Binadamu tulivyo, hata ujitahidi vipi, hata uwe mjanja wa
kuvumilia usingizi, kuna muda kwenye usiku, inafika unashindwa kuvumilia na ni
lazima utapitiwa na usingizi tu, na ndivyo ilivyotokea kwangu, ...’ Shahidi
akaendelea kuongea.
‘Japokuwa nilitaka usiku huo nikeshe, ili kuhakikisha mambo
yangu yanakwenda kama nilivyopanga. Lakini usingizi ukanipitia, kwani baada ya
shughuli za usafi, kupanga mambo aliyokuwa akihitajia Makabrasha, kuweka
taratibu za vikao vyake vya kesho, nikajikuta nimechoka sana.
Niliongea kidogo na Makabrasha kuhakikisha kuwa kila kitu
chake kipo sawa, na akaniambia hatanihitajia tena kwa usiku huo, na yeye akatoka kwenda chini kwenye sehemu ya
hoteli kujiburudisha na watu wake, mimi nikaingia chumbani kwangu kubadili
nguo, kabla ya kufanya hivyo, nikajilaza kidogo kitandani, nikiwa na mawazo
yangu, nilijiegemeza kidogo kwenye mto, nikiwa nimeweka mikono nyumba na kichwa
changu kulalia viganja vya mikono, hapo hapo usingizi ukanipitia.
Nilishituka ni asubuhi, na kilichoniamusha ni simu yangu ,
iliyokuwa ikilia, nilikuwa nimeweka mlio wa kutikisika tu, ...bila kuangalia
mpigaji , nikaipokea hiyo simu kwa haraka, ilikuwa ni sauti ya mdogo wa mume wa
familia, nikamuuliza kuna nini asubuhi hiyo, akaniambia yupo karibu na eneo la
hilo jengo alimleta kaka yake.
‘Oh, kumbe kumekucha...kwahiyo, mpo na kaka yako? ’nikamuuliza
nikipiga miayo, nikainuka pale nilipokuwa nimejiegemeza, na mdogo wa mume wa
familia, akasema wapo naye, na yeye ataondoka, na kurudi baadaye kumchukua,
kwani sio vyema kwa yeye kuonekana hapo nje. Nikamwambia sawa, hakuna shida.
Kwa haraka nikainua godoro, pale nilipoficha silaha yangu,
nikaiona ipo, nikarudishia godoro kwa haraka, kwani nilihisi kuna mtu anakuja
kwa nje, nilisikia mlio wa yayo za mtu, nikajiweka sawa, nilijua nitakuwa nahitajika
kuweka mambo sawa, kwa ajili ya wageni, ...hakuna mtu aliyeingia, nikafungua
mlango kuchungulia kwenye korido, sikumuona mtu, lakini nina uhakika kulikuwa
na mtu anakuja muelekeo wa chumba changu.
Nikarudishia mlango na kutulia kidogo, nikamigia mdowa wa
mume wa familia, nikamuuliza kama kaka yake ameshaingia ndani, na kama
anahitaji nimpe ile silaha, na yeye akasema;
‘Kwa hali ilivyo hapa nje, huwezi kunipa hiyo silaha,
..lakini ulisema utaihitajia hiyo silaha leo kama kaka akifika, kwanini unataka
kuirudisha tena?’ akaniuliza.
‘Kazi muhimu nimeshaimaliza, ila kuna kitu nataka kukufanya,
kama itawezekana, lakini sio muhimu kwa sasa nilishaongea na kaka yako, kama
akiwa mjinga na kusaini huo mkataba atakuwa kaharibu kila kitu, yote inategemea
yeye, vinginevyo, kwa vile ni mchana siweze kufanya lolote na hiyo silaha,
kwahiyo sio muhimu kwa mchana wa leo, lakini kama unaona hakuna usalama huko
nje, basi ngoja ikae kae huku, huenda nikaihitajia...’nikamwambia.
‘Sawa hamna shida, kama alisema atafanya kama
mlivyokubaliana, sijui mume kubaliana ninini,...’akasema na mimi nikamwambia.
‘Tutaongea baadaye, je unavyoona kwa kaka yako,yupo safi,
anaweza kufanya niliyomuagiza ayafanye...?’ nikamuuliza, akasema;
‘Yupo safi, skuona tatizo lolote kwake...’akasema na mimi
nikakata simu,i nikainuka kitandani na kwenda kuoga na kujiweka sawa, kiofisi
zaidi, nilimpigia simu mume wangu, kumtakia hali;
‘Mume wangu haujambo, samahani sikuweza kukupigia simu usiku
nilibanwa sana na kazi...’nikamwambia.
‘Hamna shida hata mimi nilikesha hospitalini, kulikuwa na
wagonjwa wa dharura, ndio nimefika nyumbani mara moja, kuangalia usalama,na
sasa hivi naondoka, huenda nisirudi mpaka jioni au usiku....’akasema.
‘Sawa ukiwa na nafasi, tutaonana,jioni au ...’nikamwambia.
‘Tutawasiliana kama nitakuwa na nafasi, vinginevyo, nakutakia
kazi njema,...’akaniambia na mimi moyoni nikawa naumia sana, niliumia kwa hayo
ninayoyatenda, kwa mume mwema kama huyo. Kiukweli, sijawahi kuishi na mtu
ambaye anakujali, na kukuonyeshea mapenzi ya dhati kama mume wangu, lakini
maumbile yalivyo, hisia na ...sijui niseme vipi, hakuna angaliweza kushika
nafasi ya mpenzi wangu wa asili...’akasema na kumwangalia mume wa familia
ambaye alikuwa kainamisha kichwa chini.
‘Hata hivyo, kama isingelikuwa Makabrasha, na huyo mpenzi
wangu wa asili kuja kuniharibia mipango yangu, mimi ilishafikia hatua, nikaamua
kuwa huyu ndiye mume wangu nitajitahidi kumpenda hasi mwisho, lakini ghafla
ndio akaja mume wa familia na matatizo yake, ikabidi niwe mtu wa kumliwaza, na
unafahamu damu zetu zinaendana, kuliwazana, kunaturudisha nyuma, na mnajikuta
mumevunja ahadi za ndoa.
Ilianza kama mchezo, ikawa sasa ni kawaida, akija amelewa,
au kuchanganyikiwa mimi namfarisi na akinihadithia mambo yake na mke wake,
namuonea huruma sana, nahisi kipindi hicho ndicho Makabrasha aipata mwanya wa
kuchukua picha ambazo ni moja ya kumbukumbu za picha za video alizokuwa
kazihifadhi, sikuweza kupata muda wa kuziangalia, niliziharibu bila ya
kuzianalai vyema.
Na alipokuja mume wa familia na kashifa aliyoitengeneza
Makabrsaha kuwa ataitumia kuharibu ndoa zetu, kama hatutakubali matakwa yake,
ndio ikaharibu kila kitu, hata yale mawazo yangu ya kuendelea na ndoa yangu
hiyo ikaanza kuingiwa na doa,
Kuna kipindi mume wangu alishuku, mabadiliko niliyokuwa
nayo, lakini nilimficha kabisa, japokuwa moyoni nilikuwa naumia sana, na
sikuweza kumwambia mume wa familia kuwa mimi naumia sana kuendelea kumdanganay
mume wangu...
Wakati nawaza hayo, nikasikia tena mtu akitembea kwenye
korido, na mimi nikafungua chumba haraka na kutizama nje, nikaona mtu akiongia
kwenye moja ya chumba kilichokuwepo mbele, sikuweza kumuona vyema, alikuwa ni mwanaume,ilikuwa
ni kitendo cha haraka,....aliingia kwenye chumba kilichokuwa bado kwenye
matengenezo, kilikuwa hakijamalizwa, nikahisi huenda ni mmoja wa mafundi, kaamua
kuwahi, lakini kwa uhakika, nikaona niende niangalie.
Nikarudi ndani kidogo na kuvaa nguo za kikazo, nilifanya
haraka haraka, nikatoka na kwenda hadi kwenye kile chumba, sikuona mtu, nahisi
huyo mtu alishatoka, lakini atakuwa kafanya haraka sana, na atakuwa ni mwepesi
sana, ila kulikuwa na dalili zote kuwa huyo mtu aliingia hapo, na kutoka.
Nikatoka kwenye kile chumba na kuangalia sehemu zote hakukuwa na mtu maeneo ya
karibu, nikajaribu kuangalia kila pande, lakini sikumuona huyo mtu.
Ili kuwa na uhakika zaidi nikawapigia walinzi kuwauliza kama
kuna wafanyakazi wa ujenzi wameshawahi asubuhi, wakasema hawajafika. Hapo
nikaingiwa na wasiwasi, na afadhali kama mitambo ingelikuwa ON, ningeliweza
kujua ni nani, kwa kwenda kuangalia huko.
Mimi nikaondoa wasiwasi, nikajiandaa na kuelekea ofisini
kwangu. Kabla sijafika huko, nikapitia chumba cha mitambo ya usalama, nikaingia
na kuweka ile mitambo ON, halafu kwa haraka nikarudi ofisini kwangu....
Nilikuwa na ofisi yangu na humo nilikuwa kama mhasibu,
mtunza masijala, na pia ni katibu muhutasi wa Makabrasha, kwahiyo utaona jinsi nilivyokuwa na kazi nyingi. Na hapo ndipo mara nyingi nakaa kama hakuna kazi
nyingine. ni ofisi iliyokamilika kila kitu, komputa simu, mafile..nk.
Ofisi yangu hiyo ipo mbali kidogo na ofisi ya Makabrasha, ile ni kwenye korido
moja. hiyo ni ofisi wakati nafanya kazi za kuweka kumbukumbu, ila nikiwa nafanya kazi za ukatibu muhutasi, huwa ninakuwa kwenye ofisi kubwa karibu na Makabrasha. Katika maswala ya usafi yupo mtu anafika kufanya hiyo kazi lakini kipindi hicho alikuwa likizo,
kwahiyo nilikuwa na kazi kubwa ya usafi,na kazi nyingine....
Hata hivyo kazi kubwa
nilishaifaya usiku, nikapitia pitia sehemu muhimu na kuhakikisha kuwa zipo
safi, baadaye nikataka kwenda chumba cha
Makabrasha, nilifahamu wakati kama huo yeye na rafiki yake yaani mume wa
familia watakuwepo kwenye chumba cha maongezi, wakipata vinywaji, kabla
hawajaingia ofisini kuzungumza mambo yao ya mikataba, nawafahamu sana taratibu
zao kila wanapokuja kuonana, na ndipo nafasi ya mume wa familia ya kupata
kinywaji, kwani akitoka hapo anatakiwa kuigiza kuumwa...
Nilifika ofisi ya Makabrasha nikaona kafunga na ufunguo,
kama nilivyotarajia,...huwa hataki kufanya makosa, chumba chake kama hayupo
huwa kimefungwa, na hakuna mtu anaruhisiwi kuingia kama mwenye hayupo,
hamuamini mtu, hata mtoto wake mwenyewe haruhusiwi kuingia hapo kwenye ofisi
yake kama hayupo, hata mimi sina ufungua wa chumba hicho wa akiba. Sikuwa na
kazi kubwa kwenye chumba hicho, kwani usiku nilishakifanyia usafi, haikuwa na
haja ya mimi kufanya usafi mwingine. Na hata yeye alishaniambia hanihitajii
ofisini kwake mpaka aniite,kwahiyo haikuwa na haja ya kuingia tena humo,
nikarudi ofisini kwangu
Nikiwa pale, nikapigiwa simu, na mtu ambaye hakujitaja jina,
akaniambia;
‘Acha hayo unayokusudia kuyafanya, kwani tumeshakujua njama
zako, kama utaendelea na mambo yako,utakuja kujuta, ...’halafu akakata simu,
sikumuelewa ni nani, ni sauti ngeni kabisa, na ilikuwa ya kukwaruza kwaruza,
nahisi aliweka kitambaa mdomoni, ...sikusema neno, maana mimi kutokana na akzi
yangu vitisho kama hivyo nimeshavipata sana, na mara nyingi nina hulka yangu
kuwa mtu mwoga hutanguliza vitisho, na mtu kama huyo hana lolote, mtu jasiri ni
yule, anayetanguliza vitendo.
Na wakati nimetulia nikiwaza cha kufanya, mara simu nyingine
ikalia, hii ilikuwa ya aliyekuwa bosi wangu, akaniambia yeye anaondoka,..
‘Sawa. Samahani nimeshindwa kuonana na wewe, lakini natumai
mambo yanakwenda vyema, na mtoto wako umeshampata...’nikasema.
‘Mtoto sijampata, licha ya kuwa nimewatimizia mambo yao
yote, wameniambia nitakutana naye uwanja wa ndege, kwahiyo hapa nilipo sina
amani kabisa...’akasema.
‘Mimi nina uhakika mtoto utampata na yupo salama, huyo
anayekaa naye, ni dada mwema sana anafahamu jinsi ya kulea watoto, nilimtafuta
mwenyewe, niliambiwa nimtafute...’nikasema.
‘Kwahiyo wewe upo wapi?’ akaniuliza.
‘Usijali, nakutakia safari njema, ukirudi natumai mambo
yatakuwa yamebadilika,...’nikasema na kukata simu.
Baadaye nilitwa na Makabrasha, nikaenda ofisini kwake, alikuwa
peke yake, sikumuona huyo mgeni mwingine, ...sikuuliza, yeye akasema;
‘Jamaa yako ameshafika, yupo wash-room, nimekuita mara moja, kuna kumbukumbu zangu sizioni
kwenye mtandao wetu, nimeongea na mtoto wangu anasema anakushuku huenda ni wewe
umeweza kuingia kwenye komputa ya kuhifadhi kumbukumbu na kuziharibu, hebu
niambie ukweli,mimi ninakuamini sana ...’akasema na mara simu yake ikalia, akaniangalia
na kusema;
‘Ondoka tutakuja kuongea badaye, na kama ni wewe unahuska na
hayo, kama anavyodai mtoto wangu, tutakosana, na nitakufanyia jambo ambalo hutaweza
kulisahau, nitasahau urafiki wetu wote, na kukuharibia maisha yako,...uombe
mungu kumbukumbu hizo zipatikane, la sivyo na wewe utapotea kama hizo
kumbukumbu...’akasema akiniangalia kwa hasira.
‘Mimi sijui unachokiongea, nitawezaje kuingia kwenye komputa
na kuharibu hizo kumbukumbu, mimi sina ujuzi huo, na hapo huoni ...anayeweza
kufanya hivyo, ni mtoto wako, kwanini umuamini mtoto wako, huoni ni unjana wake, kaamua
kukugeuka,baada ya nyie kukorofishana jana...’nikamweleza nay eye akiwa na
wasiwasi, kwani inaonekana hakutaka huyo mgeni wake anione hapo, akawa
ananisahiria nitoke na mimi nikasema huku natembea kuelekea mlangoni;
‘Mimi nahisi aliyefanya hivyo ni mtoto wako huenda kazificha
hizo kumbukumbu kukukomoa, kwa vile hutaki kukubaliana naye, sasa ananitupia
mimi lawama, ili kutukosanishe, hebu fikiria hilo kwa makini...’nikasema na
yeye akakunja uso kama anawaza, na kuniashiria nitoke humo ndani haraka.
Mimi nikatoka, na wakati natoka, hadi sehemu ya mapokezi ya
ofisi hiyo, huwa mimi nakaa hapo kama kuna wateja maalumu, ila kwa leo
sikutakiwa kukaa hapo, na mara mlango wa chooni ukafunguliwa akatokaa mume wa
familia, hakuniona, kwani alitoka kwa haraka na kuelekea kwenye mlango wa ofisi
ya Makabrasha na kuingia huko.
Mimi nikatoka humo haraka, na kuelekea ofisini
kwangu, ...sikuhitaji silaha kipindi kama hicho, ingenisaidia kama mume wa
familia angesema hataweza kuifanya kazi niliyomuagiza, nilitaka akatae na
kucheleweza kuweka saini kwenye hiyo mikataba, ili niweze kusafisha kila kitu
kwenye kumbukumbu zao, nikawa nimepumzika nikifanya kazi zangu zingine.
Sikuonana na hawo watu, nikawa na kazi zangu zingine za
kiofisi hadi mchana, na muda ukafika wa mimi kuondoka kurudi nyumbani hadi
jioni, nikawasiliana na Makabrasha kwenye simu kuwa mimi natoka, na yeye
akajibu kwa mkatao kwa kusema;
‘Sawa...’ na kabla hajakata simu akasema;
‘Nakuhitajia uwahi hapa jioni, nina mazungumzo na wewe...’akasema
kwa sauti iliyonitia wasiwasi, nikafahamu labda ni kwa vile kakataliwa na mume
wa familia kutii matakwa yake.
Nikaelekea chumbani kwangu ninachojipumzisha, ni chumba
kabisa cha kulala, na kuhakikisha funguo ninazo, nikarudi kidogo nyumbani
kwangu, sikuonana na mume wangu siku hiyo, kama alivyosema ana kazi zake,
nilipumzika nyumbani hadi jioni, na
baadaye nikarudi ofisini kwangu, baada ya kumpigia simu mume wa familia
akaniambia kuwa hawakuafikiana na Makabrasha,kumbe aliweza kufanya kama
nilivyomwambia hawakuelewana kabisa,
kwani Makabrasha alitaka hilo zoezi liishe leo hii, wakapanga waje kukutana
tena jioni, au usiku wa leo, nikaona tena mambo yapo pale pale, nikashukuru
kuwa silaha bado ninayo.
Niliporudi kwenye hilo jengo, nilihisi mwili ukinisisimuka,
sikuelewa ni kwanini, nikawauliza walinzi kama mtoto wa Makabrasha alifika,
wakasema hajafika siku nzima ya leo, nikashukuru mungu, na nilipofika kwa
Makabrasha akawa hayupo sawa, nahisi ni kwa vile mume wa familia alimkatalia
kusaini huo mkataba, na hakutaka kuongea na mimi kama alivyotaka asubuhi. Mimi
sikujali, nikaingia kwenye chumba changu, nikahakikisha ile silaha ipo.
Silaha ilikuwepo pale pale, sikuigusa, maana nilikuwa mikono
mitupu, nilikuwa mwangalifu sana kuigusa ile silaha, nilihakikisha kuwa siigusi
mpaka niwe nimevaa kinga kwenye mikono yangu. Nahisi hapo ndipo nilipofanya makosa,
kwani ukumbuke, kuwa nilishaweka ile mitambo ya kuangalia matukio ya humo
ndani, ON, kuruhusu kuonekana kwa matukio yote kwenye hilo jengo, na wakati
naangalia hiyo silaha, sikujali kujificha, kama nilivyofanya jana.
Ilipofika jioni mambo yakaanza, nikawa napilika pilika za
hapa na pale, na nilitaka nihakikishe kuwa mkataba huo hausainiwi, ...ndilo
lengo langu kubwa kwani yale yaliyokuwa yakitushinikiza nilishayaharibu, labda
wawe na kumbukumbu sehemu nyingine. Nilichokuwa naombea ni kuwa huyo mtoto wa
Makabrasha asionekane leo kabisa, ili niweze kulizuia hilo tendo la kusaini huo
mkataba kabisa. Nikajaribu kumpigia mtoto wa Makabrasha ili kuhakikisha kama
kweli hatakuja, na simu yake ikawa haipatikani,...
Nilipata taarifa kuwa mume wa familia keshafika,ilikuwa
jioni ya kuingia usiku, na nilijua kuwa wapo kwenye maongezi yao na Makabrasha,
na hapo nikataka kuchukua silaha, nitoke nayo, lakini isingeliwezekana kwa vile
mitambo ya kuonyesha matukio ipo ON,...ukitoka nayo tu, ving’ora vya hatari
vitaanza kupiga ukelele, kwahiyo
nilichofanya ni kutoka pale na kwenda kuchukua ufungua za kile chumba cha
mitambo hiyo.
Nilikuwa na ufunguo wa kile chumba, sikuurudisha ofisini kwa
Makabrasha, huo ufungu huo unakaa kwa Makabrasha, lakini niliuchukua siku
kadhaa, nilipomweleza kuwa nataka kufanya usafi , na yeye hakuwa na wasiwasi na
mimi, akanikabidhi.
Nilipofika kwenye hicho chumba, nikaingia na kuweka OFF kuzuia mitambo isione matukio,
nikaingia kwenye komputa na kufuta matukio ya nyuma tangu pale nilipoweka ON, ,..
Halafu nikarudi ofisini kwangu ili niweke mambo safi kabla
sijawaingilia Makabrasha na mume wa familia, ...hapo nilipanga kutumia nguvu,
kuhakikisha kuwa mkataba huo hausainiwi, na kumlazimisha Makabrasha atoe
mikataba yote aliyokuwa nayo, ...Nilishamwambia mume wa familia akiwa anaongea
na Makabrasha ahakikishe simu yake inachukua maelezo yote, na nilitaka wakati
nawavamia niwahi kuchukua ile simu ya Makabrasha anayohifadhi maongezi yake na
watu, ili iwe ni ushahidi.
Yote hayo yataweza kufanyika kiurahisi kama mtoto wa
Makabrasha hatakuja, lakini akifika, itakuwa kazi nzito kidogo, hata hivyo,
nilishapanga nipambane nao, kwani nimeshafanya mengi ambayo yatanifanya mimi na
Makabrasha tusielewane tena, hasa akija mtoto wake, na kumuonyesha kuwa ni mimi
ndiye niliyefuta mambo yake kwenye kumputa ya kuhifadhi uchafu wake, kama
atakuwa na ushahidi wa kufanya hivyo, sikuwa najali tena....
Nikiwa nimetulia ofisini kwangu nikimalizia kazi mbali
mbali, na mara nyingi unapoanza kazi za mahesabu,kuweka kumbukumbu za mahesabu kwenye
komputa, na kutayarisha taarifa mbali
mbali, masaa yanakwenda haraka bila kujua, nikawa nimesahau kabisa wajibu wangu
mwingine. Nikaangalia saa, na kuona nimetumia saa moja na nusu,...nikaacha kila
kitu, na kujiandaa kutoka mle ndani, niende chumbani kwangu ikibidi nikachukue
silaha, ili nikaweza kuwavamia Makabrasha na mume wa familia.
Kwanza nilitaka kuhakikisha kuwa hawo jamaa bado wanaongea,
au ameshaondoka, na kabla sijafanya hivyo kukasikika king’ora cha polisi kwa
mbali, mwanzoni nilijua ni polisi wanapita, lakini kilipofika maeneo ya kwenye jengo
kikasimama hapo, na mimi nikashituka,
kuna nini tena ...
Nilichofanya kwa haraka nikumpigia simu mlinzi kumuuliza
kuna nini, na mlinzi akasema hana uhakika, askari wenzake ndio wamelekea huko
juu. Mimi nikainua simu na kumpigia bosi , yaani Makabrsha, ikawa inalia bika
kupokelewa, nikahisi kuna tatizo. Sikutaka kutoka humo kwa haraka, nikapiga
simu kwa walinzi kama mtoto wa Makabrasha keshafika, huyo mlinzi akasema hana
uhakika, kwani yeye alitoka, na kumuachia mwenzake ulinzi, na huyo mwenzake ameshaondoka.
Baada ya dakika chache, nikapiga simu tena kwa walinzi kuulizia kuna nini, wakaniambia
kuna tatizo kubwa limetokea nani ya ofisi ya Makabrasha, na polisi wameshafika,..
‘Polisi!, tatizo gani la kuwahusisha polisi?, wamekuja kufanya
nini?’ nikauliza maswali mengi kwa haraka bila kujua nauliza nini.
‘Makabrasha kapigwa risasi na hali yake ni mbaya sana, sijui
kama atapona...’akasema huyo mlinzi na aliposema hivyo, kwa haraka nikajua ni
mume wa familia kafanya hivyo, lakini kwa silaha gani, kwani sizani kama
angeliweza kuingia na silaha pale mlangoni, japokuwa nilikuwa nimezima kiwambo
cha kuhisi hatari.
‘Na nani, mbona muda mfupi uliopita nilikuwa nikiongea naye,
haiwezekani..ngoja nikahakikishe....’nikasema na kutoka kwenye ofisi yangu, ili
kama mume wa familia yupo hapo niweza kutoa msaada,lakini nilikuwa nimechelewa,
kwani nilipotoa kichwa kuangalia kwenye korido, nikawaona maaskari.
Kumbe maaskari walishafika, nikarudi ofisini kwangu kwa
haraka kabla hawajaniona,na kujifungia, sikutoka kabisa, na sikutaka kufanya
lolote maana sikujua nikikutana na hao polisi nitasema nini, na cha ajabu, siku
hiyo hakuna polisi aliyekuja kunihoji. Nilisikia wakisema wameshamshika
muaaji,...yaani mke wa familia.
‘Mke wa familia, alikuja muda gani?’ nikauliza, na walinzi
wakasema alifika hapo akitaka kuonana na Makabrasha, na polisi wameshamshika,
yupo chini ya ulinzi.
‘Je yule mgeni wa Makabrasha wa mwanzo aliondoka muda gani?’
nikauliza.
‘Aliondoka, muda na baadaye ikagundulikana kuwa Makabrasha
amepigwa risasi...’akasema.
‘Ni nani aligundua hilo?’ nikauliza.
‘Hatujui, hata sisi tuliona ajabu, maana hakuna mlio wowote
wa hatari uliosikika, ina maana mitambo huko juu haifanyi kazi?’ akawa kama
ananiuliza na mimi hapo nikaanza kuingiwa na wasiwasi, maana ni mimi niliyezima
hiyo mitambo, ina maana moja kwa moja nitashikwa kwa kuhusika na mauaji hayo,
hapo nikawa na wakati mgumu.
Nikatafuta upenyo, hadi nikaupata nikatoka pale haraka
na kwenda chumba cha mitambo kwa haraka nikaweka ON, japokuwa nilijua kuwa
nimeshachelewa, na kwa haraka nikarudi ofisini kwangu, na kutulia kuwasubiri
polisi wakija kunihoji, lakini hilo halikutokea kabisa siku hiyo.
Siku hiyo nikiwa nimejifungia humo ndani nilikuwa
nikimuwazia Makabrasha, sikuamini kuwa atakufa, kwa jinsi nilivyomfahamu na
tambo zake, hata hivyo, kuna muda nilijikuta nikimuwazia kuwa huenda atakuwa
ameshakufa kama alipigwa risasi, na sijui ni sehemu gani....
Unafahamu mtu hata awe mbaya vipi, linapomfika jambo kama
hilo, la ugonjwa au umauti, hata kama ni ugonjwa tu, ila unahisi hataweza
kupona, unaingiwa na moyo wa huruma, ukizingatia kuwa mimi nilikuwa mtu wake wa
karibu, japo sikupenda iwe hivyo, japokuwa nilikuwa na kisasi naye, na chuki
iliyopitiliza kwa hayo aliyonifanyia, lakini sikuwa na dhamira ya kumuua.
Nilishangaa, kwani mambo yalikwenda harakaharaka, na
Makabrasha akakimbizwa hospitalini, na baadaye tukapata taarifa kuwa Makabrasha
hatunaye duniani. Kafariki kwa risasi, na ilikuja kugundulikana kuwa risasi na
bunduki, bastola iliyotumika kumuua Makabrasha ni ile niliyoletewa, sikujua ni
nani aliyeweza kuingia chumbani kwangu na kuiiba, na alijuaje kuwa nina
bastola!
Hapo shahidi akatulia kidogo, na mwenyekiti akamwangalia
shahidi kwa mashaka, na kumuuliza;
‘Hapo kwakweli sisi hatukuelewi, Ina maana unataka kutuambia
kuwa sio wewe uliyemuua Makabrasha,
ukishirikiana na mpenzi wako wa zamani kutokana na maelezo yako uliyoyuambia?’
akaulizwa
‘Nakumbuka, tangu mwanzo, kabla sijaongea mimi, wewe ulikuwa
ukiamini kuwa aliyefanya hivyo ni mume wa familia na mdogo wake, au sio , sasa
iweje unishuku mimi, kwa vile nimeelezea huo ukweli, ndio maana nilikuwa nasita
kusema huo kweli jinsi ilivyokuwa, ina maana kufanya hivyo nimefanya makosa?’
akauliza
‘Kutokana na maelezo yako toka mwanzo, inaonyesha ni wewe,
kwasababu silaha iliyotumika kumuua Makabrasha ulikuwa nayo wewe hadi hatua ya
mwisho, na wewe ndiye uliyafahamu wapi silaha hiyo ipo, sasa unaposema wewe
haukuwepo kipindi Makabrasha anauwawa, tunaona kama unaficha ukweli...’akasema
mwenyekiti.
‘Hivyo ndivyo ilivyokuwa, huo ndio ukweli, wa siku
hiyo,...kama mliambiwa vinginevyo ni uwongo, maana mimi nilikuwepo humo ndani,
tatizo, ni kuwa, kile kifaa cha kuchukulia kumbukumbu za matukio kilichokuwepo,
nilikuwa nimekiweka OFF, ni kweli ni mimi ndiye niliyekiweka hivyo, kwahiyo tukio zima,
halikuonekana...’akasema.
‘Huoni kuwa polisi watajua kuwa wewe ulifanya hivyo makusudi
ili ufanye mauaji na kusiwe an ushahidi au sio?’ akauliza mwenyekiti.
‘Baada ya kufikiri sana na kupata taabu ya kuwazia hilo
tukio lilivyokuwa, nikaona ni bora niseme huo ukweli ulivyokuwa, lakini nikijua
kabisa, nikielezea huo ukweli kwa yoyote vile , achilia mbali polisi,yoyote
nitakayemuelezea jinsi ilivyokuwa hataamini kuwa sio mimi niliyemuua Makabrasha,
....lakini huo ndio ukweli, hivyo ndivyo ilivyokuwa, kwa utata huo nikaamua
kukaa kimiya na nilichofanya nikwenda kukaa huko kijijini.
‘Mhh, mimi sijui, lakini nionavyo mimi polisi wakisikia hayo
maelezo yako , moja kwa moja wewe utakuwa mshukiwa namba moja, na sijui kwanini
mpaka leo hawajakukamata, ina maana hukuwahi kuongea nao?’ akaniuliza.
‘Nimeshaongea nao, lakini nilijua jinsi gani ya kuwaambia,
na hawakuwa na ujanja wa kunikamata, ila kiuhakika, itafika siku watanikamata ,
kama sio leo, ...siku yoyote watanikamata, lakini kwanini niendelee kujificha,
ukweli ndio huo...’akasema.
Mwenyekiti akaangalia saa yake, na alionekana na maswali
mengi ya kumuuliza huyo shahidi, lakini kabla hajamuuliza huyo shahidi, huyo shahidi akasema;
‘Mimi imenichukua muda kuliwaza hilo, lakini moyo unanisuta, na kila
nikiwaza sana naona sijatenda uadilifu, na watu wengine wanakamatwa ovyo, wakishukiwa
kwa hayo mauaji, na imekwenda, nona kama inafifia, ukweli unaanza kubatilishwa,
na kuna watu wengine, wanatarajiwa kukamatwa, hasa mume wa familia na mdogo wake, nikaona sasa inapokwenda ni kubaya, ni bora nijitokeze mimi mwenyewe niseme ukweli,
hata hivyo ni nani nitamwambia huo ukweli aniamini, kwenda polisi ni kama
kwenda kujifunga mwenyewe...'akasema.
'Kwahiyo umeamua kujitokeza kwa vile sasa inaelekea kumgusa mpenzi wako wa asili?' akauliza mwenye huku akitabsamu kwa utani.
'Hapana, ....mimi kama mpelelezi, hilo nilikuwa nalifanyia kazi, nilikuwa kwenye uchunguzi binafasi, kumjua ni nani hasa alifanya hayo mauaji, maana nashindwa kujua, mtoto wa Makabrasha, hakuonekana siku hiyo, na asingeliweza kumuua baba yake, ...unaona hilo...'akatulia kidogo, halafu akasema;
'Kiufupi, sikutaka kusema huo ukweli, kabla sijamaliza uchunguzi wangu, ila ninachotaka kuwaambia
hapa ni hivi, ...mimi sijamuua Makabrasha...na sikuwa na mipango hiyo, mimi
nilikuwa na mipango yangu mingine kabisa ya kumnasa huyo mtu na kumfikisha kwenye vyombo vya dola, na iwe mwisho wa mtandao wake....’akasema
‘Sasa kama sio wewe ni nani aliyemuua Makabrasha?’ akauliza
mwenyekiti.
‘Kama mtaniruhusu ninaweza kuongea nionavyo mimi,kutokana na uchunguzi wangu, lakini hamuoni kuwa hayo
ni maswala ya polisi, ambayo hayahusu hiki kikao?’ akauliza na mwenyekiti
akakaa kimiya kwa muda. Baadaye akachukua simu yake akitaka kupiga , huku
akimwangalia huyo shahidi, na shahidi akageuka nyuma kuangalia mlangoni, kama
anataka kukimbia.
NB: Ni nini kitaendelea.
WAZO LA LEO: Sio
vyema kuwa na silaha za moto kwenye majumba yetu, kama bastola na bunduki, na
kama ni lazima, kutokana na maisha yetu, tujitahidi sana kuwa na tahadhari na
silaha hizo, tuhakikishe kuwa sehemu tunaziweka silaha hizo ni sehemu za siri
na iwe unaifahamu wewe mwenyewe kama neno lako la siri. Wakati mwingine, kuwa
na silaha za moto ndani ni kama kufuga nyoka mwenye sumu. Tuwe makini.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment