Niliwasiliana na mdogo wa mume wa familia, na akaniambia
keshapewa ufungua na kaka yake na yupo njiani kwenda kuichukua hiyo silaha,
kilichofanyika ni kutafuta mbinu za kumtoa mke wa familia eneo la nyumbani
kwake na hiyo ilikuwa ni kazi rahisi tu, kwani mke wa familia hakuwa anafahamu
ni nini kinaendelea kwahiyo hakuwa na wasiwasi wowote, ukumbuke wakati huo,
mume wa familia bado yupo hospitalini anaigiza kuumwa.
Kilichofanyika ni mume wa familia kuigiza kuzidiwa, na
wakati huo akawa anataka kuongea na mkewe, kwahiyo docta ikabidi ampigie mke wa
familia simu kutoka hospitalini kuwa mume wa familia,kazidiwa ghafla, na anataak
kuongea na y eye. Ni kawaida kwa
mwanandoa akisikia mwenzake kazidiwa, hutalala, utahitaji kuja kumuona, na
ndivyo ilivyotokea, mke wa familia akaenda kumuona mume wake, na alipofika huko
ikatafutwa njia ya kumchelewesha hadi mdogo wa mume wa familia aliweza
kuichukua hiyo silaha.
Ilipoletwa .
Kwa upande wangu mimi nilishajiandaa, nilishaweka kamba ndefu,
inayofika chini, ujue lile jengo lina rosheni,lakini kwa ajili ya kuiingiza hiyo
silaha ndani, nilitumia rosheni ya pili, na jinsi ya kuifikisha kwenye chumba
changu, nilitumia njia zangu nyingine, cha muhimu ilikuwa kuhakikisha kuwa
mitambo ya kutizama matukio ilikuwa imezimwa, ..nilifanya hivyo nikiwa na
uhakika kuwa mtoto wa Makabrasha hayupo.
Nikaichukua ile silaha na kuificha chumbani kwangu, kwani
haikutakiwa kuwa mbali na mimi ili nikiihitaji nisipate taabu, nilihakikisha
kuwa hayo yote niliyafanya kwa ujanja wa hali ya juu, kiasi kwamba , hata kama
watakuwa wakinichunguza nyendo zangu kwenye mitandao yao wasifahamu kuwa nina
kitu kama hicho halafu nikatoka kwenda kuendelea na shughuli zangu, wakati
natoka, nikakutana na mtoto wa Makabrasha.
‘Mbona sipati ishara ya mawasiliano kutoka hapa, ni nani
kazima mitambo ya usalama wa jengo ?’ akaniuliza akionyesha wasiwasi
‘Mitambo ya usalama wa jengo, ipo wapi hiyo...aah, mimi
sijui mambo yenu na wala sijui kama imezimwa, na kwanini izimwe!?’ nikamuuliza
kwa mshangao, na yeye akaniangalia kwa mashaka, halafu akageuka kuelekea kwenye chumba cha mitambo hiyo ilipo
na mimi nikamfuatilia kwa nyuma kiujanja, hakujua kuwa nipo nyuma yake, mawazo
yake yalikuwa kwenye hilo jambo analilifuatilia.
Akafika na kufungua mlango, akaingia ndani, na mimi kwa
haraka nikaingia, chumba kilikuwa giza, ila kwa mngurumo wa hiyo mitambo, na
kulikuwa baridi sana....hakugeuka nyuma, akawasha sehemu ambayo mimi nilizima,
halafu akasogea kwenye meza yenye komputa, akaiwasha na kukagua kitu, akawa
anaangalia ni nani aliyekaribia hicho chumba, ni wazi kuwa ningelionekana mimi, sikuwa
nafahamu jinsi gani ya kufuta matukio ya nyuma yake, akaiweka ile komputa sawa
na kugeuka kuondoka, na ndio akaniona nimesimama nyuma yake. Akashituka na
kuniangalia akiwa kakunja uso.
‘Oh, wewe mtu, unakuwa kama mzimu, yaani ulikuwa
ukinifuatilia nyuma, huku nilishawaambia hatakiwi watu kuingia huku, niambie
umefuata nini, na inaonyesha wewe ndiye uliyefika huku, ...?’akasema kwa
hasira.
‘Baba yako alinituma kufanya usafi...kwani kuna wagen muhimu
alitarajia kuwa watakuja kumtembelea...’nikasema lakini nilifahamu kabisa kuwa
kama ni usafi, huwa eneo hilo sijawahi kufika kufanya usafi na, yeye akasema;
‘Hata kama ni usafi, toka lini ukaja kufanya usafi eneo hili,
wakati mimi sipo, haiwezekani, na hata kama ulifanya usafi kwanini ukazima
mtambo mkubwa, ?’ akaniuliza kwa mashaka.
‘Niliona kuwa eneo hili ni chafu, ndio nikaja kulifanyia
usafi, ...na sijui kama nilizima, ndio kuna wakati nadeki, nikaona nisije
nikarushwa mimi nikazima, nikijua kuwa ni swichi ya umeme, ....mimi mambo yenu
hayo siyajui’nikasema
‘Ni nani alikupa ufungua wa chumba hiki?’ akaniuliza
‘Unauliza jibu, ninapotaka kufanya usafi, nilishawahi kuja
kwako kukuuliza ufunguo, mimi ninafahamu wapi funguo zote zipo, kwanini
unaniuliza maswali mengi, mbona siku nyingine hujawahi kuniuliza, kwani ni mara
ya kwanza kuja kufanya usafi hapa, na kwanini huendi kumuuliza baba yako, kama
una wasiwasi na mimi, mbona unaniwekea vikwazao visivyo na msingi..mzee wako
ananiamini ndio maana kaniajiri niwe karibu naye.’nikamwambia.
‘Leo iwe ni mwisho kuingia kwenye chumba hiki, tatizo ni
kuwa umezima mtambio mkubwa ambao unafanya tusiwe na mawasiliano tukiwa nje, na
hili nahisi umelifanya makusudi....’akaniambia na mimi nikatabasamu kumlegezea,
nilishafahamu uzaifu wao, mtoto kama baba, akategeka, na kunisogelea, huku
akisema;
‘Tatizo lako wewe kwasababu ya tabia yako unahisi kila mtu
ni kama wewe....’nikasema huku nikijerembua. Wakati mwingine ukiwa katika kazi
kama yangu inabidi utumie kila mbinu, lakini akili kichwani mwako. Na
alipoliona lile jicho, mtoto kama baba, akasawajika, nikamuona mate yakimtoka,
akasahahu alichokuwa akiniuliza mara akasema;
‘Kwanza nikulize lile
ombi langu vipi,..?’ akanisogelea baada ya kuzima kitu kwenye mitambi, sikujua
ni kwanini, na akanisogelea kujaribu kunishika na mimi nikasogea pembeni na
kusema;
‘Ombi lako lipi, ooh, na wewe bwana, kwanini unakuwa na
tabia mbaya, nilishakuambia upuuzi kama huo, siutaki, msinione nipo humu ndani
mkafikiria mimi ni Malaya, kwanza kuhusu huo upuuzi wako nitamuuliza baba
yako...kama yupo tayari kuchangia na mtoto wake...haya,’nikasema na yeye
akageuka kuondoka, na kusema;
‘Hivi wewe baba unamuona mtu wa maana kwako, ombi langu
kwako ni siri yangu mimi na wewe, eti ukamuulize baba, unataka nilaaniwe
nini....wewe jivunge tu, ipo siku utaingia kwenye anga zangu, unafikiri mzee
yule atakuwa na wewe milele, akikuchoka anakutupa chini, wangapi walikuwa naye
sasa hawatakiw hata kumsogelea, ...wewe jidanganye kwake, ukifikiria umefika....’akasema.
‘Kama alivyofanywa mama yako au sio, hata hivyo mimi sijawahi kukuambia kuwa nina haja na baba
yako, ...baba yako ndiye kanilazimsiha kuja kwa ajili ya mambo yake, mimi nina
mume wangu, nina maisha yangu mazuri tu, na mume wangu nampenda, kama
isingelikuwa haya mambo yenu unafikiri ningelikuwa hapa, na ipo siku mtajuta
kwa hayo mnayoyafanyia....’nikamwambia.
‘Hayo unayafanyiwa ni yenu na baba, mimi siyajui, ...na
vitisho vyako, kwangu havina nafasi, nafahamu ni nini ninachokifanya kwa nafasi
gani, usinitishe kabisa, mimi ninafahamu sheria, na sijawahi kukulazimisha kwa
lolote lile, na hata hivyo ombi langu lipo pale pale, usiponinitimizia najua
jinsi gani ya kukupata...’akaniambia
‘Utafanya nini...?’ nikamuuliza
‘Siri zako zote anazozitumia baba kwa ajili ya kukupata wewe
ninazo mimi, zipo kwenye mtandao, yeye akizihitajia mpaka aingie kwenye
mtandao, na mimi ndiye nimezihifadhi, sasa utanidanganay nini, nikiamua
kuzitumia dhidi yako, siutaumbuka wewe...sasa uamue moja kuwa na mimi au na
baba..’akasema.
‘Nakuambia hivi ni bora umenifahamisha hayo, nitamuambia
baba yako hizo mbinu zako, kama atasema yupo tayari kuchangia na mtoto wake,
mimi sina hiana, mimi hapa ni mtumwa wake....’nikamwambia.
‘Hivi wewe una akili kweli,...kila kitu utamwambia baba, ole
wako umwambie....’akasema
‘Sasa tuelewane, ili nisimwambia unifundishe jinsi gani ya
kutumia huo mtandao, jinsi ya kutengeneza picha na kuziweka kwenye huo
mtandao..’nikamwambia.
‘Unataka nikifundishe ili uje uzifute, ..hilo umenoa..lakini
naweza kukufundisha kama utanikubalia maombi yangu...kama upo tayari, tuonane
usiku wa leo, nitakuja, nitakufundisha lakini malipo yake ni ...maombi yangu...na
safari hii sikubali, kama ulivyonidanganya siku ile, nikija ..nikakufundisha,
ni lazima utimize maombi yangu, la sivyo, na mimi nitaweza kukufanyia kitu ambacho
hutaweza kunisahau....ujue na mimi ni wakili kama baba’akasema na mimi
sikumjibu, nikaondoka, huku moyoni nikiwa nimeshajiweka katika nafasi nzuri.
Yeye akarudi kwenye mtandao, na kuwasha kitu alichokuwa
amekizima awali, na akawa anafuta matukio yasiyo muhimu,...nikawa namwangalia,
wakati huo alikuwa hanijali tena, alipomaliza akanigeukia na kuniuliza
ninasubiri nini
‘Nakusubiri wewe bosi kama kuna kazi ya kufanya, ...’nikasema
‘Ishia huko kaendelee na kazi zako, tutaonana baadaye ...’akasema
na kuondoka.
Mimi nina akili za
ajabu sana, ukinionyesha kitu, au nikaona unavyofanya, akili yangu hunasa
haraka sana, nilishaona jisni anavyoweka neno lake la siri, nikalinasa bila ya
hata ya yeye kujua, nilijifanya sijui lolote kuhusu kmputa na mitandao, na neno
hilo la siri nililigundua siku moja wakati anahangaika kunibembeleza nimkubalia
matakwa yake...hapo hapo nikatumia ujanja kumuomba anifundishe jinsi jengo hilo
lilivyo, maana ni jengo kubwa, na ndio siku hiyo nikagundua kuwa kumbe jengo
hilo lina sehemu ya chini ya ardhi, ...
Usiku wake, nilitaka niingie kwenye hiyo mitambo, kwani ndio
siku peke yake ningeliweza kufanya jambo, nilichofanya ni kuchelewesha kununua
mafuta ya genetaror, nilijua mara kwa mra umeme unakatika, na mimi ndiye
niliyekuwa nahifadhi fedha za matumizi madogo madogo ya ofisi, na nilitakiwa
kuhakikisha mafuta ya genetor yapo,
Nilijua ikifika saa tatu, mafuta yatakuwa yamekwisha, na
siku hiyo umeme ulikuwa hakuna, huku nikiomba huyo mtoto wa huyo jamaa hafiki, au anachelewa, nilishangaa
kweli siku hiyo kwani mpaka saa tatu alikuwa hajafika,....mara genetaror
likazima, kukawa kizaa, zaa, giza, nilijua kwa jinsi ili mitambo ilivyo ikifika
nusu saa itakuwa imezima, hapo nikajichelewesha kufuatilia, hadi nusu saa
ikapita, ndio nikajitokeza
‘Mbona generator limezima,
hujanunua mafuta..’akaniuliza Makabrasha
‘Naona nimepitiwa mambo yamekuwa mengi, ...nimemtuma mlinzi
akanunue...’nikasema
‘Huo ni uzembe, unafahamu umuhimu wa umeme kwenye hikli
jengo, huoni watu wabaya wanaweza kutumia mwanya huu kufanya lolote...’akasema
na mimi nikaachana naye na kukimbilia kwenye hicho chumba. Kama nilivyojua,
sehemu ile ya kuangalia matukio ya jengo ilikuwa imeshazima, kwa haraka
nikakimbilia kwenye ile komputa inayohifadhi matukio na kumbukumbu mbali mbali, ilikuwa bado
inafanya kazi, nikaingia sehemu ninayoitaka
Ilichukua muda kidogo kupata kumbukumbu ninazozitaka, ....nilikuta
kumbukumbu nyingi za watu mbali mbali, ambazo kama zingeliwekwa hewani,
nafikiri watu wengi wangeliumbuka, sikutaka kuangalia zaidi, kwani mambo
niliyoyaona humo yanatisha,mimi nikazifutilia mbali, na kuhakikisha hazipo
kwenye sehemu ya mabaki ya vitu vilivyofutwa, nikaangalia sehemu inayoangalia
matukio ya jengo hadi umeme ulipozimika, nikazifuta.
Nikaenda sehemu wanapohifadhia picha za video ambazo zilikuwa zinaonyesha mtu aliyefika
kwenye hicho chumba karibu, nikajiona ni mimi peke yangu nikaifuta hiyo
kumbukumbu, halafu nikatafuta sehemu ya kuzuia kamera za humo ndani zisichukue
matukio hadi itakapokubaliwa tena ,nikaiweka OFF, ina maana kuanzia hapo hadi hapo mtu mwingine
atakapokuja kuikubali kuonyesha matukio, kutakuwa hakuna kitu
kitakachoonyeshwa, nilipoamaliza nikatoka kwa haraka, na wakati natoka tu, genetaror likaanza kunguruma na umeme
ukarudi.
‘Ulikuwa wapi wewe nakutafuta sehemu zote,..naona mitambo ya
usalama humu ndani imezima, sio kawaida, hata umeme ukizimika inaweza kuhimili
hata saa nzima, ..kuna tatizo,....’akasema Makabrasha huku akielekea kwenye
chumba cha usalama, lakini baadaye akatoka huku akiongea peke yake.
‘Naona kuna tatizo kwenye mitambo ya usalama, ..siwezi
kuingia kwenye komputa ya usalama, sijui huyu mtoto kafanya kitu
gani,..kabadilisha neno la siri...’akawa anaongea huku akinipita na mimi nikamwambia.
‘Mimi sijui, lakini tunaweza kujaribu pamoja huenda
tukagundua jinsi gani ya kuingia, tukiwa wawili?’ nikamuuliza
‘Hio haikuhusu, ngoja nimpigie simu huyu mwanangu, japokuwa
tumekorofishana, lakini hili ni muhimu, ni lazima afike, nahisi kuna tatizo ,
nahisi ....akili inaniashiria kuna tatizo,..toka jana nilipoanza kukorofishana na huyu kijana,
nimehisi kuna kitu ambachp sio cha kawaida, jana kaondoka kwa mihasira, na ndio
maana hajafika mpaka muda huu..’akasema
‘Mumekorofishana nini tena na mtoto wako kipenzi?’ nikamuuliza
‘Unafahamu hawa vijana wana tamaa sana, wao wakiona kitu kipo,
hawajiulizi kimefika fikaje hadi hatua hiyo, hawafahamu kuwa sisi wazazi wao tumetumia miaka mingi
kujenga hicho walichokikuta, wao wanataka kupata kwa muda mfupi,...hata kama ni ujenzi ukiutaka uumalize kwe muda mfupi, utakuwa
hauna imara,..inahiatji muda,...tatizo kubwa yeye hajui mipangilio yangu ipoje...’akasema
akiwa kasimama karibu yangu.
‘Kwani yeye anataka nini?’ nikamuuliza na akataka kuondoka,
lakini akageuka na kuniangalia, akasema;
‘Huyu kijana analalamika, kwanini mwanangu huyu anayeishi
huko nje, ninamjali eti kuliko yeye, na kumfanya mrithi wa kwanza, kama mktaba
unavyosema, eti yeye anaona hilo sio sahihi, anataka mimi nikifa yeye ndiye
ashikilie nafasi yangu, awe ndiye kiongozi wa familia, sio huyo kaka yao
aliyepo nje, huyu ana akili kweli, hajui yule ana haki zote kuliko yeye, ...’akasema
‘Lakini hata ingelikuwa mimi ningdai hivyo hivyo, kwasababu
huyo kaka yao yupo nje, hajui chochote kinachoendelea hapa, na nakumbuka
uliwahi kuniambia huyo mtoto wako wa Ulaya hampatani, na aliondoka na kukuambia
hana haja na mali yako ..sasa kwanini unajipendekeza kwake....?’ nikamuuliza
‘Wewe hujui mambo ya wazazi na watoto, hata kama mtoto
hampatani kwasababu kadhaa, lakini yeye atabakia kuwa mtoto wangu wa kwanza, na
yeye nilimzaa na mke wangu wa ndoa, ana haki zote. Huyu niliye naye hapa
nimemzaa kwenye nyumba ndogo,..nilimsomesha na kumuandikisha kama watoto wangu
wengine, na nimeona anastahili kuwa karibu na mimi, na ndio maana nimemuweka nafasi ya pili,
atakuwa chini ya huyo kaka yao anayeishi huko Ulaya, kuna tatizo gani
hapo....’akasema.
‘Kwahiyo wewe na mtoto wako mkaishia wapi?’nikamuuliza
‘Yeye alikuja na mipango yake, uone jinsi mtoto huyu alivyo
balaa, kakaa sijui na mama yake, wakapanga mambo mengi tu, jinsi ya kugawanya
mali eti keshaandaa na mikataba ya
kifamilia, kama vile mimi ninakufa karibuni, kwenye mikatba hiyo, ambayo ni
kama urithi, , ...na yeye awe ni mrithi wangu , yaani kiongozi wa familia, mimi
nikifa...hana akili kabisa, nimemwambia huo uchuro siutaki, kama ni mikataba ya
urithi, mimi nimeshaupanga na ninafahamu ni nani awe kiongozi wa familia, kama
mimi nikifa..lakini sijafa, na sitaraji kufa leo...siumwi,, sina tatizo la
kiafya..kwanini anakuja na mipango hiyo, wana matatizo sana hawa watu....’akasema
akijiangalia.
‘Lakini kufa sio lazima
uumwe, wewe kama ulivyo, kutokana na mambo yako unayoyafanya,una maadui kila
kona, wakija kuku-ua, watu,....’nikasema
‘Kweli hilo ni la kuangalia sana, ndio maana umeme
ulipozimika, nimeshituka sana, sitaki uzembe huu utokee tena, ...unanisikia,
....sasa nisikilize kwa makini, kesh o huyu mpenzi wako anakuja, ...’akasema
‘Mpenzi wangu gani, mimi ni mke wa mtu.?’ Nikamuuliza
‘Hebu acha utoto, nikisema mpenzi unanielewa ni nani,
..nimeshamweka sawa anakuja kuweka sahihi yake kwenye hiyo mikataba ambayo itanifanya
mimi, niwe na haki ya kumiliki, hisa kwenye makampuni yao, kilaini
kabisa....kwahiyo wewe na wenzako mlitambue hilo, ...na tatizo ni huyu mtoto
wangu anakuja na sera zake za ajabu ajabu, anataka na yeye awe na hisa,...anataka
kunikorofisha,...’akasema kwa hasira
‘Mimi ninawashangaa kweli kweli, yaani mumeshaanza kugombea
mali za watu, hata kabla hamjazipata, mumeshaanza kumiliki hata kabla
humajamilikishwa, kweli akili zenu wote ni za
kishetani wewe na mtoto wako, na
mimi nahisi hamtafanikiwa kwa hilo, na mkifanikiwa mtakuja kupigana baba na
mtoto wake....’nikasema
‘Kama mimi nipo hai, hakuna cha mtoto wala mama yao
atakyeweza kunitawala, mimi ndiye mwenye amri, wote wanalifahamu hilo, najua
kabisa huyo mtoto anaendeshwa na mama yake, na mama yake nilishamwambia
simtambui tena, tulishamalizana na yeye zamani, hana nafasi kwangu tena...hatukuwahi
kufunga ndoa na yeye, alikuwa mpenzi wangu wa kupita tu, nikampa mimba ndio
akapatikana huyo kichaa.’akasema kwa
hasira.
‘Aaah, kumbe, una wangapi, huyo alikuwa mpenzi wako wa
zamani, nahisi wapo wengi wa namna hiyo, huyo wakati huo ulimuona mpenzi, sasa
hafai, au ni kwa vile kazeeka,au?’nikamuuliza
‘Namfahamu sana huyo mwanamke, ana tamaa sana, hatuivani
kabisa, na mtoto wake kachukua tabia zake zote, na kama ataendelea na hiyo
tabia sizani kama tutaivana, na...namuona atakuwa kikwazo katika mipangilio yangu ya kimaisha
kinyume na nilivyotarajia...’ akatikisa kichwa kusikitika halafu akaendelea
kusema;
‘Sijui kwanini hanisikilizi mimi, na anakuwa akimsikiliza
sana mama yake, ujue huyu mtoto mimi ndiye nimefundisha ujanja wa kimaisha , alipomaliza
kisomo chake akataka kufanya kama alivyosoma, nikamwambia dunia hii, ina
utaratibu, lakini ndani ya hizo taratibu kuna njia za mikato, uking’ang’ania,
njia hiyo hiyo, utasubiri wee, na hutaweza kufika kwa wakati muafaka, wakati
mwingine, unakatisha njia,...nikamfunza jinsi gani ya kuitumia elimu yake kutafuta
maendeleo mpaka akaiva, sasa namuona ananipanda kichwani...’akasema huku
akikunja uso kwa hasira.
‘Kwahiyo sasa mtoto kama baba yake...au kama wanavyosema mtoto wa nyoka ni nyoka’nikasema kwa dharau
huku nikijifanya kutabasamu .
‘Huyo haniwezi kabisa na hataweza kunifikia mimi, yeye
anachukulia mambo kwa pupa, mimi natumia ujanja, hekima na akili, ndio maana
unaona nimefanikiwa kwa kiasi hiki kikubwa, unaona jumba hili, ni nani anaweza
kujua nimelijnga vipi,..ni akili, ..usione watu wana majumba, utajiri,
ukfikiria ni kirahisi hivyo, ni kutumia akili, ujanja...ndio hivyo, wewe zubaa
tu,...’akashika kichwa kwa kidole chake huku akiangalia juu, kama vile
anaangalia hilo jengo.
‘Kwahiyo yote hayo umemfundisha mtoto wako?’ nikamuuliza
‘Tatizo yeye hataki kutliza kichwa, yeye anataka mambo kwa
pupa, ana tamaa za haraka, hata sijui kwanini ameweza kufaulu masom o yake ya
uanasheria, kazi hii hataiweza kama atakuwa na tabia ya namna hiyo, ya pupa, na
ninavyomuona hatafika mbali, hebu angalia, anataka kunirithi nikiwa hai...sijui
kwa hali kama hiyo, tunaweza kukaa pamoja,....lakini mimi kama baba,
nitamdhibiti tu, ninamfahamu vyema na wapi pa kumnasa, hana ujanja mbele yangu,
hanijui akili zangu zilivyo...’akasema.
Na mara simu yake ikalia, akaipokea bila kuiangalia, na mara
akakunja sura ya uso wake na kuonekana kukasirika, akasema kwa sauti ya
iliyojaa hasira;
‘Kwanini unasema hutafika leo, wakati unafahamu umuhimu wa
wewe kuwepo leo, nataka uje hapa haraka,...kwanza kuna matatizo kwenye mitambo
ya usalama, na pia ni wajibu wako kuwepo hapa, ili tukamilishe kazi , achana na
tamaa zako hizo, nasema mimi kama baba uje hapa haraka,.....’akasema
‘Unasema nini, unanijibu mimi hivyo, kuwa hutafika,mpaka
nikubaliane na matakwa yako, ina maana unanilazimisha kufanya unavyotaka wewe,
hivi unaelewa unaongea na nani...unasema nini, ina maana umeshaota mapembe sasa
eeh,...’akawa anaongea huku mwenzako huko anaongea, na mwisho akasema;
‘Sikiliza wewe mtoto, kama nimekuzaa mimi, utakuja hapa,
kama una baba yako mwingine usije , usijione kuwa umekuwa sasa,...na kujiona
hunihitaji tena, hujui ninaweza kukufanya
lolote ukasahaulika katika hii dunia..’akasema na kusikiliza simu kwa muda
halafu akaibamiza simu chini , na simu hiyo ikapasuka vipande vipande, na
kusema;
‘Mwanaharamu mkubwa wewe...tutaona,....’akageuka na kuelekea
ofisini kwake, ukumbuke hapo tulikuwa tunaongea kwenye varanda, na mimi
nikachekelea kimoyo moyo, na kurudi chumbani kwangu, sikutaka kumfuata ofisini
kwake, kwani nilijua kwa hali aliyonayo hatutaweza kusikilizana.
Mimi kwa hali kama hiyo , ilikuwa kama vita vya kunguru,
faraja kwangu, kmoyomoyo nikijua sasa sehemu muhimu imekamilika, japokuwa
sikuwa nimeamini kabia kuwa huyo mtoto wa marehemu hatafika, namfahamu sana,
yeye na baba yake hawaeleweki, wao ni waarabu wa pemba, wanajua sana, kwahiyo
nikachukua tahadhari,..
Nilikwenda kuongea na mlinzi mmoja ninayemuamini ,
nikamwambia , kama huyo mtoto wa bosi akija , anipigie simu kwa haraka,...kwani
sehemu kubwa ya mitambo ya kunasa matukio ilikuwa haichukui picha, kwahiyo
ningeliweza kufanya lolote bila kujulikana, kwa kiasi fulani nilikuwa na amani
kidogo, nikasuburia muda muafaka, wa kumalizia kazi ambayo nilishaianza.
Nilikuwa najiamini maana sasa nina silaha, na nikiwa tayari , au nikisikia kuwa huyo
jamaa kafika nitakwenda kuichukua, sikuwa na haraka nayo sana, nikatembea
kuelekea ofisi ya siri ya Makabrasha,
nikafungua, na kulitafuta kabati maalumu anapoweka nyaraka zake, nikachukua
kile ninachokihitajia, na kurudi chumbani kwangu.
Kabla sijafika huko nikakumbuka kazi nyingine ya kufanya,
kwani siku hiyo niliipanga iwe siku ya mwisho ya kukaa kwenye hilo jengo,
nikaelekea sehemu ninapoweka vitu vyangu muhimu ambavyo nimevihifadhi mbali na
chumba changu, sikutaka waje wavikute chumbani kwangu, kama ikitokea
kuvitafuta, nikaviweka sawa, halafu nikarudi chumbani kwangu,sasa nikijiandaa kwenda
kuichukua silaha yangu, sikutaka iwe mbali na mimi na wakati nafika chumbani
kwangu, simu yangu ikaita, alikuwa mtoto wa Makabrasha,
‘Unasemaje?’ nikamuuliza kwa sauti isiyotaka kuongea,
‘Samahani sitaweza kufika kwenye shule niliyokuahidi, lakini
ombi langu lipo palepale,na kwanini mitambo hapo haifanyi kazi, ...umeingia tena humo ndani?’akasema na
kuniuliza
‘Umesema hutakuja, ina maana mkataba huo umekufa, labda
useme kuna jingine..na kuhusu swala la mitambo hayo unayafahamu wewe, wewe ndio
mtaalamu, huenda ulifanya hivyo makusdi kumuonyesha baba yako kuwa wewe ni
zaidi au..?’nikasema kama namuuliza
‘Wewe nimeshakufahamu, wewe unajifanya ni mjanja, lakini
ujue kuna wajanja zaidi yako, kuna kazi naifanya ikimalizika nitaangalia, kama
nitakuja au la, ..lakini kwa vile hatujaafikia na mzee ninaweza nisifike, na
kama nikifika, nitahitaji maelezo ya kina kwanini umezima mitambo, na kwasasa
siwezi kuona chochote kinachoendelea hapo, utakuwa ni wewe tu...na hilo
litakufanya utimize ombo langu, la sivyo, ...’akasema
‘Una uhakika gani na hilo?’ nikamuuliza
‘Utaona....mimi huwa sichezewi, mimi ni mtaalamu, nafahamu
sana hiyo mitambo, na kawaida yangu, nikitaka jambo ni lazima nilipate, muulize baba atakuambia, ndio maana nipo naye karibu, ananifahamu sana, lakini naona kama kanisahau kwenye mikataba yake, nitamkumbusha hilo,
na ,..’akasema lakini akawa kama anakatiza, inaonekana alikuwa akiongeleshwa na
mtu mwingine, aliyekuwa karibu naye, nahisi atakuwa ni mama yake au kuna
mwanamke yupo naye. Mimi nikacheka na kusema;
‘Hahaha..mtoto kama baba, mnagombea mali ya dhuluma eeh,
nina uhakika kuwa dhuluma hiyo itawapeleka pabaya...na mwisho wake umeshafika,
..wewe njoo nakusubiri kwa hamu, kwanza baba yako ameshakushitukia, ....’nikasema
na nikasikia akikata simu kwa hasira huku akisonya.
NB: Je huyo jamaa alifika? na kama alifika kulitokea nini na je ombi lake lilitimizwa,ni nini kitatokea kwa Makarasha, tuonane kwenye sehemu ijayo ya hitimisho la kisa hiki.
WAZO LA LEO:Tuwe
makini na malezi ya watoto wetu, kama tunafanya shughuli zisizo na manufaa kwa
watoto wetu kwa maisha yao ya badaye, ni bora tusiwahusishe. Tuwajengee watoto
wetu misingi mema ya maisha yao ya baadaye, tukikwepa makosa tuliyoyafanya, ili
wao waweze kuishi maisha bora, na kujenga kizazi bora cha baadaye.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment