Ilikuwa kipindi bosi ameshaondoka, nikabakia mimi
na mgonjwa, mgonjwa tulikuwa tumemuingiza chumbani kwake akiwa bado usingizini,
inaonekana hizo dawa zina nguvu sana, kwani tulimuinua bila ya yeye kuamuka na
kmweka kitandani kwake;
‘Sasa mimi naondoka, nikaangalie familia yangu,
wewe utabakia na huyu mtu, unaweza kukaa chumba cha maongzi huku ukimikilizia,
kama kuna lolote litatokea usisite kunipigia simu au kumpigia docta ..namba
yake hii hapa....’akanipa namba yake, halafu yeye akajiandaa kuondoka.
Mimi niliodoka na kwenda chumba cha maongezi,
nikawa najaribu kuona kama nitapata kausingizi, lakini niliogopa kulala huenda
nikapitiwa na usingizi, na huyo mgonjwa akaamuka na kufanya lolote,..japokuwa
dakitari amesema akiamuka hataweza kulete madhara, tatizo lile halitokei wakati wote.
Nilikuwa chumba cha maongezi, nikisubiria nikajiegemeza
kwenye sofa kwenye chumba cha maongezi, mara simu yangu ikaita, nilikuwa
nimeiweka mlio wa kunguruma tu, ili nisije kumsumbua mgonjwa, nikaangalia ni
nani kanipigia,..ilikuwa simu kutoka kwa mchumba wangu, na sikutaka kabisa
kuongea naye hapo, lakini kwa vile nipo chumba kingine na mgonjwa bado kalala,
nikaona niipkei tu nikwa naongea naye kwa sauti ya chini chini:
‘Hali yako mchumba wangu...’nikasema kwa sauti hiyo
ndogo
‘Sijambo sijui huko ....’nikasema
‘Mbona unaongea hivyo kwa sauti kama sio
yako...’akasema huyo mchumba wangu
‘Nilikuwa nimepitiwa na usingizi, na...ohoo, ina
maana wewe hujalala...?’ nikauliza
‘Nilale saa hizi mbona bado mapema sana...’akasema.
‘Kweli bado mapema, lakini wewe unatakiwa
upumzike, usijichoshe sana, ujue una lea...vipi hali yako, na mtoto na familia
yako?’ nikamuuliza na akawa hakunijubu swali la salamu yangu akasema;
‘Mbona kimiya, iku hizi hupigi simu kama
zamani, ...huku nyumbani kwenu sioni maandalizi yoyote ya kuonyesha kuna harusi
inatarajiwa, au kutakuwa tutaoana kimiya kimiya..au kuna nini kinaendelea huko ulipo?’
akaniuliza na mimi nilikuwa nimeshajiandaa kwa swali kama hilo niamjibu
‘‘Kuna mambo nayamalizia, umeona mwenyewe ule
ujenzi, nataka tukioana, uingie kwako, kwenye nyumba yako...au unasemaje....’nikasema
kama namuuliza
‘Kwani ukinioa huwezi kujenga, na ni vyema vitu
vya maendeleo kama hivyo vifanyike na mimi nikiwemo, huwezi jua, mimi naweza
kutoa msaada, ushauri, na mambo mengina yakafanikiwa zaidi ya unavyofikiria....’akasema.
‘Ni kweli, ..usijali, ngoja niweke mambo
mengine sawa, hata hivyo, siwezi kuja huko mpaka nipate likizo,..na pia
niliongea na baba yako, nikamwambia kuwa hiyo nyumba itaisha kabla ya likizo,
na mahari na kila kitu kitafika kabla ya likizo yangu...ila faini, mmmh, ....’nikasita
kidogo, na yeye akasema;
‘Siku hizi nimekuwa nikiota ndoto mbaya sana,
kuwa unanisaliti, kuwa nimekufumania, mara umemtuma mtu kuniua...sijui kwanini,
nahisi kuna jambo linaendelea huko...’akasema bila kujali maelezo yangu ya
awali.
‘Hizo ni ndoto tu, usipende kuamini ndoto,
utajenga tabia ya kishirikina,...nikiulize, kwani kila unachoota kinatokea
kiukweli, hakuna kitu kama hicho...’nikajitetea.
‘Nikukumbushe tu, kuwa wewe ulinikatisha masomo
yangu, kwa kunilazimisha kufanya kitendo ambacho kiliniharibia maisha na ndoto
yangu, sikupenda kukifanya, ulinishika kwa nguvu,....sasa hivi nikiwaona
wenzangu wapo sekondari na nilitakwia niwe nao naumia sana....’akasema.
‘Hayo tulishaongea na tukayamaliza kwanini
unapenda kuyarudia tena, ...hata mimi naumia sana, sikutegemea kuwa itakuwa
hivyo, nilizidiwa nikajikuta nimefanya hivyo, na ndio maana najitahidi ili tuje
tuishi pamoja..’nikamwambia.
‘Nakukumbusha tu, kuwa kama utanisaliti, ujue
na mimi sitakubali...nimeshamwambia baba kuwa akisikia lolote huko, achukue
hatua ambayo hutaweza kuisahau, na kweli baba bado hakuamini, kuwa upo kweli na
azima ya kufanya hayo unayomwambia, japokuwa umeanza kujenga, ila anajiuliza
umepata wapi pesa nyingi kiasi hicho cha kujenga nyumba kubwa vile....anahisi
kuwa huenda kuna jambo lisilo la kawaida unalifanya, niambie ukweli hizo pesa
ulizipata pata vipi, ....?’akaniuliza
‘Kwanini unasema hivyo, ina maana huniamini, na
kwanini baba yako aseme hivyo, hajui ninavyohangaika kwa ajili yako,...cha
muhimu ni wewe uje uishi kwenye nyumba nzuri, hilo nalo ni baya...?’
nikamuuliza.
‘Sio baya kama unayoyafanya ni ya halali,
wasiwasi wangu isije ikawa ni geresha au umejiunga na makundi mabaya,...sitaki
mtoto wangu asikie kuwa baba yake ni jambazi au anauza madawa...’akasema.
‘Wewe niamini, ....mimi ni yule yule
sijabadilika, nitahakikisha mtoto wetu hasikii vitu kama hivyo, ..niamini
mchumba wangu...’nikasema.
‘Baba hakuamini kabisa, anasema anakufahamu
wewe kuwa sio mtu wa msimamo, ni rahisi sana kurubuniwa na kufanya lolote baya,
nakuonya tena, ukumbuke una mtoto na mimi ...usija ukaleta sifa ambayo siitaki
kuisikia,...’akasema.
‘Ataniamini, ngoja hiyo nyumba imalizike, na
hatua nyingine ni kupata gari, nataka familia yangu ijisifie kuwa baba anajua
kutafuta maisha bora, wewe hupendi kutembelea gari lako...la kwenu, la
familia..?’ nikamuuliza.
‘Napenda lakini liwe la pesa za halali, sio kwa
pesa haramu...’akasema
‘Usisikilize ya kuambiwa, mimi sio mtu mbaya,
sipendi kabisa pesa haramu,...’nikasema mara nikasikia sauti, ...ilikuwa sauti
kama ya mtu analalamika, na huko kwenye simu, mchumba wangu akawa anaendelea
kuongea mimi nikaikata ile simu,maana nilikuwa siwezi kumsikiliza yeye tena.
Nikatoka
pale nilipokuwa nimekaa na kwenda chumbani kwa mdada, tulishamuhamisha mdada na
bosi, usiku ulipoingia, kabla hajaondoka, na tulitarajia kuwa anaweza
kuzindukana haraka kama dakitari alivyosema lakini haikutokea hivyo, na bosi
akaondoka na kuniacha nikiendelea kuwepo hapo.
Nikatoka pale kwenye chumba cha maongezi na
kuelekea chumba cha mdada , kwanza nikasita kugonga mlango, maana nikigonga
kama bado kalala nitamumbua, nikasikilizia kidogo, nilipoona kimiya nikaufungua
mlango wa chumba, na mdada alikuwa hayupo...
*****
Sikuamini, ina maana mdada alishaamuka, na kama
kaamuka kaenda wapi, nikahisi kuwa huenda kaenda chumba cha haja, nikasubiri,
lakini ikapita kama dakika tano hivi, hakuoenekana, nikaingia hicho chumba nilichohisi
ni cha haja, sikumkuta, nikatoka na kwenda chumba cha maongezi, nilimkuta akiwa
kashikilia laptop yake, akiwa anandika.
‘Umeamuka saa ngapi...?’nikamuuliza.
‘Wakati unaongea na mchumba wako...’akasema na kunifanya
nishituke, kwani sikujua kuwa alikuwa akinisikiliza, au kasikia kwa kiasi gani
hicho nilichokuwa nikiongea.
‘Oh, sikujua kuwa umeshaamuka, sasa oh,,...unaendeleaje?’
nikamuuliza nikiwa na mashaka.
‘Ninaendeleaje...mmmh, sikuelewi, kwani vipi,
?’ akawa kama anafikiri jambo.
‘Wewe unaumwa, au sio, na ulitakiwa upumzike, ..’ nikasema
‘Ni nani kakuambia ninaumwa, hilo lililotokea
ni jambo la kawaida, ni mshituka tu, huo unakuja na kuondoka, ukiondoka huwezi
amini, ninakuwa kama kawaida tu, mimi sijambo na maisha yanaendelea...’akasema
na kushika kichwa akawa kama anajinyosha, na kupumua kidogo, akageuka kwani
kitu alichokuwa kakalia kinazunguka, akaniangalia na kusema;
‘Sasa hivi nilikuwa nawasiliana na huyu muhuni,
nilimwambia alete mzigo wangu naona hajaleta, sasa kesho asubuhi na mapema,
atakuja na wewe unahitajika kuonana na yeye, ...’akasema.
‘ Kuonana na mimi, hapana, kwanza ni nani
huyo?’ nikamuuliza
‘Umeshamshahau eeh,...unapokea pesa zake
uantumia, unajengea na sasa unataka kununua gari...sio mbaya ndio maendeleo
hayo, ni vyema, mwenzangu akawa na kwake, na mimi,..nikawa na
kwangu...inapendeza kabisa,...zote hizo ni juhudi zangu au sio...’akawa kama
ananiuliza
‘Sijakuelewa, mwenzako, kwa vipi?’ nikamuliza
‘Tatizo lako unajifanya huelewi,
unakumbuka,...nitakukumbusha tu, uifikiri ulivyoambiwa ni utani,..hata hivyo, unafikiri
bila hivi tuatishije, nataka nyumba yangu iishe mapema, kama ilivyo nyumba ya
mwenzangu.., siwezi kukaa kwenye nyumba hii ya kupanga...’akasema na mimi
nikawa kimiya nikijiuliza hiyo mwenzangu ina maana gani, na aliponiona
nimeduwaa akasema;
‘Bosi alikuambia nini?’ akaniuliza
‘Mhh, kuniambia kuhusu nini,..ok, alisema
ulipozindukana kidogo ulimwambia nitume ujumbe kwa mtu wako, alete mzigo wako, mimi
sikuelewa nitume ujumbe kwa mtu gani...’nikasema.
‘Ina maana kweli humjui huyo mtu,hahaha wewe
unatumia pesa tu, mipango mingi,nyumba , gari, kutaka kuoa, na ndoa zipo mbili
kumbuke hilo,...’akasema na kabla sijamuuliza ana maana gani akasema;
‘Sikiliza huyu mtu nimeshawasiliana naye, na
anadai akileta hUo mzigo na mimi nimpe picha zote nilizochukua kwake,
...’akatulia kama anawaza jambo.
‘Picha gani na ni mtu gani huyo?’ nikamuuliza
na yeye akageauka na kiti chake akafungua laptop yake na kuangalia kitu, halafu
akageuka tena kuniangalia na kutabasamu kidogo akasema;
‘Unajua nawashangaa watu kama nyie, mnaojifanya
ni wasafi, wakati kula vya haramu hamuogopi, mnajifanya hamjui kuwa ni vya
haramu.. eti vya haramu, wao wanavyowaibia wanancho kodi zao, hatusemi ni
haramu, ...,kutumia sio kubaya au sio, kutumia sio haramu au sio..., ila
kutafuta ndio kubaya, au sio,...?’ akawa kama ananiuliza na alipona nipo kimiya
akasema;
‘Unajua mimi nina kubeba sana wewe, na hutapata
mtu kama mimi katika maisha yako, hebu jiulize hizo pesa nilizokupa uliwahi
kuota kuzipata kabla, na ungezipatapataje, hilo hulifikirii, ukaona umuhimu
wangu kwako, sasa hivi unatamba kuwa unajenga nymba ya bai mbaya, ni kutokana
na nini, ukumbuke hilo katika kichwa chako....’akasimama na kutembea hatua
mbili.
‘Sasa nikuambie kitu,...hili uliweke akilini,
kuwa hakuna kitu cha bure,...licha ya kuwa hawa watu, wanajiita wanaume,...eeh,
wakubwa eeh, waheshimiwa eeh, ...wanakula tu, wanaomba hata rushwa bila aibu,
ndio maana nipoagiza huyu muhuni alete hizo pesa mimi siogopi, najua nachukua
mali ya waliyoichuma kwa dhambi...
‘Sasa na wewe ulijue hilo kuwa hakuna cha bure
hapa,... usione najitolea kwako ukaniona mimi najipendekeza kwako, ...ndio
huenda nimefanya hivyo kwa vile nakupenda, na ....kumbuka,nafanya hivyo kwa
ajili ya kukujali, vinginevyo, ijui kama ungelikuwa hai, nahisi nyota yangu
inakuhitajia wewe...mmmh’akasita kidogo, halafu akasema;
‘Sijui utafanyaje, lakini ndivyo inatakiwa iwe
hivyo, wewe uwe wangu, sasa sijui huyo mchumba wako, itakuwaje, lakini tutaona,
yote ni hatua kwa hatua, kwanza maendeleo, au sio, ...?’akatembea hadi
dirishani akaangalia nje, halafu akaangalia saa yake, halafu akageuka
kuniangalia.
‘Huyu mtu akifika asubuhi, na najua atawahi
mapema,...nahitajia hizo pesa kuna watu wanatakiwa kulipwa pesa
zao,....akichelewa kidogo, natamlipua,...naona hajanielewa, yeye hanijui mimi
eeh, siogopi kitu, siogopi mtu, kwani nina nini cha kuogopa..’akawa anainua
mikono juu kama kukata tamaa.
‘Eti, mhasibu,...mimi nina kitu gani cha
kuogopa, cha kujutia, ...unaona nilivyo, sina mume, sina mtoto,...na sitakuwa
na mtoto...ila mume ni muhimu, hata kama sitapata mtoto...’akasema huku
ananisogelea, sikuelewa kwanini anasema ‘sitapata mtoto, akawa ananisogelea kwa
hatua ndogo ndogo sikutaka kumuuliza swali nisije nikamkumbusha mambo yake.
‘Huyu mtu akija, utakwenda kuongea naye,
utauchukua huo mzigo na kuniletea,sitaki kuonana naye, ninahisi tukionana naye,
lolote linaweza kutokea, hisia zangu ni kali, kwahiyo, kama unanijali, kama upo
hapa kwa ajili yangu, ufanye hivyo, vinginevyo, lolote likitokea, ujue wewe
ndiye utakayebeba dhamana...’akasema na kunifanya nibakie mdomo wazi....baadaye
nikasema;
‘Lakini mdada, tulishakubaliana kuwa huyo mtu asinijue,au
sio ...sasa kwa kufanya hivyo huoni unaniweka kubaya, ....’nikasema
‘Una uhakika kuwa hawajakufahamu, ...hahaha
usiwe mtoto mdogo wewe, wameshakufahamu na kama isingelikuwa mimi kuwatisha,
sasa hivi ungelishakuwa mzoga, walishapanga kukumaliza....kinachotakiwa ni
kuliondoa hilo pikipiki lako hapo nje...’akasema na kutoka nje, sikuelewa ni kwanini
anasema hivyo.
Mimi nilibakia humo ndani nikiwaza hayo
anayotaka mdada niyafanye, nilishaamau kujitoa kabisa na mambo yake, japokuwa
nilikuwa nahitaji pesa, kwa ajili ya kumaliza nyumba, na maandalizi ya harusi,
na hilo kwangu ni muhimu ili wakwe waniamini....
Baadaye
mdada akarudi ndani na kusema;
‘Ikifika asubuhi nataka kila kitu kiwe safi,
nimeshaongea na mlinzi, ...’akasema
‘Kuhusu nini mdada, ukumbuke kuwa unaumwa,
unahitajika kupumzika...’nikamwambia.
‘Pikipiki limeshafichwa, wakija hawatajua kuwa
ni wewe, ni lazima ufiche sura yako kama hutaki wakufahamu kuwa upo na mimi,
ngoja nikifundishe ujaja wa mjini....’akasema huku akienda kwenye kabati,
akatoa kiboksi na kukifungua.
‘Wakati mwingine, tunafanya mambo kwa ajili ya
kufanikisha jambo, sio kwa nia mbaya, bali ni kwa ajili ya kuokoa pesa ya
walalahoi,....’akasema na kutoa kiboksi kwenye kabati, humo ndani, kulikuwa na miwani, nywele, na
vitu vingi vingi, akanisogelea na kutoa kitu kama nywele, akanibandika
kidevuni, ..
‘Unaona, sasa una ndevu, ...na hapa...’akapitisha
kitu sehemu ya pua yangu, akawa ananibadika kitu, na kusema
‘Na hapa pia kunatakiwa kuwe nandevu za puani,
au sio...halafu eeh, machoni utavaa haya mawani, ukijiangalia sasa hivi huwezi
kujitambua kuwa ni wewe..lazima uwe mjanja...’akasema na mimi nikawa nashika
shika zile ndevu alizoniwekea
‘Sasa sikiliza, huyu mtu kaniambia anahitajia picha
zake zote sinema ya tukio lake lote, na mimi hilo tukio lake nimeligawanya sehemu
tano, hivyo akija, utampelekea sehemu ya kwanza tu, na akisema maneno mengo
unaweza kumwambia kuwa akitaka sehemu nyingine, alipe kiasi kama hicho ambacho
nataka aje nacho kesho asubuhi...’akasema akiangalia juu.
‘Kama kweli atafanya hivyo, akanilipa kiasi
hicho mara tano, mimi nitampa kila kitu chake, ila atalipa mara
hizi....’akaonyesha vidole vitano, halafu akasogea kwenye sofa, akachukua mfuko
wa Rambo, na kuniambia, badili hizo nguo, vaa hizi hapa,;
‘Kwanini nifanye hivyo?’ nikamuuliza
‘Tumia akili kidogo, wakati unaingia huenda
kuna watu wake kawaweka hapo nje wakinichunguza na kuchunguza ni nani anaingia
hapa mara kwa mara, nina uhakika huo,...sasa kuficha ficha mambo unatakiwa
kubadilika kila kitu, hata hivyo viatu uvue, utavaa ndala zile pale mlangoni,....usitake
nikufundishe kila kitu...fanya hivyo haraka...’akasema
‘Mhh,mimi siwezi kufanya hivyo hapa...’nikasema
nikiona aibu kubadili nguo hapo mbele yake.
‘Utaweza tu,...unaogopa nisione mwili wako,
kwani itakuwa mara ya kwanza kukuona hahaha, huo mwili wako wote ninao, kila
siku nauangalia, ....hahaha, hebu badili hizo nguo usicheze na muda, hizi kazi
zinakwenda kwa muda...’akasema na mimi nikafanya hivyo.
‘Hata hivyo, hilo la kuonana na huyo mtu, mimi
sikubaliani nalo...siwezi kufanya hivyo, hapana, mdada kwanza unaumwa, sio
vyema kujiingiza kwenye hayo mambo haya wanaweza kutumia nguvu, huoni wewe
unajiweka kwenye wakati mgumu...’nikasema na yeye akaniangalia huku akikunja
uso, kuonyesha kukerwa, na nikaogopa nitamkasirisha na hilo halitakiwi kwake
kabisa.
‘Usitake nikakasirika, sitaki kukasirika, na
sitaki huyo mtu aje tuoanane na mimi ni kweli tukionana anaweza kujifanya
mjanja, sitaki kabisa nionane naye, ....nimehisi hivyo, atanikasirisha, na
hasira zangu zitaishia kwake, sijui nitamfanya nini,....’akasema na akawa kama
anawaza jambo, halafu akakuna kichwa na kusema;
‘Haya mimi naenda ndani kupumzika, kazi
iliyobakia ni ya kwako,upo hapa kwa ajili ya afya yangu, hilo ni mojawapo,
dakitari anataka pesa, walinzi, kuna watu wa hapa na pale, unafikiri nitapata
wapi hizo pesa, ni kutoka kwa hawa hawa mafisadi ...’akasema na kuelekea
chumbani, na kuniacha nikiwa nimesimama, baadaye nikakaa kwenye sofa, na
usingizi ukanipitia.
Niliona sura ya mtu akinijia, sura
isiyoelezeka, akawa anapanua mdomo, na midomo inakuwa mingi, meno yanakuwa
mengi, na alipoanza kuongea sauti yake ikawa kama inapaa, akasema;
‘Unakumbuka nilichowahi kukuambia kabla...’akatoa
sauti ambayo iliniumiza hadi masikio, sikumjibu, akaendelea kusema;
‘Nilishakuambia ukitaa haya yaishe nikupe dawa,
....na dawa ni rahisi kwako, huenda leo ukapata muda wa kulitekeleza hilo,
kabla hujawahiwa,...ukizidi kuchelewa, ujua unalo,...tatizo linazidi kuwa
kubwa, shauri lako, .... hahahahahaaaa’ mara mlango ukagongwa
Nikazindukana kwenye usingizi na kupangusa uso,
nikashituka niliposhika ndevu kidevuni kwangu, nikakumbuka, nikatabasamu
kidogo, na kutamani kuwe na miwani nijiangalia,
‘Nahisi ndio huyo keshafika, mtu wa mdada kazi
imeanza,..’nikasema kimoyo moyo, nikausogelea mlango na kuufungua, na mlinzi
akaniangalia kwa mashaka, halafu akawa anachungulia kwa ndani kupitia sehemu
yamlango iliyopo wazi, na baadaye akauliza;
‘Bosi keshaamuka...i?’ akaniuliza huku
akiniangalia kwa mashaka
‘Bado kalala, unamuhitajia kwa jambo gani...?’
nikamuuliza
‘Kuna mtu anataka kumuona,..halafu wewe umeingia
saa ngapi humu ndani?’ akaniuliza akiniangalia kwa mashaka
‘Kwanini unaniuliza hivyo...’halafu nikakumbuka
zile ndevu, nikajikauha na kusema;
‘Hiyo sio kazi yako, ninakuuliza huyo ni nani anataka
ninii?’ nikamuuliza huku nijaribu kubadili sauti
‘Anataka kumuona bosi, ..unasema hiyo sio kazi
yangu, wakati mimi sikufahamu, sikukuona ukiingia pale mlangoni, uinifundishe
kazi bwana, nakuuliza tena wewe ni nani na uliingije humu ndani... ?’
akaniuliza akiendelea kuniangalia kwa makini.
‘Hivi wewe unataka kazi au ....maana kama mtu
aliingia hapo mlangoni hukumuona, halafu unakuja kumuulizia huku ndani huoni
kuwa kazi imekushinda,..itasaidia nini sasa, kama angelikuwa na nia mbaya,
angelishafanya, usiwe na wasiwasi na mimi...’nikasema.
‘Hujapita pale mlangoni, mimi nina uhakika na
hilo,...hawezi kupita mtu pale mlangoni bila ya mimi kumuona, labda uwe umeruka
ukuta, na ukuta una umeme...umepitia wapi,...’akasema akionyesha kushangaa.
‘Niambie huyo mgeni ni nani..kama una maswali
mengine, nitamuamusha bosi wako umuulize, ukumbuke anaumwa, hatakiwi
kusumbulia, na mimi nipo hapa kufanya kazi zake....’nikasema.
‘Haya bwana,...lakini ni muhimu mimi nifahamu
kazi yangu sijaanza leo, tatizo nyie watu mnazarau sana kazi za wenzenu, mimi
nina uhakika hukupita pale mlangoni hilo nina uhakika, nahisi kuna kitu hapa,
na yule mhasibu yupo wapi,...?’ akauliza akiangaza macho huku na kule kuangalia
ndani kwa kupitia mlangoni, nikasema;
‘Yupo ndani na bosi..’nikasema nikielekeza
kidole huko ndani
‘Ohoo, wanaongea au wanafanya nini?’ akauliza
sasa akirizika kidogo, lakini bado akanitupia jicho na akawa kama anawaza jambo
‘Hayo maswali utamuuliza yeye mwenyewe, nenda
kamuulize huyo mtu kaleta mzigo ?’ nikasema
‘Mzigo..mzigo gani?’ akauliza akionyesha
kushituka.
‘Fanya ninavyokuambia, hivi wewe askari vipi...ina
maana bosi wako akikutuma jambo ndivyo unavyomjibu hivyo, au nimuamushe akutume
yeye mwenyewe...’nikasema kwa ukali, na huyo askari akageuka na kuondoka,
baadaye akarudi, na kusema;
‘Kasema kama walivyokubaliana na bosi, mzigo
anao, lakini na yeye anataka kuonana na bosi, kuna mzigo wake kwake...nipe
nikupe, ndivyo alivyoniambia....’akasema na mimi nikatulia kidogo nikiwaza
nifanye nini sasa, kasha nikaufungua mlango kwa mapana yake, na kutoka nje,
Niliona
gari limesimama na jamaa kasimama pembeni yake, akiwa kashika bahasha, alikuwa
kainama chini, akichezea chezea kitu kwa miguu, na aliposikia sauti ya mtu
anamjia akainua kichwa kuniangalia, aliponiona kwanza alibadili sura ya kawaida
na kuweka sura ya chuki, mimi nikawa nimeshamkaribia nikamasalimia;
‘Habari ndugu, nikusaidie nini ndugu yangu?’
nikamuuliza
‘Nimeshaongea na mlinzi shida yangu, na mimi
sio ndugu yako...’akasema akionyesha kukerwa
‘Sawa yeye ni mlinzi wa getini, na mimi ni
mlinzi wa ndani, mimi ndiye ninayeangalia maswala ya ndani ya mwenye nyumba hii,
kama kuna lolote uniambie, ...’nikasema
‘Mimi nataka kuongea na yeye mwenye nyumba hii,
maswala hayo ni kati yangu mimi na yeye hakuna mtu kati...’akasema
‘Huwezi kuongea na yeye kwasasa,unafahamu kuwa
anaumwa,kama hufahamu ndio hivyo, anaumwa kapumzika, ila kaniachia maagizo ...’nikasema
‘Haumwi bwana, nimewasiliana naye kwa simu, kwa
ujumbe wa simu hajaniambia kuwa anaumwa, hayo unatunga wewe....unasikia mimi
sitaki kupteza muda wangu wa kuongea na huyu na huyu....hivi hamnijui mimi
eeeh,..’akasema kwa ukali.
‘Ukweli ni kuwa anaumwa ndio maana akanituma
mimi, kwa hali yake, hakuna mtu anayeruhusiwa kuongea naye zaidi yangu mimi, na
kila kitu chake anachohitajia kitapitia kwangu, umekuja na mzigo wake?’
nikamuuliza na hapo akawa kama kashituka nilipotaka swala la mzigo.
‘Mzigo gani?’ akaniuliza akiniangalia kwa macho
yaliyojaa hasira na kutahayari akawa kama kama ananikagua
‘Sikiliza ndugu tusipoteze muda, unafahamu ni
mzigo gani, au unataka nimwambie afanye anavyojua yeye,...unafahami ni kitu
gani atakifanya....’nikasema na huyo jamaa akaniangalia kwa makini, akionyesha
wasiwasi, akaniuliza
‘Kwani wewe ni nani, sijawahi kukuona kabla?’
akauliza sasa akiniangalia moja kwa moja usoni
‘Hiyo sio kazi yako, cha muhimu kama umeleta
mzigo, nipe, nikamkabidhi, mengine mtawasiliana naye kwenye simu...’nikasema
‘Siwezi kutoa kitu chochote kwa sasa mpaka
tuingie kwenye makubaliano, nimeshaongea naye kwenye simu tayari sawa lakini
mimi sikufahamu, hatuendi hivyo, hujui ni makubaliano gani yaliyopo kati yangu
mimi na yeye, je ukija kuniruks kuwa sijakukabidhi huo mzigo, ikufahamu,...’akasema
‘Una uhakika na hilo,...?’ nikamuuliza na
nikashika simu na kupiga mlio mmoja kwa mdada, ndivyo alivyoniagiza na
haikupita hata sekunde simu ya huyo jamaa ikalia kuahiria ujumbe umeingia,
akautizama, na nikaona sura yake ikibadilika, akaniangalia na kusema;
‘Hivi wewe unanifahamu mimi?’ akaniuliza
akionyesha hasira, na mimi nikajikakamua na kusema;
‘Nakufahamu sana, zaidi ya unavyojifahamu
mwenyewe, na sizani kama utafurahi kukosana na mke wako,...kazi yako ni muhimu
sana kwako,au sio...’nikasema
‘Eti nini, ...mke wangu achana naye,..ok, ..ok,.’akawa
anauangalia ule ujumbe na sasa alionyesha wasiwasi halafu akabenua mdomo kama
anatabaamu lakini usoni alionyesha chuki,..macho yaliyoashiria kuua, nahisi
akipata mwanya wa kufanya hivyo, hatasita kufanya hivyo, akasema;
‘Ohooo, kumbe mpo wengi, ok, mimi sijaja hapa
kwa shari, ninachotaka ni makubaliano, ninachotaka ni huo mzigo wangu ili
niwape huo mzigo wenu...unao hapa...?’akainua ile bahasha ambayo nahisi ina
pesa ndani yake, mimi nikauangalia na sikuonyesha dalili ya kuufuata,
nikatulia, aliponiona nimetulia akasema;
‘Nyie si mnachotaka ni pesa, pesa sio
tatizo,...ila...ila nawaonya, kama mtanisaliti,....kama huu mzigo haupo wote na
kuna mabaki huko,...sijui...’akasema akiwa kashikilia ile bahasha mkononi,
akiwa kama anaichezea chezea mkononi.
Mimi nikatoa bahasha aliyonipa mdada, nilikuwa
nimeiweka mfukoni wa koti, na kumwambia;
‘Mzigo wako huu hapa, natumai upo sawa kama mlivyoongea
na mdada, kama kuna zaidi mpigie mtaongea naye sio mimi ....’nikatoa mfukoni
bahasha nafikiri ilikuwa na CD’s, nikamuonyesha na kusema;
‘Nipe huo mzigo wake nimpelekee , mimi nina
kazi zangu nyingine sitaki kupoteza muda hapa nje,...nina mambo mengi, siwezi kulalia
jambo moja ambalo unafahamu ni nini cha kufanya...’nikasema na yeye akainua ile
bahasha na kunielekezea, akasema;
‘Sikiliza, kama mnanifanya mimi mjinga,..sawa
hivi sasa mumenipata, lakini mjue halitaihia hapa, na leo nimepanga iwe ni siku
ya mwisho,....kama lengo na nia yenu ni kuniharibia maisha yangu, nawaambia
hivi, kabla sijafikia huko, nitahakikisha kundi lenu lote mnakwenda kusiporejewa,
hilo ninakuhakikishia,...’akasema na mimi nikataka kumjibu, lakini akanikatiza
na kusema;
‘Hayo hayajaanza leo, na hilo sio mara yangu ya
kwanza kukutana nalo,ingawaje kanihika pabaya, lakini, mjiwekwe tayari....’akasema
‘Maneno mengi ya nini, hayo ongea na mwenyewe
sio mimi, mimi sijui...’nikasema.
‘Hujui eeh, waulize waliojaribu kunifanyia
hivyo wapo wapi, wameshasahaulika,sembuse nyie, sasa kama hujui utakuja kujua,...nyie
ni watu wadogo sana...ni kwa vile tu, ...ok, ..mwambie huyo malaya wako, vita
haijaisha ndio imeanza, peleka huo ujumbe kwake, simuogopi ....’akasema na
kunisukumia ule mfuko kifuani,
Moyoni
nilikuwa nafikiri, alikuwa akisema hivyo, aikijua kuwa hakuna uchafu mwingine
aliobakia nao mdada,...alijua keshapewa kila kitu, hata hivyo, kwa jinsi
alivyoonyesha inaonyesha kakwazika kweli, na anaweza kufanya lolote baya.
Hapo
nilipo kijasho chembamba kilikuwa kikinitoka, japokuwa nilikuwa najitahidi
kujiaminisha,kwa kutokuonyesha uwoga,
lakini kiundani nilikuwa na naogopa sana, nikiombea mungu jamaa asije
akachachamaa, taratibu nikaauchukua ule mfuko, na yule jamaa alipohakikisha
nimeushika, akarudisha mkono wake na kugeuka kuelekea kwenye gari lake, nikajua
sasa anaondoka, na mambo yamekwisha, iliyobakia ni yeye na mdada.
Nilimuangalia yule yule jamaa akiondoka kueleka
kwenye kwenye gari, na alipofungua mlango kuingia mimi taratibu nikageuka
kuelekea ndani, huku nikiwa nimeshika ule mfuko, kama mtu aliyeshika kitu cha
hatari,...huyu akili nyingine ikianiambia ‘hizi ni pesa na wewe una fungu lako,
lakini akili nyingine inanionya kuwa hili bomu, likilipuka litanimaliza mimi na
maisha yangu yajayo...
Nikawa nainua mguu, na niliona kama mguu hauna
nguvu, miguu ilikuwa kama inataka kutetemeka, nikajitahidi kiume, na kwa hatua
za kujikwamuakwamua, nikielekea ndani, mara nikahisi kama kuna mtu anakuja
nyuma yangu, nilihisi mwili ukianza kutetemeka, lakini nikakumbuka iri moja ya
ujasiri hata kama huna nguvu, ni kujiamini, kwa haraka nikageuka kupambana kwa
lolote...
Nilipogeuka tu, ...nikakutana na bastola ikinitizama.....
NB: Itakuwaje,? tuweni pamoja kwenye sehemu ijayo, na samahani kidogo, simulizi la mpendwa halikuwepo kwenye sehemu hii tutakutana nalo sehemu inayokuja, akihitimisha sehemu ya kwanza ya simulizi la maisha yake.
WAZO LA LEO: Mali ya dhambi, ukianza kuitumia ni kama muonja asali,
haonji mara moja,anatamani kulamba tena na tena. Tukwepe tamaa za kupata mali
kwa njia isiyo halali, kwani tamaa zake haziishi haraka, ...ukifurahia kupata vitu vya dhuluma ukumbuke kuwa
kuna wanaoumia kwa kukosa kutokana na
dhuluma hiyo.
No comments :
Post a Comment