‘Natumai mumekuja na taarifa kamili, kama
nilivyowaagiza, kuhusiana na upotevu wa
stakabadhi za malipo, na kwanini hundi za malipo ziliandikwa bila ukamlifu
wake, hadi benki wakazikataa...’akaanza bosi, nikamwangalia mdada, ambaye
alionekana hana wasiwasi kabisa.
‘Nataka niliweke hili wazi, kuwa baada ya
makosa ya nyuma ambayo yalileta hasara kwenye kampuni na hata wateja kujenga picha
mbaya dhidi ya kampuni, kwasababu ya udanganyifu wa baadhi ya wafanyakazi,
waliokuwa sio waaminifu, nimeamua kuweka taratibu mpya za malipo, ambazo
hazitaruhusu hundi kupita benki mpaka benki wawasiliane na mimi, na hni hiyo ni
lazima iwe na viambatishi maalumu, mlipwaji anahitaji kuwa navyo..’akasema
‘Kwahiyo kama mlivyoona, hundi zingine zote
zilipita, lakini hizo hundi mbili zikawa na walakini, mlipwaji hakupeleka hivyo
viambatishi, pili hata nilipouliza habari zao hao wateja, walionekana ni kama
kampuni hewa, na mimi kwa kumbukumbu zangu sina taarifa za mikataba yao, huenda
ni hawa wa karibuni kutokana na huo mzigo mpya, ndio maana nataka maelezo
kutokwa kwenu, kabla sijaruhusu hizo hundi zipite benki...’akasema.
Bosi akageuka kuniangalia mimi, halafu
akamwangalia mdada, mdada, alikuwa kama hayupo, hakuwa anaangaliana na bosi,
alikuwa kaangalia nje, kwa kutizama dirishani, naona bosi anamfahamu tabia
yake, hakumsemesha akasema;
‘Niliwaambia toka awali kuwa tushirikiane
kuhakikisha kuwa kampuni hii inaendeshwa kwa haki na ukweli, na taratibu zote
za kikazi ziwe zinafuatwa...taratibu hizo sio kwa hapa tu, ukienda kwenye
kampuni yoyote, hizo taratibu utazikuta...sasa nashangaa inakuwa kama vile
hatujui ni nini tulichokisoma....’akageuka kumwangalia mdada.
‘Mdada, wewe ndiye umepewa jukumu la uofisa
utawala, nilitarajia sana wewe uwe karibu sana na mimi katika maswala ya
utendaji, na usimamizi wa mambo ya kampuni...haya matatizo tusingeyaongea hapa
sasa kama wewe ungelifanya kazi yako vyema,....sawa labda kuna wateja wapya,
waliofika kwako, ulitakiwa utoe taarifa hiyo idara ya masoko,nimewauliza idara
ya masoko wanasema hawana taarifa ya wateja wapya...ni wateja gani hao,
utuambie...’akasema bosi, na kunigeukia mimi.
‘Na wewe mhasibu, mimi nilikuwa nakutegemea
sana, katika mambo ya malipo, wewe unafahamu ni nini kifanyike kabla hundi
haijaandikwa, ...sio kwasababu tuna pesa bila kila anayedai analipwa, siku ile
nilisema tuwalipe wanaotudai, ulielewa nina maana gani, ...wewe kama mhasibu
ulitakiwa kusimamia hilo...haya niambie hao wateja ulikuwa na kumbukumbu zao,
viambatishi vyao sijui utaniambia nini, ...’akasema na kuniangalia.
‘Sasa nataka mniambie ukweli kuhusu hao
wateja, na kwanini stakabadhi zao, zikapotea, ni nani
kazichukua...’akaniangalia na kumwangalia mdada.
‘Bosi mimi nina uhakika kuna mtu kazichukua,
na kuhusu hao wateja ni nani, nafikiri mdada atanisaidia kwa hilo, ..nakiri
nilifanya makosa ya kumwamini mdada moja kwa moja, nikijua kuwa kila kitu kipo
sawasawa, nakiri hilo kosa, na nahitajika kuwa makini ...’nikasema na bosi
akamwangalia mdada, ambaye alikuwa kama hayupo, hajali, hana wasiwasi, na
alipotuona sote tunamwangalia akasema mdada akasema;.
‘Hao wateja ni kweli ni wateja wapya, na
nilijua kuwa mhasibu anawafahamu, kwasababu kumbukumbu zake , viambatishi vyote
vilikuwepo,...nawashangaa hao watu wa idara ya masoko,wanakataa bure,
nilishawaambia kuwa kuna wateja wapya ambao watasaidia kuhakikisha hiyo mizigo
mipya inafikishwa sehemu husika kwa wakati, nikaongea nao nikakubaliana
nao....sasa naona kama wanakwepa majukumu, kwa vile tu, hili
limetokea,...’akajitetea mdada.
‘Kwahiyo baada ya tukio hili, wewe ukaamua
kuchukua kumbukumbu zao...?’ akauliza bosi.
‘Ndio ilibidi nizichukue nizirudishe kwa
wenyewe, ili wazilete upya kwa jinsi unavyotaka wewe, kwani kama nilifanya vile
inavyoonekana ni sahihi, na umeona sio sahihi, kwanini nyaraak za watu
ziendelee kuwepo ofisini...’akasema mdada kwa nyodo kama anaongea na mwenzake
tu.
‘Kwanini sasa hukusema awali, maana nimeuliza
mara mbili hizo kumbukumbu zao zipo wapi, mpaka nikawapa muda wa kwenda
kuzitafuta,sikuelewi mdada, ....?’ akauliza bosi kwa hasira.
‘Bosi wiki mbili hizi nimekuwa na mambo mengi
yaliyonichanga kichwa, kuna kazi nyingi zipo mbele yangu, nina matatizo mengo
ya kifamilia, kama nilivyokuelezea,...mimi nilipotimiza wajibu wangu, nilijua
mhasibu naye atafanya kazi yake, ..kamaa kulikuwa na makosa angeniuliza,
hakuniuliza akaandika hundi,....na ilipotokea hilo, kwa haraka ili nisiwakwaze
hao wateja, nilichukua hizo kumbukumbu kwenda kuongea nao, ....’akasema
Bosi akataka kumuuliza swali jingine akasita,
akaniangalia mimi, halafu akashusha ile hasira aliyokuwa nayo na kusema;
‘Kwahiyo hizo kumbukumbu unazo, ...baada ya
kuwapelekea na kurekebisha walikupa kumbukumbu nyingine, au ni zile zile,
nilitaka nizione...?’ akauliza bosi.
‘Nimesema nimeshawapelekea wahusika, na
kuwaarifu kuwa wafuate utaratibu unaotambulikana na wewe, wao walikuwa hawaujui
huo utaratibu wako, kwahiyo watazileta kwa jinsi nilivyowaelekeza...watakuja
kwako moja kwa moja..’akasema mdada mdada kwa sauti kama ya kukasirika.
‘Mdada uwe makini na kazi zako, kwa jinsi
unavyotenda, nakuona kama haupo na sisi, unaposema taratibu zangu, kama
ninavyotaka mimi, ..huo usemi unaonyesha kama ahupo hapa, kwani
nilishawaelezea, na tukaanza kufanya hivyo,...pili kwanini uwakubalia kiasi hiho kikubwa cha pesa, wakati kazi
hawajaimaliza,ilikuwa jukumu lako kuwaulizia, au hiyo kazi huiweze niwape watu
wengine, kama umezidiwa na kazi useme ...’akasema bosi.
‘Sijasema siwezi kuzifanya hizp kazi...na
maswala ya kawaida yaliyonikwanza, ...’akasema na kutulia.
‘Hebu nikuulize hao wateja walifanya kazi gani,
na kwanini majina yao hayapo wazi,mikataba haipo, mikataba ni jukumu lako, ndio
maana nasema hiyo kazi tuwape watu wa masoko, ulidai kwa vile uliisomea
utaifanya, naona majukumu kwako yamekuwa mengi, utawala na kusaidia kazi za
masoko hutaweza.....’akasema bosi.
‘Bosi mim naomba niwafuatilie hao watu, kila
kitu kitajieleza pindi wakileta kumbukumbu zao, ni nini walichokifanya , na
wamefikia wapi, hayo watajieleza wenyewe, mimi kazi haijanishinda, ni kazi
ndogo sana hiyo, ni kwa vile sikupata msaada wa akribu kutoka kwa wenzangu,
ndio maana lawama zote zinaangukia kwangu....’akasema mdada kwa sauti ya
kukereka.
‘Lakini ni kweli kuwa ulikwenda kinyume na
utaratibu wetu wa kiofisi, kwa vile wewe uliona ha wateja ni muhimu sana,
ukakimbilia kuwalipa, sijui labda kwa vile mizigo hiyo ilitakiwa kufika mahali
fulani kwa haraka, hata hivyo, bado, ulikuwa na nafasi ya kuongea na wenzako,
au kuniambia mimi, hilo ni kosa na unahitajika kukiri, ni sawa si sawa...?’
akauliza bosi.
‘Mimi sioni kosa langu lipo wapi hapo,
ilitakiwa mhasibu baada ya kuona kuwa kumbukumbu hizo hazipo sawa, anirejeshee,
ili niweze kumpa maelezo, au nifuatilie, ....unakumbuka nilitakiwa kuzileta
hizo kumbukumbu haraka kwa vile ulikuwa unataka kusafiri, na kama
nilivyojieleza, nilikuwa nimetingwa na mambo binafsi, kwahiyo nilichofanya
nikuchukua bahasha yenye kumbukumbu za maombi ya malipo, na kuzifikisha kwa
mhasibu,...’akasema akiniangalia.
Bosi akatikisa kichwa kama kusikitika, halafu
akanigeukia na kuniangalia, akasema;
‘Mhasibu nafahamu mwisho wa siku lawama zote
zitaelekezwa kwako, ...ni kweli kwa swala la malipo wewe ulitakiwa uhakikishe
kuwa vimbatishi vyote vipo, hakuna swala la kumuamini mtu hapo, ...ninaweza
kukutetea, maana bado hujawa na uzoefu wa kutosha wa taratibu za hii kampuni,...lakini
hizi ni za kawaida popote, na hata vyuoni vimefundishwa,..sasa lawama zinakuangukia
wewe, kama alivyodai mdada,...’akaniambia lakini bado akamgeukia mdada.
‘Mdada, mimi badi nipo na wewe, je mikataba ya
hao watu ipo, maana hiyo tunakuwa na nakala yake, unaweza kunipatia mikataba
yao...au uliamua kuwalipa kwanza halafu ndio make, mjadili, sijui huo ni
utaratibu wa wapi,...nikuambia ukweli, makosa yote yametokana na wewe, kwani
kama wewe ungetimiza wajibu wako vyema haya yasingelitokea, ...’akasema bosi.
‘Mimi sioni kosa langu bosi,...na hata
tukilaumiana kosa limeshatokea, cha muhimu, ni kurekebisha hayo makosa, sio
kunilaumu, haya umenilaumu, nio kusema hilo kosa litajisahihisha, na isionekane
kulikuwa na kosa, hilo limefanyika, kila mmoja keshajirudi,...’akasema mdada
akionyesha kukereka zaidi, ni kama hakutaka kuulizwa.
‘Tuchukulie mfano kama hundi hizo zingepita,
na hao walipwaji wakaja kugundulikana kuwa sio sahihi, tungelisema nini, hizo
gharama ungezibeba wewe...ndio maana nataka kila mtu ajione, na aone uzembe
wake, ili hili kosa lisirejewe tena, ....’akasema bosi na mimi nikaitikia kwa
kichwa.
‘Mimi nilishahisi kuwa kuna malipo bandia
yametengenezwa, ...na bado nafuatilia, kama nikigundua kuwa hilo lipo, sitasita
kuwachukulia wote wanaohusika hatua za kisheria, wewe mdada, na mhasibu
mtawajibika kwa hilo...’akasema bosi akimwangalia mdada, halafu akaniangalia
mimi.
Mdada akageuka pembeni akiwa kakunja uso,
hakusema neno, na bosi akasema;
‘Ok, hilo tumeelewana, lakini kuna hundi hii
ya mwisho iliyolipwa bila hata nakala moja ya stakabadhi,..hebu niambieni, hilo
nalo lilikuwaje...nimewaambia benki hiyo hundi wairejeshe kwetu, nataka
kuiangalia mwenyewe, ilikuwaje, mhasibu...?’ akauliza bosi na mimi kabla
sijafungua mdomo mdada akasema
‘Hao wateja wapya walitaka kianzio, na
walisema hawataweza kuendelea na kazi bila kupata chochote, nikaona ni bora
nichukue hizo pesa, nikawape,....walikuwa wakinikera sana kwenye simu,
nikamwambia mhasibu, ...yeye alikuwa na kazi zake, hakulichukulia umuhimu,
...’akasema mdada.
‘Ninachojiuliza wewe uliipataje hiyo hundi, na
kwanini ukaiandika wewe , na sio mhasibu, toka lini ukafanaya hiyo kazi, ndio
kuna dharura, ninaweza kutoa kibali uandike, ...na hapo ni mpaka upate kibali
kutoka kwangu, ...na hiyo ni dharura kama mhasibu hayupo...je mhasibu alikuwa
kaenda wapi...?’ akauliza bosi.
‘Muulize mhasibu mwenyewe ,yeye alikataa, hilo
lisifanyike, na akaniambia kama mimi ninaweza kulithibitisha hilo, niongee na
wewe, hivi kulikuwa na haja gani ya kuwepo na hizo hundi, si kwamba kukitokea
malipo ambayo ni muhimu, tuzitumie, ...ndivyo nilivyofanya,... mimi kwa vile
nafahamu umhimu wa hao watu nikaamua nichukue hiyo stakabadhi niandike
mwenyewe....’akasema mdada.
‘Hilo ni kosa jingine umefanya mdada,
unachukua maamuzi, bika kibali cha mdhamana wa majukumu hayo, ...mimi
mwenyewe,siwezi kuja kwa mhasibu na kuchukua kitabu cha hundi, na kujiandikia
mwenyewe hata siku moja, hilo ni kosa kubwa sana la kiutendaji....’akasema
bosi.
‘Kwanini ulimdharau mhasibu kwenye majukumu
yake..., huyu ndiye tumempa majukumu hayo, na anawajibika kwa hilo,..hilo ni
kosa kwa wote wawili...ninaliweka kwenye kumbukumbu zangu, na nitatoa onyo kali
kwa maandidshi...’akasema akiniangalia.
‘Hiyo hundi kama imerejeshwa, mkabidhi mhasibu
, haitalipwa tena,mpaka nione kumbukumbu za hao watu, na mikataba
yao...’akasema bosi.
‘Sawa bosi, ...’nikasema
‘Na muelewe hilo nalifanyia kazi, maana
sijapata taarifa iliykamilika, ...mnaweza kwenda,..’akasema na mdada alikuwa wa
kwanza kuondoka akiwa kakasirika, na mimi nikamfuataia nyuma, bosi akasema;
‘Mhasibu baadaye nataka kukuona.....’akasema
na sisi tukatoka chumba cha bosi, huku siamini kuwa hayo yamepita kwa amani,
moyoni nikaapa kuwa sitafanya hayo makosa tena.
Tulipofika
ofisini kwangu, mdada akapiga ngumi ukutani na kusema;
‘Ssshit, sasa huu ni ujinga mtupu......haya
yote umeharibu wewe...huyu bosi wako anajifanya hii kampuni ni yake peke yake,
hajijui....’akageuka na kuniangalia.
‘Na wewe zumbuekuku, unaona ulivyoharibu, kama
nisingeliingilia kati ungeropoka ovyo..huna maana kabisa...’akasema
akiniangalia kwa hasira
‘Nimeharibu nini mimi, wakati yote umeyatunga
wewe mwenyewe, unafanya mambo ya kitoto, huoni kuwa hayo hayapo na hukustahili
kuyafanya, unaniharibia kazi yangu....’nikasema
‘Ni kuambia wewe mwanaume, utakufa
masikini,...ukiendelee kufanya hivyo, utabakia kusindikiza wenzako, utaona
wenzako wanajenga, wana magari, wana miradi wewe unakalia kuangalia
makaratasi,...’akanisogelea kama vila hataki sauti ifike mbali.
‘Huyo bosi wako anasema hivyo kwa vile
unamjengea maisha yake na miradi yake, wewe unapata nini hapo , ndio huo
mshahara eeh?’ akawa kama aniuliza
‘Eti mshahara, ni mshahara gani huo unaopata, mhasibu mzima, ...mshahara ambao
huwezi hata kuweka akiba, amuka mwanaume, kama hawakulipi vizuri, tafuta njia
ya kujilipa, mimi ndio nimeanza kukufundisha, lakini naona kama napigia gitaa
mbuzi,.....’akasema.
‘Nikuambie ukweli usiponisikiliza mimi ,
ukajijenga, ukawa na wewe na kitu chako, utakuja kunikumbuka, na utanikumbuka
kipindi ambacho umeshaharibikiwa na kukosa kila kitu, huku una mke, una watoto,
na majukumu kibao, ndio hapo unashituka na kuanza kuhaha..’akasema huku
akiniangalia moja kwa moja usoni.
‘Utaamuka wakati wenzako wanakimbia hujui
uende wapi, kiwanja huna, sijui utajenga wapi na kwa vipi, amuka mwanaume, ni
mwanaume gani wewe usiyebebeka, hivi uhasibu wako ndio huo wa kushika
makaratasi, nikuambia ukweli, sio kila kitu ufundishwe, mengine unatakiwa
utumie akili yako, hata bosi anafahamu hataki kukuambia tu, unafikiri yeye
angelifika hapo alipo, kama hakuyafanya hayo, ...’akasema huku akiniangalia kwa macho makali.
‘Kwa hili lililotokea mimi nimeamua moja, hiyo
ndoa yako unayoisubiria haitakuwepo tena...labda nifanikiwe...sijajua kwa vipi,
vinginevyo, ndoa itakuwa kati yangu mimi na wewe, na siku nitakapoamua mimi, naona
kabisa wewe ni kichwa ngumu,...na unahitajia kuishi na mtu kama mimi,...tatizo
lako wewe hujanielewa mimi ni nani,...umenikasirisha sana leo,...’akasema
‘Kwanini unasema hivyo , ndoa yangu inahusiana
nini na hayo mambo yako...?’nikamuuliza
‘Huoni eeh, unataka nikuonyeshe,...hivi
hujaona ulichokifanya, umenicheleweshea kufanikisha mipango yangu, hivi sasa
naumiza kichwa nitapatia wapi hizo pesa, ...wewe bado unaona huna kosa, na hapo
ulipo mchumba wako ni muhimu sana...sasa sikiliza kwa makini, kama nisipopata
hizo pesa, ...nitahakikisha kuwa baba mkwe wako anafahamu kila kitu...’akasema
akiniangalia kwa macho makali.
‘Mimi mbona sikuelewi, ninakuuliza, hili
linahusiana vipi na ndoa yangu, ...na baba makwe hapa anakujakujaje, na ulitaka
mimi nifanye nini....?’ nikamuuliza na yeye akabadili uso na kuongea ka
tabasamu, na kama ananong’ona akasema;
‘Ngoja nikuambie kitu, kwa kujikosha, ..leo usiku
kuna dili moja nataka kuicheza, na wewe ni lazima uhusike, .....nitakupigia
simu nikiikamlisha, usipofika nitaituma ile barua,...yenye upuuzi wako kwa baba
mkwe wako...tuharibikiwe sote.....unasikia tuharibikiwe wote...’akasema
akiniangalia huku akitabasamu, utafikiri sio yeye anayeongea huku akinipitisha
kidole tarataibu usoni.
‘Unafahamu mimi nakupenda sana, sijui kwanini
vinginevyo nisingelipoteza muda wangu kwako, ni wangapi wananitaka mimi,
lakini.....oh, kweli penye miti hakuna wajenzi,...’akasema huku akipitisha
vidole vyake mdomoni kwangu, nilitamani niuondoe mkono wake, lakini yeye
akauondoa haraka na kusema;
‘Hata hivyo, mimi sitaharibikiwa kwa maana
nimeshajipanga vyema nafahamu ni nini ninachokifanya..., je wewe, ukikosa kazi hapo kwa bosi wako utakwenda wapi, bado
unatarajia kuishi kwenye nyumba ya kupanga hata kiwanja cha kudanganyia huna, na
hapo ulipo maisha yako, yanategemea kubebwa na baba mkwe,....’akasema
akiniangalia kwa dharau.
‘Sawa mimi nimekubali kashifa zako, na hayo
ndio maisha yangu niliyokubaliana nayo, hayakuhusu, kwahiyo, ...’nikataka
kusema na yeye akaniangalia huku akitabasamu na kusema;
‘Masikini mhasibu, unatia huruma...mmh,...akawa
kama ananisogelea, na mimi nikarudi nyuma na kusema;
‘Mimi nimeshakuambia sitaki kujihusisha na
mambo yako, na hilo la kumpelekea baba mkwe hayo mapicha, limetoka wapi...?’
nikamuuliza na yeye akatabsamu akataka kusema kitu, lakini mimi sikumpa nafasi
nikamwabia
‘Hebu mdada achana na huo upuuzi wako, hivi
kwanini unanitafuta ubaya, nini lengo lako, unataka nikuchukie,....nikuambie
ukweli nikiamua kupambana na wewe, hutaamini....na nikikuchukia hutaamini kuwa
ni mimi....’nikasema kwa kujipa moyo.
‘Nataka uamue hivyo,tupambane,...yaani
ninavyoombea itokee hivyo,...lakini nafahamu kuwa huna ubavu huo,mtu mwenyewe
umeshazimia kwangu, sema ukweli....pili nina siri zako nyingi, nikiziweka
hadharani hata huyu bosi wako, hatatamani kukaa na wewe...unabisha ?’ akaseme
an kuniuliza huku akijiangalia na kuniangalia usoni, mimi sikumjibu nikawa
namwangalia tu, na alipoona namwangalia akasema;
‘Tutaonana usiku...’akasema huku
akinikonyesheza na kuondoka, huku akitingisha maungo yake kimiondoko ya
kinamna, akitikisha makalio yake,...nikabaki nimeduwaa, na kuhema muhemo wa mtu
alitoka kupandisha mlima....
********
Baadaye nilikwenda kumuona bosi, na niliingia
bila kugonga mlango, kumbe alikuwa akiongea na simu, ikabidi nitoke na wakati
natoka nikasikia akisema;
‘Una uhakika hakuna kampuni kama hizo, na je ulifuatilia account zao ukagundua ni
watu gani....ni kweli beni jawawezi kuruhusu kuangalia accounti ya mtu , lakini
nafahamu wewe unaweza kupata hizo taarifa, nakuomba unisaidie kwa hilo...’akasema
na kukata simu.
‘Mhasibu unaweza kuingia...’akasema, na
nilipoingia akawa kainama kama anasoma kitu kwenye komputa yake, alionekana
kutokuwa na furaha kama siku nyingine, alionekana mwingi wa mawazo, sijui ni
kutokana na hilo lililotokea au ana mambo yake mengine binafsi
‘Inabidi mambo mengine niyafuatilie mwenyewe,
na hayakuwa na umuhimu wa mimi kuyafuatilia sio kazi yangu, lakini bila kufanya
hivi, kampuni haitaenda, wakati mwingine natamani nitafute watu wengine,
niondoe wafanyakazi wote wabovu, lakini, sio vizuri,...unapokuwa bosi unakuwa
kama mzazi, ...huwezi kumfukuza mtoto wako kwa tabia mbaya, unatakiwa kumuadibu
kwanza, ikishindikana ndio unasema, ngoja dunia imfunze......’akasema.
‘Bosi ina maana ndio unawaulizia hawo wateja, ambao
nyaraka zako hazionekani....?’ nikamuuliza
‘Kuna mambo mengi nafuatilia, na hilo ni
mojawapo, mimi nilitarajia wewe na mdada mtaweza kunisaidia kwa kiasi kikubwa,
lakini kwa tukio hili lililotokea, naanza kuwa na mashakanyie, inaonekana wewe mwenyewe
huna msimamo, kwanza wa maisha yako na pili wa kazi yako na usipoangalia kazi,
itakushinda, na maisha yako yatakuwa ya kuyumba yumba....’akasema
‘Bosi, nakuhakikishia hilo halitarejea tena,
wakati mwingine unapofika sehemu ngeni, inabidi kukutana na changamoto kama
hizi, kwasababu bado sijawajau vyema, ni nani wakuaminika, na ni nani ana tabia
gani, nimeshaanza kuwasoma wafanyakazi wa humu tabia na nyendo
zao....’nikasema.
‘Sizani, ...kama huyu uliye naye karibu,
ambaye muda wote mpo naye umeshindwa kumsoma, utawezeje kuwasoma hao wengine,
ambao mnakutana mara moja moja...’akasema.
‘Kwanini bosi?’ nikauliza
‘Mfano mzuri ni huo, inawezekana vipi mtu aje
kwako na kuchukua hundi ya benki, ambayo ipo kwenye himaya yako na kuandika
mwenyewe, huoni kuwa ana mamlaka juu yako...kitu ambacho hata mimi mwenyewe siwezi
kukifanya, siwezi nikaja nikachukua hundi na kujiandikia bila ya rizaa yako,
lakini yeye anafanya hivyo, ...’akasema bosi.
‘Bosi huyo nimeshamsoma, sikuwa na uhakika
kuwa alichukua hiyo muda gani, nilikuja kugundua baadaye..mwanzoni wakati
tunaongea mimi nilijua ni utani tu, kumbe wakati nahangaika na mambo mengine, ndipo
hapo aliweza kukichukua hicho kitabu cha hundi na kuchana hiyo nakala moja,
....’nikajaribu kusema uwongo.
‘Mhh, haiingii akilini, ...lakini ok
nitahakikisha hilo linakoma, na wewe uwe makini, maana hili swala nitalifuatilia
kwa karibu, nataka kuhakikisha hii kampuni hii inaendeshwa kisheria, na
utaratibu uliokubalika, kama watu hawawezi kufanya hivyo, sitakuwa na namna
nyingine, nitawaondoa, ili niajiri watu wenye kukubaliana na taratibu za
kazi,...’akasema
‘Bosi usilichukulia hivyo, ni bahati mbaya,
nita....’nikajitetea.
‘Hiyo sio bahati mbaya, jambo la bahato mbaya
linajionyesha, hapo kuna dhamira ya kweli ya kulifanya hilo, lakini kwa bahati,
limetokea wakati nimeshaweka huo mfumo mpya..vinginevyo, sasa hivi tungelikuwa
tunahangaika na polisi...’akasema.
‘Oh....’nikasema hivyo.
‘Ndio hivyo ikitokea tena, sitasita kuwaita
polisi,waje wawakamate hao wote wanaohusika,..wakaishi jela kidogo, na wakitoka
ajira hakuna tena....’akasema.
‘Bosi nitahakikisha hilo halitendeki tena,
naithamini sana ajira yangu, nimehangaika sana kuipata, na nihitajia sana kwa
maisha yangu ya baadaye......’nikasema na yeye akasema;
‘Kusema ni rahisi, lakini vitendo ndivyo
vinavyohakiki ukweli wa mtu,kila mtu anaweza kusema naweza, lakini je ni kweli
anaweza,kama anaweza vitendo vyake vitamuhukumu...’akasema bosi, huku
akiniangalia kwa makini.
‘Bosi mimi naweza....nakuhakikishia
hilo....’nikasema huku kichwa kikianza kuniuma.
‘Kuna kitu nimejifunza kutoka kwa wafanyakazi
wangu, japokuwa sasa kidogo wanaaza kubadilika, kuna tabia ya kufanya kazi kwa
nia ya kumuonyesha bosi kuwa wanafanyakazi, sio kwa nia ya kutimiza wajibu
wao..hili linanikera sana, ...maana bosi ukiondoka, ina maana kazi hazifanyiki mpaka urudi, huo ni utumwa wa akili , ...na
kwa hali kaam hiyo,hatutaweza kufikia malengo..’akasema.
‘Natumai watu watabadilika, mimi sina tabia
hiyo...najituma wakati wote, tatizo ni changamoto za watu wengine,...’nikasema
‘Ni vyema ukajitambua, upo wapi unafanya nini,
na kwanini, anyway,...nataka iwe
hivyo, mimi nitajitahidi kadri ya uwezo wangu,
ili wafanyakazi wangu wabadilike, wajitambue,wajue wajibu wao ni nini, nahisi
ni vyema, kila mmoja awe na utashi wa kujitambua, na kuwa tayari kujituma, na
hili litawezekana kama kila mmoja ataweza kuweka mbali matamanio yake binafsi,
na kujua kuwa hii ni kampuni, inayoendeshwa na watu, kwa manufaa ya wote, sio
kwa manufaa ya mtu mmoja...’akasema
‘Matarajio yangu ni kuwawezesha kila mmoja aweza
kupata mahitaji muhimu, kila mmoja kutokana na kipato chake aweza kupata
mahitajio yanahitajika kwa mwanadamu, chakula malazi,na matibabu,...nafahamu
kabisa, kama familia, zikiwa hazina
matatizo, mfanyakazi ataweza kujituma vyema, akili yake itatulia kazini, lakini
kama kaacha matatizo huko nyuma, ni dhahiri, akili yake haitauwa kazini...
tatizo ni kwa wale wenye tamaa kubwa, wanataka zaidi, ya uwezo wa kampuni....’akasema
bosi.
‘Nashukuru kusikia hivyo bosi, inanipa moyo
kuwa nimefika sehemu inayojali mfanyakazi...’nikasema
‘Tuyaache hayo kwa muda, nataka nikusimulie
sehemu ndogo ya makaribisho yangu kwa mama mkwe...’akasema bosi,....
‘Unakumbuka tulipoishia kwenye kisa changu,
baada ya kikao cha wanafamilia, wakakubaliana kuwa twende huko huko kwa mama
mkwe, kutoka hapo tulipokuwa kwa shemeji, hadi huko kwa mama mkwe, ilikuwa ni
safari ndefu, iliyotakiwa kuchuka meli, na safari hiyo ilikuwa ni ya usiku....,
haya tuendelee......
****
Ilipofika usiku tuliondoka na meli, na pale
nilipokuwa nimekaa,akili yangu haikuwa sawa, kwani nilikuwa nikiwaza mengi, nilikuwa
nikiwazia yaliyotokea na yanayoendelea kutokea, na huko sijui nitakwenda
kukutana na majanga gani, hasa hayo yaliyoanza kujitokeza ya mama mkwe.
Kwa ujumla nilikua sina raha, nilikuwa sina
amani kabisa kwenye nafsi yangu, sikuelewa ni kwanini mimi nikutwe na mitihani
yote hiyo, je mimi nilikuwa na kosa
gani, au kwa vile mimi ni mwanamke, lakini mbona wasichana wengine hawakukutwa
na masahibu kama yaliyonikuta mimi, kama kweli hayo yanatokea kwa vile mimi ni
mwanamke.
‘Mbona haupo sawa, ...unatakiwa ufurahi,
unakwenda kuanza maisha mapya...’akaniambia mmoja wa jamaa wa mume wangu.
‘Ningeliomba iwe hivyo, na ndivyo matarajio
yangu yalivyokuwa, lakini sijui kwanini mnasema mama mkwe hanitaki, hilo ndilo
naliwazia...’nikasema.
‘Unafahamu tena akina mama, huenda yeye
alikuwa na mipangilio yake, lakini wenzake hawakumsikiliza...’akasema
‘Kwanini wasiseme mapema...’nikauliza
‘Tulijua ni maswala ya muda tu, mama
atakubaliana na hiyo hali, ...lakini usijali, hayo ukifika huko yataisha tu, ni
hasira za muda...’akaniambia.
Niligeuka kumwangalia mume wangu aliyekuwa
kasimama akiangalia dirishani, alionekana na yeye katingwa na mawazo. Kwa namna
fulani nilimuonea huruma, maana mama ni mama, kama hamkubaliani na mama ni
lazima utakuwa na wakati mgumu sana, sikujua ni kwanini hawakuwa kitu kimoja,
je ni kuhusu mimi, kuwa hanitaki, kuna mtu mwingine alimtaka yeye, au kuna
mengine ... ..
Basi nikajitahisi kujizuia, maana kila
nilivyozidi kuwaza, niliona machozi yakikaribia kunitoka, na sikutaka watu
wanione ninalia, nikajipotezea, na huku safari ikiendelea.
Tulifika huko tunapokwenda asubuhi,na hapo
nilipo moyo ulikuwa ukinienda mbio, jinsi gani nitaweza kukabiliana na huyo
mama mkwe asiyenitambua, asiyenitaka...
Tulipofika nyumbani, tulipokelewa na baadhi ya
wanafamilia , ilionekana nyumba haina raha, tofauti na ilivyotakiwa kuwa, kwani
nilitarajia kuwa kutakuwepo na shamra shamra za kumpokea bibi na bwana harusi,
lakini hilo halikuwepo,na hata dalili ya kuwa kunakuja mgeni, ilikuwa kama watu
wa kawaida tu wamefika.
‘Huyu ni wifi yako mkubwa na yule anayefuatia,
ni wifi yako pia....’wakaanza kunitambulisha juu kwa juu,
‘Hilo litafanyika baadaye...wageni wafike
watulie, familia ikutane, ndio utambulisho uanze, mnafanya kama anaondoka
leo...’akasema mke wa shemeji.
‘Hicho kikao cha familia kitakalika kweli,
mama atakubali...’akasema wifi na kukatishwa na mwenzake, kama kumkanya asiongee.
Alyekuwa karibu nami zaidi alikuwa shemeji wa
mume wangu, nahisi ni kwa vile na yeye ni mtu wa kuja kama mimi...., na kama
alivyosema wifi, hakukuwa na kikao cha wanafamilia, au hata ile shamra shamra,
na kwa vile nilijichokea, nikaona bora iwe hivyo tu
Tukakaribishwa ndani, kwenye varanda kuu,
hakukuwa na mpangilio kama kuna wageni muhimu wanakuja, kila kitu kilikuwa kama
kawaida tu,....mimi kwasababu ya kuchoka, nikajipweteka kwenye kiti hata bila
kuambiwa karibu ukae, nilikuwa nimechoka, kiakili na kimwili.
Nilitizama huku na kule kama nitamuona mama
mkwe, lakini hakuwepo karibu, nikawa nimetulia kusubiria nini kitakachoendelea,
baada ya kutulia kidogo, mume wangu akaniambia twende ndani chumba kingine, ili
tukamsalimia mama yake. Hapo moyo ukaanza kunienda mbio, nakwenda kumuona mama
mkwe.
Kwasababu ya kuogopa, kukutana na huyo mtu,
nikawa kama nasita, na mume wangu akatangulia, kuelekea kwenye hicho chumba, na
mimi nikamfuatia kwa nyumba na mume wangu akagonga mlango, karibu mara tatu,
hakuna mtu aliyeitikia, mwishowe akaamua kufungua mlango.
Tukaingia kwenye hicho chumba, nikamuona mama kakaa
pembeni ya kitanda, kashika shavu hakutuangalia, alikuwa kainama chini, na
mtoto wake alipomsalimia, akainua kichwa na kumwangalia kwa uso uliojaa hasira,
kanuna kabisa hakuitikia hata salamu ya mtoto wake, sembuse ya kwangu. Baadaye
tukatoka bila hata ya kusikia neno moja kutoka kwa mama mkwe, nikaona sasa hapo
ipo kazi.
‘Sasa tufanye nini, kwani kwanini mama
hanitaki mimi?’ nikamuuliza tena mume wangu.
‘Usijali yatakwisha hoyo...’akasema inaonyesha
hakutaka kuniambia ni kwasababu gani mama hanitaki.
Tukarudi varandani, na kukaa kidogo, kwani
kuna watu walifika, ni wanandugu wengine kwa baba mdogo au mkubwa, wakawa
wanatusalimu na kutambulishwa; Wengine walionyesha furaha zao, lakini wengine
niliwaona wakiniangalia kwa jicho baya, nikawa najiuliza kuna nini kuhusu mimi
kwa hawa watu,...,
Tulipomaliza kusalimia na watu mbalimbali,
nilionyeshwa chumba changu, na kwa jinsi nilivyokuwa nimechoka nikaenda moja
kwa moja chumbani kupumzika, nikiwa na dukuduku moyoni la kujua kulikoni,
hakuna aliyeweza kunieleza, nikasikia nikiitwa kuwa chai ipo tayari.
Nilitoka chumbani, na hapo kidogo niliona
maandalizi ya kifamilia, tulikaa pamoja, akiwemo mama mkwe, na kwa mara ya
kwanza nilisikia sauti yake, lakini alikuwa akiongea na watoto wake wa kike, na
hao mawafi zangu niliwaona wakiniangalia kwa macho ya husuda, na ilionekana
wapo upande wa mama yao.
Muda wote wa kunywa chai hakuna
aliyeniongelesha, walikuwa wakiongea na mama yao, na kunifanya mimi kama sipo
kabisa hapo, nilikuwa na wakati mgumu hata hiyo chai ilikuwa hainyweki vyema,
nikajitahidi hivyo hivyo hadi nikamaliza kunywa hicho kidogo nilichoweza.
Mume wangu alikuwa akinywa chao na wanaume
upande wao mwingine, kwahiyo sikuwa na mtu aliyeweza kabisa hata kuniuliza chai
vipi, nikajitahidi hivyo hivyo tu.
Tuliendelea kunywa chai hivyo hivyo, huku mama
mkwe hataki hata kuniangali, na ikitokea bahati kageuka upande wangu, uso
niliouona ulikuwa wa chuki, na hali ilivyoendelea hata mawifi nao wakawa
hawaniangalii kwa tabasamu, walianza kufanya kama anavyonifanyia mama yao,
kuniangalia kwa chuki,..., kiadabu, nilisubiria hadi wote walipomaliza kunywa
chai, na nilipotaka kuondoa vyombo, mmoja wa amwifi akasema;
‘Wifi wewe nenda kapumzike, ...’akasema mmoja
wa mawifi, na ndipo nikaondoka na huku nyuma nikasikia wifi mwingine akisema
‘Kwanini unajipendekeza kwake, muache aondoe
vyombo, kwani kaolewa hapa kuja kufanya nini, ukianza kumvimbisha kichwa
atajiona kafika...’akasema huyo wifi
‘Sio vizuri,tusimfanyie ubaya mapema mapema
hivyo,...ngoja akusanye nguvu, sijui kaka kampendea nini, kati ya wanawake wote
, anakuja kumuoa huyu, kweli kaka hana maana...., ‘ akasema huyo wifi mwingine
‘Tutaona ...’ilikuwa sauti ya mama,
.....lakini alikuwa akiongea kwa sauti ya chini sana kama ananong’ona, sikuweza
kumsikia vyema.
‘Dada, huyu tusimpe muda, ikiwezekana akimbie mapema,
eti mama eeh, .....?’ nikasikia akimuuliza mama yake,
Mama yake aliongea jambo lakini sikusikia
alichoongea ni nini, mimi kwa muda huo nilikuwa bado nimesimama mlangoni
sijaingia chumbani kwangu,...’nikageuka kuwangalia nilipogeuka uso wetu
ukakutana na huyu wifi aliyeonekana kunichukia sana, na niliona akiniangalia kwa
dharau na mama mkwe kwa muda huo nay eye alikuwa akinitizama, uso wake
ulionyesha chuki kabisa...
.
Moyoni nikasema kama maisha yenyewe ndio hivi,
basi ni heri niachike, nirudi kwetu, na hata kama wazazi wangu hawanitaki,
nitakimbilio kokote nikaishi, lakini sitakubali kunyanyaswa tena, nitamshauri
mume wangu kama kweli ananipenda tutafute sehemu nyingine ya kuishi, na hapo
nikasikia sauti ikisema;
‘Kwa vile tutakuwa naye humu ndani, ...hawana
sehemu nyingine, tutahakikisha, anakimbia mwenyewe,amuache kaka yetu , .....
NB: Ni hayo kidogo kwa leo
WAZO LA LEO: Kwanini tuchukiane, kwanini mioyo yetu, haitaki kujenga urafiki
wa kweli, na kuondoa mafundo yaliyojikita nafsini kwetu. Urafiki, raha,
tabasamu na kupendana, huleta murua mwema usoni, na matokeo yake ni upendo na
amani, lakini chuki, fitina, hasira visasi, dharau, ...hujenga sura mbaya
usoni, na matokeo yake ni vita, uhasama na baraka katika ardhi huondoka.
Tupendane kiukweli siku zote,bila unafiki na ajenda za siri, ili dunia iwe
kisiwa cha amani chenya baraka na upendo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment