Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, February 19, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-14


 
Nilifika ofisini mapema, nikiwa bado na usingizi, akili ilikuwa kama sio yangu nikikumbuka mambo yaliyotokea usiku, sikuamini kuwa mdada anaweza kufanya mambo kama yale, mabaya na ya hatari...

Yaani, unavyomuona mdada kwa nje, urembo wake, na matendo yake ni tofauti kabisa, lakini hata hivyo, hata baada ya kugundua hayo, bado nilimuona sijui kanipa nini, maana licha ya yote hayo, kila nikimuwaza nahisi moyo ukinienda mbio...

Mhh...hivi ni kwanini...mbona huyu dada kaniteka akili yangu hivi...hapana, siwezi kumuacha mchumba wangu kwa ajili yake, japokuwa naona oh, sijui kwanini navutika kwake sana,...hapana, siwezi, nitafungwa, hapana....’nikapiga ngumi kwenye meza. 

Hata hivyo, licha ya kuwaza hayo yote, nikijaribu kupigana na nafsi yangu, bado akili yangu kwa upande mwingine, ilikuwa na hamu ya kumuona mdada, leo yupoje, kwanini kachelewa,....lakini pili nimuonye kwa hilo alilolifanya, nimuonye, na kumwambia kabia kuwa mimi sitaki anitumie kama ngazi ya machafu yake,...

‘Ile aliyofanya mdada usiku ni hatari...sijui huyu mwanamke anajiamini nini, oh huyu mwanamke ni balaa, hata siamini,.....’nikasema nikitikisa kichwa.

‘Ngoja aje, nimuonye, nitamueleza ukweli...’nikasema na kufungua kuchungulia nje, kama ameshafika...

Mdada alikuwa hajafika, alikuwa kachelewa, sio kwaida yake, mimi nikawasha komputa yangu, na kuamalizia, kazi zilizokuwa zimebakia jana, nikawa sina kazi za ulazima, na nilipotulia, mawazo yakianza kuja, nikahisi kichwa kikianza kuniuama, nikachukua dawa za maumivu nikameza, na kikaanza kutulia, huku nikiwaza yale yaliyotokea usiku....

Nakumbuka ilikuwa usiku wa kama saa tano, wakati nimeamua kujilalia, kwani mdada alisema atanipigia simu niende kuonana naye kwa kile alichokiita `dili yenye pesa nyingi’i, sikuwa nafahamu ni dili ya namna gani, na kwa kusubiria kwangu huko, sikuwa na maana kuwa nilikuwa na haja ya kuenda huko, hapana, hapo nilipokuwa nilikuwa natafuta njia ya kukwepa kufika huko kwa mdada.

Nikazima taa, na wakati navuta shuka mara simu yangu ikalia, nikapuuza, lakini ikaendelea kuita, nikaziba amsikio, hadi ikanyamaza yenyewe, baadaye nikasikia mlio wa sauti wa ujumbe, nikatulia nijiuliza niusome au nipuuzie, lakini inawezekana ni bosi, nikainuka kitandani na kuufungua huo ujumbe;

‘Fika haraka hotelini, ile dili ipo tayari, .....’ umbe huo ukaishia hivyo, nafikiri baada ya kunionanipo kimiya akaamua kutuma ujumbe mwingine ukisema

‘Hapa nilipo nina barua mbili za kutuma moja kwa mchumba wako na ya pili kwa baba mkwe wako, ...uje uzichukue au nimpe huyu mtu wa hapa hotelini azipeleke posta kesho...unafahamu mwenyewe ni kitu gani kipo kwenye hizo barua....’ujumbe ukaishia. Niliposoma huo ujumbe hasira zikanishika, maana hapo sikuwa na njia nyingine ni lazima niende huko, kwani nilikuwa na uhakika huyo binti hatanii, aatzituma hizo barua.

‘Hivi kwanini huyu mwanamke , anayeitwa mdada ananichezea akili yangu, kwanini anatumia hizo picha kunitishia, hivi kweli nisipoenda atazituma,....’nikajiuliza na wakati nawaza hivyo mara ukaingia ujumbe mwingine , kwanza niliuupuzia nikijua unatoka kwa mdada , lakini baadaye hamasa ikanijia kuusoma, huo ujumbe ulikuwa ukisema;

‘Mchumba wangu, natumai sasa hivi umelala, pole na majukumu ya kazi, nakupenda sana, na natumai ahadi yetu ya ndoa ipo pale pale. Ninachokumba ni  kuitunza ahadi yetu, nakuomba usije ukasahau na kujitumbukiza kwenye maasi, kwani nikija kufahamu, sitakusamehe,unamfahamu baba alivyo..... nakutakia usiku mwema, mimi mchumba wako..’ulikuwa ujumbe kutoka kwa mchumba wangu.

Sitakusamehe...oh, sitakusamahe,...mungu wangu, unamfahamu baba alivyo...oh,...'nikashikashika kichwa kwani kilikuwa kinaanza kuuma.

'Sasa huyu mdada, akiamua kweli kuyatuma hayo mapicha machafu kwa mchumba wangu itakuwaje....mungu wangu nitaishia jela, hapana, ni lazima niikomeshe hii hali,huyu mwanamke anataka kunipanda kichwani, kwanini nisiyaharibu, ni lazima nione wapi ameyahifadhi ni yaharibu...'nikasema huku akilini nikijiuliza kwa vipi.

'Nimafanye nini huyu mwanamke, kwani sasa naona ananichanganya kabisa kichwa changu, huyu mtu, anaweza kuyatuma hayo mapicha na kunimaliza...’nikasema na hapo kichwa kikaanza kuniuma, na humo ndani nilikuwa sina kinywaji, hapo nikapata kisingizio cha kutoka, ...kwa haraka, nikavaa nguo za kutokea na kutoka nje,..

‘Unaenda wapi saa hizi...’nilishituka karibu kulibwaga lile pikipiki, ilikuwa sauti ya mwenye nyumba, iliyonishitua, nigauke kumwangalia, nikaona kasimama kashika panga,  akilini nikajiuliza huyu mzee analala muda gani, mbona kila muda nikitoka namkuta yupo nje, ...nikamwambia.

‘Natoka kidogo mzee, kazi zetu hizi hazina saa maalumu, nimeitwa kuna dharura ....’nikasema nikiwa nimehawasha hiyo pikipiki, na yeye akasema;

‘Kama ingelikuwa ni mimi nisingelikubali, maana kazi za kuitwa usiku na muda kama huu sio nzuri,mara nyingi zina ishara mbaya, kwa uhauri wangu rudi ukalale utakwenda kesho..’akasema.

‘Hapana ni muhimu sana mzee..ni lazima niende...’nikasema huku nimeshaanza kuondoka.

‘Huyo atakuwa ni msichana anakusumbua kichwa chak, hakuna lolote..achana naye...’akasema huyo mzee, huku nikiwa nimeshaanza kuondoka, sikugeuka nyuma ila ujumbe wa mzee, ulikuwa umenifikia, na kunifanya niwaza, huyu mzee kafahamu vipi,.... sikujali nikaondoka.

Nilikwenda kwa mwendo kasi hadi kwenye hiyo hoteli, nikapitia sehemu yangu ya siri, na kuliegesha pikipiki , nilihakikisha nimelifunga na mnyororo, ili lisije likachukuliwa tena, nikatoka pale nikamwendea mlinzi ;

‘Wewe umepitia wapi?’ akaniulza

‘Umenisahau mkuu, ni ile ile njia yetu...’nikasema huku nikimshikisha kitu kidogo.

‘Na wewe bwana, hujaacha ule utundu, wako, sasa chombo umekiacha wapi?’ akaniuliza

‘Pale pale niangalizie...’nikamwambia

‘Hapo utaongeza chochote....’akasema

‘Usikonde, ...wewe wangu  , nikasema huku nikipanda kuelekea juu..

Mhaibu umeshafika, ilikuwa sauti ya bosi, iliyonishitua kutoka kwenye dimbwi la mawazo, nikawa kama mtu aliyetoka usingizini.

‘Ndio bosi...shika...mooh, oh, samahanani bosi, nilikuwa mbali...’nikasema na bosi akacheka, na kusema.

‘Ndugiu yangu kama imefikia hatua hiyo, ...utakufa siku sio zako.....nione ofisini kwangu mara moja...’akasema na mimi nikajiandaa, nikampa nusu saa nikaelekea ofisini kwangu kwangu, na wakati nafungua mlango nikasikia ujumbe wa simu ukiingia kwenye simu yangu,...kwa vile nilihafungua mlengo wa bosi, sikuweza kurudi kuusoma, kwani simu niliiacha mezani.


**********

‘Hebu niambie jana ulikuwa wapi?’ akaniuliza
‘Nilikuwa nyumbani...kichwa kinanipa shida, sana, nikaamua kulala mapema...’nikamdanganya.
‘Mhasibu, usinidanganye, ...jana hukuwa nyumbani, na hali uliyo nayo, sizani kama uliweza kulala..’akasema na kuniangalia kwa macho ya kunichunguza.
‘Bosi, kwani nipoje....?’ nikauliza
‘Unafahamu nikuambie kitu, unapokuwa umeajiriwa, ina maana nguvu zako umeziuza kwa mwajiri wako, ...na kwahiyo kila siku inayoingia unatakiwa uwe na nguvu sawa kwa ajili ya kulipa dhamana, kwa mawajiri wako...’akasema.

‘Ajira ni dhamana, ni deni kwa mfanyakazi kwa muajiri wake, ambalo makubaliano yake ni mshahara kwa ajili ya kazi utakayoifanya, sasa jiulize, kweli kwa hali kama hiyo, uliyo nayo, unaweza ukatekeelza wajibu wako, ....?’ akawa kama ananiuliza.

‘Ukiwa katika hali kama hiyo, ni wazi kabisa utendaji wako utakuwa sio wa kiwango kinachostahili, hapo unamuibia muajiri wako,...dhamana ya watu unaihini, na mwisho wa mwezi unataka kulipwa, ...hiyo sio sahihi...jaribu sana, kuwa waadilifu, uadilifu wa kweli, ni ule wa kuangalia, jinsi gani unavyoitunza dhamana ya watu, kwa kutelekeza majukumu yako kama inavyotakiwa...’akasema bosi.

‘Mimi nimekuita asubuhi hii, kukukanya kuwa hayo yaliyotokea hapa ofisini, yasitokee tena, nimegundua ukweli ulivyokuwa, zile hundi, hazikuwa za mteja halali,.... sitaki kukuelezea zaidi,nimeongea na baba yake mdada, na nimekubaliana naye, hili liwe onyo la mwisho, ikitokea tena, sitakuwa na jinsi nyingine,.....' akasema.

'Nafahamu kabisa wewe na mdada mnaufahamu hu ukweli, cha msingi, ni kuhakikisha kuwa kosa hili halitokei tena, pili, achana na vishawihi vya mdada, mwenzako ni mwalimu, ....’akasema na kuangalai nje, kulikuwa na mngurumo wa gari.

‘Unaona huyo anaingia,...oh, ana gari jipya, na inaonekana halijasajiliwa namba zake..'akasema bosi.

'Gari jipya...ni la kwake kweli?' nikauliza na mimi nikijaribu kuchungulia dirishani.

'Inawezekana ni la kwake,..., sasa jiulize hizo pesa kazipatia wapi za kununua gari kama hilo, kama sio ujanja, hujuma na dhuluma,.....mimi sitaki kuingilia maisha ya watu....kuwa kwanini, amezipata wapi, ilimradi awe anatimiza wajibu wake,wa kazi, ilimradi hayo mambo, ya magari, nyumba, yasitokene kutokana na masilahi ya kampuni, ...’akasema bosi akiangalia saa, na kusema;

‘Nataka kutoka kidogo, kabla sijaondoka, nitakuhadithia kidogo ni nini kilitokea kwenye ndoa yangu...kama unakumbuka, tulipoachia kuwa nilishaonana na mama mkwe, na sio mama mkwe tu aliyekuwa mbaya wangu, kumbe pia walikuwemo mawifi zangu, na wao pia walikuwa hawanitaki, ....haya sasa tuendelee kuanzia hapo, au kama una kazi mezani kwako, nikuacha ukazifanye?’ akaniuliza

‘Hapana bosi, kazi nilishazimaliza tangu jana, nasubiria mdada aje anipe baadhi ya nyaraka za kazi,kuna stakabadhi za malipo, na nyaraka za madeni, alisema atanipa leo,  ...’nikasema, huku nikihisi usingizi mnzito machoni.

‘Ok, basi, ngoja,tuendelee kidogo, ukimsubiria huyo mdada, maana leo hatuongei, kama hilo gari ni lake, leo atajitahidi kila mtu amuone kuwa ana gari...’akasema bosi huku akitizama nje, kuliangalia hilo gari.

********

‘Kwa ujumla, tofauti na nilivyokuwa nimefikiria awali, kuwa kuolewa ni kwenda kujitegemea, na kuachana na hali ya utegemezi kutoka kwa wazazi, kwahiyo unakwenda kuwa na sehemu yako, kuwa huru...ukizingatia kuwa mimi nimekulia kwenye mateso kwahiyo niliichukulia ndoa kama sehemu ya kuyakwepa mates hayo.

Nikuambie ukweli, hali niliyoikuta huko kwa mume wangu, ni kama ule usemi wa kuruka mkojo na kwenda kukanyaga mavi, hali ya hapo, haikuwa ya amani kwani mama mkwe na mawifi zangu hawakuwa na mapenzi na mimi hata chembe, japokuwa nilijitahidi sana kuwa mwema kwao, japokuwa nilijitahidi kuvumilia madhila yao.

Siku zilienda na kama baada ya mwezi hivi mimi nikakaribishwa jikoni;

‘Hapa kuna zamu, za kupika, za usafi na majukumu yako na mume wako unajijua wewe mwenyewe, lakini kupika , usafi wa nyumba, vyombo, inatakiwa kile mtu na zamu yake...’akasema mama.

‘Na kwa vile yeye kampumzika sana, inabidi aanze mara moja...’akasema mke wa shemeji.

‘Ni kweli, ikibidi aongeze siku mbili zaidi...’akasema wifi

Mimi sikuwa na pingamizi basi nikajiunga kwenye zamu za kupika, na usafi wa nyumba, vyombo  kwangu mimi hilo halikunipa shida kwani mimi nilikuwa mpenzi sana wa mapishi,wa kupika haikuwa tabu kwangu. Kazi kubwa ilikuwa kwenye vyombo, maana kutokana na familia yenyewe, na wao wakijua kuwa ni zamu yangu, wanafanya makusudi kuchafua vyombo, ili nikomoke, ..hata hivyo, niliweza kumudu kazi zote bila kulalamika.

Kilichokuwa kikinikera zaidi, ni kero zao, kusimangwa, hakuna nitakalofanya lionekane jema, japokuwa mimi ni mpishi mnzuri, na hapo walilifahamu hilo, lakini hawakuacah kutoa kasoro, mara vyombo havijatakata, ...wakati mwingine, wanavichafua makusudi, ili nionekana sijaviafisha.

Nilifanyiwa vitimbwi, visa, na vurugu na masimango ya kila aina, kila aina ya vituko unavyovifahamu wewe, nilifanyiwa mimi, na mawifi, wakishirikiana na mama yao na hata mke wa hemji yangu alijiunga nao, sijui na yeye nilimkosea nini...

Siku moja nilikuwa nimefua nguo zangu na mume wangu nikazianika kwenye kamba, nikawa ndani, nafanya usafi, nilimuona wifi na mama mkwe wakitoka nje, na baadaye wakaingia ndani, huku mama mkwe akisonya...nikajiuliza kuna nini nimekifanya tena huko nje, nikatoka kuhakikisha, ...

Nilipoangalia kwenye kamba, nikakuta nguo zangu hazipo, lakini za mume wangu zipo kwenye kamba, nilipoangalia pembeni, niliziona zikiwa zimezamishwa kwenye matope,...

‘Jamani ni nani kafanya hivi...?’ nikauliza nikiwa nimeshitushwa na kitendo hicho japokuwa haikuwa mara ya kwanza, ila sasa wamezidi, siku nyingine wanazitupa tu chini, sasa hivi wamezigaragaza kwenye matope.

Mke wa shemeji muda huo alikuwa ndio anatoka nje, akaniona nimesimama, naangalia hizo nguo, hakusema neno yeye akaendelea na hughuli zake, na akasema;

‘Unalo hilo, umeingia kwenye anga za watu, hawatachoka kukufanyia visa, mpaka utoke humu ndani...’akasema.

‘Kwani wamenioa wao..mbona wewe hujaondoka.’nikasema

‘Sasa usilalamike,mimi babu wee, ni chaguo lao, wamenipenda wote, mume wangu, mama mkwe na mawifi zangu, sina shida...’akasema na kuingia ndani

Wakawa wananisema huk ndani, mimi nikachota maji, na kuanza kuzisuuza tena, nikazianika, na nilipomaliza, nikaingia ndani, niliwakuta bado wananisema na waliponiona wakakaa kimiya na nilipokuwa naingia ndani,  mara  wakaangua vicheko, na wifi yangu mmoja akasema

‘Na bado, mpaka aikimbie hii nyumba ....’ moyoni nikasema hakimbii mtu hapa, nitavumilia hadi nione mwisho wake.

Siku zikaenda hali ikazidi kuwa mbaya, hata hivyo sikukata tamaa, na miezi mitani ikapita, na mimi nikajihisi nina mabadiliko ya kimwili, nikajua kuwa nina ujauzito, hali hiyo nilishaihisi, mapema, lakini sikuwa nimezingatia, kwani ile hali ya pale,ilikuwa vigumu hata kuulizia, na kwa vile ni mimba ya kwanza, na sijui ukiwa hivyo inakuwaje.

Nilipokwenda hospitalini, wakaniambia nina mimba ya miezi mitatu, ilikuwa kama nimechokoza, maana japokuwa kuna muda nilikuwa najisikia vibaya kabla, lakini sikuwa nimetilia maanani, lakini nilipoambiwa na dakitari kuwa nina mimba, hali ikaanza kunibadilikia.

Nilianza kujisikia vibaya, ...nikawa nashikiwa na kizunguzungu, hata kudondoka, na hapo dakitari akanishauri, nisiwe nafanya kazi nzito, nipunguze kazi, na nipate muda wa kupumzika, nikamwambia mume wangu, na yeye akaniambai nifanye hivyo.

Ukumbuke nyumba hiyo tulikuwa tunaishi kifamilia, kuna shemeji na mke wake, kuna hao mawifi zangu, kuna mama mkwe,....na tulikuwa tumepangiwa zamu kila mtu na siku zake, walipopewa hiyo taarifa kuwa mimi natakiwa nipumzike, wao wakagoma kabia, wakasema siku zangu zipo pale pale, kama naweza nitafute mfanyakazi wa kunifanyia siku zangu.

Mimi ni mchapakazi, sikuwa na tatizo na hilo, japokuwa kwa ujumla, hapo nyumbani kulikuwa na kazi nyingi sana, kwa vile familia ilikuwa ni kubwa, na hali ya kipato cha mume wangu isingeliwezekana kutafuta mfanyakazi, nikamuomba mungu, anisaidie, nifanya hivy hivyo kwa kadri nitakavyoweza.

Kwakweli nilikuwa na wakati mgumu, pamoja na vitimbwi, visa kusimangwa, na sasa nina ujazito, hakuna aliyenijali;

‘Oh mungu wangu nakuomba uniwezeshe niweze kuilea hii mimba hadi mwisho, kilinde kiumbe chako tumboni, nijifungue salama,...’ilikuwa dua na maombi yangu kwa mungu kila siku. Nikawa najitahidi hivyo hivyo, mpaka nikakamilisha miezi 9.

Muda wa kujifungua ukawa umekaribia, na zamu yangu ipo pale pale,nikaona hapo sasa hakuna usalama, nikakaa na mume wangu kushauriana, tufanye nini;

‘Mume wangu mimi nina ombi, naomba ulipokee kwa mikono miwili kwa ajili ya hiki kiumbe, nafahamu kabisa kama nitajifungulia hapa, itakuwa ni matatizo, huwezi kujua ni muda gani uchungu utanishika,...’nikasema

‘Una ombi gani...?’ akaniuliza

‘Ni bora nikajifungulie kwetu...’nikasema

‘Eti nini....?’ akauliza akionyesha kukasirika....

NB: Je ilikuwaje


WAZO LA LEO: Ubaya na matendo maovu hayalipi, na kama yakilipa ni kama mtu kunywa maji machafu, akapooza kiu, lakini kaingiza ugonjwa tumboni, siku yoyote atapatwa na madhara. Tusipende kuwatumbukiza wenzetu kwenye majanga, tusipende kuwatendea wenzetu mabaya, kwani matendo hayo ni dhambi, ni deni, ipo iku na wewe yatakukuta hayo hayo, kwako au kwa kizazi chako. Kwanini tusifanye kinyume chake, tuwe wema, tupendane, tusaidiane, ili tuwe na akiba nzuru mbeleni. Wema kamwe hauzi.

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Swali langu..Je inawezekana yule atendaye mabaya kwa mtoto wa mwenzake au kwa mwenzake hakumbuki kweli au ndio makusudi tu? Maana ingesaidia sana kama siku moja akamwomba radhi.....Hata kama wanasema mtenda husahau ....

emu-three said...

@Yasinta, Kwa nionavyo mimi, wakati mtendaji anapotenda huo ubaya kwa watoto wa wenzae, huwa hajioni, haoni kuwa anachokifanya ni kibaya kwa muda ule,...lakini baadaye nafsi humsuta.