke humo ndani haraka..lakini kabla
sijafika mlangoni akanidaka,na sauti ile ile ya kiume ikaniambia;
‘Nilichokuita hapa ni
kuwa,...ni lazima na wewe ufe,.....lakini huyu kiti wangu anajifanya kukupenda,
sasa kama kweli anakupenda,... nataka umuoe huyu kiti wangu, na mimi
nitamuachia kabisa, vinginevyo, kama usipomuoa yoyote utakayemuoa, hataweza kuishi
na wewe atakuwa maiti...hahahaha..haya ondoka kajiandae kwa harusi...’akanisukuma
kwa nguvu nikadondokea nje...
Nilidondokea nje, na
haraka haraka nikiwa na wasiwasi..., na mara sauti kama ya yowe ikatoka ndani kwa
mdada, nikasimama kugeuka kumwangalia,...wakati huo mlango bado ulikuwa wazi,...
nilimuona mdada akiwa kama anayumbayumba na mara akadondoka sakafuni, akatulia
kimiya, na mimi pale niliposimama nikawa najiuliza nifanye nini...
Simu yangu ikaita,
...nikaangalia alikuwa ni bosi, nikaipokea na kusema
‘Ndio bosi...
‘Kuna usalama huko,
mdada anaendeleaje?’ akaniuliza
‘Hali imebadilika
ghafla...’nikasema
‘Ondoka hapo haraka,
....nitampigia simu dakitari wake, aje hapo...’akasema na kukata simu, na mimi
nikaushika mlango na kutaka kufunga, mara mdada akajitingisha, na kuinua
kichwa, akasema kwa sauti yake ya kawaida;
‘Usiondoke,
...sitakuambia nilichokuitia....’akasema
********
Nilikuwa nje ya geti
la nyumba ya mdada, nikiwa najiandaa kuondoka, mara gari la bosi likaja, na
nyuma yake kukaja gari jingine likuwa na mwendo kasi, likasimama nyuma ya gari
la bosi na kupiga honi, bosi akasogeza gari lake, na hilo gari jingine
likaingia ndani,nahisi lilikuwa gari la huyo dakitari wa mdada, bosi akaniuliza.
‘Vipi bado upo hapa,
mdada anaendeleaje?’ akaniuliza hakuingiza gari ndani, na bado alikuwa ndani ya
gari,lakini alikuwa akiongea na mimi akiwa kashusha kiyoo cha gari lake.
‘Mdada alikuwa kama
kapoteza fahamu hali ilipomrejea, na alipozindukana akaniambia nisiondoke, hata
hivyo mimi naogopa huenda akizindukana anaweza kufanya lolote dhidi yangu....’nikasema
‘Kwani ilikuwaje?’
akaniuliza
‘Nilipofika tu, akawa
anaelezea, kuwa alikuwa na wasiwasi, kuwa huenda aliniumiza au hata
kuniua...nilijaribu kumsihi asiongelee hayo mambo, lakini kila tulipojaribu
kuongea mambo mengine, ikawa mara kwa mara anajikuta akiongea jambo linalogusa
mambo yake ya huko nyuma...’nikatulia kidogo
‘Kama lipi
aliloliongelea ambalo lilifikia hatua ya kumfanya abadilike...?’ akaniuliza
‘Alisema mimi
nisimuogope maana sipo kama wanaume wengine, kama ningelikuwa sawa na wanaume
wengine, huenda angalishanifanya kitu kibaya,...’nikatulia
‘Hivyo tu,..nahisi kuna
jambo atakuwa akliongelea likampandisha hasira, mliongea nini zaidi...?’akauliza
bosi
‘Alisema huenda huko
nyuma alishawahi kuua....’nikasema
‘Kuua, hapana...hiyo
sio kweli...!?’ bosi akawa kama kashituka kusikia hivyo, akageuka kuangalia
kule mlangoni, akasema
‘Hilo liachie hapo
hapo....kama alisema hivyo, huenda alisema kwa kuchanganyikiwa, usije
ukamsimulia mtu hayo maneno tena,...je kuna jingine zaidi ya hilo?’ akaniuliza
‘Mhh, hilo jingine ni
kubwa zaidi, linanifanya niogope,...’nikasema
‘Lipi hilo,...amesema
na wewe atakuua, au kitu kama hicho, ndio unaogopa?’ akaniuliza
‘Kasema ni muoe...la
sivyo...’nikatulia
‘Atakuua..’akamalizia,
bosi,
‘Mhh, kitu kama hicho,
..ila kwa kauli ya moja kwa moja alisema nitakaye muoa na kumuacha yeye, huyo
mwanamke atakuwa maiti...’nikasema
‘Mhh,....unaonaeeh,
kazi ipo, lakini, hayo ni maneno tu, yasahau kwa sasa...cha muhimu ni huyu mtu
apone na asahau mambo yake ya nyuma, na mimi naanza kuhisi kuwa wewe unaweza
kuwa msaada wake mkubwa, maana naona kakuamini sana..’akasema bosi.
‘Lakini bosi mimi nina
mchumba wangu tayari, ambaye siwezi kumuacha,...na kama akisikia hivi nitakuwa
matatani....’nikasema
‘Sasa utafanya
nini..hata hivyo sijakushauri kuwa umueche mchumba wako, yote ni maswala ya
muda, cha muhimu, ni kumsaidia huyu mtu apone,...mengine yatajileta yenyewe....’akasema
‘Mhh, hayo sasa
yananiweka kubaya, hujui yaliyotokea huko kijijini, .....mkwe wangu hataweza
kuvumilia haya,akisikia ataniweka ndani...’nikasema
‘Lakini kama ulifahamu
hivyo,..kwanini ukajenga urafiki na mdada, unakumbuka tangu mwanzoni
nilishakukanya sana kuhusu mdada, ....’akasema bosi.
‘Sasa nitafanya nini
bosi?’ nikamuuliza
‘Kwanza malizana na
mdada,...ni muhimu mkamalizana naye haraka iwezekanavyo, ili ajijue nafasi
yake, ...’akasema
‘Kwa vipi?’ nikamuliza
‘Katika maisha hakuna
jambo jema, kama kuambiana ukweli, ...nikuanavyo wewe kiukweli unampenda sana
mdada, na huenda kuliko hata huyo mchumba wako,...kosa mnalolifanya ni tamaa,
mnashindwa kudhibiti tamaa zenu,...’akasema bosi.
‘Tamaa, lakini mimi
sikuwahi, kumtaka mdada, ni yeye....’nikakatisha maneno.
‘Alikushika kwa nguvu,
alikutaka yeye kwa nguvu, siamini kuwa mdada anaweza kufanya hivyo, yeye ni
mwanamke tu,...au hiyo hali iliwahi kutokea ikakulazimisha kumtaka huyo mdada
kwa nguvu...?’ akaniuliza.
‘Hapana haijawahi
kutokea kabla, kama ilivyotokea hivi sasa...’nikasema
‘Sasa ni hinikizo gani
lilitokea hadi uwe mpenzi wako, maana sizani kama anaweza kukuambia maswala ya
kuoana, kama hakuna mapenzi, mahuiano ya karibu,..hebu niambie ukweli kulitokea
nini?’ akaniuliza
‘Bosi hakuna kitu kama
hicho, naona mdada ananishinikiza tu, na sizani kama anafanya hivyo kwa ajili
ya mapenzi ya kweli....’nikasema
‘Mimi namfahamu sana,
mdada, kiukweli anakupenda sana,...na nina uhakika mkiwa naye pamoja, hilo
tatizo lake litakwisha, nahisi anakuona wewe kama msiri wake, na unaweza
kumvumilia, kama hakuna shinikizo jingine ambalo hutaki kuniambia...’akasea
bosi.
‘Hakuna shinikizo
jingine bosi...ningekuambia...’nikasema
‘Haya kama unanificha
shauri lako,..’akasema na tukawa kimiya kwa muda, halafu akasema;
‘Ingia ndani ya gari, wakati
tunamsubiria dakitari akimalizana na mdada, nikuhadithie sehemu nyingine ya
mfulululizo wa visa vya maisha yangu...’akasema bosi
‘Kwahiyo nisubiri?’
nikauliza
‘Kama mdada
alipozindukana alikuambia umsubiri, ni vyema ukafanya hivyo, huenda kuna kitu
muhimu anataka kukuambia...’akasema
‘Sawa haya
...nitashukuru kusikia simulizi la maisha yako huenda likaniondoa haya mawazo na
wasiwasi niliyo nayo..’nikasema
*******
‘Kwenye sehemu
iliyopita, unakumbuka vyema kuwa tulifikia pale nilijifungua, kuwa mungu
alinijalia nikajifungua salama, na kesho yake ndio nikaruhusiwa kutoka hapo
hospitalini maana sikuwa na tatizo lolote. Na muda wa kutoka mume wangu alikuwa
hajui, kwani niliporuhusiwa tu mimi nikaondoka hapo hopitalini, hata hivyo, kwa
vile nilikuwa nafahamu kuwa mume wangu alikuwa anaumwa, sikupenda kumsumbua
kuwa aje kunichukua.
Nilipotoka hapo
hospitalini, nilielekea moja kwa moja nyumbani,
na nilipofika nyumbani ilikuwa muda wa mchana, niliwakuta wanafamilia wote
wakiwa wanapata mlo wa mchana,hakuna aliyejali kusimama kunipokea mtoto, au ile
hali yakuonyesha kuwa nimemleta mgeni, basi kila mmoja awe na bashasha ya
kumuona, na kumpokea, hawakufanya hivyo, tofauti na alivyopokelewa mtoto wangu
wa kwanza.
Sikujali, mimi nilipitiliza
moja kwa moja na kuelekea kwenye kibanda changu, kile kibanda ambacho kila kitu
kinafanyika humo humo, nilijua hakutakuwa na huruma kuwa kwa vile nina mtoto
mchanga, nikalale nyumba kubwa yenye nafasi, hata mimi sikupendelea iwe hivyo,
maana ningelikuwa sina amani zaidi.
Nilipofika kwangu,
nikishindwa hata nianzie wapi,nikaona ni bora kwanza niondoe kwa kujimwagia
maji, nilipofanya hivyo, nikamuogesha mtoto wangu.
Bahati nzuri nilikuta
ndizi, nahisi mume wangu alinunua kwa ajili yangu, lakini hakuweza kuzipika,
mimi nikazichemsha, ili niweze kupata japo kitu tumboni ili mtoto apate maziwa..baada
ya hapo nikaona nipate usingizi kidogo...
Kweli nikapumzika na
kujihisi kama mtu aliyetua mzigo mkubwa ..mzigo niliokuwa nao miezi tisa,
nikamgeukia mtoto wangu, kumwangalia alikuwa kalala, na nikimwangalia nikawa
naona faraja na kujihisi mwenye bahati, nikukumbuka kauli ya dakitari ya
kunikatisha tamaa, kuwa nimechelewa kufika.
Huku namwangalia mtoto
wangu, huku nawazia maisha yaliyopo mbele yangu, maana hapo nina mtoto mchanga,
nina mwingine ambaye naye bado mdogo,...ina maana natakiwa kuwahudumia, bila
kukata tamaa, na kazi yenyewe ni ya duka, na hivi sasa ina maana kazi imesimama,
maana mume wangu ana migangaiko yake, asingeliweza kukaa dukani
Na hali kama hiyo,
ilinifanya niombe mungu niwe na nguvu haraka, hata ikiwezekana kesho yake nikaendelee
na kazi yangu, ili tupate riziki,..lakini isingeliwekana kutokana kiafya,
....hata hivyo kazi za nyumbani zipo pale pale, usafi wa ndani, kufua nguo,
hasa za mtoto, hilo sikuwa na mtu na kunisaidia, na wakati nawaza hilo, mara
mlango ukagongwa.
‘Karibu, mlango upo
wazi...’nikasema
Akaingia msichana wa
kazi, ...wa familia, akiwa kabeba chakula, nikashangaa sana, nikajua hapo huenda
wameingiwa na huruma na ndugu yao,ambaye anaumwa, ndio maana wameleta chakula,
kwa mshangao nikakipokea hicho chakula.
Nikamuamusha mume
wangu kuwa ajaribu kupata hicho chakula , na kwa ujumla hicho ndicho
tulichoweza kupata kutoka kwao, bila kujali kuwa mzazi ana chakula chake
maalumu, lakini sikujali.
Usiku huo nikalala
fofo, ilikuwa kama mtu ambaye hajawahi kulala kwa muda mrefu na akapata mwanya
wa kulala,..unalala hata bila kugeuka, na kulipopambazuka tu, nilipomaliza
kumnyonyesha mtoto, nikasema hakuna kupoteza muda,nikaanza kazi za ndani kufua
nguo chafu, kwani unapojifungua nguo nyingi zinakuwa chafu, usafi wa ndani...
kazi ilikuwa kama kawaida.
‘Mke wangu utajiumiza,
kwani ni lazima ufanye kila kitu, muombe huyo mfanyakazi wa familia
akusaidie....’ akasema mume wangu.
‘Nitafanyaje, huoni
wanavyotusimanga, ni lazima nifanya kazi zangu mwenyewe...’ nikasema na yeye
akawa hana la kujibu. Ilibidi niwe ninaamuka asubuhi kufanya usafi kufua nguo
za mtoto, na pilika pilika zote za nyumbani bila kupumzika, kwani yule
mfanyakazi wetu alishaondoka kwao, kwa vile hatukuwa na cha kumlipa, aliyekuwa
akisaidia mara moja moja ni mfanyakazi wa familia.
Nilifanya kazi zangu
zote bila kuchoka na kujisahau kama nimetoka jana tu kwenye leba ya uzazi,ila
sikuwa na jinsi niliangalia nyumba kama mtu niliye kuwa mzima wa afya
kabisa,ila kama unavyojua hasara yake inakuja badae nilipoanza kupata maumivu
ya mgongo kupita kiasi. Mgongo ukawa unaniuma, lakini nitafanya nini.
Kuna muda niliingiwa
na wazo la kuwaambia wazazi wangu kutokana na hali iliyokuwa hapo, ili kama
wanaweza kunisaidia,lakini nilikumbuka nilivyowaambia mwanzoni na kauli yako
ilinikatisha tamaa;
‘Unasema nini, hayo
ndio maisha ya ndoa, vumilia, ndoa ndivyo ilivyo, kuna mitihani ya kukosa na
kupata...’akasema baba.
‘Lakini baba ni msaada
wa muda, nikijifungua, maana nijuavyo, pale sitapata msaada wowote...’nikamwambia.
‘Tulishakusaidia mtoto
wa kwanza, huyu sasa ni jukumu la familia yako,....’nikaambiwa
Nilihangaika na kazi
za nyumbani, na kidogo kilichopatikana kutoka kwa mume wangu, tukawa tunakula
hicho hicho, kwani alishajisikia vyema na kwenda kuhangaika.
Baada ya mda kidogo nilirejea katika biashara
zangu na kazi zangu za kila siku, hapo ilibidi nijipange jinsi ya kule watoto
na jinsi ya kuhangaika na biashara, hakuna aliyetaka kunisaidia, na wakiona nahangaika
hivyo bila kulalamika, ndio wanzidi kunipandikizia fitina.
Sikujali niliwaangalia
watoto wangu wawili kadri ya uwezo wangu, japokuwa kuna muda shemeji alikuwa
akimchukua huyo mtoto mkubwa, lakini sikuwa na amani kwani hata akimchukua na
kwenda kukaa na wenzao, yeye alikuwa akitengwa, na kunyanyapaliwa;
‘Wewe mdowezi, wewe
upo hivi....’akawa anaambiwa, na mimi hali kama hiyo sikuweza, niliona ni bora
nikae na watoto wangu wakati wote.
Kuna mda watoto
wanacheza pamoja, ikitokea ugomvi tu, anayeangaliwa kuwa ni mbaya ni mtoto
wangu, vurugu zikawa kila siku, visa vya kuzuliwa vikawa vinaongezeka kutoka
kwa mawifi.
Mimi nikawa nasononeka
moyoni, kwani sikufahia kuona watoto wangu wanatengwa na kunyanyaswa na ndugu
za mume wangu niliumia ila sikuwa na jinsi ,nilikaza moyo na kukabiliana na
kila linaloninijia...hata hivyo, ilikuwa kama wanataka kunikomoa kwani kila
siku kulikuwa na jipya la hakuna aliyekuwa upande wangu niliona hata mume wangu
hakuweza kunisaidia tena.
Mambo yalikua magumu mpaka
nikakumbuka usemi kuwa kuolewa ni tabu ,ndoa ni ndoana,..na kama ni taabu bai
mimi ilizidia, na kama ni ndoa basi mimi ilikuwa imenishika pabaya.
‘Mungu wangu nakuomba
unisaidie niondokane na mateso haya...’nikawa mara kwa mara namuomba mungu
wangu.
Ilikuwa kama walikamia
kuwa wanionyeshe kila aina ya uovu kwangu, zaidi sasa walilenga kwa watoto,
nikawa sina amani, nikiona watoto wangu wanapigwa, wanatukanwa, hawana raha na
wenzao, nikasema sasa basi, lakini basi nifanye nini
Wazo likanijia, kuwa
nihame kabisa kwenye hiyo nyumba, maana kinachotutesa , hasa watoto, ni kuwa ni
lazima watataka kucheza na wenzao, na wakicheza na wenzao, ndipo kunapotokea
visa, ili waonekane wao ni wabaya, na kusimangwa kuwa wao ni masikini, omba
omba....
Nikaona basi, ...
nikasema basi sasa inatosha, ni lazima nitafute njia nyingine, ni lazima nitoke
hapo, nikaanza kutafuta chumba au nyumba ya kupanga. Hilo kwanza nililifanya
kimiya kimiya bila hata kumjulisha mume wangu
Kwa bahati nzuri
nikapata nyumba ya bei rahisi kati kati ya mjini, nikauza baadhi ya vitu vyangu
vya dhahabu vilikuwa vimebakia na kupata kodi ya kuanzia na nilipohakikisha
nimefanikiwa hilo, ndio nikaja kumwambia mume wangu kuwa nimepata nyumba,
kwahiyo tunahitajika kuhamia kwenye nyumba hiyo;
‘Wewe una akili kweli,
tutapata wapi kodi ya kulipia hiyo nyumba?’ akaniuliza
‘Swala la kodi niachie
mwenyewe, cha muhimu ni kujiandaa kesho tunahama hapa...’nikamwambia na yeye
akaniangalia kwa mashaka, hakusema neno, akakubali shingo upande.
Kuondoka hapo, sikuchukua chochote zaidi ya godoro, tukaenda kuanza maisha
mapya, ya kununua kila kitu...ilikuwa ni kazi nzito lakini hatukuwa na jinsi,
tukajitahidi hivyo hivyo,lakini tukiwa na uhuru, hakuna mtu wa kutunyanyasa
tena.
Tukiwa katika maisha hayo magumu, nikawa
naingiwa na hamasa ya kufanya kitu kikubwa zaidi, nikijiuliza iweje wengine
wafanikiwe, waweze mimi nihindwe, na hapo wazo la shule, yale tuliyojifunza
kuhusu mikopo, na jinsi nilivyosikia kwa watu wengine, kuwa mikopo inaweza
kutumika vyema, na kuleta maendeleo, hilo wazo lilinijia kichwani na hamasa ya
kupata mkopo ukanijia....nikaona na mimi lazima nijaribu kuchukua mkopo.
Baada miezi kadhaa ya kuliwazia hilo huku
nahangaika na biashara yangu hiyo, ikafikia muda nikasema sasa naweza,
....nikichukua mkopo nitaweza kupata marejesho ya miezi kadhaa, hadi deni
kuisha,...hata hivyo sikutaka kukukimbilia mikopo mikubwa, na sikutaka
kukimbilia benki, nikaona nimtafute rafiki yangu yoyote mwenye uwezo, nichukue
kutoka kwake.
Nikamkumbuka mmoja wa marafiki zangu, yeye ni
mfanyabiashara na alikuwa yupo kiwango cha juu, nikaona nimjaribu yeye kwanza,
na siku hiyo nikamtembelea kwenye shughuli zake,na nikaongea naye;
‘Rafiki yangu, nimekuja nina wazo ...nina
maombi, naona bishara yangu inasua sua, na wateja kweli wapo, lakini nina
shida, ya mtaji, mtaji wangu ni mdogo sana...’nikasema
‘Kwahiyo unataka kusema nini?’ akaniuliza.
‘Kama unaweza kunikopesha mkopo kidogo, ili niweze kuongeza bidhaa kidogo’nikamwambia.
‘Lakini mimi sio benki, na wala sifanyi kazi ya kukopesha.....'akasema
'Nafahamu hivyo, lakini unaweza ukawa na akiba, au ukajitolea ili kunisaidia mimi rafiki yako..'nikasema.
'Ni kweli, wewe ni rafiki yangu na napenda sana kukusaidia, lakini maswala ya mikopo yana mitihani
yake, mikopo imevunja udugu, na urafiki, ninaweza kukukopesha,ikaja kuwa mtihani kwangu, hasa kwenye marejesho, je ulishaongea hilo swala kwa mume wako? 'akaniuliza.
‘Mume wangu hana matatizo, yeye ana shughuli
zake, na shughuli ya duka ndio tegemezi letu, hata nikimwambia hataweza
kulipinga....’nikasema.
‘Ili nikukopeshe ni vyema umwambie kwanza mume
wako akikubali sawa...mimi nitakukopesha kiai nitakachoweza..., sio kwamba sikuamini, lakini maswala
ya mikopo yana mitihani yake kuna leo na kesho...’akasema
NB, je mume atakubali, na akikataa itakuwaje,
...
WAZO LA LEO: Maendeleo hayaji kirahisi, wakati mwingine, kuna vikwazo
vikubwa ambavyo vinaweza kukufanya ukafikiria mambo mengine mabaya. Tujue kuwa
matatizo ni sehemu ya maisha, na huenda kwenye matatizo hayo ndio unaweza
ukajenga usugu,ujasiri na uzoefu, wa mafanikio . Badala ya kukata tamaa, tuyatumie matatizo na shida zetu, kama njia ya kutufunua akili, kwa mafanikio,...Tujaribu, tusiogope kwa nia njema,
tutafanikiwa.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment