Kesho yake nikafika
ofisini, huku nikiwa bado nawazia, jinsi mdada alivyoweza kulitoa hilo gari
lake, ...nikakumbuka jinsi ilivyokuwa siku ile, baada ya kufika kwenye hiyo
hoteli, na kuongea na mlinzi, halafu nikapanda kuelekea juu.....
Nilipanda hadi rosheni ya pili, nikaelekea
kwenye chumba alichonielekeza kwenye simu, nikagonga mlango, na haraka mlango ukafunguliwa,
na kukutana uso kwa uso na mdada, akiwa anameremeta, kajipamba, utafikiri sio
yeye, akaniangalia juu chini, na halafu akasema;
‘Upo tayari?’ akaniuliza huku akiendelea
kunikagua
‘Nipo tayari kwa nini?’ nikamuuliza huku
nikiwa nimekunja uso, sikupenda hali niliyoikuta humo , maana kulionekana
kabisa kuna mabaya yanayoendelea humo, na kama ingeliwezekana, ningeondoka
haraka, lakini mdada alishanitega, ....
‘Kushika milioni tano, hivi...kwa siku moja
tu, kwa kazi ndogo tu, ...kinachotakiwa ni ujasiri na kujiamini,...’akasema
huku akiniangalia moja kwa moja usoni, na sipenzi kumwangalia huyu mwanadada
usoni, maana nikiyaangalia macho yake, mdomo wake...oh, nashindwa hata kuhema.
Hapo nikasema ngoja nijipe ujasiri, maana
sijui huyu mwanamke anataka nifanye nini, anaweza kunitumbukiza kwenye biashara
haramu,...nikimuangalai hizo nguo alizovaa na mshahara wake haviendani kabisa,
na sasa anasema ana gari, pesa anazipatia wapi, kama sio biashara haramu..ni
lazima niwe mwangalifu...nikawa nawaza hivyo, na kumwambia;
‘Kwanini unichague mimi, na unafahamu kuwa
mimi sipendelei mambo yako, kwanini hukuwaita jamaa zako wengine?’ nikamuuliza
‘Maswali ya polisi siyataki, nimekuitia hapa
kwa kazi, moja, ...hii ni kwa kukusaidia tu,...nisingelikuwa na haja na mtu
kama wewe....’akasema na kunishika mkono akanivutia ndani.
Mikono yake ilipogusa mwili wangu, ilikuwa
kama kitu cha ajabu kimeingia mwili wangu, kwanza nilihisi nimeshikwa na mkono
wa mtoto mchanga, mikono yake ilikuwa laini sana, na nilihisi kama ina kitu cha
ziada cha kunifanya mwili wangu uwe hauna mawasiliani na akili yangu
tena...sikuweza kupinga, nilijikuta
nikimfuata nyuma kama mbwa anavyomfuata chatu.
Tulifika karibu na kitanda, na hadi tunafika
hapo, nilikuwa kama mtu aliyezibwa akili, hadi aliposema;
‘Sasa sikiliza, unamuona huyu mshamba
aliyelala hapo kitandani, keshazidiwa hana ujanja, nimeshamchukua picha za
awali, bila kujua,....sasa hatua iliyobaki, ni kumbeba na kumtoa humu ndani,
tunakwenda kumlaza nje...sehemu ile ya mapumziko,sitaki azindukane, akiwa
humu,..’akasema.
‘Mimi ..mimi..mambo yako sitaki
kabisa...’nikasema kwa kigugumizi.
‘Pili, kwenye nguo zake, kuna milioni kumi, alilipwa
na jamaa mmoja tukiwa huko chini, hizo nitazichukua kufidia pesa zangu,
alizozichukua,....lakini cha muhimu kwanza tumtoe humu ndani........’akasema.
‘Hapana mimi siwezi kufanya hayo, kwanza huo
ni wizi, na...hapana....tabia ya wizi,mimi siijui...kama ndicho ulichoniitia
hapa, mimi naondoa...’nikasema na kugeuka kutaka kuondoka, na mara nikasikia
ujumbe ukiingia kwenye simu yangu, nikaitoa imu yangu na kuangalia ni nani
kanitumia ujumbe muda kama huo, nikaangalia ni nani mtumaji, kulikuwa hakuna
namba;
Nikaanza kuusoma huo ujumbe, ulikuwa ukitoka
kwa huyu,.. huyu mdada, sijui aliutuma vipi na wakati huo nipo naye humo ndani,
nikainua kichwa kumwangalia, yeye akatabasamu na kusema;
‘Mambo ya digitali hayo, kila ukipinga jambo
ninalokuambia, mimi natoa ishara, meseji inaingi kwako, na zikizidi meseji
tatu, moja moja ujumbe unakwenda kwa baba mkwe wako, na kwa mchumba wako...’akasema
huku nikiwa naufungua huo ujumbe kwani ulikuwa na picha, ...loooh, ....yale
yale mapicha mabaya.
Nikageuka kwa hasira nikimwangalia mdada, yeye
akawa kanilegezea macho na kutabaamu, huku akisema kwa sauti ya kulegeza;
‘Masikini, mhasibu, ...ukikasirika sura
inatisha,....’akasema, halafu akabadili sura na kuondoa tabasamu, akasema kama
bosi anayeamrisha jambo
‘Upo tayari, tunakwenda kwa muda mpenzi hapa,
... au nitoe ishara nyingine...?’ akaniuliza na mimi nikawa bado namwangalia
kwa hasira, akageuka kunipa mgongo,mara kweli sauti ya kuashiria kuwa kuna ujumbe
umeingia kwenye simu yangu ukasikika, sikuamini kuwa ni yeye aliyetuma huo
ujumbe.
Nikiwa bado namwangalia, nikabonyesha simu
yangu, kufungua ujumbe, nikainama kuusoma, ni kwelu ulikuwa ukitoka kwake, na pembeni
yake kuna sekunde zinajihesabu, na chini yake kuna maandishi mekundu, yakisema kumebakia
ujumbe mmoja, kwenda kwa....nikaona namba ya baba mkwe...
‘Hivi wewe...’nikaanza kusema lakini yeye
akaniwekea kidole chake kwenye mdomo wangu kama kuninyamazisha, na kusema;
‘Anza kazi, sitaki utani,....’akasema huku akimsogelea
huyo jamaa na kuanza kumuinua...nikamwangalia baadaye nikaona haina haja, si
kazi ndogo tu,nikasogea nikamsaidi kumuinua huyu jamaa na kumbeba,nikatoka naye
nje, huku mdada akinifautilia kwa nyuma...
Yeye hakwenda mbali, alisimama pale mlangoni,
akiniangalia, kuniacha niendelee mwenyewe.
Nilimbeba huyo jamaa hadi sehemu iliyopangwa
viti, ni sehemu ya kumpumzika, kuna meza na viti, na pool table, nikambeba huyo jamaa hadi kwenye ile meza na kumlaza
hapo, alikuwa uchi,na taulo ndogo tu, ambayo kwa muda huo ilikuwa begani
kwangu.
Nilipomlaza pale juu ya ile meza ya kuchezea
pool, nikachukua hiyo taulo na kumfunika sehemu zake za siri, na wakati nataka
kuondoka mara mkono ukanishika kwa nyumba, hali hii ilinishitua,maana kulikuwa
hakuna mtu mwingine, na huyo jamaa alikuwa kapoteza fahamu, hajijui,
nilishituka karibu nidondoke, nikageuka kuangalia ni nani kanishika.
Alikuwa ni huyo huyo jamaa, ....inaonekana,
ana fahamu kidogo, na aliweza kuinua mkono, na kujaribu kunishika, lakini
tatizo la hayo madawa ukiyanyweshwa, mwili wote unalegea, unashindwa kuwa na
nguvu, unaweza ukawa na fahamu kidogo ya kuona kinachoendelea lakini huwezi
kuinua hata mkono, ...jamaa akasema kama vile mtu anaota usingizini;
‘Nisaidie ...simu yangu..... mpigie
rafiki...’akasema na sauti ikakatika
‘Mpigie rafiki, rafiki yake ni nani, mimi
nitamjuaje huyo rafiki...nikainama kumwangalia na wakati huo, alianza kukoroma
kama vile mtu anakata roho, nikaona sasa haya ni makubwa,huenda jamaa ndio
anakata roho...haya sasa ni mauaji.
Nikasita kuondoka, nikaona, ngoja nihakikishe,
isije kuwa kweli, jamaa amekufa,nikamsogelea, nikainama kumchunguza, alikuwa kimiya na
nilihisi mapigo ya moyo kwa mbali sana, nikawaza sasa nimfanyie nini...
‘Unafanya nini hapo, unapoteza muda, umebakia
muda mchache, nguvu za madawa zitaisha akizindukana hapa, hutamuweza huyu,
jamaa huyo ana nguvu za watu watatu..’ilikuwa sauti ya mdada, kumbe alishafika
na mimi kwa haraka nikageuka, na kumwangalia, kabla sijasema neno akasema;
‘Mwache hapo, ....kuna mambo mengine ndani,
...’akasema kwa sauti ya kutoa amri.
Nikainuka pale nilipokuwa nimemuinamia huyo
jamaa, nikamwangalia mdada kwa hasira, nikatembea hadi pale alipokuwa kasimama,
nikampita na kurudi kwenye kile chumba,
Baadaye akaja, na kunishika shika mgongoni
akasema;
‘Nafikiri hapo ulipo unafikiria mengi, na
huenda umehaniweka kwenye kundi baya, kuwa pengine ....mmmh,, labda mimi ni
muhuni au mimi ni jambazi, lakini nikuambie ukweli, mimi sina tabia hiyo
kabisa...’akaendelea kunishika shika.
‘Nikuambie ukweli, hili ninalofanya ni katika harakati
za kuwakomoa watu kama hao, nina usongo sana na watu wanaoitwa wa-na-u-me, . Nyie watu nyie, ....nina
uongo sana na nyie,...ninawa-mind kichizi,
walichonifanyia wenzako huko nyumba, nimeapa kuwa kila nikipata nafasi kama
hii, nitafanya kila niwezalo, kulipiza kisasi...’akasema na kuniachilia,
akasogea pembeni, huku akiwa kaangalia mlangoni.
‘Unamfahamu huyo jamaa...?’ akaniuliza huku
akiwa kanipa mgongo.
‘Ninamfahamu, nani,...mimi simfahamu...nitawafahamu
wapi wanaume zako...na mambo yako...kama walikufanyia mabaya na hao hao, sio
mimi...?’ nikasema kwa sauti ya kukerwa.
‘Hahaha, sio wewe eeh, ndio maana nimekustahi,ila
kama utashirikiana na mimi la sivyo, ...’akageuka kuniangalia.
‘Halafu,sauti yako hiyo inaonyesha wivu eeh,mmmh,
masikini mhasibu, ananionea wivu, mmmh, ...nikuambie ukweli, huyo jamaa na
wengine, waliowahi kuingia kwenye makucha yangu, hawana lolote kwangu...baada
ya unyama niliofanyia huko nyuma, nilishaapa kuwa sitaki tena mtu anayeitwa
mpenzi,...mwanamume..’akanisogelea na kunitoa na kidole kifuani.
‘Nikuambie wewe mtu, huyu mtu, ni katika wale
watu, nilio-apa kuwa nikipaat mwanya wataipa fresh,na nahisi kwa jinsi ulivyoona, unahisi huyu jamaa kala
ndizi,...kwa taarifa yako tu, hakuwahi hata kuimenya, zaidi ya kuibonyeza
bonyeza akiangalia kama imeiva, na alipoona imeiva, akataka kuila...wewe sio
kwa mdada, sio rahisi hivyo...’akakunja ngumi na akawa kama ananipga piga
kifuani.
‘Huyo jamaa alikuwa na pupa, nikamtuliza,...,
na wakati anataka kuimenya hiyo ndizi, dawa nilizomwekea bila ya yeye kujua, zikaanza
kufanya kazi, na hapo hapo mimi nikaanza kufanya mambo yangu, mjini hapa...’akaongea
bila wasiwasi.
‘Unaongea utafikiri ni jambo nzuri, ungelijua
ninavyojisikia moyoni uingelipoteza muda kunisimulia..’nikasema na yeye bila
kujali maneno yangu hayo akaendelea kunielezea;
‘Alipozidiwa, akawa hana ujanja, nikawa
namfanya ninavyotaka,...ukiwa na akili na ujanja, mijitu kama nyie, naipeleka
ninavyotaka...nyie si mna mikono, mna nguvu, mnaweza kuishika ndizi na kuiminya
na kuimenya, na kuila mtakavyo,...wapii, ni kwa wajinga sio mimi, ...’akageuka
na kunipa mgongo.
‘Lijamaa kikawa linakuja lenyewe, bwata-bwata,
halina nguvu, kabla halijadondoka, nikaomba msaada kwa jamaa walinzi;
‘Jamaa yangu kalewa sana, naomba mnisaidie
tumpeleke kwenye chumba chake...’nikamwambia mmoja wa walinzi anayenifahamu.
‘Umepata mdondo mwingine..wewe dada wewe...’akanitania,
huku akimbeba hadi kwenye hiki chumba.
Nilipofika sikupoteza muda, nikamsalula nguo
zote, huku akiwa na kimuhemuhe,..hizi dawa zilivyo, ni kuwa mwanzoni unaweza
ukawa na hali ya kuweza kufanya jambo, na unaweza kuamrishwa fanya hivi, au
vile na wewe unafanya tu...ila baadaye zinakuvunja nguvu kabisa, ...’akasema na
kunifanya nikumbuke kile walichoawahi kunifanyia.
‘Jamaa muda huo linatokwa na mate kama mbwa
koko,,...tamaa, umalaya umemjaa, lakini hakuweza kufanya alichokitamania,
madawa yalishamlegeza, wakati huo nilishaweka mambo yangu safi,...picha zikawa
zinachukuliwa..’akasema huku akitabasamu, na kuonyesha dharau mdomoni.
Mimi nikatikisa kichwa kama kumsikitikia,
halafu nikageuka kuangalia pembeni, nikimuwazia huyo jamaa alivyokuwa, hajijui
yupo uchi, ..ina maana siku ile na mimi nilifanyiwa hivyo.
‘Nilichofanya ni zoezi la kuigiza, kama jamaa
anakula ndizi vile, kumbe hakuna kitu, ilimradi upatikane mtaji,...picha ninazozihitajia,...nikamaliza
kazi ya kwanza, lakini hatua nyingine nisingeliweza kuifanya peke yangu, ni
lazima nipate msaada ndio nikakupigia simu...’akaniangalia.
‘Nilipanga nikuite mapema, lakini nikaona wewe
bado mshamba, halafu ...sijui labda ni kupenda, nakuonea huruma, ...vinginevyo,
ningelikufanya kama ninavyowafanyai hawa, watu wanaoitwa wana-ume...nakaona
nifanye hatua hii ya mwanzo peke yangu, nakufahamu sana,hujawa na akili za
kutafuta pesa, ila sasa ujue umeshakuwa mtu wangu....’akasema.
‘Sikuelewi..unachoongea....ni upuuzi mtupu sitaki
hata kuusikiliza...mimi sio mtu wako, niache kabisa na mambo yako...’nikasema
nikitaka kuondoka.
‘Hahaha, sasa unataka kwenda wapi, hutaki pesa
yako eeh, ....’akasema akiwa kashikilia bulungutu la pesa mkononi,
nikamwangalia kwa hasira na kusema;
‘Japokuwa nina shida ya pesa lakini siwezi
kuchukua hizo pesa chafu, ....’nikasema na yeye akanisogelea, akanishika shika
,safari hii, nikajarubu kumzuia, na muda huo nilikuwa bado nimevaa koti langu
la kuendeshea pikipiki, ...huwa nikiendesha pikipiki muda kama huo, huwa navaa
koti kubwa, kwa ajili ya kujikinga na baridi.
‘Nafahamu unaona aibu, lakini usijali, utazoea
tu, saa hivi umeshayafulia maji nguo, huna budi kuyaoga, ...nilitaka
nikuhusishe kwa kiasi hicho, ila kuna kazi moja nataka uifanye...’akasema
‘Kazi gani tena!?’ nikamuuliza nikiwa na
wasiwasi.
‘Huyu jamaa alitaka kuniingiza mjini,
nilishamlipa pesa za awali, kwa ajili ya kulitoa hilo gari, nilimtumia yeye,
kwa vile ni bosi wa kitengo hicho, ni kweli, anawasaidia watu wengi, kwa mtindo
wa nipe pesa nikufanyie chapuchapu,...pesa za uwani, hizo haziingii kwenye
mahesabu ya kampuni.
‘Tatizo ni kuwa siku hizi amekuwa ghali sana,anadai
mambo sasa yanafuatiliwa sana, kwahiyo anabeba hatari kubwa kuwasaidia watu,
yeye anaita `kusaidia’, nilipokutana naye, akajifanya hana muda, huku anatamani
kukutana na mimi, nikamjaribu tena ndio akapanga tukutane sehemu, tukaongea, akanipangia
kiwango changu..na bado akitaka na rushwa ya ngono,...’akaangalia saa.
‘Nikahangaika weee, mpaka nikapata kiasi
kidogo,...nikampa, alisema nimtumie kwa mtandao, kwenye namba zake za muda, ni
mjanja sana,...namba hiyo akishaitumia mara moja, anaiharibu, haisajiliwi,....
nikamlipa kianzio, ...ili alitoe hilo gari halafu nitakuja kummalizia nikipata
pesa nyingine,..akanishitukia,... unafahamu alichosema;
‘Huwa mimi silipwi nusu nusu, kama huna pesa
basi na hizo ulizotoa usahau, kwani kiendacho kwa mganga hakirudi....unaona
alivyo,..jamaa huyu ni tajiri kweli, lakini hatosheki, ana majumba ya
kifahari,...magari, kwa ajili ya pesa hizo za magumashi...kodi ya mlalahoi
inateketea...na sasa anataka kunilia pesa yangu, hajui nilivyoipata...’akasema
huku akiangalia saa.
‘Nikamwambia hapa umepotea maboya, utazitoa
hizo pesa na nyingine nyingi, na nitahakikisha utajiri ulio nao,
tunagawana....nilimwambia hivyo wazi wazi, akajua natania, nikawa namuwinda,
ndio wewe ukaja kuajiriwa...
‘Wale wenzako waliofukuzwa, walinisaidia sana
hadi nikalipata hilo gari, nikajua saa wewe kazi yako ni kuhakikisha linatoka
bandarini...lakini kumbe oh, anyway,
tuyache hayo...kwani huyu jamaa saa anamaliza kazi, ...’akasema na kuangalia
saa yake.
‘Jana huyu jamaa kajileta mwenyewe, akaingia
kwenye anga zangu, ...’akasema huku akijiangalia kama anajikagua, huku akitabaamu.
‘Alikuwa ananitafuta sana huyu jamaa,
ananitamani, ....lakini mimi sikuwa namtaka, simpendi, namchukia, nina usongo
naye....japo kuwa ni tajiri,na wanaume matajiri wanapendwa, lakini sio kwangu
mimi, ninachopenda ni pesa, hata hivyo mimi, namuhehimu sana mke wake, ...isongelikuwa
hivyo, ningelishamfanyia kitu mbaya siku nyingi.
‘Aliponichoharibu ni kunitapeli mimi pesa
zangu, nikaona sasa kamchefua mtoto wa mjini, atalisugua gaga, nikaapa kuwa nitamuonyesha,...’
‘Alikuja akanikuta nakunywa, na aliponiona na
nilivyovalia,mhh, macho hayakuficha uchu wake, ....akaisha, na mimi nikajifanya
nipo tayari naye, tukanywa pamoja, ...nikajaribu kumkumbushia kuhusu gari langu
akasema atanisaidia kulitoa gari langu, lakini kwa masharti kwanza anifanye
hawara yake, na akirizika nami, gari atalitoa bila hata ya kutoa pesa nyingine,
..’akasema
‘Wakati nipo hapo tunakunywa nikimweka sawa, ili
nipate muda wa kufanya mambo yangu, mara akaongea na jamaa mwingine...’akasema
‘Jamaa gani?’ nikamuuliza na yeye akaangalia
saa, na alikuwa kama hakusikiliza wali langu akaendelea kusema;
‘Wakati tunakunywa, simu yake iliita, akaongea
kwenye simu na huyo jamaa, na akamwambia huyo jamaa alete huo mzigo hapa kwenye
hii hoteli..nikasema sasa jamaa kaisha huo mzigo ni wangu, anarudisha pesa
yangu, na riba juu...’akasema
‘Ulijuaje kuwa ni mzigo wa pesa...?’
nikamuuliza.
‘Walikuwa wanawasiliana nawasikia,hadi
kuwekeana kiwango, jamaa alitaka kunionyesha kuwa yeye ni mtu wa mapesa kimoyo
moyo nikasema....hizo ni zangu,
alipomaliza kuongea na huyo jamaa nikwambia;
‘Kweli wewe kiboko, yaani unadai pesa zote
hizo, halafu unataka akuletee huku kwenye mabaa, huogopi vibaka...yeye
akanicheka, na kusema;
‘Hizo nazo pesa....hahaha, milioni kumi ni
pesa ndogo kwangu, ..hivyo ni vijisenti kwangu, na hata sina haja ya kuzipeleka
benki, ...’akasema, nikasema kweli nchi yetu inaliwa, kuna watu mabadhirifu,
wanakufuru,wanakula bila huruma ...lakini mimi nitapambana nao....’akasema huku
akikunja uso kuonyesha chuki
‘Hivi hizo pesa zote sizingesaidia shule,
madawa, ...angalia kijijini watu wanavyoteseka, watu wanajenga
mahekalu...kwanini na mimi nisichukue nafasi hii kuzimega,..maana ukiwaachia
hawa mafisadi, watakula huku wanatuanifu kuwa sisi hatujaenda shule, utaenda
shule na nini....’akasema kama ananiuliza.
‘Na
kweli haikupita muda, mara huyo jamaa aliyeongea naye kwenye simu akaja,...akampa
hizo pesa kwa siri, na kuondoka, lakini mimi nilishaona, na wakati huo
nimeshafanya vitu vyangu, nilipoona jamaa yupo lepelepe, nikamshika mkono na
kuelekea huku kwenye chumba, alicholipia yeye mwenyewe...ndio nikafanya vitu
vyangu...’akasema.
‘Sasa unataka kumfanya nini,...?’ nikamuuliza.
‘Huyu jamaa ana mke, na mke wake sio mtu wa
ovyo,...akiligundua hili, kutawaka moto, ...ndio maana nimemfanyia hivi, ili
gari langu litoke haraka iweakanvyo, huyu jamaa ana uwezo huo...’akasema.
‘Nataka akizindukana hapa, ayakute machafu
yake kwenye simu yangu na nyingine nimeshazituma mahali salama, hata kama simu
hii itaibiwa au kupotea, bado mapicha hayo yapo mahali...mimi
mjanja...’akasema huku akionyesha
mbwembwe.
‘Akizinduka hapo atakutana na picha ya matendo
yake kwenye simu yake...japokuwa hayakufanyika kiukweli..lakini kwa jinsi
nilivyoigiza utafikiria ni kweli kafanya hivyo...hata wewe nikikuonyesha
utafikiria kuna kitu kimefanyika, lakini hakuna kitu kama hicho mimi sio
mjinga...’akasema huku akionyesha kidole kwenye kichwa chake.
‘Kwahiyo unataka kumfanyia kama ulivyonifanyia
mimi?’ nikamuuliza akatabasamu na kusema;
‘Huyu jamaa ni malaya, mwizi, na tapeli
..anatumia wadhifa wake, kwa masilahi yake,...mkewe ni muheshimiwa, ana heshima
zake, na alishamwambia mume wake huyu, akija kugundua kuwa anamsaliti,
atamuumbua na hata hiyo kazi anayotamba nayo, ...’akaniangalia.
‘Hawa watu hawa,...mungu atawalaani sana, kazi
aliyo nayo ndio anayoringia,....hataki kabisa kutoka kwenye hicho kitengo, anajua
jinsi gani ya kula na vipofu, wakubwa wanamlinda kwa vile anajua jinsi gani ya
kuwaweka sawa,...yupo kwenye idara nyeti, anachota mapesa anavyotaka, lakini kibaya
ni kuwa hatosheki....’akasema huku akikunja uso.
‘Sasa akiyaona matendo yake hayo, na
nikimtishia kuwa nampelekea mkewe, nina uhakika atafanya kila
ninachokitaka...mimi namfahamu sana, pamoja na yote hayo, lakini kwa mkewe,
kafika...namfahamu kuliko navyojifahamu yeye mwenyewe...zaidi ya hayo
nitamtishia kuwa nitayaweka hayo machafu yake hadharani...kwenye maudaku...atasugua gaga, nakuambia ukweli..., ndio
maana nikakuhitajia hapa....’akasema huku akiangalia saa yake.
‘Unanihitajia nini mimi..hapana nililofanya
linatosha na ninajuta kwanini nimekuja, mimi sitaki kujiingiza kwenye mambo yako
ya kipuuzi, mimi nataka kuondoka...’nikamwambia.
‘Unaondoka? Wewe vipi bwana, kazi
hatujamaliza, ...nafahamu sasa hivi atakuwa kazindukana, kinachotakiwa wewe ni
kujifanya mwandishi wa habari....atakuja mbio mbio akijiona yupo kwenye hiyo
hali,atapita wapi, nataka akitika huko alipo akukute upo hapo nje,...wewe kaa
hapo nje mlengoni, akitokea anza kumpiga picha...’akasema na akaenda kwenye
mkoba wake akatoa kamera ndogo.
‘Unaiona hii hapa..., ni kamera ya kisasa
kabisa..., utakuwa nayo hapo nje, ....akijitokeza tu,...anza kazi yako, usitake
nikufundishe kila kitu....hapo nitamzima makali yake ya kuleta vurugu,...wewe
hakikisha unajitambulisha kama mwandishi wa habari...’akasema na mara akatoa
kitambulisho cha kuning’iniza akanivalisha.
‘Unaona kitambulisho hicho ni geresha, hatakuwa
na muda wa kukikagau kuwa ni halali..muda atakuwa kachanganyikiwa, nafahamu
kabisa atakimbia...nitamsamehe avae nguo zake....’akasema
‘Mengine niachie mimi, ni lazima gari kesho
nilipate, keshaingia kwenye anga zangu....’akainua ngumi juu kuashiria ushindi,
mimi akilini mwangu nikawa najiuliza ana maana gani kusema kuwa ameshanilipa
malipo ya kazi yangu, sikumuelewa....
Nilizindukana kwenye mawazo hayo, nilipoitwa
na bosi...
*********
Jioni nilikutana na bosi, ...
‘Vipi mbona nakuona kama umechanganyikiwa,
kuna nini tena, maana kila siku nakuona uanazidi kuwa kama sio yule mhasibu wa
awali, niambie ukweli, kuna kitu gani kinakusumbua?’ akaniuliza bosi.
‘Mambo ya kawaida tu bosi ....’nikasema.
‘Ukiwa na tatizo, kama limekushinda, jaribu
kumtafuta rafiki mwaminifu , mwambia, huenda uapata msaada, lakini hakikisha
kuwa kweli huyo ni rafiki wa kweli, kwani wengine, wanachukulia matatizo yaw
engine, kufadikia...’akasema bosi.
‘Mimi nipo tayari kukusaidia kimawazo kama
unaniamini...’akasema
‘Nakuamini sana bosi kama kweli nina tatizo
nitakuambia, kwa hivi saa,... najaribu kuyatatua mwenyewe...’nikasema.
‘Cha muhimu, angalia afya yako kwanza,
...kuwaza sana, ni ugonjwa, na madhara yake ni makubwa sana, kuliko hata hicho
unachokiwazia,..fika sehemu uone kama kuna uwezekano wa kulitatua hilo jambo au
la, kama haiwezekani, basi...na usibebe mzigo usiouweza, usijiingize kwenye
mambo usiyoyafahamu, hasa yale yenye utata, achana na ushabiki, achana na
ushindani, kujionyesha kuwa na mimi nimo au ni zaidi...’akasema bosi.
‘Mimi sitaki kukulazimisha sana kuniambia
mambo yako, nataka tu tuendelee na kisa chetu...
‘Unakumbuka tulipoishia, wakati, nimefikia
muda wa kujifungua, na nikamshauri mume wangu kuwa ni bora nikajifungulie
kwetu, kuliko kujifungulia hapo. Mume wangu alionekana kutokukubaliana na
ushauri wangu mwanzoni.
‘Mume wangu nimetoa ushauri huo kutokana na
hali ya hapa nyumbani ilivyo, kiusalama, kama unavyoona, mimi sina mtu
anayenijali, au kunisiliza, ....mama bado hanitambui, ananitambua kwenye kazi
tu, ....je ikatokea nimeshikwa na uchungu,na wewe haupo, ni nani atanisaidia,
...?’ nikamuulza
‘Mama yupo, dada zangu wapo, watakusaidia,
hawawezi kukuacha ukiwa kwenye hali hiyo, wao ni binadamu...’akasema
‘Unasema hivyo kwa vile hushindi hapa
nyumbani, nikuambie ukweli, mama mpaka sasa hajaniweka moyoni, kuwa mimi ni mke
wako,...mawifi zangu, ndio kabisa, wote wanatafuta kila mbinu niondoke hapa,...
unafikiri nikishikwa na uchungu watahangaika kunisaidia?’ nikamuuliza
‘Hakuna mtu anayeweza kukuacha ukiwa katika
hali kama hiyo, ....nina uhakika mama atakusaidia...’akasema mume wangu.
‘Hapana mimi hilo sikubaliani nalo, nataka
nikajifungulie kwetu, mama yangu yupo atanisaidia....’nikasema
Baada
ya majadiliano marefu, mume wangu akakubali niende nikajifungulie kwetu, kazi
ikawa jinsi ya kulifikisha hilo kwa familia yake, ambayo, walijifanya kuwa
nawazarau, kwanini, niamue kwenda kwetu, wakati wao wapo, hata hivyo, shauri
hilo likapita,nikafunga safari kwenda kwetu.
Mungu alinisaidia nilipofika kwetu,
nikajafungua salama, mtoto wa kike, nilikaa kwetu hadi nikamaliza siku 40 ndipo
mume wangu akaja kunichukua tukarudi huko ukweni, napaita ukweni, maana, ni
sehemu ya familia ya mume wangu, sio sehemu yake ya kujitegemea, na nilipofika
nilishangaa , safari hii walinipokea kwa furaha, na wakawa na hamu sana na
mtoto.
Japokuwa lilikuwa jambo jema, lakini mimi kama
binadamu nilijiuliza hayo mabadiliko yametokea wapi, huku nyuma kulitokea nini
, hadi wafikie kunikubali, na kumfurahia huyo mtoto, nikahisi labda ni kwa vile
alikuwa ni mtoto wa kike
Kwenye familia hiyo kulikuwa hakuna mtoto wa
kike aliyezaliwa katika kipindi changu hicho, kwahiyo huyo alikuwa mtoto wa
kwanza wa kike, katika wanawake waliokuwepo hapo wa umri wangu, nahisi ndio
hivyo, kwahiyo wakaonyesha aina fulani ya upendo kwake, na mtoto wangu akawa
anashinda kwa mama mkwe siku nzima na kipindi hicho kukawa hakuna taabu, na
siku zikaenda. Nikamshukru mungu kwa hilo.
Siku moja kukatokea ugomvi baina ya wifi yangu
na mume wangu sasa hapo kesi yote ikaniangukia mie na mama mkwe akaniita na
kuniambia eti nimemroga mtoto wake na kuanzia leo nisikanyage kwao.
‘Mama mbona mimi sielewi mambo hayo,
...nitamlogaji mtoto wako?’ nikamuuliza nikiwa hata sielewi, huko kuloga
unaloga vipi, huwa nasikia tu, uchawi, lakini sijaujua jinsi unavyofanya kazi.
‘Unafikiri mimi ni mjinga, katika umri wangu
huu, nafahamu mengi, mtoto wangu hakuwa vipi, nilikuwa nikimshauri kitu
ananisikia, ...ulipokutana naye tu, akabadilika, ..angalia jinsi alivyo,
utafikiri zezeta fulani, ...hanisikii kabisa, anakusikiliza wewe....’akasema
mama mkwe.
‘Mama nakuapia kwa mungu, mimi mambo hayo
siyajui, na mtoto wako sikumtaka mimi, yote hayo ni mapenzi ya mungu kapanga tu
tuwe naye, lakini kiukweli, yeye andiye aliyekuja kwetu kunioa, na sikuwa
namfahamu kabla...’nikajitetea.
‘Huniambii kitu hapa, kuanzia leo sikutaki
hapa nyumbani kwangu, hapa hapakai wachawi, nimemwambia mume wako, kama
anakung’ang’ania kwa vile haelewi kitu, kwa jinni ulivyo mtengeneza basi atafute
sehemu nyingine ya kuishi...’akasema mama.
‘Mama sasa sisi tutakwenda wapi,..unajua hali
yetu ilivyo, mume wangu hana nyumba, hana uwezo huo kwa sasa...’nikasema.
‘Hilo mtajijua wenyewe, ulipokwenda kwenu
kuutafuta huo uchawi, ulituambia...sasa hiyo ni amri, uondoke kabisa
hapa,..sitaki hata kukuona, mchawi mkubwa wewe..’akasema kwa hasira, na
alionyesha kweli, anahisi hivyo,..
Niliumia sana, maana tangu nizaliwe sijawahi
kuamini hayo mambo, na hata wazazi wangu wapo mbali kabisa na mambo hayo, leo
hii nasingiziwa uchawi, na kuambiwa nimeenda kwetu kuchukua huo uchawi, ina
maana familia yetu ni wachawi....sikuweza kuvumilia shutuma hiyo,...nikasema
mume wangu akija ni lazima nimwambie, aamua moja wazazi wake au mimi.....
NB: Nakabiliwa na mitihani mbali mbali ya
kimaisha, ikiwemo tatizo la mtandao, mtandao kwangu umekuwa mgumu kupatiana, ni
tatizo...ndio maana ile spidi ya
awali inapungua..hata hivyo nitajitahidi tuwe pamoja.
WAZO LA LEO: Uzushi, fitina, imani za kishirikina na uwongo, ni adui mkubwa
wa amani katika jamii. Mambo haya yakizoeleka, amani, huyumba, watu
watachukiana, na kuwekeana visasi, ndio maana wanasema fitina ni mbaya hata
kuliko uchawi.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Huyu mkaka ananiudhi kweli yaan jail ile inamwita
Post a Comment