Docta alipotoka, akatuambia mdada, anatakiwa
kupumzika, dawa alizopewa ni za usingizi, kwahiyo atalala sana, lakini
inahitajika akiamuka kuwe na mtu anayemfahamu;
‘Cha muhimu akiamuka kuwe na mtu wa karibu
anayefahamu matatizo yake, na akwepe sana kumuuliza mambo ambayo yatarejesha
kumbukumbu zake nyuma...’akaema docta, na nikamwangalia bosi, nikijiuliza je
yeye ndiye atakaa na mdada, au kuna ndugu zake wengine.
‘Mhh, kiujumla ndugu za mdada wapo mbali, na
mimi ndiye mtu wao wa karibu kwa sasa,...sijui nitafanyaje, lakini anyway, nitaangalia
nitakavyoweza...’akasema bosi.
‘Kila siku ninapokuja hapa nasahau kuuliza,
maana wakati mwingine unaweza kuuliza swali ukajuta kwanini uliuliza,
inategemea na mtu,...lakini sasa naona niwaulize, hivi huyu binti anaishi na
nani hapa?’ akauliza akimwangalia bosi, na kuniangalia mimi, halafu akageuka
kumwangalia bosi.
‘Mwanzoni alikuwa akiishi na ndugu yake, na
ndugu yake, aliondoka kwenda kusoma, kwahiyo akabakia mwenyewe, na mfanyakazi
wake wa ndani, ....mfanyakazi wake, kwasasa yupo likizo hajarudi..na huenda
asirudi tena....’akasema bosi.
‘Kwanini asirudi tena, kafukuzwa?’ akauliza
docta
‘Hapana hajafukuzwa, aliondoka akiwa kaomba
kwenda likizo, na akiwa huko ikaja taarifa kuwa kapata mchumba, kwahiyo
anatarajia kuolewa,na akiolewa ina maana ndio basi tena ...’akasema bosi na
docta akawa anaiangalia ile nyumba na kusema;
‘Maana naona hii nyumba ni kubwa sana,ni nyumba
ya kifamilia,..na hali yake ilivyo ni vyema akawa na mtu, vinginevyo....labda
akalazwe, na akilazwa kwa matatizo kama hayo, itabidi apelekwe chumba cha
wagonjwa wenye matatizo ya akili...na sizani kama atakubali...’akasema docta.
‘Kwani unahisi tatizo hilo ni kubwa sana kiasi
hicho, cha kulazwa, nakumbuka mwanzoni ulisema hilo tatizo ni la muda tu
litakwisha....?’ akauliza bosi.
‘Mhh, kutokana na hali hiyo,...siwezi kusema
kuwa hali ni mbaya,kama angelikuwa anafuata masharti, huenda hilo tatizo huenda
lingelikuwa limekwisha...’akatulia kidogo, na baadaye akasema;
‘Kwa jinsi inavyojionyesha, tatizo kujirudia
tena na tena, ingelifaa, na ni muhimu, akakaa hospitalini ambapo atapata
usimamizi wa kutosha, tatizo ni kuwa kwa hivi sasa kila anayekuja au hata akiwa
na maongezi na wenzake, kuna ile hali ya kuuliza, maisha yaliyopita, ilikuwaje,
kwanini...na hujui nani atamuuliza nini, bila kujali kuwa hilo analomuuliza
litamkwaza au vipi...’akasema docta.
‘Wewe ndiye dakitari wake, na mtaalamu wa mambo
hayo, na wewe ndiye unayeweza kumshauri hivyo, ...sizani kama ukimwambia akalazwe
kwa ajili ya uchunguzi zaidi anaweza kukataa,....’akasema bosi,
‘Nimeshamwambia hivyo, akakataa kata kata, na
kudai kuwa yeye sio mgonjwa, na hayo yanayotokea sio kusudio lake,...lakini
anahisi, kama anavyodai, kuna dawa ambayo akiipata atapona kabisa....’akasema
docta.
‘Dawa gani tena ambayo anaijua yeye, mimi
nijuavyo wewe ndiye unayestahili kumpatia hiyo dawa...?’ akauliza bosi.
‘Hayo matatizo yake ni ya kiakili zaidi, na
wakati mwingine, anavyoona yeye anaweza kukipata kitu,kikawa ni dawa, na kweli
akikipata kinaweza kumsaidia,...kwa maono yake, kutokana na hisia hizo za
kichwani, maana pale alipo anaweza kuona vitu ambavyo sisi hatuvioni,
vinajengwa kwenye ubongo wake,..kutokana na msongo,wa mambo yanayokutana kwa
kasi, na kushindwa kuhimili.....’akatulia kidogo akiangalia saa.
‘Lakini docta, wengine wanasema huenda ana
mashetani, sijui hilo unatuambieje?’ akaulizwa.
‘Kuna maswala ya imani za watu, hayo kila mtu
ana yake, lakini kuna maswala ya ugonjwa na unajulikana kisayansi...hilo alilo
nalo, sio swala la mashetani...’akasema
‘Kwa, jinsi mwili ulivyo, na kila sehemu ya
mwili ina kazi zake....ubongo ni sehemu muhimu ya mwanadamu ambayo ndio
kiongozi wa kila kitu kwenye mwili wa mwanamu, kila jambo ili lifanyike ni
lazima taarifa zifike kwenye ubongo...kwahiyo sehemu hiyo ni muhimu sana kwa
mwanadamu na hauhitajiki kubughudhiwa...sasa kuna matukio yanaweza kuathiri
sehemu hiyo nyeti,na kumfanya binadamu abadilike kabisa, afikie hatua kuwa kama
mnyama...’akasema.
‘Siwezi kukataa kuwa kuna mambo hayo ya
mashetani, lakini sio wakato wote hali kama hiyo ikawa ni hayo mashetani, ni
muhimu sana ukaangalia upande wa vipimo vya kitaalamu, kwani huenda ni tatizo
linalotibika kwa dawa za kawaida, ukilichelewesha linaweza lisitibike tena,
...mwisho wa siku utahangaika na hao waganga, na usipone kabisa...’akasema.
‘Kwahiyo ulivyomuona wewe ni tatizo la kawaida
linalotibika, au kunatakiwa njia nyingine?’ akaulizwa.
‘Linatibika...cha muhimu pamoja na madawa,
lakini masharti yake ni muhimu, tunaweza tukatumia dawa nyingi , lakini kama
hatukufuata masharti, ikawa ni kazi bure....huyo kwa sasa anahitajia utulivu wa
akili, na nashauri, kama angelipata mume muelewa, ingelikuwa ni bora
zaidi...lakini awe muelewa, awe ni mtu anayemfahamu, awe mtu mvumilivu, mwenye
hekima...’akamwangalia bosi, na baadaye akaniangalia mimi, mimi nilikuwa kimiya
tu
‘Tumekuelewa docta, hayo ni maswala ya ushauri,
maana hatujui yeye ana mipangilio gani kichwani mwake, lakini pamoja na hayo,
wewe kama dakitari wake, ungekuwa mshauri mnzuri kwake, ukamshauri hilo na
mengine, akisikia kutoka kwako, inakuwa na nguvu zaidi...’akasema bosi.
‘Yote hayo nimeshamwambia mapema kabisa,lakini
kutoka na hayo yaliyomkuta huko nyuma ambayo ndio chanzo cha haya yote, bado
nafsi yake haiamini kuwa mume ni mtu muhimu kwake...bado kajenga hisia kuwa
mume ni mtu mbaya kwake, na kwake mume ni adui...sasa anahitajika mtu kuivunja
hiyo hali....sijui...kuna mtu anamtaja taja sana, mhasibu, ni nani huyo?’
akauliza docta, na bosi akaniangalia na kutabasamu.
‘Anamtaja kwa mabaya, au kwa ....?’ akauliza
bosi
‘Kwa mazuri, inaonekana anampenda sana huyo
mtu, sijui yupoje, lakini hata kama anampenda, huyo mtu kabla ya kukubaliana na
mdada, ni vyema akamfahamu, na kufahamu matatizo aliyo nayo na cha muhimu akiwa
naye asije akajaribu kumghadhibisha, akamrejeshea machungu ya nyuma..huyo binti
anahitajia kupetiwa na kuengeuliwa kama mwali mbichi...’akasema docta na
kutasamu...
‘Tumekuelewa docta, tutajitahidi kumshauri, na
huenda akampata mtu kama huyo, japokuwa wanaume wa namna hiyo ni nadra
kuwapata, wengi, wanapooa, wanajua kuwa huyo mke kakamilika, anaweza kila
kitu...hawaangalii madhaifu ya kibinadamu kuwa huyo naye alilelewa, na katika
malezi kuna kutofautiana..’akasea bosi
‘Ni kweli...umesema kweli, natumai ukikaa nao,
yeye mgonjwa na huyo atakayebahatika kumuoa ukawafunda, wanaweza wakasaidiana
na taizo hilo likaisha kabisa...kama kuna janga lilitokea huko nyuma, ni bora
lisitajwe..kabisa, mkitaka huyo mtu asipone, na ageuka kuwa mnyama mnyama,...mjaribu
kuchimba alichowahi kufanya...’akasema docta.
‘Kwanini unasema hivyo docta?’ akauliza bosi
‘Kuna hawa watu wa usalama, mara kwa mara
wananijia niwaelezee kuhusu aliyowahi kufanya huyo mgonjwa, nahisi wanahisi
kuna jambo baya aliwahi kufanya...’akasema
‘Je ni kweli lifanya?’ akauliza bosi
‘Siwezi kusema kwa uhakika,....sio kazi yangu
na hizo ni siri za mgonjwa, ...kama yapo, msije mgamgusia, au kumuulizia, hilo
ni jambo muhimu, lakini pia, asijihusishe na madawa ya kulevya, pombe
....nilishamkanaya sana hilo...na zaidi, asije akajiingiza kwenye mambo ya
kuhatarisha maisha yake nay a watu wengine....damu kwake, ni moja ya viashiria
vya kumkubusha majanga yaliyowahi kumtokea..’akasema docta
‘Damu, ina nini damu....?’ akauliza bosi
‘Cha muhimu, ni kuwa asije akaingia kwenye
mapigano, akamtoa mtu damu, au yeye kutolewa damu, ...ni vitu ambavyo akiviona
anakumbuka jambo....sasa ni vyema, asijiingize kwenye makundi mabaya, yatakayoleta
umwagaji damu...ni hayo kwa leo, nyie mumeshamuelewa natumai mtakuwa na moyo wa
kumsaidia, kwani wewe umeshaoa...?’akaniluza docta swali la kunishitukizia na
kunifanya moyo wangu uende mbio, niliogopa hata kumjibu, nikasema;
‘Nipo mbioni....’nikasema.
‘Nikuanavyo wewe ungemfaa huyo dada,...’akasema
na mimi nikajitahdi kutabsamu na bosi akawa ananiangalia kwa jicho la kujiiba
kuona kama nitasema kitu, na docta akageuka kuondoka.
Dakitari
alipoondoka tukabakia mimi na bosi, wakati huo tulishaingia ndani nyumbani kwa
mdada, na mdada alikuwa kalala kwenye sofa, naona docta alipendekeza alale hapo
kuliko kulala chumbani kwake na kwa vile hatukutakiwa kumsumbua, tukaingia
chumba cha maongezi, na bosi akasema;
‘Inabidi hapa tupange zamu,...kwanza naanza
mimi, maana baadaye natakiwa kufika kuiangalia familia yangu, ..baadaye
utashika hiyo zamu, ..kama itakuwa bado, tutaangalia hiyo kesho ni nani anaweza
kukaa na yeye...’akasema bosi
‘Lakini mimi ni mwanaume, na kama ujuavyo
kwasasa hataki wanaume, karibu yake,..huoni nikiwa naye peke yangu muda huo, akizindukana
kunaweza kutokea tatizo..’nikaanza kujitetea
‘Umeshafika hapa mara mbili kuonana na yeye kwa
namna hiyo ni kuwa umeshajenga akili ya kutambua ufanye nini kwa mtu kama
huyu...usikwepe majukumu. Kukwepa majukumu ni uzembe,..na uzembe wa namna hiyo
hauna tija. Katika maisha yako ukiwa mtegeaji, kuwa mwenzangu atafanya, au
nitafanya kesho, au kutafuta viingizio, hutafanikiwa kabisa katika maisha, yako
na ukifanikiwa hutajiamini, hutakuwa na amani moyoni....’akasema bosi
‘Jitume kila inavyowezekana, kila jambo la
kufanya jione wewe unastahili kulifanya, kuliko mwenzako, na kama ni la
kitaalamu basi mtafute muhusika, ..ile kuhangaika kumtafuta huyo mtaalamu, hapo
umejituma, na umetimiza wajibu wako, ..lakini kujifanya huhusiki na
usihangaike, hata kumtafuta mtaalamu, ujue wewe una kasoro, na huo ni uzembe,
na uzembe ni zambi...’akasema bosi
‘Kwahiyo
bosi, ...sasa ni saa...’nikaangalia saa
‘Kama huna haraka sana, nikusimulie sehemu
muhimu kwenye sehemu hii ya kwanza katika mfulululizo wa visa katika maisha
yangu....’akasema bosi
‘Nitafurahi sana,....’nikasema.
*******
‘Katika simulizi la maisha yangu, kuna sehemu
hii ya kwanza ambayo tunaenda nayo, ikielezea machungu niliyoyapata toka
utotoni hadi kuolewa,....na sasa tupo kwenye sehemu ya mwisho ya sehemu hii ya
kwanza, ambapo nimeshaanza maisha ya kujitegemea, nimeshaamua kujitosa kwenye
ulingo wa kuwa muwekezaji..’akaanza kunisimulia
‘Ni
hatua ya namna yake, kuamua kuwa sasa najiwekeza, naanzisha biashara yangu, na ukumbuke
ni mama mwenye familia, na majukumu hayo bado ni yangu. Inahitajia ujasiri
fulani, wa kujituma na mimi najituma, sikulala, nikawa nahangaika, najibidisha
kwenye shughuli zangu,..
Hata hivyo pamoja na hayo, ile kasumba ya
kuajiriwa, kupata kazi, bado nilikuwa nayo, nilikuwa mara kwa mara nikitamani
nipate kazi ya kuajiriwa japokuwa nilikuwa an hizo biashara zangu..na hii ni
hulka ya wengi..hasa unapokuwa umesoma.
Japokuwa mimi kwa bahati mbaya, nilisoma kwa
vipande vipande kutokana na yaliyonikuta huko nyuma kwa wazazi wangu, hata
hivyo, nilikuja baadaye kusoma hadi chuo, kwahiyo nilikuwa na vyeti
vinavyoniwezesha kuajiriwa,..
Pamoja na akili ya darasani, lakini pia akili
ya uzoefu, akili ya majanga, akili ya matatizo, ikawa ni mwalimu wangu mkubwa, nikajifunza
kuwa matatizo, yanaweza kutumika, kuwa sehemu ya zana za kufanyia kazi,
..huwezi amini hilo, kwani nahisi kama isingeliwa hayo matatizo huenda
nisingelifanya hayo niyoyafanya..
Basi
nilipomuendea yule rafiki yangu na kumuomba mkopo, na yeye akawa tayari
kunikopesha, ila kwa sharti moja kuwa ni lazima nimuhusishe mume wangu, nikafanya
hivyo.
Nilifahamu ni kwanini, alihitajia mpaka
nimuhusishe mume wangu, maana mkopo, una masharti yake, na mojawpo ni ushahidi,
unaweza ukawepo ushahidi wa maandishi, lakini ni muhimu kukawepo watu wa
kudhamini ....ikizingatia kuwa mimi ni mke wa mtu basi mume wangu anawajibika
kufahamu hilo, nikamuelewa na mimi nikaenda kuongea na mume wangu.
‘Mume wangu kama unavyoona, duka sasa
linachanganya, lakini mtaji wetu ni mdogo sana, tunahitajika kuongeza bidhaa, lakini
hatuna pesa..’nikasema.
‘Sasa tufanyeje, kama hakuna pesa, basi
tuendelee hivyo hivyo, hadi hapo tutakapoweza kupata pesa nyingi, au wewe
ulikuwa na wazo gani?’ akaniuliza.
‘Tukope pesa....’nikasema.
‘Unasema tukakope..., hapana, mimi naogopa sana
madeni,..nilishawahi kukukopa, na kushindwa kulipa, matokea yake nilinyang’anywa
kila kitu ndio maana ulinikuta sina kitu, .....’akasema.
‘Ulikopa bila malengo, usikope,....ukiwa
hujajipanga, kwanza kabla ya kukopa, panga ni kitu gani cha kufanya, je
kinalipa, ili uweze kupata hayo marejesho...usikope kwanza ndio upange, panga
kwanza kabla ya kupata huo mkopo. ....’nikamwambia mume wangu.
‘Sawa haya niambie, utakopa wapi, ujue sisi
hatuna dhamana, na ndugu zngu hawawezi kukubali nyumba yetu ichukuliwe kama
dhamana,na nafahamu kabisa ukienda benki watahitaji dhamana...?’ akaniuliza.
‘Dhamani ni mimi na wewe...’nikamwambia.
‘Ni yale yale...mimi nina nini hapa....usinipe shinikizo
la damu, na vidonda vya tumbo, ...’akasema
‘Ni hivi, nimeshaongea na rafiki yangu mmoja,
yeye kidogo kajiweka vyema, na yupo tayari kutukopesha, anachohitajia ni wewe
kukubaliana na mimi, na ukawa shahidi, basi mambo mengine, niachie
mwenyewe,...usiwe na wasiwasi..’nikamwambia.
‘Unataka mimi nikawe shahidi, wakati sina mbele
wala nyuma...hapana,kama unakopa kopa kwa malengo yako, usiniweke rehani..’akasema
‘Sikiliza mume wangu, duka umeliona lilivyo, je
wateja wapo hawapo?’ nikamuuliza
‘Nimeona wapo,....lakini nijuavyo ukikopa tu,
mambo yanaanza kubadilika...’akasema
‘Hizo ni imani za kukata tamaa,...cha muhimu ni
kuwa tuna sehemu ya biashara tayari, na sehemu hiyo ina wateja, ina maana, tuna
soko tayari..., na tayari tuna nini cha kufanya, ikiwa na maana kuwa tuna bidhaa,
kinachohitajika ni kuongeza juhudi, ..huo mtaji utatusaidia sana, wewe mwenyewe
utaona...’nikamwambia .
‘Sawa nimekubali, unataka nifanye nini,
tuongezane kwa huyo rafiki yako?’ akaniuliza
‘Ndio maana yake...’nikamwambia,
Kesho
yake tukaenda kwa huyo rafiki yangu, na taratibu zote zikakamilika nikapata huo
mkopo na kuongeza bidhaa na kazi ikapamba moto. Hali ikaanza kuwa nzuri, na
kila siku tukaweza kununua kifaa hiki au kile kwa ajili ya nyumbani, na nyumba
ikakamilika kila kitu muhimu kikawepo.
Akilini
mwangu bado nilikuwa na wazo la kuajiriwa, maana nilisoma, sasa elimu yangu
itakuwa ni hivyo hivyo tu, hapana nikajiwa na wazo la kutafuta kazi ya
kuajiriwa. Nikawa hivyo, na bila kupoteza muda, nikaanza kutuma maombi sehemu
ninazozitaka.
Wakati nasubiria hayo maombi ya kazi, bado
nilikuwa najituma kwenye biashara zangu Hata hivyo nikaona sijakamilika ili
niweze kufuatilia biashara zangu na kufuatilia baadhi ya mizigo nahitajia kuwa
na usafiri wangu. Nikiona wenzangu wana magari yao, hawahangaiki sana, na mimi
nikasema ni lazima na mimi niupate huo usafiri, nikaweka malengo na juhudi.
Wazo hili la kuwa na gari lilikuja kama amasa
fulani, na kwa vile muda huo nilishalipa deni, na hatua tuliyofikia ilikuwa io
haba,nikapiga mahesabu yangu nikaona tunaweza kununua gari, na tukiwa na gari
tutakuwa tumepunguza gharama nyingi za kukodi gari wakati wa kuagiza bidhaa, ni
kweli nikatafuta gari, na haikupita muda, tukalipata...tukawa na gari.
‘Huwezi amini, ...kila siku ikawa ni neema,
kila hatua na malengo yake,
...nilipopata gari watu hawakuamini, wale mawifi, na ndugu za mume wangu bado
wakawa na imani ile ile kuwa huenda huyu mtu sasa anatumia uchawi ,.....mpaka
katajirika, je inawezakana kweli uchawi ukamtajirisha mtu,...kama ingelikuwa
hivyo, basi wengi wanye tabia hiyo wangelikuwa na maendeleo makubwa. Tembelea
sehemu zenye imani hizo, uone kama wana maendeleo, hakuna kitu.
Nikiwa na gari, nikaweza kufanya mengi, hata
hivyo akilini mwangu bado nilikuwa na ile ndoto ya kuajiriwa kwenye kampuni
kubwa kubwa,...nikaendelea kutuma maombi ya kazi, huku biashara zangu
zikiendelea, nina watu nimewaajiri sasa, wanaonisaidia kuuza duka, na sio duka,
nilishaanzisha jingine, nikawa na maduka mawili...dhiki ikaanza kupotea, kidogo
kidogo....
NB: Je baada ya dhiki huja nini...mambo bado
hapo, tutamalizia sehemu hii baadaye, tukiubiria sehemu ya pili kwenye
simulizi, sehemu itakayoonyesha changamoto, na mitihani ya kuwa
nacho....unacho, na unajiona wewe ni zaidi ya mume wako..
WAZO LA LEO: Maendeleo huja kwa maarifa, kujituma, na kuwa na malengo ya
kusonga mbele, usirizike na hapo ulipo, jitahidi kuongeza kipato kwa kubuni
njia mbadala, na mikopo ni njia mojawapo ya kuwekeza zaidi. Lakini tuchukue
mikopo tukiwa na malengo tayari.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment